Mlango wa mashahidi ulipofunguliwa akaingia shahidi mwingine akiwa kafunga
bandeji kubwa upande wa mkono wa
kushoto, toka begani hadi ubavuni, japokuwa
alikuwa kavaa koti, lakini koti hiloo lilikuwa kama limeegeshwa tu, nafikiri
alikuwa na kaliegesha hilo koti hivyo makusudi, ili ionekane ile sehemu
aliyopigwa risasi, …alitembea polepole huku mkono wa kulia umeshikilia mkono ule wa sehemu
yenye jeraha, akasogea hadi sehemu ya kuapishwa na baada ya kukamila zoezi hilo
akasogea sehemu aliyotakiwa kukaa.
Mwanadada alitulia akisubiri amri ya kuanza, na hakimu
alikasema mwanadada anaweza kuendelea na shahidi wake…mwanadada akainama kidogo
kama kutoa heshima na kumsogelea shahidi wake huku akitabasamu kumpa faraja
huyo shahidi aone ni jambo la kawaida;
‘Hebu taumbie wewe ni nani na shughuli zako ni zipi, na
jitahidi kusimamia kwenye kesi yetu, maana muda haututoshi,….’akasema wakili
mwanadada, huku akigeuka kidogo kichwa kuangalia upande ule wa watetezi, na alimuona
mshitakiwa mkuu, akiwa kama ndio katoka kwenye mshituko mwingine, na kwa muda
huo alikuwa akijaribu kujiweka sawa, ..
Shahidi huyu alitaja jina lake halisi halafu akendelea
kusema;
‘Mimi ni mlinzi na mtekelezaji wa maswala ya ujasusi ya
kiongozi wetu wa kijiji,…..’akasema na mwanadada akawa kama anatabsamu,
anageuka na kuwa kama anataka kutembea, lakini akiwa vile vile akauliza;
‘Hebu tufafanulie vyema, maana hivyo vyeo, ni vyeo vikubwa
sana, tunavyovisikia kwenye vyombo va habari na hatukutazamia kuwa kwenye
kijiji kama hicho kuna watu wenye vyeo kama hivyo’ akaambiwa.
‘Ni kweli, na hakuna anayejua cheo hicho zaidi ya watu wa
kundi letu na sio watu wetu wote wanaonifahamu kwa cheo hicho, wao wananiona
kama mlinzi tu wa mzee, na ndivyo wanavyojua kuwa kazi yangu kubwa ni usalama
wa mzee wetu,…’akatulia kidogo na kabla mwanadada hajamuuliza swali akasema kwa
haraka haraka.
‘Lakini hilo la usalama ilikuwa ni kwa mara chache sana,kama
imetokea mzee kunihitajia , akiwa kwenye safari ambazo anahisi kunaweza kusiwe
na usalama,….ila mimi nilikuwa na maalumu, hiyo ni kazi ya siri, kazi yangu hiyo
ya siri, ndio inatokana na cheo hicho, cha ujasusi, huwa nilikuwa nikitumwa
kwenda kufanya jambo, sehemu ambayo haiendeki ovyo….’akatulia kidogo.
‘Una maana gani kusema sehemu ambayo haiendeki ovyo na ni
kazi gani hizi ulikuwa ukitumwa ?’ akaulizwa
‘Kwa mfano mimi ndiye niliyetumwa kwenda hospitalini,
kumpelekea Jemedari juice yenye sumu, na hebu angalia ulinzi wake ulivyokuwa,
ni nani angeliweza kupenya hadi kuingia humo ndani, …lakini mimi kwa uzoefu
wangu niliweza kuingia humo ndani, na kumpa Jemedari juice hiyo, na yeye bila
kujua kuwa kuna kitu ndani yake, akainywa….’akatulia.
‘Hebu tuambia ulipenya penya vipi, na wakati kulikuwa na
ulinzi mkubwa kiasi hicho?’ akaulizwam na huyo jamaa akacheka kwa dharau.
‘Ule sio ulinzi wa kunifanya mimi nishindwe kuingia….niliingia
wakijua kuwa mimi ni mmoja wa wakuu wa usalama, waliokuja kukagua, …na ukumbuke
kuwa tuna mtu wetu ndani ya kituo ….hakuna aliyenitilia mashaka….’akasema
‘Ulipoingia ukampa juisi na yeye akapokea na kunywa, bila
kukuuliza wewe ni nani na …nakumbuka alikuwa hataki kula?’ akaulizwa.
‘Kwa muda ule alishaanza kukubali kula, na mimi nilipofika
nilimwambai kuwa kuna mtu kamletea kinywaji, na nimethibitisha kuwa hakina
tatizo…..na yeye akanywa hata bila ya kuingiwa na wasiwasi….’akasema
‘Kwanini alikunywa bila kufikiria, au bila ya
kuogopa?’akaulizwa.
‘Hata mimi nilishangaa, maana aliponiona tu….kwanza hakujua
ni mimi, lakini nilipotoa kofia yangu, akanigundua akasema ;
‘Afadhali umefika, najua ni nini kusudio lako, hata mimi
nilikuwa nasubiria iwe hivyo, maana nimechoka, ….ni bora nikapumzike, maana
watu hawanielewi,….., ‘..akatulia na kuonekana kukerwa na maelezo hayo, au
kujisikitia kwa kitendo hicho alichokifanya.
‘Kwakweli, nilitamani nimwambia kuwa asinywe, na tusingizie
kuwa amekunywa, lakini wakati huo Jemedari alishaipokea ile juisi na kuanza
kuinywa kwa fujo,na hapo sikutaka kumhoji zaidi nikachukua chupa ile kuondoka
zangu…..’akasema
‘Uliondoka na chupa yako, hukuiacha hapoo hapo?’ akaulizwa
‘Niliondoka nayo…nisingeliweza kuiacha hapo, …najua vyema
kazi yangu’akasema na wakili mwanadada, akawa kama anashangaa, halafu akauliza
swali jingine;
‘Je uliwahi kutumwa kufanya hivyo kwa watu wangapi, katika
kumbukumbu zako?’ akaulizwa
‘Aaah, sio wengi sana, kazi ya kupeleka juizi iliyochanganywa
na sumu sio kazi yangu sana, hiyo ni kacha ndogo, angeliweza kuipeleka mtu
yoyote tunayemwamini, lakini kwa hali kama ile, hakuna angelwieza kuingia kwa
kujiamini, kama mimi…. ‘ akashika kichwa kama anawaza jambo, halafu akasema;
‘Hata hivyo mambo kama hayo yamekuja kutokea muda wa
karibuni, kulikuwa hakuna tatizo kipindi cha nyuma, mambo yalikuwa yanakwenda
bila matatizo, wengi walikuwa watiifu tu, lakini baada ya kuchomwa moto mama
mkunga, ikaonekana kuna mgawanyiko ndani ya kundi, na hapo nikaanza kutumwatumwa
kwenye mambo kama hayo, hasa kwa wale watu wakorofi waliojaribu kuwa wasalati….’akasema
‘Na ulitumwa kuwapa sumu,au kuwafanya nini ….?’ akaulizwa
‘Kuna njia nyingi za kuwanyamazisha watu wa namna hiyo,
inategemea na mtu huyo yupoje, wengine hutumii hata nguvu, unatumia mkono
mtupu, wengine inahitajia silaha, na wengine sumu….na wengine vitisho…..wengine
kuteka nyara na kupelekwa kwenye mateso kidogo tu….ni mambo ya kitaalamu
kidogo, siwezi kuyaelezea kwa maneno ….’akasema huku akiangalia bandeji
alilokuwa kalifunga .
‘Nakuona umefungwa mkono, ulifanya nini mpaka ukafungwa hilo
bandeji?’ akaulizwa
‘Ilifikia sehemu nikaona, hii kazi hainifai tena, …..unajua
ubinadamu, upo, hata uwe mkatili kiasi gani, kuna muda unajishuku, unajiona
kuwa sasa imezidi, ….unaogopa na kuogopa, na ndivyo ilivyonitokea mimi, nikawa
najiuliza kwanini mimi nitumike kuwauwa watu, na wengine hawana hatia kabisa, wakati
mwingine damu za watu zinaniandama, …silali mpaka nilewe sana, sasa maisha gani
hayo, hata kama ninalipwa pesa nyingi kiasi gani, lakini sina raha…..nikaamua ni
bora niachane na maisha hayo, …lakini uamuzi wangu huo ulikuwa ni wa siri,
hakuna aliyefahamu….’akatulia kidogo.
‘Hata hivyo nilikuwa sijafahamu nifanyeje, maana kuacha kazi
kweny ekundi hili ina maana nikubali kuuwawa…hasa kwa mtu kama mimi, ndio
ningetoroka na kwenda mbali,….au nchi za nje, lakini niliona nikifanya hivyo,
bado moyo, nafsi ya kibinadamu itakuwa ikinisuta kila siku,….sasa nifanyeje…’akatulia
kidogo.
‘Mimi nikaona ni bora nifanye jambo la wema,….kwani niliwahi
kumsikia mtu wa imani za dini , akisema ukifanya makosa, fanya wema, huenda
wema huo ukafuta hayo madhambi yako, na kawaida wema huwa hauozi, …hata kama
watakuja kuniuwa hawa watu, lakini angalai nitakuwa nimefanya wema mdogo katika
maisha yangu…..’akatulia kidogo.
‘Niliazimia moyoni nikijua tendo hilo, litanipeleka ahera,
na ilivyo, muuaji atakufa kwa kuuwawa, hilo nilikuwa siku zote nalijau, ….basi
, nikasema kabla sijauliwa ni bora nitoe siri zote kwa watu wa usalama, …’hapo
akabetua mdomo kama anatabasamu.
‘Hapo napo nikajikiuta kwenye kikwazo, niende kwa watu wa
usalama wepi…..maana nijuavyo mimi, mkuu mwenyewe yupo kwenye
kundi…..’akatuli huku akicheka kwa
dharau.
‘Jamani kuna mambo humu…..ni wa vile mnasema kuwa muda ni
mdogo, ningewaambia mengi yaliyojificha, hasa kwenye kundi hilo, lakini kwa
vile mumesema kuwa nahitajika kuongelea yale tu yanayohusiana na hii kesi basi
nisipoteze muda…’akasema huku akiwa kainama chini, kama mtu anayetubu dhambi.
‘Ndio nikafikia uamuzi wa kumpigia simu Mwanadada, na ndio
nikakuita wewe nikukabidhi ushahidi wote, …na huo ni cha mtoto,…maana
nisingeliweza kubeba kila kitu, lakini huo unahusiana nah ii kesi, cha ajabu
kabisa, ilikuwa siri yangu na wewe niliyekupigia simu, sasa sijui ilikuwaje,…na
nilikuonya kuwa usimwambia mtu mwingine, maana nakifahamu kituo chetu….wengi
wapo mikononi mwa baosi wao…..’akatulia kidogo.
‘Ohh, nahisi uliwapigia watu wa usalama ukiogoap kuwa labda
mimi nilikuwa na dhamira mbaya, ukaharibu, na mengine unayafahamu kuwa
nilipokuwa nakukabidhi huo ushahidi ndipo, wakanipiga risasi,…..’akasema huku
akijiangalia
‘Kwa bahati nzuri risasi hiyo haikuniathiri ndani, nashukuru
madakitari walinifanya upasuaji na sasa ninaendelea vyema….labda muda wa mimi
kuhukumiwa ulikuwa bado, maana hapa najihisi ni mchafu…muuaji, japokuwa
nilikuwa nafanya kama mtumwa…..anyway…,
sasa nipo tayari kuelezea kila kitu, ..na ushahidi wote wa hii kesi nimeshakukabidhi….’akasema
na wakili mwanadada akawageukiwa watu wa utetezi, na wakili wao, alikuwa bado
akiteta na mteja wake, walionekana kuwa kuna kutokuelewana , kwani hawakuwa
makini kusikiliza hicho anachoongea huyo shahidi.
‘Wakili mtetezi, mbona hampo makini na shahidi huyo, kuna
tatizo gani……..?’ akuliza hakimu.
Wakili mtetesi akasema;
‘Samahani muheshimiwa
hakimu, mshitakiwa mzee, kiongozi wa kijiji, alikuwa akinikataza
kumuhoji huyo shahidi, kwasababu zake, na mimi nimeona kama ananiingilia kazi
yangu,lakini yeye bado anasisistiza kuwa anaomba kwanza aonane na ndugu yake,
yaani mama mkunga, ili athibitishe kuwa ndio yeye kweli, na anahitaji kuongea na
yeye kwani anahisi mengi yanayoongolewa hapo, anasingiziwa tu, na eti mimi
siweki pingamizi,….
'Pili, anataka asimame mwenyewe kujitetea maana anaona kuwa mimi
simtendei haki….kwahiyo...’akasema wakili wa utetezi na kabla hajamaliza,
akaingia mwanasheria wa familia ya merehemu mume wangu, aliongea kidogo na mzee
huyo na baadaye akamsogelea huyo wakili mtetezi, akamnong’oneza jambo, na huyu
wakili akatikisa kichwa kukubali.
Na wakati huo hakimu, alikuwa akiandika jambo kwenye
makabrsaha yake, na alipoinua kichwa aligeuka kumwangalia wakili mwanadada, na
kuuliza;
‘Je mumemalizana na shahidi huyo?’ akauliza.
‘Niliona ni vyema niwapishe wenzangu wamuhoji shahidi huyu kwanza
, kabla sijaendelea naye zaidi, na sioni kwanini wanang’ang’ania nimlete
shahidi huyo mwingine, wakati huyu bado hajamaliza…’akasema wakili mwanadada.
‘Kwani wengine walikuwa wamemaliza, mfano mama mkunga hatukupewa hata muda wa kumuuliza
maswali, hakuwa amemaliza maelezo yake,….ilikuwa bado, imeonakena ni tabia yako
kukatisha katisha mashahidi wako ili upate mwanya wa kutokuulizwa maswali
kutoka kwa watetezi wa hii kesi, kwa namnahii haki haitatendeka vyme….’akasema
wakili yule ambaye alionekana kuendelea na kazi yake baada ya kuongea na
mwanasheria na mzee kukubali wakili huyo aendelee.
Muheshimwia hakimu, akamwangalia wakili huyo, na alionekana
kukerwa na kauli yake hiyo, lakini hakusema neno, akamgeukia wakili mwanadada
na kusema;
‘Naona bado una mashahidi wengi, je utamsimamisha lini
shahidi wako ambaye mshitakiwa anahitajia kumuona?’ akaulizwa
‘Baada ya shahidi huyu, tukimalizana naye , tutamuita
shahidi huyo wanayemuhitajia, nitamleta huyo mama, mbele yako muheshimiwa, na
ushahidi wake, kuthibitisha haya yote yaliyotokea, na ataelezea jinsi gani
ilivyotokea siku hiyo, ili muone unyana wa mshitakiwa mkuu na wenzake…’akasema wakili
mwanadada na wakili wa utetezi,
akamgeukia mteja wake, wakawa wanateta kidogo, baadaye wakili huyo wa utetezi
akageuka kumwangalia hakimu, na kusema;
‘Kwa shahidi huyo hatuna maswali naye kwa sasa kama
alivyotaka mteja wangu, samahani sana muheshimiwa hakimu, kwani nilifikia hatua
ya kusitisha azi yangu hii, lakini baada ya maongezi, imeonekana niendelee, lakini
huenda huko mbele akaja wakili mwingine, ….samahani kwa usumbufu huu…’akainama kidogo
na halafu akageuka kumwangalia wakili mwanadada, ambaye alikuwa akiwasubiri.
‘Kama hamna maswali naye, basi ngoja nimalizane na shahidi
yangu huyu, kabla hatujamleta mama mkunga, kama muda utaruhusu….’akasema na
hakimu,akaonekana kungalia saa na akawa anaandika jambo kwenye makabrsaha yake,
halafu akasema;
‘Endeela na shahidi yako…’
‘Je katika kundi leni unapokea kazi kutoka kwa nani,?’
akaulizwa
‘Mara nyingi ni kutoka kwa kiongozi wetu wa kijiji….na mara
chache kutoka kwa watu wengine’akasema
‘Watu wengine kama akina nani?’ akaulizwa
‘Viongozi wa kundi, yupo katibu, yupo, ….mtaalamu, hata
hivyo sikuwa napokea kazi ovyo, kwani mimi ninapewa kazi iliyoshindikiana, na
wakati mwingine ninaweza kupewa kazi, nikaona haina nguvu sana, …nakaamua kumtuma
kijana wangu mwingine…..’akasema.
‘Kwahiyo kazi yako ilikuwa haiingialiani na majukumu ya
jemedari?’ akaulizwa.
‘Hapana, jemedari ni kiongozi wa serikali, ya kijiji, mimi
ni kiongozi, wa kundi la siri, ni vitu viwili tofauti…..’akasema.
‘Je kundi hilo unaloliita ni la siri lina mahali gani maalumu….yaani
makao yenu yalikuwa ni wapi, au mlikuwa mkikutana nyumbani kwa mzee, kiongozi
wa kijiji kama sehemu yenu maalumu?’ akaulizwa.
‘Hatukuwa na makao maalumu, ….kama kuna jambo tunaweza
kuamua kukutana popote, hata mashambanii, maporini….ilimradi kusiwe na shuku
yoyote….’akasema.
‘Je unahisi ni nani aliyekupiga hiyo risasi, maana watu wote
unawafahamu ?’ akaulizwa.
‘Kwakeli hadi sasa nimeshindwa kumfahamu ni nani…..kwasababu
hakuna anayefahamu ujio wangu kwako,…..labda ni watu wa usalama’akatulia kama
anawaza.
‘Je katika kundi lenu ni nani mwenye shabaha, maana
inaonekana kuwa risasi hiyo haikupigwa kwa karibu kama tulivyoona awali,
uchunguzi uliofanyika tena kwa makini, umeonyesha kuwa risasi hiyo ilipigwa
mbali kutoka jengo la pili, ….’akasema mwanadada na kumfanya huyo shahidi
kushituka kidogo.
‘Ina maana nilipigwa risasi hiyo kutoka mbali, nilijua tu, ….lakini
kwanini,ina maana watu wenu hawakuwa na utaalamu wa kugundua hilo,…nilijua
tu,..nina utaalamu wa kujua nguvu ya risasi, hiyo ilikuja kutoka mbali, lakini
sikuweza kuthibitisha pale mliposema kuwa mpigaji alipiga kwa kupitia
dirishani,?’ akawa kama anasikitika au kulalamika.
‘Mwanzoni ilionekana hivyo, lakini uchunguzi uligundua
tofauti, kwahiyo hilo dirisha huenda lilikatwa kimakosa kwa dhamira nyingine,au
kama mbinu tu ya kuhadaa…..’akasema wakili mwanadada.
‘Sasa kwa vile unalifahamu vyema kundi lenu, kwa mtizamo
huo, ….ni nani unayemfahamu anaweza kulenga shabaha, ndani ya kundi lenui
…’hapo wakili wa utetezi akaweka pingamizi, lakini hakimu akasema swali hilo
lijibiwe kwani muhimu sana kwenye kesi hiyo.
‘Ninayemfahamu sana, ni…mkuu wa kituo, wengine sina uhakika
nao, maana hatujawahi kuwa na kazi kubwa ya namna hiyo ya kulenga shabaha kwa
mbali….’akasema bila ya uhakika.
‘Ina maana viongozi wako wote hawajui shabaha, kiongozi wa
kijiji, ndugu yake mtaalamu, na …..’aksema.
‘Kwakweli sina uhakika na hilo, haijawahi kutokea jambo kama
hilo, japokuwa nafahamu kuwa wanajua kutumia silaha, …..’akasema huyo shahidi.
Na wakili mwanadada akatoa vielelezo mbali mbali alivyokabidhiwa na huyo shahidi,
na kila kimoja shahidi huyo alipewa nafasi ya kutoa maelezo yake, zikiwemo
kanda mabli mbali za video, alizowahi kuzirekodi, kwa ajili ya ushahidi au
kuwatishia watu….na ilikuwa ni ajabu kwa kambi ya utetezi, ambao walikuwa
kimiya, wakiwa kama wasikilizaji tu
Wakili mwanadada alipotoa chupa mbili ambazo zilikuwa na
mabaki kidogo ya kinywaji, alimgeukiwa shahidi na kumuuliza
‘Kati ya hizi chupa mbili ni ipi uliyoipeleka kwa Jemedari?’
akaulizwa.
‘Ni hiyo ya mkono wa kushoto….yenye kifuniko cheupe’akasema
‘Una uhakika gani , maana naona chupa zote zinafanana…?’
akauliza.
‘Kifuniko chake kilikuwa hakifungi vyema, nikabadilisha,
…kama unavyoona vifuniko havifanani vyema…’akasema.
Wakili mwanadada akaziangalia zile chupa, na akataka kusema
jambo, lakini akasita na kumsogelea msaidizi wake, akamnongoneza jambo, na huyu
shahidi yake akaziangalai zile chupa na kutikisa kichwa, na hapo wakili
mwanadada akasema;
‘Muheshimiwa hakimu, tumemalizana na shahidi huyu, lakini
tulikuwa tunahitajia kufanya uchunguzi zaidi katika vielelezi hivi, tuna imani
kuwa kuna jambo jingine limezuka, na huenda likatusaidia kuhakikisha kuwa haki
inatendeka vyema…’akasema na hakimu akaonekana kushangaa na kuuliza.
‘Lakini mumeshawakilisha vielelezo hivyo kama ushaidi, kuna
tatizo gani na ushahidi wenu huo, hamna uhakika nao?’ akauliza hakimu kwa sauti
ya ukali.
‘Muheshimiwa hakimu, tutaelezea zaidi tukija kumsimamisha
shahidi wetu aliyepita, ambaye ana utaalamu wa hizo sumu,…kwani inaonekana
chupa, aliyopelekewa Jemedari, na huyu shahidi wetu, haikuwa na hiyo sumu, …na
shahidi wetu anakiri kuwa aliondoka na chupa hiyo…lakini uchunguzi wetu ulikuta
chupa ikiwa karibu na marehemu jemedari,…..’akatuliwa wakili mwanadada na
hakimu akawa kama anawaza jambo.
‘Unataka kusema nini?’ akauliza hakimu, alipogeuka kuwaangalia
watetezi, ambao hawakuwa makini na mazungumzo hayo.
‘Inaonekana kuna mchezo ulichezwa, inaonekena Jemedari
hakufa na juisi aliyopelekewa na huyu shahidi, …atakuwa aliuwawa na sumu
nyingine,….ina maana kuna mtu mwingine alikuja kuleta chupa yenye sumu, na
alikuwa anafahamu kuwa huyu shahidi huenda hatafanya hilo alilotumwa, au
alikuwa anajua kuwa juisi hiyo aliyopeleka huyu shahidi haikuwa na sumu….’akasema
wakili mwanadada.
Hakimu akaangalia saa yake, na kusema;
‘Hakikisheni mnafanya uchunguzi wa kina kabla hamjaleta
vielelezo vyenu, je kesho mnaweza mkawa mumekamlisha uchunguzi wenu huo?’
akaulizwa.
‘Muheshimiwa hakimu,….tuna uhakika na hilo….leo hii kila
kitu kitakamila na kesho tutakuwa tayari na kielelezo hicho’akasema wakili
mwanadada.
‘Sawa kesi yetu itaendelea kesho, tukianzia kwenye hivyo
vielelezo na shaidi mama mkunga atasimama tena kukamilisha ushahidi wake,
….tunahitaji kesi hii iishe haraka iwezekanavyo maana inaleta hisia kubwa kwa
raia, na hatupendi haki isitendeke kama wanavyodai watu…’akasema hakimu, na
mawakili wote wakakubali na hakimu akasema;
‘Kesi imeahirishwa hadi kesho yake.....'akasema hakimu
Wakili mwanadada alipotoka hapo, akachukua simu yake na
kuanza kuongea na vyanzo vyake vya haabari, huku akitembea kuelekea kwenye chumba cha mashahidi, na alipofika
aliwakuta watu kama wamesindia, na ni watu wote wakiwemo walinzi, akauliza kwa
mshangao;
‘Mtaalamu yupo wapi?’ akauliza huku akiangalia huku na kule.
‘Ametoweka kiajabu…’akasema mlinzi ambaye alikuwa akipikicha
macho na kupiga miayo
‘Kwa vipi ametoweka kijabu?’ akauliza mwanadada.
‘Hatuelewi, maana ilitokea kitu kama upepo, tukajikuta wote
tumesinzia, na tulipofumbua macho , hatukumuoan tena….’akasema mmoja wa
walinzi.
Wakili mwanadada akatoka nje, na kuanza kuwasiliana na
vyanzo vyake vya habari na watu wa usalama wakawa wanahaha huku na kule
kumtafuta huyo mtaalamu.
NB: Je kama mtaalamu katoweka, ni nani atathibitisha sumu
hizo, je ni kweli hayo yanaweza kutokea….au wewe unahisi ni kisa cha kubuni tu.
…kazi kwako, tuwe pamoja.
WAZO LA LEO:
Tuchungeni sana uvumi usio na ushahidi, watu siku hizi wanaona ni jambo la
kawaida tu kuongea, au kuandika, bila hata ya kuwa na ushahidi na hayo
wanayoyaandika, ilimradi kasikia tu basi yeye anakuwa wakala wa propaganda potofu,
ilimradi hayo anayoyaongea au kuyaandika yanakidhi haja zake…na anayaandika hayo kama taarifa ya kweli na sio hadithi ya kutunga.
Kwa kufanya hivyo, sio haki, tusihukumu kabla ya hukumu,
tusiwazushie watu uwongo, kwa vile sio wenzetu, au sio ndugu, au sio mtu wa
heshima,kwani kwa kutenda hivyo, tunakiuka miiko ya uandishi, tunakuwa
tumetenda dhuluma, na hii ni dhambi, na
yatakayotokea baadaye ujue ni wewe uliyesababisha hivyo, na utawajibika kwa
yote hayo,…napenda kuwaasa wenzangu na kujiasa mwenyewe, kuwa tuwe makini na `kalamu’….
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment