Wakili mwanadada akiwa nyuma ya pikipiki, aliendelea
kuwasiliana na watu wake, na nyuma yake kulikuwa na pikipiki nyingine mbili, kila
moja ikiwa na watu watatu yaani dereva na watu wengine wawili nyuma ya dereva
huyo, na mmoja wa watu hawo alikuwepo mwanasheria wa familia ya marehemu mume
wangu.
Mwanasheria huyo baada ya kesi ya siku hiyo, alikuja moja
kwa moja kwa wakili mwanadada, na kumkuta wakili huyo akiwa anaongea na simu,
hakujali,au kusubiri, au kusikiliza ni
nini mwenzake anaongea kwenye simu, yeye moja kwa moja alianza kuongea kwa
kusema;
‘Nasikia Mtalaamu katoweka,…nina hamu sana ya kumhoji huyu
mtu uso kwa uso….’akasema na huku akiangalia upande ule walipokuwa wamekaa
mashahidi , ambao wengine walishaanza kuondoka ili kusubiria hiyo siku ya
kesho.
‘Na kwakweli baada ya kusikia kuwa yeye kahusika na kifo cha
kaka yangu, akishirikiana na kiongozi wa kijiji, siwezi kukubali atoke hapa
bila kushitakiwa, na ilibidi ashikiliwe moja kwa moja, …sasa mnaona eti katoroka,
huyu alitakiwa kushitakiwa, kama
alivyoshikiliwa kiongozi wa kijiji na wenzake….’akasema na safari hii akimgeukia
wakili mwanadada na kumwangalia na kipindi hicho wakili mwanadada alikuwa
kshikilia simu sikioni, akiwa kaangalia chini, akisikiliza jambo kwa makini.
Wakili mwanadada, akainua kichwa na kumwangalia mwanasheria
huyo, akakunja sura na kuangalia pembeni huku akiwa bado kashikilia simu
sikioni, na mwanasheria akawa bado anaendelea kuongea.
‘Wewe mtu atatorakaje mbele ya ulinzi wa watu wanaoaminika, …hii
ni ajabu kabisa, na hili mimi sitalikubali…kama mna njama na yeye, ili eti
awasaidie , ili eti aje asamehewe, mimi sitakubali …wale wote waliohusika ni
lazima wawajibike…..’akasema huku akiendelea kumwangalia mwanadada.
Wakili mwanadada, akawa sasa haongei na ile simu, alikuwa
akisiliza tu huyo aliyekuwa akimpigia simu anavyoongea na kuitikia neno moja
moja, kama `mmmmmh’, `sawa,’ `kabisa’…`hakuna shida….’, na alipoona huyo
mwanasheria anazidi kuongea na isingelikuwa rahisi kwake kusikilizana na huyo
anayeongea naye kwenye simu, akasema;
‘Samahani kidogo tutaongea baadaye kidogo, kuna mtu hapa,
baadaye…..’akakata simu na kumgeukia mwanasheria huyo, wakawa wanaangaliana uso
kwa uso na mwanadada akauliza;
‘Vipi kuna tatizo?’ akauliza wakili mwanadada.
‘Eti kuna tatizo,…!?, wewe huoni kuwa hili ni tatizo,kwangu
mimi sawa ninaweza kusema hakuna tatizo, ndio maana nimekuja kwenu ili kuongeza nguvu kwa upande
wenu…..kwa maana kama watu kama hawa wanatoweka kiajabu, mnafikiria haki kweli
itatendeka’akasema.
‘Hatujasema kuwa tunahitajia nguvu mpya, tena zaidi kutoka
kwa wapinzani…halafu ni nani kakumabia kuwa mtaalamu katoweka, na ukumbuke yule
kaitwa kama shahidi, na yupo tayari kuwepo kama akihitajika, kuondoka kwake,
sio maana katoweka moja kwa moja…’akasema mwanadada akimwangalia mwanasheria
huyu, ambaye alionekana kukonda, …na kutokuwa na raha.
‘Una uhakika na hilo unalolisema , au unajipa tumaini….wewe
unamfahamu vyema huyo mtu,…na unakumbuka alisema nini wakati anatoa ushahidi,
kuwa huenda ikawa ndio mara ya mwisho kuonekana…’akasema mwanasheria na
kumfanya wakaili mwanadada azidi kumwangalia kwa mashaka.
‘Kwahiyo unasemaje?’ akauliza wakili mwanadada, akiwa bado
bado anamtizama moja kwa moja huyo mwanasheria machoni.
‘Mwanadada, nakuomba sana unielewe, kesi hii imenifungua
masikio, na …kiukweli, sikujua kuwa nipo kwenye kichaka cha mbwa mwitu….na
nilipogundua hilo, nisingeliweza kutoka tu, bila ya kuwa nauhakika wa njia ya
kutokea,….ilibidi nitafiti njia ipi bora ya kutoka hapo kichakani, na pia
angalau nitoke na kitoweo….’akasema kwa mafumbo mafumbo.
‘Kwahiyo unasemaje?’ akauliza mwanadada huku akiangalia saa,
alijua hana muda wa kupoteza, kwa vile wameshamuahidi muheshimiwa hakimu, kuwa
kila kitu kitakamilika leo hii hii, na kesho kesi inaendelea kama kawaida, sasa
mtu muhimu aliyemtegemea kwa ajili ya kusaidia kukamilika kwa uchunguzi wa
baadhi ya vielelezo ndio huyo hayupo.
‘Nataka huyo mtu akamatwe kama alivyokamatwa
mwenzake….’akasema mwanasheria.
‘Haya mkamate…..’akasema mwanadada kwa sauti ya kejeli.
‘Sikiliza mwanadada, usinione kuwa nasema haya kwa
kukupotezea muda, kama uliniona ndani ya mahakama, nilikuwa naingia na
kutoka…nilikuwa nafuatilia mambo haya kwa karibu sana kuna jambo nimeligundua,
nitakuja kukuelezea baadaye, ….baada ya kusikiliza ushahidi wa huyo mtaalamu
nimegundua mengi, na bado nafuatilia…huyo mtu kweli katoka, lakini kuna watu
wangu wanamfuatilia kwa karibu….hawezi kutupotea hii leo’akasema na hapo
mwanadada akaingiwa na hamu ya kumsikiliza.
‘Kwanini mnamfuatilia shahidi wetu, anawahusu nini?’
akauliza.
‘Siamini maneno yake kuwa katekwa na mizimu…..’akasema na
wakili mwanadada,akakunja uso kwa mshangao.
‘Ehe, kwa vipi?’ akauliza mwanadada sasa akiwa katulia
kumsikiliza, aliona huenda jamaa huyo ana mambo ambayo yatamrahisishia kazi
yake, japokuwa bado alikuwa hamuamini.
‘Huyu mtu ni mjanja sana….wewe huoni kwanza kaamua
kuwasaliti wenzake, kiujanja-ujanja, ili aonekane yeye ni mtu safi, …kweli mtu
huyu anastahili kuitwa mtu msafi….na eti yupo na mizimu inamlinda na ili
kuhakikisha anasema ukweli, na sasa katumia mbinu kuwapotea ili mumuamini, hayo
yoye ni ujanja wake, …..nyie hamlioni hili, au kwa vile ni shahidi wenu,
mnayachukulia mengine kirahisirahisi tu..?’ akauliza huku akiwa kashika kiuno
‘Mhh, sasa unayaona haya, tulipokuwa tunakushauri uliziba
masikio,na hata hivyo una gani na hayo unayoyasema au ni hasira za kutaka
kulipiza kisasi…kwa vile kasema yeye ndiye aliyetoa maelekezo ya kutengenezwa
sumu, ambayo ndiyo iliyomuua kaka yako?’ akauliza wakili mwanadada
‘Kama ningelichukulia hasira na kutaka kulipiza kisasi,
ningelishachukua hatua mbaya zaidi, hebu fikiria, unasikia kuwa watu wamehusika
kumuua ndugu yako, halafu wapo nje, unafiria utafanya nini…?’ akauliza.
‘Sasa sema tufanyeje, au umenijia kwa shauri gani, maana
muda unakwenda mbio….’akasema wakili mwanadada.
‘Hapo sasa tupo pamoja, cha muhimu kwanza ni kuhakikisha
kuwa huyu mtu anakamatwa, tukamtafute huyu mtu awepo rumande, nahisi atakuwa
yupo mahali kajificha…’akasema
‘Kajificha wapi…na kwanini ajifiche?’ akauliza mwanadada kwa
mshangao, halafu akasema
‘Sijui ni nani kakuambia,lakini ni kweli wanadai kuwa
katoweka kiajabu ajabu….haijulikani wapi alipo na sikuweza kupata muda wa
kuongea na yeye kuwa bado anahitajika’akaambiwa.
‘Mimi kama nilivyokuambia kuwa nina watu wangu,
…watamfuatilia huyo mtu kwa karibu watampata tu..nimekuwa nikimfuatilia kwa
karibu tu, na ndani ya hawo watu wangu kuna mtu ambaye anafahamu mambo hayo ya
mizimu ni mkali, na anayajua haswa, japokuwa siyaamini …, yeye kadai kuwa anaweza
kutambua wapi alipokwenda….’akasema.
‘Sawa basi tusipoteze muda, lakini nakuonya, kama ni moja ya
mbinu zenu, utakuja kuumbuka mwenyewe…sikutishii, ila ninakuambia, ….’akasema
mwanadada, huku akitaka kupiga simu, na mwanasheria huyu akasema.
‘Niamini mwanadada,…kuanzia sasa tupo pamoja, nitahakikisha
sheria inafuata mkondo wake, nimechoka na haya mambo, nahitaji mambo haya
yaishe tuweze kuendelea na maisha mengine, na nimechoka na haya mambo ya kijiji
chetu,….kinahitaji mageuzi, uchafu huu uondoke, ili tukiendeleze kijiji chetu,…mbona
mambo haya ni kale, hayastahili kuwepo kwenye dunia hii ya sasa…’akasema huku
akikunja uso, na mwanadada akawa anafauta namba kwenye simu yake na mwanasheria
huyo akaendeela kusema.
‘Na hilo halitafanikiwa kama tukiwakumbatia watu kama hawo…watu
wa namna hiyo wote,wasafaishwe, waonywe, wafungwe, wakitoka watakuwa
wamejifunza jinsi gani ya kuishi na watu wengine kistaarabu, na sio kiujanja
ujanja…’akasema huku akionyesha kidole kule walipokuwa wamesimama kambi ya
utetezi.
‘Haya twendeni…lakini tunahitajika kujiandaa, …una
silaha,?’ mwanadada akamuuliza huyo
mwanasheria na huyo mwanasheria akatabsamu na kusema.
‘Sina silaha, unanitega nini, lakini watu wangu waliopo huko
wanazo silaha, usiwe na shaka na mimi,…nisingeliweza kuja hapa mahakamani na
silaha…’akasema mwanasheria huyo akionyesha hasira usoni.
‘Lakini ..ujue bado hatupo pamoja,wewe una kambi yako
….tunachohitajia ni wewe kutuonyesha huko alipoelekea huyo mtaalmu, na wewe
ukae pembeni kabisa…usije ukajiingiza katika maswala yasiyokuhusu ukatuharibia
utaratibu wetu…’akasema mwanadada na mwanasheria huyo akacheka na kusema.
‘Hauna haja ya kuniambia hilo, wewe mwenyewe utakuja
kuniomba nisaidie,…mwenyewe utaona, wewe hujawahi kuuingia huo msitu….’akasema
huyo mwanasheria.
‘Wewe uliwahi kuuingia huo msitu, kwani kuna nini cha
kutisha, wanyama wakali, au kuna nini…?’ akauliza mwanadada akiwa na mashaka.
‘Mimi ni mzaliwa wa huku,…na nimewahi kufanya matembezi
ndani ya huo msitu, hadi kwenye hayo mapango ya watu wa kale, …’akasema na
kutulia, wakati simu ya mwanadada ilipolia, na mwanadada huyo akaipokea na
kusikiliza, akasema;
‘Tunakuja,….hakikisha wote wamekamilika, na wasifanye lolote
mpaka tufike…wasije waharibu bado tunamuhitaji huyo mtu …..’akasema huyo
mwanadada na kabla hajaendelea kuongea mara mara akaja jamaa mmoja,akiwa
kashikilia usinge, ni aina ya fimbo, lakini imefunikwa na ngozi ya mkia wa
mnyama, na alikuwa akiizungusha zungusha hewani, na mwanasheria akasema;
‘Huyu ndiye mtu atakayetusaidia kufika huko, ni mtaalamu wa
mambo ya mizumu…na mashetani’akasema na wakili mwanadada akamwangalia huyo mtu
kwa mashaka, na hakutaka kusema kitu, maana macho ya yule mtu yalikuwa
yanatisha, na shingo yake ilikuwa imekakamaa utafikiri anainua kitu kizito. Na uso
wake ulikuwa umekunjamana kama mzee, alikuwa anatisha.
‘Sawa twendeni, ..lakini hatukuwa tunahitajia watu wengi
ambao wanaweza kuharibu mpangilio wetu, nia na lengo letu ni kumpata huyo
mtaalamu ili atusaidia katika kuviangalai hivyo vielelezo, na si vinginenvyo…huyo
sio mhalafu, hatuna kibali hicho….’akasema mwanadada. Na yule mtu akacheka na
kukatiza mara moja, kama vile kaambiwa nyamaza, akasema.
‘Sivyo hivyo unavyofikiria mwanadada, ndio jina lako kama sikosei,
eheee, mimi nimeona mbali, kuna tatizo, ….lakini siwezi kulisema hilo tatizo
hapa, mpaka hapo utakaposhuhudia mwenyewe…maana nyie watu mnahitajia ushahidi
wa kuone, lakini ukumbuke kuna mengine hayawezi kuonekana kirahisi, bila ya
msaada wetu….’akasema huyo mtu.
‘Tusipoteze muda, twendeni…’akasema mwanadada na kutaka kupanda
pikipiki na nyuma yake alikuwa kijana mmoja shababi, alikuwa na silaha,
akionyesha kuwa ni mwanausalama, huyu ni mlinzi wake, anayemuamini sana.
Yule mtu aliyeletwa na mwanasheria akamsogelea mwanadada, na
huyo mlinzi akamwangalia kwa makini, ….na mwanadada naye akawa kama anashangaa
kwanini huyo mtu anamsogogelea na huyo mtu akasema;
‘Huko tunapokwenda kunahitajia ujuzi wa ziada, ni vyema wote
nikawapaka mafuta maalumu ya kuondoa harufu zetu za kibinadamu,..vinginevyo
tukifika huko hatutaona kitu , au tutapoteana au lolote baya linaweza
kutokea,….silaha zenu, hazitasaidia kitu, kama wenyewe wakigundua kuwa mpo huko
kwa nia fulani…..mtajikuta wote mumelala, na mkizindukana mnaweza kujikuta wote
mpo uchi, huku mumefungwa kama wafungwa….’akasema
Kabla mwanadada hajasema kitu, huyo mtu, akaanza kuwapaka
mafuta, na alipomaliza zoezi hilo, akasema ;
‘Haya tunaweza kuondoka…lakini kila mmoja amuombe mungu wake
kwa imani yake,maana huko tuendapo sivyo kama mnavyofikiria, mnakwenda vitani,
na mnakwenda kupigana na watu wasioonekana….’akasema huyo mtu .
‘Tusianze kutishana hapa, kama mnaogopa kaeni,sisi tunajua
ni nini tunakwenda kufanya, hatuna nia mbaya na lengo letu ni kuongea na
shahidi wetu…mnanielewa…’akasema wakili mwanadada na kukaa vyema kwenye
pikipiki yake akamgeukiwa mlinzi wake, kumuashiria kuwa yeye yupo tayari.
‘Tunaweza kuondoka….’akasema huyo mlinzi baada ya kuangalia
saa yake na kuangalia huku na kule,
Msafara ukaanza.
**************
Wakati wanaelekea huko akili ya mwanadada ikawa inaunganisha
matukio haya na yale aliyoyasikia ndani ya mahakama, akawa anajaribu kumuwaza
huyo anayeitwa mtaalamu, japokuwa ni shahidi yake, lakini akili yake ilikuwa haikubali
kumwamini moja kwa moja.
Na kabla hajamaliza kumuwazia huyo mtalaamu, mara akili yake
ikakumbuja jambo, ikamkumbuka binti ya mkuu wa kitengo cha upelelezo kwenye
kituo hicho cha usalama,Akakumbuka siku aliyomtembelea binti huyo, na akakumbuka
maongezoi yao, na tukio la ajabu lililotokea siku hiyo.
Nia na lengo lake lilikuwa kutaka kujua, jinsi gani ilivyotokea kwa huyo binti, ilikuwa katika kuhangaika
hangaika kutafuta ushahidi, na akaona labda huyo binti anaweza kuwa na lolote,
basi katika kuongea na binti huyo, akataka kujua jinsi ilivyotokea hadi binti
huyo kutoweka hapo nyumbani.
Yule binti alionyesha kuogopa, alipoulizwa swali hilo na
hapo mwanadada akahisi kuna jambo huyo binti analificha, na huenda analificha
kwa kumuogopa baba yake.
‘Naomba uniambie ukweli, maana kama una jambo linakuogopesha
au kukupa mawazo, au kukuumiza, njia rahisi ni kulitoa moyoni, na ni bora ukamtafuta mtu unayemuamini ukajaribu
kumwambia ili akupe ushauri, nakuona una jambo, ….niamini mimi, nina uhakika
nikilisikia ninaweza kukusaidia…niaini, au huaniamini mimi?’akamuuliza
‘A-a-ah…sina tatizo ila tu nikisikia mambo ya huko,….ya
tukio hilo nahisi kuogopa…mimi nakuamini kweli nimesikia sifa zako, unasaidia
sana watu,….hata hivyo, mimi sina tatizo’akasema huyu binti akikwepa
kumwangalia huyo mwanadada machoni.
‘Kwanini uogope, na wewe ulisema kuwa hujui ulipopelekwa na
hujui kulitokea nini?’ akaulizwa.
‘Ndio hivyo, ndio maana naogopa,isije ikatokea
tena….’akasema huyo binti na wakili mwanadada, akamwangalia huyo binti, na
kuhisi kuna jambo.
‘Mimi ni mwanamke mwenzako, japokuwa ni mkubwa kuliko wewe,
lakini ninaweza kukusaidia, je ulifanyiwa kitendo chochote kibaya?’ akaulizwa,
na huyo binti akaguna na kusema
‘Nitajuaje na mimi nilikuwa sijijui…’akasema na kuangalia
pembeni
‘Je uliporudishwa, baba yako alikupeleka kupimwa,
kuhakikisha kuwa hakuna lolote baya ulilowahi kutendewa?’ akaulizwa na huyo
binti, akaangalai chini, na alipoinua kichwa, machoni kulikuwa na dalili ya machozi.
‘Nakuomba usiendelee kuniuliza hayo …natamani nife,
nikiyawaza hayo…tafadhali, usije….oh’akasema na hapo wakili mwanadada,
akamsogelea na kumkumbatia na yule binti, akamshikilia mwanadada kwa nguvu,
kama vile anaogopa jambo..na hapo akili ya mwanadada ikahisi kuna jambo
lilitokea kwa huyo binti, lakini hakupenda kumshurutisha kuliongea, akaona ampe
muda.
Ni wakati mwanadada akiwa anataka kuondoka na yule binti
akiwa anamfuatilia kwa nyuma kama anamsindikiza, mara yule binti akadondoka, na
kuanza kutikisika na akawa kama mtu aliyepagawa, na mwanadada, akawa
anahangaika kumsaidia, na mara yule binti akaanza kuongea sauti ya mwanaume;
‘Ehe…umesahau eeh, nilikuambia nini…wewe sasa ni mke wangu,
sitaki ukiuka masharti…’ile sauti ya kidume dume ikasema. Na mwanadada akawa
anashindwa asema nini, lakini wazo likamjia, na akakumbuka hadithi za watu
waliopandwa na mshetani kuwa unaweza ukawauliza, na wakakuambia jambo.
‘Je ulimwambia nini mke wako?’ akauliza mwanadada kwa
mashaka maana hakujua anavyofanya ndivyo au sivyo.
‘Muulize mwenyewe,…alipokuja kwangu na kutambulishwa kwangu,
alikubali kuwa mimi ni mume wake, na tukaozeshwa, na ghafla akanikimbia….na
nilimwambai sitamuacha..kamwe….na hakutakiwa kuongea siri ya mume wake..’ila
sauti ikasema.
‘Lakini huyu bado mdogo, ataolewaje…?’ akauliza mwanadada.
‘Hahahaha…huyu bado mdogo!?, wewe wasema hivyo, …alipokuja
kwangu, alikuwa keshajua mambo ya kikubwa,…nyie wanadamu mnajifanya na siri
kubwa, huyo sio mtoto, alishajua tayari mambo ya kikubwa….alikuwa na mtu wake wanadanganyana,
wanakutana naye mara kwa mara, wakijifanya wanasoma,..kwahiyo huyo sio mtoto
kama unavyofikiria wewe, na mimi nikaona ili kumuokoa ni bora tu ni
muoe….sijafanya makosa, …’ile sauti ikasema.
‘Huyo kijana anayesoma naye yupo wapi?’ akauliza mwanadada,
akitaka kuhakikisha
‘Huyo kijana, keshahama hapa, baada ya kupata vitisho kutoka
kwangu, lakini jana alikuwepo hapa, eti kaja kusalimia,anadanganya kaja kwa
ajili ya mke wangu, na huyu mke wangu akaanza kumsimulia mambo yangu,
nimekasirika sana, na huyo kijana nimempa adhabu kali sana, hatanisahau na
hataweza kuongea na binti huyu tena..na kuokoka kwake ni kwa huyu mke wangu
kunrejea, na akichelewa baada ya siku mbili atakufa…’ila sauti ikasema.
‘Je sasa wewe unaishi wapi?’ akauliza mwanadada.
‘Nyumbani kwangu ni mapangoni, nyumba ya mizimu, ambapo
ndipo tulifunga ndoa na huyu binti, kama huyu binti angetulia, angekula raha
zote za dunia , lakini akawa mjanja, eti anajifanya mtu wa dini, …nimempa siku
tatu tu, kunirejea akiwa hai, ….asipofanya
hivyo, atarejea kwangu akiwa mfu,..na hapo atakuwa wangu wa kudumu…’ile sauti
ikasema, na mara huyo binti akatulia kimiya.
Baadaye huyo binti alizindukana, na akawa kama anashangaa, na
kuuliza
‘Nipo wapi hapa…kwani kumetokea nini?’ akamuuliza mwanadada
‘Upo nyumbani kwenu, kwani vipi?’ mwanadada akamuuliza.
‘Naona kama nilikuwa mapangoni..kwenye nyumba nzuri…..kuna
kila aina ya vitu vizuri na nikaambiwa nichague moja, niishi huko, na rafiki
yangu apone, au nikatae rafiki yangu afe, na mimi nitakwenda kuishi huko,
nikiwa maiti..nikaogopa kujibu, …na ndipo nikazindukana…’akasema.
‘We binti hebu niambie ukweli, ulipokuwa huko mapangoni
kilitokea nini na huyo rafiki yako ni nani?’ akamuuliza na huyo binti akawa
kama kashituka na kuuliza
‘Eti nini mapangoni…nani kakumbia nilikuwa mapangoni…..’na
akageuka na kukimbilia ndani, na mwanadada hakuweza kumuona tena, na huyo binti
hakutaka kuongea na yeye tena, hata alipojaribu kumbembeleza,basi akaondoka
kwenda kuulizia nyumbani kwa huyo kijana anayesoma naye
Alipofika nyumbani kwa huyo kijana, aliwakuta watu wakiwa na
majonzi,na alipoulizia kuhusu huyo kijana akaambiwa huyo kijana kapatwa na
matatizo, alianguka ghafala, na kuanza kupatatapa, na amekuwa kama kapagawa, ..
‘Ni kama mashetani, lakini sio ya kawaida…’akasema ndugu wa
karibu wa huyo kijana
‘Sasa yupo wapi?’ akauliza mwanadada.
‘Imebidi asafirishwe haraka, maana ikipita siku mbili
anaweza kupotea moja kwa moja…’jamaa huyo akasema.
‘Kwanini?’ akauliza
‘Hatujui, wanajua wazazi wake…ni mambo ya mapepo, na
wasipohangaika, wanaweza kumkosa kijana, huenda kaingilia nyumba za watu….’akasema
huyo jamaa na mwanadada akamwangalia kwa mashaka, na kujiuliza kajuaje yote
hayo.
‘Kwao ni wapi?’ akauliza
‘Kwani wewe ni nani na kwanini uanmuulizia ….ooh,
nimekukumbuka wewe ni wakili mwanadada, …achana na mambo hayo, hayatakusaidia
kwenye kesi yenu’akasema.
‘Kwanini unasema hivyo hivyo?’ akamuuliza.
‘Nimekuona tu,….huko unapokwenda ni kubaya, chunga sana….’akasema
huyo mtu na kuondoka.
Mwanadada hakuweza kupata taarifa zaidi, za huyo kijana au
huyo binti, na alitaka ajue ni nini hatima ya hayo yote.
‘Tumeshafika msituni, sasa mnifuate mimi…tuache hizi
pikipiki hapa….’yule mtu wa mwanasheria akasema na zile pikipiki zikawekwa na
mmoja akachagulia kuzilinda…
‘Haya twendeni…..’safari ya miguu ikaanza, na kabla
hawajafika mbali, kukaanza kusikika kitu kama upepo, ukivuma kwa kasi kuelekea
hapo walipokuwa na ukawa unafika na kupotea , unafika na kupotea, na yule mtu
akawa anachezesha ile fimbo yake, kama kuufukuza….
NB: Dunia hii ina mambo
WAZO LA LEO: Kuna
ammbo mengi sana ya ajabu yapo hapa duniani, na mengi yanasababishwa na sisi
wanadamu, kuna wanadamu wanaamini mambo yasiyotufaa, ya viumbe vingine, vyenye
maisha yao, na hatukuwa na mamlaka navyo, na hata kujiingiza kwenye mambo
ambayo mwisho wa siku yanakuja kuwaathiri, na sio kuwaathiri wao tu, na watu
wengine wasiohusika,….
Kwanini tujiingize kwenye mambo hayo, kwanini tujiingize
kwenye matatizo, wakati maisha yetu yenyewe ni ya matatizo matupu, …ni
kwasababu ya kutafuta utajiri, kutafuta umaarufu au ni kwasababu gani, kwanini
tusifanya mambo ya ugunduzi wa kisayansi, yenye tija kwetu….jamani wangapi
walifanya hivyo na sasa hawapo hapa duniani, utajiri, mali, watoto, vyote hivyo
havikuwasaidia kitu, tukumbuke kuwa vyote hivyo ni mitihani, vilikuwepo, vipo,
na utaviacha,…cha muhimu, ni kuwa mtu mwema tenda mema , kwani kamwe wema hauozi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment