Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, October 2, 2012

Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi-2
‘Mwanangu ni bora tu uende ukaishi na mama yako huyu mdogo, maana maisha ya hapa hutayaweza, kama unavyoona huyu mume wangu ni mlevi kupindukia, na siku zote amekuwa akiniamurisha nikufukuze hapa nyumbani uende kwa baba yako, kwani hataweza kulea mtoto wa mtu mwingine, ambaye sio wa kwake, wakati baba yake yupo, na kama nionavyo watoto wake mwenyewe ni mzigo kwake’hiyo ilikuwa kauli ya mama yangu siku tunaagana.

Kwangu mimi siku hiyo ilikuwa ya furaha, nikiwa na ndoto kichwani kuwa naenda Darisalama, mji ambao sifa zake zimeenea kila kona ya kijiji chetu. Nilijua kuwa ukifika Dar, utapata starehe za kila namna, na nilijua kuwa kila anayeishi mji huo mashuhuri ni tajiri.

‘Mama nitakwenda na mama mdogo, na nikipata pesa nitakuwa nakutumia, ili usiteseke tena, najua huko Dar pesa zipo nyingi’nikamwambia huku nikiwa na furaha tele.Na hata wadogo zangu, watoto wa mama na baba huyo wa kufikia, wakawa wanalilia na wao waondoke hapo.

‘Mwanangu ninakuasa huko Dar, kuna mitihani yake, sio kweli kuwa ukifika huko utapata kila kitu, kama ingelikuwa hivyo wote wanaotokea huko wangelikuwa matajiri, au kila mtu angelikimbilia huko. Cha muhimu mwanangu ukumbuke maisha haya tuliyo nayo, wewe sasa ni mkubwa, ujua jinsi gani ya kujichunga, usije ukapatwa na madhara yaliyonikuta mimi. Nakuasamwanangu, ukaishi vyema na mama yako huyo mdogo, uwe na adabu na umtii, kama mama yako’akasema mama.

‘Mama sasa kwanini sisi tunaishi hivi, kwani baba yangu yupo wapi?’ nikamuuliza swali hilo tena, ingawaje nilikuwa nimeapa moyoni kuwa sitamuuliza swali kama hilo tena, kwani kila nikimuuliza, kilichofuata hapo ni machozi na siku hiyo mama hatakuwa na raha siku nzima. Sijua kwanini na hakupenda kabisa kuniambia.

‘Mwanangu nilishakuambia kuwa  swali hilo silitaki, kwasababu linanitia uchungu, linanikumbusha mbali sana, ..na nisingelipenda kukusimulia machungu ya maisha yangu kwani yatakuumiza tu mwanangu.’akasema mama huku  machazi yakianza kumtiririka usoni.

‘Kwanini mama, nikikuuliza hilo swali unalia, kwani kuna nini kuhusu maisha yako, na baba yangu mzazi, amekufa au yupo hai? Mama mimi sasa ni binti mkubwa na nina haki ya kujua wapi alipo baba yangu au kwanini baba alitutelekeza na sisi kuja kuishi na huyu baba asiye na mapenzi kabisa na mimi, na wewe huna raha kabisa licha ya kuwa unaishi naye?’Nikawa nataka kujua kulikoni, sikujali tena kama mama atalia au vipi, mama akaangalia huku na kule kuhakikisha kuwa baba hayupo karibu.

‘Mwanangu, licha ya kuwa baba yako huyu hana mapenzi na sisi, lakini ndiye aliyeniokoa kipindi ambacho nilikuwa karibu ya kufa. Yeye alijitolea na kuishi na mimi nikiwa magonjwa karibu ya kufa, kipindi hicho ndio nimejifungua wewe. Mwanangu, sipendi kabisa kukusimulia maisha yangu, kwani ni ya uchungu kiasi kwamba hayafai kusimuliwa mtoto kama wewe’akasema mama.

‘Lakini mama mimi sasa sio mtoto, nimeshavunja ungo, na akili yangu ni ya kiutu uzima, na sasa najiandaa na safari ya kwenda mji mkubwa duniani, mji wa Darisalama’nikasema huku nikiwa na furaha.
Mama aliniangalia na machoni kukawa kumeshatanda kiwingu cha machozi, akatulia kwa muda , halafu akasema ;

‘Baba yako nasikia yupo huko Mererani,ni mmoja wa matajiri wa madini, na anaishi na mke wake, na watoto wao,  hanijui tena…‘akasema mama. Na mimi nikaingiwa na hamu ya kumjua huyo baba yangu, kumbe baba ni tajiri , sasa kwanini sisi tuteseke na umasikini, nikajiuliza na kumuuliza mama.

‘Mimi sikuwahi kufunga ndoa na baba yako, ..’akatulia mama kwa muda, huku akiwaza, nahisi alikuwa akivumilia uchungu wa kumbukumbu zilizopita, na baada ya kufikiri kwa muda, ndio akaanza kunisimulia maisha yake yaliyopita ambayo ndiyo yaliyosababisha machungu aliyo nayo.

**********

Mwanangu usijisikie vibaya nikisema hivyo, lakini ndivyo ukweli ulivyo, kuwa kila ninapokuona ninakumbuka machungu yaliyonikuta katika maisha yangu, hata wakati mwingine nakuona kama wewendiye mkosi wamaisha yangu. Samahani sana mwanagu kusema hivyo, hata kama ungelikuwa wewe, ukahisi hivyo. Hizo ni hisia tu mwanangu kutokana na maisha yangu yaliyopita.

Siku mwanangu ulipoingia tumboni kwangu ndipo siku ambayo kila kitu kinachoitwa raha, amani na upendo vilipotoweka kabisa katika maisiha yangu. Ilifikia kipindi nina mimba, nikiiangalia hiyo mimba nakulaani, nikisema sitaki utoke salama, ….unisamehe tu mwanangu ndivyo nilivyokuwa nikiwaza.,

Sikujua haya yote yangelitokea, kwani kipindi hicho nilikuwa mdogo tu, na siku hiyo ambayo nakumbuka ndiyo siku niliyopata hili doa, ilianzia siku ile tulipokuwa tukifurahia  kumaliza darasa la saba , ilikuwa siku tuliyokuwa tukisherehekea kumaliza daras ala saba. Kwangu mimi ilikuwa siku ya pekee sana, kwani ndiyo siku ninaikumbuka sana kuwa ilikuwa mwisho wa maisha yangu ya ubinadamu.

Siku hiyo, mimi na baba yako, yaani huyo baba aliyenipa mimba yao, tulikuwa tumetoka kwenye sherehe ya kumaliza darasa la saba, na siku hiyo tulishajiona tumekuwa na tulikua tukijiita LY, yaani last year. Nilikuwa nimejipamba ipasavyo, na shingoni nimevalisha shada ya maua, nililovikwa na wazazi wangu.

Shuleni nilikuwa na akili sana, hata zawadi ya mwanafunzi bora nilipewa mimi, na hata baba yako huyo ambaye tulikuwa darasa moja alikuwa hanifikii kabisa. Kwahiyo kipindi napewa zawadi yeye alikuwa na wivu wa ndani kwa ndani, licha ya kunipongeza na kujivunia kuwa ana dada mwenye akili.

Mimi na huyo baba yako tulikuwa marafiki sana, toka utotoni hadi kufikia darasa la saba, wengi wasiotujua vyema walizania kuwa sisi ni watoto wa mzazi mmoja, labda sisi ni ndugu, lakini hatukuwa  na udugu wowote. Mimi nilikuwa sioni raha, kama sikumuona baba yako huyo,lazima ili siku ikamilike ni lazima tuonane, kama sio bombani ni wakati tunakwenda shule.

Baba yako huyo alinipenda kiukweli kwani hakupenda kabisa nionewe na mtu yoyote, hata kama nimekosa shuleni na mwalimu anataka kuniadhibu, yeye aliweza kumuomba mwalimu achapwe yeye badili yangu. Na nyumbani kwao wakila chakula tofauti ambacho labda ni kizuri, atanifichia ahakikishe kaniltea kidogo, na ikawa hata mimi nafanya hivyo.

Mwanzoni wengi walijua kuwa ni utoto, tukiwa wakubwa hayo yataisha, lakini haikuwa hivyo,kwani kila umri ulivyozidi kuwa mkubwa ndivyo mapenzi yetu yalivyozidi. Licha ya kuwa moyoni mwetu, hatukuchukulia kama mapenzi ya sasa, ya kiukweli, tuliyachukulia kama mapenzi ya dada na kaka. Mapenzi yasiyotafsiriwa vibaya , na hatukujua zaidi ya kupendana kama kaka na dada  hadi pale tulipofika mwisho wa darasa la saba.

‘Maua unajua mimi nakupenda kweli, naona tukimaliza darasa la saba tuoane kabisa, naogopa utakuja kuolewa na mtu mwingine’akaniambi baba yako huyo.

‘Eti nini tuoane, hivi wewe unajua maana ya kuoana kweli, unaanza kuleta mambo ya dhambi hapa. Na ujue kuwa kuoana ina maana kubwa ,nijuavyo mimi, mkitaka kuoana mnatakiwa mlipe mahari,muwe na nyumba ya kuishi,muwe na pesa ya kujitunza wenyewe, sasa sisi bado wadogo,huoni kuwa unawaza mambo ya kikubwa wakati sisi hatujafikia huko’nikamwambia.

‘Pesa tutatafuta wenyewe, mahari mimi nitatafuta, nitafanya vibarua hadi nitaipata,, sitapenda kabisa nikukose wewe, ni heri nife kuliko kukuona unaolewa na mtu mwingine. Au wewe hunipendi?’ akaniuliza Adam, ndilo jina la baba yako huyo.

‘Mimi nakupenda sana, lakini sikuwa nimewazo huko, nakupenda kama kaka yangu, hata hivyo ni kweli hata mimi sioni raha nisipokuona, na nitasikitika sana kama na wewe utamuoa mtu mwingine badala yangu, sijui nitaishije, lakini tusiwe na haraka ya mambo hayo, tusubiri, kwanza mimi nategemea kufaulu, na kwenda sekondari’nikasema.

‘Ndio hapo naanza kuogopa,maana mimi sina uhakika wa kufaulu, natarajia kuwa mfanyabisahara, na ndoto zangu ni kwenda kuchimba madini Mererani kama alivyo mjomba. Sasa nataka nikiondoka niondoke na wewe,sitapenda wewe uende sekondari, maana ukifaulu, utakwenda kukutana na wasomi wenzako na utakuja kunisahau kabisa’akasema.

‘Adam mimi siwezi kabisa kukusahau, nakupenda kama ninavyoupenda mwili wangu, wewe utaona tu, hata nikifaulu, kama nitakwenda sekondari ya mbali nitakuwa nikikuandikia barua kila siku. ‘nikamwambia.

‘Hapana kama kweli unanipenda lazima tufunge ndoa, ili hata ukiondoka nijue wewe ni mke wangu,’akasema.

‘Hilo haliwezekani, sisi bado wadogo,na hata wazazi wetu wakisikia hayo wataanza kutufikiria vibaya, wao wanajua tunapendana kama kaka na dada, hayo ni mabaya tusiyaongelee …’nikamwambia.

‘Mimi nina wazo moja,…’akaniambia huku akiona aibu

`Wazo gani?’ nikamuuliza.

‘Ili tudumishe mapenzi yetu, inabidi tuwe wapenzi wa kweli, na hili litafanikiwa kama ….’
Basi ushawishi ulianzia hapo, ikawa kila tukikutana na baba yako lazima anishinikize kuwa tufanye mapenzi ya kiutu uzima. Na mimi niliogopa sana nikijua madhara yake, licha ya kuwa nilikuwa nikimpenda sana baba yako huyo na sikupenda kabisa nimuuzi.

Siku matokeo ya mitihani yalipotoka, ndipo siku baba yako huyo aliponishinikiza, na siku hiyo alinichukua hadi kwa jirani mmoja rafiki yake ambaye alikuwa akionyesha kanda za video, na sijui kuwa walipanga iwe hivyo, kwani waliweka mikanda mibaya, ambayo baada ya kuiangalia, nilijikuta nikikubali kufanya alichotaka yeye na hapo nikawa nimeingiza balaa mwilini mwangu, kwani tendo hilo la siku moja, lilikuwa kama sumu mwilini mwangu,

Siku hiyo sitaisahau maana sikutarajia kuwa matokea yake yatakuwa hivyo,.nilipiga ukelele wa maumivu, maumivu ambayo, hayakuishia kuniharibia usichana wangu tu, bali yalikwenda moja kwa moja hadii kuniharibia maisha yangu.

Ujauzito huo uligunduliwa nikiwa shuleni, kidato cha kwanza, wakati huo nimeshafika sekondari, na kilikuwa kipindi cha kupimwa wanafunzi afya zao. Siku hiyo baada ya kupimwa, nilibakai bwenini, nikiwa na wasiwasi, kwani nilishajihisi vibaya, sikuwa na uhakika wa kuwa nina mimba, lakini ile hali yangu ya kuumwa umwa,na kujsikia kichefuchefu, na dalili nilizozisikai kuwa ukiwa hivyo ni dalili za mimba, nikajua tayari.

Mara nikasikia nikiitwa, nikaambiwa naitwa na mwalimu wa utawala, nikajua sasa mambo ndio hayo. Nikafika kwake, na yeye hakuniambia kuwa nina tatizo gani, yeye alichosema ni kuwa, marakwa mara wanapofanya uchunguzi kwa watoto, na kugundua tatizo, huwa inabidi mwalimu akutane na mzazi, kujadili jinsi gani ya kulitatua hilo tatizo’akasema.

‘Mwalimu kwani mimi nina tatizo gani,maana siishi kuumwa?’ nikamuuliza.

‘Ndio jambo tunalotaka kuongea na wazazi wako, tuone tutakusaidia vipi, kwahiyo jiandae, tutaondoka pamoja’akaniambia huyu mwalimu. Mimi moyoni nilijua tu mambo yameshaharibika, na ninavyowajau wazazi wangu, basi tena, ndio nakwenda kuuwawa.

‘Mwalimi mimi siwezi kwenda nyumbani, baba ataniua mwalimu’nikasema huku nikianza kupiga piga miguu chini.Mwalimu akaniangalia, nafikiri alitaka kuniambia nani aliyekutuma kufanya hivyo, lakini akatumia busara ya ualimu, kwa kunificha, kwani sikuambiwa kwanini narudi nyumbani na mwalimu.

‘Kwani wewe una wasiwasi gani, kwani unahisi kitu kitu gani kibaya ulichofanya, ?’ akauliza mwalimu na alipoona nipo kimiya akasema;

‘Mimi nataka kwenda kuonana na wazazi wako ili kuwaelezea hali yako ya kiafya , kama unavyoona akribu kila siku wewe ni mgonjwa, na pia kuongea nao kuhusu matokea yako ya mitihani, usiwe na wasiwasi hao ni wazazi wako hawawezi kukua,kwani kila mzazi ana uchungu na mwanae’akasema mwalimu lakini nilijua anaongea vile kunipa matumaini tu. Kama angelimjua baba yangu asingelisema hivyo.

Mimi nilipanga kumtoroka tukifika njiani, kwani nilijua ukali wa baba yangu, …

NB: Je ilikuwaje

WAZO LA LEO: Jamii njema huanzia kwa watoto, ikiwa na maana kuwa watoto ndio msingi wa familia , watoto ndio msingi jamii,watoto ndio msingi wa taifa. Tukilijua hili, ni vyema tukahakikisha kuwa msingi huu ni imara. Je tufanyeje ili msingi huu uwe imara, ndilo swali analotakiwa kila mzazi kujiuliza.Hii ni dhamana,..tusifurahie tu kupata watoto, lakini tujua jinsi watoto hawo waatishi ile kiwe kizazi bora baadaye.

Ni mimi: emu-three

7 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Nasubiri kusoma ilikuwaje...Nimependa sana wazo la leo hasa hapa "tusifurahie tu kupata watoto, lakini tujue jinsi watoto hao wataishi ili kiwe kizazi bora baadaye".

samira said...

ndio m3 hujambo ,nakujuwa huwezi kutusahau hata iweje upo nasi,nami nafatilia mkasa mpya ,kwani dunia duara inazunguka na hatujuwi mwisho wake
tuombe kheri

emu-three said...

Imekuwaje ndugu inakuja mungu akipenda, nashukuru kuwa tupo sote.

Ndiyo mpendwa Samira kama kawa tupo pamoja,je ww maisha yako hayakuwahi kukutana na mitihani kama hiyo?

Jamani kama kuna ambaye aliwahi kukutana na mitihani kama hii atupe ushahidi ili kisa kikolee utamu.

Karibuni wote kwenye kisa hiki kipya

Shukuru Hamisi said...

Haya hayaa! Tupo pamoja mkuu hatua kwa hatua, mpaka mwisho!

Shukuru Hamisi said...

Tupo pa1 mkuu, hatua kwa hatua mpaka mwisho!

Rachel siwa Isaac said...

Nikweli kabisa Ndugu wa mimi,Wazo limetulia.

Mmmhh Kisa hiki Ndugu wa mimi kina mambo mengi sana yaani kinagusa mno.MUNGU azidi kubariki kazi za mikono yako;Pamoja sanaaaaa!!

Anonymous said...

Gгeat beat ! I ωish to appгentiсe even as
уou аmеnd your web sіte, how can i subscгibe for а blog wеbsite?
The account аided me a apρlicаblе ԁeal.
ӏ have been tiny bіt familіar
of this your broadcаst provideԁ vіbrant clear idea
My website - cincinnati bail bonds