Katika maisha haya, unaweza ukakutwa na majanga na kufikia
hata kukufuru, ukizania wewe tu ndiye unayeonewa, lakini ugumu na matatizo ya
kimaisha yapo katika watu wengi, ila ni kwasababu tu hujawahi kusikia au
kukutana na watu kama hao. Nalisema hili pale nilipokumbuka kisa cha huyu
mwanadada ambaye nilimkuta akiwa kainama upembezoni mwa nyumba huku kashika
shavu na michirizi miwili ya machozi ikiwa imeshajichora mashavuni.
Niliingiwa na huruma nilipoona ule ukaaji aliokuwa kaka huyo
binti, hasa kwa binti mkubwa kama yule, na ile nguo nyepesi aliyovaa asubuhi
kama ile licha ya baridi kali. Pembeni
yake kulikuwa na ndoo ya maji, iliyo tupu. Niliingiwa na moyo wa huruma nikamsogelea
kwa tahadhari, kwani dunia hii haina wema, unaweza ukajitia una huruma, na
huruma hiyo ikakutokea puani.
Wakati namsogelea kwa tahadhari,nilikumbuka kisa cha jamaa
yetu mmoja, ambaye alienda kusota jela, baada ya kujifanya msamarai mwema, kwa
kumoenea huruma binti kama huyu. Yeye alimkuta huyo binti njiani, akiwa analia, na hali aliyomkuta
nayo, ilikuwa ya kusikitisha, kwani kama alivyodai, ana siku mbili , kula hali,
anachoambulia ni makombo. Yule jamaa yangu alipomuona kwenye hiyo hali
akamchukua kwake, lakini kabla
hajatahamaki polisi hawa wapo mlangoni pake.
‘Tumeskilia wewe umemchukua msichana wa watu, umemficha hapa kwako , yupo wapi?’
akaulizwa.
‘Afande, mimi nimemuona huyu binti njiani, akiwa analia, nikajaribu
kumuuliza ana tatizo gani, akawa hanijibu, lakini kwa hali aliyokuwa nayo
ilionyesha dhahiri kuwa ana njaa, nikaona nimchukue kwangu, ili anywe chai,
halafu atanielekeza kwao, au polisi ikibidi, kwani hali aliyokuwa nayo hata
wewe ungelimuonea huruma, inaonyesha wazi ana njaa, na pia mahala kama pale nilipomkuta
hapana usalama’akajitetea huyo jamaa yangu.
Wale maaskari wakaangua kicheko, na kusema;
‘Hivi wewe kweli una akili, ukutane na binti wa watu,tena msichana,
badala ya kwenda naye polsi unampeleka kwako, kwanza wewe una mke, au ndio ulitaka
awe mkeo wa muda baadaye umeshamuharibia maisha yake unamtelekeza!’ akasema
yule askari huku akiangalia huku na kule
kama ataona mke wa jamaa yangu huyo.
‘Mimi ninaye mke, na kwasasa hayupo kaenda kwao, hivi sasa nipo peke yangu, alikwenda kwao kusalimia.’akajitetea
jamaa yangu huyo
‘Kwahiyo ukaona uchukue mwanya huo, kutorosha mabinti za
watu,wewe huoni hilo ni kosa kubwa, linalinganishwana kuteka nyara. Na wewe hujui
kuwa utakuwa na mtoto kama huyo siku za baadaye?
’akasema yule askari huku
akitikisa kichwa na mwenzake akatikisa kichwa kukubaliana naye.
‘Jamani, huyu binti wala sijamtorosha, sivyo kabisa
mnavyozania nyie, kwanza yupo hapo ndani anakunywa chai, hebu ingieni mumuhoji
wenyewe‘akasema na wale maaskari wakaingia ili kuhakikisha, na wakamkuta yule
binti akiwa anakunywa chai, na alipowaona wale maaskari, akakurupuka pale
mezani akitaka kukimbia, wakamshika.
‘Wewe ulikuwa wapi muda wote huo, ulikuwa na huyu muhuni,
ndiyo yeye anayekuhadaa kila siku ehe, utatumabie vyema?’akasema yule askari
huku kamkazia macho yule binti.
‘Naogopa..hapana, niliku….njiani’akawa anasema yule binti
akiwa na wasiwasi. Baadaye walikuja walezi wa huyo binti na kusema kuwa huyo
ndiye binti yaoo wanayemtafuta , na mtego wao umeshagundua kuwa huyo jamaa
yangu ndiye anayemuhadaa huyo binti, na
walikuwa hawajajua kuwa ni nani.
‘Lakini mimi ni mara yangu ya kwanza kukutana na huyo
binti’akajitetea jamaa yangu huyo.
‘Wote Huwa wanasema hivyohivyo, utuambie ukweli maana
tuliamua kumwekea mtego, kwani tabia zake zimebadilika siku hizi, …’akasema
baba mlezi.
‘Unajua huyu binti alianza kubadilika ghafla, ukimtuma dukani
au sokoni anakawia kurudi, na tukienda kazini tukirudi hakuna kilichofanyika,
tukasikia kwa majirani kuwa kuna mwanaume anaonekana akiwa naye mara kwa mara,
basi tukaona tuweke mtego, na leo umenaswa…kumbe ndio wewe, sasa utumabie
ukweli,mtu mzima kama wewe huna haya kutembea na mabinti wadogo kama hawa …’akasema
mama ambaye kumbe ni mama anayeishi na huyo binti kama mama mlezi.
‘Lakini muulizeni mwenyewe huyo binti, kwanini
mnanishinikiza mimi kuwa nimemtorosha, wakati mwenyewe yupo hapa anaweza
kujielezea, jinsi ilivyokuwa, nakuomba tafadhali wewe mama usikashifu, mimi
siwezi kutembea na huyo binti’akajitetea huyo jamaa na yule binti alikuwa
kainama chini akionyesha aibu na kuogopa.
‘Tumuulize mara ngapi, kwani ukimuuliza anasema ukweli, yeye
ukimtuma mahali iwe dukani au sokoni, akichelewa, au akifanya kosa, ukimuuliza yupo
kama bubu, hivyo hivyo unavymuona, ainaimana chini akama anatunga sheria zake,
hasemi kitu, akini akiwa na wenzake, huwezi amini, au akikutana na wavulana, ni
muongeaji hodari, ngoja mfike, anakuwa kama hajui kuongea, ‘akasema huyo mama.
Mabishani hayo hayakusaidia kitu, na hakuna kilichokubalika
hapo, ikibidi jamaa yetu huyo, akakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi, huko
jamaa kama unavyowajua walianza kumtesa huyo jamaa eti asema ukweli, mateso
ambayo yalimuathiri sana, na ilibidi asema uwongo kukubali tu , ili asiendelee
kuumizwa.
‘Ilibidi nikubali tu, maana mateso yalikuwa makubwa, hata
sasa hivi ubavuni nina maumivu makali, ’akajitetea
Raia wema majirani wanaomjua huyo jamaa waliposikia ikabidi
wafike kituo cha polisi kwenda kumtetea,
na baadaye hyo binti aliitwa na mkuu wa kile kituo ili ahojiwe vyema. Yule
binti aliulizwa, akasema ilivyokuwa, lakini walezi wa huyo binti walisema huyo
binti sio mkweli, kwani mara nyingi akifanya kosa hukana, na kusema uwongo hadi
ukweli ukidhirika, ndipo anajikanyaga.
‘Sasa nyie mna uhakika gani kuwa huyu mwanaume ndiye huyo
anayemuhadaa huyu binti yenu?’ akauliza mkuu wa kituo.
‘Ni baada ya kuweka huu mtego, ndio tumemnasa huyu jamaa,atakuwa
ni yeye tu, kwani wanaume wana maana’akasema mama mlezi.
Baadaye ya siku mbili jamaa akaachiwa kwa dhamana,huku akiwa
kateswa, kadhalilika kwa huruma yake.
Mke wa jamaa huyu aliporudi akayasikia hayo yaliyomkuta mume
wake, na siku kabla hajaondoka, alishasikia kwa watu kuwa mume wake hajautulia,
na alipomuhoji mume wake, alikana kabisa, na leo hii kasikia jambo kama hilo,
akajua kweli kumbe mume wake ana tabia za namna, hiyo.
‘Kama ni hivyo, mimi wala sikai hapa, narudi kwetu, kwani
huko ninaye baba na mama na kuna wanaume wengi tu walikuwa wakinihitaji, na
hata leo naweza kuolewa, nenda kwa hawo mabinti wa mitaani unaowataka’akasema mke wake huku akijiandaa
kuondoka.
‘Mke wangu sio kweli, hayo waliyosema watu ni uwingo, ni
fitina za watu, mimi sina tabia hiyo kabisa, hata kama ni kuapa naweza , twende
tukaapishwe kwa watu wa dini, mimi nipo tayari’akasema lakini haikuwa rahisi
keshi yake mke wake akarudi kwao, na ilibidi asubiri kesi hiyo ya huyo binti
iishe ndio aende nyumbani kwa huyo mkewe wakasuluhishwe.
‘Huyu jamaa kasingiziwa, mimi namfahamu sana, kwani nafanya
akzi naye, kuna mabinti wanamtaka huyu jamaa, na kwa msimamo wake ulivyo,
wakaona dawa ni kumpakazia ubaya. Sasa ukiongezea na hili, ndio wamezidi
kumtangaza kwa kusema; `Sasa mnaoana anajifanya msafi kipo wapi, na bado...mpaka
akome ubishi, mjini hapa’
Basi watu ikabidi wamshauriu huyu jamaa, ili awahi kuikoa
ndoa yake, ni bora akaongee na walezi wa huyo binti,;
‘Ukiongea na walezi wa huyo binti, yataisha kienyeji, kwani
wao bado hawana uhakika kuwa kweli wewe ndiye unayemuhadaa binti yao, ukamaliza
nao, waatenda kuifuta hiyo kesi huko polisi, kama ujuavyo kesi
kifika huko polisi ina utaratibu wake, na nimesikia wakisema kuwa kesi hiyo
wataifikisha mahakamani, kwani matendo kama hayo yanazidi kila siku, inatakiwa
kutolewa adhabu kali kama fundisho’akasema jamaa mmoja.
‘Mimi nipo tayari kwenda huko mahakamani, hata nikifungwa
nifungwe tu, lakini siwezi kukubali jambo ambalo sijalifanya,na tutaongea nini
na hawo walezi wa huyo binti, wakati wameshashikilia kuwa mimi ni mkosaji,
yaaani huruma yangu ndiyo inaniponza’ akasema huyu jamaa kwa sauti ya huzuni.
‘Hapo huna jinsi ni vyema ukajishusha, na kwenda kuongea na
hawo wazazi,maana hata kama ingelikuwa ni wewe binti yako kakutwa hivyo,
usingelikubali, moja kwa moja ungelifikiria hivyo, sisi tupoo na wewe
tutakutetea’ wakasema wenzake wanaomjau vyema.
********
Basi nilipokumbuka hilo tukio, nikawa na tahadhari ya kuongea
na huyu binti, hata hivyo moyo wa huruma ulinituma angalau nimuulize huyu binti ni nini
kilichomsibu asubuhi kama ile yupo upenuni mwa nyumba huku akiwa kavaa nguo ambazo
baridi ilikuwa ikimpenya bila ya huruma, akiwa analia.Mimi kama mzazi moyo wa
huruma uliniingia nikiwaza mbali, kuwa haya yanaweza kutokea kwa mtoto wa
yoyote yule na lililojema ni kusaidiana. Ukiwa mzazi hisi akama hizi zitakujia
tu, kwani uchungu wa mwana anayeujua
vyema ni mzazi.
‘Habari yako binti?’ nikamsaili na akawa kama kashituka aliposikia
sauti yangu na kitu cha kwanza alichofanya nikujiweka vyema.
‘Sija-shikamoo..’akainuka pale na kusimama huku akisalimia
kwa kigugumizi akaishika ile ndoo na kuangalia huku na kule.
‘Samahani nilikuwa napita tu, bahati nikakukuta ukiwa katika
hiyo hali, kwanini upo hivi na asubuhi hii, na jinsi ulivyovaa, huoni kuwa
unaweza kuumwa na magonjwa ya ubaridi?’ nikamuuliza.
‘Kama nikuumwa nimeshaumwa sana, na taabu niliyo nayo
anayejua ni mungu, iliyobakia ni siku ifike roho yangu itolewe tu, ili
nikapumzike huko ahera, ingawaje sijui kuwa kuna kumpumzika huko mbeleni lakini
naona ni heri tu nijifie…na ipo siku tu, nitaamua moja, maana nimechoka,kwanini
mimi…’akasema huku machozi yakimtoka.
‘Kwanini uwaze hivyo,hujui kujiua ni dhambi, ni sawa na kuua
mtu’nikasema nikiwa nahisi kuwa anaweza kweli akafanya hivyo.
‘Mungu ndiye anyejua
ni kwanini nawaza hivyo, kwani hakuna ambaye nitamsimulia matatizo niliyo nayo
akanielewa, hakuna atakayejua jinsi gani ninavyoteseka, na ninaendeela kuteseka,
hakuna anayejali, …. Ina maana mimi nilizaliwa katika dunia hii ili nije
kuteseka, hapana,….labda sistahili kuishi’akasema huku akifuta machozi.
‘Kwani wazazi wako wapo wapi?’ nikamuuliza.
‘Wazazi wangu..?, sijui wapo wapi, baba keshaoa mke
mwingine, mama naye kaolewa na mume mwingine, na….ooh, Lakini yote maisha,
kwani hata hivyo siwezi kuwalaumu sana, kwani hayo yaliyotokea huko nyuma huenda
hawakuyatarajia, lakini adhabu naipata mimi‘akasema na kuniacha nikiwa na
maswali mengi kichwani.
‘Kwani hapa unaishi na nani,?’ nikauliza.
‘Nimechukuliwa na huyu mama , ni ndugu tu, wa karibu,
alinichukua akidai atanilea na hata kunisomesha, lakini tangu nije kwake ni
mwaka wa tatu sasa, sijui cha kusoma wala nini, nimegeuka kuwa mfanyakazi wake
wa ndani, aheri angeliniacah tu kule kijijini nikaishi kama alivyonikiuta’akasema.
‘Ohh, kama mfanyaakzi wa nyumbani, ina maana anakulipa mshahara?’
nikamuuliza.
‘Hahaha, anilipe mshahara, yeye anadai kuwa nakula chakuala
chake cha bure, na nalala kwake bure, gharama yake ni kubwa kuliko huo
mshahara’akasema.
‘Sasa kwani huna jinsi ya kukutana na wazazi wako ukawaambia
maisha unayoishi, kama inawezekana ukaishi na mmoja wa wazazi wako, kwani wao
ndio watakuwa na uchungu na wewe kuliko huyu mtu baki, wao ndio watakuwa na
uchungu na wewe kama wazazi?’nikamuuliza.
‘Hayo mengine tena, hujui jinsi gani wazazi wangu hawo walivyokuwa,
siku ile kiumbe mimi nilipoingia tumboni mwa mama yangu, …huenda mimi
naadhibiwa kwasababu yao, na hapa nilipo nahisi hakuna kati yao anayenihitaji
tena,kwani kila wakiniona hasa mama, huwa anaishia kulia, akikumbuka machungu
yalimkuta.
Ama kwa baba naye sijui anawaza nini, maana keshaoa mke wake, mkewe ni mbaya kuliko hata huyu ninayesihai naye hapa,
nakumbuka siku moja nilikwenda kuwatembelea akasema waziwazi kuwa yeye hajaza,
kwani kipindi hicho alikuwa hajapata mtoto, alisema yeye hataki kuishii na
mtoto ambaye sio wake..’akasema na kuinama chini na mara sauti ikatoka ndani
‘Wewe Maua unafanya ninii huko nje, hujui nachelewa kazini,
umenishanileta maji nataka kuoga niondoke, na hizo nguo nikija nizikute hapo
hapo, utazifua kwa mate yako …na vyombo hivyo, vyote usafishe, na huyu mdogo
wako hakikisha umemnyoshea nguo zake, atachelewa shule……?’ sauti ya mwanamke
ikaita toka ndani, na yule binti alikurupuka utafikiri kasikia sauti ya nani,
nikabakia nimeduwaa.
Kwakweli nikawa na hamu kubwa ya kutaka kujua historia ya
huyo mtoto, naifuatilia kwa karibu tuzidi kuwemo ili tuweze kuisikia.
NB: Hiki ni kisa kingine, sijajua kitakuwa na ukubwa gani,
ambacho kina ujumbe maalumu, hasa kwa jamii yetu hii. Naombeni tuwe pamoja .
WAZO LA LEO: Ujumbe kwa vijana wetu na wale ambao hawajaingia kwenye ndoa: Tusiwe
wepesi kukimbilia tamaa za kimwili, tukishajiona tumependana, kwanza tujenge tabia ya kutafakari matokeo
ya hilo tendo. Tujiulize Je tumeshajiandaa na hayo matokeo, je kweli ni sahihi kwa muda huo, Je likitokea lolote tutafanyaje, tusiwe wepesi wa kukidhi
mataminio ya nafsi zetu, kwani majuto huja baada ya kitendo, na majuto ni mjukuu.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Duh! nimesoma hiki kisa huku machozi yakinitiririka kama huyo mtoto..kuna mambo mengi nimeyakumbuka...ni kweli katika maisha watu tusiwe wapesi kama wazo lisemavyo...kwa vile wanaoteseka ni watoto/wengine...FIKIRI KWANZA NA BAADAE TENDA.
Post a Comment