‘Baba Maua hapa nilipo moyo wangu haunitulii, nahisi kama
tutapokea taarifa mbaya’akasema mama Maua, huku akiwa kashikilia shavu.Mumewe
akamwangalia kwa muda huku akiwa ananoa panga lake.
‘Hizo hisia zako mimi sizitaki, kwanini uwe unajipa
wasiwasi, kabla ya jambo, huoni unajiumiza mapema, hata kama jambo hilo
litatokea, kwanini usilisubiri kwanza, cha muhimu ni kukubali kuwa kila jambo
kama limepangwa kutokea litatokea tu, jambo jema ni kulisubiri, ‘akasema.
‘Mimi namuwaza mwanagu huko shuleni, kwani taarifa hizo za
mara kwa mara kuwa anaumwa, na hadi kufikia kudondoka mara mbili na hata kupoteza
fahamu zinanitia wasiwasi sana’akasema mama mtu.
‘Lakini kule yupo shuleni, yupo na wasomi, walimu wao
wanajua jema na baya kwa watoto, wanajua kulea hata kuloko wewe mzazi, na pia ukumbuke
kuwa shule yao ipo karibu na hospitali kubwa ya wilaya, kwahiyo akizidiwa
atapelekwa hukohospitalini, mimi hilo halinitii wasiwasi sana, labda kaam kuna
jingine’akasema baba mtu.
‘Tatizo lenu wanaume, hamjui uchungu wa mtoto, sisi wanawake
kwa vile tulibeba ile mimba miezi tisa na kupambana na machungu ya kuzaa, huwa
kila ukiwa na wasiwasi na mtoto wako yale machungu ya uzazi unayahisi mwilini, ndio maana wanasema uchungu wa mwana aujue
ni mzazi’akasema mama.
‘Lakini hapo uelewe
kuwa mzazi ina maana baba na mama,
kwasababu wakati upo kwenye uchungu na mimi huwa nakuwa kwenye uchungu pia japo
ni wa kimawazo, nakuwazia wewe afya yako, na kuwazia wewe uzima wako, na hatima
yake. Wewe huwezi jua jinsi gani tunavyojihisi wanaume pale mnapokuwa kwenye
uchungu, sio kwamba kwa vile sisi hatubebi mimba ndio hatuhisi huo uchungu au
kubeba mimba tumboni miezi sita ndio hatuna hisia ya watoto wetu,tunayo huenda
hata zaidi ya nyie’akasema baba mtu.
‘Mimi kwa kweli namuwaza sana mtoto wetu, kama hatutapa
taarifa nyingine inabidi kwenda huko kusikia nini kinaendelea’akasema mama huku
akiinuka na kuweka vyombo vyake sawa, na baadaye akaingia ndani, na mumewe
akamfuata, akitaka waliongelee hilo swala
vyema, kwani alishahisi kuwa huenda kuna jambo mke wake aanamficha.
‘Sawa mimi nitakwena kujua nini kinaendelea hatuwezi
kuondoka sote, wewe utabakia na nyumba na mifugo, inabidi nikajue kuna nini, na
kwanini mtoto wetu ashikwe na maradhi kama hayo wakati alikuwa hata tatizo kama
hilo kabla’akasema baba mtu. Na mama akatulia kwa muda bila kusema neno, na
mumewe akamkazi macho na kusema;.
‘Au una mawazo gani, maana ulivyotulia unanipa wasiwasi, na
maneno yako kuwa wanawake ndio wana uchungu sana yananipa wasiwasi, usije ukawa
unajua nini kinachimsumbua mtoto wetu, halafu hutaki kuniambia’akasema baba mtu
akizidi kumkazi macho mke wake,ambaye alikuwa kainama chini.
‘Mume wangu ningelijua nisingelikuwa na wasiwasi huu
hapa,kama ulivyo wewe ndivyo nilivyo mimi, ningelijuaje wakati mtoto yupo
shule, lini mimi nilikwenda huko shuleni’akasema mama mtu
Mke wake akainua kichwa kumwangalia mume we, na moyoni akawa
anahisi uwoga,uwoga ambao ulimtinga baada ya kusikia kuwa mtoto wao amedondoka
mara mblli huko shuleni na kupoteza fahamu, na
amekuwa akindamwa na homa za mara kwa mara, moyoni alishaanza kuhisi
jambo jingine, ingawaje alijipa moyo kuwa huenda ni hisia tu.
‘Hizi sio dalili za uja uzito kweli?’ akawa anajiuliza
akilini, akainama chini akiwaza, na hapo hakutaka kumwangalia mumewe machoni,
kwani mumewe akimwangali tu machoni, huwa ni mwepsi kugundua nini unachokiwaza,
na mara nyingi alikuwa anaona ajabu kweli, jinsi gani mumewe alivyokuwa na
ujuzi wa kumgundua nini anachokiwaza.
‘Mume wangu wewe una nyota ya uganga, ungelikuwa na tamaa,
ungeshajiingiza kwenye mambo ya uganga wa kienyeji, maana ukimwangali mtu
machoni, unagundua kuwa anawaza nini, na hukosei ,unajuaje?’ siku moja
alimuuliza.
‘Babu yangu alikuwa mtaalamu wa kijiji, enzi hizo, huenda
nimerithi toka kwake, ila mimi mambo hayo siyataki’akamwambia.
Basi ili kuhakikisha kuwa mumewe hagundui nini anachokiwaza,
akawa anajitahidi kumkwepa ili wasiangaliane, na huku kichwani akiwa katingwa
na mawazo mengi, akajisemea moyoni;
‘Mungu wangu kama ni ujauzito mbona itakuwa ni
balaa,…..sijui kutakuwa na usalama gani hapa nyumbani, nimjuavyo mum e wangu,
hatakuwa na subira, ni bora kama ni mimba nitafute njia za kuondoka hapa
nyumbani mapema, nikajifiche mahali hadi hasira zake zipoe,na sijui huyo binti
atakwenda kuishi wapi….hili ndilo linanifanya nisiwe na amani’akajisema
moyoni, akikumbka jinsi mume wake alivyompiga dada yake wa tumbo moja karibu ya
kumuua pale alipogundulika kapata mimba kabla ya ndoa.
Mume wake anasifika hapo kijijini kwa hasira za haraka , na
akipandwa na hasira hakuna anayeweza kumuingia. Huwa akikasirika anakuwa kama
mnyama, na watu wote humkimbia, kwani anaweza kuua, alishafungwa kwa kosa la
kuua, ingawaje baadaye iligunduka kuwa mwenzake ndiye aliyesabaisha hadi yote
hayo yakatokea, na baada ya kutumikia miaka kadhaa jela akatolewa kwa msamaha
wa raisi.
Ilikuwa ni kosa la utani, wakati wanamgombea yeye kama mke
mtarajiwa, na huyo rafiki yake, akasema kuwa yeye ni mwanaume zaidi ya
mwenzake, ukazuka ugomvi, ugomvi ulisababisha mapigano ya hali ya juu, ni nani
zaidi ambaye anaweza kumuoa yeye. Mapigano hayo yaliweza hata kuingiza vita vya
familia mbili, hapo ndipp kijiji kikamjua huyu mtu kuwa akipandwa na hasira
anakuwa kama simba. Aliweza kupambana na mgambo kumi wa kijiji na wote
akawatupa chini kama takataka, na hakuna aliyeweza kumsogelea. Huyu mtu alipambana
na Simba peke yake na kumuua.
Siku dada yake alipogundulikana kuwa kapata ujauzito na
aliyempa mimba hiyo ni mtu ambaye hakutakiwa amuoe, kaka mtu alitoka hapo mbio
hadi kwenye hiyo familia ya huyo mwanaume na kuanza kumpiga huyo mwanaume, hata ndugu za
hiyo familia ilipoingilia haikuweza kumshinda nguvu,…aliwasambaratisha wote,
ikabidi waite polisi, na hata polisi walipofika walishindwa kumkkamata, hadi
wlipotumia risani za moto na kumjeruhi, na kupoteza fahamu kwa siku mbili.
‘Huyu mtu bwana akiongea huwezi jua kuwa ana hasira za kuua
mtu, huwezi kabisa kumfikiria hivyo, ole wako akasirika, anabadilika kabisa,
anakuwa sio yeye tena, ana hitilafu fulani kwenye ubongo wake, ni kama kichaa, lakini hakitokei mpaka akasirika, hiki ni cha kurithi, hakitibiki, cha muhimu huyu mtu msije mkamkasirisha’alisema mmoja wa madakitari, waliokuja kumpima huyu mtu kipindi alipoumizwa kwa risasi.
Mkewe anamjua vyema mume wake, ndio maana kila mara akiwaza kuhusu
mtoto wake,aliombea mungu isije ikawa ni mambo ya uja uzito. Lakini hilo
hakulipa uzito sana, kwani anamjua vyema mtoto wake, walijitahidi sana kumlea
katika maadili mema, na moyo hakutarajia kuwa anaweza kujiingiza kwenye
mahusiano ya kimapenzi, na hata siku anaondoka walimtahadharisha na mambo kama
hayo na yeye aliahidi kuwa kamwe hata danganyika, sasa ni nani kamdanganya, au
ni hisia zake tu.
‘Haiwezani, haiwezekani, mungu niepushia na haya mawazo
mabaya kwa mtoto wangu’akasema mama mtu.Mama mtu alishituka pale mumewe
alipomshika bega, na kusema;
‘Hebu niambie kama unahisia zozote kuhusu mtoto wetu,
unahisi anasumbuliwa na nini, au kakumbwa na mashetani’akasema baba mtu
akijaribu kupata nafasi ya kumuangalia mkewe machoni, lakini mkewe alilijua
hilo akajifanya anashughulika, ilimradi mumewe asimwangalia machoni.
‘Hapana mtoto wetu hawezi kukumbwa na vitu kama hivyo,
nahisi kuna tatizo jingine’akasema mama mtu.
‘Tatizo gani, mbona huniweki wazi, ….usije ukawa unalijua
hilo tatizo na mimi huniambii, nakuomba tafadhali, kama kuna tatizo uniambie
mapema, maana mimi sitakuwa na msamaha, sitakuwa na msamhana, narudia tena,
mimi sitakuwa na msamaha, kama ni tatizo kama lile la shngazi yake, na ole wake
ije itokee kuwa ni mambo yenu nyie wanawake ya kudanagnyika na wanaume, sijui
itakuwaje, sitapenda nimuone huyo binti kwenye nyumba yangu,….hilo naliweka
wazi kwako’akasema mumewe ka hasira.
‘Baba Maua unaongea kitu gani, huyo ni binti yako, na kama
likitokea jambo kama hilo tunatakiwa tuwe na subira, tujue jinsi gani ya
kumsaidia’akasema mama mtu.
‘Unaona….mimi nilishahisi kuwa una jambo unalijua na hutaki
kuniambia, ndio maana unaongea hivyo, hutaki hata kuniangalia machoni, nakuapia
kuwa kama ni hilo tatizo huyo binti asikanyage hapa nyumbani kwangu. Sitaki
kabisa huo mkosi hapa nyumbani kwangu. Mtoto wa kwanza anizalie kihuni,
haiwezekani, hilo kwenye family ayetu ni mwiko’akasema huku akishika kiuno.
Baba Maua usiseme hivyo, kumbuka huyo n binti yetu’akasema
mkewe sasa akihisi miguu ikimwishia nguvu.
‘Najua huyo ni mtoto wetu, lakini katu sitakubaliana na
uchafu huo, unajau kwenye familia yetu toka enzi za mababu, haijawahi kutokea
hilo, aliyekuja kuharibu ni huyo dada yangu,na kiutaratibu alitakiwa ama
auwawe, au afukuzwe kabisa kwenye familia yetu,watu wakalikumbati hilo,na
matokea yake ni kuwa ni lazima litakuja kujitokeza tena, sasa sitaki lijitokeze
tena kwenye family yetu, hasa ya kwangu’akasema huku akigonga ukuta kwa ngumi.
‘Hiyo ilikuwa zamani, kumbuka hizki kizazi cha sasa hivi
kina mitihani mingi, mtu anaweza akabakwa,au akaingizwe kwenye vishawishi
ambavyo atashindwa kuvumilia’akasema mama, na mumewe akamwangali mkewe kwa
macho ya kutisha, akasema;
‘Mimi ,labda isiwe ni mimi, ikitokea hivyo, unavyowaza wewe,
….nitahakikisha naichachana hiyo mimba yake kwa mikono yang,hadi hicho kiumbe
kitoke humo tumboni, na nitahakikisha huyo aliyempa hiyo mimba anakitafuna
hicho kiumbe na kukimeza…..naomba isje ikawa hivyo, maana sijui..mungu wangu,
naomba sije ikawa hivyo, maana ndoto za kuua zinaniandama…’akasema na kuanza
kuondoka huku akihema kama samba, na kabla hajaugusa mlango kuufungua mara wakasikia
hodi toka nje.
Mama akasimama kwa wasiwasi, na kumwangalia mumewe na mumewe
akaangalia ule mlango , halafu akamwangalia mkewe, akasikiliza ni sauti ya
nani, utafikiri ni usiku wakiwa na wasiwasi
wa mgongaji, lakini ilikuwa mchana wa saa nane, hisia zikawa
zimegongana, kuna mtu na mtu huyo anataarifa zisizo njema;
‘Hodi hapa wenyewe , mimi ni mwalimu….’ile sauti ilipopenya
masikioni mwa mama, ilikuwa kama mtu akamzaba kofi masikioni , na kuziba
masikio yake, kichwa kikatanda ukungu, akahisi mwili ukimuishia nguvu.
Mama akaanza kutetemeka, akahisi damu ikimwenda mbio,
shinikizo likaanza kupanda, na mara akashikwa na kizunguzungu, na kabla
hajasema karibu akadondoka chini, baba mtu akawa kaduwaa,
macho yakamfunguka kama vile kaona kitu cha kutisha, akainama
kumwangalia mkewe, akageuza kichwa na kungalai pale alipoweka panga lake, na
kabala hajatulia mlango ukafunguliwa……
NB Hebu niambie kama wewe ungelikuwepo hapo ungelifanya
nini, sijui kulitokea nini, naomba tuvute subira.
WAZO
LA LEO:
Tahadhari ya jambo lolote ni bora, kuliko kusubiri litokee jambo, Kama kuna
njia ya kujihami, kama kuna uwezekano wa kujikinga, ni bora tukachukua
tahadhari ya kujikinga. Tusiwe wepesi w akuzarau, eti litakuja na litazoeleka,
eti, ni tamaa, zinaweza zikazuilika. Tujue kuwa biandamu tonatofautiana, hulka
tabia na uvumilivu. Tusicheze na maisha yetu ,tusicheze na afya zetu, …Wahenga
walisema, kinga ni bora kuliko tiba
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
My bгοthеr suggested I might
like this website. Ηe wаs entirely right. Thіs post truly madе my dаy.
You cann't imagine just how much time I had spent for this info! Thanks!
Here is my web site :: quick loans
Kama unaangalia muvie, napenda weye!
Post a Comment