Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, October 16, 2012

Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi-10 Nikawa naandamwa na maumivu ya kichwa, na hata kuwa napoteza fahamu mara kwa mara, au kuweweseka usiku,nahisi ni kutokana na zile fimbo alizonipiga nazo mama yangu wa kambo,ingawaje yeye alikataa kuhusu hilo.Na ikizingatiwa kuwa mama yangu alishaondoka,basi hakuna aliyekuwa akijali sana na baba likuwa akiondoka asubuhi sana na kurudi usiku na wakati mwingine analala huko huko.
Akirudi haambiwi ukweli, anaambiwa kuwa nimekuwa kama mtu aliyekumbwa na mashetani.

Nilikuja kuhadithiwa kuwa mama yangu aliondoka siku baadaye , baada ya kuhakikisha kuwa nimezindukana, na kwa vile alishapigana na mwenzake, na mwenzake akalifikisha hilo kwa wazee, kuwa kapigwa na mama hata kumsababishia ubovu kwenye tumbo wakati yeye ni mja mzito. Ikabidi baba amfukuze mama haraka nyumbani kwake.

Mimi niliposkia hivyo, nikaanza kulia, nikijua kuwa mama akiondoka nitakuwa katika maisha magumu, hasa kutoka kwa yule mama, basi nikawa namlilia mama, na mama akamuomba sana baba niondoke naye, hata kumpigia mgoti,akisema;

‘Nakuomba sana nipo chini ya miguu yako, nakuomba niondoke na mwanangu, maana simwamini huyu mke wako. Siwezi kuondoka, kumuachia mke wako, mwanangu,unaona jinsi gani alivyomfanya ,mkeo hana huruma kwa mtoto wangu,angalia jinsi alivyompiga, anapiga kama anaua nyoka’akasema mama.

‘Hapa utaondoka wewe mwenyewe, mmaana ukikaa hapa utaniuliwa mke,huoni ulivyomfanya, karibu apoteze uzazi wake’akasema mbele ya wazee ambao waliitwa kusuluhisha.

Baada yamaongezi marafu, ikakubaliwa mama aondoke, maana mimi nilishafkisha umri wa miaka mitatu na nusu, na kwa vile mama alishapewa talaka hakustahili kubakai hapo tena, na hakuwa na mamlaka na mimi.

‘Mama yaani unataka kuniacha, mimi sikubali kubakia hapa, nitaondoka na wewe, mama usiniache hapa nitauliwa na huyo mama wa kambo ’nikamwambia mama yangu.

‘Mwanangu inabidi ubakia na baba yako, ndio utaratibu ulivyo, unachotakiwa ni kuwa mtoto mwema tu, na mungu atakulinda, na kama ukionewa mwambie baba yako yeye ndiye mwenye mamlaka na wewe, hata hivyo baba yako sio mtu mbaya, ubaya upo kwa huyo mke wake, namjua sana’akasema mama.

‘Hapana mama mimi sitaki kubakia peke yangu na hawa watu wataniua, kila siku unaona yule mama anavyonifanya, hanipendi kabisa ‘nikawa nalia, lakini haikuasaidia kitu kwani mama asubuhi na mapema nikiwa bado nimelala ,akaondoka, hakutaka kuniamusha maana alijua kuwa ningelikuwa macho nisingelikubali kubakia.

‘Wewe chokoraa bado umelala, unafikiri upo hapa kwa ajili ya kulala, mama yako hayupo keshakuacha, sasa ujue kuwa utazifanya kazi ambazo mama yako alikwua akizifanya, siwezi kukufulia nguo, au kukuhangaika, amuka anza kufagia na usafishe vyombo’nikaamusha asubuhi na mapema. Na hayo yalikuwa maagizo ambayo yalikuja kuwa kazi zangu za kila siku.

Mimi licha ya udogo wangu kiumri, lakini niliweza kufanya kazi zote, mama yangu tulipokuwa naye alikuwa akinifundisha kidogo kidogo, huwa aliniasa kuwa niwe mchapakazi, na nijitahidi kujua kila kazi, kwani kuna leo na kesho. Watu walimshangaa kwanini alikuwa akinifundisha kazi wakati bado nina umri mdogo. Yeye aliwaambia ni bora anifanyie hivyo, ili nisije nikapata taabu baadaye.

Kwakweli juhudu za mama zilinisaidia sana,kwani hata mama huyo aliponiambia nifenye hizo kazi, alijua kuwa nimefundishwa , nilijua kuosha vyombo, kufagia na kazi nyingi za nyumbani, na watu wengi walinishangaa sana, maana nilijua kazi nyingi kama mtu mzima, na huyo mama ndio akapatia nafasi ya kunifanya mimi mfanyakazi wake.

Mimi sikujali maana nilipenda kufanya kazi, kilichoniumiza ni kule kusimangwa, kwasababu ya umri wangu, hata kama nilijua kuzifaya hizo kazi, lakini nisingelikuwa na uwezo wa haraka kama mtu mzima, basi ikawa ni tatizo, mara nyingi anakuwa nyuma yangu na fimbo. Hali hiyo ilinipa shida sana nikawa nafanya vitu kwa kuogopa, kinyume na alipokuwepo mama yangu.

Kila mara nilikuwa nikimkumbuka mama, na kujiona mkiwa,nikawa nalia huku nafanya kazi, na wakati mwingine walikuwa hawanipi chakula, napika mimi, lakini mwisho wa siku nambulia kuonja tu, lakini hilo halikunipa shida sana, nilipowajulia tabia zao,  maana mimi ndiye mpishi wao, niliweza kula kidogo kidogo, licha ya kuwa mama yangu mzazi alinifundisha kuwa ukipika usiwe unapenda kulia jikoni..

‘Baba , mbona mama ananifanyisha kazi mimi peke yangu, wakati wenzangu wapo hawafanyi kazi, mimi naamushwa asubuhi sana na kufanya kazi zote za nyumbani, wakati mwingina hata shuleni nachelewa au naambiwa nisiende kabisa’ siku hiyo nikamwambia baba. Baba akamuita mama nakumuuliza kwanini ananifanyia hivyo, na mama akakataa katakata akisema yeye kazi zote anafanya yeye, mimi nasingizia tu , kwasababu sitaki kutumwa kazi ndogo ndogo.

Baba hakuwa mjinga akaanza kuchunguza na kweli akagundua hilo, na alianza kumfokea mama , na kila ikitokea hivyo, baba akiondoka tu nafuatwa kwa fimbo, na kuandamwa kwa kazi, ikawa nipo kwenye hali ngumu sana. Hali yangu kiafya ikawa inazorota, na hata mahudhuria ya darsani yalikua mabovu, kwani hata nikifika shuleni wakati mwingine najikuta nimechoka sana, lakini nilikuwa na akili ya ajabu, mitihani nilikuwa nafanay vizuri.

Sikupenda kulalamika kwa baab tena. Nikawa najifanyia kazi zote, ili tu nisikosane na huyo mama, lakini huyo mama hakuwa na jema, bdo alikuwa akiniandama kwa masimango, na sasa akawa ananisingizia mambo ya uwongo, kikiharibika kitu au kupotea kitu nasingiziwa mimi. Nilijitetea sana , lakini walivyokuwa wakifanya ilimfanya baba aamini kuwa eti mimi ni mdokozi.

Siku mbili walinitegea pesa za baba, kwani mara nyingi baba akirudi kuna sehemu yake maalumu anaweka pesa zake, siku hiyo aliporudi akakuta pesa zake zimepungua, akaanza kuuliza ni nani kachukua pesa zake, na kwa haraka mama akasema huenda ni mimi akisema bila aibu;

‘Labda ni huyo binti yako mdokozi’akasema mama akiniangalia kwa jicho lachuki.

‘Huo udokozi kauanza lini, ?’ baba akauliza na mama akamwambia ndio tabia yangu, nadokoa hata nyama jikoni, naiba pesa nikienda sokoni na kuzitumia.

‘Mimi sijachukua pesa zako baba, mimi sio mwizi, sijawahi kuiba hata siku moja ‘nikajitetea,

‘Kama kuna mtu kachukua sizani kama atakuwa kazitumia zote, labda tufanye msako, chumbani kwao’ akasema mama. Na kwa vile sikuwa na wasiwasi mimi nikasema ufanyike huko msako, na hakupita muda baba akaja akiwa na hasira, huku kashikilia mfuko wangu wa shule.

‘Pesa hizi ndani ya mfuko wako umezitoa wapi?’ akauliza kwa hasira.

‘Baba mimi sijui na sijui zimefikaje hapo kwenye mfuko wangu, lazima kuna mtu kaziweka humo’nikasema huku nikiwa na wasiwasi. Cha ajabu baba alinikemea  tu siku hiyo na kunionya kama ikitokea tena hatakuwa na msamaha na mimi. Nilishangaa kwanini hakuchapa siku hiyo, tofauti na siku nyingine ambazo, nikishitakiwa kwake anachapa kweli kweli. Nilijua kabisa hakuamini hayoo maneno ya mama, kwani alionyesha kujihami mapema. Hata hivyo mama alichukua fimbo na kuanza kunichapa akisema ninamuabisha, na ataonekana yeye hajui kulea.

Baada ya tukio hilo nikawa muangalifu sana kila mara nachunguza mfuko wangu na sehemu ninayoalala ili wasije wakaniwekea tena mtego kama huo. Lakini dhamira yao ilifanikiwa siku moja. Siku hiyo nilipewa barua ya matokea ya mtihani, nilimpa mama, mama akasema niende nikaweke chumbani kwao.

Kumbe mama alikasirika kwa vile mimi kwenye mtihani nimefanya vizuri zaidi ya watoto wake akaona anikomoe. Mimi bila kujua nikaingia chumbani, na kumbe alishaongea na baba kuwa mimi huwa naingia chumbani kudokoa pesa, kwahiyo ajifiche mahali ataniona mimi nikingia chumbani.Mimi nikaingai kama alivyonielekeza mama.

Nilipofika chumbani ikakuta nguo zimedondoka chini,mimi nikaziokota na kuzikunja vyema na kuziweka kweney kabati,sio mara ya kwanza kufanya hivyo, nilipomaliza, nikatika na kuingi achumbani kwangu nikiwa na furaha kuwa baba akirudi akiona matokea yangu ya mtihani atafurahi sana na ataniruhusu nikamtembelee  mama yangu.

Mama yangu alikuwa kaolewa na mume mwingine, na walikuwa wakiishi kwa amani, na furaha, na huyo mume wake alikuwa tayari niende nikaishi nao, lakini baba yangu alikataa kabisa, akidai kuwa anazalilishwa kuwa yeye hajui kutunza watoto.

Basi maranikasiki sauti ya baba akiongea nje, na mimi nikasubiri, nikijua baba akiingia ndani atakuta amtokea yangu ambayo niliyaweka sehemu ya wazi, ili ayaone, ikapita muda, na mara nikasiki baba akifoka, na mara nikaitwa kwa sauti ya hasira.

‘Wewe leo hujawahi kuingia chumbani kwagu,na kama uliingia ulifuata nini huko na ulifanya nini?’ baba akaniuliza maswali mengi kwa haraka haraka.

‘Nilileta barua ya matokeo yangu ya mtihani, baba hukuyaona nimefaulu vizuri sana, hiyo barua ipo chumbani kwenu’nikaanza kuongea nikionyesha uso wa furaha nikijua kuwa baba atanisifia kwa kazi nzuri niliyofanya, lakini …..kabla sijamaliza nikajikuta nimezabwa kofi la nguvu shavuni, nikapepesuka huku nikiwa nimeshikwa na mshangao, vipi tena.

‘Leo nimekufuma mwenyewe maana pesa zangu zilikuwa kwenye nguo,na wewe ndiye uliyeingia na nimekuona kwa macho yangu ukizikunja hizo nguo, nipe pesa zangu kwanza tena kwa haraka kabla sijakutafuna mzima mzima’akasema huku akiwa kashikilia fimbo.

‘Baba mimi sijachukua pesa zako, kweli niliingia chumbani kwenu, nikiwa na nia ya kuweka barua ya kutoka shuleni, humo ndani nikaona nguo zimedondoka nikaziokota nakuzikunja vyema,lakini sikuchukua pesa zako baba , mimi sio mwizo’nikajitetea.

Niliposema kuwa niliingia na kukuta nguo nikazikunja, hapo baba akaamini kuwa kweli nimezichukua pesazake maana zilikuwa kwenye hizo nguo,mimi nilikuwa sijui, huenda mama walifanya hivyo makusidi ili ionekane nimezichukua kwenye hizo nguo!

‘Leo utaniambia ukweli, kwanini tabia hiyo huiachi,mwanzoni nilikuwa nakutetea lakini sasa naona kuna ukweli ,maana nimekushuhudia mwenywe ukiingia chumbani kwangu, na ukatoka ..’akasema baba na kwenda ndani ambapo anaweka fimbo yake maalumu ambayo haivunjiki ukichapwa nayo, na nimjuavyo baba akianza kukuchapa anaweza akakuumiza vibaya sana,nikaona ni bora nikimbie.

Nikachomoka, na kukimbilia kwenye kichakani kilichopo karibu na hapo nyumbani, nikajiingiza humo, na muda huo nikamuona baba akitoka akiwa na panga, nikajua kuwa baba kweli kazamiria kuniua, na aliponiangalia huku na kule bilakuniona akaingia ndani, nikajua anakwenda chumbani kwetu,ninapolala na wadogo zangu, watoto wa mke wake na punde akatoka huku kashika pesa mkononi, na kusema kuwa kaziona kwenye nguo zangu, lakini nusu imetumika.

‘Huyu mtoto leo atanitambua, kumbe kweli ana tabia hiyo mbaya ya udokozi, kumbe ana tabia mbaya kiasi hiki, yupo kama mama yake, kiburi, hasikii akiambiwa jambo….sasa hiyo tabia nitaokomesha leo, moja kwa moja , ni bora nijulikane sina mtoto….‘akasema baba yangu huku kashika panga mkono mmoja na bakora upande mwingine.

Niliumia sana kusikia hiyo kauli kuwa eti mama yangu alikuwa na tabia mbaya, kitu ambacho sio kweli. Mama yangu alisifika hapo kijijini kama mke mwema, mama mwenye tabia njema na hata alipoachika kwa huyo baba wanaume wenge walimfuata kutaka kumuoa. Na baba aliposikia hivyo aliingiwa na wivu, akawa anamtangazia ubaya, lakini hakuna aliyemsikiliza, ilijulikana ni kwa sababu ya huyo mke wake mpya.

Kwa kauli hiyo nikamchukia baba, sikutaka tena kuonana na yeye na hata ile kauli kuwa kabadilika kwa ajili ya mke wake huyo nikaiondoa kichwani, nilimuona kuwa ni baba mbaya, asiye na maana kwangu tena.
Pale nilipojificha nilimuona akihangaika huku na kule akinitafuta na fimbo yake mkononi. Mimi nilikuwa nimetulia kimiya nikiwa nimeuma kucha kidole kidogo, wanasema ukifanya hivyo, kama umejificha mtu hakuoni.

Kauli ile ya baba ilinichefua, nikaona niondoke kabisa hapo nyumbani, sikuweza kuvumilia, nikalia sana huku nikikimbia, kuelekea nisipokujua nilikuwa nakimbilia tu, nilikimbia, hadi nikafika karibu na huu msitu, sehemu ambayo watu hutafutia kuni, na wakishakusanya hufika kwenye miti ambayo inatoa kamba. Na mimi nilifikia mti mmoja wa hizo kamba na kujikuta nachuna kamba na kuzikusanya hadi nikapata mzigo unaonifaa. Kamba hizi ni imara sana kwani hutumika pia kujengea.

Wakati nimetulia chini ya ule mti, nilianza kuwaza nini cha kufanya.

‘Mimi naona sina maana katika hii dunia, maana kila nilifanyalo hakuna heri, nimejitahidi kadri ya uwezo wangu kutimiza wajibu wangu, lakini sifanikiwi, hivi huyu mama anataka nimfanyie nini ili anione mimi ni sawa na mtoto wake, au nimemkosea nini kikubwa, labda mimi sistahili kuishi naye, labda nikifa atafurahi. Maana yeye ni mmojawapo ambaye hataki niende kuishi kwa mama yangu mzazi. Sasa anataka nini kwangu…’nikashika shavu.

‘Kwanini kama hanipendi, hataki nikaishi na mama yangu mzazi, nimeshagundua huenda raha yake ni mimi nipotee hapa duniani. .labda nikifa atafurahi.’basi nikawa naongea peke yangu, huku ninalia, huku ninasokota kamba, mwanzoni nilikuwa najisokotea tu hiyo kamba bila kujua ni ya nini.
Kidogo kidogo nikajikuta nimesokota kamba moja ndefu, nzuri, na hapo ndipo wazo la kujinyonga likakolea kichwani, nikakumbuka msichana mmoja aliyejinyonga hivi hivi kwa kamba, sasa hivi watu wameshamsahau;

‘Basi ngoja na mimi nijue, ili mama huyo asiyenipenda afurahi na moyo wake, na najua baada ya muda watu watanisahau na hawatajua kuwa nilikuwepo kwenye hii dunia’nikasema huku nikiitayarisha ile kamba vyema.
Nilipohakikisha imekuwa vyema, nikapanda nayo juu ya mti , hadi kwenye tawi kubwa, nikaifunga ile kamba kwenye lile tawi upnde mmoja na upande mwingine niliokuwa nimetenegneza kitanzi, nikajivika shingoni, nikatulia huku nikiwaza jinsi mama yangu atakavyolia, lakini sikujali nikijua kuwa atalia kwa siku kadhaa na baadaye atanisahau na watu wote watakuja kunisahau na mimi nitakuwa nimeokoka na hayo mateso.

Nikasogea kwenye sehemu ambayo nilijua nikiachia tu ile kamba inanikaba halafu kitakachofuatia ni kupteza uhai. Nikamuomba mungu anisaidi nife kwa haraka, na kuomba kuwa  mama yangu asihuzunike sana, anishau kwani nampenda sana  ,lakini watu hawo wabaya hawanipendi ndio maana naona ni bora nikajipumzikie huko ahera,

Nikahesabu moja mbili tatu, nikajiachia, …nakweli kamba ikashikilia vyema shingoni na kunifanya niwe naelea hewani, pumzi ikaanza kuisha na shingo ikawa inauma kwa jinsi ile kamba ilivyonikaba, jasho, likaanza kunitoka pumzi ikawa haitoki, nikajaribu kuitoka ila kamba shingoni,lakini haikuwa kazi rahisi nikajaribu kupiga kelele ya kuomba msaada, lakini sauti haitoki, mkojo na hata haja,vikaanza kunitoka,

Nikawa sasa nahangaika kwa kujipiga piga miguu ili kama ikiwezekana ikatike, lakini ndio ikazidi kunikaba vyema, maumivu ya kichwa, kukosa pumzi, na hali ngumu ambayo sijawahi kuihisi kabla vikaniandama, niliomba roho itoke haraka, lakini haikuwa hivyo, na kitu kama mnguruma ukaanza kusikika kichwani, nikajau sasa muda umefika, lakini sikujua ningelipata taabu kiasi hicho, na kabla sijapoteza fahamu  nikahisi nikipaa hewani ,na kichwa kikaginga kitu, sikuweza kujua nini kilifuata baadaye...


NB: Hivyo hivyo siku zinakwenda.

WAZO LA LEO: Tupende kuwafundisha watoto wetu tabia njema, na kuwazoesha kazi ndogondogo, ili baadaye wasije wakapata taabu, tukue kuwa maisha ni kupanda an kushuka, kuna leo na kesho ambayo hatuijui, tukiwadekeza watoto wetu, wanaweza wakapata taabu badaye, kama walivyosema wahenga,samaki mkunja angali mbichi
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Kazi nzuri M3, natamani ungeliendelea kidogo.