Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, October 17, 2012

Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi-11



Ilikuwa ni usiku wa baridi kali, na upepo ulioandamana na manyunyu. Hali kama ile iliwafanya wale waliopo ndani kutokutamani kutoka nje, na waliopo kitandani kutamani usiku uendelee kuwepo, lakini ilikuwa kinyume na kijana wetu huyu. Yeye alipoaangalia saa yake na kuona ni muda wa kuondoka, aliinuka pale kitandani na bila ya kumgusa rafiki yake , ambaye alijitolea kumuhifadhi kwa muda.

Yeye akaamua kujitosa nje bila kujali baridi.

Akiwa na mfuko wake mdogo wa safari ukiwa na suruali yake moja, na shati, na vitu vingine vidogovidogo, hakuhitaji mzigo mkubwa, akaanza kutembea kuelekea huko kwenye usafiri. Hakutaka kupata shida ya kukimbiza magari huku akiwa na mzigo usio kuwa na faida, kwanza mzigo wenyewe angeupatia wapi, wakati kakimbia kwao ni hilo shati na suruali moja.

‘Huu ndio mzigo wa mtu kama mimi, mtu ninaye kwenda kutafuta maisha,..’akasema huku akiweka mfuko wake begani huku akihesabu hatua. Kulikuwa kimiya kwani muda kama huo watu wengi wamelala,ni muda ambao karibu kila kiumbe huwa kimeshazama ndani ya dunia nyingine ya kufikirika, labda wale wenye matatizo, labda wale wenye mambo yao ya usiku, na labda wale wenye safari zao maalumu kama huyu kijana.

‘Waache walale, wakiamuka mimi nipo aridhi nyingine, aridh ya mategemeo..’akasema huyu kijana huku akichepuka,na kuongeza mwendo. Alitaka afike hiyo sehemu kwa huyo jamaa ambaye alielekezwa kwake,na alitaka afike mapema, akasubirie huko huko. Hakutaka kuchelewa hata dakika moja. Na kweli alipofika hapo nyumbani kwa huyo mtu,hakukuta watu, na mlango ulikuw aumefungwa, akatafuta sehemu akajiegemeza, hakutaka hata kukaa, aliona akikaa huenda akapatwa na usingizi, akaachwa na huo usafiri wa kudandia.

‘Nimeshaongea naye, unachotakiwa ni kufika pale nyumbani kwake, yeye huondoka saa kumi na nusu, kwani anahitajika huko kazini kwao saa moja asubuhi, kwahiyo hakikisha unafika pale mapema’akakumbuka maneno ya rafiki yake ambaye alimuunganishia kwa huyo dereva wa lori, ambalo hufika Mererani kila siku kupeleka mizigo kwa tajiri wa huyo dereva.

‘Nashukuru sana rafiki yangu, nakuhakikishai kuwa nikifanikiwa tu, nitakutoa, nitalipa fadhila zako’akamwambia rafiki yake huyo.

‘Wewe usijali, cha muhimu ni kuwa makini,na uhakikishe unawahi,maana huyo jamaa kasema hasubiri mtu,ukiwahi uanakuchukua hadi huko unakokwenda…’akayakumbuka hayo maneno huku akitikisa kichwa kuwa bahati yake inaanza kumnyookea.

‘Na kweli nimewahi..’akasema na kukatishwa mawazo yake na sauti ya mtu akija pale aliposimama, akakaa vyema kujiandaa kwa lolote, maana usiku kama huo, huwezi kumwamini mtu,hata kama ni biandamu mwenzako, na siku hizi wabya zaidi ni binadamu wenzako.

Kumbe alikuwa ni mwanadada,akiwa kajifunga kanga, kujizuia na baridi, na alipofika pale aliposimama yeye akachuchumaa bila kusema neno, huku akipuliza mikono yake kuongeza joto.

‘Baridi laleo sio mchezo, linahitaji moyo kutoka nje, lakini hakuna jinsi,….lazima niondoke leo, maana kukipmbazuka tu, huyo mshenzi atanijia na maneno yake yasiyo kuwa na thamani’akawa anaongea yule dada kama vile mwenzake aliyesimama hapo pembeni anajuana naye na anakijua hicho anachokiongelea.

‘Eti mtu, unaitwa toka huko machimbo,hawajui mtu unavyohangaika na maisha yako,unafika huku unaambiwa huyu mwanaume anataka kukuoa, hivi hawa watu wana akili kweli, ….uolewe tu kama mzigo sokoni,hapana hilo mimi sikubali’akawa anaongea huyo dada, na huyo kijana pembeni yake alikuwa katulia kimiya, hakutaka kuongea na mtu.

‘Na huyu mshenzi bado yupo kitandani na mkewe, haamuki tu, hajui sisi tunamsubiri yeye, sitaki kupambazuke nikiwa hapa. Wazee wameshakula hela za watu, eti ni mahari yangu, wale wao mimi niende kuwa mtumwa wa mtu mwingine, eti hivi kweli dunia ya leo mambo kama hayo bado yapo..aah,mimi sikubali’akasema huku akipuliza mikono yake.

‘Unajua huyo mume anayetaka kunioa yupoje, ni libaba lizima, eti linioe kibinti kama mimi,angelijua thamani yangu asingelithubutu hata kunitamkia hilo neno, eti nakupenda, nataka uwe mke wangu, eti jamani hiyo inakuja akilini’akasema yule binti na kuinua kichwa kumwangalia huyo kijana machoni.

Yule kijana akatikisa kichwa kukataa,hakusema neno, alitulia kimiya, hakutaka kujiingiza kwenye shida za watu wengine, kwani hapo alipo anashida zake, ambazo hajui jinsi gani atazitatua, akatulia kimiya akitamani huyo dereva atoke, waondoke, lakini huyo binti alikuwa akiongea sana, ikabidi atulie amsikilize na porojo zake.

‘Yaani nilipopigiwa simu kuwa nahitajika huku nyumbani haraka ,nilijua dingi au mazeri keshakitoa, lakini cha ajabu nafika hapa, nakutana na huyo mjomba na anti, wananiambia eti kuna posa,eti kuna mtu kaleta barua, anataka kunioa, natakiwa kuolewa haraka, kwahiyo nikubali, eti ni bahati imeniangukia.Nikawauliza nani kawaambia nataka kuolewa,wakanitolea macho, na kuanza porojo zao,…

‘Eti huyo mwanaume ni mtu mwenye uwezo, anajua kutunza mke,na natakiwa eti, unasikia hapo, eti- nikawe-mke- wake-wa-pili, na halafu nikiolewa kama mke mwenza,nitapewa duka langu, sijui duka la nini,…kikashuka kipapanda, nilitamani nianze ukurasa wa maneno, lakini nikatulia, hadi wakamaliza,nikawauliza mumemaliza ,….basi jibu nitawapa kesho, yaaani leo hii,wakajua nimekubali,..

‘Mara mida ya mchana mchana huyo mwanaume akafika hapo home,kaja kuniona, kaja na vijizawadi vyake mbuzi, eti, ananiletea kishika uchumba,..kishika uchumba ndani ya fuko wa Rambo,hahaha, nikzainia labda ni mabulungutu ya pesa,  nikauangalai ule mfuko, sikutaka hata kuuchungulia, maana upepo ukija ulikuwa ukipepea, basi nikajua ni vinguo, vya kike,nikamuita mdogo wangu, nikamwambia

‘Chukua huo mizigo, kauweke chumbani kwako…ni zawadi yako’nikasema huku nikimnyaa yule mbaba,alipoona nimetulia akaanza maneno ya kizamani, utafikiri anasoma mashairi ya shuleni,unajua ansemaje;.

‘Unajua mimi nakupenda sana, nataka uwe mke wangu maalumu, nikitoka kwenye safari zangu uwe pamoja na mimi, nikikuangalia nahisi raha, …lalalala,akasema huyo mwanaume maneno mengi akijua kuwa namsikiliza, mimi nikawa natabasamu tu,ile ya kujivunga, akaona kweli keshapata.  Yaani sikusema neno na huyo mwanaume alikuwa akiongea peke yake, maana nilijua nikifunua mdomo wangu,atatamani ardhi ipasuke, azame, mimi nikawa kimiya kama sio mimi.

‘Baadaye akatoka na kwenda kuongea na wazee, nikaitwa kuwa mahari yangu na …yaani hata kuitaja pesa yenyewe nashindwa,yaani wao wameniona mimi ni mtu wa kutolewa mahari laki, laki, sijui ngapi vile, na sijui na mbuzi, sijui na ngombe,nikacheka, na kusema, chukueni kama mnavihitaji hivyo vitu, mimi sihitaji chochote.

‘Walijua kuwa sijakubali, wakaanza poroji zao, eti kunibemebeleza ili nikubali, kwani wanahitaji sana pesa, wanahitaji ngombe, nikawaangalia wee, kwasababu nilikuwa nimefika kwa haraka, sikuwa nimekuja na pesa nyingi, nikatoa milioni moja nikawakabidhi wazee. Nikawaambia lengo lenu ni pesa, au sio, basi pesa  hii hapa, mengine niachieni mimi mwenyewe’

‘Hawakuamini,hasa huyo mama wa kambo,kama angelikuwepo mama yangu mzazi angelishanielewa, lakini hawa mama wa kufikia bwana wananikera rohoni, wanachojali ni pesa, wanachojali na tamaa zao, kwanini hawakwenda kuolewa na wanaume wengine, mpaka wafike kwenye ndoa za watu na kuziharibu…huyu mama aliharibu ndoa ya baba yangu , tena kwa uchawi, na hatafaikiwa….’akasema yule mwanadada .

‘Basi yule mama akazipokea kwa furaha, huku akimwangalia mume wake kwa macho ya mshangao, kwani hajawahi kushika pesa kama ile, hakutaka hata kuuliza pesa hizo zimetoka wapi, yeye akawa analambalamba mdomo wake kwa tamaa, angelijua jinsi gani wenzake tunavyohangaika, asingelizipokea hizo pesa, na nilijua tu, anazishika hapo kwa masaa, nitazichukua mwenyewe muda sio mrefu, na zinarudi kwenye pochi yangu, mimi sio mjinga bwana, nihangaike mimi wale waengine.

‘Baba ni mjanja, akamwambia mama anachukua hizo pesa anajua zimetoka wapi,mama akasema ni zawadi ya mtoto, kwanini asipokee.Mimi nikatoka pale na kuwaacha wakiongea, nikachomoka hadi hapa kwa huyi mshikaji namfahamu sana, nikajua yupo, na leo ni safari, nikarudi nyumbani, kufika nakuta familia imejaa hapo, mjomba , shangazi, mababa kibao, wakanikalisha chini na kuanza kunihubiria mambo ya ndoa.

Niliwasikiliza wee,mwisho wa siku nikawauliza, hivi ni nani kawaambia nataka kuolewa, na kama ni kuolewa ni mimi au wao wanaoolewa,ni mimi au ni wao, ni nani anakwenda kuishi na huyo mume ni mimi au ni wao, nikaawambia kama ni mimi basi huo mchezo waniachie mimi mwenyewe, nitajua jinsi gani ya kuucheza, ila mahari ya watu wasiipokee.

Hawa wazee bwana, hasa huyu mama wa kambo, na mwingine baba mkubwa, wananikera,unajua baba mkubwa alisemaje;

‘Tusipokee wakati tumeshakula. Tumeanza kupokea hiyoo pesa siku nyingi, wewe binti unataka kutuumbua , sasa sikiliza utaolewa utake usitake, kama sio binti yetu, ukatae, …tunajau ni jinsi gani unavyotuzalilisha huko Mererai, unajiuza, unatutia aibu…wakaongea wee, mimi nawasikiliza tu, sikutaka kubishana na hawo madingi, baadaye nikawauliza mu-me-ma-li-za

‘Eti nini…’akasema yule mnoko,baba mkubwa ni mnoko kweli, akainuka kutaka kunipiga kibao, nikamwamgalia kwa jicho la dharau,mwenyewe alirudi na kukaa, hakunigusa, ole wake angenigusa, nilikuwa an usongo na huyo dingi, maana yeye  ndiye alifanya mama yangu aachike,eti mama hazai, mbona kanizaa mimi , walitaka wamzalishe  mama kama mbuzi. Mbona huko alipoolewa ana watoto wawili.

‘Mchezo ukaishia hapo,wao wakakubaliana kuwa nijiandae kwa ndoa, kwani mahari imeshapokelewa na wao wameshamkubalia huyo mwanaume,na nakwenda kuwa mke mwenza, na mke mwenza huyo ninayekwenda kwake ni mama mmoja kajichokea, ….unajau kuchoka, yaani we acha tu, nyie wanaume, mnajua kuwatesa wanawake, hamna maana kabisa, ndio maana nikimpata mwenye kutoa, namtoa kiukweli .

‘Yule mama ni muhangaikaji kweli kweli, hapa kijijini wote wanamjua , amehangaika na mume wake yule, hadi wakatajirika, na ule utajiri pale,asilimia kubwa ni jasho ya yule mama,maana yule baba anachojua yeye ni kutumia,ni umalaya tu, sasa huyo mama kampa kibali kuwa aoe mke mwingine ili atulia, eti ndio wanakuja kwangu..kote huko hawajaona mtu ,wanakuja kwa malikia wa Mererani,hahahha, nicheke miye.

‘Basi wakati masindikiza tukafika mahali anavua viatu vyake vibovu kumwaga mchanga, anasema kuwa anataka kwenda mjini kununua viatu vipya vya kisasa na mimi ataninunulia eti nimwambia navaa namba ngapi, nikamwangalia kwa machale, nikamwambia mimi sihitaji viatu, akamnunulie mkewe, na kumuacha akiwa kabakia mdomo wazi.

‘Unajua hawa watu, ukiwachekea wanakuona huna maana, bora na wewe uende hivyo hivyo wanavyotaka wao, maana kama wanafikia kukuzalilisha wanakuita Malaya, wao wanajua kuwa sisi tukiwa huko machimbo kazi yetu ni kujiuza,hawajui maisha, sio lazima ujiuze, kuna mbinu nyingi za kupata pesa, ikitokea bahati mbaya, …ndio hivyo tena, lakini….huyu dingi ipo siku

‘Eti ananiita mimi Malaya, kwahiyo wanataka na mimi  nikaolewe na Malaya mwenzangu, lakini yeye keshaoa, keshawahi kuishi na mke, na katembea na wanawake kibao, hilo hawalioni,…huyo sio Malaya kweli, au hawajui maana ya Malaya nini. Malaya ni yule kaoa,au kuolewa,nab ado anatemeba nje ya ndoa, eti …au mimi nakose’akasema na kuniua kichwa kumuangalia yule kijana.

`Mimi mbona sijawahi kuishi na mume, kama wanataka niwaletee mume nitawaletea, lakini sio mume kama huyo, nawaletea mtu mwenye thamani, mtu ambaye akikohoa anatema pesa,sio watu ovyo ovyo, kama yule, ambaye hapa kijijini wanamuona eti ni tajiri….hahaha…tajiri, kweli yule naye tajiri, labda kwa hapa kijijini.

‘Hivi wewe siunamfahamu yule jamaa, mwenye maduka ya jumla pale stendi ya basi, basi ndio yule eti anataka kunioa mimi,….mimi labda sio mtoto wa Kinyaturu mchanganyiko wa Kirangi, damu Osama,ilikuja huku kimakosa..’ akasimama na kusogea mlengoni mwa ile nyumba huku akiongea akasema;

‘Sasa huyu jamaa mbona hatoki, mbona kunaanza kupambazuka, hawajui tumeshaharibu mambo huku, maana yule mama akiamuka anajua pesa anazo, atakuta pochi lake, kumebakia laki moja, tena hizo nimemuonea huruma, hizi pesa anatakiwa azipate mama yangu mzazi sio mwanamke kama yule’akasema huyo binti na kwenda kugonga mlango wa huyo dereva.

Na mara mlango ukafunguliwa, yule jamaa akatoka akiwa kashika mfuko wa safari,akajinyosha na kutuangali, hakuuliza zaidi kuwa sis ni nani, huenda alishajua ni akina nani, akasema.

‘Samhanini nimechelewa kidogo, simnajau tena majukumu, haya pitieni huko nyuma, gari nime liweka nyuma ya nyumba, nyie ingieni nyuma ya hilo gari, maana mbele kuna mke wa bosi tutamcchukua njiani.
Mimi nikaangia kwenye hilo gari huku nikiomba mungu, safari yangu iwe salama, yule deerva akasema;

‘Muwe tayari huko nyuma, mimi nikiwasha gari,sina muda wakusubiri, mtu, hili sio gari la abiria, nawasaidia nyie tu kwa vile ni wanakijiji wenzangu, na mkiulizwa na askari wa barabarani mseme nyie ni maotingo,na mjue huko njiani tukikwama mtanisaidia kusukuma.’akasema kwa utani.

‘Hivi wewe jina lako nani mbona sura yako ni ngeni machoni mwangu, na sijui kwanini nimekusimulia mambo yangu wakati hata sikujui’akasema yule binti na kuniangalia machoni, na hapo nikawa nimevutika na sura ya huyo binti,maana muda mwingi wakati anaongea sikuwa nimemwangalia sana machoni,kweli alikuwa mrembo.

‘Mimi naitwa Adam,  ni mwenyeji wa hapapapa,labda hujaniona kwasababu naishi kijiji cha mbeleni,i mwanzoni  kabisa ukitokea mjini ..nataka nifike Machimbo, nikahangaike kidogo’akasema yule kijana.

‘Mungu wangu wee, wewe, uende machimbo, …na mwili kama huo ulivyo,nakusikitikia,wewe rudi kanyonye ziwa la mama yako, hujakomaa wewe, utakwenda kujifia huko bure,’akasema huku akichekakwa dharau.

‘Nikuambie ukweli, huko hakuendeke hivi hivi, vijana wengi waliofika huko bila mpango,wamekuwa kafara la wenzao’akasema yule binti huku akisjishika vyema kwenye vyuma vya hilo lori. Tulikuwa tumeshakaa ndani ya hilo lori, likaanza kuondoka, na moyoni nikajua sasa nimeshaanza safari ya kutafuta maisha.

‘Ndani ya lile lori kwa nyuma tulikuwa wawili,lakini kila hatua walikuwa wakiingia watu wengine, na kuongezeaka abiria.Mimi nikawa na hamu sana ya kujua maisha ya huko Mererani, kwa kupitia kwa huyo binti, kwani huyo binti alionekana kujua mengi, na wakati namsikiliza ndio nikakumbuka mjomba alivyosimulia kuwa watu wakifa ndani ya migodi inakuwa kama kafara la kupata madini kwa watu wengine.

*******

‘Mjomba wangu, mimi siku ile nilikuwa niwe kafara la wenzangu,maana ukifa ndani ya migodi,basi wenzako wananeemeka,na nikijua kuwa kwenye mwili wangu nimeshajifunga madini ambayo sikujua kuwa yana thamani kiasi gani, lakini nilijua kabisa kuwa madini yale ni yenyewe na yanaweza kuwa na thamani nyingi sana.

‘Mjomba siku ile nilipoingia ndani ya lile shimo na kuanza kujifukia kwa ajili ya maji ya mvua,nilijua ndio mwisho wangu.Maana maji yalianza kujaa ndani ya lile shimo na sehemu kubwa ya lile shimo ilishaanza kujifukia, hali ya hewa ikawa nzito,na mimi mwili ukawa unatetemeka kwa baridi, nilijua kabisa kama nisipowahi hopsitalini, basi sizani kama nitamaliza mwezi, lakini kwa vipi, sina pesa.

‘Sina Pesa,pesa si hizi hapa’nikasema  na kujishika sehemu ile nilipofungia yale madini kiunoni.

‘Lakini hata kama ni pesa, nitatokaje humu ndani?’ nikajiuliza. Nikaangalia huku na kule,na maji yakawa yemshajaa mle ndani, na ina maana hilo shimo kwa muda wowote huenda litaanza kutitia.Iwe tu ni bahati, mvua itulie haraka, lile shimo lilikuwa bado ni jipya, halikuwa imara, tulishaliona kabla.Mvua ilionyesha kuwa bado inanyesha maana maji yaliyokuwa yakiingia mle ndani kwa kasi ya ajabu na kila mara yalikuwa yakiongezeka.

Nikaona nisijipweteke,nikaanza kupambana na maji, nayafuta huko huko yanapotokea, kuna muda narudishwa nyuma,kuna  muda naangukiwa na kifusi,lakini sikukubali, nikawanayafuta hayo maji nikijua ndio njia ya kutokea, nilifanya hivyo kwa muda mrefu, hadi nikajikuta mwili umeisha nguvu.

Kwa mbali nikahisi ubarudi,upepo,kuashiria kuwa nimefika karibu na sehemu ya kutoke,a nikajivuta, nikajivuta, nikajitahidi hadi nikatokeza kichwa nje,kwa ndani nikasikia nikiminyw ana kifusi, ina maana hiyo sehemu imeshajifunga, kazi ikaw ajinsi gani ya kutoa kiwili wili change , kwani nilikuwa nimefukiwa nusu mwili.

Mvua ilikuwa kubwa , na maji yale yakanisaidia kwani sehemu ile ilikuwa bado na uwazi, na maji yakachimba nikaweza kujivuta hadi sehemu ya juu, na mara kama vilenilikuwa nasubiriwa mimi shimo likaanza kutitia, na kuziba kabisa,nikahema huku nikimshukuru mungu,…nikajikongoja hadi kwenye uwazi, chini ya mti,aili kujizuia na mvua.

‘Nilishikwa na usingizi wa jabu,sijui kamaulikuwa ni usingizi au ni kupotewa na fahamu, lakini ninachokumbuka ni kuwa machoyalikuwa mazito,nikashindwa hata kuinua kope za macho,na kujikuta nimelalafofo, niliamshwa na moto. Kulikuwa na moto karibu, na ule moto ulitaka kuniunguza unyanyo wangu, nikausogeza mguu haraka.

Mara nikasikia mtu akisema;’Umeona maajabu, ule udongo pake unacheze cheza, au ni kwasababu ya mvua mashimo ya hapa yanatitia nini?’

‘Hapana kile sio kitu cha kawaida,nii mashetani ya huko mchimbo’mmoja akasema.

‘Wewe mashetani yatoke wapi huku, kilasiku watu wanayakemea, wanatambika, wanaomba, hayo ni macho yako yanachezacheza,mmh,hapana lile ni jitu,lipo kama udongo’mmoja akasema na mimi hapo hapo nikajiinuka na kukaa.

Wale watu walipoona hivyo, hawakusubiri, walitimua mbio za ajabu,nikabakia nimeshangaa, nikajau sasa hapo hakukaliki, maana hawo watu wataenda kuwafahamisha wenzao, na watakuja hapo, wataanza kumuhoji, na mipango yangu itakwama, nikajizoa zoa,na kuanza kutembea kama roboto, hadi kutafuta maji.Na nyuma nikasikia watu wakipiga kelele;

‘Shetani shetani,…’ lakini mimi sikuwasubiri nikatimua mbio kama mwehu.


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Mkuu pole sana, nimesikia mitihani uliyo nayo kwa sasa, usijali sana yote mkabidhi mungu ukijua kuwa MPAJI WA RIZIKI NI MUNGU

Anonymous said...

Wow, amazing blog layοut! Ηow long have you been
blоgging fοr? yоu make blogging
lοok easy. Thе overаll loοk of youг web ѕitе is
mаgnificеnt, let alone the contеnt!
my website - short term loans