Hali ya Dalali iliendelea kuwa mbaya, sasa ikabidi
ahamishiwe kwenye wodi maalumu, bado akiwa kwenye hali hiyohiyo, japokuwa sasa
alikuwa hapumulii mashine ya gesi, na mapigo ya moyo yalikuwa yakifanya kazi,
ajabu mtu mwenyewe sasa alikuwa hawezi kuongea au kujiinua, yupo yupo tu.
‘Hii hali sio ya kawaida…tumejaribu kila njia, lakini
mtu yupo kama alivyo hivyo…sasa sisi tumeshauriana na wenzangu, tumeona
ahamishiwe hospitali za juu…’akasema docta.
‘Haya sisi tunawasikiliza nyie…’akasema muongeaji wa
familia.
Wakati utaratibu wa uhamisho wa mgonjwa huyo kwenye
hospitalini za juu ukifanyika,
Wandugu wakakaa kikao kijadiliana, na mmoja akasema;
‘Jamani hivi hamuoni, hili tatizo ni kama lile la mke
wa marehemu, si ilikuwa hivi hivi jamani…’akasema mmoja wa wanafamilia.
‘Mhh,… yule mwanga, au ndio kageuza kibao kwa shemeji
yake, …inabidi tulifuatilie hili jambo kwa watalaamu,, ..lakini kipindi kile
aliyefuatilia tatizo la huyo mwanga, alikuwa ni huyu huyu mgonjwa, sasa nani anaweza
kufahamu wapi alikwenda, ili na sisi twende huko…?’ akauliza mwanandugu
mwingine.
‘Mimi nafahamu ni kule kwa yule mtaalamu wa bondeni,
maji machafu…’akasema jamaa mmoja
‘Oh, ndio yule, mimi wala simuamini…?’ akauliza mzee
mmoja na kutoa hoja zake.
‘Ndio…nakumbuka mara kwa mara Dalali hupenda kuenda kwa
huyo jamaa, labda tujaribu kwake kwanza tumsikie…’akasema huyo jamaa,
‘Sasa nani atalifuatilia hili…?’ wakauliza na kamati
maalumu ikaundwa kulifuatilia hilo, akiwemo mke wa Dalali. Na baadae taratibu za uhamisho kwa mgonjwa
huyo zikakamilika,…Dalali akahamishwa, …
Hayo yakiendelea huko,
**********.
Huku kwa watu wa usalama,mambo yalikuwa nayo
yakiendelea…
Mara taarifa zikawa zimevuma, kuwa Dalali hali yake
ni mbaya sana ni ya kusikilizia,…na kwa umaarufu wa Dalali watu wakakimbilia
hospitalini kuuliza….na walipofika hapo wakaambiwa Dalali hayupo hospitalini
hiyo , na iliposikiwa hivyo, ndio ikaja taarifa nyingine kuwa Dalali hatupo
naye duniani.
Siki hiyo ndio
nami nimeitwa kituo cha polisi kuonana na wapelelezi,..wakati naingia, ndio
nakuta majadaliano makali, humo
nikawakuta wapelelezi wale wawili na wakili wao, na mbele yao kuna nyaraka
mbali mbali, na nilipofika tu,…nikamsikia wakili akisema kwa hasira;
‘Huu ushahidi hauwezi kushindana na ushahidi wa
benki, hapa mnataka kunita mimi aibu tu…, mimi siwezi kufanya kazi kama
hii…’akasema huyo wakili muendesha mashitaka, na aliponiona naingia akanyamaza.
Nikasalimiana nao, na ndio wakaanza kunielezea hali
halisi..
‘Kiukweli, hapa hatuna kesi kabisa, tunapoteza muda
wetu bure na gharama, ambazo mwisho wa siku mtatakiwa kuzilipa…ushahidi wa
benki una nguvu za kisheria, unaonyesha kabisa kuwa hilo deni ni la
marehemu…’akasema huyo wakili
Nikabakia kimia;
‘Sasa nimeambiwa wewe ndiye msemaji wa familia kwa
hivi sasa, ..mimi nashauri, kwa vile deni lipo, na linaonyesha ni la marehemu,
hakuna haja ya kujiingiza kwenye gharama za kuendesha hii kesi, ujue ukishindwa
utalipa deni na gharama zote za hiyo kesi…’akasema wakili.
‘Samahani kidogo, nikuulize tu,…je kwa kusema hivyo,
una maanisha kuwa wewe umejiaminisha kuwa, hilo deni ni la marehemu si ndio
hivyo…?’ nikauliza
‘Sio mimi, ni vielelezo na ushahidi…’akasema.
‘Ok,..unajua mimi, bado sikubaliani kabisa…sasa labda
bado nikuulize wewe, kwa jinsi ulivyoona, hivyo vielelezo, nafsini mwako
unaamini hivyo, kuwa hilo deni ni la marehemu …wewe kama wakili, wewe kama
mzazi,.?’ Nikamuuliza tena hivyo, aliona kama namkera fulani hivi, akaniangalia kwa macho ya kushangaa, halafu
akasema;
‘Sikiliza ndugu, hapa hatuongei kiusanii,
kinachoongea hapa ni ushahidi, ni sheria, na jinsi gani ya kumshawishi hakimu,..mimi
nimepitia ushahid uliopa hapa, ..huu, hauwezi kusaidia lolote,…sasa kutoa hisia
zangu haitasaidia kitu hapa…’akasema.
‘Nimekuuliza hilo swali nikiwa na maana moja,…hii
kesi, ukitaka upate ushahdi wa kimaandishi, hutaweza kuupata, maana
ulishaharibiwa na hao waliokusudia kufanya hivyo..’nikasema
‘Kama ni hivyo, ulitaka mimi nitetee vipi maandishi,
nyaraka, au mashahidi wa kuaminika, ndio kitu cha kusaidia hapa, sio hisia
ndugu yangu, ujue sisi ndio tunakwenda kufungua kesi ya kupinga hukumu,… kuwa
hilo deni sio sahihi, sio la marehemu…’akasema.
‘Unajua mimi awali, niliomba hizo barua mbili
ambazo nahisi zinaweza kuwa na…namna
fulani ya kuupata huo ushahidi…, pili nilishauri juhudi zifanyike ili tuwapate
hao watu wawili, waliotoweka,… sasa sijui mumefikia wapi..’nikasema.
‘Hizo barua hazitasidia kitu, nimshazipitia,….kwasababu
zenyewe hazina viambata vya kuzibeba,, unanielewa hapo,...ukiangalia hiyo barua
ya benki, ina kiambatishi cha statement, lakini hiyo statement yenyewe inakuwa
ushahid wa benki…’akasema.
‘Naomba niipitia kidogo…’nikasema na walisita kidogo
baadae nikakabidhiwa,..ilikuwa imewekwa ndani ya karatasi ya nailoni,…kabla
sijaipitia nikauliza swali.
‘Je kwenye alama za vidole, hamkupata kitu cha
kusaidia,.?’ nikauliza
‘Hakuna cha kusaidia,..alama kwenye barua ya benki ni
alama za vidole za marehemu , na juu ya bahasha kuna alama zingine, lakini
hazijulikani ni za nani, …’wakasema
‘Kama hamjampata ni alma za nani, huo ni moja ya
ushahidi..kama ingelikuwa ni marehemu peke yake tungelisema yeye ndiye
aliyejaribu kuchoma huo ushahidi..ina maana kuna mtu yupo nyuma ya hili
jambo..’nikasema.
‘Je alama za Dalali kwenye hiyo barua hazipo..?’
nikauliza
‘Kwenye hiyo barua ya benki hakuna alama za Dalali,
au mtaalamu, …’akasema mpelelezi.
‘Ni nani sasa…washukiwa wote alama zao haziendani na hizo alama zilizopo
kwenye hiyo barua, ya benki…na kwenye ajali, alama zilizopo ni za Dalali, na ni
uhakika kwa vile yeye ndiye alikuwa na hiyo barua, kwa mara ya mwisho…ila kuna
alama nyingine inayofanana na hiyo barua nyingine…’akasema
‘Na ndio kusema hiyo alama ni ya huyo mchomaji wa
hizo barua,,….na sio alama ya mama mwenye nyumba, Dalali au mtaalamu…’akasema;
‘Na hapo mpelelezi, akauliza swali, hivi ni kwanini
mama mwenye nyumba alichukua tahadhari ya alama zake zisionekane kwenye hizo
barua, alipoziona kwenye hilo shimo…?’ akauliza mpelelezi
‘Ni tahadhari tu, huyo mama kaenda shule, anajua
tahadhari ya hilo…mimi sioni kama mama mwenye nyumba anaweza kuhusika na
hilo..’nikasema
‘Usimtetee…hapa yoyote anaweza kuhusika…’akasema
mpelelezi
Basi nikawa nazipitia ile statement na barua,
…niliona kiasi ambacho mlalamikaji alikuwa akikilalamikia, na kwenye statement
inaonyesha hivyo, ..na ikaja salio, kuna statement nyingine mpya ambayo, ndio
inabeba deni la nyuma, na kiasi kilichokopwa,..ni kiasi kikubwa sana,…
‘Je benki hawawezi kupata..statemeny mpya kama hii,
ya nyumba ambayo inaendeleza bila kukata sehemu mbili, salio la zamani na la
sasa..?’ nikauliza.
‘Benki wao wanasema haiwezekani maana mashine yao
iliharibika, na kumbukumbu zilichukuliwa hivyo kama salio kutoka kwenye taarifa
za kimahesabu, na wakati wanachukua taarifa hizo, salio lilikuwepo ndio
hilo…’akasema
‘Salio lilikuwepo bila deni, au sio..?’ nikauliza
‘Ndio..hilo deni lilikuja kujitokeza kwenye statement
hiyo ya pili, kwahiyo sio rahisi kupata maelezo ya awali yakiendeleza hadi
sasa..’akasema.
‘Je kuna kumbukumbu gani za zamani zilizopo, kwa
mfano barua kama hii je ipo benki, barua ambayo aliandika marehemu kulalamika..?’
nikauliza
‘Kumbukumbu zote za zamani ziliharibika..ikiwemo faili
zilizopo barua kama hii, na banki imesaidiwa kupata hii nakala....’wakasema
‘Sasa kuna ushahidi gani wa kusadikisha kuwa hilo
deni ni la marehemu kuacha hii statement iliyoambatishwa hapa…?’
‘Upo mkataba, …zipo nyaraka za kuonyesha kuchukuliwa
kwa hizo pesa na sahihi ya mchukuaji, hiyo haina shaka, ndio maana benki wana
kila sababu ya kuamini kuwa deni hilo ni la marehemu….’akasema.
‘Mhh..kumbukumbu za zamani ziliungua, lakini
kumbukumbu hizi zipo, …kwanini hizi hazikuungua..?’ nikauliza
‘ Kuna kumbukumbu ambazo zilikuwa kwenye kabati la
ndani,hizo hazikuungua, na nyaraka zake ni pamoja na mikataba ya mikopo huo…’akasema
wakili.
Nikaipitia tena ile barua na statement..sikuona cha
kusaidia..kiukweli hapo nami nikaanza kuhisi mtihani mkubwa jinsi gani ya
kuthibitisha huo ukweli kuwa hilo deni kweli sio la marehemu…moto umeunguza
vitu vya ofsini, moto umeunguza gari na kuua mtu…moto…moto ukaja kuchoma hata kumbukumbu
za marehemu nyumbani kwake
‘Kuna nini kwenye moto…’nikasema na wao wakaniangalia
tu
‘Moto si moto bwana, ili uharibu kumbukumbu kabisa
inabidi kuchoma moto…’akasema mpelelezi.
‘Mimi naona
watu wa kutusaidia kwa hii kesi ni hao jamaa wawili…’nikasema
‘Bila kumbukumbu za maandishi itasaidia nini, hata
kama tukiwapata, maana wao wanajua hizo kumbukumbu hakuna, kwahiyo kwa vyovyote
iwavyo hawatakubali....’akasema wakili
‘Ina maana ushahidi wote ni lazima uwe wa
kimaandishi..?’ nikauliza kama vile mimi sijui lolote kuhusu sheria.
‘Kwa ajili ya hii kesi ya benk, maandishi ni kitu
muhimu sana, bila maandishi hatuwezi kushinda, benki wana maandishi,..nikiwa na
maana mkataba, na hati ambazo zinaonyesha kuwa kweli marehemu alichukua huo
mkopo..’akasema
Na mara simu yangu ikalia..nikapokea kwa haraka
nilijua ni nani kapiga hiyo simu
‘Vipi umemfuatilia hadi wapi..?’ nikauliza
‘Wapi, hospitalini gani…?’ nikauliza na kusikiliza
kwa makini baadae nikawageukia wenzangu, na kusema;
‘Mtu wenu namba mbili aliyetoroka mahabusu
kapatikana..’nikasema
‘Kapatikana wapi..?’ wakuliza wale wapelelezi wawili
kwa pamoja.
‘Yupo hospitali ndogo ya wiliya, ila kwa hivi sasa, kaandikiwa
uhamisho wa kwenda hospitali kuu ya
muhimbili…hali yake ni mbaya sana…’nikasema
‘Anaumwa nini huyo mtu.?’ Akauliza wakili.
‘Alikuwa na jereha la risasi,…wakati anatoroka
alijeruhiwa kwa risasi,..sasa lile jeraha limeozesha mguu…na hataki huo mguu ukatwe…’nikasema
‘Oh…sasa tumempata mmoja…’akasema mpelelezi
akionyesha furaha fulani.
‘Sawa, lakini hata kama mumempata huyo mtu mmoja,,
bado kuna kazi ya kumshawishi, nyie awali mlikuwa naye au sio.. , mlimuhoji
alisema nini…hapa sioni maelezo yake, zaidi ya kuwa alitoroka..?’ akauliza
wakili
‘Hakupenda kuongea…kila jambo alimtupia Dalali…hata
baada ya kufinywa kidogo,…aliishia kusema anayejua zaidi ni Dalali,.. na
alipoona kuwa anaweza kuongea , maana asingeliweza kuvumilia, ndio
akatoroka…’akasema mpelelezi.
‘Kwahiyo mnahisi kuna jambo analifahamu ..kwa jinsi
mlivyomuhoji…?’ akaulizwa
‘Ni mjanja sana..alikuwa makini kwa hilo…kiukweli
hakuna tulichopata kutoka kwake, yeye anadai kazi yake ni kuhudumia wateja, na
kuhusu hilo deni , Dalali ndiye alifika kwake kuomba msaada wake, ..’akasema
‘Msaada gani…?’ akauliza wakili
‘Hilo deni lipotee, na yeye akasema, akamwambia
Dalali hilo deni ni kweli la marehemu, na alisema hivyo kutokana na jinsi
alivyoona kwenye kuangalizia kwake,…unasikia, kuangalizia kwake, akiwa na maana
ya ramali.
‘Kwahiyo yeye anakiri kuwa aliona hivyo, kuwa deni ni
la marehemu, na hayo mambo ya mizimu je.?’ Nikauliza
‘Alisema,.. yeye alivyoangalia, ndio alijua kuwa
matatizo yote yanatokana na hilo deni, ndio maana mizimu ilifika kuitesa hiyo
familia,..ili deni lilipwe, ili marehemu aweza kupata makazi mema…’akasema.
‘Kwahiyo maelezo yao yanafanana na ya Dalali…?’
nikauliza
‘Yanafanana ndio..’akasema mpelelezi.
‘Sasa kumuona sasa hivi itasaidia nini…?’ akauliza
wakili
‘Kwanini alitoroka, hiyo inaweza kumfanya
aongee…ngoja tujaribu kumuona…’akasema mpelelezi
‘Itasaidia tu..nahisi anajua zaidi ya hicho
alichokisema, tukimbana sana kwa maswwali…’mimi nikasema
Wapelelezi wale wawili wakasimama, na wakili akawa
anawaangalia tu
‘Inabidi tukuache muheshimiwa, unaweza kuongea na mtu
wa jamii kumalizana naye huenda tukarudi hapa haraka iwezekanavyo…’akasema
mpelelezi
‘Na mimi nataka niandamane nanyie kama hamtojali…,
nataka nisikilize anachoongea au hata mimi nimuhoji pia..’nikasema na
wapelelezi wale wawili waliangaliana
baadae wakakubali;
‘Sawa twende…’wakasema
Basi tukaondoka na hao wapelelezi wawili, tukamuacha
wakili muendesha mashitaka akipitia vielelezo vilivyopo mbeleni mwake.
Wakati tunatoka nikapokea simu ya mama mjane.
‘Vipi dada..?’ nikamuuliza
‘Kuna taarifa kuwa mnada utafanyika, kwenye wiki hii,
hakimu aliyetoa hukumu kawakubalia benki wapige hii nyumba mnada…’akasema.
‘Nani kakupatia hiyo taarifa..?’ nikauliza
‘Wakili…’akasema
‘Wakili yupi..?’ nikauliza
‘Yule wa zamani…’akasema
‘Hamna shida,….nakuuliza jambo moja, unafahamu mzee mtupe ana uhusiano
gani na mtaalamu..?’ nikamuuliza hilo swali.
‘Mhh, mimi sijui…labda nije kumuuliza mpangaji wake
mmoja anayemfahamu ..’akasema
‘Hapana, usifanye hivyo, …nitajua mwenyewe
tu..’nikasema na kukata simu.
Tukafika hospitalini, na kujitambulisha, ..kwanza
ilionekana kama madakitari hawataki kusema kuwa huyo mgonjwa yupo au hayupo, na
walipobanwa sana, wakasema jamaa zake hawakutaka mtu huyo afahamike kuwa yupo
hapo.
‘Sisi ni polisi, na huyo mtu anatafutwa kwa
uhalifu..’akaambiwa docta, na docta hakuwa na la kufanya akawaonyesha wapi huyo
mgonjwa alipolazwa.
‘Lakini bado hawezi kuongea, kwasababu imebidi tukate
huo mguu wake…’akasema docta
‘Kwanini ..?’ akaulizwa.
‘Ulishaanza kuoza, na unatoa harufu kali, sio kawaida…na
kuoza huko kumetengeneza kansa,…’akasema docta.
‘Oh, kansa hiyo ina athari gani kwake…’akauliza
mpelelezi.
‘Kiukweli kansa hiyo imeenda mbali sana, na
tunaangalia jereha lilivyo, ili ikiwezekana aanze matibabu ya mionzi, kiukweli
hali yake sio nzuri…’akasema docta.
‘Tunaweza kuongea naye…kama hali ndio hivyo..?’
akauliza mpelelezi
‘Kiukweli, haiwezekani kwa hivi sasa…’akasema docta.
‘Docta, kama uwezekano wa huyo mtu kuishi ni mdogo,
tunataka tupate maelezo yake kidogo, fanya ufanyavyo, huyo mtu anashukiwa kwa
uhalifu…’akasema mpelelezi.
‘Ngoja kwanza tuone…’akasema docta, na akaingia huko
ndani, na baadae docta akatoka, na kusema;
‘Sawa mnaweza kuongea naye, lakini kwa haraka, dawa
niliyompatia haiwezi kudumu kwa muda mrefu..’akasema docta.
************
Tuliingia kwenye hicho chumba alicholazwa huyo
mgonjwa, pamoja na madawa ya hospitalini, bado harufu ya kitu kuoza ilisikika…
Wapelelezi wakamsogelea mtaalamu..mtaalamu alikuwa
kafungua macho, na alipowaona hao watu wawili nikaona macho yakimcheza cheza;
‘Mtaalamu, sema ukweli wako, ili tuweze
kukusaidia..hali uliyo nayo unahitajika wewe kwenda India kwa matibabu zaidi…,sasa
ongea ukweli ili tuweze kukupatia hiyo nafasi…’akasema mpelelezi.
‘Si-s-wezi ku-ku-pona,..na si-s-na cha kuwaambia, Da-la-li,
ata-wa-wasai-diaah, ni-ni acheini, ni-ni fe tu, ta-tayari…si-sipo-poni…ma-ma-teso
ya.ya me-zidi, bo-bora ku-kufa tu…’akaweza kusema hivyo.
‘Je kweli deni ni la marehemu, ujuavyo wewe…?’
akaulizwa.
‘Mi-mi…Si-s-i..ju-ju—iii, si-we-zi..kku-se-ma…’
akasema hivyo
‘Kwanini huwezi kusema, upo tayari ufe , hutaki
kutibiwa wewe..?’ akaulizwa
Akabakia kimia…
‘Ajali ya gari, lililomuua marehemu alisababisha
nani…?’ akaulizwa
‘S-si jui…si-we-zzz-ku-kusema..mi-i-i-ko…’akasema
hivyo.
Na mimi hapo nikaona nijaribu bahati yangu.
‘Mtaalamu, ukweli unaweza ukawa dawa ya matatizo uliyo
nayo, kuumwa sio kufa, lakini wakati
mwingine inabidi kujiandaa na kifo…ukifa, unakwenda kukutana na yule asiyedanganyika,
ni heri ukatubu kabla ya siku haijafika,..mtaalamu huenda kauli yako
ikasaidia,...sema ukweli wako ujisaidia, hapa duniani na kesho ahera…’nikasema.
Hapo mtaalamu akabakia kimia, …nikaona machozi
yakitoka machoni mwa huyo mtu.
‘Mtaalamu, sema ukweli wako kabla mlango wa toba
haujafungwa…kumbuka ukweli unaweza ukawa ndio dawa ya matatizo uliyo nayo,
miiko mbele ya mungu haitakusaidia…’nikasema.
‘Mo-mo-to,…’akasema
‘Moto una nini…?’ nikauliza
‘M-mtu wa-wa wa…wa…ba..ba..benk…’akasema hivyo kwa
kujitahidi sana,..pumzi ilikuwa haitaki kutoka,,…na alipotamka hivyo, akatulia…
nikaona machozi ya kitoka machoni mwake, …na hakuweza kuongea tena, na ikawa
ndio maneno yake ya mwisho.
Docta alikuja akatuambia tutoke nje, na baadae akaja
kutuambia Mtaalamu hayupo duniani tena
***********
Ikabidi tuanza safari ya kurudi ofisini, na wakati
tunatoka, nikamuona mzee Mtupe…alikuwa hajatuona..nikawaambia wapelelezi hao,
kuna mtu nataka kuonana naye mara moja..
‘Sisi hatuwezi kukusubiria…’wakasema
‘Hamna shida…’nikasema..huku nikielekea kule alipo
huyo mzee,..huyo mzee alikuwa akitembea kwa haraka..nikawa ninamfuata nyuma, alikuwa
akielekea wodi nyingine, nikawa namfuatilia, …mpaka kwenye wodi aliyokuwa
akienda.
Nikatulia,….baadae akaongea na mlinzi anayelinda hiyo
wodi maana ulikuwa sio muda wa kuona wagonjwa, nikaona akiruhusiwa kuingia, na
alipoingia ndani nikaenda kuongea na yule dakitari.
‘Baba yangu kafika hapa, ..?’ nikauliza
‘Baba yako nani..?’ akauliza
‘Mzee mtupe..’nikasema
‘Mimi simjui mzee yoyote anayeitwa mzee
Mto-pe..’akasema.
‘Docta mzee wangu kaja wodi hii,… kuna mgonjwa
tunamtafuta sasa nataka kuwa na uhakika tu…’nikasema na huyo mlinzi akasema;
‘Kuna mzee kaingia hapo wodini, anamtafuta mgonjwa,
msubirie akitoka utamuona..’akasema akilini nikawaza ni mgonjwa gani mwingine
kaja kumuona huyu mzee, na mara simu yangu ikalia, nikaona ni mama mjane tena;
‘Unasemaje..?’ nikauliza.
‘Nasikia mtaalamu naye amafariki..’akasema
‘Nani mwingine kafariki..?’ nikauliza
‘Sina uhakika lakini…, kuna uvumi kuwa Dalali naye
kafariki…ila ndugu zake hawataki kuliongelea hilo…’akasema mama mjane.
Hapo, nikajua ni kwanini mzee huyu kaingia humo, nikasogea
pale alipo docta na mara kwa nyuma yangu nikaona wapelelezi wakija pale nilipo.
Nikawa najiuliza hao watu wanakuja wodi hiyo kufuata nini,na niliwaacha
wakisema wanarudi ofisini.
WAZO
LA LEO: Tumeshajua kuwa tumekosa, kwanini hatutaki kutubu,
kuomba msamaha kwa wale tuliowakosea, na huenda tumeshapata dalili kabisa kuwa
dhambi ndio sababu ya mitihani tuliyo nayo, bado hatutaki kutubia,..
..kwasababu gani, kwasababu ya mali…!!!, Je tuna uhakika gani kuwa tukiipata mali
hiyo tutaweza kuitumia,…inawezekana ukaipata hiyo mali, lakini usiweze
kuitumia, mwenye mamlaka akachukua roho yako..halahala jamani,..tuwahi kutubia
makosa yetu, kabla milango ya toba haijafungwa, hatujui lini milango hiyo
itafungwa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment