Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, August 21, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-35


Hali ya Dalali iliendelea kuwa mbaya, alikuwa kalazwa chumba cha wagonjwa mahututi na baadae akaingizwa kwenye wodi maalumu, bado akiwa hajitambui, akiwa anapumulia gesi.

‘Hali ikiendelea hivi itabidi tuondoe tu hii mashine, haisaidii..’alisema docta, na wanandugu wakabembeleza, ..na madocta wana muda wao, wakaendelea kumuhudumia hivyo.

Kiukweli…, kwetu sisi tuliomuona hali yake ilipoanzia, bado tulikuwa tunajiuliza, jinsi gani mtu unavyowezakubadilika ghafla hivyo, na kuchungulia kaburi. tujuavyo sisi, hali ya Dalali, ilianza kama mchezo tu… ilianza kwa kwikwi tu,…na kuna muda mimi nilimuona akitoa macho sana, kama kaona kitu,…na kwa mujibu wa wakili wake, yeye alisema kuna muda alimuona akishika upande wa moyo kuashiria anahisi mumivu.

Na watu wa nje ambao hawajui kilichotokea wakawa wanaongea yao mengine, unajua tena.. Dalali ni mtu mashuhuri, habari zake zilishazagaa kila kona,….

‘Je huyo mtu alipatwa na mshituko gani…?’ akauliza docta anayemshughulikia. Tukaelezea ilivyokuwa kwa kila mtu, jinsi alivyomuona, na docta akasema;

‘Yaonyesha huyu mtu alipatwa na mshtuko mkubwa…na hadi kutokea hivi ina maana huo mshtuko umeathiri mishipa ya damu, iri mishipa ya damu, siwezi kusema zaidi,…mpaka vipimo vitokea, bado tunamchunguza, ila kwa hivi sasa tusiendelee kujazana hapa na kuongea maneno ambayo yatamzidishia hali yake kuwa mbaya…’akasema docta.

Na hapo sisi tukatoka nje..na tokea siku ile hatukuruhusiwa kuingia kumuona zaidi ya mke wake, na ndugu yake mmoja wa karibu.

Siku ikapita na siku zikapita, wiki sasa, mara mwezi…

Tuendelee na kisa chetu…

*************

Mimi nikawa nawasiliana na mama mjane, na siku hiyo nilipofika kwake nikamkuta analia,

‘Vipi shemu..kwanini unalia tena, nilishakukataza kuwa hivyo…?’ nikamuuliza

‘Nashindwa kaka yangu…mengine hayavumiliki..’akasema na moyoni nikahisi labda ile ajenda ya kuuza hiyo nyumba imerejea tena,..tulishaomba zoezi hilo lisitishwe mpaka uchunguzi wa kina ufanyike, na kweli mahakama ikaridhia hilo kwa muda, japokuwa benki waliendelea kushinikiza tena baada ya kuona mwezi umepita na hakuna kinachoendelea.

‘Yapi hayo kwani kuna taarifa gani mpya..?’ nikamuuliza.

‘Ama kwa taarifa mpya sijaipata ila nasikia tu, benki wameandika barua ya kulalamika, wakiomba kesi hiyo isikilizwe haraka maana muda umepita, na hakuna jipya..kwahiyo wanaomba ama kesi irejeshwe mahakamani au hukumu ya awali ifanye kazi yake..kwasababu wao wana ushahidi wa kutosha, kuwa deni hilo ni la marehemu..nimesikia nilipokwenda kuonana, na yule wakili…’akasema.

‘Ok..hilo sawa, ..kesi itasikilizwa, lakini yote yanategemea watu wa usalama, kwani waliniambia wanalishughulikia wao wenyewe hilo swala…, na mimi nisiendelea kulishughulikia, nikaona haina haja, ngoja niwaachie wao, maana wamenithibitishia kuwa wao wana ushahid wa kutosha, kuhakikisha haki inatendeka…’nikasema.

‘Wenye pesa ndio wenye nguvu..’akasema mama mjane.

‘Hapana , pesa haiwezi kuishinda haki..’nikasema hivyo.

‘Sawa mimi yote nimemuachia mungu, najua yote yatatendeka kwa mapenzi yake..’akairejea kauli yake ya  mara kwa mara, na mimi nikajua labda hilo ndilo linamliza, lakini…

‘Kama ni hivyo basi, una imani hiyo thabiti,  kwanini unalia, maana naona hata macho yamevimba kwa kulia…’nikasema na kabla sijaendelea  yeye akanikatiza na kusema;

‘Kinachoniliza ni hawa ndugu wa mare-….mume wangu…’akasema nikaona anasita kuitamka hiyo marehemu, nahisi bado akili yake haikubali …

‘Wamefanya nini tena..?’ nikauliza

‘Hawataki mimi niende kumuona mgonjwa, je hivi ni haki hiyo, huyo shemeji ndiye alikuwa msimamizi wa familia, na ndiye aliyekuwa karibu na mimi,leo hii hajiwezi , mimi nikae tu, bila ya kumuona, japokuwa mpaka sasa hajaweza kuongea au kumtambua mtu, yupo yupo tu…’akasema

‘Kwanini sasa wanakukatalia…?’ nikauliza

‘Ndio hicho kinaniliza,…na  kwanini wani zalilishe hivyo…’akasema na mimi hapo bado nikawa gizani, na alipoona nasubiria maelezo yake zaidi akasema;

‘Mimi mjane, ..na watoto wangu hawa mayatima, nina uwezi gani wa kumfanya huyo mtu awe katika hiyo hali…je kweli ni mimi nilisababisha hayo yote…eti pia ni mimi niliyechangia mume wangu kufariki…leo hii nimepakaziwa maneno mengi zaidi ya ile ya kwanza..hadi mimi sasa naitwa eti mimi ni mchawi…’hapo machozi yakaanza kutoka.

‘Shemu, maneno sio njia,..nakuomba tena na tena, usiyaweke akilini mwako yakakuvunja imani yako, kwenye vita hapakosi mambo kama hayo, nia yao ni kukuvunja nguvu, huelewi hilo…kumbuka dada, ..hivi ni vita vya kuitafuta haki yako na watoto wako, kamwe usikate tamaa…’nikasema.

‘Unasema tu hivyo ndugu yangu, maneno mengine yanaumiza…fikiria nilikwenda hospitalini, na sikuenda kwa hiari yangu, maana walishanikataza hao ndugu zake kuwa nisifike hapo kumuona huyo mgonjwa,.’akasema.

‘Sasa kwanini ulikwenda..?’ nikamuuliza

‘Docta alinipigia simu akasema. Dalali kuna muda alipata ufahamu kidogo, akawa analitaja jina langu…kwahiyo akaona labda nikifika hapo, inaweza kusaidia akaweza kuzindukana, au hata akizundukana, huenda kuna ujumbe anataka kunipatia..’akasema

‘Mhh, sasa kwanini hukuwaambia hao ndugu zake kuwa umeitwa na docta, na huenda kuwepo kwako kutasaidia mgonjwa kuzindukana..’nikasema.

‘Nilijaribu kuwaambia hivyo, lakini hakuna aliyetaka kunisikiliza, walinitoa mle hospitalini kama mwizi, hata docta alipofika,…alikuta nimeshafukuzwa mbali, na nje nikakutana na watu waliotayarishwa kunizomea,…wakiimba ‘mchawi , mchawi…’…hebu fikiria kama ingelikuwa wewe ungekuwa na ujasiri gani wa kuyavumilia hayo.

‘Mhh..oh....huenda ikangelisaidia kweli kumzindua, kama alivyoshauri docta, ina maana hao ndugu hawataki ndugu yao apone …’nikasema.

‘Mimi nilikwenda nikijua hivyo, nikafika na kuongea na mlinzi kuwa mimi nimeitwa na docta nije nimuone mgonjwa,  mlinzi  akaniruhusu, ile nataka kuingia tu, mmoja wa ndugu yao, sijui ndiye aliwekwa kulinda hapo nje,akaniona,.. akaja kunifurusha,, huku akiwaita wengine, ni kama walijiandaa kunifanyia fujo…’akasema

‘Ina maana muda huo docta hakuwepo…?’ nikauliza

‘Docta aliyenipigia simu kumbe alishatoka, ila alicha maagizo kuwa mimi nikifika nijitahid kukaa hapo karibu na huyo mgonjwa…tatizo nahisi huyo docta hakuwaambia wengine,au hata sijui….na kwanini hakuwaambia hao wanandugu kuwa, mgonjwa alinihitajia mimi…’akasema.

‘Huyo docta unamfahamu na una namba yake siku zote..?’ nikamuuliza.

‘Hapana, ila alijitambulisha hivyo, kuwa yeye ni docta anayemshughulikia Dalali…’akasema.

‘Oh…nahisi hapo kuna jambo..huenda hata huyo docta aliyekuita akawa ni docta au sio docta, huenda kuna mtu mwingine alipanga hilo lifanyike, ..lakini najiuliza ili iweje..nahisi hapa kuna kitu…nahisi…ngoja tutakuja kuliona hilo,...’nikasema hivyo

‘Yaani ni aibu…aibu, …unajua nilivyojisikia…, hebu lifikiria wewe hivyo, kama ingelikuwa wewe umfanyiwa hivyo..jamani mimi..nimewakosea nini hao watu..na hadi sasa watu wengine wameshanifikiria hivyo, …ujue Dalali ni mtu maarufu sana, ana washabiki wengi..yaani ungeliona hilo tukio, aah.., walinifurusha mimi kama mwizi,…huku wakiananiita mchawi….eti nimefika kumuua ndugu yao.

‘Duuh…hakuna askari aliyekuwepo karibu, maana Dalali analindwa na askari, kwasababu yeye ni mtu anayetakiwa na watu wa usalama, kuhojiwa, hatakiwi kukimbia au kitokee kitu kibaya dhidi yake..?’ nikauliza

‘Sikuwahi kumuona huyo askari..’akasema.

‘Pole sana…’nikasema.

‘Nilijisikia vibaya sana, ..haya mambo nilijua wanafanyiwa wazee,..kumbe hata sisi wakina mama…oh, sijui nitaishije mimi jamani,..maana kila nikipita mahali watu wakiniangalia nahisi ni yale yale, kumbe watu wengine wanauwawa tu bure kwa shutuma za uwongo..hebu fikiria, …..’akasema kwa uchungu.

‘Pole sana…’nikasema

‘Kinachoniuma zaidi …wamefikia, kuwaita hata watoto,…hawa watoto wangu eti ni watoto wa mchawi, wameanza kujenga fitina kwa watoto wengine wadogo, wawe wanavumisha hivyo, jamani hata hawa watoto wana kosa gani…’akainamisha kichwa chini.

‘Shemu…mmh samahani mimi…, nimezoea kukuita hivyo, ‘nikasema na kabla hajasema neno, nikaendelea kuongea;

‘Hizo ni mbinu za maadui zako za kukuvunja nguvu,…siri ya ushindi ni kutokuvunjika imani yako uliyo nayo, hivi wakikuambia wewe hivyo kuwa wewe ni mchawi kweli utakuwa hivyo,…mambo kama hayo yakuongezee ujasiri, na nina imani mwisho wa siku utasimama shujaa…’nikasema kumpa nguvu.

‘Lakini inauma sana, sijui kama nitaweza kuwa na ujasiri huo tena…’akasema

‘Nikuulize tu…wakati hayo yanafanyika, hao watu,..unaweza kumkumbuka yoyote miongoni mwao, je hao ndugu kuacha hao ndugu za mume wako, hao uliowakuta nje, unaweza kumgundua yoyote mwingine unayemfahamu,..?’ nikamuuliza

‘Ningeliwezaje , nilichanganyikiwa kwakweli,…halafu iweje, nikawashitakie au, hapana mimi siwezi kufanya hivyo,..kama ni kuwajua, haina haja, ni ndugu za mume, ndio chanzo cha hayo yote, lakini siwezi kabisa kuwashitaki,…’akasema.

‘Unajua kuna kitu nimekiona hapa,…hao watu ni washabiki wa muhalifu anayetaka kutengeneza uwoga fulani dhidi yako…na hatuwezi kusema ni washabiki wa Dalali….kuna muhalifu ….kawapanga hao watu wafanye hivyo..sasa ..ngoja…’nikasema na kuchukua simu.

Niliwapigia watu wangu nikawaelekeza jambo, halafu nikarejea kwa mama mjane, naye akaniuliza;

‘Unataka kufanya nini, wewe si umesema polisi wamekukataza kuingilia haya mambo…?’ akaniuliza

‘Hii ina maanisha,hizo vurugu zitakuwa zimepangwa na hao watu tunaowatafuta, kwahiyio mmojawapo, au wote wapo karibu,…na najaribu tu kubahatisha, huenda miongoni mwa hao watu waliokufanyia vurugu wanaweza kutusaidia kuwapata hao watu…’nikasema.

‘Kwanini usiwaambie polisi..wao waifanye hiyo kazi…?’ akaniuliza.

‘Polisi hawataki mimi niwafundishe kazi…’nikasema  hivyo tu, na kabla huyo mama hajasema neno, nikaendelea kuongea

‘Unajua wao sasa hivi wanatengeneza propaganda potofu dhidi yako…wameshaanza kuogopa,…wanatumia ile mbinu ya ukitaka kumuua mbwa kwanza umuite majina mabaya…’nikasema

‘Ina maana wanataka kuniua mimi…?’ akaniuliza

‘Sio lazima kukuua,..kwa maana ya kuua… ila kukumaliza nguvu…ila usiogope, nitaongea na wale wapelelezi,.. ubaya wao utashindwa, maana haki haipo mbali muhimu kwa hivi sasa, kama nilivyokuambia awali..kuutafuta ukweli wote unaoufahamu ili uje kutusaidia kwenye ushahidi, ungamgundua kiongozi wa hizo vurugu ingelisaidia sana…’nikasema.

‘Nilimuona mtu mmoja, wakati mwingine huwa anatembea na Dalali..ni msaidizi wa Dalali,…halafu nimekumbuka, wakati nakimbia, nilipogeuka nyuma, nilimuona mzee Mtupe..aliponiona, akageuka kama vile hajaniona…’akasema.

‘Mhh…ok…mzee Mtupe eeh,alikuwa kwenye kundi au ..?’ nikauliza
‘Hapana yeye nilimuona mbali na hilo kundi, yawezekana ndio alikuwa anakuja hospitalini, akaiona hiyo vurugu, na pale asingeliweza kufahamu kuwa mimi ndiye nilikuwa nafanyiwa hizo vurugu, labda walikuja kumuambia baadae, maana mimi nilikuw nakimbia mbali na hapo, baada ya kuwaponyoka,...’akasema.

‘Lolote lawezekana…mzee mtupe…huyu mzee, huyu mzee..ok, ngoja nitampitia, ila kila tukio likifanyika hakikisha unakusanya ushahidi, hujapata kitu chohote cha kusadia huko ndani, popote pale ..?’ nikasema na kumuuliza hivyo.

‘Nitaupatia wapi tena ushahidi mwingine…, mimi..nilijua zile karatasi zingelisaidia, ..kumbe bado haziwezi kufanya lolote ..’akasema

‘Bado zitasaidia sana, …sema wao hawajanipatia hizo barua, nikaweza kuzipitia vyema, nahisi kuna jambo ndani yake,…lakini ngoja nitaona ni nini la kufanya,…ila nataka nionane na huyo mzee…’nikasema

‘Mhh..mimi bado ninaona giza,…nahisi ndoto mbaya mbaya, na huamini, huyo mzee nimeshawahi kumuota, akiwa kageuka sura ya kutisha, lakini kwangu ndoto ni ndoto tu…’akasema

‘Uliota hivyo, ulimuota huyo mzee, mmh, labda ni kwa vile ilitokea hilo tukio, halafu ukamuona,..usijenge hisia hizo mbaya, mimi nataka kumuhoji, kama anaweza kutusaidia kwenye ushahidi ..’nikasema.

‘Hata sijui, wakati mwingine…nahisi kukabwa..hata sielewi..na kila ikitokea hivyo anayeniokoa ni mume wangu…na akishaniokoa ananiambia…usivunje ahadi yako..au, usiniache, au uwe makini,..kitu kama hicho, sielewi,..kifupi mimi  bado..nina mashaka kweli…’akasema

‘Yah…usivunje ahadi yako, maana yake, nyie mlimuamini kuwa yeye ni mkweli kwenu, hasemi uwongo,..au sio? ..je leo iweje asingiziwe hilo deni…natafsiri kihivyo,…na hiyo usiniache, ..ni hii nyumba, hii nyumba kwa hivi sasa yasimama kama yeye, ukiacha ikichukuliwa umemuacha yeye, na uwe makini,..ni onyo tu, nahisi hivyo…’nikasema.

Huyu mama akaniangalia kwa makini…halafu akasema;

‘Umesema kweli…lakini tufanyeje sasa.., maana wakili alivyoniambia, bado sisi hatujaweza kuupata ushahidi wa kutosheleza, hizo barua hazina uzito wa kuweza kushinikiza hilo deni, na wakili wao kasema hawataweza kutumia ushahidi walioupata dhidi wa ushahidi wa benki tukashinda…’mama mjane akasema.

‘Najua sana hilo….kiukweli, mimi niliwaambia hao watu wa usalama,..cha muhimu ni kuhangaika kuwatafuta hao watu wawili..bila hao watu wawili , bado tutakuwa hatuna ushahid wa kutosha, maana ushahidi wa kimaandishi umeshaharibiwa wote..nimeshafika hadi huko benki hakuna …mtandao wao wa zamani uliharibika, wanatumia mtandao mpya…kumbukumbu za mafaili, hazipo, wanasema kulitokea moto, kumbukumbu halisi za karatasi zote ziliteketea…’nikasema.

‘Kwahiyo …mimi hapo naona hakuna jipya,…’akasema mama mjane.

‘Yah….ndio maana mimi nataka hao watu wawili, na watatu wao ni Dalali, wasimame kizimbani, ..hao wakiulizwa maswali, tutawanasa tu..’nikasema

‘Je ukikutana nao utawezaje kuwashawishi waongee ukweli, wewe unawafahamu jinsi walivyo,..ni wajanja , Dalali kasingiziwa…’akasema

‘Ujanja hausaidii….’nikasema.

‘Na hao watu wa usalama,  walisemaje, jinsi walivyomuhoji huyo mtaalamu, hawajakuambia lolote, alichoongea wakati wanamuhoji...?’ akaniuliza.

‘Hawajaniambia lolote, …hata nikiwauliza hawataki kusema,… wanasema hiyo ni kazi yao kwahivisasa…’nikasema

‘Mimi nilijua watakushirikisha baada ya kugundua kuwa uliyosema yaweza kuwa ni kweli…’akasema

‘Nawafahamu sana hao watu, kwa namna moja, hawataki kuonekana hawawezi kazi, kwa namna nyingine wananichukia kwa vile, eti napenda kuingilia majukumu yao..lakini ngoja tuone…’nikasema

‘Mhh..hata sijui, tufanyeje sasa, mimi naona tumuechie mungu tu, …’akasema mama mjane.

‘Usikate tamaa, kama tuliweza kumnasa Dalali, japokuwa hajakubali kabisa.., lakini kwa kupitia kwake, tumeweza kubaini kuwa kuna udanganyifu kwenye hilo deni,…mpaka polisi wakawa upande wetu, nina imani kwa kupitia hao watu wengine wawili,.. tukiwapata tu…tutakuja, kubaini ukweli…’nikasema.

‘Hivi wewe ulishawahi kukutana na huyo mtu wa benki….?’ Akaniuliza.

‘Hapana, …wewe unamfahamuje  huyo mtu?’ nikamuuliza

‘Ni mjanja kupindukia, kasomaa…na anapenda kutumia elimu yake kwa faida.., na anajua jinsi gani ya kujilinda, kujihami hivi....ukiongea neno la ovyo keshakugundua wapi unaelekea,..ana akili za ajabu-ajabu, kwa jinsi alivyo, hata watu wanamuogopa, maana kwanini anaweza kugundua unachofikiria dhidi yake…’akasema  na mimi nikasema;

‘Hata mwenye akili sana, kwenye haki atagwaya tu,..naombea nikutane naye, nimjue vizuri..’nikasema.

Na mara simu yangu ikaanza kuita, ilikuwa namba ngeni kwenye simu yangu…nikasema;

‘Mhh…hizi namba ngeni kwenye simu yangu sizipendagi,,..mara nyingi zinakuwa na mitihani fulani, nahisi kuna jambo..’nikasema nikiiweka simu hewani.

‘Halloh, mtu wa jamii..mimi ni mpelelezi ninayeshughulikia ile kesi ya mama mjane..nakuhitajia hapa ofisi kwangu haraka iwezekanavyo…’sauti ikasema

‘Kuna nini mkuu…si nyie mlishasema mimi nisijishughulishe na chochote au..’nikasema

‘Ndio…hutakiwi, ila kwa hivi sasa tunakuhitajia kwa haraka kidogo, ..ni katika kutimiza wajibu wetu..’akasema huyo mpelelezi

‘Haya ninakuja afande, kwahiyo niage kabisa, isije ikawa nakuja kuwekwa ndani…’nikasema na hakujibu kitu,  simu ikakatika.

Nikamuangalia mama mjane, naye akaniangalia, akiwa na shauku ya kujua kitu geni nimeambiwa huko…

‘Ni nani hao…?’ akaniuliza

‘Wananihitajia huko kituoni, polisi…’nikasema na kumuaga mama mjane,..

‘Kuna la heri huko..?’akasema kwa kuuliza

‘Hata sijui…ngoja nifike nitakufahamisha kitakachotokea,...’nikasema nikianza kutoka na wakati natoka mara simu ya huyo mama mjane ikaita..nilikuwa sina muda tena hapo mimi nikatoka nje kwa haraka.

Na wakati natoka nje, nikamuona Mzee mtupe akiwa anakuja kuelekea kwenye hiyo nyumba,, aliponiona tu akashtuka, ..hakuwa na ujanja, maana tulishakuwa uso kwa uso .
‘Oh, bahati mzee, nataka kuongea na wewe…’nikasema.

‘Mimi!!!…kuhusu nini, mimi sijui lolote, na..na…nina haraka, nataka kusafiri…’akasema

‘Lakini nakuona kama unakuja hapa kwa huyu mama mjane au, unasafiri kwenda wapi…?’ nikauliza.

‘Ndio, ndio..Nataka kumuaga huyo mama, …’akasema huku anatembea na mimi nikawa najaribu kumfuatilia nyuma.

‘Wapi huko unaposafiri,,..?’ nikamuuliza na hakutaka kabisa kuongea na mimi

Cha ajabu sasa, badala ya kungia hapo kwa huyo mama akapitiliza, alionekana ana haraka sana…na mimi nikachukua simu yangu nikampigia kijana wangu mmoja amfuatilie huyu mzee.

NB: Mhh, mambo yanakuja tu,


WAZO LA LEO: Hata ukiwa mjanja vipi, hata ukiwa na akili vipi, huwezi ukafahamu kila kitu..huwezi ukawazidi wote, na hasa pale akili zako, na ujanja wako unapouelekeza kwenye mabaya badala ya mema.
Ni mimi: emu-three

No comments :