‘Kuna uvumi kuwa Dalali naye kafariki….’
Hiyo ilikuwa sauti ya mama mjane iliyonifanya nihisi
mwili ukiinisha nguvu…shahid muhimu kama huyu kafariki, na ndiye tulitegemea
kuwa atatusaidia kutoa ushahidi…sikuweza kusikiliza mengine aliyokuwa
akinieleza, maana kwa muda huo, hisia ziliniambia niangalie nyuma….
Tuendelee na kisa chetu…
************
Niliwaona wapelelezi wale wawili wakija pale
niliposimama kwa mwendo wa haraka, kwa jinsi walivyokuwa wakija, nikajua kuna
jambo limetokea na huenda linanihusu na mimi, na mawazo ya haraka, yakahisi hao
watu wanakuja kunikamata mimi, kwa jinsi walivyokuwa wakija uelekeo wangu..lakini
kwa kosa gani..nikajiuliza hivyo tu.
Wakati nawaza hayo…, yule mlinzi, ambaye awali
nilikuwa nimemkweza kwa kumuita docta,… yaonekana labda anawafahamu wawili hao…,
kwani nilimuona naye akiwaangalia hao wapelelezi kwa uso wa mashaka..akiwa kaduwaa..
Wale wapelelezi walitukaribia, yule mlinzi sasa akawa
ananiangalia mimi kwa kunishuku, nahisi alikuwa akiwaza ninayowazia mimi, kuwa
huenda hao watu wanakuja kunikamata mimi, kama kweli anawafahamu kuwa ni
wapelelezi, maana wao walivalia kiraia.
‘Umefanya nini..?’ akaniuliza huyo mlinzi, na kabla
sijamjibu kitu, mara jamaa hawa hapa, mbele yangu..…
Sasa cha ajabu, walinipita mimi, wakaelekea pale
aliposimama huyo mlinzi, sasa ikawa zamu yangu kutaka kumuuliza huyo mlinzi wa
hapo hospitalini,..’na wewe umefanya nini’…lakini kabla mawazo hayo hayajatoka,
mara mlangoni wa hiyo wodi ukafunguka na kwa haraka akatoka mtu.
Huyo mtu kainamisha kichwa chini…, kashikilia nguo
mkononi, na kipande cha sabuni, kama
vile anakwenda kufua, huku kajifunga shika na jingine kajifunika sehemu ya
kichwani…nikahisi kitu kichwani,…ule utembeaji..lakini sikuwa na uhakika na
wazo hilo.
Unajua hapa ni hospitalini, wagonjwa wengine huwa
wanaweza kuwa kama wamechanganyikiwa, kwa muda ule hakuna aliyeshuku kitu, huyo
mtu hakutaka hata kutuangalia, kwa haraka akawa anatembea, kuelekea sehemu wanapofulia
nguo, kwanza akaanika nguo moja ilikuwa mbichi, nyingine akabakia nazi
mkononi..na huyo mlinzi, akasema;
‘Muda huu, haturuhusu kufua ngua unasikia wewe
mgonjwa, huu sio muda wake…hizi za kufua utafua baadae…’akasema huyo mlinzi, na
kabla hajajibiwa na yule mtu, askari hawa wawili wakajitambulisha, maana
walikuwa wamevalia kiraia, ilionekana kama huyo mlinzi anawafahamu. Hakujali kuangalia
vitambulisho vyaoa, akasema;
‘Afande ni wasaidie nini…?’ akauliza, lakini sasa
macho yake yalikuwa yakimuangalia yule mgonjwa, ambaye alionekana kukaidi..sasa
alikuwa karibu na bomba, ..na …
‘Kuna mgonjwa wetu kalazwa hapa, tuna haraka kidogo…’wakasema
wale wapelelezi.
‘Mgonjwa wenu gani huyo.., mimi siwezi kujua hilo
labda …’kabla hajaelezea zaidi mpelelezi akaendelea kuongea.
‘Huyo mgonjwa kaletwa huku bila taarifa yetu, kuna makosa
yamefanyika hivyo, sasa twataka kuthibitisha tu, tumuone kama yupo humu au la..ni jambo la haraka
kidogo…’akasema mpelelezi…sasa akielekea mlangoni, hakusubiria huyo mlinzi,
aulizie kwa dakitari..
‘Ni muhalifu au…?’ akuliza yule mlinzi akimuangalia
huyo mpelelezi mwingine.
‘Ni mshukiwa …wewe kamuone docta wako, lakini sisi
twataka kuingia,..huyo docta atatukuta huko ndani, kama huyo mtu wetu yupo humo
ndani…je huyo docta yupo wapi,..?’ akauliza huyo mpelelezi mwingine wakati yule
mwingine alishaingia ndani.
‘Mhh…mimi nimeingia leo, sina taarifa za tokea
jana,..unajua tena,..mimi kazi yangu ni kulinda hapa mlangoni..’akasema lakini
sasa akawa anaangalia kule alipoelekea yule mtu aliyetoka humo wodini,
akionyesha uso wa mashaka.
‘Hawa wagonjwa wengine bwana…sijui kaelekea wapi,..nimemuambia
muda huu hakuna ruhusa ya kufua,..au hata kutoka nje..lakini
hajanisikia,..sijui ni kiziwi huyu mtu…sijui ni yule mgonjwa
aliyechanganyikiwa, niliwaambia juzi kuwa huyo mgonjwa hatakiwi kwenye hii
wodi, unaona sasa..sijui kaenda wapi…’akasema huyo mlinzi, sasa akitembea
kuelekea kule alipoelekea huyo mtu.
Haikupita muda, huyo mlinzi akarudi kashikilia shuka…huku akionyesha uso
wa kushangaa. Na mimi nikamuuliza;
‘Vipi…’ nikasema hivyo, na mimi nikiwa na mashaka
fulani…
‘Yule mtu haonekani na hii shuka ndio alikuwa
kajifunga, …sijui kachanganyikiwa, hata sijui..ngoja niwasiliane na wenzagu
getini…’akasema sasa akipiga simu.
‘Mzee
Mtupe…’nikasema hivyo tu bila uhakika
Wkati huo yule mpelelezi mwingine alikuwa mlangoni
akitaka naye kuingia, aliposikia hivyo akanigeukia, na kuniangalia…
‘Vipi kuna nini…?’ akauliza.
‘Hata sijui..hisia zangu zanitatanisha, mwenzako
anasemaje huko ndani…?’ nikauliza.
Yule mpelelezi akawa kafungua mlango, akiangalia
ndani…na mimi nikasema kwa sauti sasa;
‘Ni bora , muhakikishe, hatujui huyo mzee kafanya
nini humo ndani, na kwanini katoka kinamna hiyo,..huenda mkakuta…’nikasema hivyo
na huyu mlinzi akanikatisha na kusema;
‘Sio yule mzee bwana…huyo mzee atakuwa huko huko
ndani, hajatoka…’akasema
Yule mpelelezi aliyebakia nje naye akaingia huko ndani,
na haikupita muda, mmoja akatoka, na kuniangalia;
‘Mbona Dalali hayupo humu ndani…’akasema
‘Yupo nani kitandani kwake..?’ nikauliza
‘Unasema ni nani huyu mzee…, unamfahamu vyema, umemjuaje..?’
akaniuliza maswali hayo mfululizo. Bila kujibu swali langu.
‘Namjua, lakini simfahamu sana,…nilimuona akija
kuelekea huku, nikawa najiuliza anakuja huku kufanya nini, na wakati namuuliza
huyu mlinzi, ndio nanyie mkafika hapa..’kabla sijamaliza huyo mlinzi akasema;
‘Wewe si umesema huyo mzee ni baba yako…?’ akauliza
huyo mlinzi kwa uso wa kushanga.
‘Nilikuwa nataka kujua anachofuata humo ndani, …ndio
maana nikakudanganya hivyo,ila niweze kuonana naye, ..mimi nafahamu wapi anapoishi,
anaishi karibu na yule mama mjane tunayefuatulia kesi yake..’nikasema na
mpelelezi akasema;
‘Oh….’akasema hivyo na akawa anapiga simu yake
kuelekeza watu wake, na alipomaliza, akageuka kuniangalia mimi.
‘Hebu nielezee vyema, ..’akasema huyu mpelelezi
akinishika mkono kunisogeza pembeni, mabli na huyo mlinzi.
.
‘Afande utakuja kunielewa tu…mimi najaribu kuutafuta
ukweli kivyangu, bila kuingilia kazi yenu, nikiwa tayari nitawaambia kila kitu.
‘Unasikia hapa tuna…’kabla hajamaliza docta akaja kwa
haraka akiongozana na wasaidizi wake, wakatupita na kuingia ndani,..yule mlinzi
akawa anahangaika naye kivyake kipiga simu huko getini.
‘Hajatoka mtu mzee huko getini…kuweni
nauhakika,..kuna tatizo huku ndani,…ndio afande, bora uje…’akasema huyo mlinzi.
Sasa akionekana kachanganyikiwa.
Yule mpelelezi, akasema;
‘Kuna tatizo kubwa,…na ni kwanini umefanya yale
tuliyokukataza, unajua mimi nitashindwa kukulinda tena, mwenzangu hakuelewi…’akasema
‘Kwani mumegundua kuna tatizo gani mkuu..?’ nikauliza, na huyo mpelelezi
akawa hanisikiliza alikuwa akihangaika kupiga simu kwa watu wake…na mimi
nikasema;
‘Je ningelikaa kimia haya yangelijulikanaje…, au….ila
mimi sijakiuka maagizo yenu, nimefanya kazi yangu kama raia mwema, kuchunguza
tukio, ili niwe na uhakika nalo, baadae nije kuwaambia.
Mpelelezi sasa akawa anaendelea kupiga simu
kuwasiliana na watu wake…na baadae akaingia ndani ya wodi, bila kunisemasha
kitu.. na mimi nikataka kumfuata, huyo mlinzi akanizuia;
‘Wewe huwezi kuingia ndani kwa hivi sasa..’akasema.
‘Wewe vipi, huoni tupo kazini, au unanielewaje mimi…?’
nikamuuliza, na huyo mlinzi, akawa kama hanisikiliza. Nikataka kuingia
akanizuia..
‘Sasa kwanini unanizuia hujui mimi nipo na hao watu,
au,..’nikasema, lakini sikutaka kubishana naye, nikasubiria tu hapo nje…,
baadae nikaona askari wengine wakifika, na haikupita muda mpelelezi akatoka ,
sasa akiwa na docta wakawa wanaongea;
‘Anaweza kupona..?’ akauliza
‘Siwezi kuwa na uhakika,…sumu aliyopewa ni kali sana,
ngoja tuone, kama haijafanya madhara yake…’akasema
‘Lakini ni nani huyo mtu, maana sio…?’ akauliza
mpelelezi kabla hajamaliza docta akasema;
‘Kwa taarifa za kadi yake anaitwa..mmh…’akataja jina,
halafu akamalizia kwa kusema
alimaarufu,.. Dalali…’akasema docta
‘Hapana…haiwezekani akawa ndio yeye, mimi ninamfahamu
huyo Dalali, huyo sio yeye,..kuna makosa yamefanyika hapo..’akasema mpelelezi
‘Hizi hapa ni nyaraka zake, tulizozipokea na huyo
mgonjwa, sasa hatuwezi kujua kuwa ndio yeye au la,…’akasema docta docta
akionyesha kadi aliyoandikiwa.
Mpelelezi akaikagua ..na kutikisa kichwa cha
kushangaa
‘Mhh..kuna tatizo hapa…’akasema mpelelezi.
‘Mimi sijui…’akasema Docta akichukua ile kadi yenye
maelezo.
**********
Mpelelezi akawa sasa anapokea siku kutoka kwa watu
wake,…na badae alipotulia,akanifuata, na kuniambia;
‘Usiondoke,…nina maswali ya kukuuliza wewe, nahisi
kuna kitu unatuficha, huyo mzee katoweka watu wake wa karibu wanadai mzee huyo
aliaga nyumbani kwake kuwa anasafiri, na wewe umesema umeomuona…’akasema
‘Ok, kwahiyo kwa hivi sasa atakuwa yupo safarini huko
aliposema anasafiri..’mimi nikasema hivyo.
‘Tumeshaweka watu huko njiani wanafuatilia magari
yote yanayokwenda huko..’akasema
‘Yeye sio mjinga, atakuwa ametafyta usafiri wa haraka
ili afike huko mapema…’nikasema na huyo mpelelezi akawa anapiga simu kwa watu
wake..na mimi nikasema;
‘Kwanini kwanza unasema kuna kitu nawaficha,
niwafiche kitu gani mimi, wakati hili swala linaniumiza kichwa na mimii, huyo
mzee nimemuona mimi mwenyewe akielea huku na nikamuona akiongea na huyu mlinzi
akaruhusiwa kuingia ndani…, muulizeni hata huyo mlinzi…?’ nikamuuliza
‘Wewe ulituacha pale ukawa unamfuatilia huyo mzee,
kama ndio huyo mzee kweli,…ni kama ulifahamu kuna jambo linakwenda kufanyika,
hapo mimi unanitia mashaka, ulijuaje hayo yote…?’ akaniuliza
Hapo ikawa sina budi… nikamuelezea ilivyotokea tokea awali
hadi nikamtuma mtu wangu wamfuatilie, huyo mzee…mtu wangu akasema huyo mzee kaelekea
huku hospitalini…nikawa na mashaka nahilo..na bahati nzuri ndio nikamuona…
hapo, nikahisi kuna jambo linaloendelea;…’nikatulia
‘Ok…’akasema huyo afande hivyo.
‘Nahisi huyu mzee, alikuwa kwenye wodi ya huyo
marehemu, na alipotoka huko ndio akaelekea huku…kwa mawazo mengine, yeye
alitaka kumuwahi huyo mtu kabla nyie hamjafika hapa…’nikasema
‘Lakini…’mpalelezi akataka kuongea lakini
hakuendelea..baadae akasema;
‘Kwahiyo inavyoonekana huyo mzee, ndiye kamnywesha
huyo mgonjwa sumu, kwanini atake kumuua huyo mtu…?’ akauliza huyo mpelelezi.
‘Hiyo ni kazi yenu kutafuta, nikianza kuelezea ninavyofahamu
mimi ninaweza kutunga kitabu, ila…muhimu ni kumtafuta Dalali…..’nikasema
‘Dalali, Dalali…sijui kwanini walinzi hawakuwa makin
naye,…wao wanasema kwa hali aliyokuwa nayo, asingeliweza kufanya lolote ndio
maana hawakutaka kumfuatilia,…’akasema.
‘Huyo mlinzi aliyekuwa anamlinda mnamuamini kweli..?’
nikauliza
‘Kwanini unasema hivyo, yule mtu wetu, hawezi….’akataka
kuendelea na mimi nikamkatiza kwa kusema;
‘Ndio hivyo, kwa hisia zangu, nahisi huyo mzee,
labda,…kwa hoja nyingine, labda alitumwa kuja kumuua Dalali,…lakini akakosea,
lakini hapana kwanini amuue Dalali, mmh, nahisi hivi, huenda, huyo mtu
alitakiwa auwawe.., ili hiyo propaganda ya Dalali kufa iaminike,… ije kuonekana
kuwa kweli Dalali, kafariki…’nikasema.
‘Sijakuelewa hapo…’akasema mpelelezi.
‘Dalali aliletwa hapa, akiwa ana hali mbaya,..kwa
mujibu wa taarifa za hospitalini alipokuwepo awali..kama ni kweli alikuwa hivyo,
atawezaje kutoroka, na je ni kweli alifikishwa hapa,…?’ nikauliza;
Wakati huo huyo mpelelezi mwingine alikuwa akiongea
na docta, na wakawa kama hawaelewani jambo….na baadae huyo mpelelezi akaja pale
tulipokuwa tumesimama, …akasema;
‘Mhh,.. huyo mgonjwa hali yake ni mbaya sana, sijui
kama atapona, na wagonjwa walimuona huyo mzee, aliyeingia awali,…wanasema huyo
mzee, alifika akawa anamywesha huyo mgonjwa juice..maana huyo mgonjwa alikuwa
hajiwezi, akawa kama anamlazimisha kunywa....’akasema mpelelezi.
‘Huyo mgonjwa alifika lini…kwa taarifa ya docta..?’
nikauliza
‘Ni jana, muda ambao Dalali alikuwa analetwa huku…’akasema
mpelelezi
‘Kwahiyo Dalali hakuwahi kufikishwa hapa hospitalini,
na huyu mzee basi atakuwa analifahamu hilo, au sio…?’ nikauliza
‘Ndio hivyo…aliyeletwa hapo ndio muhanga wa hiyo
sumu, lakini vielelezo ni vya Dalali…’akasema
‘Gari gani lilimchukua Dalali kule hospitalini…?’
nikauliza
‘Ni gari lililotafutwa na wanandugu sio la wagonjwa,…’akasema
‘Sasa kwanini, ,maana huyo ni mshukiwa wenu, si
alikuwa kwenye ulinzi wenu au…?’ nikauliza
‘Unajua kutokana na ushahidi uliopatikana, hatukuona
umuhimu wa kumshikilia Dalali kama mshukiwa, kwahiyo hata walinzi wetu,
walishaondoka, tungemshikilia kwa kosa gani…’akasema huyo mpelelezi.
‘Oh, afande..afande…sasa hamuoni kuwa nyie ndio
mumesababisha haya yote..’nikamlaumu na yeye akaniangalia kwa uso wa
kutahayari, akasema;
‘Sisi tunafanya kazi zenu kwa utaratibu maalumu, huyo
sio mhalfu, na hakuna jambo la kumshikilia kama muhalifu….’akasema
‘Sasa mumeweza kuongea na hao ndugu waliomchukua,..?’
nikamuuliza
‘Kwa kosa gani sasa…?’ nikamuuliza
‘Udanganyifu…walitakiwa wamlete huyo Dalali hapa, lakini
hawakufanya hivyo, ni kwanini walifanya hivyo…hapo ndio tutaanzia kesi
yetu,..maana sasa imeleta sura nyingine..hiyo ni kazi yetu, huna haja ya
kuniuliza hilo swali..’akasema huyo mpelelezi
‘Lakini
tutawakamata wote…’akasema huyo mpelelezi mwingine akiendelea kuwasiliana na
watu wake.
‘Kwahiyo sasa mnasemaje, maana mliniambia hii kesi
haina mshiko, je kwa haya yanayotokea bado mtaendelea kuwa na msimamo wenu huo,
na..…?’ nikauliza
‘Hatujajua kuwa hili lilitokea lina uhusiano na hiyo
kesi yako,. Kama tutathibistiha hivyo, basi tumeshajua kuwa kuna kesi ya
kufuatilia…’akasema huyo mpelelezi. Na mara docta akafika, na kumuita huyo
mpelelezi pembeni, wakawa wanaongea.
Baadae huyo mpelelezi akamuita mwenzake, wakawa
wanaongea kwa muda hivi, baadae docta akaambiwa jambo, na huyo docta akaondoka
kwa haraka
‘Unamuamini huyo docta lakini..?’ akauliza mpelelezi
‘Namuamini, hakuna shida, sasa hivi tutafuatilia kitu
kila kitu…’akasema huyo mwenzake,
‘Kwahiyo sasa hivi tunaweza kuondoka, …’akasema huyo
mpelelezi, akimgeukia huyo mlinzi;
‘Sasa wewe sikiliza…hapa atakuwepo mtu wetu..mtasaidiana
naye, na…kama atakuja ndugu wa huyo mgonjwa, mwambie aongee na huyo mtu wetu,
unasikia…’akaambiwa, na huyo mlinzi akasema.
‘Sawa afande…’akasema huyo mlinzi kiukakamavu sasa
maana awali alishaanza kuogopa.
‘Tunakwenda wapi sasa..?’ nikauliza
‘Inabidi twende wote kituoni, kuna maswali
tunahitajia majibu kutoka kwako…’wakasema na mimi sikutaka kuwakaidi,
tukaelekea kwenye gari lao na kuelekea kituoni.
‘Wewe mtu wa jamii unasemaje sasa..?’ akaniuliza na
mpelelezi mwenzake ndiye akamuelezea yale niliyomuambia;
‘Mzee Mtupe..huyo mzee, anataka nini..?’ akauliza
mpelelezi.
‘Mimi nahisi anatumiwa, na ..yawezekana ni mpelelezi
wa mshukiwa mkuu..’nikasema.
‘Mshukiwa mkuu kwa mtizamo wako ni nani…?’ akaniuliza
mpelelezi
‘Kama ningekuwa namfahamu kesi hii ingelikuwa
imekwisha, na siwezi kusema maoni yangu kwa hivi sasa, maana nikiyasema
yanaweza yakawa hayaaminiki,..sasa hiyo ni kazi yenu au sio, na mimi siwezi
kuiingilia,..ila kwangu mimi, hili tukio, ni ushahidi tosha kuwa ..hilo deni
lipo nyuma ya madeni mengine nyuma yake…, au kuna jambo jingine zaidi ya hilo
hilo deni, na hilo deni ni kiini macho tu..’nikasema.
‘Ukiwa na maana gani…?’ akauliza mpelelezi.
‘Je hilo deni la marehemu linaweza kuyafanya haya
yote, watu wafikie mpaka kuuana, na ni watu wangapi wapo nyuma ya hilo deni,…,..hebu
lifikirieni hili..mimi nahisi …kuna tatizo kubwa, na hilo tatizo nahisi
limejificha huko-huko benki…’nikasema
‘Ndugu wa jamii, sisi tumeshafanya uchunguzi wa kina
huko benki…kwa hivi sasa wafanyakazi wote waliopo pale ni wageni, hawajui
lolote kuhisiana na mambo ya kipindi hicho, zaidi ya kumbukumbu za maandishi…’akasema
‘Hizo kumbukumbu za maandishi zina viambatishi gani
vya kusaidikisha hizo taarifa za madeni..?’ nikauliza
‘Taarifa zipo, kuna nyaraka halali,na sis
tumezithibitisha kuwa nihalali, hakuna ubishiwa hilo….’akasema
‘Hivyo tu…hamjiuliza ni kwanini kwa mfano madeni
yawepo na nyaraka zake ziwepo, wakati huo wanadai kumbukumbu za nyuma
zimeharibika…’nikasema
‘Sikiliza sisi tumefanya kazi yetu kwa mujibu wa
taratibu zetu… tumejaribu kuwatafuta wafanyakazi wa zamani,..wengi tulioweza
kuwapata wanakiri kuwa kweli humo benki kulikuwa na tatizo,…ndio maana wengi
walifukuzwa,..na walioshitakwia wakishitakiwa,..na wengi walishamaliza kifungo…na
hao waliomaliza kifungo, wengi, hawapo kwenye hali nzuri..’akasema
‘Uliwahi kuongea nao…?’ nikauliza
‘Kwa mujibu wa hao tulioongea nao, ambao wanalalamika
pia kuwa walionewa, wakidai kuwa waliohusika walikuwa wakubwa wa vitengo , wao
walitumiwa tu....’akasema
‘Je uliwahi kukutana na hao wakubwa wa vitengo..?’
nikauliza.
‘Hawapatikani, na hawajulikani wapi walipo…wengine
walikuwa ni wageni wamesharudishwa kwao….’akasema
mpelelezi.
‘Kwa maana hiyo hata hilo deni litakuwa sio sahihi
kwa marehemu, benki wanatakiwa wawajibike kwa hilo, na wanashinikiza hivyo, kwa
vile kuna mtu kapewa hiyo zabuni ya kufuatilia hayo madeni, kazi yake kubwa ni
kuhakikisha hayo madeni yamelipwa, sasa,..kuna haja ya kumuangalia na huyo mtu……’nikasema.
‘Hilo deni kwa ushahidi wa nyaraka na kumbukumbu
zilizopo ni deni la marehemu…’akasema mpelelezi
‘Sasa kwanini haya yanatokea, mbona hamjiuliza hilo…na
huyo mzabuni, atasema hiyo, na atajitahidi kuthibitisha hilo..je nyie mumefanya
juhudu gani kupambana na huyo mtu..maana yeye hapo yupo kwa ajili ya pesa,
akipoteza mdaiwa mmoja kama huyo atakuwa kapoteza pesa nyingi sana…je..mliwahi
kumuhoji huyo mtu..?’ nikauliza
‘Ndio maana tunasema, hadi sasa hatuna uhakika wa
moja kwa moja kuwa haya yanayotokea sasa hivi kweli yana uhusiano na hiyo kesi
yako, kama tutapata ushahid wa kutosha basi, …tutalifanyia kazi..’akasema
mpelelezi, bilka kujibu swali langu.. na wakati huo wakili wao wa kuendesha
hizo kesi alikuwa anawasikiliza tu.
Baadae huyo wakili akasema;
‘Kwa taarifa niliyoipokea, mahakama inasema hukumu
iliyotolewa awali ya kupiga mnada hiyo nyumba ni ya halali,…kwa mujibu wa
mkataba, na kwa mujibu wa sheria, kwahiyo, zoezi hilo linatakiwa kuendelea,…’akasema
wakili.
‘Lakini mwenyewe si umeona haya yanayotokea,..kama
hilo zoezi litafanyika haki za watu zitapotea bure, ni lazima zoezi hili
lisimamishwe mpaka upelelezi wa kina ufanyike,…’nikasema.
‘Ukumbuke kuwa ni mahakama imeamua…sasa kama kuna
ushahidi wa kumshawishi hakimu,..abatilishe uamuzi wake, … nipeni, ili niweze
kuweka pingamizi…siwezi kuongea maneno tu, na ushahidi kama huu ambao hauna
mshiko…’akasema huyo wakili, na hao wapelelezi wawili wakaangaliana na mara
simu ikalia..
‘Ndio..nani…Dalali,..kafanyaje, una uhakika, hospitali
gani…na nani....…’mpelelezi akawa anasikiliza huku akionyesha uso wenye
mashaka.
Tukawa tunasubiria amalize kuongea…
NB: Mambo hayo…
WAZO
LA LEO: Haki ya mtu haipotei bure,…inaweza
kucheleweshwa tu..hadi muda muafaka.., lakini mwisho wa siku haki itabakia kuwa
haki na mwenye haki yake ataipata haki yake kama ni haki yake.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment