‘Yeye kanisakama kuwa sikuwahi kuiona hiyo
taarifa…kiukweli mimi nimeshabatika kuiona,..'akasema
'Mimi nakumbuka awali, hisia tu, japokuwa sikupenda hivyo, maana sikuwa na ushahidi, nilijitahidi sana kumsihi shemeji kabla
ya kuziona hizi bahasha,aniambie ukweli, lakini hakutaka, kufanya hivyo,...sasa je kwa kuziona hizi
bahasha mbili bado hatapenda kuusema ukweli...…’akasema mama mjane
‘Ina maana gani shemeji…nisema ukweli gani,..shemeji ina maana unanishuku mimi vibaya, kuwa nahusika na huo.....hapana siamini macho yangu...’ akauliza Dalali
akimuangalia shemeji yake lakini mama mjane hakujibu swali lake, yeye akaendelea kuongea kwa kusema.
‘Ushahidi ulioutaka wewe …ndio huu hapa, taarifa,... uliyosema kuwa mimi sikuwahi kuiona, taarifa ya polisi, ndio hii hapa, sasa niambie wewe …’akasema mama mjane.
‘Umeipatia wapi?’ akauliza mpelelezi akiwa na hamasa kubwa sana.
‘Pale nyumbani kuna shimo alitengeneza mume wangu la
kuchomea takataka, kwa bahati nzuri, mimi sijaweza kulitumia tena tokea mume wangu afariki….na nilifika pale kwa bahati tu,...ni baada ya kukumbuka ndota moja, iliyozoea kunitokea kipindi cha nyuma..ni ndoto ya ajabu
kweli, huku kudharau mambo..mmh…ama kweli mungu akitaka jambo lake liwe litakuwa tu,..yote kiukweli ni kwa mapenzi yake mungu…’akasema huyo mama akiangalia juu
‘Uliota ndogo gani…?’ nikamuuliza
‘Unajua ni kwanini ulipozungumzia maswala ya nyumba,
…ilinifanya nizimie, ..ni baada ya kuhisi ukweli wa ndoto hiyo, ikanijia kichwani, hadi nikashindwa kuvumilia…’akasema
‘Uliota kuhusu nini…?’ akauliza sasa mpelelezi
‘Niliota nikiwa na mume wangu….’akatulia
Tuendelee na kisa
************
‘Mke wangu, upo tayari kuniacha…?’ akaniuliza mume
wangu.
‘Kukuacha..!!, kwanini nikuache…?’ nikamuuliza nikiwa
nashangaa kwanini mume wangu ananiuliza swali kama hilo.
‘Kwa matendo yako…’akasema na mimi nikawa nashangaa
kwanini mume wangu ananiambia hivyo, mume wangu ananiamini, na mara nyingi
ananisfia kuwa mimi nampenda kimatendo, leo hii anaongea hivyo, nikawa na
shauku.
‘Hapana mimi siwezi kukuacha…’nikamwambia hivyo tu.
‘Mhh…haya..ila wapo walionipenda kama wewe,
wakaniahidi hivyo hivyo, lakini kwa matendo yao wameniacha…’akasema.
‘Ni nani, lakini mimi mbona sijakuacha mume
wangu…’nikasema kujitetea, akili ikikumbuka tukio moja huko nyuma lakini ilikuwa ni uzushi wa watu, nikajua labda
ndio hilo.
Mara nikamuona mume wangu akitoa machozi, na sio
machozi ya kawaida, machozi ya damu…nikawa kwenye mshangao, nikamuuliza,
‘Mume wangu vipi mbona unalia, na unatoa machozi ya
damu…?’ nikamuuliza
‘Naumia,…nateseka kwasababu ya wale waliosema wapo na
mimi, wameniacha na wamenifanya vibaya…’akasema hivyo, hapo nikawa na wasiwasi
kweli nikamuuliza
‘Wamekufanya nini mpaka utoe machozi ya damu,
wamekupiga…?’ nikamuuliza
‘Wameniumiza kweli, lakini hicho cha kuniumiza sio
kosa lao ni mapenzi ya mungu tu, ilitakiwa iwe hivyo..’akasema na mimi hapo
nikawa sina amani, nikamuuliza
‘Wamekufanya nini mume wangu..?’ nikamuuliza hilo
swali tena
‘Watu hao..wamechukua matofali ya nyumba yangu
wanakwenda kujengea kwao, na mengine wameyaharibu, kunaiharibia ndoto yangu ya
nyumba…’akasema huku akiangalia nyumba, na kweli nilipoinua uso kuangalia nyumba
yetu ikiwa imebomoka, matofali yamechomolewa.’akasema
‘Oh nani kafanya hivyo…mimi sijawahi kufanya hivi..?’
nikamuuliza nikionyesha mshangao
‘Ipo siku utajua hilo…’akasema hivyo
‘Haya matofali kaiba nani…?’ nikamuuliza
‘Aliyeiba kaenda kujengea nyumba zake…’akasema
‘Nyumba zake ngapi hizo nyumba…?’ nikajikuta nimeuliza
hivyo
Akanionyeshea vidole hivi…viwili, no vitatu,
kavinyosha vizuri, lakini kidoge na dole gumbe kama vimepinda hivi…sikuelewa
hapo, ni nyumba tatu, au tano..na hivyo vitatu..kwanini vinyooke, na hivyo viwili
kwanini vipo hivyo, nikawa najiuliza tu, ..nikadharau, halafu nikasema;
‘Mume wangu , hakuna ambaye anaweza kukufanyia hivyo,
ilimradi mimi nipo hai nitahakikisha kuwa hilo halifanyiki…’nikamwambia huku
nikiangalia nyumba ikionekana kama inataka kuanguka.
‘Sawa….ila nisemayo ni kweli,je niliwahi kukudanganya
mke wangu..?’ akaniuliza hivyo.
‘Hapana mume wangu, hujawahi kunidanganya..’nikasema
‘Basi nikuambiayo ni kweli..’akasema
Basi hapo, nikawa najiuliza tena, ni kipi
alichoniambia, yaani muda huo nimeshasahau, …akili za ndotoni, nimeshasahau
kile alichoniambia,..najiuliza, na kabla
sijamuuliza, akawa sasa ananionyeshea kwa kidole, akisema;
‘Unaona pale…nenda utapata ukweli wa haya
ninayokuambia..’akasema hivyo na mimi nikageuka kule aliponionyeshea kwa kidole,…nikaona
shimo la takataka, likiwaka moto, mataka taka yanaungua,..sikuelewa hapo ana
maana gani, nikageuka ili nimuulize, lakini sikumuona tena
‘Mume wangu upo wapi…’nikauliza na hapo nikazindukana
kwenye njozi.
Hii ndoto imenitokea mara nyingi kama mbili hivi, na nikizindukana nasahau kabisa…sasa huyu mtu wa
jamii, aliponiambia nijaribu kutafuta kila mahali kama ninaweza kupata
ushahidi, ndio nikakumbuka hiyo ndoto ya mume wangu….
Haraka nikaenda pale shimoni, nilikuta mataka taka
yamechomwa, kabisa...nikawa nazunguka na kijiti nikipekenyua , pekenyua, sehemu moja kwa pembeni, nilipopekenya nikaona kitu kigumu, nikapekenyua zaidi ndio nikaona fukuto la mataka taka
halijaungua kabisa, nikaanza kuondoa majivu, ndio nikaziona
hizi bahasha mbili…
Kwa haraka akili ikaniambia, usiziguse kwa mikono
…nikarudi ndani nikachukua hizi, gloves nikazivaa, nikarudi pale na kuzichukau
hizo bahasha…hutaamini, karatasi, zingine zote ni majivu, ila hizi bahasha
mbili, ziliungua kidogo kama unavyoziona…’akasema mama mjane.
‘Hukuona kitu kingine…?’ nikauliza
‘Mhh, vingine ni …huwezi jua, ni mabaki ya karatasi
zilizoungua…zaidi ni majibu tu…’akasema
‘Afande …yapiti upitie hapo…kabla ushahidi wote
haujapotea…’nikamwambia mpelelezi…kwa haraka akachukua simu na kumpigia mtu
wake mtaalamu, akamuelekeza la kufanya.
Mpelelezi, akainuka kidogo,akavuta droo za kabati
lake, akatoa nailoni,…na kwanza akavaa kinga za mkononi, akawa anaifungua ile
bahasha, na kutoa karatasi, ni mbili zimeshikana, na kuna maelezo ndani yake…
TAARIFA YA AJALI ILIYOSABABISHA KIFO CHA
MAREHEMU….akatajwa mume wa mjane jina…’niliona hayo maandishi , mengine
sikuyaona vyema kwani mpelelezi alikuwa akisoma na mkono wake mmoja umeshikilia
kichwa umeniziba.
‘Yah…hii ndio taarifa niliyoandika mimi, nimeitafuta
sana, ni ajabu kabisa, hii taarifa niliitayarisha mimi mwenyewe , lakini cha
ajabu huko ofisini hakuna nakala yake, …’mpelelezi akawa anaongea na mimi kwa
sauti ya chini.
‘Mhh..naanza kupata picha hisia zangu zinaanza kuonekana
ni za kweli…’nikasema
‘Yaani, afadhali nimeiona hii nakala, ya taarifa hii,
maana taarifa iliyokuja kutolewa baadae sio yangu, ikawekwa hapo kama ni mimi
niliitoa, sasa hii ndio niliyoandika mimi, sio hiyo ambayo ipo huko ofisini, ni
ajabu kabisa, sijui ni nani alifanya
hivyo, ok…sasa tutalimaliza hili tatizo…’akasema mpelelezi.
‘Ina maana afande hiyo taarifa ilitoweka kituoni
haiwezekani !?’ nikauliza kwa mshangao.
‘Haya ni maswala ya ndani ya ofisi…nashukuru tu
nimeipata hii nakala, itanisaidia sana kutimiza wajibu wangu…ilishaonekana mimi
nimetoa taarifa ambayo haipo kamili,…kwenye hii taarifa utaona, kila kitu kipo wazi, nilikuwa na shaka sana na
hiyo ajali….’akasema.
‘Umeona eeh…nahisi itakuwa sio ajali ya
kawaida…’nikasema huku nikigeuka kumuangalia Dalali
‘Yah…nahisi kuna tatizo mahali, sasa hii kazi ,
tutayamaliza kwa haraka tu…’akasema mpelelezi
‘Nimekuelewa afande, nahisi hali kama hiyo itakuwa imetokea
hata huko benki, huenda kwenye hiyo bahasha nyingine kuna kitu kama hicho, na
huenda hata huko benki nakala kama hiyo haipo pia…’nikasema
‘Umejuaje..?’ afande akaniuliza kwa mashaka.
‘Hivi wewe huoni…kuna ujanja umechezwa hapo, ili kila
kitu kiharibike kabisa, kisije kuonekana ili ukweli halisi upotee, fanya kazi
yako vyema utaligundua hilo..’nikasema.
‘Naelewa, hadithi zako wakati mwingine
zinasaidia…lakini lazima tupate uthibitisho…’akasema huyo mpelelezi.
Mpelelezi sasa akamgeukia mama mjane na kusema;
‘Na hiyo nyingine…’ akauliza mpelelezi
‘Hii nyingine yaonyesha ni ya benki….’akasema
‘Uliisoma …?’ akaulizwa.
‘Mhh….ni barua mume wangu aliiandika kwenda benki….’akasema
‘Kwenda benki…?’ akauliza Dalali kwa mshangao, na
wakili wake akataka kusimama kuiangalai vyema ile bahasha lakini mpelelezi
akaisogeza mbele yake.
Dalali akawa
anamnong’oneza kitu wakili wake, na wakili wake akawa anamuangalia Dalali kwa
mashaka..na kuuliza.
‘Una uhakika hujawahi kuziona hizo bahasha…?’
akauliza wakili.
‘Nina uhakika,..hata sijui kitu gani kilitokea, mimi sijui jamani…’akasema Dalali, lakini wakili wake bado alionekana
mwingi wa mashaka.
‘Kama huamini basi..nitatafuta wakili
mwingine…’Dalali sasa akaongea kwa hasira.
‘Sio swala la kukuamini, ni kutaka uhakika,..lakini,
tutaongea baadae…’akasema wakili wake.
Wakati huo ,
yule mpelelezi akawa anaifungua ile barua, mimi pale nikamtupia jicho Dalali,
nilimuona kama anahema kwa haraka, nikasema
‘Dalali upo sawa kweli…?’ nikauliza na Dalali
akaniangalia kwa macho ya kushangaa, sasa kitabasamu, tabasamu sasa sio lile la
dharau tena;
‘Nipo sawa muheshimiwa, kwani umenionaje…’akasema
Dalali., huku akimgeukia shemeji yake …
‘She-she-meji, una uhakika, barua hizo,
hujazitengeneza wewe..?’ akauliza Dalali
‘Kuzitengeneza mimi, kwa vipi, ningeliwezaje kufanya
kitu kama hicho…’akasema mama mjane.
‘Huyu mzee, hana akili, nahisi atakuwa ndio yeye….’akasema
hivyo Dalali.
‘Mzee gani…?’ mimi nikamuuliza hivyo, huku akili
yangu ikianza kutunga hadithi nyingine ya kufikirika, ambayo nahisi inaweza
ikawa yakusaidikika.
‘Si huyo mtaalamu…alisema hilo deni ni la
Bro…’akasema na mimi nikatabasamu nikajua hapo kageuza kibao, mimi nikamuuliza
hivi huku natabasamu.
‘Kwahiyo unataka kusema kwa hali hiyo, kwa hivi sasa upo tayari, kukiri, kwa vile unajua kitu gani kilikuwepo kwenye? huenda ikasaidia kuonyesha ukweli kuwa kweli hilo deni lilikuwa sio la kaka yako…?’ nikamuuliza.
‘Mimi sijui…labda tusome hiyo barua tuone inasemaje…?’
akasema Dalali.
Mpelelezi akawa ameshamaliza kuisoma,…akageuka
kuniangalia mimi, huku akitikisa kichwa kama kukubaliana na mimi…akasema;
‘Kwa hili hata wewe nakutilia mashaka, umejuaje haya…’
akasema mpelelezi akiniangalia mimi kwa mashaka
‘Haki haijifichi afande… nimefahamu hayo kutokana na
mapenzi ya mungu…’nikasema nikitabasamu.
Na hapo hapo huyo mpelelezi akachukua simu yake, akawa
anapiga namba..na kitendo hicho kilimfanya Dalali asiwe na amani kabisa, akawa
anamuangalia wakili wake,…kama vile anahitajia msaada,
Wakili wake akawa anamuashiria kwa mkono atulie.
‘Upo wapi…?’huyo mpelelezi akauliza hivyo akiwa
kashikilia simu yake karibu na mdomo huku akumtupia jicho la kujiiba Dalali, na
kitendo hicho kikazidi kumchanganya Dalali…
Huyu mpelelezi akawa anasikiliza tu, anachoongea huyo
aliyempigia, baadae akasema
‘Sawa bado tupo tunaendelea, umepitia, nimemtuma
mtaalamu hapo msaidiane, yah, umeona nini, hakuna kitu..haiwezekani, ok, bora
mje tu…’akasema huyo mpelelezi, na kukata simu, halafu akatugeukia na kusema;
‘Hii bahasha ya benki,..itamsubiria mwenzangu, mimi
nataka tuendelee na maswali yangu muhimu dhidi ya Dalali…kuhusiana na hiyo
ajali…’akasema mpelelezi.
‘Je ina maana sasa mnanishuku mimi…?’ akauliza Dalali
sasa uso ukionyesha wasiwasi mkubwa.
‘Nani kasema hivyo…?’ akauliza mpelelezi
‘Kama mnanishuku mimi kuwa nimefanya kosa, niambieni,
ni haki yangu kufahamu hilo…’akasema Dalali, na kumalizia hivi;
‘Niambieni ili niweze kujieleza, kiukweli mimi nasema
na kuapa mimi sijui lolote kuhusu kupotea kwa hiyo ripoti,..hiyo bahasha,
ilikuwa ..kama ndio yenyewe lakini, ilikuwa nyumbani kwa shemeji…’akasema
akimuangalia shemeji yake.
‘Kwanini uliipeleka kwa shemeji yako, si ulikuwa nayo
wewe…?’ akaulizwa.
‘Mambo mengi baada ya msiba yalikuwa yakifanyika
nyumbani kwa shemeji, hata hiyo taarifa ilipoletwa niliisoma hapo nyumbani, wakiwemo
wanafamilia,..baada ya kuisoma, nakumbuka niliiweka hiyo barua kwenye kabati la
Bro…’akasema.
‘kwenye hilo kabati la Bro, ndio kulikuwa na kila
kitu…au sio, kumbukumbu za benki pia…?’ nikamuuliza.
‘Ndio…lakini kwa muda huo sikuwa makini kuangalia kumbukumbu
hizo,yawezekaan zilikuwepo, lakini kama zingelikuwepo mimi ningeliziona au sio…’akasema.
‘Una uhakika hukuziona hizo kumbukumbu za benki
ikiwemo hiyo barua ya benki , sema ukweli wako…?’ nikauliza
‘Aaaah, nikuambie kitu, maswala ya kufuatilia benki
yalianza baadae sana….na ndipo tulianza kutafuta hizo kumbukumbu hatukuweza
kuziona…’akasema.
‘Dalali uwe mkweli, zilikwenda wapi wakati wewe ndiye
ulikuwa na ufungua wa hilo kabati…?’akasema mpelelezi, kumuuliza Dalali, na
wakili akaingilia kati na kusema;
‘Mteja wangu kasema kuanza sasa ataongea ukweli wote,
kwahiyo kila anachoelezea hapa ndio ukweli wenyewe, naomba tumpe nafasi
hiyo…’akasema wakili.
‘Una uhakika anachoongea hapo ndio ukweli wenyewe…?’
akauliza mpelelezi
‘Ukweli wenyewe si anaufahamu yeye, na ndio huo unao-uongea
au sio…tumpe kwanza nafasi hiyo…, tusikikimbilie kumuweka kwenye makosa, ambayo
hayajathibitishwa kuwa ni makosa kweli…’akasema wakili.
‘Je tutayathibitishaje kuwa ni makosa kweli au sio
makosa…, bila ya kumuhoji kwenye maelezo yake anayoyatoa, lazima tumuhoji na
kumuelekeza, wewe kazi yako..muelekeze kwenye ukweli.
Na hayo maelezo yake moja kwa moja yanaonyesha
anaficha jambo…’akasema mpelelezi.
‘Mimi hapa naongea ilivyokuwa, ukweli mtupu…sasa
sijui nyie mnataka niongee vipi, ili
mnielewe…’akasema Dalali.
‘Hizi barua mbili unasema hukuwa unazifahamu kabla…si
ndio hivyo kwa kauli yako ya awali..?’ nikamuuliza Dalali.
‘Kwa hiyo moja, ya taarifa ya ajali,..kama ndio
yenyewe nilikuwa naifahamu…’akasema
‘Kwahiyo wewe uliwahi kuisoma, ukasoma kila kitu
kilichokuwepo humo ndani, ulivyoipokea,..au sio?’ nikamuuliza.
‘Niliisoma..ndi-ndio..’akasema kwa kutokuwa na
uhakika
‘Uliisoma vyema…?’ akauliza mpelelezi
‘Niliisoma,..lakini kama nilivyosema awali, sikusoma
ile ya kusoma kila kitu, mimi akili yangu ilichukua yale maelezo ya awali
tu…nikaridhika nafsini, na kumuachia mungu, Bro alishafariki..sasa ningefanya
nini…’akasema
‘Mtu akifariki wewe hupendi kuangalia haki zake, kama
kweli alikufa kifo cha kawaida au aliuwawa…?’ akauliza mpelelezi.
‘Lakini taarifa yenu ilisema kafariki kwa ajali ya
gari, na ilielezea kuwa ajali hiyo ilitokana na gari kuwa na hitilafu, kwahiyo sio
kifo cha kupangwa au sio….’akasema Dalali
‘Nikiuulize tena hili swali je hiyo barua uliisoma yote au sio..?’ nikauliza
‘Niliisoma ndio…’akasema
‘Awali ulisemaje..?’ nikamuuliza
‘Ndugu yangu, kusoma ni vipi..niliisoma kwani hata
ukisoma vipi , si bado uliisoma au..’akasema Dalali
‘Awali ulisema hukuisoma yote…au?’ nikauliza
‘Ndugu tuelewane Kiswahili, mimi hiyo barua
niliisoma,..sasa kwa umakini, au kwa haraka haraka haijalishi, ..yote kwa
ukamilifu wake, siwezi kusema hivyo..ila mimi nimekubali kuwa niliisoma
…’akasema.
‘Swali langu ni hili je hiyo barua uliisoma yote…?’
nikamuuliza
‘Mimi nasema hivi nili-isoma, ndio..lakini kwa
kipindi kile sikuwa na umakini wa kusoma kila kitu, si unataka hivyo….’akasema.
‘Kuna maelezo hapo, yaliyoendelea kuelezea kama
alivyoelezea afande, ambayo yaliyoonyesha kuwa hilo gari lilikuwa na hitilafu,
kuwa kuna vifaa viliegeshwa-egeshwa tu…, tena yaonekana vilikuwa vikuu,
kuu..shemeji yako anasema gari hilo lilikuwa jipya, halikuwa na vifaa
vikuu-kuu….si ndio hivyo mama mjane…’nikasema na hapo Dalali akamgeukia Shemeji
yake, na mimi nikasema kwa haraka;
‘Unataka shemeji yako na hilo akuhakikishie au…?’ nikamuuliza
‘Hapana..mimi ndiye nalifahamu sana hilo gari, sasa
nyie mkitaka maelezo ya shemeji nashindwa kuwaelewa,…yeye halijui hilo gari
lilivyokuwa ndani kama ninavyolifahamu mimi …’akasema.
‘Una uhakika gani kuwa yeye halijui hilo gari
lilivyokuwa ndani…wakati yeye keshasema analifahamu hilo gari lilivyo, na sio
kufahamu tu, hata ufundi kidogo anaujua…’nikasema.
‘Kujua huko, sio kwa kulifahamu gari, mimi mwenyewe
niliwahi kuwa mwalimu wake, namfahamu vyema, hajui kihivyo…’akasema Dalali.
‘Kihivyo kwa vipi, kama mtu unaufahamu wa gari, kwa
juu juuu, ukiangalia ndani pale kwenye vifaa vyake, utashindwa kufahamu kuwa
vifaa hivyo ni vikuu, kuu au ni vipya…?’ akaulizwa.
‘Nielewe hapo…gari lilikuja kuungua,..ndio polisi
wakaja kufanya uchunguzi, je utakuta vifaa hivyo vipoje, si lazima vitaonekana
vimechoka, au vitaendelea kuonekana vipya…?’ akauliza Dalali, na mpelelezi
akasema;
‘Gari liliungua,…na vifaa vilionekana kuungua,..ni
kweli lakini katika utaalamu wetu, unaweza kugundua kuwa vifaa hivyo,
vilikuwaje kabla ya gari kuungua, vifaa vilivyoonekana sio vipya, na hata namba
zake hazikuendana na vifaa halisi vya hilo gari…’akaambiwa Dalali.
‘Sio kweli…’akasema Dalali akitikisa kichwa kukataa.
‘Mimi nina ushahidi kuwa vifaa vya hilo gari vilikuwa
vipya….’akasema mama mjane
Wote tukageuka kwake, na wakili akadakia, kwa kusema;
‘Samahani mama mjane hapa hatupo mahakamani,..hapa
hakuna mtu aliyeshitakiwa…hatujahitajia ushahidi..au ’akasema wakili huku
akijishuku mwenyewe.
‘Mimi nataka kusaidia huo mjadala…’akasema mama mjane
sasa hakusubiria akatoa picha …na kumkabidhi mpelelezi. Mpelelezi kwa tahadhari
akazipokea zile picha, akaziangalia halafu akasema;
‘Yes….’akasema hivyo mpelelezi, na akaiweka hiyo
picha mezani, huku akitabasamu
‘Shemeji hiyo picha uliipiga lini…?’ akauliza Dalali
‘Siku ile ulipotaka kulichukua hilo gari, ukisema
unakwenda kulikagua, ni siku ile kabla mume wangu hajaondoka na kupata hiyo
ajali….’akasema hivyo mama mjane sasa akitaka hata kulia.
‘Siku kabla…au sio...?’ nikasema.
‘Ndio…’akasema mama mjane huku akionyesha kabisa
anataka kulia.
‘Sasa shemeji kwanini unalia, unataka kusema mimi
nimefanya hujuma kwenye hilo gari , mimi nifanye hivyo kwa kaka yangu mwenyewe…’akasema
Dalali kwa hasira
‘Mama mjane jitahidi kidogo, haki ya mumeo sasa ipo
mikononi mwa polisi…nikuulize swali je…ni kwanini ulilipiga picha hilo gari…?’
nikamuuliza
‘Kuna..kipindi nilianza kumshuku shemeji yangu vibaya,
kuwa anadanganya kuhusu uharibufu wa gari, sasa siku hiyo nilisikia akimuambia
kaka yake kuwa kuna vifaa vinahitajika kubadilishwa, havifai…wazo likanijia tu,
kupiga picha hilo gari, ..ni wazo tu, hata sijui kwanini wazo hilo lilinijia na
kweli nikaenda na kulipiga picha mbele nikiwa nimefundua kama inavyoonekana…’akasema
mama mjane.
Mpelelezi akageuza ile picha akaona tarehe ya hiyo
picha…akauliza
‘Hii tarehe ndio tarehe uliyopigia hii picha…?’
akauliza mpelelezi
‘Ndio maana nilizipeleka kwa jamaa yangu mmoja na
kuzitoa siku hiyo, hiyo….’akasema mama mjane na Dalali hapo akanywea.
‘Lakini shemeji, ina maana kumbe hukuniamini tokea
awali…, shemeji hivi na mimi nikianza kutoa siri zako zote hapa, utafurahia
kweli…’akasema Dalali.
‘Siri gani zangu ulizo nazo wewe…?’ akauliza mama
mjane, na mpelelezi akaingilia kati na kusema;
‘Dalali usilete hasira,..usikwepeshe mada… ukweli
utajieleza hatua kwa hatua, unasikia, hapa tunazungumzia ajali iliyosababisha
kifo cha kaka yako, je wewe hupendi ukweli kujulikana…’mpelelezi akasema.
‘Lakini na mimi nahitajika kujieleza, ni lazima
nijitee, maana hapa yaonyesha kama vile mimi nina makosa, wakati sio
kweli.’akasema.
‘Kwahiyo shemeji, ina maana hadi hapa unaendelea
kujitetea kuwa huhuski na lolote lile…shemeji?’ akauliza mama mjane kwa sauti
ya huzuni.
‘Shemeji mimi nasema ukweli wa mungu, mimi sina makosa kabisa..ila kwa maelezo ya
hawa watu wanataka kuniingiza kwenye makosa bure na mimi kiukweli bahasha hiyo
ya taarifa, niliiweka kwenye kabati…niliiweka kwa haraka, kwa muda ule,
nikasahau, na mawazo yangu nilijua labda nilikwenda nayo nyumbani…’akasema
Dalali.
‘Kwa maana hiyo hata hiyo bahasha nyingine ya benki
uliwahi kuiona hapo kwenye kabati, wakati unaiweka hii bahasha ya taarifa…?’
akaulizwa.
‘Hapana si…sizikumbuki kuiona hiyo bahasha mimi
niliiweka hii taarifa kwa haraka, nilikuwa na mambo mengi ya kufanya,….sina
uhakika sana, ..’akasema
‘Dalali, hivi vitu shemeji kaviona vikiwa pamoja ,
bahasha hizi mbili zikiwa pamoja, ina maana mchomaji wa hizi bahasha,
alizichukua pamoja, …’akasema mpelelezi.
‘Sio lazima iwe pamoja…’akasema wakili
‘Kwa jinsi invyoonekana ndio hivyo, wakai unataka
kuharibu kitu, kwa haraka,kama ingelikuwa tofauti, hata uchomaji wake
ungelikuwa tofauti…’akasema mpelelezi.
‘Hilo huwezi kulithibitisha hivyo…huwezi kushinikiza
maelezo yako hayo kuwa ilikuwa hivyo..yawezekana ilikuwa tofauti, lakini kwa
vile huyo mchamaji, labda alikuwa na hamasa na vitu hivyo viwili ndio ikatokea kuviweka
pamoja...’akasema wakili.
‘Je Dalali ndio hivyo ilikuwa,..?’ nikauliza
‘Mimi sikumbuki kwakweli…, kwa vile sio mimi
niliyechoma siwezi kusema hivyo…’akasema kwa haraka.
‘Kwahiyo unamkana wakili wako…?’nikasema kuumuliza
nikiendelea kumtega.
‘Sikilizeni niwaambie ukweli….mimi sijafanya hivyo,
na sikuwahi kuiona hiyo bahasha ya benki…’akasema.
‘Je unaweza kukisia labda hiyo bahasha ya benki iliandikwa
nini, ….maana ulipoiona tu, ulisema neno… ulisema nini vile…?’ nikamuuliza, na
hapo akabakia kimia.
‘‘…Si huyo mtaalamu…alisema hilo deni ni la
Bro…’ulisema hivyo, au sio’’ nikasema mimi
‘Hadi hapa mimi naona mumeshanifanya mimi ni mshukiwa
,, kuwa mimi nina makosa, si ndio hivyo, ila naawambia ukweli mimi sina
kosa..mungu ni shahidi yangu….’akasema Dalali.
‘Kwanini Dalali unakimbilia kusema wewe huna kosa,
ninani kakuambia wewe una makosa, bado hatujafikia huko, eeh,..je kitu gani unahisi sisis tunataka kukujengea..?’
akaulizwa.
‘Mimi nimejitahidi kuelezea ukweli wangu ulivyo,…na
labda kujitolea kwangu muhanga ndiko kumeniponza, kuwa karibu na shemeji,
kumsaidia..aah, najuta kwanini nilifanya hivyo…’akasema.
‘Lakini ukweli unao-uongea wewe, tukija kuu-hakiki, inaonekana ni uwongo, kwa hli hiyo unataka ueleweke
vipi, mimi nakushauri jambo, jitoe huko ulipojifunga, useme ukweli, wakosaji
wajulikane…’nikasema
‘Wakosaji akina nani, mimi siwajui hao watu
ningeliwajua mimi mwenyewe ningeliwafikisha mahakamani, maana aliyefariki ni
kaka yangu, na deni ni la kaka yangu, naomba wakili wangu…sasa…’akamgeukia
wakili wake.
‘Wakili wangu naona ile kazi niliyokuitia hapa
imewadia, nakuomba unisaidie..’akasema Dalali, na wakili wake akawa
anamnong’oneza jambo, wakawa wanaongea kama kutokuelewana baadae wakili
akauliza.
‘Afande mteja wangu ana kosa lolote…?’ akauliza
wakili.
‘Hapana…sisi kama tulivyokuambia awali, tumemuita
hapa kumuhoji kwa nia ya kutusaidia kutimiza kazi zetu, kama ulivyoona yeye ni
mtu wa karibu wa haya matukio, ina maana yeye ana habari nyingi ambazo
zitatusaidia sisi kukamilisha kazi yetu…’akasema mpelelezi.
‘Sawa mimi naona muendelee kumuhoji, sawa,…
ila..itanibidi kuingilia kati pale inapobidi..’akasema wakili.
‘Kama utaingilia kati ili tusitimize wajibu wetu,
sisi tutaendelea kuuliza hayo maswali mpaka yatakapojibiwa, na unafahamu tuna
maana gani kusema hivyo…’akasema mpelelezi, na hapo wakili akamgeukia Dalali na
kumnong’oneza jambo.
‘Hapana mimi sikubali, mimi siwezi kuendelea kusota
hapa..sina kosa, hapana..hapana…’akasema Dalali hivyo kwa sauti, na wakili wake
akawa anamnyamazisha.
Mara mlango ukafunguliwa,…akaingia yule mpelelezi
mwingine…na kule nje, wakaonekana watu wameshikiliwa na polis wakiwa wamefungwa
pingu. Dalali,….jicho hilo….mara….
NB:.Naona kila kitu sasa kipo wazi, je ni kweli
Dalali ana makosa, je ni kweli ndugu anaweza kufikia kufanya hivyo kwa ndugu
yake kwa ajili ya mali….lakini tujiulize kama deni ni la benki..je Dalali
atapata nini hapo..
WAZO
LA LEO: Watu wengine kwa sababu ya masilahi wanaweza
kuwalinda wakosaji, wakabeba mizigo ya lawama kwa ajili ya hao wakosaji,(matajiri), kisa
wanapata kitu kupitia wao. Je watu hao wadhulumaji, kama wanadhulumu wengine , huoni kuwa na
wewe utaubeba huo mzigo wa dhuluma, kumbuka hata kama huna jinsi, hata kama hujafanya lakini kwa namna moja unajua, ujue na wewe una mzigo wa dhambi, maana,…ukikaa na muuza uturi, na wewe utakuja
kunukia uturi, au sio….
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment