Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, August 14, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-32


 ‘Je wewe Dalali,  ulirizika na taarifa ya uchunguzi wa polisi kuwa ajali hiyo iliyosababisha kifo cha kaka yako ni sahihi,.…?’ akaulizwa Dalali.

Dalali, alibakia kimia kwa muda, na pale wakili wake alipotaka kuingilia kati, akamuashiria huyo wakili  atulie kwanza, na taratibu akaanza kuongea;

‘Ni yale yale kama ilivyokuwa kwenye hilo deni….ni yale yale wanayonishutumu watu kwa kusema kuwa mimi nashadidia kupigwa mnada nyumba ya marehemu kaka yangu,…lakini hatusemi kuhusu mahakama ilisemaje…’akatulia kidogo.

‘Swali linaulizwa, je mimi nilikubaliana na uchunguzi wa polisi  kuhusiana na kifo cha marehemu kaka yangu, …jamani, hivi mimi ni nani aliyejuu ya ya sheria, je mimi ni nani aliye juu ya uchunguzi wa polisi..mbona mnataka kunitwika mzigo mnzito ambao siuwezi kuubeba…’akamuangalia mpelelezi.

‘Mnataka nijibu au sio..sisi kama wanafamilia…wana-nini, wanafamilia…hatukutaka kupekenyua zaidi, maana mimi ninawafahamu nyie mlivyo, kama tungeanza kubishana na nyie, ..tungelifika wapi,eeeh, hebu niambieni,….ina maana kwa kufanya hivyo, tunawakosa kwenye kazi zenu, mimi sio mtaalamu wa maswala ya ajali za barabarani, ni ningelisema nini hapo…’akatulia

‘Ila…narua tena ila… kama nyie mlikosea kwenye hiyo taarifa yenu ya uchunguzi,..mtuambie…’akatulia.

Mpelelezi, akawa anamsubiria Dalali, kama ataendelea kuongea zaidi, lakini Dalali akabakia kimia, akitikisa kichwa kama kujisifia kwa kile alichokiongea, lakini kwa upande wa pili wakili wake alionekana kama kutatizika fulani hivi.

‘Ndugu Dalali,…nilikwisha kuelezea ilivyokuwa, na kukuarifu kuwa jalada la uchunguzi wa kesi ya kaka yako lilikuwa halijafungwa, kwasababu kulikuwa na maswali ambayo yalikuwa hayajapatiwa majibu yake..hii ni kutokana na mimi kupatwa na dharura….sasa ili kuendelea na uchunguzi wetu, na baadae kuhitimisha kabisa , …kwanza nilitaka kusikia kauli zenu…’akatulia mpelelezi.

 Dalali akacheka kwa dharau…na kusema;

‘Je kauli zetu zitasaidia nini….kuwa kaka atarejea tena, kuwa kama mlikosea nyie, eeh, nyie…eeh,…kwenye uchunguzi wenu, tutawashitaki,….eeh,… je tukiwashitakia, mtafanywa nini…toka lini kesi ya ngedere ukampelekea tumbili,…sijui mnanielewa…’akawa kama anauliza na mpelelezi akabakia kimia tu.

‘Kiufupi, ni kuwa tutakuwa tunajihangaisha tu…mimi kama mkuu wa hio familia tuliyokabidhiwa, kwa niaba ya wanandugu wote,.. ninasema hilo kwetu tuliamua kuliacha kama lilivyo,yote yaliyotokea eeh, tuliyachukulia kuwa ni mapenzi ya mungu....labda nyie sasa, eeh…mtuambie kama kuna lolote limejitokeza…’akasema Dalali.

‘kwa kusema hivyo ina maana wewe kama mkuu wa hiyo familia, uliwaarifu wenzako kuhusiana na taarifa hiyo, mkakaa na kuijadili, mkakubaliana hivyo…au sio, au wewe ulipoisoma kwa niaba ya wenzako ukarizika hivyo, kuwa kifo kimeshatokea basi,…?’ akaulizwa.

‘Ni hivi….taarifa imeshafika, kuwa kaka alifariki kwa kifo cha ajali ya barabarani, ..ajali ni ajali, ajali kwani ina kinga, eeh, ndio kila mtu atakufa kwa sababu maalumu..bro kafariki kwa ajali ya gari, ndio mwisho wake ulipangwa uwe hivyo… na tuliridhika hivyo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi kutoka kwenu,..je nyie mlitaka sisi tufanyeje au wewe niambie hapo..?’ akawa kama anauliza.

‘Je shemeji yako naye alikubaliana na hilo…?’ akaulizwa hilo swali badala ya kujibiwa swali lake.

‘Mhh, yeye kipindi taarifa hiyo inaletwa kiukweli hakuwepo, kutokana na hali yake ilivyokuwa…, ila sisi wanandugu tulikubaliana na hilo,  sisi tulitosha kuwakilisha wanafamilia wote, tulikubalia na uhalisia, yaishe tu…, unajua tena, mtu akifa, hata ufanyeje..haisaidii kitu jamani, kwanini haya yazuke tena, ….’akageuka kumuangalia shemeji yake.

‘Je shemeji yako aliporejea kwenye hali yake uliwahi kukaa naye mkaliongea hilo, ikizingatiwa kuwa yeye hakuwepo kwenye hicho kikao cha awali,…na hakuwa na ufahamu kuhusu huo uchunguzi huo wa polisi,..na huyo ni mke wa marehemu, ni muhimu kwa kulifahamu hilo, je uliwahi kukaa naye mkaliongelea hilo..?’ akaulizwa.

‘Afande, naona ni maswali ya kujirudia rudia tu….’akalalamika hivyo.

‘Tunaweza kujirudia mara nyingi, kutokana na utaalamu wetu ulivyo…’akasema mpelelezi.

‘Haya….shemeji kutokana na hali yake, haikutakiwa kukaa na kuanza kumuongezea mawazo, sisi tulifuata maagizo ya docta, kuwa tuwe makini katika swala lolote linaloweza kumrejeshea mawazo mama mjane…na sisi tukaliona hilo, kwahiyo mimi sikuona kama kuna haja ya kukaa naye na kuanza kusema ya moyoni, kuwa hatukurizika, au tumerizika…’akasema.

‘Ukisema ya moyoni, kuwa mumerizika au hamkurizika, inanifanya nikuulize tena hilo swali kama wewe, nataka kufahamu ya kutoka moyoni mwako kama wewe,..je wewe ulirizika na hiyo taarifa ya uchunguzi wa kifo cha kaka yako …?’ akaulizwa.

‘Nilishakujibu hilo swali lako afande..’akasema Dalali….alipoona wakili wake anataka kuingilia kati.

‘Kuwa…?’ akauliza hivyo mpelelezi

‘Kuwa sisi wanafamilia, tuliamua kurizika na hiyo taarifa kwa vile nyie ndio wataalamu, nyie ndio mliofanya uchunguzi, na tulikubali kuwa mlivyoona nyie ni sahihi kwetu, tungelifanya nini zaidi ya hapo eeh…, ila kama..nyie mlifanya makosa, sasa wewe ndio utuambie…’akasema.

‘Uliisoma vizuri hiyo taarifa ya uchunguzi..?’ akaulizwa na hapo akashtuka kidogo, halafu akabenua mdomo kizrau vile.

‘Ndio eeh, ndi- ndio…sijui,…nasita kukujibu hilo swali kwa maana yangu…’akasema

‘Kwa maana gani, tuambie tu..?’ akaulizwa

‘Kipindi kile kilikuwa kigumu kwetu kama familia,…ndio niliisoma, eeh mbele ya wanafamilia,..lakini nakumbuka hatukutaka kuisoma yote kwa ujumla wake, unajua tena, siwezi kusema ni kwanini, lakini kwa mtu ambaye kapitia hali kama hiyo unaweza kutuelewa tu…muhimu ni yale maelezo ya mwanzo kuwa ndugu yetu, alifariki  kutokana na ajali ya gari…’akasema.

‘Ndio ni kutokana na ajali ya gari,… na hilo gari lilikuwaje, mpaka likasababisha hiyo ajali, kulikuwa na melezo hayo, kwahiyo wewe uliyekuwa ukiwasomea wenzako hukutaka kuendelea kuyasoma, ni kwanini ulifanya hivyo, maana yalikuwa na umuhimu wake kujulikana…?’ akaulizwa.

‘Mhh…unajua…’akataka kujitetea.

‘Je ulisoma, wewe kama wewe, ..na ukaona hakuna umuhimu kuwasomea wenzako au hata wewe hukusoma kabisa…?’ akaulizwa

‘Nikuambie ukweli, nilipoyapata hayo maelezo, nilifika kwa wenzangu nilichokifanya ni hivyo, kusoma yale maelezo ya juu, sikutaka kuingialia undani wake, na nikarejesha hiyo karatasi kwenye bahasha yake,…basi…sijasumbuka tena…’akasema

‘Hiyo taarifa unayo….?’ Akaulizwa

‘Wala sikumbuki nimeiweka wapi, ni mpaka niitafute…’akasema

‘Kwahiyo kumbe hukuichukulia maanani, ..au ulifanya hivyo kwasababu gani,….hiyo sio taarifa muhimu ambayo ulitakiwa kuja kumuonyesha shemeji yako, ambaye kwa muda huo hakuweza kuiona…?’ akaulizwa

‘Nina mambo mengi afande,…sio kwamba niliitupa, hapana, ..sijui niliiweka wapi maana niliitafuta baadae sikuweza kuiona tena…’akasema

‘Ni kwasababu haikuwa na umuhimu kwako tena na labda hukutaka shemeji yako aje kuiona tena, ikaja kumsumbua, si ndio hivyo…au sio…?’akaambiwa na kuulizwa.

‘Ili iweje , labda nikuulize hivyo,  maana ajali imeshatokea, ni kweli ajali yaweza kutokea kutokana na gari lenyewe, uzembe wa dereva au bahati mbaya,…nakumbuka ndio..kuna sehemu nilipitia, ..yah ..kuna maelezo kuwa gari lilikuwa na hitilafu..’akasema

‘Kwahiyo kumbe wewe kama wewe uliisoma, lakini hukutaka wenzako walielewe hilo…?’ akaulizwa na Dalali akabakia kimia, na kabla hajafanunua mdomo kuongea mpelelezi, akasem

‘Ok….kabla sijaendelea  na wewe…, nataka nirejee kwa mama mjane kwanza…’akasema mpelelezi.

‘Lakini yeye hajui zaidi ya ninavyofahamu mimi…’akajitetea Dalali

‘Ni kweli,… ndio maana yeye akalalamika…’akasema mpelelezi

‘Alilalamika nini sasa…mimi ndiye nafahamu yote kuhus gari, yeye anafahamu nini, anaongea tu…na kwanini alalamike kwako, na sio kwangu, ..?’ akauliza akimgeukia mama mjane
‘Utasikia maelezo yake nikimuhoji, wewe tulia kwanza nitakuja kwako…’akasema mpelelezi.
***********
 Mpelelezi akamgeukia mama mjane, na kumuangalia kwa makini, nahisi alikuwa akitafakari kuhusu hali ya huyo mama, akasema

‘Shemeji…vipi khali yako kwasasa..?’ akaulizwa mama mjane.

‘Nzuri tu…nipo sawa..’akasema mama mjane kwa kuongezea hayo, ‘nipo sawa’ kwa msisitizo.

‘Upo sawa kuelezea ukweli wote, na kwa hili nataka usifiche kitu, maana ndio hitimisho lake..baada ya hapa, tutafunga hii kesi…labda kuwe na zaidi…mimi sitaki tena baadae kusikia malalamiko zaidi ….’akasema huyo mpelelezi,  na mama mjane akamkatiza na kusema;

‘Naelewa, na ndio maana nimekuja hapa, nipo tayari kwa lolote lile..’akasema huyo mama mjane sasa kwa kujiamini zaidi na Dalali akamuangalia kwa macho ya mashaka.

‘Je wewe ulirizika na taarifa ya kuhusu ajali iliyosababisha kifo cha mume wako,…maana shemeji yako anasema taarifa hiyo waliipata wao, na wao kwa mtizamo wao, kama alivyodai, kutokana ushauri wa dakitari, wao hawakupendelea kukuonyesha hiyo taarifa , je uliipatia wapi, hiyo taarifa kuhusiana na ajali ya mume wako…?’ akaulizwa.

‘Kiukweli …kama alivyosema shemeji mimi nilikuwa naumwa kipindi hicho,na maelezo zaidi ya kifo cha mume wangu nilikuja kuyasikia zaidi watu wakiongea…na nikawa na hamu ya kujua zaidi,..…’akatulia.

‘Ulisikia nini awali ..na baadae ukasikia nini mpaka ukavutika kutaka kujua zaidi..?’ akauliza.

‘Kwa mazungumzo ya wanafamilia, nilisikia kuwa mume wangu alifariki kwa ajali ya gari, ..na ni ajali ya kawaida tu..baadae nikasikia kwa watu kuwa gari lilikuwa na hitilafu, baadae nikasikia kuwa , mume wangu hakuwa makini na gari, hakulichunguza vyema, ni kama kumlaumu mume wangu kuwa hakuwa makini....ni mkanganyika wa maneno ya hapa na pale..’akatulia.

‘Ehe, kwanini ukakanganywa na hayo maelezo…?’ akaulizwa.

‘Kwasababu gari la mume wangu, lilikuwa jipya,…na maswala ya kuchunguzwa kama gari lina hitilafu, mara nyingi alikuwa akilifanya shemeji..kwa vile yeye ni mtaalamu wa magari…sasa sijui kwanini mume wangu alaumiwe kwa hilo…’akasema hivyo na hapo Dalali, akahema kwa nguvu. Na alipotaka kusema neno, wakili wake akamuashiria atulie.
‘Wewe unafahamu lolote kuhusu gari, kuendesha, …?’ akaulizwa

‘Nafahamu kiasi, wakati napata mafunzo ya kuendesha gari, nilijifunza kidogo kuhusu gari lilivyo, hata kutengeneza, japo sio saana…’akasema na Dalali akatikisa kichwa kama kusikitika

‘Kwahiyo ulifanya nini baada ya mkanganyiko huo..?’ akaulizwa

‘Mim sikuweza kuvumilia, nikaamua kwenda polisi ili nipate maelezo zaidi ili kujirizisha…’akasema.

‘Kwanini ukimbilie polis wakati taarifa alikuwa nayo shemeji yako, yaani huyu Dalali..?’ akuliza.

‘Kwasababu nilimuomba maelezo, na ikibidi anipatia hiyo taarifa, akawa ..mara nitakupatia, mara sijui ilipo, mara nahisi imepotea,..mara subiri mimi nina shughuli nyingi, ilifikia mahali mpaka tukawa hatuelewani kwa sababu ya hilo…’akasema.

‘Kwanini mkosane..?’ akaulizwa

‘Aliona kama namsumbua, maana tupo kwenye kutafuta ukweli wa deni, na wakati huo huo natafuta mambo mengine..nilimuelewa kwa wakati ule… , lakini baadae nikasema kwanini nisifuatilie mimi mwenyewe, ndio nikaona nije huku kituoni kufuatilia mimi mwenyewe…’akasema.

Hapo Dalali hakuweza kuvumilia

‘Najua tu, kama ulivyofanya kwa deni, ndivyo hivyo hivyo kwa hilo gari, kunizunguka,..sawa tu…samahani afande, hapo nataka kujitetea kidogo, mimi sikumwambia shemeji , kwasababu ya kuhofia hali yake..kutokana na docta alivyosema, kuwa tuwe makini na hali ya shemeji…’akaongea kwa taratibu

‘Ni kweli hata mimi nililiona hilo, kuwa maelezo ya uchunguzi ya ajali iliyosababisha kifo cha Bro, yalikuwa na upungufu kidogo…, lakini ingelisaidia nini tena…sasa labda mimi nimuulize shemeji, mimi kwa kumuonea huruma huko, kuwa nisimpatie mawazo ya kumuumiza zaidi, nilifanya kosa,  …?’ akauliza Dalali.

Mama mjane akamuangalia Dalali, moja kwa moja usoni na kusema;

‘Shemeji, unakumbuka siku moja tuliliongelea hili jambo, ukaniambia kama nina shaka nalo kwanini nisiwaulize wale waliolishughulikia hilo tatizo…, je hao waliolishughulikia ni akina nani, kama sio..hao polisi,..?’ mama mjane akamuuliza Dalali, na pale Dalali alipotaka kujitetea shemeji yake  akaendelea kuongea;

‘Na kwa vile nimeona kuna utata, …na niseme ukweli, kilichonisukuma zaidi  ni kutokana na kufuatilia hilo deni la nyumba, hilo deni lilinifungua  macho,…maana nilikutana na watu wengi…wakanishauri hili na lile, na kila nikiwazia zaidi nahisi , nilihisi hivyo, hapa kuna jambo nyuma ya pazia…akilini,niliwazia hivyo..’akasema mama mjane.

‘Jambo gani hilo, ambalo hukutaka kuniambia mimi shemeji, …mpaka ukakimbilia polisi, huoni kwa kufanya hivyo, ndio maana hawa watu wananishuku mimi vibaya, je shemeji huniamini mimi..kuna kitu gani kibaya nimewahi kukufanyia shemeji…?’ akauliza Dalali, sasa akiwa  kakunja uso kwa hasira.

‘Nimeshasema, sikupenda kubakia na duku duku moyoni, na kilichonisukuma nifanye hivyo ni kutokana na hilo deni, hilo deni sio halali kwa mume wangu, hata wewe kiundani unalifahamu hilo…’akasema mama mjane na Dalali akatikisa kichwa kukataa.

‘Utapinga tu…lakini najua, hukubaliani na hilo deni…kuna siku uliwahi kusema kuwa huenda kuna mtu kafanya mbinu zake, kumbambikia kaka yako, …hukuwahi kusema hivyo…?’ akauliza mama mjane

‘Ni kabla sijapata huo ushahidi…’akasema Dalali.

‘Sawa…na hili la ajali je…kwanini hukutaka kuniambia ukweli…kutokuniambia ukweli kwako, ndiko kulinisikuma  mimi kufuatilia, je unakubaliana na hilo, waanlosmea watu kuwa kaka yako, alikuwa mzembe kwenye gari lake,…anaendesha bila kulichunguza kaam lina hitilafu….mimi sikubaliani na hilo, hata wewe hukubaliani na hilo..ndio maana nikataka kuujua ukweli…, wewe mwenyewe unamfahamu kaka yalo alivyokuwa makini kwenye gari lake.. ..’akasema

‘Sasa mimi ningelijuaje hayo..eeh, walioleta taarifa ni benki, mimi nahusikanaje hapo, na kuhusu ajali, ..taarifa ya uchunguzi walileta hawa polisi wenyewe, kwa kile walichokigundua, na taarifa ya mwanzo tu, inasema Bro alifariki kwa ajali ya gari lake, sasa hapo mimi nina kosa gani…?’ akauliza Dalali

‘Haya,…nisubirie na mimi nielezee vyema…’akasema mama mjane.

‘Tatizo shemu, unavyoelezea, uwe makini,....wewe hujui tu, unawapa kichwa hawa watu, na kuendelea kunifikiria mimi vibaya…hayo maelezo yako ni kama yananishitakia mimi…’akasema Dalali, na mama mjane akatulia, lakini badae kwa kujiamini mama huyo akaendelea kuongea.

‘Mimi nilivyohisi , na sio kuhisi..ni kwa jinsi nimjuavyo, mume wangu, kama ilivyokuwa deni, na naamini hivyo sio halali yake, ndivyo nilivyohisi hata kwenye taarifa ya ajali  kutokana na maelezo niliyosikia kuhusu ajali hiyo, moyoni nikahisi pia sio sahihi…’akasema

‘Taarifa hiyo uliiona wapi,…?’ akauliza Dalali

‘Kwanza nilisikia kwa watu…’akasema mama mjane

‘Hahaha, kusikia kwa watu, ndio uamini wayasemayo, wewe hukuwahi kuisoma hiyo taarifa vyema…labda kama polisi walikupatia ukaisoma,…lakini kwa kauli yako wewe ulisema, taarifa haikuwepo, …walidai mapaka aliyehusika areeje, sasa niambie wewe uliipatia wapi hiyo taarifa, acha kusikiliza maneno ya mitaani…’akasema Dalali.

‘Hata kama ni maneno ya mitaani, lakini kama yana utata, mimi kama mke wake, ningelitakiwa kufanya nini…ndio nikae kimia tu…hapana mimi sipendi kuwekeza duku duku moyoni mwangu, nikaamua kufuatilia, na nilifanya hivyo baada ya kuona wewe hutaki kuniambia ukweli…’akatulia kidogo.

‘Shemeji shemeji…usinilaumu kabisa kuwa mimi sikuweza kukusaidia,  mimi nilikuwa tayari kwa lolote lile, nimekusaidia mangapi eeh …’akasema Dalali

‘Ndio lakini hilo la kuhusu ajali iliyosababisha kifo cha mume wangu hukutaka kabisa kunielezea ukweli,  kila nikitaka kukuulizia hayo maswali, wewe ulitoa udhuru fulani, shemu sema ukweli wako, kila nilipokuwa nataka kukuulizia hayo maswali ulikuwa unasemaje…?’ akamuuliza Dalali.

‘Nimeshakueleza sababu kubwa ni ushauri wa kitaalmu kutoka kwa docta….sijasema mimi hapo, sijaelezea hilo, usiongeze chumvi…?’ akauliza Dalali.

‘Kwa kiasi kikubwa wewe ulikuwa kama upo pembeni, kwa hilo , hata kwenye deni kwa asilimia kubwa ulikuwa kama unajiweka pembeni…, haya umefikia wapi, haya twende, huko mahakamani kama itawezekana, ilikuwa hivyo, hata hivyo sio kwamba nakulaumu, mimi nakutetea kuwa ni kutokana na majukumu yako…ndio hukuweza kufuatilia na mimi bega kwa bega, kwa kila kitu nilivyotaka mimi…’akasema mama mjane.

‘Shemeji hapo ina maana unanilaumu tu, usijitetee, usikwepe huo ukweli…mpaka mimi sasa naanza kujihis vibaya, nimekufanyia nini kibaya cha kustahiki hayo unayonifanyia sasa, eeh, niambie ukweli shemeji…?’ Dalali sasa akawa anauliza maswali mengi kwa mfululizo.

‘Shemeji, mimi nina haki yangu kufuatilia, ..na sikufanya hivyo bila kufuata utaratibu, ni wewe unasahau tu, kuwa nilikuwa nakuuliza na kauli zako zilikuwa hivyo,..nenda kauliza benki sio wao wanadai…eeh nenda kauliza polisi si wao walichunguza…, je hapo mimi ningelifanya nini…?’ akauliza mama mjane.

‘Sawa…nimekuelewa shemeji yangu,..tenda wema uende zako, lakini shemeji, ujue hayo uliyoyafanya matokea yake ndio haya, mimi nashikiliwa kwa makosa ambayo mimi sijawahi kuyafanya, ina maana hadi hapa ilipofikia, wewe umeshaniweka kwenye kundi la uhalifu, ina maana umenishitakia mimi , je kwa kosa gani…’akasema Dalali.

‘Mimi sijakushitakia wewe..haya mengine ya kukuhoji wewe ni kazi zao polisi, na mimi nililalamika kwao hilo…kuwa wasije kukushuku wewe vibaya, nionavyo mimi wewe huna kosa…sasa kiutendaji wao, mimi nisingeliweza kuwazuia…’akatulia

‘Khaa….’akasema hivyo Dalali.

‘Ndio ningeliwezaje kuwazuia kuwa wao…, wasikuhoji , ila kiukweli mimi niliwaambia kuwa wewe huna kosa, …nakufahamu vyema…wewe ni msaada wangu mkubwa,..zaidi ya hapo, ni majukumu yao, yaliyowasukuma kufanya hivyo ..’akasema mama mjane.

Hapo mpelelezi akaingilia kati na kusema;

‘Hebu kwanza Dalali tulia, nimekuacha tu, uingilie kati,. Ili tukuone hisia zako zipoje, na hata wakili wako amejaribu kukuzia bila mafanikio..unavyofanya hivyo, unajichora wewe mwenyewe bila kulijua hilo…’akasema mpelelezi.

‘Mimi sija-jichora hapo…, ni lazima niwajibike, huyu mama yupo mikononi mwangu, amefanya makosa sana, kuniruka hadi kuja huku kwenu..huyu .she-shemeji umesahau nilivyokuhangaikia, ndio maana hata Bro, alikuwa akikulalamikia, kuhusu tabia yako…’akalalamika Dalali


‘Tabia gani!!!…mume wangu hajawahi kulalamika kwa hilo, hana tabia hiyo ya kuwalalamikia watu wengine kunihusu mimi..na tabia gani mbaya hapa, kuutafuta ukweli ni kosa…unajishuku wewe mwenyewe tu shemeji, usinilaumu kabisa kwa hilo…’ akauliza mama mjane na kuelezea hayo  kwa sauti ya hasira, na mpelelezi akaingilia kati.

‘Shemeji…mama mjane, nisikilize kwanza, mamaah…, tuachane na Dalali, ni kweli yeye mwenyewe  anajishuku bure hatujasema yeye ana kosa hapa, ni katika taratibu zetu tu za kumuhoji yeye kwanza ili  kutusaidia kaika kazi zetu, sasa sijui kwanini anajishuku bure…’akasema mpelelezi

‘Wala! …Mimi sijajishuku kitu, ila ni lazima niongee pale inapobidi…mimi ninajua ninachokifanya, nina uhakika sina kosa, ndio maana sina wasiwasi na hilo…’akasema Dalali.

Mpelelezi akanigeukia mimi, alipoona nataka kuongea na kabla hajanipatia nafasi, au kunizuia, nikawa nimeshaanza kuongea…

‘Mama mjane, je ni kitu gani zaidi kilikusukuma kisheria,..ni ushauri au ni wewe mwenyewe tu,.. hadi kuamua kufuatilia maswala ya mumeo..?’ mimi nikauliza hilo swali na mpelelezi, akaniangalia kwa sura ya kukereka, kuwa nimeingilia kazi yake.

‘Ni kutokana na ushauri wa kitaalamu pia..,..ilibidi niende kwenye vitengo vya haki za binadamu, ustawi wa jamii,  vitengo vya sheria, jinsia na watoto , ..sehemu nyingi nilipitia kuona jinsi gani nitasaidiwa kwa vile mimi  sikuwa na pesa,…za kumtafuta wakili…, ndio wao wakanishauri, hili swala nilifikishe kwanza polisi,..hasa hili la uchunguzi wa ajali , iliyosababisha kifo cha mume wangu…’akasema.

‘Kwahiyo wewe ulifanya hivyo kutokana na ushauri wao,  kuwa uende polisi,…au ni duku duku zako za moyoni ndio zilikusukuma kufanya hivyo?’ akauliza mpelelezi kutaka uhakika zaidi.

‘Pamoja na duku duku zangu za moyoni,..kutaka kuwajibika kujua ukweli wote… pia hata ushauri wao,wa kitaalamu, ndio ulionifanya niwe na moyo zaidi wa kufuatilia…waliniambia ni haki yangu kufuatilia kisheria,..na nina haki  ya kufungua malalamiko,  ili uchunguzi ufanyike zaidi, nikikaa kimia, itaonekana tumerizika, je kwa kufanya hivyo, si nitakuwa nimemdhulumu mume wangu…’akasema mama mjane.

‘Baada ya ushauri huo ndio ukaanza kufuatilia, au sio..?’ akaulizwa

‘Ndio nilianza kufanya hivyo..lakini baadae nikashindwa…’akasema

‘Kwanini ulishindwa…!?’ akaulizwa

‘Kutokana na hali iliyokuwa ikitokea ndani ya familia yangu..mara ghafla watoto wangu walianza kuumwa, magonjwa ya ajabu ajabu…na mimi mwenyewe  nikaanza kuona vitu vya ajabu ajabu vya kunitishia amani…’akasema mama mjane.

‘Kutokana na hali hiyo ukakata tamaa kufuatilia ina maana uliamini hayo mambo, sio mambo ya kishirikina hayo..?’ akaulizwa

‘Kiukweli nilijitahidi sana..na hata kumuomba shemeji ushauri, na..ndio shemeji akasema hayo maswala sio ya kunyamazia, ni bora tutafute njia mbadala, maana kama mtoto anaumwa, ukifika hospitalini hakuna ugonjwa,..sio kitu cha kawaida…’akasema na mara  Dalali aakasema;

‘Ni mimi nilikushauri hivyo au ni ndugu yako..?’ akauliza kwa hasira.

‘Ndugu yangu pia alisema hivyo hivyo…’akasema mama mjane.

‘Aaah, ni nani wa kwanza kukushauri hivyo, ni mimi au ni ndugu yako…?’ akauliza.

‘Shemeji…kabla ya kile kikao mimi na wewe na ndugu yako, wewe hukuwahi kunishauri hivyo,..?... kuwa haya mambo yanavyoonekana sio ya kihospitalini, …ulianza wewe lakini sio kwa siku ile tulipokutana, ilikuwa siku kabla..’akasema mama mjane

‘Sikumbuki kuongea na wewe kuhusu hilo wazo kabla…sikuwahi…huo ndio ukweli, sema kwa vile unataka kunishinikiza nionekane mimi ndiye mkosaji, ni lazima utasema hivyo…’akasema Dalali.

‘Je ni nini zaidi kilikuvuta, hadi kuomba uchunguzi huo wa polisi kuhusiana na ajali iliyosababisha kifo cha mume wako,..hadi ukaomba uchunguzi huo ufanyike upya…?’ akaulizwa

‘Muhimu ni hiyo taarifa ya polisi kuhusiana na gari lenyewe lilivyokuwa,…na mimi mwenyewe nliwahi kufika sehemu gari linapotengenezewa, kuulizia, wakaniambia nimuulize shemeji , wao kama mafundi hawajui lolote kuhusiana na gari hilo…’akasema.

‘Hiyo sio kweli shemeji…umeelezea kuhusu taarifa, sasa umekimbilia kuwalamu hata mafundi…tarifa yenyewe hukuwahi hata kuisoma, na wewe unahisi ina mapngufu, yapi sasa wakati hata kuiona hukuwahi kuiona.. , usichanganye mambo hapa, hizo shutuma ni nzito sana, ‘ akasema Dalali.

‘Oh nilisahau…’akasema mama mjane… akachukua mkoba wake,..kwanza akavaa kitu kaam soksi mkonononi, halafu taratibu, akatoa bahasha mbili zilizoungua upande…akachukua mojawapo, akaisoma juu, akamkabidhi mpelelezi

‘Ni nini hii,…?’ mpelelezi akasita kuipokea kwanza

‘Kasema mimi hata hio taarifa ya uchunguzi sikuwahi kuisoma…natoa ushahidi wangu…na nimejitahidi kutokuzigusa bila ya kinga mkononi...wasije kusema ni mimi niemfanya hivyo...’akasema mama mjane.

‘Hii bahasha mbona imeingua umeipatia wapi…?’ akaulizwa mpelelezi naye akiwa na tahadhari ya kuigusa.

Hapo Dalali, akajiinua ile ya kutaka kuona hicho alichokitoa mama mjane ni kitu gani, hata wakili wake akafanya hivyo, ..na hapo hapo wakili wake akawa wa kwanza kusema;

‘Samahani kwa hilo, nilivyoelewa tokea awali, ndio maana sikutaka kuingilia ni kuwa nyie mnachofanya hapa  ni kuchukua  maelezo ya kuhojiana…mnamuhoji mteja wangu,  anaulizwa maswali ya kuweza kuwasadia, kumalizia uchunguzi wenu, sasa haya ya kutoa ushahidi, yanakujaje, je mteja wangu anashukiwa kwa kosa lolote..?’ akauliza wakili

‘Ndio maana nimemuuliza huyu mama mjane,…hizo bahasha kazipatia wapi,…na majibu yake yatatusaidia kuendelea na maswali yetu,..je mteja wako ana wasiwasi gani kuhusiana na hiki alichokitoa mama mjane..?’ akauliza mpelelezi.

Dalali…..akabakia kimia…macho yakiwa yanaziangalia zile bahasha…

NB: Haya niishie kwanza hapa, swali je hiyo ajali ilikuwa ya kawaida au ina mkono wa mtu,..je mkono huo ni wa nani, na kwanini.


WAZO LA LEO: Mwenye uwongo wa dhambi, wakati wote huishi kwa mashaka, hajiamini, na hata akijiamini ni swala la muda mfupi tu…kwani nafsi yake huhisi labda labda nyingi, kuwa labda keshagundua, labda….maana dhuluma inamsuta nafsi yake wakati wote..
Ni mimi: emu-three

No comments :