Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, August 11, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-31


Yule askari, yaonekana alitaka kuhakikisha kuwa wahusika wote wanaohitajika kwa kikao hicho wameshafika, kwani baadae aligeuka na kuondoka, huku akifunga mlango bila kusema neno

Wakili, aliyeingia, pamoja na kushikana mikono na mwenzake, ya kusalimiana, cha ajabu wakili huyo hakuongea neno, akawa ananiangalia tu , baadae akasema;

‘Huyu ni nani….?’ Akauliza akiniangalia mimi

‘Ni yule Peku peku niliyekuambia…’akasema Dalali, akimsogezea huyo wakili kiti ili aweze kukaa,…huyo wakili akakaa lakini bado akiendelea kuniangalia mimi, na mimi nikawa kimia tu…

‘Nilishaonna naye mahali fulani, najaribu kumkumbuka nyema, anyway, its ok…haya niambie….’akasema sasa akimgeukia Dalali.

‘Kama nilivyokuelezea awali kwenye ujumbe wa maneno, japokuwa simu yangu waliishikilia kwa muda, hili nalo ni jambo la kuwalalamikia hawa watu, kwanini wachukue simu yangu…’akalalamika Dalali

‘Wameshakurejeshea…?’ akaulizwa

‘Ndio, lakini najua wamechunguza kila kitu, hata hivyo mimi sijali, sina makosa na kwa vile wewe umeshafika,…nitakuelezea unachotakiwa kukifanya..’akasema Dalali, na hapo wakili akanigeukia mimi

‘Unaweza kutupisha mara moja…?’ akasema huyo wakili akiniangalia mimi

‘Muheshimiwa, hapana, muache tu awepo,…kwa kifupi,  hakuna muda wa kuongea, mimi na wewe hapa, nilichokuitia wewe ni ili uweze kusikilizia maongezi yangu na polisi, wakinihoji,….’akasema Dalali

‘Kuhusu nini, kosa gani wanakuhoji nalo…?’ akauliza wakili

‘Hutaamini hadi sasa hawajaweza kuniambia kosa langu ni lipi..lakini mimi sijali, maana mimi sina kosa lolote kama nilivyowahi kukuambia awali,..na,..na utakuta maswali yao mengi ni ya kunitega tu,  ili mimi niingie kwenye kosa ambali sijalifanya, na mimi ni mjanja, hawaniwezi…’akasema akigeuka kuniangalia mimi.

‘Sasa ni hivi, kwa vile wao ndio wamelianza hili nataka wanifahamu kuwa mimi ni nani….sijataka haya, na …kiukweli mimi muda mwingi,…nipo na familia yangu, nimekuwa nikijitahidi kujenga maisha yangu kwa jasho langu…lakini wivu wa watu ndio umechangia haya…’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo..?’ nikajikuta nimeuliza hilo swali.

‘Kwanini ukaniuliza maswala ya nyumba…unajua nilivyohangaika kuzijenga hizo nyumba, hata Bro, alifikia hatua ya kunipongeza…ni juhudi zangu mimi mwenyewe, sikupata hata senti moja ya bro au ya mtuto yoyote…nimezijenga kwa jasho langu mimi mwenyewe….’akasema

‘Nilikuuliza nikitaka ukweli…na lengo langu halikuwa wivu kama unavyofikiria wewe, lengo langu ni ukweli wa uhalali wa hilo deni, …’nikasema

‘Kwahiyo unafikiria mimi nilijenga hizo nyumba kwa hilo deni au , hayo ni mawazo ya kijinga, samahani kwa hiyo kauli, lakini nitasemaje hapo…?’ akasema hivyo.

‘Yawezekana yakawa ni mawazo ya kijinga ya mtizamo wa mtu, kwa vile haelewi, na mtu asiyejielewa, anajulikana kitaalamu kwa kauli yako hiyo…ila ukweli utajuliakana na aliyemjinga atabainika, au sio...’nikasema.

‘Nina kila ushahidi wa mali zangu…ndio maana nikataka huyu wakili awepo, ili kila jambo liwekwe sawa, najua utakuwa umshamdanganya shemeji…sasa nataka baada ya hapa kila kitu changu kijulikane kisheria, na uhalali wake…’akasema akimgeukia wakili wake.

‘Unasikia muheshimiwa nataka uyafanye hayo, na uwathibitishie uhalali wa mali yangu yote kisheria, hati zipo,hati za gharama ya ujenzi zipo…, kila kitu nilishakupatia, au sio..?’ akasema

‘Ni kweli kila kitu kipo sawa,…’akasema huyo wakili

‘Na baada ya hapo nataka ufungue mashitaka dhidi ya huyu mtu, kwa kunisumbua, kwa kunijengea chuki na familia yangu, na zaidi kunishuku kwa jambo ambalo mimi sijawahi kulifanya…nilipwe milioni 90 kwa kashfa hizo,…, mengine utajua wewe , jinsi gani ya kuyaweka kisheria…’akasema

‘Sawa hilo halina shida, nitalifanyia kazi..’akasema wakili.

‘Utakuwa umeturahisishia kazi Bwana Dalali..’nikasema hivyo na Dalali akaniangalia kwa uso uliojaa kuuliza halafu akakunja sura na kusema kwa dharau.

‘Tatizo hunijui vyema nilivyo..mimi ni mtu mpole sana, mimi najua kuishi na watu wa aina mbali mbali, ndio kazi yangu ilivyo, ila ukinigusa kubaya,…hutaweza kuamini…na wewe umeshanigusa kubaya, uliza na hizo nyumba nilijenga kutokana na watu kama nyie..walinilipa, kwanini unidharau, kwanini uniharibie jina langu, sasa kutoka kwako nitaenga nyingine, wewe si utaona tu..’akasema

‘Ni kweli,… nimegusa mali yako..lakini kwanini ufikie huko, una wasiwasi gani na mali zako,..kama ni halali yako, itabakia kuwa hivyo, ila husika yangu kubwa ni kuhusu hilo deni ambalo linadaiwa kuwa ni la marehemu..mengine ni yako wewe mwenyewe…’nikasema

Dalali akatulia kidogo kama anawaza jambo…alitupiana jicho na wakili wake sijui kama walipeana ishara gani, Dalali akasema;

‘Sawa, …kama kweli upo hivyo, sawa..tutaliona hilo, mimi sio mtu mbaya, na kiukweli niseme hivi,  samahani nimekasirika bure tu, ..ngoja tuone,ila ninachotaka mimi ni kuonyesha uhalali wa mali zangu..wakili atalisaidia hilo, ili kuondoa hisia zenu mbaya, na hilo la kufungua mashitaka dhidi yako siwezi kuliondoa…’akasema

Na mara mlango ukafunguliwa, sasa aliyeingia ni mpelelezi,anayeshughulia ajali iliyosababisha kifo cha kaka yake Dalali.

*************

Wakili akamgeukia mpelelezi , naona walishaonana huko nje kwani hawakusalimiana akasema

‘Hebu niambie mteja wangu kashikiliwa hapa kwa kosa gani…?’ akauliza

‘Ni mteja wako sio…! Ok, hajakuambia eeh,,…yupo hapa kuisaidia polisi, kuna maswali fulani fulani,…kuna mambo tunahitajia kumuhoji, lakini akang’ang’ania  hawezi kuhojiwa mpaka wewe uwepo, kiujumla sisi tuliona ni maswali ya kawaida tu, sasa huenda anahisi vinginevyo….’akasema mpelelezi na wakili akamgeukia mtu wake, na Dalali akasema;

‘Usiwe na wasi wasi, wakili wangu, ..kama nilivyokwisha kukuambia kinachotakiwa hapa ni wewe usikilize tu, kama utaona ninakosea mahali unaweza kunionyesha ishara mimi nitajua tu….sasa wewe sikiliza tu,….’akasema akitikisa kichwa kujinadi.

‘Kwahiyo…..’akataka kusema wakili wake, lakini Dalali akamuashiria kwa mkono kuwa anyamaze, na Dalali akanigeukia mimi na kusema;

‘Wewe ndugu yangu hatujamalizana,…au sio..’akasema Dalali .

Mimi nikaona nisikae kimia, hapo, nikasema;-

‘Kuna swala nilikushauri mapema sana, sasa naona ni muda muafaka wa wewe kujitakasa, kabla hujachelewa, na muda ndio huu..’ nikamwambia.

‘Kwanza nikuambie ukweli, mimi sina kosa, siwezi kukubali kosa ambalo sijawahi kulifanya,  wewe ulisema mtaalamu aliongea jambo  mbele ya polisi, hayo ni yake yeye kama yeye, sio mimi…., ‘akatulia kwanza.

‘Kwangu mimi nitaongea ukweli unaonihusu mimi tu…’akatulia hapo kidogo

‘Na kwa jinsi ninavyomfahamu mtaalamu…asingeliweza kusema jambo ambalo halipo, hata kama aliteswa,……ni kweli mimi nilikwenda kwake, kutokana na matatizo ya mtoto, na katika kuangalia ndio akayagundua hayo, sioni yeye anahusika vipi na hili zaidi ya hapo…’akasema.

 Hapo ndio mpelelezi akaingilia kati na kusema;

‘Wewe mtu wa jamii, hayo maswali yako kwa mujibu wa mpelelezi muhusika,  yasubirie kwanza,  hadi hapo atakapofika yeye,  sasa hivi nataka kumuhoji huyu jamaa kuhusiana na ajali ya marehemu, jana alikataa kuongea akidai anahitaji wakili wake awepo, sasa wakili wake ndio huyu hapa ameshafika…’akasema mpelelezi na wakili akatoa makabrasha yake kwenye mkoba.

************

‘Mhh, kwanza kabla ya kuanza haya mazungumzo,…nilitaka tukiongea na yeye awepo, kuna umuhimu mkubwa wa yeye kuwepo hapa… sijajua hali yake inaendeleaje…’akasema Dalali.

‘Shemeji yako hajambo…na kutokana na hali yake , japokuwa sio kuwa anaumwa,..ila sisi tukaona haina haja ya yeye kuwepo, kwahiyo hili jambo linakuhusu wewe, kama atahitajika ni baadae…’akasema mpelelezi

‘Oh…mnanifanya nishindwe kukifanya nilichokidhamiria,…bila yeye,…ok, wakili wangu unasemaje hapo..?’ akamgeukia wakili wake.

‘Kwa vile ni kuhojiwa tu, mimi sioni kwamba kuna tatizo,…ila itakapofika kwenye makubaliano, basi ni lazima awepo…….’akasema wakili

‘Ndio hivyo, mimi lengu langu nikumuhoji kwanza, kama kuna tatizo, basi tutalishughulikia ipasavyo…..’akasema mpelelezi.

Mara mlango ukafunguliwa na askari mmoja akaingia, akamnongeza kitu mpelelezi, na mpelelezi, akatikisa kichwa, halafu akasema;

‘Una bahati sana, mama mjane yupo hapo nje, ..’akasema mpelelezi

‘Oh, tayari keshapona, …ina …’Dalali alitaka kusema jambo akakatisha, kwani kule mlangoni aliingia huyo mwanamama, kwa haraka akatembea hadi pale alipokaa mpelelezi, akawa anamnong’oneza kitu.

Mpelelezi akasema;

‘Basi ni vyema,..ila hayo yatamsubiria mwenzangu,…’akasema huyo mpelelezi, na mama mjane akainua uso kumuangalia Dalali,…ile angalia yake ilionyesha jambo, sasa sijui ni kwa kumuonea huruma au kuna kitu kingine kimejitokeza hapo, na Dalali akawa anamuangalia shemeji yake kwa uso wa mashaka.

‘Sasa tuanze, au sio…’mpelelezi akasema

Hapo hapo Dalali akamgeukia shemeji yake na kusema;

‘Shemu usijali , mimi sina hatia, haya yatakwisha , leo hii hii,…nimeshukuru sana kuwa haujambo, sijui kitu gani kilikupata, na unisamehe kwa lugha yangu pale….’akasema hivyo , na shemeji yake akabakia kimia tu, kitendo hicho kilizidi kumtia mashaka Dalali, na kabla hajasema neno, mpelelezi akasema;

‘Sawa wanafamilia nyie, … mjue hiki ni kikao tu cha kuulizana maswali, haikuwa na haja ya mawakili nk…lakini hatuwezi kumnyima mtu haki yake, ….’akasema mpelelezi.

‘Sawa  mimi nipo tayari, maana wakili wangu yupo, nimependelea hivi, baada ya kuona nashinikizwa kwenye makosa ambayo sikuwahi kuyafanya, na sijui shemeji yangu ana nini , naona kama bado hayupo sawa….’akasema  Dalali akimuangalia shemeji yake.

‘Mimi nipo sawa,..tuendelee tu …’akasema mama mjane

‘Haya wanandugu…’akasema mpelelezi akimuangalia Dalali

‘Ndugu Dalali, je una uhakika kweli kuwa  kaka yako alifariki kwa ajali tu…?’ mpelelezi akauliza hilo swali hivyo kwa Dalali

Ilivyojionyesha, Dalali hakutegemea swali kama hilo..maana nilimuona Dalali uso wake ukibadilika, ni kama alipatwa na mshtuko fulani, na aliyeokoa hiyo hali  alikuwa ni wakili wake aliyesema;

‘Kwanza kabla hajajibu hilo swali, hebu tuwekane wazi hapo…, umesema kuwa  mteja wangu kashikiliwa hapa kwa kuisaida polisi na awali alikuwa akiyajibu maswali yanahusiana na deni, nikajua hayo ndio mteja wangu aliyoitiwa, lakini sasa naona unakuja na hoja nyingine mpya…’akasema wakili.

‘Mimi nilichomuitia bwana Dalali ni hicho, kumuhoji kuhusiana na ajali iliyosababisha kifo cha kaka yake, na ni kweli…kuna ajenda ya  deni la marehemu, ajenda hiyo mimi sihusiki nayo mimi,  atakuja mwenzangu ndiye mtaendelea naye….’akasema mpelelezi.

‘Kuna makubaliano kuwa matatizo yaliyojitokeza, yamalizwe kinyumbani,..je na hili mnalikiuka,..au imekuwaje,..nataka niwekwe wazi kwanza, kabla ya hayo maswali yako…’akasema wakili.

 ‘Sisi tunajua wajibu wa kazi yetu, na hili jambo lilikuwa la kifamilia, ilitakia tatizo hili limalizwe kifamilia, lakini kutokana na ukweli uliokuja kubainika baadae, ikaonekana kuna upelelezi unahitajika kufanyika, na upelelezi unahitajia kuwahoji watu…huyu tumemuita hapa kumuhoji, ..lakini akagoma ndio maana akakuhitajia  wewe…’akasema mpelelezi.

 ‘Sawa, kwahiyo kwa leo hii, utamuhoji wewe kuhusiana na ajali ya marehemu, na baadae atahojiwa na mwingine kuhusiana na deni, je itachukua muda gani, maana kwa hli ilivyo, mteja wangu kachoka…’ Akasema wakili.

‘Mteja wako hajalalamika hilo, kama atahitajia siku nyingine ya maswali kutoka kwa mwenzangu ni hiari yake,, ila hawezi kuondoka hapa kwa vile bado anaisaidia polisi…’akasema mpelelezi

‘Haiwezekani, hamuwezi kumshikilia mteja wangu zaidi, ..kama kuna kei ya kujibu, sawa, hata hivyo, yeye ana haki ya dhamana…’akasema wakili

‘Nimeshakuambia mteja wako, hajashitakiwa bado, sasa hivi anaisaidia polisi,..kama itafikia huko tutawaambia..’akasema mpelelezi.

Mara mama mjane akanyosha mkono kutaka kuongea, mpelelezi akasema

‘Samahani mama mjane,…hayo yako yasubirie mwenzangu, usijali, …’akasema mpelelezi.

‘Jamani,…mimi nimekuja kwa haraka, na huko nyuma nimeacha vurugu, watu wamefika wakitaka mnada ufanyike, na mara wakaja wengine wakidao, wao ndio wenye haki…sasa siwezi kuendelea kukaa hapa zaidi, kwa vile sina uhakika wa huko nyumbani kwangu….’akasema mama mjane

‘Ni nani hao wanataka kufanya mnada bila mimi kufahamu..?’ akauliza Dalali.

‘Mimi siwajui, wanasema wewe uliongea nao, ukawaruhusu huo mnada uendelee, maana ni amri ya mahakama…’akasema mama mjane.

‘Shemeji hawa watu watatupotezea muda, hawana ushahidi wowote hawa watu, na baada ya hapa hata tukifika mahakamani, tutaombwa ushahidi, na mashahidi je kweli tunao hao mashahidi.’akasema Dalali.

‘Kwa uwezo wa mungu utapatikana tu….’akasema mama mjane…kauli hiyo ilimfanya Dalali, ashituke na kutulia kimia, akabakia hivyo, …wakili wake ndiye akaingilia kati, na kuuliza;

‘Je tunaanza kipi, maana huyu mama anakuja na ajenda yake, hatuwezi kumchanganya mteja wangu, kwa mambo mawili…’akasema wakili

 ‘Wakili wangu, usiwe na wasiwasi, mimi yote haya nitapambana nayo,..hamna shida, ila nimepata jambo la kunifanya nifarijike kidogo, kusikia kauli ya shemeji kuwa huenda kaupata ushahid ,…’akasema Dalali akimtupia shemeji yake jicho.

‘Ushahidi utapatikana tu, kwa uwezo wa mungu maana haya yote yametokea na kutendeka ….kwa mapenzi yake,, …’akasema mama mjane

‘Shemeji, hayo maneno tu hayawezi kutusaidia, ..nilijua labda umepata kitu,..kumbe ni maneno tu,..hahaha, shemeji naye bwana, mimi nilishafarijika ..’akasema Dalali, na shemeji yake akabakia kimia.

‘Mama mjane wewe kuwepo kwako hapa ni kuhusiana na nini, ni Deni au ajali….’akauliza wakili, ni kama anataka kupoteza muda.

‘Ni deni….’akasema hivyo mama mjane.

‘Sawa basi hilo litasubiria kwanza…au sio afande, kama ni lazima abakie hapa kusikiliza tu sawa, ila kama ana dharura anaweza koundoka tu au sio …’akasema wakili

‘Ni kwa vile kuna hilo tatizo la hao watu watu wa mnada, ndio maana , wasiwasi wangu ndio huo nisije kufika nyumbani, nikute huo mnada umeshafanyika…?’ akauliza mama mjane.
Mpelelezi akamgeukia mama mjane…
‘Nimeshamtuma mtu huko, unajua hapo kuna amri ya mahakama, sisi kama watu wa usalama, hatuwezi kuipinga moja kwa moja…inabidi tufuate sheria,…tunalifuatilia hilo, usijali…’akasema mpelelezi.

‘Lakini afande, mimi sio kwamba nashabikia hilo, ila naungana na shemeji yangu hapo,hapa tunaongea kimaneno tu…, Mahakama ndio ilitoa amri, ndio maana mimi nimemuita mwanasheria wangu, ili kama kuna pingamizi basi liende kisheria, sijataka maneno tu, je hilo pingamizi huko la mnada limefanyikaje…?’ akauliza Dalali.

‘Usiwe na shaka na hilo,…kinachoendelea huko ni vurugu tu , kuna watu wanadai pesa zao kutokana na zoezi hilo,…hilo ni jambo jingine litafanyiwa kazi, kwanini watu watoe pesa kuzuia mnada, kama kweli ulikuwepo kisheria,… , je ni rushwa, lakini pia kumejitokeza namna ya kutufanya tuweke pingamizi,ndio taratibu zinafuatwa na mwenzangu…’akasema mpelelezi.

‘Lakini hakuna mtu aliyetoa pesa hapa afande…’akasema Dalali

‘Waliahidiwa pesa, hao watu wanalalamika hivyo, sasa kuahidiwa pesa kwa kazi gani,…kama watu wa usalama, inabidi kulichunguza na hilo ..’akasema mpelelezi

‘Waliofanya hivyo, ni hawa watu…’akasema Dalali akinionyeshea mimi kidole

‘Hawa watu, waliwaahidi pesa hao watu wa mnada ili zoezi hilo lisifanyike, sasa …kwa hilo wa kumuuliza hapa ni huyu mtu wenu wa jamii..’akasema Dalali.

‘Sasa hilo kundi jingine limetokea wapi..?’ nikauliza

‘Mimi sijui….’akasema Dalali…

‘Tuendelee…’akasema mpelelezi, akimgeukia mama mjane

‘Samahani, shemeji… nataka kuliweka hili wazi kwanza, nauliza hivi, kutokana na uchunguzi uliofanyika, tunahitajia kujirizisha kwa pande zote, sisi wachunguzi kwa upande wetu na nyie jamii, raia kwa upande wenu, sasa nauliza hivi,…’akatulia kidogo hapo huyo mpelelezi

‘Je  mama mjane...japokuwa Dalali, hajaweza kunijibu hilo swali nililomuuliza, lakini naona nikuulize wewe kwanza…’akasema mpelelezi.

‘Afande mimi nitakujibu swali lako…’akasema Dalali

‘Subiria kwanza , nataka kumweka mama mjane sawa tu, ili aone umuhimu wa yeye kuwepo kwenye hiki kikao…, je wewe mke wa familia, baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa kifo cha mumeo, …najua ulikuja kuupokea baadae sana, ulipopona, je ulirizika  na uchunguzi huo uliofanyika, ..kuwa mume wako alifariki kwa ajali ya kawaida tu…?’ akaulizwa

Mama mjane kwanza akatulia baadae akainua uso,…uso wake ulionyesha wazi mama huyu leo ana jambo…

‘Awali mimi nilikubaliana na hilo, maana mtu sasa  ameshafariki..utafanyaje eeh…na taarifa ilishatolewa, na sijui zaidi ya hiyo taarifa…, baadaye nilipo-pona vyema, nikaanza kujiuliza mimi mwenyewe kuhusiana na ajali hiyo na hiyo taarifa ilivyotolewa, ….’akatulia Dalali alitaka kuongea jambo.

‘Endelea,  Dalali,hili sio swali lako kwanza, nitakuja kuuliza …’akasema mpelelezi.

‘Mimi nilipoanza kusikia maneno ya watu…kiukweli iliniuma sana, lakin kwa vile muda ulishapita nikaoana haina haja,…ila nakumbuka siku moja wakati nafuatilia haya maswala ya deni, nilikutana na askari mmoja, simkumbuki jina laki ni nani,…alinihoji kidogo, kuhusiana na hiyo ajali, akisema jalada lake halijafungwa…’akasema mama mjane

‘Alikuhoji kuhusu nini hasa…?’ akauliza mpelelezi.

‘Kuhusu hisia zangu kuwa je kweli, nimerizika na uchunguzi uliofanyika, …nilimuambia kuhusu hisia zangu,  kuwa kiukweli mimi sikuwa nimerizika na uchunguzi huo..’akasema

‘Kwanini labda, elezea kwa ufupi tu…’akauliza mpelelezi

‘Kwanza…gari la mume wangu ni jipya, halina tatizo,..nijuavyo mimi…sasa uchunguzi unasema kuna nyaya sijui za umeme …zilikatika, kuna vitu vilichomolewa vikawekwa sivyo ndivyo.., inaonekana hilo gari, lilikuwa kwenye matengenezo na halikufungwa vyema, kitu ambacho mimi sikubaliani nacho…maelezo hayo yalinifanya nishikwe na mashaka…’akasema

‘Basi inatosha..’akasema mpelelezi, na kuwageukia Dalali na wakili wake..

‘Kwanini nimemuuliza mama mjane hilo swali,..ni ili mfahamu kuwa sisi hatukurupuki tu, na wakati mwingine tunaifanya hii kazi yetu kutokana na nyie, msaada wetu wa kutoa malalamiko ndio unatusukuma sisi kufuatilia jambo,…’akasema mpelelezi

‘Ina maana shemeji…’akalalamika Dalali.

‘Subiria kwanza…’akasema mpelelezi na Dalali akawa anamuangalia shemeji yake kwa macho yaliyojaa mashaka.

‘Ni kweli uchunguzi wa awali ulionyesha hivyo, kuwa marehemu alifariki kwa ajali, na chanzo cha ajali ni gari lenyewe, lilipochunguza lilionyesha udhaifu wa baadhi ya vifaa vyake kutokuwa imara,…ama vilichomolewa na kuachwa kurejeshewa vyema, au kuna hujuma ndani yake na mimi niliachia hapo kwenye uchunguzi wangu..’akasema mpelelezi.

Dalali akataka kuingilia lakini wakili wake akamzuia

‘Na maswali hayo yalitaka kumsubiria mtu anayelifahamu vyema hilo gari, na zaidi ya mkewe ni wewe mwenyewe bwana Dalali…’akasema mpelelezi.

‘Samahani kidogo hapo,…’Mimi nikaingilia kati

‘Bila samahani…’akasema afande

‘Ni nani awali alifanya huo uchunguzi …?’ nikauliza

‘Ni mimi, ila …sikuweza kuumalizia, maana nilipatwa na dharura ya safari…’akasema mpelelezi

‘Sasa niliporejea kutoka safari, nikakuta hii kesi bado ipo..hajafungwa, na uchunguzi zaidi haukuwahi kufanyika tena..na kuna makubaliano kuwa kesi hii itamalizwa kinyumbani, lakini hapa kwenye ajali…sio swala la kinyumbani, hili ni swala letu…’akasema mpelelezi.

‘Ni sawa, sasa ukweli unaanza kujitokeza…’nikasema

‘Ukweli gani huo …’akasema Dalali, na mpelelezi akaendelea kuongea;

‘Ni wajibu wangu, kujirizisha kwa hili tukio, ndio nikaanza kufanya kazi yangu ili ikibidi niweze kuimaliza hii kesi kabisa na kuimaliza kwake ni kukamlisha uchunguzi wangu…, nilifanya juhudi za kuonana na mama mjane,..lakini kwa kipindi hicho bado hakuwa na afya njema…nikaisubirisha, na kwa bahati nzuri, ikatokea sababu ya mimi kuiendeleza hii kesi…’akatulia

‘Sababu mojawapo ni hilo deni….’nikasema

‘Hahaha….sio kweli…huo ni uhadithi wako tu bwana mzee, unapotezea hisia zako bure, utaumbuka bila kutegemea…’akasema Dalali, akicheka kwa dharau

‘Kwahiyo ni muhimu sana kukuhoji wewe Dalali, na shemeji nilishamuhoji tayari….’akasema mpelelezi

‘Ina maana shemeji, uliongea na polisi, mbona hukuniambia…’akalalamika Dalali

‘Usijali….sisi kazi zetu hazisubirii mtu, na wewe leo ni zamu yako…’akasema mpelelezi

 ‘Sawa, uliza hayo maswali yako afande…’akasema wakili akimuashiria Dalali kuwa hakuna tatizo.

Mara mama mjane akasimama na kuenda pale alipo mpelelezi akawa anamnong’oneza kitu, wakawa wanaongea, kwa sauti ya kunong’ona, …baadae mpelelezi akatikisa kichwa kukubali.

Dalali alipoona hiyo hali hakuweza kusubiria akasema;

‘Shemeji…sio kwamba nalalamika, lakini kwanini kila jambo unafanya bila kunishirikisha mimi.., ?’ akauliza

‘Usijali Dalali, mama mjane alikuwa bado na anahangaika kivyake kutafuta ushahidi wa madai yake,…na alitaka kutoka kidogo nimemzuia kiusalama,…mpaka anayehusika aje, ni mambo ya kawaida tu..na sasa kakubali kuwa tayari kusubiria…’akasema mpelelezi.

‘Sasa yeye kapata ushahid gani ..nataka kulifahamu hilo…?’ akauliza Dalali

‘Dalali…hayo mtakuja kuongea akija mwenzangu, sasa hivi tunaulizana kuhus hiyo ajali, sawa,..nijibu swali langu nililokuuliza awali….’akasema mpelelezi

‘Swali gani afande, ambalo mimi sijaweza kulijibu…?’ akauliza Dalali

‘Je wewe ulirizika na uchunguzi wa polisi kuwa ajali hiyo iliyosababisha kifo cha kaka yako ni sahihi,..je unakubaliana na taarifa iliyotolewa kuwa kifo cha kaka yako ni ajali ya kawaida tu…?’ akaulizwa Dalali.

Dalali, akabakia kimia….na wakili wake akataka kuingilia kati, lakini ….


WAZO LA LEO: Uwongo mwingine unakuwa mgumu sana kuutamka kwa haraka, ukijua kuwa uwongo huo, madhara yake ni makubwa zaidi ya matamshi yenyewe….wengine hawajali, ulimi wao ni mwepesi kutamkatu, hata kujiapiza…lakini uthabiti wa kauli, unaweza kusubirishwa na mwenyewe aliyetuumba ili tu tuweze kujirudi maana baada ya kauli hiyo huenda usije kupata muda wa kutubu, mengine sio  kwa kupenda kwetu tu…Tupo pamoja hapo
Ni mimi: emu-three

No comments :