Tulifika kituo cha polisi…, na tulipofika tu, tukaona
gari la yule mpelelezi wa awali likitaka kutoka, walipotuona wakasimama gari, na yule
mpelelezi akateremka kwenye gari lake kwa haraka akatufuata.
‘Vipi mbona mumechelewa hivyo, napiga simu yako haipatikani,….unajua
kumetokea tatizo kubwa sana, na ndio hivi nafuatilia, yule mtu anajulikana kama
mtaalamu katoroka…’akasema
‘Katoroka…!!, kwanini atoroke…?’ akauliza mpelelezi mwenzake
‘Yaani ni vitu vya ajabu kabisa, walinzi hawana la kusema, wao wanadai
huenda walipuliziwa dawa…, wakashikwa na usingizi..na…lakini tutampata tu, na
hili limenifanya nianze kumshuku vibaya huyu mtu na wenzake, maana tulishafikia
hatua ya kutaka kumuachilia, …hatukuwa na kesi dhidi yake, sasa kwanini atoroke ..’akasema mpelelezi.
‘Oh,…. huo ni uzembe…na….’akasema mpelelezi tuliyekuja naye…kabla
hajamaliza kuongea, huyo mpelelezi mwingine akageuka kumuangalia Dalali,…
‘Wewe Dalali, unafahamu wapi mtaalamu anaweza kwenda, maana hajaweza
kutoka nje ya hili jiji, njia zote zimehakikiwa hajatoka nje ya jiji hili…?’
akaulizwa Dalali
‘Mimi siwezi kufahamu afande…, sana sana ni huko kwa mwanamke wake…zaidi
ya hapo mimi sijui…’akasema huku akionyesha uso wa mashaka.
‘Ni kwanini mtaalamu atoroke, maana sisi tulimshikilia tu kwa muda, ili
kupata maelezo sahihi, kutokana na shutuma dhidi yake, na hatukuwa na kesi kubwa
dhidi yake, nilitaka niwakutanishe tu, ili kulinganisha maelezo yenu,… sasa
kwanini akatoroka…?’ akaulizwa
‘Mimi siwezi kujua afande..,..maana hata hivyo, mimi kiukweli sijui
mumemkamata kwa kosa gani..’akasema Dalali.
‘Dalali,..kila hatua inayopita inazidi kunisukuma kwenye kuamini kuwa
nyie mna makosa, sikuwa nimefikia hatua hii awali, nia yetu ni kulimaliza hili
tatizo ili haki ipatikane, kwa vile deni lipo liangaliwe ni la nani hasa…sasa,
naanza kuamini kuwa kuna kitu kipo nyuma ya hili deni,..na tutagundua tu….’akasema
mpelelezi.
‘Mimi nina uhakika sina kosa, na ..mimi sijui kwanini huyo mtaalamu
kakimbia, na kwanini afanye hivyo….kapaniki tu…, kiukweli afande mimi sijui
kitu, ananitia mashaka hata mimi…’akasema.
‘Mtaalamu nirafiki yako mkubwa sana….kweli si kweli.?’ Akauliza
mpelelezi
‘Nimeshawajibu hawa wenzako…yule sio urafiki yangu kivile ni rafiki wa kikazi tu jamani, imetokea hivyo kwasababu ya
shughuli zangu,…tafadhali nawaombeni msinipandikizie jambo ambalo
halipo…’akasema Dalali.
‘Sawa ..umeshafikishwa hapa,..ukweli wako ndio utakaokuokoa,…na kwa
ajili ya huyo mwenzako, itakubidi sasa unisubiria mpaka nirudi,..na wewe sasa
utoroke…’akasema huyo mpelelezi
‘Sasa mimi nitakusubiria humu kwa vipi..eeh, yaani hata usipofika mapema
ina maana mimi nilale humu kama mfungwa, hapana afande msinifanyie hivyo,
mnanishikilia kwa kosa gani eeh, ngoja wakili wangu afike, sikubali ,..?’
akauliza Dalali, na huyo mpelelezi akaanza kuondoka, bila kujibu swali hilo
aliyejibu alikuwa mpelelezi huyo tuliyekuja naye.
‘Kiukweli mimi ndiye niliyekuwa nikikuhitajia hapa…si nilikuambia kule
wakati tunaondoka…ni kuhusiana na ajali ya marehemu kaka yako, kuna maswalii
nitakuuliza…sasa haya yaliyotokea kwa mwenzako yanakugusa na wewe…’akasema
mpelelezi anayeshughulikia kifo cha mume wa mjane.
‘Haya sasa mapya…yaani hamjui mnavyoniingiza kwenye hali mbaya ya
kiuchumi, hivi mtailisha familia yangu, mnafahmu mimi sijaajiriwa nimejiajiri,
na kipato changu chategemea kuzunguka, sina ofisi ya kusema inajiendesha hata
kama sipo, jamani hebu jaribuni kinifikiria na mimi….’akalalamika Dalali
‘Tutaona hilo, …ushirikiano wako ndio utarahisha kuyamaliza haya mambo
yote, na kama utatoa ushirikiani, mbona rahisi tu, wewe utakuwa huru,hatuna
kosa la kukushikilia muda wote..’akaambiwa
‘Hapana, najua kabisa mlivyo, ndio maana mtaalamu akatoroka, mnamuweka
mtu ndani, hammfungulii mashitaka, ..maneno yenu ndio hayo, unaisaidia polisi,
mpaka lini, mtu anateseka, familia yake inateseka mwisho wa siku huna
kosa,..mtamlipa nini huyo mtu….sasa sikilizeni msimamo wangu utakuwa ni ule
ule… mimi sitajibu swali lolote kutoka kwenu, hadi hapo wakili wangu atakapofika…’akasema
‘Sawa,mimi nitakuuliza maswali, ukikaa kimia, nitaweka maelezo yangu,…na
nitaendelea kukuuliza mpaka hapo utakaponijibu,… na Dalali, sisi hatutaki tu,..tukitaka
utaongea tu,…’akasema mpelelezi na Dalali akamuangalia mpelelezi huyo kwa
mashaka.
‘Lakini sisi kwa uungwan wetu, tunakupatia nafasi ya wewe kujituma ,
kushirikiana na sisi, ….unajua Dalali, lengo langu mimi, ilikuwa tu,… ni
kumalizia uchunguzi wangu, kuhusiana na kifo cha kaka yako…’ akasema mpelelezi
‘Vyovyote iwavyo, mimi sitajibu swali mpaka wakili wangu awepo, ndio
msimamo wangu…’Dalali akagoma kuongea
******
Ni siku ya pili nikafika kituoni, nikitokea
hospitalini, kumuangalia mama mjane, ambaye alikuwa kumbe kesharuhusiwa, jana
hiyo hiyo..jana hiyo hiyo alizindukana, na kuomba kurudi nyumbani, na kwa vile
nilihitajika kufika kituoni, sikuweza kwenda kuonana naye tena…kuna ndugu yake
alifika kumsaidia.
Nilipofika kituo cha polisi nikaambiwa nisubirie
kwanza, kwani Dalali anamsubiria wakili
wake na amesema hawezi kuongea jambo lolote mpaka awepo huyo wakili wake ,
lakini baadae nikaambiwa huyo Dalali anataka tuonane naye.
Niliingia kwenye chumba maalumu cha maongezi, na humo
sikumkuta mtu baadaye kidogo, Dalali akaletwa na askari, nilishangaa kidogo kwa
jinsi alivyowekewa ulinzi wa namna hiyo, labda ni kutokana na kutoroka kwa huyo
mtaalamu;.
Dalali aliponiona
akajitahidi kutabasamu, ile ya dharau, japokuwa ya maumivu, alionekana
uso umakunjamana, nahisi ni kutokana na hali ya humo ndani,…yeye ndio akaanza
kuongea;
‘Ndugu yangu….,
umakuja sio, nimewaambia wewe naweza kuongea nawe, wala sijali
kitu…japokuwa mimi nakutupia lawama wewe, kuwa wewe ndiye chanzo cha haya yote. Sawa mimi
mimi wamenishikilia hapa, nimekubali kuyabeba haya mateso kwa ajili ya familia
yangu na marehemu..lakini kwanini, kosa langu ni lipi…, nataka wewe unijulishe
hilo, kosa langu ni lipi, eeh, nimefanya dhambi gani..?’ akaniuliza
‘Kwani mimi
ndiye nimekuweka ndani, ungewauliza hao polisi, uliona nilivyokuwa nafanya kule
nyumbani, nilitaka tuongee tu, tutafute uhalali wa hilo deni, hukutaka kusema
ukweli,…huo ndio ukweli, hujasema ukweli… kuna kitu unatuficha…’nikasema.
‘Kitu gani nakificha ndugu yangu,… eeh, niambie….au
labda unahisi hili na hili, kuwa labda mimi nahusika na hilo deni, au…niambie
hivyo ili mimi nijue, nahusika kwa vipi, haiji akilini, mimi nihusikanaje na
deni la benki…hebu tumieni akilizenu vyema jamani…’akasema
‘Nafsi yako inalifahamu hilo zaidi yangu mimi,..ila
kiukweli unachosema sio sahihi, nimekuuliza maswali mengi, ukawa
unadanganya,..na kwa ushahidi mbele ya polisi,sasa kwa ushauri tu, Dalali hebu kuwa mkweli, usisubirie hadi hali iwe mbaya zaidi, milango ya toba ikifungwa, utaumbuka, na sijui itakuwaje…’nikasema
‘Niliwaeleza ni kwanini niliongea vile,...ni kawaida, hata afande alinielewa, wakati mwingine inabidi uongee vile, ili kulinda masilahi yangu, lakini sina jingine zaidi ya hayo, sijui lolote kuhusu hilo deni zaidi ya huo ushahidi wa polisi,..huo ndio ukweli na ndivyo nitakavyosema popote pale…’akasema
‘Jana shemeji yako kapoteza fahamu, unajua ni kwanini
alipoteza fahamu..?’ nikamuuliza, nay eye akatabasamu, halafu akaniangalia moja
kwa moja usoni…
‘Mizimu hiyo,…imeshaanza kurejea hakuna zaidi
pale…’akasema.
‘Mbona kaponea hospitalini, bila hata kutumia hizo
dawa zako…’nikasema.
‘Unajuaje kuwa sikufanya dawa, kuna vitu
alinifundisha mtaalamu ikitokea hivyo nafanya vipi, shemeji sio lengo sana la kutoa ujumbe wa mizimu, mizimu wao walilnga mtoto, unajua ni kwanini, ni kwasababu yeye atagusa hisia za wengi, na yeye ndiye damu hasa ya marehemu, shemeji...anatikiswa tu,...ndio maana nilipowaomba hao mizimu, walikubaliana na mimi, wanatupatia muda…’akasema.
‘Hahaha, Dalali..unajua unaongea sana, hivi huogopi kudanganya, unataka nini hasa, mali, utajiri...Dalali, Dalali, kumbuka haya maneno yangu....haki ya mayatima na wajane, ni bomu ulilolilalia..likilipuka, huponi,..’nikasema.
‘Ndio hapo tunapokosana mimi na wewe, mimi nawajali wale watoto kama watoto wangu, kawaulize kama hawatakuambia, wale watoto wananipenda sana mimi, nawajali ..hata mama yao,...sasa huko kunishutumu hivyo, sijui inatokea wapi,..ni kuhusu hiyo nyumba, ndugu yangu, nikuelezeje ili upate kunielewa, sio mimi,..ni benki..huo ndio ukweli,’ akasema akionyesha kuchoka.
‘Unajua ni kwanini shemeji yako alipoteza fahamu..ngoja nikuambie ukweli wake, ...na nilishangaa pale ulipofika na kukimbilia kashfa, unaonaeeh, ndio maana alichelewa huku nyuma, kumbe ndio hivyo, mnashikana kimahaba, ...Dalali, usifikrie watu wote wapo kama ulivyo wewe...'nikasema
'Ni hali ilivyojionyesha pale...'akasema
'Kuwa humuamini shemeji yako hadi ufikie kumkashfu, tuombe mungu hakuyasikia hayo maneno yako machafu, ...maana pale alishapoteza fahamu, hata hivyo, inakubidi wewe mwenyewe umuombe msamaha kwa kauli zako chafu…’nikasema.
‘Kwa jinsi mlivyokuwa pale, kwa yoyote yule
angeliwafikiria hivyo, najua nimekosa,...kwa hilo mimi mwenyewe nitamuomba shemeji,anisamehe…lakini…mimi
na wewe tutawindana kama paka na panya, umeshatangaza uadui na mimi..’akasema.
‘Mimi sijui hilo…kwanza nikuulize huo uadui ni wa
nini..kwasababu ya kuutafuta ukweli eeh?...ndio hapo naamini, kuwa ukweli na
uwongo huwa haviivani, au sio.?.haya niambie umesema unataka kuongea na mimi,
ni kuhus nini…?’ nikamuuliza.
‘Si nimeshakuuliza, mimi nina kosa gani, mpaka
nafikia kushikiliwa hapa…?’ akauliza.
‘Jibu lake nimeshakupatia, au sio, waulize polisi
waliokuleta hapa…’nikasema.
‘Sio kweli ndugu…kuna zaidi ya hilo, ..’akasema.
‘Zaidi ya hilo ni…wewe umekataa kutoa ushirikiano,
kwanini unakataa kusema ukweli, kwanini unakataa kuhojiwa tu, na sasa unadai
mpaka wakili wako awepo, huoni kwa watu kama hao, watakuwa wanakutilia
mashaka…’nikasema
‘Sikiliza sasa nikuambie jambo moja, mimi nitatoka
hapa, na kila kitu kitafanyika kama mahakama ilivyo taka, na sio mimi,…ni
mahakama, na sio mimi, ni bro, ni deni lake lilipwe, na mimi kwa hilo
nitapambana na kila mtu anayenizuia, siwezi kukubali kaka yangu ateseke huko
alipo…, eti kwa vile kafariki, hapana lazima hilo deni lilipwe….’akasema
akijikuna, suti ilikuwa imejikunja kunja.
‘Ni kweli kama ni deni lake la halali, litalipwa, na
tutajitahidi kuongea na watu benki tuone jinsi gani watasaidia hilo…lakini
kabla ya hapo, ni lazima tujirizishe, au sio….na…na…hadi hatua hii , kwangu
mimi naona hilo deni sio halali kwa marehemu…’nikasema
‘Sawa, kama
umeona hivyo, mimi sikupingi, ila sasa, kwa nia njema tu, toa ushahidi, ili
tuweze kulimaliza hili, mimi sina tatizo na hilo..sio kwamba nalazimisha
hapana, ushahidi upo wapi…eeh, niambie…’akasema
‘Hatua kwa hatua,…ushahidi utatolewa, na ushahidi
mwingine utakuja kujitoa wenyewe bila hata ya kutumia nguvu, nina imani hiyo…’nikasema.
‘Maneno matupu hayatasaidia ndugu yangu, wewe
mwenyewe unafahamu utaratibu wa kimahakama…. hebu nielewe ndugu yangu…, mimi
nipo tayari kusaidia hapo, kama utapatika ushahidi… lakini sio kwa maneno, mimi
nilikuwepo mahakamani, wao wanahitajia ushahisi, …sasa unao, sijui kama
tunaelewana hapo…’akasema
‘Ushahidi utakuwepo, wa kimaandishi na mashahidi, na
mimi nilishakuambia wewe ni mmoja wa ushahidi wangu..hujanielewa tu…’nikasema
Dalali akaniangalia, akionyesha uso wa kukata tamaa,
baadae akasema;
‘Sasa kuna jingine ambao nilitaka kukuambia… . ile
familia ilikuwa ikinitegemea mimi,
nibangaize huku na kule, ndio ipate kula, mama mjane na watoto wake,.ni
watu wa kuhudumiwa, eeh..unanisikia sana…’akasema na mimi nikabakia kimia
‘Sasa kwa vile mimi nimeshikiliwa hapa,..hilo sasa ni
jukumu lako, hakikisha ile familia inapata kula, na huduma zote za msingi…unasikia
ndugu ?….ndio hivyo, ili muone ni kwa
jinsi gani nilikuwa napata shida, …mimi ndio ilifikia nifanye hata yale
yasiyofanyika, watu hawajui tu…’akatulia kidogo.
‘Je kama ulikuwa unaionea huruma kihivyo,..hiyo
familia mbona unaacha wanafukuzwa kwenye sehemu yao halali ya kuishi , na
unashabikia kwa nguvu zote , hiyo nyumba yao ipigwe mnada….au ulitaka uwapatia
nyumba yako moja wapo,..kama umeweza kumjengea hata bibi yako wa nyumba
ndogo,sizani kama utashindwa hilo,…’nikasema
kama utani na yeye akacheka, akitikisa kichwa
‘Wewe mjanja sana wewe, eti nyumba ndogo, acha hiyo kabisa…najua
unaelekea wapi….hahaha hunipati ng’ooo…’akasema sasa akipiga miayo, na akawa
ananyosha-nyosha tai yake vyema, halafu, akaniangalia na kusema;
‘Dalali nikuulize jambo…sio kuuliza, bali ni
kukushauri je …upo tayari kutubu dhambi zako, ukausema ukweli wote, kuhusiana
na hilo deni, ili haya mambo yaishe kwa haraka….?’ Kwanza akatabasamu, halafu
akanikazia macho na kusema;
‘Kutubu dhambi,…hahaha, dhambi gani hiyo.., eeh, mimi
sina kosa wamenishikilia hapa bure tu, na mim nitawashitakia kwa hili, yaani
kutii amri ya mahakama ndio nipata adhabu hii, nitamuuliza hakimu, je mimi
kufanya hivyo, kutii amri yake nimekosa nini…’akatulia kama anasubiria jibu
kutoka kwangu, na mimi nikawa nimetulia tu, halafu kwa sauti ya chini,
akaniuliza
‘Hebu hata wewe niambie mimi nina kosa gani hapo… ,
maana haya yote umeyaanzisha wewe…na sio mimi , kiukweli wanaoharakisha hilo ni
watu wa benki, mimi naingia hapo kwa vile mizimu imenijia na kunihakikishia
kuwa hilo deni ni la marehemu..sasa ulitaka mimi nifanye nini hapo eeh, nia-ambie..?’
akauliza akinikazia macho.
‘Hivi hukusikia kuwa mtaalamu katoroka, hebu jiulize
ni kwanini akatoroka, na kabla ya hapo alishahojiwa, je unajua aliongea nini,
na baada ya kuhojiwa sana, hadi kufikia kuongea ukweli…sasa aliongea hadi
polisi wafikie kukuleta huku kituoni…? ‘ nikamuuliza , akacheka kweli kweli,
halafu akatikisa kichwa, akasema
‘Mtaalamu katoroka kwa vile anaona anateseka bure, na
polisi hawawezi kumuachia kirahisi…hawana jipya hawa watu, hwana shitaka dhidi
yaken hali kama hiyo, ..hata ingelikuwa mimi, …kama kuna upenyo huo..wa ku-roka
aah.., kwanini nisitoroke, sema yeye anaweza kutumia utaalamu wake, mimi
siuwezi huo huo utallamu wake unaoneeh….’akasema hivyo
‘Ni hivi ngoja nikuambie ilivyotokea kwa mtaalamu..’nikasema
‘Hadithi….’akasema hivyo, na mimi sikumjali
nikaendelea kuongea
‘Mtaalamu alipobanwa sana na maswali na mbinu za
kipolisi, akaongea mambo mengi tu…, na aliyoyaongea, anajua yatamuweka yeye
matatani, na kwa vile kaambiwa mtakutanishwa wewe na yeye, akaona sasa
keshakusaliti, ndio akaamua kutoroka…’nikasema
‘Hahaha…kaongea mambo gani ya kunisaliti mimi…?’
akauliza
‘Kuwa wewe unafahamu kuhusu hilo deni, ..wewe ulifika
kwake, kuomba yeye afanye mambo yake ili hilo deni liendelee kuwa ni la kaka
yako,..alipoulizwa hilo deni hasa ni la nani, akasema wewe ndiye unafahamu
ukweli wa hilo deni…, wewe hukutaka kuusema huo ukweli kwake…, ila wewe ulitaka
ifanyike namna deni hilo liwe ni la marehemu, zifanyike hujuma za kushinikiza,
na ndio hivyo, nyumba ipigwe mnada,…’nikasema.
‘Hahaha, wewe mtunga hadithi kweli….lakini kiuhakika
hiyo hadithi yako, haijakaa vyema kabisa, ifikirie tena…..mtaalamu haweza
kuogopa kukutana na mimi, …na kwanini asingeliniambia hilo hata kwa simu, kuwa
kafanya hivyo…kwahiyo hayo maneno yako umeyatunga
wewe, yeye hajasema hivyo…’akasema.
‘Wewe kwanini hujiulize ni kwanini akatoroka,…..ina
maana yeye hafahamu kosa la kutoroka polisi lilivyo kubwa, kama kweli hana kosa…?’
nikauliza.
‘Tutakuja kulifahamu hilo…ngoja wakili wangu afike,
maana analifanyia hilo kazi, na mimi mwenyewe nitakuja kuufaham ukweli wote…’akatulia
kidogo
‘Ndugu yangu,..unapoongea hivyo, kuwa sijui eti mimi
nafahamu ukweli wote kuhusu hilo deni, eeh, ina maana wewe unawafanya benki ni
wajinga, hawana kumbukumbu za uhakika, haah, ndugu yangu wewe, fikiria hadithi
nyingine sio hiyo…’akasema.
‘Dalali wewe una nyumba ngapi…?’ nikamuuliza na hapo
akashtuka kidogo, halafu akatabasamu, akatikisa kichwa na kusema;
‘Unaona…wewe hadi hapo huna hoja tena…, sasa
unakimbilia kuangalia mali zangu, unatakia nini hilo…nikiwa na nyumba moja au
mbili inakuhusu nini…’akasema
‘Inanihusu sana, maana shemeji yako alipofahamu kuwa
wewe una nyumba tatu za kifahari, ulizopangisha mashirika , nyumba moja
umemjengea nyumba ndogo yako, na wewe unaishi na ile nyumba, ile nyumba yenyewe
unayoishi, ni ya gharama sana, shemeji yako…alishtuka sana, …’nikasema hivyo na
Dalali, nikamuona akihangaika.
‘Ina maana..umemdanganya shemeji…ku-ku---wa..’kabla
hajamaliza mlango ukafunguliwa, na jamaa mmoja mwenye suti kali, aliingia
mkononi kashikilia briefcase yake,…naona ni jamii za akina Dalali, watu wa
kujiona
‘Karibu wakili
wangu…’akasema Dalali akijaribu kuwa na tabasamu mdomoni na mimi nikasema;
‘Hatakusaidia kitu,…ukweli wako ndio utakusaidia,…kumbuka
hujajibu swali langu…’nikasema
‘Muheshimiwa,…karibu, sana…’akasema akisimama
kusalimiana na huyo jamaa.
Mimi nikawa bado nimemkazia macho Dalali.
Na kabla huyu jamaa hajapata muda wa kuongea, mara mlango
ukafunguliwa, akatokeza askari mmoja, na kutuangalia, hakusema kitu..
NB: Kazi imeanza, je kuna nini kwenye haya yote;
nyumba, kupoteza fahamu kwa mama mjane..na kutoroka kwa mtaalamu?
WAZO
LA LEO: Tunaweza kuuficha ukweli kwasababu ya masilahi
madogo tu, tukasahau haki za watu wengine,..tukashindwa kuwa na hata huruma na
jinsi gani watu hao wanavyoteseka, kwa kukosa haki zao, na huenda haki hizo
zingeliwasaidia wahanga hao kwenye haja zao muhimu, ikiwemo matibabu, na
mengineyo, na huenda kwa kukosa haki hizo wengine watafikia kupoteza maisha,
kwasababu hiyo tu….huwezi jua,..je utawezaje kulilipa hilo deni mbele ya mola.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment