‘Wakili
wako atakukuta huko huko kituoni, mimi
sina muda tena wa kupoteza hapa,…unasikia Dalali…’akasema mpelelezi akitumia
sauti yake ya kikazi zaidi.
Dalali,
akajua sasa hana la kufanya, …na akawa anataka kuongea, mpelelezi akamkatiza
kwa kusema;
‘Unajua
nilipofika hapa, nilitaka mazungumzo yangu ikibidi yaishie humu humu ndani,
japokuwa kulikuwa na shinikizo jingine…’akasema mpelelezi akimgeukia mama
mjane.
‘Nilijua
haya mambo yanaweza kuisha kifamilia zaidi, lakini kwa vile nimeona nyendo zisizo za
kawaida, basi twende hivyo hivyo unavyotaka
wewe…’akasema mpelelezi sasa akimshika mikono Dalali na Dalali hapo akawa hana
jinsi bali kukubali, lakini kabla hajaanza kutembea kutoka nje, akageuka
kumuangalia shemeji yake akasema;
‘Usijali
shemu, haya yatakwisha…mimi sina kosa lolote , hawa wanajisumbua bure, muhimu
ni deni lilipwe, hilo nitalipigania kwa nguvu zote, najua hilo ni dhima kwangu,
na kama ikitokea mtoto kuumwa tena, wewe tumia hiyo dawa, itamsaidia tu…’akasema.
‘Sawa
shemeji, jichunge tu..na uwe mkweli…’akasema mama mjane.
‘Ahsante,…usijali,
nitakuwa mkweli kwa ajili ya familia yetu, mimi ndiye nimeachiwa majukumu yote
na Bro, hawa watu hawajui tu…’akasema na kuanza kutembea kutoka nje. Na
mpelelezi alipoona mimi nimebakia nyuma akasema kwa sauti akiwa huko huko nje…
‘Wewe mtu wa jamii, twende, ni lazima na wewe
ufike huko kituoni, umesahau kuwa na wewe unahitajika huko …’akaniambia
mpelelezi
‘Nakuja afande,
ngoja niweka mambo mengine sawa, nivumilieni kidogo tu…’nikasema
‘Haya
nakupa dakika tatu…’akasema mpelelezi
‘Anataka
kufanya nini na shemeji yangu,…’akasema Dalali,
‘Ingia
kwenye gari….atakuja…’nikasikia sauti ya mpelelezi sasa ikitoa amri.
Tuendelee
na kisa chetu
**************
Mimi huku
ndani, nikamsogelea mama Mjane, kama
vile sikutaka sauti yangu isikike huko nje maana mlango ulikuwa wazi,…mama
mjane alikuwa kasimama huku akiangalia kule mlangoni, na alipoona nimemsogelea
akaniangalia kwa mashaka kidogo….
‘Shemeji…oops,
Dada…mambo sasa ndio yameanza hivyo, hakuna kurudi nyuma tena, kama na lolote
la kuniambia muda ndio huu…’nikasema
‘Kama
lipi, mimi nimeshakuambia kila kitu, au…?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho ya
kujiiba iba.
‘Ni hivi,
wewe…, jaribu uwezavyo, sijui kwa vipi, lakini jaribu kwa kadri ya uwezo wako,
ukijua hili ni pambano muhimu kwako, jaribu, na jaribu,…kumbuka kila kitu,
..chochote chaweza kusaidia hii kesi,… usiogope kusema kitu chochote, unanielewa,
huwezi jua,…? ’nikasema.
‘Sa-sawa..lakini…’akawa
anataka kuongea jambo lakini anasita kuliongea.
‘Lakini
nini….usiogope kabisa, sasa hivi hakuna cha mizimu au uchawi wao, mtegemee
mungu tu, hayo yalikuwa mambo yao ya kutishia watu, huyo mtu wako kabanwa, na
kitisho alichokipata huko, sijui tena..kama yakitokea tena basi kweli yaweza
kuwa hiyo mizimu, lakini sio kwa kupitia kwake,…na inavyoonekana mtaalamu ana
kitu kinahusiana na hili tatizo, deni…bado nashindwa kuunganisha, lakini
tutakuja kuona,…’ nikasema.
Nilipoongea
hivyo huyo mama mjane akageukia kuangalia kule mlangoni, nikahisi huenda hayo
majinamizi yamemrudia tena, kwa jinsi alivyokuwa akiangalia sana huko nje....lakini….
‘Mimi
ninawasiwasi sana na hao ndugu zake shemeji…’akasema mama mjane, na hapo ndio
nikamuelewa ni kwanini yupo vile.
‘Unaogopa
lawama au sio…mbona bado haupo makini kuna nini unakiona…?’ nikauliza
‘Ndio,…wewe
huwajui hawa watu walivyo,…’akasema.
‘Je
inajalisha kitu, ni hilo kuhusu hao watu au kuna kitu kingine hujaniambia
shemeji , maana mimi sasa nakwenda vitani, na wewe ndiye msaidizi wangu…’nikasema
‘Hakuna
kitu kingine ni kuhusu hiyo familia ya akina shemeji,..inabidi nifanye
jambo,..niwapigie simu…’akasema
‘Ok, sawa…na
je ukiwapigia simu utawaambia nini, kuwa shemeji yako kakamatwa kwa kosa gani,
inatakiwa afikishwe huko na huko watasema wamemchukua kwa kosa gani, au…?’nikasema
na kabla hajajibu nikaendelea kusema;
‘Sawa sio
mbaya unaweza kuwapigia tu…ila nikuuliza jambo, hivi tangia haya matatizo
yatokee, wao kama ndugu wanakusaidia nini…?’ nikamuuliza.
‘Hakuna
wanachonisaidia, wao ni lawama tu, wengine ndio hufikia kunisema vibaya kuwa
haya nimeyataka mimi mwenyewe, mara nimemriuni hata huyu shemeji, haambiliki
tena, yaani binadamu mie nina damu ya kunguni…’akasema
‘Umeona
eeh…lakini wapigie tu…’nikasema
‘Nimewaza
sana hilo…she-..kaka yangu, huyu Dalali ni mtu mwema kwa kweli, amekuwa
akinisaidia bila kujali maneno ya ndugu zake, yupo tofauti na ndugu zake kabisa…,
amenisaidia pale nilipohitajia msaada , kwahiyo kwangu mimi nashindwa kuelewa,
itakuwaje,…je ndio …sijui unanielewa hapo…’akasema.
‘Lakini
moyoni mwako unahisije, kuwa …huyu mtu hana hatia, au ana hatia…je unavymjua
yeye alivyo, kweli …eeh, hawezi kufanya lolote baya, dhidi yako , hasa kwenye
hii nyumba, au…hahusiki kwa lile,..kwa jinsi ulivyomsikia nikimuhoji…?’
nikamuuliza.
‘Aaah,
sasa atahusikanaje maana yeye ndiye ..katika kusaidia kashika nafasi ya
marehemu, katika kuwajibika na hii familia, mimi kama mimi siwezi kumshuku
yeye,…huenda wapo watu wanamtumia,…sijui , nasema tu, huenda….naah…na-na kwa
tamaa zake ndio kajiingiza huko, lakini kwanini afanye hivyo..nashindwa kusema
lolote baya dhidi yake..’akasema
‘Nikuulize
tu dada,…usinielewe vibaya, …Dalali hajawahi kukutamkia neno, kutokana na tamaa
zake, neno la mapenzi..?’ nikamuuliza na hapo akashtuka, na akatikisa kichwa,
halafu akasema;
‘Khaa,
kwanini unasema hivyo…Dalali, japokuwa alikuwa mkubwa…walikuwa wakiishi hapa,
wakawa wananiheshimu…mimi namzidi umri, na …ndio namfahamu alivyo, nimekuwa
nikimkemea sana, ana tabia hiyo ya tamaa, ..na, na…uhuni siwezi kukuficha hilo,
lakini ilikuwa ni ujana,…’akasema
‘Hahaha,
shemeji…oh, unajua ushemeji umekaa zaidi ya udada, unamtetea sana shemeji yako,
hapo kiushahidi yaonyesha ana nyumba ndogo, …unajua nikuambie kitu dada, tabia na hula za watu hazijifichi, .ok, hebu
niambie kwa tabia hiyo ya tamaa na uhuni, tuseme hivyo, yeye hakuwahi
kukutongoza…?’ nikamuuliza
‘Mimi
naona …sipendi kuyaongea hayo, ila naweza kusema ujanahuwa unakuwa hivyo…’akasema.
‘Dada
nina maana yangu kubwa sana kukuliza hilo, nimekuambia kila kitu kinahitajika
usikizarau, je aliwahi kukufanyia hivyo,..?’ nikamuuliza
‘Ndio…aliwahi
na nilimfokea sana, akajuta sana, na alijua labda nitamuambia kaka yake, lakini
sikuwahi kufanya hivyo, nilijua ni ujana…wakati mwingine nilikuwa namfuma
akichungulia mlangoni,..sasa vitu kama hivyo, mimi na akili yangu nitasemaje..ni
ujana, namkanya , na kumsihi,…’akasema na niliona alijisikia vibaya kuongea
hayo, yaonekana hakutaka kuyasema hayo.
‘Nakuelewa
sana Dada, unajua nataka unifahamu, kwanini nakuuliza haya, tabia ya mtu
hujengeka na hulka yake, tokea utotoni, ujanani…..kuna matendo yanajijenga
hivyo, yapo ya kihulka, wengine hujidhibiti, jinsi umri unavyokwenda, wengine
wanashindwa, vitu kama wivu,.uwongo, uhuni nakadhalika, haya yanaweza kuleta
picha ya mtu alivyo..’nikasema.
‘Lakini kwangu
mimi niliona kuwa ni ujana tu, na tokea siku ile …aliniogopa sana….nahisi ni
kwa vile alijua labda, nitakuwa nimemuambia kaka yake au nitamuambia kaka yake…na
ingelitokea hivyo, , ningekuwa na tabia ya kuwachukia, …wangeondoka hapa mapema
sana, kaka yao hataki mchezo, kuna maswala ya kusamehe, alishawaambia, lakini,
wizi…umalaya, ushirikina,…mmh..’akasema.
‘Je
katika maisha mengine, maana hapo kuna wizi, na uwongo..…hajawahi kukushawishi
jambo, …au kufanya jambo la aina hiyo, na ikafikia hadi kumkalisha chini na
kumkanya, jambo ambalo sio la kawaida…kufanya kitu kama hicho,….’nikaachia hapo.
‘Kama
nilivyosema huyu mtu nimeishie naye…alionyesha tabia kama hizo, lakini kwa
kulinganisha , yeye alikuwa na afadhali sana, nilimweka vizuri, akaja kuwa tu
mwema kabisa,…kuna kipindi niliamua kuwa naye karibu sana, ili kumbadili…mpaka
watu wakanishisi vibaya…sikuwa na nia mbaya…’akasema
‘Je aliwahi
kukushauri kitu, mfano kakosea, …au kutokana na tamaa, kuwa mfanye
jambo,kinyume na matakwa ya mumeo,…sisemei mambo ya mahusiano hapo,
nazungumzia, tabia nyingine,…?’ nikamuuliza.
‘Kuna
kipindi alikuwa na shida kubwa sana…karibu afungwe…akaniomba nifanye jambo, ili
aweze kupata pesa, kwa kupitia kwa kaka yake, …maana asingeliweza kumuambia
kaka yake kitu kama hicho,….na mimi nilikuwa kama mzazi wao, mtu wao wa karibu
wa kulilia shida zao…lilinipa shida sana hilo tukio….’aliposema hivyo, moyoni
nikasema safi kabisa.
‘Hebu
niambie hapo…ilikuwaje,….kuna kitu hapo tunaweza kukiunganisha kikatusaidia…’nikasema
na hapo nikaona mdada akinywea, nahisi alijuta kwanini kaniambia.
‘Lakini
nilimpinga sana, sitaki kwenda kiundani ilikuwa ni kitu gani, tafadhali
nielewe, ..na mimi…nikatafuta mbinu nyingine za kumsaidia, nikakopa kwenye
vikoba, nikawa nakatwa, kidogo kidogo, na likaisha hivyo, kutokana na hilo,
akawa ni mtu anynijali sana,..sasa mimi siwezi kufahamu zaidi kama kuna mengine
,na yangelikuwepo ningeyafahamu…’akasema.
‘Dada…niambie
ukweli…mume wako hajawahi kukulamikia lolote kuhusu maswala ya benki, kupotea
pesa, na kitu kama hicho..?’ nikamuuliza na hapo akabakia kaduwaa kidogo, kama
anatafakari.
‘Mhh…mume
wangu ni msiri sana hasa kwa ndugu zake..wakikosea jambo, yeye alikuwa akiwaita
sirini, kwenye maktaba yake, atamsema wa kumsema, na hapendi kuwaita wengi, ni
kila mmoja kwa zamu yake, alikuwa hapendi kabisa kumsema mtu mbele ya watu
wengine,…’akatulia
‘Na wewe
ukikosea ilikuwaje..?’ nikamuuliza , na hakuelewa lengo la swali langu akasema;
‘Hata
mimi nikikosa, atatafuta nafasi, hata kunitoa nje, anaweza kusema anataka
tukale nje, hotelini, huko mtakula, baadae unaanza kukuambia hilo jambo,
atakusema weee, kiukweli mume wangu alikuwa mtu wa peke yake, nilimpenda sana…na
hata sijui kama atatokea mtu kama huyo,…kiukweli, hapana …’hapo machozi
yakaanza kumtoka.
‘Naelewa …umemkosa
mume muhimu sana katika maisha yako…’nikasema
‘Kiukweli
hapa nilipo nimekufa nusu… isingelikuwa watoto wangu, niliona ni heri nimfuate
tu…kiukweli..nilijaribu hata kujiua..lakini nilipofikiria watoto
wangu..nikashindwa,…nilikimbilia kunywa maziwa… sasa hebu fikiria hii hali,
nipo hai wanafanyiwa hivi, je ningekuwa sipo ingelikuwaje…’akasema.
‘Sawa
dada..ila nikuulize tu, wewe kwa uoni wako, huoni kuwa shemeji yako, anaweza
kuwa kaungana na huyo mtaalamu, ili kufanikisha hili tatizo….?’ Nikamuuliza.
‘Mimi
sijui..ukisema hivyo, unataka mimi nimuhisi shemeji yangu uchawi…maana kama ni
kweli wanahusika hivyo,..basi watakuwa ni wachawi, kama ni kweli, sijui kama
nitawasamehe,..hapana shemeji yangu hawezi kufanya kitu kama hicho…’akatulia.
‘Nakuuliza
tena, wewe kwa jinsi ulivyoona, ..haiwezekani ikawa hivyo, kuwa kuna kitu
shemei na huyo mtaalamu wamefanya pamoja,..nataka kufahamu msimamo wako hapo…’nikasema
‘Ni tamaa
ya kupata pesa, kwa vile hilo deni lipo, ila…siamini kuwa ni deni la marehemu
mume wangu…’akatulia
‘Sasa kwa
vile eeh,…deni lipo, labda ni makosa ya
benki..mimi sijui…, japokuwa kiukweli ilivyo kwa benki, ni ngumu sana kutokea
kitu kama hicho, sasa sijui ilitokeaje…, nashindwa kuamini hilo pia,…’akatulia.
‘Sasa kwa
vile hilo deni lipo na wameona hivyo..kwa ushahidi wao kuwa ni deni la
marehemu, na wao wanataka pesa yao irudi wao watafanya nini…, ndio wakafikia
hapo kuwa hii nyumba ipigwe mnada,…sasa huyu Dalali anaingiaje hapo,
ninavyohisi mimi, yeye anaingia hapo kwa vile anataka na yeye afaidi huo ujira
wa mnada…’akasema
‘Unaamini
hivyo,…kuwa yaweza kuwa hivyo…mhh…hapana, ni kiasi cha gharama ya kupiga huo
mnada, sizani kama ni pesa nyingi hivyo, za kutolewa macho na watu wengi hivyo…mhh,
anyway…nimekuelewa…’nikasema hivyo.
‘Hawa
watu walivyo, wanafanya kazi kwa asilimia ya lile deni…na huenda kuna zaidi ya
hapo, waliahidiwa hivyo na benki, …hapo siwezi kujua,…ulipoongea hapo, hata
mimi najiuliza kwanini awaambie watu wengi, …mmh, hapo hata mimi naanza
kuingiwa na mashaka…’akasema mama mjane
‘Umeona
eeh…ni zaidi ya ushuru wa mnada,..ni zaidi ya …kulipwa deni lenyewe, maana deni
litalipwa benki, wao hawawezi kupata sehemu ya hilo deni, …sasa ni kitu gani
kipo nyuma ya hilo deni…ndio maana nataka wewe ufikiria sana, ukumbuke
sana..unanielewa…usinione hivi, kuwa namuandama shemeji yako bure…nahisi kuna
jambo…’nikasema.
‘Mhh….mimi
sijui zaidi ya hapo…nifanyaje sasa…?’ akauliza
‘Sasa
hivi wewe wapigie hao ndugu zake simu…waambie Dalali kachukuliwa kituo cha
polisi, wakikuuliza kuhusu nini, waambie hata wewe hujui kitu…usiongee
sana…’nikasema
‘Ina
maana polisi wameshagundua kitu, kuwa huenda shemeji anahusika na …na, lolote
lile kuhusiana na hilo deni,…?’ akauliza mama mjane
‘Kiukweli
siwezi kujua hilo, hawajaniambia bado, ila..…kiukweli shemeji yako amejitahidi
sana, kukuonyesha kuwa anakujali…amejitahidi kwa vile anakufahamu, udhaifu wako…ila
uelewe kitu hapo, nafsi ya mtu ina siri kubwa sana, watu wengi wanavyotenda,
wanavyojionyesha kwa wenzao, sivyo hivyo walivyo ndani ya nafsi zao,…’nikasema
‘Ni kweli…’akasema.
‘Wengine
wanaigiza tu…hawa wanaofanya hivyo…kuigiza wema…lakini nafsini mwako wana
chuki…,waogope sana, ni aheri yule anayekuonyesha waziwazi, sisemi hivyo, kwa
nia mbaya ya kukujengea chuki wewe na shemeji yako, hapana,..na hadi sasa
sijawa na uhakika huo , kuwa huenda shemeji yako ana nia hiyo mbaya, bado
tunatafuta ukweli…’nikasema
‘Sawa
nimekuelewa kaka yangu…’akasema
‘Unajua
Dalali ana nyumba ngapi…?’ nikamuuliza
‘Mhh,
nyumba ngapi…hapana yeye ana nyumba yake anayoishi na mkewe, …’akasema
‘Ok..labda
aliwajengea….ila ilivyogundulikana ana nyumba kubwa tatu, kapangisha
makampuni,..na hiyo moja anaishi nyumba ndogo…’nikasema
‘Nini….una
uhakika…!?’akainamisha kichwa chini kama anawaza jambo
‘Ndio
maana nakuambia hivi…umjuavyo shemeji yako …sivyo alivyo, yawezekana ni
kutokana na kazi zake,…sio shida…hilo hatuliangalii sana..ila kwa hali kama
hii, inabidi atuambie kajengaje…’nikasema
‘Siamini….ina
maana, hata haiwezekani…’akasema
‘Je sasa
upo tayari kusema ukweli, kuhusu shemeji yako, vinginevyo atawafanya nyote
wajinga,..na watakaoumia ni wewe na mtoto,…’nikasema
Mama
mjane taratibu akachuchuma, mara akakaa chini….pale nilipo niakaanza kuingiwa na wasiwasi ...ni kitu gani tena hiki...ikanibidi na mimi nichuchumae karibu yake...nikawa nasita kumshikilia, na kabla hata sijafanya kitu ..mara akawa anayumba kama anataka kudondokea sakafuni, nikamzuia kwa mkono, kwa kitendo hicho, karibu nidondoke chini.
Kwa jinsi nilivyochuchuma,...ilibidi niwe na balansi ya kutosha, kumzuia, ...maana alikuwa kama kalegea hivi...ila machoni alionekana yupo sawa,...
'Una nini tena...?' nikauliza.
'Ku-kumbe ni kweli...hapana haiwezekani...'akasema na mara huyo akanidondokea sasa...uzito ukanifanya na mimi nikae sakafuni, akawa kalaza kichwa kwenye magoi yangu...kwa haraka sasa najitahidi nisimame ili nimweke sawa, na mara mlangoni sauti ikatoka
‘Mwanajamii
unafanya nini muda wote huo huku ndani...oooh,…’ilikuwa sauti ya Dalali, alikuwa kasimama mlangoni, na nyuma yake yupo
mpelelezi.
NB: Tuendelee
WAZO LA LEO: Watu wengine walivyo nafsini
mwao sivyo walivyo kivitendo,…wanaweza kuongea tu, ili kurizisha watu wengine,
ili kuonekana ni wema, ili…kujenga ujiko....kuhakikisha wanafanikisha malengo
yao, lakini nafsi zao zimejaa usiri mkubwa, …usiri unaweza kuwa wa chuki,
husuda, nk…, na..kama wangeliweza kufichua hicho walichokadria ndani ya nafsi
zao, huenda ungelikimbia. Nafsi ni kichaka cha hisia mbali mbali, nzuri na
mbaya. Muhimu tuweni na subira kwa kila jambo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment