‘Afande, Dalali
anadai kuwa hakumbuki kuwa muhasibu aliyekuwepo awali, kipindi marehemu akiwemo
ndio huyo huyo aliyekuja kukutana naye…wakati anafuatilia hilo madeni…’nikasema.
‘Ndio
sikumbuki…’akasema Dalali kwa sauti ya kunikatisha.
‘Una
uhakika bwana Dalali, maana kauli zako nyingi ulizosema zimekuja kuonyesha wewe
sio mkweli, na mimi naanza kukutilia mashaka, sasa niambie ukweli je ni kweli
hukumbuki hilo…?’ akauliza mpelelezi.
‘Afande,
hivi wewe unawakumbuka wahasibu wa benki waliokufanyia kazi ulipoenda benki,
ndio unaweza kumkumbuka mmojawapo kama ulifanya naye jambo la kukumbuka au sio,
lakini mara nyingi ilivyo,..ukitoka benki umetoka na mambo yako, …naweza labda,
nikimuona tena, lakini kwa vile sina kazi naye kwanini nimuweke akilini…unanielewa
hapo afande…’akasema Dalali.
‘Umesikia
jibu lake mtu wa jamii..’akasema mpelelezi.
‘Dalali,…kinachonisikuma
zaidi niendelee kukuhoji wewe ..na kinachonifanya nihisi kuwa kuna jambo
limejificha kupitia kwako kwenye hilo deni, ni kauli zako…jinsi unavyoficha
mambo, hutaki kusema ukweli, najiuliza ni kwanini..’nikasema
‘Ukweli
upi ndugu yangu, wewe umeniuliza swali na mimi nimekujibu kadri ya
ninavyofahamu , sasa kama maelezo yangu huyaamini, mimi nifanyaje…’akasema.
‘Awali
ulisema wewe huna usuhuba na mtaalamu, ushahidi umetoka kuwa huyo mtaalamu ni
rafiki yako wa karibu tu…je huo ndio ufahamu wako, …na kwanini ulituficha hilo…?’
nikauliza.
‘Nilishaelezea
sababu zangu, kuwa huyo jamaa ni mganga wa kienyeji, na wengi hawapendi
kujionyesha kuwa wapo karibu na watu hao, ni kutokana na udhaifu wetu
tu..lakini wao ni wenzetu, wanatusaidia sana, sema kazi zao hazipo rasmi
kivile..unaonaeeh..na wengine wanaweza kukuhis vibaya kuwa umekuwa karibu naye
ili kazi zako zifanikiwe,..kuondoa hizo hisia ndio maana tunaficha…’akasema na
kugeuka kumuangalia mpelelezi.
‘Haya
sawa, kwa utetezi wako huo kwa mtaalamu..ila najua ni kwanini ulilificha
hilo..sasa nauliza tena kwa huyo muhasibu, je ni kweli ulivyosema kuwa
hukumbuki,..na hilo nalo kwanini unalificha…?’ nikamuuliza.
‘Sikuelewi…maana
jibu la hilo swali nimeshalitoa…na..sijui wataka nisemeje, labda nikuuliza wewe
una ushahidi gani kuwa hayo ninayoyasema sio ya kweli…maana ..eeh, nini
ninyeufahamu huo ukweli ndio maana ukaniuliza, au..mimi sijui, wataka mimi
nisemeje..’akasema.
‘Kwenye
simu yako una namba ya huyo mhasibu,…kweli si kweli..?’ nikamuuliza, kiukweli
nilimuuliza tu , na sikuwa na uhakika huo,…nikaona matokea yake, jamaa
akashtuka na kuiangalia simu yake…
‘Umeonaje
ndani ya simu yangu…?’ akauliza.
‘Nijibu
ukweli, …je wewe huna namba yake kwenye simu yako…?’ nikauliza
‘Sina
uhakika, nina namba za watu wengi sana, huenda..unajua tena, hata hivyo, kuwa na
namba ya mtu sio sababu yak um-eeh, kukumbuka huenda nilichukua tu…’akasema na
kusita kidogo.
Mpelelezi
sasa akaichukua ile simu ya Dalali, na alipoona imezimwa akamuangalia Dalali,
Dalali akaangalia chini.
‘Kwanini
umezima hii simu…bwana Dalali?’ akauliza mpelelezi.
‘Niliona
inasumbua, maana kila dakika hapa utasikia simu yangu ikiita, na matokeo yake
naanza kuadhirika mbele ya shemeji yangu hapa, nyie hilo hamlioni hapa, mimi
namuheshimu sana shemeji yangu…’akasema.
‘Usinitumie
mimi kwenye mambo yako, wanaume wote ndivyo mlivyo…’akasema mama mjane
Mpelelezi
akamtupia jicho mama mjane na mama mjane akaangalia chini, na Dalali akasema;
‘Lakini
kaka alikuwa hana tabia kama zangu au sio shemeji…’ akasema Dalali akionyesha
utani, mimi nilishajua lengo lake ni kupotezea lengo.
‘Mume
wangu sio sawa na wanaume wengine ndio maana mpaka kesho sitakubaliana na hilo
deni kuwa ni lake…’akasema mama mjane sasa kwa kujiamini.
‘Shemeji,
chunga ulimi wako, hao mizimu….’akata kusema na mpelelezi akamkatisha kwa
kusema;
‘Dalali
iwashe hiyo simu na unitafutie namba ya huyo muhasibu wa benki…’akasema
mpelelezi,na kumfanya Dalali sasa abakie mdomo wazi, …alitulia kidogo baadae
akasema;
‘Afande,
nina namba za wahasibu wengi wa benki, sasa sijui ni yupi….’akasema
‘Ambaye
ulienda kwake kufuatilia hilo deni ,…’akasema mpelelezi.
Dalali,
akatulia kwanza kwa muda, halafu akachukua simu yake na kuanza kutafuta namba..,
akapata namba, na kusema;
‘Nahisi
namba yake ndio hii hapa, unajua nilichukua namba yake maana ingelinisaidia
kwenye kufuatilia hilo deni, kama namuhitajia…’akasema huku akisita kumkabidhi
mpelelezi.
Mpelelezi
akaiangalia ile namba, na kuona jina, mbele ya hilo jina kumeandikwa,mhasibu wa
benki, halafu akatikisa kichwa, kitendo kile kilimfanya Dalali awe na mashaka
kidogo, akawa kama anataka kuongea jambo, lakini mpelelezi akamuwahi kwa
kusema;
‘Mbona
ulisema hukumbuki, Dalali, unajua kila hatua unanifanya nianze kukuhis vibaya,
watu wetu walishachunguza na kubaini kuwa hilo deni la marehemu,..lipo, na
ushahid ulivyo, hilo deni, ni deni la marehemu kweli…, lakini wewe unavyofanya,
inanifanya hata mimi niingiwe na mashaka..’akasema mpelelezi.
‘Afande,
nimechoka kwakweli…hebu nioneeni huruma na mimi..maswali yamekuwa mengi sana,
wakati mwingine najihami tu, kukataa ili isije ikawa ni swali la mtego,..mhh…’akajitetea
‘Kwahiyo hivi
sasa umemkumbuka huyo muhasibu uliyeulizwa, kuwa ndio yule yule aliyekuwepo
kipindi cha marehemu…?’ akaulizwa.
‘Huyu
muhasibu nina namba yake, maana ilibidi nichukue namba yake wakati tunafuatilia
uhalali wa hilo deni, sasa hilo la kukumbuka kuwa ni yeye aliyekuwepo kipindi hicho
akiwepo marehemu,…mmh, sijui kwakweli,…unajua ningelijua kuwa hilo swali
nitaulizwa, ningelimuuliza,..…’akasema.
‘Una
uhakika Dalali…?’ akaulizwa
‘Sina
uhakika ..siwezi kujibu uwongo..sikumbuki kwakweli…’akasema
Mpelelezi
akanigeukia mimi na kusema;
‘Ushahidi
wako huo,…niambie sasa…’akasema mpelelezi
‘Naomba
uipige hiyo namba…’nikasema na nilivyosema hivyo hata mpelelezi mwenyewe
akaniangalia kwa mashaka, na kabla hajasema neno,…Dalali ndiye akadakia na
kusema.
‘Kwanini..hiyo
ni simu yangu bwana, kama unataka kuongea naye piga kwa simu yako…kwanza
unataka kuongea naye kitu gani?’ akauliza akionyesha mashaka, hakujua kuwa
kitendo hicho kimemfanya mpelelezi amshuku vibaya, huenda angelinyamaza kimia
mpelelezi asingelichukulia jambo hilo ni la muhimu.
‘Ili nithibitishe
kauli yangu,…ili nithibitishe ushahidi wangu…’nikasema
Na
mpelelezi hakusubiria kibali cha Dalali, akafanya vitu vyake na kuipiga ile
namba ikaanza kuita, Dalali akawa anaangalia tendo lile kwa mashaka, na baadae
sauti ikasikika ….
‘Uncle…mbona
umenipigia tena…’sauti ikasema
Mpelelezi
akampa Dalali simu, Dalali kwanza akasita kuipokea , baadae akaipokea huku
akiuma uma maneno kama..
‘Ni-ni..ongee
naye nini sasa…’akasema na wakati huo simu ilishakuwa mikononii mwake, ndio
akasema kwa haraka;
‘Ni-ni-nili-likuwa
najaribu namba yako….nilijua labda hafanyi kazi…’akasema Dalali
‘Unajaribu
namba yangu!!! Uncle mbona siku zote unanipigia na inafanya kazi, vipi leo
ufanya kuijarbu, kwani kuna nini huko uncle…’sauti ikasema.
‘Basi
hamna shida…’akasema Dalali, kabla hajakata sauti ikasema;
‘Uncle,
…nina hali mbaya sana, huo mnada kweli utakuwepo hapo kesho, unajua ukifanyika
kwa haraka ndio unafuu kwetu, umenielewa uncle, fanyeni mambo yenu hili jambo
limalizike haraka..’sauti ikasema.
‘Sawa
nimekuelewa…’akasema Dalali.
‘Upo
wapi…mbona unaongea kwa mashaka, sio kawaida yako..?’ sauti ikauliza
‘Nipo..ofisini…’akadanganya
hivyo.
‘Sawa
..usinipigie tena, unasikia,…tuliahidiana hivyo, na iwe hivyo, na ukifanikiwa
wewe nipe ishara tu, na hadi hapo…hunijui, hatujuani, au sio, kwaheri…’simu
ikakatika.
Ukimia
ukatanda,…Dalali kainamisha kichwa, na mpelelezi, akasogea pale alipo Dalali
akaichukua ile simu na kuweka mezani,…na mimi nikasema;
‘Nawakilisha
ushahidi wangu afande…’nikasema na Dalali kwanza alinywea, lakini baadae
akazindukana, na kusema;
‘Ushahid
kuhusu nini sasa, unajua mimi nashungulika na watu mbali mbali, sasa usitake
maneno ya watu ukayaingiza kwenye shutuma zako..ndio alikuwa mfanyakazi wa
benki, na alipotoka benki akaniomba nitamfutie kazi…ndio maana pamoja na yote
huyo nina namba yake…nimeshakumbuka hilo.’akasema Dalali
‘Hahaha
Dalali, kwanini hutaki kuwa mkweli, huyo mhasibu mnafahamiana naye sana…kipindi
marehemu yupo hai, hadi hii leo,…hata kabla ya yote mnafahamiana tu, nitakuja
kulithibitisha hilo baadae….na ni kweli wewe ulimsaidia kupata kazi benki,
awali …lakini sasa yupo wapi …’niliposema hivyo nikamuona akivuta pumzi ya
kuhema.
‘Sawa….sasa,
kumsaidia mtu kupata kazi ni moja ya kazi zangu za udalali…kuna ubaya gani hapo,
kuwa wapi , yupo, ana shughuli zake, kwani, unataka kusema nini hapo…?’
akauliza
‘Tutakuja
kuliona hilo, ila lichukulie kama angalizo, kuwa kuanzia sasa, ujue mambo yako
mengi yameshagundulikana, muhimu ni wewe kutoa ushirikiano, vinginevyo,…usije
kumlaumu mtu..’nikasema
‘Afande
mimi sipendi kauli ya huyu mtu, ina maana keshanishuku tayari, tatizo huyo mtu
anaonekana ni mtaalamu wa kutunga hadithi, hapo alipoe, eeh..keshafikiria
hadithi yake na kuniweka mimi kama muhusika wake mkuu..’akasema akicheka kwa dharau
‘Sasa nakuambia
kitu,.. hapa kwangu unapoteza muda wako bure, mimi sina makosa, mengine ukiona
nayafunika ni kwa masilahi ya kazi zangu, najua dunia ilivyo, fitina nyingi,
ushindani wa biashara, ndio hivyo…’akasema Dalali.
‘Sawa…ila
tunahitajia, kukutana na huyo muhasibu,..tuambie tutampata wapi, isije ikawa
kam ya mtaalamu…’nikasema nikimuangalia mpelelezi.
‘Kwa hilo
siwezi kukudanganya, mimi sijui…’akasema
‘Dalali,
usitupotezee muda, mbona unakuwa na mashaka mashaka, unakosa gani..?’ akauliza
mpelelezi.
‘Kwanini
unasema hivyo afande, mimi sina mashaka yoyote..ila siwezi kusema huyo mtu yupo
wapi, labda. Eeh wazo zuri, mpigieni simu yake mumuulize nyie wenyewe, nitasema
labda yupo mahali fulani, kumba hayupo, mtasema mimi ni muongo…’akasema na
mpelelezi akachukua simu na kuipiga hiyo namba tena.
‘Namba unayopiga kwasasa haipatikani, jaribu
tena baadae…’ikasema hivyo
Mpelelezi,
akamuangalia Dalali,…baadae akachukua simu yake akapiga namba…
‘Ni
mimi..ndio,…nataka ufanye jambo,….uliniambia kuhusu maswala ya benki, ndio…ulishampata
huyo mtu…basi naona kuna umuhimu umtafute, ..ndio ndio…sawa, nitasubiria kutoka
kwako…’akakata simu na kugeuka kuniangalia mimi.
‘Naomba
niongee na huyu mtu kwanza kuhusu maswala yangu..unaonaje maana muda umekwisha…’akasema
mpelelezi.
‘Mhh..nilikuwa
sijamalizana naye…’nikasema
‘Najua…lakini
kuanzia sasa mazungumzo yote hayatafanyika hapa…ni muhimu na mimi nimuhoji, ila
sijamuhohi hapa, nitamuhoji kituoni..’akasema mpelelezi.
‘Afande,
samahani lakini mimi nimechoka, na huko kituoni kufanya nini,kwanini
tusiyamalizie hapa hapa, kunipeleka kituoni ina maana gani, kuwa nimefanya kosa
gani au mnanishuku nini mimi…?..’akasema Dalali kwa kuuliza hivyo.
‘Hujachoka
bado..nikuambie kitu, ..nilikuambia tokea awali, ukweli wako ndio
utakusaidia,..mimi nilipopata taarifa kuwa ushahidi wa benki unasimamia kwenye
hukumu zilizopita kuwa hilo deni ni la marehemu, nilisharizika hivyo, lakini
kwa jinsi ulivyoonyesha hapa, hata mimi naanza kushuku kuna jambo…’akasema
mpelelezi.
‘Kuna
jambo gani…?’ akauliza Dalali kwa kujiamini.
‘Ni
kwanini unadanganya…?’ akauliza mpelelezi
‘Nilishaeleza
hayo..kutokana na kazi yangu, siwezi kuongea mambo mengine mbele za kila mtu…’akasema
‘Mbele ya
watu wako,… unaogopa pia, na mimi ni mtu wa usalama, natakiwa kuufahamu ukweli,
huniamini hata mimi..?’ akauliza mpelelezi.
‘Kuna
mambo mengine ya kazi zangu, naweza nisikuamini hata wewe…unajua tena hali
ilivyo, sio kila kitu kipo sawa sawa, ili tufanikiwe wakati mwingine tuna njia
zetu, na nji hizo nyie hamtazipenda, au sio, ni hali hali, hata wewe unafahamu
afande…si unataka nikuambie ukweli, ukweli ndio huo…’akasema.
‘Dalali…mimi
sijaanza kazi leo,…kuna jambo unatuficha, nilikupatia muda,..umeshindwa
kuutumia vyema…sasa inabidi tuongozane mimi na wewe, na..huyu mtu wa jamii hadi
kituo cha polisi..’akasema na hapo Dalali jicho likamtoka.
‘Kwanini
kituo cha polisi…?, mimi nina makosa gani..?’akauliza sasa akimgeukia shemeji
yake, kama vile mama mjane atamsaidia kwa hilo.
‘Natimiza
wajibu wangu…’akasema mpelelezi.
‘Kwa
kauli hiyo, basi mimi namuhitajia wakili wangu, ngoja niwasiliane na wakili
wangu kwanza…’akasema
‘Mimi
nakuita kituoni kwa kukuuliza maswali, ..sio kuwa nakushutumu kwa kosa lolote
..unasikia, na mojawapo ya maswali yangu ni kuhusiana na ajali ya kaka yako,
iliyosababisha kifo chake…awali sikutaka kuliweka hili wazi kuwa mimi nakuhitajia
kituoni, ila nilipofika nakuona kinachoendelea, nikadhamiria na mimi kukuhoji
hapa hapa, lakini yaliyokuja kutokea yananifanya na mimi nione umuhimu wa wewe
kuhojiwa kituoni..’akasema.
‘Lakini
nilishakuambia…’akalalamika
‘Ndio,
kwani una wasiwasi gani..?’ akauliza mpelelezi
‘Mi-mi…sina
wasiwasi, laini kuitwa kituo cha polisi ina maana gani, kuwa unashuku mimi, kama
unanishuku kwa jambo fulani, mimi kama raia mwema nina haki ya kusikia kosa
langu au sio hiyo ni hali yangu..?’ akauliza
‘Huna
makosa…nakuhitajia huko ili kutimiza wajibu wangu, kuhusiana na ajali ya kaka
yako, na sasa pia kuhusiana na hilo deni la benki…’akasema.
Dalali
akasogea akitaka kuchukua simu yake
‘Unataka
kufanya nini…?’ akuliza mpelelezi
‘Nataka
kumpigia simu wakili wangu…hiyo ni haki yangu…’akasema Dalali
Mama
mjane, akawa anafuatilia hilo tukio bila kusema neno, baadae akaona asikae
kimia, akasema;
‘Kwahiyo,
mnataka kusema nini mbona sielewi kinachoendelea..?’ akauliza
‘Dada,
ndio kazi imeanza,…usiwe na wasiwasi, …shemeji yako akitoa ushirikiano hili
tatizo litakwisha, ila akiendelea kudanganya, …mimi sijui…’nikasema
‘Mimi
sijadanganya bwana, nimeshawaambia kwanini vitu vingine nafanya hivyo..ila wewe
tokea awali unanitishia sana, nilishakuona, sasa umeshatangaza vita dhidi
yangu, tutaona…’akasema.
‘Dalali,
dalali…vita ukitangaza na mimi umetangaza vita na familia yako, mimi nayafanya
haya kwa ajili ya hii familia, sio zaidi ya hapo..’nikasema
‘Mnafiki
wewe,..wewe njaa yako itakuponza, wewe ngoja tu…’akasema
‘Usijali,
pindi hivi tutapata chakula au sio, mnada ukipita na mimi siutanikatia kiasi,…usinisahau
Dalali, nimeona hata huyo mtu wa benki kasema usimsahaau..unajua ni kwanini…huyo
anajua kila kitu au sio….?’ Nikamuuliza.
Dalali
hapo akanitolea jicho, utafikiri anataka kunimaliza
‘Utaona…’akasema
Dalali
‘Huko
kituoni au, unamtegemea Mtaalamu, mtaalamu hayupo nawe sasa, anajipigania
nafasi yake, au niaona nini ndugu yangu ..?’ nikauliza.
‘Ninakuambia
ukweli…mimi sina kosa, yote niliyoyafanya nimetimiza wajibu wangu tu, na kazi
kubwa ilikuwa kuhakikisha kuwa roho ya bro, inakuwa salama, deni ukifariki ni
nani atalipa eeh, watakaomsaidia marehemu ni waliopo duniani, mimi nimefanya
kosa gani hapo…’akasema akimuangalia shemeji yake.
‘Mimi
sijui kitu…ninachotaka ni uhakika wa hilo deni, ila ..kauli yangu hadi kesho,
hilo deni sitaweza kuamini kuwa ni la marehemu mume wangu…’akasema mjane.
‘Kwahiyo
shemeji umenigeuka au sio…usifikiri kwa kufanya hivyo ukweli utabadilika, na…naenda
polisi, je yalitokea yaliyotokea kwa mtoto ni nani atakusaidia…?’ akauliza
Dalali.
‘Mungu
yupo, atanisaidia…’akasema mama mjane.
‘Ndio
hivyo shemeji umeshasahau fadhila…’akalalamika Dalali.
Mpelelezi,
sasa akamkabili Dalali..
‘Tusipoteze
muda, twende…’mpelelezi akasema na Dalali, akawa hasogei.
‘Mimi
siwezi kuondoka hapa mpaka wakili wangu afike..’akasema Dalali sasa
akijitutumua.
Mpelelezi,
akatikisa kichwa, ..akashika simu yake…akaanza kupiga namba, na Dalali kwa
haraka naye akachukua simu yake akawa anapiga namba,..
WAZO LA LEO: Njia ya muongo ni fupi…njia ya
dhuluma ina ukomo wake, hata iweje dhuluma kamwe haidumu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment