‘Hakuna
aliyekukataza kupokea simu…iwashe hiyo simu yako.’akasema mpelelezi.
Dalali
akawa na mashaka sasa, lakini akaiwasha ile simu yake, na wakati anawasha ile
simu ikaanza kuita….na sauti ikajaa kwenye chumba,...
Tuendelee na kisa chetu...
***********
‘Bosi umesikia
habari hizo, eti mtaalamu kakamatwa na polisi,mimi sikuamini ….’sauti ikasema
‘Unasemaje,
una uhakika, …kakamatwa!...khaa…, kwasababu gani, ok, ok….nipo kwenye kikao
nitakupigia…’akasema na kabla Dalali hajakata
hiyo simu, huyo mtu akasema;
‘Vipi bosi
kuhusu malipo yetu, maana mnada utafanyika kama kawaida, wale jamaa hawawezi
kuzuia tena, hawana cha kutulipa ni maneno matupu tu, sasa utatulipa lini,
unajua tena …’akasema
‘Nini…unasema
nini malipo, malipo gani, nitakupigia baadaye….’akakata simu, na kubakia
amesimama, akawa kuduwaa kama anawaza jambo, na mpelelezi akamuendea, na kunyosha mkono.
‘Hebu
nipe hiyo simu yako…nitakaa nayo, kuanzia sasa….’akaambiwa na hapo akashikwa na
butwaa zaidi, akawa kama anataka kuiweka hiyo simu mfukoni, huku akisema;
‘Kwanini
afande,…mbona una shaka sana, hao ni vijana wangu kwenye kazi zangu za Udalali…’akasema
‘Vijana
wako, wanajuana na huyo mtaalamu …?’ akauliza mpelelezi
‘Mbona watu
wengi wanamfahamu sana mtaalamu, na wameniambia hivyo kwa vile niliwatumia
ujumbe wa maneno kumtafuta huyo mtalaamu, kwa vile mkewe anamtafuta pia,..’akasema
‘Sawa
hamna shida, nikuulize tu, kakamatwa,kwa kosa gani..?’ akauliza mpelelezi
‘Hata
mimi sijui, labda wewe utusaidie kuuliza huko ofisini kwenu…vinginevyo inabidi
niende kuulizia mimi mwenyewe…’akasema Dalali sasa akionekaan hana raha.
‘Kwanini
wewe uende kumuulizia wakati awali ulishasema kuwa wewe huna usuhuba na
mtaalamu , wewe sio rafiki yake wa karibu..?’ akaulizwa.
‘Usuhuba
ni wa kikazi tu, na ndio maana mkewe akaniuliza mimi , zaidi ya hapo sina udugu
naye, au urafiki wa karibu saana, sema kutokana na kazi yangu wengi
ninapowafanyia kazi nakuwa nimeshajenga udugu wa kikazi….na mkewe kaniamini, na
mtu akikuamini hivyo utafanyaje, eeh, nafanya usamaria mwema…’akasema.
‘Haya
nipe hiyo simu nitabakia nayo, mtu akikupigia, mimi nitakupatia, hamna shida…’akasema mpelelezi
‘Hii simu
ni mali yangu, …au sio afande….’akasema na alipoona mpelelezi bado kamnyoshea
mkono wa kutaka simu hiyo ipelekwe pale alipo, Dalali sasa akasema kwa shingo
upande
‘Na
kiukweli afande hii simu yangu Itakusumbua
bure, watu wengi wananipigia mimi mwenyewe ndio najua ipi simu ina muhimu
kupokea kwa muda huu, wengine ni wasumbufu tu …’akasema.
‘Sikiliza mimi nipo kazini, na tendo lolote
utakalolifanya kuanzia sasa litachukuliwa kama kitendo cha kunizua mimi nisifanye
kazi yangu….’akasema afande.
‘Afande
mimi nina haki zangu pia kweli si kweli.., kwanini uichukue simu yangu, kwani
mimi ni mhalifu…?’ akauliza Dalali.
‘Kwasababu
huyu mwenzako kadai huo ni ushahidi wake…kama wewe unajiamini kuwa huna kosa,
kwanini uogope kufanya hivyo…?’ akauliza afande.
‘Yeye
kadai ni ushahidi wake,lakini kwa kosa gani nililofanya mimi,eeh… na je kosa
hilo limefikishwa kituoni kwa utaratibu maalumu, mimi siogopi kabisa, najiamini
kwa vile sina kosa,..?’ akauliza na kusema.
‘Usitake
kupoteza muda hapa….au kwahiyo wewe unataka huyo mtu wa jamii afanye hivyo, afungue
mashitaka dhidi yako, au…?..., maana mimi nionavyo hapa nyie mnajaribu kufanya
mazungumzo yenye lengo la kubaini ukweli wa hilo deni, kuulizana kama
yawezekana kosa limetokea hapa, na mimi hapa ni mlinzi wa usalama…’akasema
Hapo Dalali,
akasimama na kusogea hadi pale alipokaa mpelelezi na kuitoa ile simu yake na
kumkabidhi afande kwa shingo upande, huku akisema;
‘Sawa
mimi sina shaka kabisa afande….ngoja nifanye utakavyo…’akasema
‘Haya
sasa tufanye hivi,… wewe sogea ukae hapo karibu, ili simu yako ikipigwa tu, mimi
nakupatia haraka iwezekanavyo…’akasema akiiweka ile simu mezani mbele yake.
‘Mhh…sawa,
hamna shida..’akasema Dalali akisogea na kukaa karibu na alipokuwa mpelelezi.
‘Na
tuendelee na maswali , maana naona yana kitu ambacho kinaweza kunisaidia hata
mimi, nikaweza kulifunga jalada la hii kesi,…..ila sasa muda nao umekwenda...sasa
ni saa ngapi, eeh....’akawa anaangalia saa yake na mara mlango ukagongwa.
**************
Aliyeingia sasa hivi alikuwa yule Mpelelezi wa
awali. Alionekana ana haraka, kwanza akituangalia kwa haraka , sekunde kadhaa,
kama vile karizika na jambo fulani akaingia ndani.
Kwa upembeni nilimuona Dalali, akionyesha uso
wa mashaka, lakini kama kawaida yake akajipotezea, huku akimuangalia huyo
mpelelezi akiingia ndani.
Huyu mpelelezi ndiye aliyekuwa
akiishughulikia hii kesi, tokea awali, alipoingia mwenzake akasimama,
wakashikana mkono kusalimiana.
Wakati huo huo simu ya Dalali ikawa inaita, na Dalali
alionekana kama ana shauku ya kuiendelea hiyo simu yake lakini hakuweza,…akajikausha
tu, na huenda hapo alikuwa akiombea huyu mpigaji, asiendelee kupiga , lakini
simu ikaendelea kuita..simu iko hatua chache na alipo Dalali, lakini hawezi
kusimama kuichukua.
Mpelelezi akasogea pale ilipo hiyo simu, na
akafanya kama alivyokuwa akifanya awali, na akaashiria Dalali, aichukue,…na
hata kabla Dalali hajaishika, sauti ikatanda hewani. Simu hiyo ya Dalali ina
sauti kubwa sana, ilitosha sauti ile kujaa mle ndani, kila mtu akawa anasikia.
Ilikuwa sauti ya mwanamke…
'Shemeji mbona mwenzako amekamatwa na polisi, ni
kuhusu huo mchezo wenu mchafu au sio…?’ sauti ikauliza
‘Mchezo gani mchafu, mtani ..shemeji acha huo
utani wako mimi nipo ofisini na wateja, usije kuniharibia talanta yangu, ulikuwa
unasemaje…?’ akauliza Dalali na kusema huku akibenua mdomo kwa tabasamu la
uwongo…kama kweli wanataniana.
‘Hahaha..nyie wawili mkikutana hamnaga kazi
nzuri, siwaamini kabisa, jiulize ni kwanini mwenzako kakamatwa na polisi…nakumbuka
weye ulisema huyo mwenzako hawezi kukamatwa na polisi hata siku moja maana yeye
analindwa na mashetani…je mashetani wamekimbia malaika nini…hahaha..’hiyo sauti
ya mwanamke ikasema na kucheka
‘Sikiliza shemeji..’akasema Dalali.
‘Nisikilize nini wewe, sa hizi unaniita shemeji,
shemeji, upo na mkeo nini,…sasa wewe ndio usikilize mimi, mwenzako kaondoka hapa bila kuacha hata senti moja, mimi
sio kituo cha kulea waume waliokimbia wake zao...umenisikia…’sauti
ya kike sasa ikiongea kwa jaziba, huyo mwanamke ana sauti nzito.
Kwa upande nilimuona mama mjane akitikisa
kichwa cha kusikitikika. Na Dalali akaliona hilo, akasema;
‘Wewe mwanamke acha utani wako, wengine
wanaweza kufikiria ni kweli, nimekuambia nipo ofisini…’akasema
‘Hahahaha…leo unalo, na usikate simu maana nina
ujumbe muhimu sana kwako, ukinikatia simu na wewe nitakukata
pasipokatika…’sauti ikasema
Dalali akawa anahangaika kutaka kuzima hiyo simu,
mpelelezi akawa anamuashiria aendelee kuongea, na Dalali, akawa sasa kashikilia
sehemu ya kuzima simu, na sauti ikawa inaendelea kuongea;
'Shemeji unanisikia lakini, naona sauti zinakuwa
mbili mbili, sio hoja,…kama upo na mkeo mimi sijali, maana mumenifanya mimi ni jamvi la wageni, au sio, nataka na yeye
alielewe hilo, nyie watu wawili mkome kabisa na tabia zenu mbovu..isingelikuwa
ni pesa, mimi ningejua cha kuwafanya… , sasa ni hivi, nataka pesa yangu..’sauti
ikasema.
'Nitakupigia baadae shemeji tafadhali
nielewe…’akasema Dalali.
'Utanipigia ndio..ni lazima ufanye hivyo..ila
lazima ujumbe huu ufike kwako kwanza..mimi ndiye nimekupigia, kwa gharama
zangu…, huyo ni rafiki yako jana kalala hapa kwangu, najua kakimbia huko
alipotoka, nilimsikia mkiongea naye .…sasa wewe ukija kwangu…’akatulia.
Kuna mtu alikuwa akimuongelesha huko alipo,
kama anamuita … na sauti ilikuwa ya kukasirika, hivi, na yeye akasema akiongea
na huyo mtu mwingine;
‘Fanya utakayo, mimi nisipoongea na hawa
wanaume utaipatia wapi hiyo pesa, ….baadae nitakuja…’akasema.
‘Nimekuelewa shemeji….naona unataka kutuchina
kwa ajili ya wanaume wako...’Dalali akasema
‘Hahah shemeji shemeji,..uje kwangu ili ujue ni
kwanini mwenzako kakamatwa, ukienda kichwa kichwa huko polisi na wewe utaswekwa
ndani, dili yenu itawaumbua kabisa, nyie mtaona tu..’akasema
‘Dili gani na wewe…?’ akuliza Dalali
‘Wataka niiseme kwenye simu, hahaha, shauri
lako, mdomo wangu hauna zipu, wewe njoo, mwenzako alijikuta anaropoka ovyo,
unacheza na mtoto mie,.…ukija uje na pesa yangu, mimi sasa sijali kama huo
mnada utafanyika au la....kwanza niambie, huo mnada utafanyika lini ..nimesikia
umesitishwa?’ sauti ikauliza.
'Shemeji nimekuambia nitakupigia,…’akasema Dalali.
'Nataka pesa yangu, na umwambie huyo mwenzako,
ujanja wake wa kutishia watu kwa uchawi wake, mimi haniwezi kabisa…mimi siogopi
uchawi wake, kwetu nimeaga vizuri tu…na nawaambia mwaka huu mtakoma ubishi, ile
enzi ya utapeli utapeli imekwisha, sasa kazi tu, mnada, mnada, upo wapi sasa…’sauti ikasema.
.
'Shemu...'Dalali, sasa hakujali amri ya mpelelezi
akakata simu.
Wapelelezi hawa wawili, wakaangaliana na bila
kusema neno, wakasogea pembeni, wakawa wanaongea kwa sauti ya chini chini,
hatukuweza kusikia wanachokiongea. Na hapo Dalali akapata muda wa kuzima ile simu
yake. Kwani ilishaanza kuita tena.
Mimi sikujali hicho kitendo chake, akilini
nilishakuwa na yangu ya kutafakari. Hadi hapo sikuwa umuhimu sana na huyo
Mtaalamu, akili yangu ilikuwa ikitafuta jinsi gani hilo deni lilitokea, kama
limetoka kihalali, na benki wameaminisha hivyo,..je inawezekanaje hilo deni lihamie
kwa marahemu, inawezekana kweli…
Sasa kama ni
kweli hilo deni ni la marehemu,…kitu ambacho mimi bado sijaamini, inakuwaje
Dalali alishabikie …labda Dalali anasaka tonge la kupata ujira wa udalali kwa
kupitia kivuli cha madalali wenzake, na
ndio maana waunde mizimu, hapana hapa kuna kitu kimejificha, ni kitu gani hicho..?
nikawa najiuliza hivyo…
Na wakati nawaza hivyo, nikamsikia mpelelezi yule
wa awali akisema kwa sauti niliyoweza kuisikia japokuwa kwa shinda;
'Ushahidi wote waonyesha hivyo, kuwa hilo ni deni
la marehemu hakuna ubishi, lakini haya yanayotokea kushinikiza lilipwe, kinyume
na benki ndio inatia doa, au sio …’akasema mpelelezi aliyeingia.
' Ni kweli hata mimi hapo ndio natia shaka, kama ni
deni la marehem iweje haya mengine yote kutokea ..na huyu mtu wa jamii
anataka kuthibitisha nini sasa, maana maswali yake yamifungua macho, nahisi
kuna kitu kimejificha..?’ akauliza mpelelezi aliyekuwepo na kutoa maelezo yake..
‘Siunajua anavyofanya kazi zake, muache
aifanye, wala usimzuie..baada ya hapo utafanya yako unayotaka,..kama kakosea
utajua la kufanya, lakini tuone kwanza atagundua nini…na kwa vile amedai anao
ushahidi, na ni vyema tuone huo ushahidi kabla hatujachukua hatua nyingine, unakumbuka
yaliyowahi kutokea huko nyuma, yasirudie tena….’akasema mpelelezi aliyeingia.
‘Sawa, ndio maana sikutaka kumzuia kwanza kwa
kuchelea hilo, hata hivyo, nina yangu, ni lazima niifunge hii kesi kwa upande
wangu, sijui nyie huko..maana kwangu sijaona kitu cha kutilia mashaka…ila kuna
kitu nimekiona, kwa huyu Dalali, sio mkweli,..ngoja tuone kwanza..’akasema
‘Sasa ..bado mnaendelea maana mnasubiriwa
siumesikia amri ya wakubwa huko juu, nimetoa msaada bila utaratibu, ..lakini
hilo nitamaliza hamna shida,…’akasema mpelelezi aliyeingia
‘Kwahiyo ulikuja kuniarifu au kumchukua mtu wa
jamii..?’ akauliza
‘Hapana…nimepitia tu hapa, nilikuwa na safari
nyingine, kuna mzee mmoja nilimpitia kumuhoji,…na nikaona labda naweza kumuhoji
kidogo huyo Dalali, ila kama mnaendelea naye mimi naweza kuondoka, nitarudi
baadae,..’akasema mpelelezi aliyeingia
‘Kumuhoji mzee gani..?’ akauliza.
‘Mzee mtupe, kuna maswala anafunganishwa nayo,
ila haya msingi,…’akasema mpelelezi aliyeingia.
‘Na huyo mtaalamu vipi..?’ akauliza.
‘Unaju ahuyu jamaa nilikuwa natafuta namna ya
kumpata tu, amekuwa akitoa maneno ya kujinadi kuwa yeye, hata akifanya kosa
hawezi kukamatwa na polisi kutokana na nguvu zake za giza,…sasa tumeshamkamata…’akasema
‘Kwa hivyo, mbona….’akauliza mwenzake.
‘Hatujamkamata kwa kauli zake hizo…, hapaka
kuna kosa kalifanya, hujiulizi ni kwanini alikimbi akwenda kujificha,..ila
pamoja na hayo kuna haya yanayohusina na mwenzake huyo Dalali, japokuwa
keshakana na kusema yeye hahusiki, maswala yote mengine aulizwe Dalali,..…’akasema
mpelelezi.
‘Ndio nataka kufahamu kakamatwa kwa makosa
gani, ni haya haya ya deni, au kuna mengine zaidi..?’ akauliza
‘Utakuja kuliona hilo baadae,…kuna tuhuma nyingi
zimeelekezwa kwake na pia kuna makosa yanawashirikisa wote wawili sasa kuhusu
hilo la deni, bado hatuna ushahidi nalo,tunamtegemea huyo mtu wa jamii,
aliyepeleka hayo mashitaka,…na vyovyote iwavyo, ninachotaka mimi ni kulimaliza
kabisa hili tatizo kama deni lipo lilipwe, au lipate mwenye uhalali nalo. Ili haki
ije kutendeka...au sio…’akasema.
‘Kwahiyo hawa watu wameshafikisha rasmi mashitaka,
kuwa deni hilo sio halali, ofisini..?’ akauliza huyo mpelelezi aliyekuwepo
‘Ndio wakili wao kafanya hivyo….japokuwa sio
rasmi, wanasema wanakusanya ushahidi…’akasema.
‘Imekaa vizuri kweli hiyo mashitaka bila
ushahidi, huoni ..ok, ik, ila mimi nataka hili jambo limalizike haraka iwezekanavyo..linatupotezea
muda wetu bure…’akasema mpelelezi, na kugeuka kumuangalia Dalali, aliyekuwa
akiirejesha simu yake mezani ikiwa imezimwa.
***********
Dalali alipoona kaonekana akizima simu,
akajibaragua na kujifanya kama anajinyosha, na mpelelezi akamuangalia tu,
baadae alipoona mwenzake anataka kuondoka, akamsogelea na kumuuliza;
‘Sasa huyo Mtaalamu anasemaje kuhusiana na deni…sijui
mnada, maana hapo sijaona kosa lake..?’ akauliza mpelelezi aliyekuwepo
'Inavyoonyesha ni tamaa tu za mali, kupitia ujira
wa Udalali, kuwa Dalali alimjia na kumtaka amtengenezee njia za mafanikio,
kwani kuna pesa anatarajia kuipata, ila hakuambiwa ni pesa gani, lakini hiyo
pesa ina mikono mingi, sasa anataka yeye awe na mamlaka nayo, unajua tena watu
washirikina walivyo ….’akasema mpelelezi aliyeingia
‘Unayaamini hayo maneno, kuwa ni hivyo tu…?’
akauliza
‘Kuna mengine ya mizimu sijui, eti kuna deni,
hilo deni limeleta madhara kwenye familia husika,, na kaliona hivyo kwenye
vipimo vyake sijui…’akasema
‘Mhh, sasa hayo utayathibitishaje kuwa ni kweli
au si kweli…?’ akauliza
‘Ndio maana nimeamua abakie kwanza kituoni,
kuna vitu nilitaka kuhakiki kwa wawili hao, kabla sijarejea kwake,…ngoja
tuendelee naye kwanza..’akasema mpelelezi .
‘Sawa…nitawasikiliza nyie, vinginevyo mimi
nitaifunga hii kesi, hasa kwa upande wangu kuwa ajali ilikuwa ya kawaida
tu…’akasema mpelelezi aliyekuwepo, na hapo wakawa wanaongea kwa utaratibu sana.
**************
Dalali ambaye lijitahidi kusikiliza
wanachoongea wapelelezi hao, lakini kwa upande aliokaa yeye, kama aliweza
kusikia ni machache,..ni yale tu, waliyoyaongea kwa sauti, na alipoona,
haambulii kitu ndio akamgeukia shemeji yake..
'Shemeji umesikia, hakuna ushahidi zaidi ya
ushahidi wa benki, mengine ni fitina tu… na hili lina nipa nguvu
ya kuendelea kutetea haki za Bro, kama alikuwa na deni, basi lilipwe, au sio
shemeji…'akasema Dalali, akimuangalia shemeji yake.
'Ina maana kumbe ni kweli shemeji, wewe ndio unashabikia udalali ili
nyumba ya watoto ipigwe mnada, ili na wewe upate cha juu…au mimi sikuelewa hapo?’
shemeji yake akamuuliza na Dalali kwanza akanitupia jicho mimi kabla hajajibu.
'Shemeji hizo ni fitina tu, mnada kisheria ni lazima
ufanyike, na mimi ningelifanya nini hapo eeh, ningewezaje kuuzuia hilo, na mimi
siwezi kushabikia hilo,…, eti kwa vile
na mimi ni Dalali hapana hayo yanakwenda
kivyake na mimi nipo kivyangu…’akasema Dalali.
‘Sasa kwanini kila mtu anakunyoshea kidole wewe kama wewe ndiye muhusika
mkuu kwenye huo udalali wa kuiuza hii nyumba huoni kuwa ni aibu, nyumba ni mali
ya watoto na wewe ni baba yao mlezi, wewe unashabikia iuzwe…?’ akauliza shemeji.
‘Mimi ni kiongozi wa umoja wa madalali, nielewe hapo…ndio maana kila
jambo likifanyika mimi natakiwa nihusike, vinginevyo, mimi ningekaa pembeni..nilijitahidi
kufanya hivyo awali, kwa vile inanihusu nikaambiwa nijiuzulu uongozi…’akasema
'Mimi hata sielewi, ina maana umeamini kabisa kuwa
hilo deni ni la kaka yako, …maana nilivyosikia ni ajenda tu za mnada, huyo
mtaalamu kasema hivyo hivyo, na huyo hawara wenu kasema hivyo hivyo, kila mtu
aliyepiga simu hapo kakusemea wewe kuwa ndiwe msimamuzi wa huo mnada. Na wanahitajia
pesa kutoka kwako, na nikiangalia kwa makini, ninaona hivyo..kuwa wewe unafurahia
hilo jambo,..’akasema mama mjane.
'Shemeji nikuulize kitu, mnada ukifanyika pesa za
kusimamia mnada analipwa nani ..?’ akauliza Dalali.
'Mimi sijui ..na kwanini unaniuliza hivyo…’akasema
shemeji mtu.
'Atalipwa mwenye kampuni hiyo ya mnada, sio mimi
lakini, na kwa vile ni lazima mnada ufanyike…basi mimi nitapata nini hapo,
nikae pembeni, wachukue kila kitu, nyumba na pesa ya mnada,…lazima na mimi
nidai changu kama mshirika na kiongozi…’akasema
.
'Kwahiyo wewe juhudu zako zote ni ili upate hiyo
pesa ya mnada…?’ akauliza mama mjane.
‘Pamoja na hilo…pia ni kuhakikisha pesa imepatikana nzuri, ili benki
wakichukua pesa yao, na sisi, eeh, tupate salio kubwa la kuweza kujenga nyumba
nyingine hata kama ni ndogo, umeniona nilivyojipanga hapo, sio nisuse tukae kimia, kila kitu kichukuliwe, utakuwa
ni ujinga…’akasema Dalali.
‘Sasa, kwahiyo ndio imefikia hapo , mnada unafanyika kesho au..unajua
mimi …hata sielewe, ina maana…’mama mjane akakatiza kuongea pale alipoona
mpelelezi yule wa awali anataka kuondoka.
'Unajua shemeji, sisi madalali tuna umoja wetu,
baada ya kuona kuwa ni lazma mnada ufanyike, sikuweza kujitoa, nikaona ni heri
kupata chochote, kuliko kukosa kabisa…ndio lengo langu kubwa mimi sina jambo
lolote kwenye hilo deni, kama anavyodai huyo mtu wako uliyemleta…’akasema sasa
akinigeukia mimi.
Mimi nikaona hilo lisipite bure, nikamuangalia Dalali, moja kwa moja
usoni, na kusema;
‘Tatizo sio hilo deni,..deni lipo sawa… tatizo ni uhalali wa hilo deni
kwa marehemu…kutokana na ushabiki wako, mimi bado nina shaka na hilo deni, na
nataka nionane na huyo muhasibu mliyeongea naye huko benki…’nikasema.
‘Nenda benki ndugu yangu, utaongea naye sana na nina uhakika utarudi
kwangu na kuniambia, kumbe ni kweli, nilikuwa napoteza muda wangu bure,..…ila ukumbuke
haya mambo ni ya muda sasa, nahisi utakuwa umechelewa,…’akasema Dalali.
‘Kwanini nimechelewa…?’ nikauliza
‘Ile benki imepitia mabadiliko mengi sana,..nilivyosikia, baadhi ya
wafanyakazi wengi wa zamani hawapo tena…sizani kama huyo mhasibu bado yupo, sijui
lakini maana sijafika huko muda, na nikifika siingii ndani, nitaenda kufanya
nini, wakati sina salio huko,…’akasema.
‘Nilikuuliza swali, je muhasibu huyo aliyekuja kukuangalizia hilo deni, ulipokwenda
kuhakiki, ndiye huyo aliyekuwepo kipindi kile marahemu akiwepo…?’ nikamuuliza.
‘Sina uhakika huo…kiukweli sikumbuki…siwezi kukudanganya kwa hilo, sina
jibu, …nikuambie kitu majibu ya maswali yako kama hayo ya kibenki, utayapata
huko huko benki..’akasema.
‘Sawa nautmabua huo sasa, kama ushahidi wangu mwingine…’nikasema.
‘Ushahidi, ushahidi huna lolote wewe, wenzako wamenishindwa utaniweza
wewe bwana, na ushahidi kwa nani…’akasema Dalali.
Kabla sijamjibu sauti ya mpelelezi….
‘Ushahidi gani huo wewe mtu wa jamii…?’ aliyeuliza sasa alikuwa
mpelelezi ambaye alirejea kwenye kiti chake, na Dalali alikuwa kageuka kumpa
mgongo hakujua kuwa mpelelezi amesharudi, aliposikia sauti yake alishtuka hadi
kiti kikatikisika.
WAZO ZA
LEO: Kila mtu nafsini mwake hupenda kuangalia yale yanayomrizisha, wengine hata
hawajali uhalali wa hayo mambo, ilimradi atafanikiwa kwenye malengo yake. Wapo
wacha mungu wanaofanya ibada lakini kwenye nafsi zao, wanajua kabisa kuna
matendo hawapo sawa, wanadhuluma, kimatendo wapo mbali na ucha mungu wao. Ukiwauliza,
watasema, tumekubaliana, amekubali, amerizika, lakini nafsini anajua kukubali
huko, kwa mwenzake yeye kamdhulumu. Tunamdanganya nani hapo, kuwa sisi ni
wajanja sana…imani ya kweli ya ucha mungu hupimwa hapo, kujali wengine kama
unavyojijali wewe mwenyewe, kuitenda haki , haki yake, na mwenye haki apate
haki yake, hata kama wewe utakosa kwa vile ulitakiwa ukose..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment