Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, July 27, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-26


‘Je huyo aliyekupigia simu …na kusema,… ‘‘,…..ila mimi nitapotea kwa muda…mpaka hali itulie, na sitaki uongee lolote kunihusu mimi tena,..haya uliyataka wewe….na kuendelea…’’,..akitumia namba ya mwanamke, akikulaumu kuwa alikuonya…je huyo  sio mtaalamu?’ nikamuuliza tena.

‘Nimeshakuambia huyo sio Mtalaamu…’akasema akinitolea macho

‘Ni nani huyo…?’ nikamuuliza

‘Nahisi ni mmoja wa wateja wangu, sina uhakika….’akasema hapo nikatikisa kichwa kusikitika, nikageuka kumuangalia mpelelezi,…mpelelezi alikuwa akimuangalia Dalali kwa uso wenye kushangaa.

‘Afande umeweka sawa hilo swali na majibu yake, huyo ndiye Dalali, na huo..ni mmoja wa ushahidi wangu mwingine, kuonyesha ni kwanini nimeona kuna haja ya kuliangalia hilo deni tena kama kweli ni la marehemu…ndio maana nimeshinikizwa na uhalisia, kuutafuta ukweli wa hilo deni,…’nikasema

‘Aaah…unajua usitake kunitega mimi…hapa mimi nimepigiwa simu na watu wengi, sasa..wakati mwingine nyie mnanichanganya, mimi  sijui ni nani unayemsema hapo…’akauliza

‘Unamfahamu sana Dalali mtu ninayemuongelea hapo…na muda mfupi umemuelezea kuwa aliwahi kusahau simu kama ilivyotokea kipindi hiki, umekubali kuwa alisahau simu, akatumia ya mtu mwingine ambaye mimi namuita nyumba ndogo..huko alipojificha..je huyo sio mtaalamu..’nikasema na hapo Dalali, akainamisha kichwa chini.

Tuendelee na kisa chetu.

**********

‘Sijui, sina uhakika na hilo….’akasema na mpelelezi akatikisa kichwa na kitendo kile kilimfanya Dalali, akune kichwa na kusema.

‘Samahani kwa hilo…nilitakiwa nijibu hivyo, kuwa sina uhakika, maana hata mimi nilihisi labda ndio yeye, lakini je kama akiwa sio yeye, na…sauti ipo tofauti,..je..hamuoni kuwa tutakuwa tumetenda dhambi, tukisadikisha kuwa ndio yeye…’akasema kama anauliza

‘Sawa…..,baada ya kulithibitisha hilo, kuwa mizimu sio chochote bali ni mbinu za kuogopesha watu tu kwa masilahi yao,..na wakati mwingine najiuliza ni kwanini mizimu itumike  hapo kwenye kushinikiza deni lilipwe, lakini tutakuja kuliona hili kwa jinsi tunavyokwenda na majadiliano yetu…’nikasema

Dalali alitaka kusema jambo, lakini akaghairi, akijifanya kuangalia saa.
‘Tuje kwenye maswali yetu…sasa hivi nataka kuhakiki, uhalali wa hilo deni,…na hap ni sehemu ya kuwa makini sana, nitapenda kusikia kila kitu…mnisamehe kuwa hapa ninaweza kuchukua muda,…unasikia  ndugu Dalali..naomba utoe ushirikiano, kama alivyokuomba shemeji yako…’nikasema

‘Tokea awali nimekuwa nikitoa ushirikiano, kama ningelikuwa mtu wa hasira , ningeshaachana na haya maswali yako, maana mnavyouliza ni kama vile mimi nina makosa, wakati hata mimi ningelifurahia kama ingelipatikana njia ya kweli ya kulitatua hili jambo, na deni likalipwa kama ni la bro..’akasema.
‘Labda kabla sijaanza …hapo umeniweka njia panda, nikuuliza ili niwe na uhakika moyoni, je hadi hapo ulipofikia wewe, unaamini kuwa hilo deni ni la kaka yako…?’ nikamuuliza.

‘Kutokana na ushahidi, ndio….’akajibu hivyo

‘Sawa….sasa tunaanza,  je wewe ulijua lini,  kuwa kaka yako anadaiwa huko benki?’ nikamuuliza

‘Nilijua lini kwa tarehe hilo siwezi kukumbuka,… ila kiufahamu hasa, … nilijua pale nilipokwenda kuchukua pesa benki, naweza kujibu hivyo…’akasemaakijionyesha ni muungwana.

‘Ilikuwaje..nataka ufafanuzi kidogo hapo…’nikasema

‘Ok,… mimi ndiye niliyachaguliwa na wanafamilia wote kuwa niwe msimamizi wa hii familia ya kaka,…kwa taratibu rasmi, za kikao, najua hilo linaeleweka, ila nataka afande aliweke kwenye kumbukumbu zake au sio?’ akauliza na mimi nikabakia kimia yeye akaendelea kusema.

‘Hapo sasa nikakabidhiwa majukumu yote, kwa vile shemeji alikuwa hajiwezi, anaumwa, na kwenye kikao, yeye pia alitakiwa awe msaidizi wangu..lakini kipindi hicho alikuwa hajiwezi…’akatulia

‘Kikao kiliweka wazi hilo, kuwa kwa vile hajiwezi basi mimi nitachukua majukumu yote,..kusimamia familia, kuhudumia, na matumizi ya kila siku,…hayo yote  yalikuwa mikononi mwangu.

Kwa muda huo…. nikawa natumia pesa zangu, maana hii ni familia yangu, au sio , na hapo nilijifunza jambo, watu wanaongea tu, awali, kuona wanajali, lakini ikifikie kwenye vitendo, wewe uliyepewa jukumu hilo, unalo…wenzako haoo, unaumia peke yako..’akatulia.


‘Matumizi…hapa ndio umiza kichwa, maana  matumizi yanahitajia pesa, kwahiyo ilinibidi mimi nifanye juhudi za ziada, kubangaiza huku na kule, sio kazi rahisi kama unavyohisi…’akatulia

‘Na awali kwa vile, tuliuza maeneo, na kwenye kikao cha wanafamilia tulikubaliana hilo, sio kwamba nilijiamulia mimi mwenyewe, hapana, kikao kilipitisha kuwa pesa za eneo la bro, zitumike kwenye matibabu ya shemeji na dharura nyinginezo…nina kumbukumbu za matumizi hayo, kama mutahitajia…’akasema

‘Lakini matumizi yalikuwa makubwa,..gharama za dawa, ada za watoto, kula nk..ikafikia mahali nikazidiwa,…mzee mzima, nikawa naongea peke yangu njiani, ukiwaendelea ndugu kila mmoja ana lake,…san asana watasema, ‘mungu ataleta heri zake…’akachuka kidogo hapo.

‘Ndio hapo nikakumbuka, Bro ana akaunti benki,..kwanini nisiende huko,..aah, sikuchelewa, ikabidi niende benki, nikiwa na maana ya kwenda kuchukua pesa , …’akatulia akiniangalia, alijua hapo nitauliza swali, lakini sikutaka kumuuliza swali kwanza,nilitaka nisikie maelezo yake.

‘Kiukweli…ninafahamu hivyo kuwa kuna akiba ya Bro…, lakini mimi sikujua ni kiasi gani kipo huko,…hata wakati bro yupo, hakuwahi kunielezea kuwa ana salio gani, hata anaponituma kuchukua pesa,…hayo alikuwa akiyafahamu yeye mwenyewe, ….’akatulia.

‘Benki hawakuwahi kukuulizia au kukuambia kuwa kuna salio kiasi gani, je haikutokea pesa ulizotaka kutoa kuwa nyingi na kitu kama hicho…najua utataka kuniuliza hivyo…haikuwahi kutokea, huo ndio ukweli….’akasema

‘Nilikuja kuona ajabu kuwa hata shemeji alikuwa hafahamu hilo..maana…nilikuja kumuuliza baadae kipindi tunafutilia mahakamani, akasema hata yeye, alikuwa hajui kiasi gani kilikuwa benki….’akatulia akimgeukia shemeji yake.

‘Nataka hilo lieleweke….ili muone ukweli wa mimi kuamini kuwa deni lipo na huenda, na hii huenda, imekuja kuondoka baada ua kupata ujumbe wa mizimu…jamani hilo deni lipo na ni deni la Bro..’ akasema
************
‘Ok,…endelea..’nikasema na niliposema hivyo, akamgeukia mpelelezi huku akionyesha ule uso wa kuomba …kama muomba kura kwenye uchaguzi.

‘Sasa…eeh…tulipoishiwa kabisa, ndio nikajiwa na hilo wazo, kuwa niende benki…..’akaangalia saa yake.

‘Siku hiyo alifajiri, nilidamkia benki…nafika nikajaza fomu zao, nikiimbatisha na nakala ya barua kuwa mimi sasa ndiye msimamizi, unajua tena, sikutaka rudi rudi…’akatulia

‘Na mara nikaitwa jina, nikasoga kauta, nikambiwa nisubiri…baadaye ndio nikaambiwa kuwa siwezi kuchukua pesa kwasababu kuna deni kubwa….’akatulia.

‘Alikuambia nani…?’ nikamuuliza na yeye akacheka kwa dharau kama vile nimemuuliza swali lisilo na maana

Kaniambia nani…! Si huyo mtu wa benki, …ok,..labda unauliza jina lake nani,…sio ndio hivyo, kiukweli sikuweza kumuuliza jina lake,….na ukumbuke kuwa ni siku nyingi, huenda hata sura nimeshaisahau, sijui labda nikimuona nitamkumbuka…’akajibu  akibenua mdomo wa dharau

Ulipoambiwa hivvyo ulichukua hatua gani?’ nikamuuliza

‘Kama umeshapewa jukumu la kulea familia,…tena familia mbili,.. utafanya nini hapo…huna kitu nyumbani, na unahitaji pesa,… na nimeshafika sehemu ambayo tulijua ndio msaada wetu,..mfukoni sina kitu …haah,… hapana sikukubali ..’akatulia

‘Hata ingelikuwa ni wewe, ungelifanya jambo, au sio…?’ akaniuliza na mimi nikabakia kimia, alipoona simjibu akaendelea kutoa maelezo.

‘Mimi sasa kama mkuu wa familia ikabidi akili ya ziada ifanye kazi yake…ukumbuke na mimi nina familia yangu nayo inahitajia kula na kila kitu, na nilishawaahidi kuwaletea pesa…kulea familia mbili sio mchezo ndugu zanguni, na ukumbuke familia hii malezi yake yalikuwa ya juu…’akatulia

‘Sio kwamba nalalamika,..ila ndio hali halisi…lakini ningelifanya nini na mimi ni baba yao, ni mlezi wa familia zote mbili, na kaka hayupo, na kidini , kiutu na kiubinadamu nilitakiwa niwe na tahadhari, nisije kuonekana nanyanyasa,..ndio maana nilipofika benki, …ilibidi hahaha, nijizalilishe, nikafikia hata kumpigia magoti meneja…,’akatulia sasa akimuangalia shemeji yake.

‘Lakini mimi sikujali kwa vile hawa pia ni watoto wangu, watoto wa kaka yangu ni watoto wangu pia, au sio…kiujumla, ilibidi nianze kutafuta njia, ili watu hawa waweze kuishi, mgonjwa aweze kuendelea na matibabu…’akasema akimuonyeshea shemeji yake kwa mkono.

Nikaona anaendelea kuongea yasiyo muhimu, akijipigia debe,  ndio nikamuuliza;

‘Je ulipopata taarifa hizo uliwahi kumwambia shemeji yako…maana licha ya kuwa hajiwezi lakini najua kuna mambo ulikuwa unafika kumuambia au sio,…na alikuwa anasikia, ukumuuliza kitu anatikisa kichwa au sio… je kuhusu hilo deni uliwahi kumwambia shemeji yako?’ nikamuuliza

‘Hapana mimi sio mjinga kiasi hicho ndugu yangu,….sikumwambia shemeji….nilikwepa kabisa hilo, …maana lingemchanganya akili, mtu keshachanganyikiwa unamzidishia dozi, ulitaka nimuue shemeji yangu..hapana mimi sikumwambia kabisa…’akatulia

‘Hukuamwambia mpaka lini…?’ nikamuuliza

‘Ilifikia hatua niliona nisimuambie nipambane mwenyewe tu, lakini deni lenyewe kubwa, …lakini hata hivyo, maswala hayo hayana siri, wakaja kutuma barua ya kukumbushia hilo deni, na ndio shemeji akaja kufahamu, ….lakini mimi bado nilikuwa na mashaka, , ndio maana tukafik ahadi mahakamani ...’akatulia.

‘Hiyo barua ilifikaje kwa shemeji yako…?’ nikauliza

‘Barua hiyo, sasa walileta nakala nyumbani, tofauti na zile za awali ambazo zilikuwa zinapitia posta, ni baada ya kuona hazijibiwi..ni baada ya utambulisho wangu kwao, na kwa vile walifahamu nyumba hiyo ipo wapi, na nahisi ni kwa vile pia,walishafahamu kuwa mwenye deni hilo hayupo tena duniani…’akasema

‘Hebu nikumbushe kidogo, siku hiyo ulipofika benki ulifanyaje awali kabisa, kabla hujapewa taarifa hiyo ya deni na watu wenyewe wa benki..?’ nikamuuliza

‘Ni kama vile unachukua pesa,…nilifika pale nikajaza fomu za kuchukkulia pesa, ile fomu nikaambatisha na ile barua ya kuwa mimi ndiye msimamizi wa mirathi….ok, ..au wataka nieleze nini zaidi..?’ akauliza

‘Ina maana ilivyo wewe ulipewa barua na kikao cha wanafamilia, upeleke benki, au sio…kwenye hiyo barua ukatambulishwa wewe na picha yako,..na sahihi  yako au sio…,na benki wana taratibu zao, huwezi kuchukua pesa mpaka uwe umeidhinishwa kama.;muwekaji sahihi-signatory, unanielewa ninachotaka kukifahamu hapo, ni kwanini ukakimbilia kuchukua pesa kabla hujapeleka hivyo vielelezo,…?’ nikamuuliza.

‘Nilishapeleka hivyo vielelezo kabla ya siku hiyo, nilijua ni vyema hivyo vielelezo vifike mapema ili nikiwa na haja ya pesa, nisianze upya, unanielewa..mimi ni Dalali hayo yote nayafahamu sana…na…jamani mimi sio mjinga….’akasema kwa kusita

‘Labda swali la kujikumbusha, nyie mpo ndugu wengi, na kuna wakubwa zaidi yako au sio, ni kwanini walikuchagua wewe uwe ndiye msimamizi wa familia?’ nikamuuliza akatabasamu kidogo, lakini akilini alihisi kuna mtego, akawa makini kulijibu, akasema;

‘Nimeshakuambia  kwenye kikao hicho walikuwepo ndugu wa pande zote mbili, hakukuwa na swala la kampeni hapo, ni wao wanavyokuona,…upande wa shemeji …walimtegemea ndugu yao, lakini alikuwa eeh,..wenyewe wakaona hatafaa, wakatutupia mpira sisis,…sasa kwa upande wetu..’akatulia akikohoa kidogo.

‘Kwa upande wetu…, nahisi ni kwa vile mimi nilikuwa karibu sana na marehemu,labda ndio sababu kubwa ya msingi ya kunichagua mimi…na labda ni kwa vile mimi najulikana sana kutokana na shughuli zangu za hapa na pale,…ndio wakaniteua mimi…’akatulia

‘Hebu sasa turudi huko benki, wewe ukafika pale wakakuambia kuwa kuna deni wewe ulifanyaje hapo..nataka kujua kila kitu hapo…, kwa siku hiyo, ni muhimu sana kwangu?’ nikamuuliza

‘Ilikuwaje kwa vipi!! Ok, ok, nimekuelewa,… ni pale nilipotaka kuchukua pesa, … ndio nikaambiwa kuna deni kubwa, nikashituka kuna deni, wakasema ndio tena deni kubwa na kutokana na mkataba, hilo deni lilitakiwa kulipwa kila baada ya muda fulani,  lakini halikuwahi kulipwa,…’akatulia kidogo.

‘Ndugu yangu kiukweli mimi mwenyewe nilishangaa, kaka achukue mkopo mkubwa hivyo bila ya mimi kujua, na, sijui alichukua kwa minajili gani, mimi  sijui, na  hata shemeji hapa hajui, hata kwenye taarifa za madeni msibani hilo halikuwahi kutangazwa, unaona ilivyo… ‘akatulia kidogo akitaka nisema neno lakini mimi nikabakia kimia ndio akaendelea kusema;

‘Pale pale nikawaambia watu wa benki ,… mimi sijui kuhusu hilo deni,…nikaja juu kweli, …namfahamu kaka yangu vyema , asingelikopa bila kuniambia, mimi,…yawezekana kuna makosa, wajaribu kuchunguza hilo,…wakaniambia hayo yameshafanyika, hilo deni halina shaka...’akatulia
‘Nikaamua niende hadi kwa meneja wa tawi…wanionyeshe kila kitu…’akasema

‘Kila kitu kwa vipi…?’ nikamuuliza

‘Nilitakaa kuthibitisha hilo deni kama kweli ni la kwake…nikaambiwa nisubiri, baadaye nikaambiwa niingie nikaonane na mhasibu mkuu wa tawi, sio meneja kama nilivyotaka…..nikaingia na huko nikaonyeshwa vielelezo vyote,…’akatulia

‘Ujue mimi kutokana na kazi zangu nimezoea sana kukumbana na makaratasi,…na macho yangu huwa mapesi sana kunasa vitu muhimu …niliyapitia yale makaratasi kwa macho kwa haraka nikaona  kila kitu kipo sahihi….kwahiyo hata alipoanza kunionyesha kwa hatua, nilisharizika, japo kwa mashaka, iweje bro afanye hivyo,..lakini hata hivyo, nilikubali tu kwa shingo upande…’akatulia

‘Baadaye nikaomba huo mkataba….maana pale mtu wa benk alikuwa akinionyesha nyaraka nyingine, mimi kitu muhimu, kwa wakati huo ikawa ni mkataba, nikauomba  huo mkataba,…’ akatulia

‘Hapo nili chukua muda kuusoma,…kutokana na mkataba ulivyo, kuna mkopo mkubwa lakini pia mteja alipewa nafasi ya kuchukua zaidi ya salio lake, na hiyo zaidi inaongezewa kwenye huo mkopo, unaona ilivyokuwa, mkopo bado anaweza kukopa zaidi, walimuamini…’akatulia

‘Haya dhamana ya mkopo ni nini,..?’ akajiuliza mwenyewe na kujibu hivi;

‘Dhamana ya mkopo ni ya nyumba, na kulithibitisha hilo, kuna nakala ya hati ya nyumba, na picha ya nyumba…utasema nini hapo mpendwa,ndio maana mimi nasema haya yote kunishuku mimi, eeeh, blabla eeeh..haitasaidiia  kitu,..mnapoteza muda, nendeni huko benki, kila kitu kipo wazi, mimi nisngeling’ang’ania tu……’akasema, sasa akimuangalia mpelelezi.
Kukawa na ukimia kidogo, halafu Dalali, akaendelea;
 ‘Naendelea, kama ifuatavyo.. huyo mhasibu akasema mimi kama msimamizi wa familia niliyekabidhiwa hayo mamlaka, natakiwa kulisimamia hilo deni lilipwe kwa wakati, na wamenisaidia tu, kutokana na hali ya msiba, la sivyo kama wangelifuata utaratibu, wangelipiga mnada hiyo nyumba iliyowekwa dhamana,…’akatulia

‘Hata hivyo…tujitahidi..kwani ni muda mrefu hakuna malipo yaliyofanyika…akaniambia hivyo huyo muhasibu, kiukweli, akili yangu siku ile haikuwa sawa,….nilichanganyikiwa, niliongea ovyo..hata hivyo ingesaidia nini..hebu…’akatulia.

Mimi nikamsimamisha kidogo, na kuuliza….
‘Hebu hapo….kwahiyo walikuambia hayo, siku ile ulipowenda kuchukua pesa au ?’

‘Kiukweli hayo maelezo walinipatia siku ile nilipokwenda kuchukua pesa, huku nyuma, hawakuniambia,maana sikuchukua pesa, niliwapelekea hizo barua na vielelezo tu kuwa mimi ndiye msimamizi ..basi wakapokea, na mimi nikaondoka,hayo yakuuliza na kufuatilia ni siku ile nilipokwenda kuchukua pesa….’akatulia kama anawaza jambo.

‘Kwahiyo hilo deni, ulivyofuatilia, huko nyuma kaka yako akiwa hai,  lilikuwa linalipwa…kwa jinsi ulivyoona ..?’ akaulizwa.

‘Ndio lilikuwa linalipwa…alijitahidi kulipa, inaonyesha mtoririko wake kwenye benki statement…’akasema.

‘Ikawaje sasa….?’ Nikamuuliza, hapo akatabasamu ile ya dharau, na kuangalia saa, kuashiria napoteza muda, lakini akaendelea kuongea;

‘Ndio hapo nikawaomba waniruhusu nichukue kiasi kwa ajili ya kusaidia familia,wakakataa, ..nikaomba na kuomba, nikaona hawa hawanifahamu, nikawaambia nataka nionane na meneja wao wa benki….’akatulia

‘Mnafahamiana  na huyo meneja wa benki, au…?’ nikamuuliza akasema

‘Sio swala la kufahamiana hapo, wewe huoni jamani…’akasema na kutulia

‘Ok,..ni kweli huyo meneja alikuwa akifahamiana na bro, sio mimi, hata nilipomuambia Bro kafariki, alisikitika sana..na nikamuhoji hoji kuhusiana na hilo deni, yeye alisema hana uhakika, kwani kipindi hicho, huo mkopo unachukuliwa, yeye hakuwepo, ila anamfahamu Bro,sasa sijui kikazi au kiurafiki hapo sikumuuliza zaidi..’akatulia

‘Ndio nikamuomba tupatiwe chochote,…kwa huruma zake sasa, ndio akatufikiria,..kiukweli hali yetu kiuchumi ilikuwa mbaya,..ndio hapo ikafikia hadi kumpigia magoti huyo jamaa…huwezi amini, ndugu yangu, shida, njaa, majukumu ya familia mbili, ningelifanya nini…’akasema

‘Sawa nimekuelewa, ikawaje?’ nikamuuliza, na niliposema hivyo, akatikisa kichwa kwa kuonyesha furaha fulani.

‘Nikaambiwa nitapewa pesa kiasi fulani,..lakini niandikishe sasa kuwa kinaongezea deni, ndio maana kukaonekana muongezeko wa deni, kipindi hiki Bro, hayupo duniani, nakumbuka umenilaumu kwa hilo, kwanini nikope wakati kuna deni…’akatulia.

‘Ngoja kwanza hapo…umesema uliambiwa hivyo siku ya kwanza, si ndio hapo kuwa huwezi kuchukua pesa kwa vile kuna deni..si ndio hivyo?’ nikamuuliza

‘Ndio…kwani kuna tatizo gani hapo…?’akasema na kuniangalia kwa mashaka.

‘Na tangia marehemu afariki, hukuwahi kuchukua pesa kabla..?’ nikamuuliza hapo akasita na akawa kama anawaza

‘Jibu swali….hilo halihitajiki kufikiria je tangia  kaka yako afariki hukuwahi kuchukua pesa kabla ya kuja kuambiwa kuna deni…?’ nikamuuliza

‘Kuchukua pesa, …hapana,….hapana,  sikuwahi kuchukua pesa…nilikuwa natumia pesa zangu, hilo nina uhakika nalo….…’akasema.

‘Na wakati kaka yako yupo hai, wewe si ulikuwa unatumwa kuchukua pesa, hukuwahi kuona , au kusikia kuwa kuna deni huko benki…?’ akaulizwa.

‘Sikuwahi kabisa…hata bro hakuwahi kuniambia hilo..hata shemeji hakuwahi kuambiwa, au hata kusikia…’akasema.

 ‘Shemeji yako alikuwa mgonjwa, asingeliweza kuchukua pesa,…kwahiyo baada ya kaka yako kufariki kama kuna pesa zimechukuliwa, zitakuwa zimechukuliwa na wewe, au sio…..na kwenye statement ya benki itakuja kuonekana hivyo, wewe unadai pesa ya kwanza kuchukua ilikuwa ya kuongezea mkopo, au sio…, kama ikionekana hivyo, kuna pesa imechukuliwa utasemaje hapo…?’ nikamuuliza

‘Kama kuchukua, atakuwa kachukua yeye mwenyewe sio mimi…’akasema

‘Kuja kuchukua kama mzimu au..nimeuliza baada ya kaka yako kufariki, si tarehe ya kufariki kwake inajulikana, au sio?’ nikamuuliza.

‘Sikiliza….wapi umeona kuwa pesa zilichukuliwa baada ya yeye kufariki, ..unayo banki statement…hakuna bwana…ni nani angelichukua, hakuna,..mmh, hakuna nina si-kumbuki?’ akasema.

‘Nimekuuliza hilo kama angalizo tu…na huo ni ushahid mwingine…’nikasema

‘Ndio maana nikahimiza kuwa ili tuwe na uhakika, na tuwe na ushahidi mnzuri ni bora twendeni benki..ili hata na mimi niwe na uhakika na majibu yangu, siwezi nikakumbuka kila kitu.., mimi nipo tayari twende pamoja, sina mashaka na hilo..’akasema kwa kujiamini.

 ‘Kwenye mtiririko wa kuchukua pesa, deni litaonekana kukua, hadi wewe unachukua pesa, hilo deni liliongezeka mara ngapi,…?’ sikumbuki
‘Mimi niliomba mara..mmh, mbili..ndio, ile ya kwanza, na pili nikaenda tena kupiga magoti…sikumbuki zaidi ya hapo..’akasema

‘Na wewe kwa mara ya mwisho kuagizwa na kaka yako kuchukua pesa ilikuwa ni lini,…akiwa hai?’ nikauliza

‘Siwezi kukumbuka pia, mpaka niangalie statement, ila ninachoona siku ya kabla ya kifo chake alichukua pesa nyingi sana, kuacha hilo deni…’akasema

‘Huyo mhasibu wa benki uliyekutana naye, sib ado yupo benki, tukienda kukutana naye tutamkuta,…?’ nikamuuliza

‘Yawezekana mimi sina uhakika na hilo, maana mimi sio mfanyakazi wa benki, na ni siku nyingi ukumbuke, wao wanabadilishwa, wanaacha, wanahama, sasa mimi siwezi kuwa na uhakika huo...’akasema

‘Nakumbuka ulisema kutokana na kazi zako wewe huwaga husahau hasa watu, sura za watu hasa wale mnaoingia nao kwenye mikataba huwezi kuzisahau au sio…., rejea nyuma kabisa, kipindi hicho Bro akiwa hai unamkumbuka mtu uliyezoea kuchukua pesa kwake, pale benki……?’ nikauliza

‘Siwezi kujibu hilo..sikumbuki…’akasema

‘Huyo muhasibu uliyekutana naye, kipindi hicho alikuwepo, labda kama uliwahi kufika kwake…?’ nikauliza

‘Mhh..kumbuka jambo moja hadi kwenda kwa muhasibu inatakiwa kuwe na tatizo, na sikumbuki kutokea tatizo kipindi hicho hadi kufika kwa muhasibu…’akasema

‘Una uhakika…?’ nikamuuliza

‘Kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza

‘Hukuwahi kufika kwa muhasibu wewe na kaka yako..?’ nikamuuliza hapo akawa kama anashtuka hivi, halafu akasema

‘Labda kipindi natambulishwa kuwa mimi nitakuwa nikichukua pesa…’akasema

‘Ina maana wewe ulitambulishwa kwake, je alikuwa huyo muhasibu..?’ akaulizwa

‘Sikumbuki…unajua ilikuwa ya haraka ilikuwa tu kujieleza na wala haikuwa na umuhimu …kitu kama hicho, sina uhakika kwakweli..’akasema

‘Swali je alikuwa ni huyo huyo muhasibu…uliyekwenda kuonana naye benki..?’ nikamuuliza…
Kabla hajajibu simu yake ikaita, alipoangalia mpigaji, akasimama, na kusema;

‘Nahitaji kuujibu hii simu nje ni mmoja wa wateja wangu..huyu ni mteja wangu muhimu sana, naomba tafadhali.. afande….’akasema na afande akasema

‘Unaweza kuijibu hiyo simu hapa hapa, kama huwezi mwambie utampigia baadaye,  au sogea pale , sisi hatuwezi kusikia mtakachoongea ,…kwani  tukisikia kuna ubaya, ni mambo halali au sio?’ Akauliza mpelelezi.

‘Ni haki yangu afande, mimi sio mhalafu, au..mimi ni muhalafu, siwaelewi..hata kusikiliza simu yangu ya faragha siruhusiwi…kwanini…’akawa analalamika

‘Sogea pale uisikilize…sijakukataza kusikiliza…mwenzako keshasema hiyo simu ni ushahidi wake, sitaki kuharibu ushahidi hapa..unanielewa…’akasema mpelelezi.

‘Ok, basi haina haja kuipokea…’akasema na kuizima hiyo simu.

‘Kwanini unazima hiyo simu kabisa…?’ akauliza mpelelezi

‘Itanisumbua sana,ataendelea kunipigia na nyie hamtaki nipokee simu. Si ndio hivyo…’akasema

‘Hakuna aliyekukataza kupokea simu…iwashe hiyo simu yako.’akasema mpelelezi.Dalali akawa anaiwasha akionyesha uso wa mashaka...hata hivyo, hakuwa na jinsi akaiwasha ile simu yake

Sasa alipoiwasha tu, ikaanza kuita….akawa hataki hata kuangalia mpigaji, akasema

'Mnaona...ni kero sasa...'akasema na mpelelezi akainuka na kuja pale alipo Dalali, akaichukua ile simu akaibonyeza kama kawaida yake na kusema;

'Sasa pokea...'akasema mpelelezi kwa sauti ndogo.

'Hapa hapa...huyu ni....'akalalamika kumbe mpelelezi alishaiweka hewani.

NB: Kibano kingine...simu inafichua mambo..ogopa simu...Na kwa namna nyingine,maswali yanaendelea...tuzidi kuwa wavumilivu, kwani ukweli uligundulika humo humo kwenye maswali…ndivyo ilivyokuwa!


WAZO LA LEO : Moja ya dalili za mnafiki ni uwongo, akiongea hupenda kudanganya, uwongo kwake ni jambo la kawaida, na hujiona mjanja kudanganya, na hajali kupata kipato kwa njia hii ya urongo, kwake uwongo ni fani.…lakini tabia hii haishii hapa, mtu huyu hata uaminifu wake utakuwa na walakini, na huwezi kumwamini kwasabbau haaminiki,, hawezi kutunza siri…maana hulka ya uwongo imeshajijenga.  Tumuombe mungu atunusuru na tabia ya uwongo, na kama tunayo tuiache, kwani tabia hii inakuwa mama wa dalili nyingine za mnafiki, na athari yake ni kubwa. Ijumaa njema
Ni mimi: emu-three

No comments :