Shemeji alibakia kimia, na Dalali, akasema;
‘Shemeji mimi nimekuwa nikiishi nawewe...unanifahamu
sana tabia yangu ilivyo, hata kaka aliniamini sana, mimi siwezi kuwa kinyume na
hii familia, siwezi kufanya kitu kimachoweza kuiumiza hii familia, na wasiwasi
wa huyu mtu tu..’akasema
‘Kwahiyo sasa unataka mimi niseme nini…maana
ulishanionya nisiongee baadhi ya mambo…naogopa nisije kuongea hapa yakaja
kutokea mengine..?’ akauliza na kusema mama mjane kwa sauti iliyojaa huzuni.
‘Nataka niwe na uhakika shemeji, nijue nipo peke
yangu au na familia yangu...'akasema na kuonyesha uso wa hasira hivi.
'Kwani...'akataka kuongea shemeji yake lakini akamkatiza kwa kusema
'Ninachotaka kufahamu ni...., je wewe, ulimtafuta huyu wakili, maana …mwanzoni
alijifanya yeye ni ndugu yako, kumbe mlikuwa mnanichezea shere, eeeh, shemeji, ndio tumefikia hapo…sasa naona sio ndugu tena , bali ni …niambie ukweli shemeji..’akasema
akimuangalia mama mjane.
Mama mjane akawa kainamisha kichwa chini tu, na alipoona shemeji yake yupo kimia anasubiria jibu, akainua uso kidogo na kusema;
‘Kwa hali ilipofikia, sikuwa na jinsi, yoyote mwenye
kutaka kunisaidia, nisingelikataa, …na wewe mwenyewe unaona hali ilivyo... wote waliofika
kabla hakuna aliyetusaidia kwa jinsi hii,..huyu angalau naona kuna matumaini,
…lakini..’kabla hajamaliza Dalali akasema.
‘Kuna matumaini gani shemeji, huko kuongea tu, kama kuongea, hata mahakamani tuliongea sana, lakini mwisho wa siku tuliulizwa nini..ushahidi....hatukuwa nao...shemeji tunapoteza muda bure...'akasema Dalali.
'Mimi naona tumpe nafasi tu, atusaidie, yeye anaweza kuwa msaada mkubwa kwetu....'akasema mama mjane.
'Kwahiyo mimi sikukusaidia kitu..hayo niliyoyafanya hayana maana..., na kwa
hatua hii ina maana gani,...shemeji kwa tafsiri ya haraka ni kuwa huniamini tena..au sio shemeji?’ akauliza.
‘Sio swala la kutokukuamini hapa shemeji,..hivi wewe
huoni kuwa kwa hali ilipofikia tunahitajia msaada, na sijui kwanini
unaukataa msaada shemeji…?’ akauliza
'Msaada !! Shemeji unaamini hilo, kuwa huyu mtu anafanya hili jambo kama msaada tu, hatahitajia malipo..?' akauliza akinigeukia mimi.
'Hajasema anahitajia malipo...'akasema mama mjane.
‘Hakukuwa na haja ya msaada shemeji,... mimi mwenyewe
nilishafikia hatua ya kulimaliza hili jambo kwa manufaa yetu sote na marehemu,
ina maana wewe humjali tena marejemu…’akasema Dalali.
'Simjali kwa vipi...?' akauliza mama mjane.
'Wewe huoni hilo...na kwa jinsi hiyo hili tatizo halitaisha kamwe...mimi nilishafikia nafasi nzuri tu ya kulimaliza kabisa, deni lilipwe, tuwe huru, na bro huko alipo awe huru...'akasema
‘Kulimaliza kwa kuachia nyumba ipigwe mnada, nyumba
ambayo kaka yako aliapa hataiuza, na alitamani idumu hadi vitukuu, kulimaliza
kwa kukubali kuwa kaka yako alikopa,..hivi kweli hapo ulipo unaamini hilo, kuwa
hilo deni ni la kaka yako,?…hapana sio mimi, niliogopa tu....?’ akauliza Mjane.
‘Ina maana ulivyokubali kule mahakamani ilikuwa ni
geresha…na hata ushahidi wote ule waliouleta benki hujauamini, si uliambiwa uukague, ukathibitisha kuwa ni ...…shemeji…?’ akauliza na hakumalizia hapo.
‘Lakini mimi nilikuambia…kuwa mimi sitakubaliana na
lolote lile, maana mimi ninamfahamu sana mume wangu..na hadi kuja kukubaliana
na hayo ni baada ya kuona familia yangu inateseka, ningelifanya nini sasa…’akasema mama mjane.
'Lakini ukweli si ulionekana, na mizimu ikathibitisha, kuteseka kwa familia tuliambiwa ni kwasababu gani...si hata ndugu yako alikuambia, alivyoambiwa huko, ..shemeji, mimi nilijua tumeshaafikiana...'akasema
'Sasa...kwanini tusimuachie huyu mtu akajaribu....tumuache tu shemeji..kuna ubaya gani...'akasema mama Dalali
‘Haya sawa, lakini nikuulize tu shemeji yangu,..hilo deni si lipo..?' akauliza
'Ndio lipo..lakini siamini kuwa ni la mume wangu...'akasema mama mjane.
'Kimaandishi na kwa ushahid i inaonyesha hivyo,...swali la kujiuliza hapo ambalo ndilo la muhimu, hilo deni litalipwaje..hilo ndilo la
muhimu,..sasa nikuuliza shemeji yangu, maana tunatwanga maji kwenye kinu,...niambie wewe, tutalipaje hilo deni..?' akauliza
Hapo mama mjane akabakia kimia
'Shemeji, nijuavyo mimi, kesi ikifika mahakamani,…tutashindwa
tu,..Sasa Shemeji yangu pesa ya kulipia hilo deni na gharama ya hiyo kesi itapatikana
wapi, umelifikiria hilo…?’ akauliza, na shemeji akabakia kimia
'Mbona hapo unabakia kimia...mambo mengine msikurupuke tu,...hilo ni swala langu, na nilishajua nifanye nini...tatizo, shemeji...umesahau kuwa mimi ni nani kwako, hata wanafamilia wameniamini, wewe unafiki hadi kunidharau, sawa wewe ni mkubwa kwangu kwa vile umeolewa na kaka,lakini...ilibidi uniombe ushauri kwanza...sio vizuri shemeji..'akasema
'Sasa niambie...maana hapo ulipo huna mbele wala nyumba, kula , maisha yenu yote yananitegemea mimi,...au nasema uwongo,..haya tumeenda huko mahakamani kesi tumeshindwa tena, unahisi ni nani atabeba huo mzigo...mbona unataka kuniua, maana nimechoka shemeji...'akasema
‘Yote mimi namuachia mungu, …maana yote ni kwa mapenzi
yake…’aliposema hivyo mama mjane akaanza kulia.
‘Shemeji, nimekuuliza tu, ndio inakuliza, …'akasema
'Maneno yako yanaitesa, yananisimanga...'akasem
'Hapana huo ndio ukweli,..inavyoonekana wewe
humjali tena marehemu , kwa vile keshafariki,hushukuru kuwa katuma mjumbe kutufunulia huo ukweli...sasa wewe bado huamini..au kwa vile hayupo tena duniani tumuache tu ateseka, asiyekuwepo na lake halipo au sio...'akasema.
Mama mjane akabakia kimia
'Shemeji nioneeni na mimi huruma...,
maana sasa nashindwa,..., tuache hata hawa watoto wateseke tu, na hatujui hatima yake
itakuwaje hao mizimu wakicharuka tena, itakuwaje, mimi sijui….’akasema.
‘Una uhakika gani kuwa hilo deni lilikuwa la mume
wangu,.....mimi ninachopigania ni hicho...akasema mama mjane.
‘Shemeji mbona tunarudia kule kule…uliuliza hayo….
hadi tukafika mahakamani, wakathibitisha kisheria, wewe si umesoma, eeh, unafahamu sheria, eeh…sasa wewe ulitaka mimi
nifanye nini, eeh..vielelezo vyote vipo..'akasema
'Lakini bado kuna mashaka kwangu...'akasema mama mjane.
'Haya sawa una mshaka na huo ushahidi au sio...na usione hivyo, kuwa kwanini mimi nakubali tu yaishe,… mimi nakubali kweli, kuwa kaka
hakuwa na tabia hiyo, lakini tutaithibitishaje hilo mbele ya mahakama, na
uzuri, eeh, mambo ya asili yametusaidia, tumeonyeshwa kwa kupitia mizimu, wewe
huiamini hiyo…?’ akauliza
‘Ina maana hadi hapo tumeshashindwa, au sio shemeji….sasa
kama tumeshindwa na katokea mtu wa kutaka kutusaidia, kwanini tusitoe ushirikiano kwake eeh,…mimi
sioni kama hapo kuna tatizo, au wewe ulikuwa na maamuzi gani..?’ akauliza mjane.
‘Maamuzi gani…! ungeliniuliza hilo kabla hujatafuta
mtu..unajua madhara yake, huyu atataka malipo yake, na tukishindwa kesi
tutahitajika kulipia gharama zake,za usumbufu,....bado hutajasahau, hayo yanayotokea kwa
mtoto,…una maana huumii mtoto akiteseka, na je itakuwaje huko baadae,..hawa
wakiondoka,..na tatizo jingine hata huyo
mtaalamu hapatikani tena…’akasema
‘Labda kaona haina maana tena, kuwatesa watu wasio
na hatia..’akasema mjane
‘Nini!!….shemeji, unasema nini,? una maana gani,?.... ina maana umeshamuamini huyo
mtu..huyo sijui ni wakili, shemeji, uwe na huruma na watoto..usipende mali
kupitiliza, hii tabia sio nzuri, hata bro alikuwa akikukanya sana kuhusu
hilo, na kwa vile umeona mimi sina mali unanidharau au.....’akasema
Mama mjane sasa akainua uso na kumuangalia Dalali
moja kwa moja usoni, na niliona keshabadilika,…
‘Shemeji,..mimi napenda mali,khaa! ..kweli unasema hivyo,
nimeishi na nyie nikajinyima ili mfanikiwe,…leo hii unasema hivyo, hivi kama
ningelipenda mali nyie mngefikia hapo mlipo…sijapenda hiyo kauli yako shemeji,
kabisa kabisa…’akasema mama mjane.
‘Nimesema hilo, kwasababu kwa hali ilivyo, hatujali
utu wa marehemu, hatujali haya yanayotokea kwa watoto, na ili haya yote yaishe
ni deni lilipwe, na deni hilo limethibitishwa kuwa ni la kaka…mimi sijaona
ushahidi mwingine wa kulitengua hilo, kama ushahidi mwingine upo nionyesheni
mie,ukiwepo kwanini ning’ang’ania hilo, itasaidia sana..ndio maana naona kama
wewe unachopigania ni mali zaidi…’akasema.
Hapo mimi nikaona niingilie kati, na kusema;
‘Dalali ulichotaka shemeji yako umeshakipata..haina haja ya
kumueleleza shemeji yako, yeye hapo alipo, anachopigania ni haki,..haki ya mume
wake. aliyemfahamu vyema tu, na haki ya familia yake, kuhakikisha kile alichokiacha mumewe kinabakia salama…’nikasema
‘Naomba tafadhali, msiingilie kati, …hili ni swala
langu na shemeji yangu, mimi ndiye mwenye mamlaka ya hii familia, nyie baada ya
hili mtaondoka, ni nani atawatunza hawa watu, nataka niwe na uhakika kuwa kweli
shemeji kakuchukua kwa dhamira ya kweli au ni hadaa zako…’akasema Dalali.
‘Mimi nitajitunza mwenyewe shemeji, kama unafikia
kuniona kuwa mimi nina tamaa ya mali, ..sitaki tena msaada wako, nashukuru sana
kwa huduma zako zote, nashukuru sana…’akasema mama mjane.
‘Shemeji…sasa hivi hutaki huduma zangu au sio…wakati
umelala huwezi hata kujiinua ..ni nani alikusaidia,..shemeji mimi sio kwamba
naongea haya kwa nia mbaya,…au kutaka fadhila baada ya hayo yote niliyojitolea,
.. kiutaratibu eeh..wewe ulitakiwa uongee na mimi kwanza, hapo mimi nina makosa
gani shemeji…?’ akauliza
‘Huna makosa, kwa vile..wewe huna tamaa ya mali,
mimi nina tamaa ya mali, lakini bado nasema siwezi kukubaliana na hilo deni,
moyoni mwangu nahisi hilo deni sio la kaka yako, je sitakiwi kuwa mkweli..najua
hukutaka niyasema hayo, kwa saabu ya mizimu, lakini nataka mizimu ijue kuwa
mimi sina kosa, …’akasema mama mjane.
‘Sawa shemeji mimi nimekuelewa,...ngoja tuone, si tupo,...na... na kama nimekosea
kwa kauli yangu hiyo naomba unisamahe tu shemeji yangu…nitakuwa mkosaji sana,
wewe kwangu ni kaka yangu ambaye hayupo duniani…nisamahe tu shemeji,
nimeshachanganyikiwa,..mimi naogopa sana yakitokea tena...’akasema.
‘Hamna shinda, nimekuelewe na mimi nimeshakusamehe…’akasema
shemeji yake.
‘Lakini kwa
hali inavyokwenda inabidi nimuite wakili wangu …maana sasa najiona nipo peke
yangu, nayasema haya kwa nia njema tu, ili kila jambo liende kisheria, najua huko
mbele tutakwama, sasa isije kuja kutupiwa mimi lawama, ningelipenda haya yote yaende
kisheria..’akasema.
‘Shemeji mbona mimi sijafikia huko..kwanini
tusimuache huyo mtu akatusaidia, huenda akafanikiwa, kwanini hilo likuumiza
kichwa, mpatie ushirikiano huyu msamaria mwema,…tuone kama tufanikiwa,
ikishindikana basi..’akasema mama mjane.
‘Tatizo sio hilo, tatizo, kwanza nikuzarauliwa, pili
ni kukiuka sheria, hukumu ilishapitishwa,sasa tunakiuka je ikienda na kuonekana
ni sahihi, nii nani atalipa hizo gharama wewe hulioni hilo, jingine ni hayo
mambo ya mizimu, wewe huyaogopi, lakini inaniumiza nikiona mtoto anateseka, je
wewe hata hilo hulioni ..?’ akauliza.
‘Huyu aliyejitolea analifahamu hilo…na sizani kama
atafanya hivyo kwa nia ya kutukomoa sisi, ..kaona kama kuna namna ya kushinda,
tumuache tu aifanye hii kazi, na sisi tumpa ushirikiano, na hayo mambo ya
mizimu nakuachia wewe, ufanye uwezavyo, ili tuone tumefikia wapi…’akasema mama
mjane
‘Kwahiyo kwa kauli hiyo, wewe umerizika naye, sio...sawa, na kama umekubali kuwa ulimtafuta wewe kwa lengo hilo, hata bila kunishirikisha, sawa pia...'akatulia kidogo.
'Haya… sawa
shemeji..ngoja tuone, mimi sina shaka kwa upande wangu....ila bado msimamo wangu wa wakili upo
pale pale,maana huyo wakili nilishamtafuta nilishaingia naye mkataba kuhusu hili tatizo, ngoja
awepo kutusaidia zaidi, wapambane wakili kwa wakili …’akasema akinitupia jicho mimi
‘Lakini huyu hapa sio wakili…’akasema mama mjane
akinionyeshea mimi, lakini ni kama hakuwa na uhakika na kauli yake hiyo.
‘Ni nani sasa..mbona unanitia mashaka…!?’akasema
kwa mshangao na kuuliza
‘Ni msamaria mwema tu..kaliona hili tatizo na ni
mwerevu wa kulitafutia majawabu…na yeye anawatumia mawakili…au…?’ mama mjane
akasema na kuniangalia mimi.
‘Naruhusiwa kuingilia kati..?’ nikauliza
‘Haijalishi,… ila bado mimi nitamuita wakili wangu
aje hapa…’akasema
‘Wa nini, unawasiwasi gani.?’ Aliyeuliza sasa ni
mpelelezi
********
Dalali akageuka kumuangalia mpelelezi, huku
akitabasamu kuonyesha hana wasiwasi na akasema;
‘Wasiwasi wangu ni kuwa kwa hali inavyokwenda, kuna
kuja kulaumiana hapa, na mimi sina uwezo wa kulipa gharama..na najiona kama
vile nashinikizwa kwenye matatizo,…’akatulia.
‘Matatizo gani…?’ akauliza mpelelezi.
‘Mhh…naona kama nashutumiwa , ..na hatua iliyofikia
hapa, kiukweli…inahitajika mtu anayefahamu sheria, sitaweza kujidanganya kuwa ninafahamu kila
kitu..’akasema Dalali.
‘Lakini….’nikataka kusema , nikakatizwa na mlio wa
simu, ilikuwa ni simu ya Dalali
Dalali, akamuangalia mpelelezi,..halafu akaangalia
simu yake ni nani mpigaji, ..
‘Naweza kupokea hii..?’ akamuuliza mpelelezi
‘Endelea tu..’akasema mpelelezi
Dalali,…akapokea, kwa sasa hivi sauti ya nje ya
spika ilikuwa haijawekwa, kwahiyo alichokuwa akiongea huyo mpigaji, tulikisia
kwa mbali tu..lakini sio rahisi kuelewa vyema, na Dalali alikuwa kageukia
upande mwingine kutupa sisi mgongo.
Akawa anasikiliza bila yeye kusema neno, na wakati
anasikiliza akageuka kutuangalia,.. niliona uso wake ukibadilika, halafu
akasema;
‘Una uhakika,…ndio nakuuliza una uhakika hayupo
kwake, kaenda wapi sasa, mimi sijui, tafuteni kaenda wapi, eeh, unasema,
hajui,..haiwezekani, nani,, ….?’ Akauliza na akawa anasikiliza halafu akasema;
‘Ndio….nimemtumia ujumbe wa maneno hajajibu,
nikampigia simu yake, hipatikani,…..kuna nini kwani..?’ akasikilza baadaye akakata simu,kwa hasira …usoni akawa
kakunja ndita, makunjazi,kuashiria kukasirika... akageuka kuniangalia mimi ,
akajaribu kukunjua hizo ndita, akasema;
‘Haya niambie kinachofuata maana sioni haja ya
kuulizwa maswali ya kunikandamiza mimi…ni lazima wakili wangu afike kwanza, au
unasemaje wewe muuliza maswali…na afande, nataka kufahamu jambo moja.., je mimi
ni muhalifu…?’ akauliza
‘Tukuulize wewe je wewe unajihisi vipi, kuwa
muhalifu, je kuna kosa umelifanya..?’ nikamuuliza
‘Mimi sina kosa…’akasema
‘Sasa kama huna kosa, wewe una wasiwasi gani, na
kwanini kama huna kosa ,kwanini ukimbilie kuita wakili….huoni huo ni ushahidi
kwangu ..’nikasema
‘Hahaha..ushahidi ushahidi, sasa hivi kila kitu ni
ushahidi na wewe huo ushahidi ni wa nini, kama kweli huna nia mbaya na mimi…?’
akauliza
‘Siliza Dalali, tusipoteze muda mwingi,…mimi nataka
tuende sawa, sio kwa ugomvi, na nia hapa ni kuelimishana , ili tuupate ukweli
halisi, mimi nina mbinu zangu za kuupata ukweli, hasa kwa njia hii ya maswali..’nikasema
‘Unafanya makosa sana…’akasema
‘Usiwe na shaka Dalali,…tulishaanza kuulizana awali,
au sio, na hadi hapo umeshanielewa nia yangu ni nini…kwahiyo tuendelee tu, na
mwisho wake tutaupata muafaka,..’nikasema halafu nikamgeukia Mpelelezi,
‘Au sio afande…?’ nikamuuliza mpelelezi.
‘Nyie endeleeni tu, ila wakubwa huko
wananishinikiza, leo iwe ni mwisho, na wewe tukitoka hapa twende kituoni,….’akasema.
‘Hamna shida afande…’nikasema na Dalali akawa
anatabasamu ile ya dharau, akasema;
‘Ni kweli afande,..hata mimi simuamini huyu
mtu..kamghilibu shemeji hapa, na anaweza kutuingiza kwenye matatizo…’akasema,
na mimi sikujali hayo maelezo yake nikasema;
‘Sasa nataka tuanze kuliangalia hilo deni, baada ya
kuona kuwa, hayo mambo mengine ya kiimani,..mizimu sijui… hayana msingi kwenye
hilo deni….’nikasema
‘Hapana,..yana msingi , huwezu kutulazimishia
hivyo,..usitake kuniweka mimi matatani, hayo yana msingi wake, sema wewe
huelewi tu…’akasema
‘Nimeshaelewa,…ila nikuulize kwa hilo ni kwanini
mtaalama kakimbia na kujificha, kama kweli hana jambo na hili jambo, kama kweli
anayoyafanya ni sahihi, kwanini akimbie, kujificha huoni inatia shaka…?’
nikamuuliza
‘Hilo la kukimbia na kujificha, ni wewe unasema
hivyo, hakuna ushahidi kuwa kweli kakimbia, au kajificha, mimi sijaupata ushahidi huo, ni dhana zako tu…’akasema.
‘Kwahiyo wewe una uhakika kuwa huyo jamaa
hajakimbia, kuna sehemu yupo, sasa kwanini akaacha simu yake nyumbani…, kwanini
akawa akatumia namba nyingine..?’ nikauliza.
‘Kusahau simu ni jambo linatokea kwa kila mtu..., hata mimi niliwahi
kumpigia siku moja.., akawa hayupo, na mkewe akapokea, hilo sio sababu ya
kumdhania vibaya, …na huko alipo angelitumia namba gani sasa, hebu uwe mwerevu
kidogo..’akasema Dalali.
‘Hana simu, ila kaweza kukumbuka namba yako,…na wewe
ulidai kuwa yeye sio rafiki yako wa karibu..?’ nikamuuliza
‘Mimi nitajuaje, labda aliandika hizo namba
mahali,..na kiukweli…ukiwa nashida unaweza kupiga namba yoyote..mbona kitu kipo
wazi, ..ndugu yangu, mimi nina mashaka na shule yako…’akasema
‘Hiyo namba aliyopigia ina jina la
mwanamke…’nikasema
‘Umejuaje…?’ akauliza
‘Shule yangu niliyopitia imefundisha hilo…na kama
tumefahamu kuwa hiyo namba ni ya mwanamke..na pia tumefahamu ni wapi
alipo….’nikasema
‘Hahaha..sawa fanyeni muwezavyo, hata mimi
itanisaidia ili kufahamu kama hayupo kwenye matatizo, na ni muhimu kwangu
pia…’akasema
‘Kwa vile ni rafiki yako au sio..?’ nikasema
‘Hilo sio muhimu, hata wewe nimekutana nawe hapa,
nikisikia huonekani, kwa vile nimeshazoeana nitajitahis kusaidia kukutafuta,
hukusikia mkewe alivyo sema
‘Mkewe alisema nini…?’ nikamuuliza
‘Uwe na werevu bwana…hata hilo nikuambie, ina maana wewe
hukusikia, mkewe akisema ana wasiwasi, hajui wapi alipo mumewe..’akasema
‘Lakini wewe si umeshawasiliana naye, kwanini
hukumuondoa wasiwasi huo mkewe, ili ajue kuwa mumewe hayupo kwenye matatizo,…si
umeongea naye au?..akakuambiaje..?’ nikauliza
‘Hajasema wapi alipo, …na unajua tena wanawake,
ningelimuelezea hivyo, ningelizi kumtia wasiwasi..kwanza hiyo namba aliyopiga
haiaminiki…hata nikimpatia mkewe, anaweza akapiga asimpate…atakuwa kaomba kwa
jirani, sio vizuri kumpatia hiyo namba kwa hivi sasa…’akasema
‘Lakini hiyo namba ni ya mwanamke au sio…nahisi
unamfahamu , unaogopa utawagombanisha, au sio,…sema ukweli bwana…’nikasema
‘Hahaha, hayo unayasema wewe…na aliyeongea sio
mwanamke, ni sauti ya kiume…’akasema
‘Una uhakika ni sauti ya mtaalamu mwenyewe..?’
nikamuuliza.
‘Kwanini nisiwe na uhakika nayo au….’akasema na kusita,
‘Basi huo
ndio werevu, ...mimi nilikutega tu, na wewe umetegeka,…kumbe unafahamu kabisa huyo aliyekupigia
kwa namba nyingine ndiye mtaalamu, kwanini ulitaka kutuficha sisi…?’ nikauliza
‘Nimeshawaambia…hayo ya mtaalamu huko alipo mimi
sijui, ..hayanihusu mimi…yeye ana shughuli nyingi, na anaweza kafanya hivyo
kwasababu zake, siwezi kujua…’akasema
‘Swali hapo tunahitajia jibu, je huyo aliyekupigia
baadae ni mtaalamu au sio mtaalamu..?’ nikauliza
‘Sio mtaalamu…’akasema, nikageuka kumuangalia
mpelelezi, na mpelelezi akatabasamu kidogo.
'Kama huyo sio mtaalamu, ni nani basi....unataka tulithibitishe hilo kuwa aliyeongea ni mtaalamu...?'
NB: Ngoja niishie hapa maana nipo kwenye mitihani ya
maisha.
WAZO
LA LEO: Kauli inaweza kuleta sintofahamu , kwa jinsi
ulivyoitoa, hata kama ulikuwa na nia njema tu. Ni busara sana pale tunapoongea
tukajaribu kuangalia mazingira, hali halisi ..isije ikawa kauli yakuumiza
sehemu ya kubembeleza, isije ikawa kauli yakuongea majonzi kwenye kutoa pole. Isije
ikawa kauli ya dharau,..kwenye kuelimisha jambo. Ulimi uchingwe sana kwenye
kuongea. Ndio wazo la leo
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment