‘Sii hii hapa..inaita, ulisema haipatikani, eti mtaalamu
kajificha, hahaha, kwanini ajifiche, eeh… tatizo lako wewe, humfahamu vyema huyo mtu, mtaalamu sio mtu wa
kuogopa ogopa mambo, hahaha …uwongo mwingine bwana. hauna maana kabisa ndugu yangu…’akasema sasa
akiwa anacheka, na mpelelezi
akamsogelea;
‘Nataka nihakikishe, hebu nipe hiyo simu…’mpelelezi
akasema na Dalali kwa haraka akampa simu huyo mpelelezi, na mpelelezi
akaichukua hiyo simu, akajifanya anaikagua ile namba, na niliona akibonyeza
kiwambo cha spika ya nje.., wakati huo Dalali, yupo kwenye kucheka.
‘Hahaha…umeiona afande eeh, hiyo hapo inaita eeh…,
hiyo sasa ndio namba yake halali, sio ile uliyokuwa ukiishuku,..sasa kama
inaita, hiyo namba nyingine ni ya nani, hebu niambieni…’akasema Dalali.
‘Labda ana simu mbili je…’akasema …mpelelezi, halafu
kwa haraka akasema;
‘Hebu tusikie akipokea kama ndio yeye…’akasema mpelelezi,
simu ilikuwa inaendelea kuita tu, haipokelewi..
‘Sawa hamna shaka,
ngoja… atapokea sasa hivi, mara nyingi anakuwa na wateja wengi…kwahiyo
anaweza asipokee hapo hapo…ila nakuthibitishia afande hii ndio namba yake
aliyonipatia mimi…’ na mara sauti ikasikika..
Tuendelee na kisa chetu.
*********
‘Halloh, nani mwenzangu…’sauti hiyo ilitufanye sote
tuangaliane, na Dalali hakujua kuwa mpelelezi kaweka sauti ya spika ya
nje…kwahiyo sauti hiyo tuliisikia sote…na Dalali alivyoona hivyo…, akageuka
kutuangalia,…
‘Sauti ya kike, huyo mtaalamu ni mwanamke kumbe.…’akasema
mpelelezi.
‘Labda yupo nyumba ndogo…’nikasema kiutani, na
Dalali akanitupia jicho, huku akijigonga gonga, kuipokea hiyo simu.
‘Ni..ni-na...eeh, …nataka kuongea na Mtalaamu…’akasema
‘Wewe ni nani…?’ sauti ikauliza na mtaalamu akabenua
mdomo kidogo, nikajua ni kwanini anafanya hivyo.
‘Ninaweza kumpata mtaalamu, nina shida naye,
….’akasema
‘Ni wewe shemeji,….nimeigundua sauti yako,.. hebu
niambie,mwenzako yupo wapi..’sauti ya kike ikauliza
‘Kwa-kwani, hayupo hapo nyumbani..?’ akauliza
Dalali.
‘Angekuwepo nisingelikuuliza hivyo…watu wengi
wanamtafuta, kwani kuna nini kimetokea, mbona mnaniweka roho juu,..mimi,…nilijua
wewe upo naye, mbona sauti inasikika hivyo..’akasema
‘Kwani kuna nini, hakuna kitu shemeji
…nita-nitakupigia baadae?’ akauliza Dalali, na alipoona sote tunasikiliza
akasema hivyo na kukata simu.
Akawa
kainamisha kichwa chini, hakutaka kutuangalia machoni.
‘Kwanini umekata simu Dalali…., kwanini hujaongea na
shemeji yako..?’ nikauliza
‘Kuongea na yeye kuhusu nini, huyo ni mke wa mtu, na
sisi tunamtafuta Dalali, au sio…sikiliza…nahisi kuna tatizo limetokea..’akasema
Dalali.
‘Basi ungelimuuliza huyo shemeji yako…, si rafiki
yako, na mkewe anafahamu kuwa mpo naye,..awali ulisemaje..?’ nikamuuliza
‘Kwani mimi nilisema nini kibaya,…mimi najuana naye
kwenye kazi zangu za udalali,..na nikaja kujuana naye zaidi, pale mtoto
alipoanza hayo matatizo yake..’akasema Dalali.
‘Naomba hiyo namba yake…tafadhali..’nikasema
‘Namba ya nani..?’ akauliza Dalali akionyesha uso wa
kushangaa.
‘Namba ya mtaalamu..’nikasema
‘Yanini..?’ akauliza
‘Nataka niongee naye, huyo shemeji yako..’nikasema
‘Afande,..huyu anataka mimi nionakane mbaya, kuwa
nagawa namba za watu, halafu anataka kuongea na mke wa mtu, je mtaalamu akijua
nimefanya hivyo, mimi nitakuja kueleweka vipi ..’akasema Dalali.
Dalali, akawa akimuangalia mpelelezi, na mpelelezi
akabakia kimia tu. Na mimi nikasema;
‘Isiwe shida, hiyo namba yake ninayo, nilishapewa na
watu wangu..’nikasema na sasa nikawa naitafuta kwenye simu yangu, sio simu ile
niliyokuwa nimeiweka mezani..hii ni simu ndogo tu naitumia kwa dharura.
Nikasogea pale mezani nikachukua hiyo simu ya mezani
nikaifauta namba…na kuiweka kwenye hiyo sim ndogo,nikawa naipiga hiyo
namba..Dalali akawa ananiangalia kwa uso wa mashaka.
‘Halloh nani mwenzangu..?’ ilikuwa sauti ile ile ya
kike
‘Naomba kuongea na Mtalaamu..’nikasema
‘Wewe ni nani..?’ akauliza
‘Mimi ni mmoja wa wagonjwa wake, kuna maagizo
alinielekeza ..sasa kuna kitu nimekwama..tafadhali ni muhimu sana nataka
kuongea naye, nisije kuvunja miiko..’nikasema na kukawa na ukimia fulani,
baadae akasema;
‘Mtaalamu hayupo…’akasema
‘Oh,… kaenda wapi jamani nataka kuonana naye ni
muhimu sana kwangu..’nikasema
‘Nimesema hayupo na wala sijui wapi kaelekea…kwani
kuna kitu labda naweza kusaidia..?’ akauliza
‘Kwani na wewe unafahamu maswala ya matatizo ya mizimu..kama utaweza kunisaidia nitashukuru
sana..?’ nikamuuliza
‘Oh…hayo sijui kwakweli…kama ingelikuwa ni dawa hapo
ningeliweza kujua jua kidogo…’akasema
‘Yamenitokea tena, na sijui nifanye nini… mimi haya
mambo nilikuwa siyataki, lakini mke wangu akang’angania tu….sasa hata sijui
tufanyeje…’nikasema, huku nikimuangalia Dalali, alikuwa akitaka kufanya kitu
kwenye simu yake lakini anashindwa,..
‘Oh..kwakweli hayo mambo hata mimi siyajui, hayo ni
mambo ya maruhani, ..na ni mpaka mwenyewe awepo apandishe ndio akuelekeze,
siwezi kukusaidia kwa hilo, samahani…’akasema.
‘Oh, sasa huu ni mtihani,…samahani…nitakusumbua sana
kwa maswali…’nikasema
‘Wewe uliza tu kama naweza nitakujibu..’akasema
‘Haya…mambo niliambiwa ni mizimu ya marehemu,
anataka mambo fulani yafanyike, ..na mimi sikupenda kwakweli…kuna madhara
yoyote naweza kupata..?’ nikauliza.
‘Kama uliambiwa yafanyike, nakushauri kaka yangu,..sijui
ni kaka au ni baba, yafanye kama ulivyoelekezwa tu…, hayo mambo ya mizimu yana
miiko yake,…’akasema
‘Ndio kuna miiko niliambiwa…sikupenda haya mambo
kwakweli..’nikasema
‘Ina maana ni ya kutengeneza au ni ya kutumiwa au ni
ya…mambo ya jadi..?’ akauliza
‘Mhh..hapo ndio nakwazika, …sikutaka kufahamu
zaidi…’nikasema
‘Unajua kama ni ya jadi, ina maana wahenga
wanahitajia jambo fulani, na ..kwa hilo ni muhimu ufanya wanavyotaka,..ila kama
ni ya kutengeneza…ili upate jambo fulani..ni bora utekeleze hivyo vinginevyo
yatakugeukia wewe mwenyewe…’akasema
‘Hapo sasa ndio sielewi, maana aliniambia ni mizmu,
inamadai, marehemu ana kitu alikiacha, sio deni, lakini ni kitu aliahidi kwa
mtu..’akasema
‘Kama ni kitu au ni deni ni lazima ifanyike
ilivyosema mizimu,..kama ni deni ni lazima lilipwe, na kama ni maagizo kuwa
jambo fulani lifanyike ni lazima lifanyike la sivyo …kuna matatizo mwaweza
kuyapata…mabaya ni hayo ya kutumiwa,..sasa sijui wewe ni lipo kati ya hayo…?’
akauliza
‘Ni hilo la maagizo,…’nikasema
‘Unajua kuna watu wengine, wao wanapenda tu
wafanyiewe kutimiza haja zao..wengine ndio hivyo ni kweli wanatokewa na
matatizo,..kwahiyo kila mtu na tatizo lake, ndivyo nilijuavyo mimi…’ akasema.
‘Mhh…mimi hapo sasa nakuwa na wakti mgumu…sasa
kwanini mtu aje kutengenezewa mambo ya hatari hivyo, mimi sitaki kabisa mambo
hayo, ila kwa hili sikuwa na jinsi...’ nikasema.
‘Mimi nakushauri tu,…kama nilivyokuambia, sina ujuzi
nayo zaidi, nisije kukudanganya…’akasema
‘Hakuna mtu mwingine ambaye aliwahi kufanyiwa, ambaye
anayafahamu hayo mambo, ili niweze kumuulizia..?’ nikauliza
‘Mhh, ..mbona wapo wengi tu, mimi siwezi kukumbuka
kila mtu na mambo kama hayo ni siri za watu na kila mtu anakuja na mambo
yake,....siwezi kukusaidia kwa hilo..’akasema
‘Kuna jirani yangu mmoja naye alikuwa na matatizo
hayo kwa mtoto wake anasumbuliwa sana, ..sijui naye nitamkuta labda anaweza
kunisaidia…’nikasema
‘Ni nani huyo..?’ akauliza
‘Ni Dalali mmoja hivi….’nikasema, huku nikimuangalia
Dalali, kiukweli alionekana hana raha, na mpelelezi alikuwa akimtupia jicho
kuhakikisha hafanyi kitu.
‘Ok…kama ni huyo dalali ninayemfaamu mimi,..huyo ni
rafiki yake mume wangu mkubwa, ukimpata huyo anaweza kufahamu wapi alipo huyo rafiki
yake, lakini sasa, kuna tatizo…’akatulia
‘Tatizo gani tena…?’ nikauliza
‘Huyo Dalali, kanipigia simu, kasema na yeye hajui wapi
alipo huyo rafiki yake, nay eye anamtafuta…, ila nikushauri kitu. mpigie au
umpitie huyo huyo Dalali, anaweza kukusaidia …kweli naliwahi kusikia kitu kama
hicho…’akasema
‘Kitu gani…jamani huenda kikaweza kunisaidia na
mimi…?’ nikauliza
‘Kuna matatizo yake ya kifamilia… ana mtoto wake
anasumbuliwa hivyo hivyo..ila sijui zaidi maana nilisikia juu kwa juu, mara
nyingi wawili hao wakikutana nakuwa sipo….’akasema.
‘Yeye alinunua au ni tatizo tu la …kama unaweza
kufahamu..?’ nikauliza
‘Hapo siwezi kukujibu..sijui kwakweli…’akasema
‘Unajua ni hivi kuna dawa huwa nilipewa ikitokea
basi naitumia,sasa nimevukisha muda, niliambiwa isizidi mara tatu, sasa
imeshazidi, hata sijui nifanyeje,, naogopa kuitumia tena..’nikasema
‘Mhh, hayo ndio masharti yake,..ila kiushauri ,
muone huyo huyo rafiki yake, ..anaweza kukusaidia…mengine wanasema tu, ukiona
vipi humpati, wewe itumie tena tu hiyo dawa…huenda ikasaidia,…lakini sijui
zaidi ya hapo mimi sijui..’akasema
‘Sawa ngoja nimpitie huyo rafiki yake, nashukuru
sana kwa msaada wako, na kama umesema ni rafiki yake huenda akawa anafahamu
fahamu kidogo…’nikasema
‘Huenda, …maana wanafahamiana sana,…wewe kamuulize
tu na huenda keshamtafuta kwenye simu, mimi nitaendelea kumtafuta mume wangu, maana
kuna watu wanamtafuta sana, nikimpata nitakupigia…’sauti ikasema
‘Ahsante sana…, nikimkosa huyo rafiki yake…,
nitakupigia tena huenda ukanisaidia, maana hapa naogopa kweli na …nahitajia
msaada wake kwa haraka..’nikasema
‘Pole sana…’sauti ikasema na mimi nikakata simu.
***************
‘Dalali, Dalali..wewe ulisema nini, kuwa huyo mtu
hamjuani sana, mkewe anasema wewe ni rafiki yake mkubwa…’akasema mpelelezi.
‘Urafiki wetu ni kwenye kazi hizo za
Udalali…’akasema
‘Na huyo MTAALAMU, ni shahidi wangu wa pili….’mimi nikasema
hivyo kwa sauti nikisisitizia neno ‘mtaalamu’.
‘Shahidi wa nini sasa…?’ akauliza Dalali,
akiniangalia kwa uso uliojaa mashaka.
‘Kuthibitisha madai yangu..kuwa hilo deni sio halali
ya marehemu, na wewe na Dalali mnaweza
kuahamu jambo..’nikasema,
‘Hahaha,..unajua usijifanye mbumbumbu…hilo deni
linatoka benki na benki wana taratibu zao, sasa mimi nitahusikanaje na hilo
deni eeh…’akasema akiniangalia, baadae akamgeukia mpelelezi na kusema
‘Afande hii kweli inaingia akilini, hebu nisaidie
hapo kidogo,..na naah…mimi kwenda kwa mtaalamu eeh….ni kutokana na tatizo la
mtoto,..unasikia sana,… vinginevyo, ..mimi ningeendelea kujuana na huyo mtu
kwenye kazi za udalali tu..’akasema
‘Kwahiyo kujua jinsi gani hizo dawa zinatumika,…na
ikitokea ufanye vipi, eeh… ni kutokana
na hilo tatizo, kabla ya hapo ulikuwa hufahamu chochote kuhusiana na
matatizo kama hayo..?’ nikamuuliza.
‘Sikuwahi…mhhh, usilinganishe tatizo la mke wangu na
hili, tatizo la mke wangu ilikuwa ni mashetani, alikumbwa na mashetani…lakini
hili la hapa, ni mzimu ya marehemu ..yenyewe ilikuja kuwakilisha huo ujumbe wa
hilo deni…’akasema
‘Swali ni kwanini awali ulikana kuwa wewe na huyo
mtaalamu hamkuwa na usuhuba..?’ akaulizwa na mpelelezi.
‘Afande hayo ni mambo ya uganga wa kienyeji, sio
mambo ya kujitangaza-tangaza ovyo….hakuna mtu anapenda kusema mimi najuana na
mganga wa kienyeji, kweli s kweli, japokuwa watu hao wanatusaidia sana,….na
kutokana na kazi zangu watu wanaweza kunifikiria vibaya..’akasema
‘Kwahiyo , kiuhalisia, huyo mtaalamu ni rafiki yako
wa siku nyingi..?’ akaulizwa
‘Sio kivile…ni katika namna tu, siwezi kuelezea
zaidi..’akasema
‘Dalali unanifahamu…mimi sipendi uwongo, kwa jinsi
unavyolielezea hilo inaonekana kabisa kuna kitu unaficha, …mimi ninaweza kuamua
kulichunguza hilo nikapata ukweli wake,…sasa nikiamua kufanya hivyo nikaja kugundua,
sizani kama nitakuelewa, ..’akasema mpelelezi.
‘Afande mimi nifiche nini..siwezi kukuficha kitu afande..huyo
mtu kujuana kwetu ni kutokana na kazi yangu ya udalali tu.. zaidi ni pale huyo
mtoto alipoanza kuumwa..’akasema Dalali.
Mpelelezi akanigeukia mimi, …na mimi sikupoteza
muda, nikamtupia swali Dalali,
‘Ni wapi unaweza kufahamu Dalali yupo..?’
nikamuuliza
‘Mimi sijui…’akasema
‘Afande unaweza kuniruhusu nikasoma mawasiliano yake
kwenye simu yake..?’ nikauliza na hapo Dalali, akashikilia simu yake imara,…na
afande akasema;
‘Hilo sio rahisi, labda Dalali awe kashukiwa na
jambo fulani, je wewe unamshuku Dalali, kwa kosa lolote..?’ akaniuliza afande.
‘Mimi nataka kufahamu wapo alipo huyo mtaalamu, huyo
mtaalamu ..ni shahidi yangu muhimu
sana..’nikasema
Mpelelezi akageuka kumuangalia Dalali, akasema;
‘Kuna namna moja ya kukuweka wewe salama; ama
utuambie wapi alipo huyo mtaalamu, au utupatie hiyo simu yako…tusome jinsi gani
mlivyokuwa mkiwasiliana naye..’akasema mpelelezi.
Dalali, akabadilika sura…halafu akasema
‘Kwanini mnataka kufanya hivyo, mimi nina kosa
gani..?’ akauliza
‘Ndugu yetu hapa kakushuku kuwa wewe unaweza ukawa
na namna fulani ya hilo deni,…shutuma hizo kakuelekeza kwako na kwa
mtaalamu…’akasema mpelelezi
‘Kama una shutuma kama hizo, basi yeye afuate
taratibu,…si taratibu zipo jamani,.. je mimi ni mhalafu, ni mhalifu wa kosa
gani, hayo yapo wazi au sio afande…?’ akauliza Dalali sasa kwa kujiamini.
‘Unashukiwa…’akasema mpelelezi
‘Je huu ndio utaratibu..afande,…maana mimi sina
wasiwasi kwa hilo..kama wewe utaona kuwa huo ndio utaratibu sawa, mimi
nitakupatia hii simu usome kila kitu, lakini kama sio utaratibu, mimi nitalifikisha
hili jambo huko kituoni kwenu..’akasema mpelelezi,
Mpelelezi akaniangalia mimi..
‘Afande..wewe upo kazini, unamekuja kumuhoji Dalali,
na katika kazi yako, unaruhusiwa kumchunguza mtu, kuhakiki maelezo yake, je
hapo umekosea..?’ nikauliza
‘Huwezi kunifundisha kazi, na ukiona sifanyi jambo
fulani, ujue kuna namna ambayo ..natakiwa kuifuatilia, sioni kama kuna umuhimu
wa mimi kuchukua simu yake huyu jamaa na kuanza kuisoma, labda unithibitishie
kuwa huyu mtu ni mhalifu..’akasema Mpelelezi.
‘Nimeshakuambia kuwa Dalali, ndiye anaweza
kutufikisha huko alipo huyo mtaalamu, na mtaalamu ni shahidi wangu ..’nikasema
‘Kwenye kosa gani..?’ akauliza Dalali.
‘Nafuatilia uhalali wa deni..’nikasema
‘Deni la nani..?’ akauliza
‘NI deni linalokisiwa eti ni la marehemu, kitu
ambachp nataka kukihakikishia kuwa sio sahihi kwake hilo deni sio la marehemu..’nikasema
‘Wewe kama nani..?’kauliza Dalali
‘Kama mtu niliyeteuliwa na mama mjane kulifuatilia hilo
na kulinda haki zake mama mjane na mayatima, ..’nikasema
‘Na mimi ni nani wa marehemu..kabla sijamuuliza
Shemeji kuthibitisha kauli yako..?’ akauliza Dalali.
‘Wewe ni ndugu yake marehemu..’nikasema
‘Mimi na wewe ni nani ana uchungu zaidi kwa
marehemu..?’ akauliza Dalali
‘Huo ni mmoja wa ushahidi wangu mahakamani..’nikasema
‘Kwa vipi sasa mbona hueleweki.?’ Akauliza
‘Kama nilivyoelezea awali…unataka nikufafanulie
tena..’nikasema
‘Wewe bwana usilete ubabaishaji hapa, mimi
nimeshaelewa lengo lako, ni kutafuta pesa tu, ..hupati kitu hapa..’akasema
‘Kutafuta pesa za nini…?’ nikauliza
‘Si za uwakili au…wewe hapa siumesema unafuatilia
uhalali wa hilo deni, sasa unafanyaje hilo…eeh, niambie,..au,..usiniambie kuwa
wewe unafanya kazi hii bure, ujue mimi ndiye mwenye mamlaka ya wewe
kulipwa..’akasema
‘Wapi nilisema nafanya hii kazi kama wakili, au wapi
niliandikishiana na wewe kuwa naifanye hii kazi kwa malipo kadhaa..?’ nikauliza
‘Ndio maana niliwahi kusema wewe ni tapeli..kwanini
uje kuingilia familia hii na kujifanya unatafuta ukweli, wakati mimi mwenyewe
sijakuruhusu..shemeji hawezi kufanya jambo bila ridhaa yangu, mimi ndiye
msimamizi wa hii familia.
‘Na huo ndio ushahidi wangu mahakamani…’nikasema
‘Afande unemuelewa huyu mtu…’akasema Dalali
akiniangalia mimi machoni, na afande akawa kimia,na mimi nikasema;
‘Tuambie ni wapi mtaalamu kajificha..’nikasema
‘Mimi sijui…’akasema
‘Basi tupatie simu yako, tusome ujumbe,..maana kuna
ujumbe umetumwa kwako, utakaousaidia sis kufahamu wapi huyo mtu
kajificha..’nikasema
‘Una uhakika na hiyo shutuma yako..?’akauliza Dalali
kwa kujiamini
‘Kama huna wasiwasi na hilo, kwanini unaogopa kutoa
hiyo simu yako..?’ nikauliza
‘Kwasababu hii simu ni yangu, kuna mambo yangu mengi
ya kikazi, na mimi sikuamini,..unaweza ukawa ni tapeli wa kutaka kufanya
jambo…’akasema
‘Kwahiyo wewe huamini kuwa mimi nafanya hili jambo
kwa masilahi ya familia, kwa nia ya kutafuta ukweli wa hilo deni..?’
nikamuuliza
‘Mimi sikuamini, ..maana sijakutafuta kwa kazi hiyo,
sijui labda shemeji aniambie..’akasema akiashiria kwa shemeji yake bila
kumuangalia usoni.
‘Utanitafutaje wakati unafahamu fika kuwa wewe
unahusika kwa namna fulani …’nikasema
‘Kuhusika kwa vipi, mimi sasa nataka uwe muwazi
kwangu, je unanishuku, je mimi nina kosa gani, uweke wazi, kwa uthibitisho,
vinginevyo mimi sasa nitalifikisha hili jambo mbele ya sheria..’akasema kwa
kujiamini kabisa
‘Nitathibitisha ukinipatia hiyo simu yako, tukasoma
ujumbe uliondikiwa na mtaalamu…na hiyo simu kuanzia sasa ni ushahidii wangu mahakamani, afande, mimi
ninakuarifu kuwa simu hiyo ina ushahidi wa ninachokishuku kwa huyu mtu..’nikasema
‘Kwahiyo wewe unanishuku, kuwa nina kosa..kosa gani…?’
akauliza Dalali
‘Ukinipatia hiyo simu nitalithibitisha hilo,..hiyo
simu ina ushahidi wangu muhimu wa kulithibitisha hilo..’nikasema, na mara …
Dalali sasa akamgeukia shemeji yake, na kusema
‘Je shemeji wewe umemchukua huyu mtu …?’ akauliza
‘Kumchukua…?’ shemeji akauliza kwa mshangao
‘Ndio nataka kufahamu je umemchukua huyu mtu kuwa
wakili wa kutafuta ukweli wa hilo deni,..niambie ukweli shemeji, maana mimi
nina haki ya kulifahamu hilo,..vinginevyo wewe uniambie kuwa mimi huniamini..’akasema
sasa akimuangalia shemeji yake usoni.
NB: Tuishie hapo kwa leo.
WAZO
LA LEO: Unapojikuta upo kati kati ya kutoa ushahidi wa
pande mbili, ushahid ambao, ukiutoa unaweza kuleta sintofahamu kutoka kwa pande
mbili, za marafiki wako wakubwa…marafiki ambao ni maadui wenyewe kwa
wenyewe..ina maana ukisema hivi utamkwanza mwingine na ukisema hivi utamkwanza
mwingine,..je utafanya nini…?
Wakati wote fahamu jambo moja, HAKI ina thamani
kubwa sana, na haki husimamiwa na UKWELI. Ongea yaliyo ukweli hata kama utavunja
urafiki wako kwa rafiki yako mkubwa , na haki hiyo itakuja kukulinda baadaye
kwa huyo huyo rafiki , pale ukweli utapokuwa bayana.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment