Dalali akawa anasita kuitoa hiyo simu, na mpelelezi sasa akawa
kamkabili kasimama mbele yake, wanaangaliana.
‘Afande hiyo sio haki…’akawa analalamika Dalali, huku taratibu akitoa
simu yake mfukoni…, na niliona vidole vikihangaika kubonyeza batani za ile
simu, na mpelelezi kwa haraka akanyakua mkononi mwake..
‘Lakini afande hiyo sio halali, kuna kibali gani cha kuichukua simu
yangu, mimi sio muhalafu, au nimefanya kosa gani, na …’akalalamika, na
mpelelezi, akawa kaishikilia tu ile simu, bila hata kuiangalia, na wakati huo
huo hiyo simu ikaanza kuita. Kwa mngurumo,ina maana hakuweka sauti ya kengele
au mlio wa simu.
Mpelelezi, akatizama namba,…na alibonyeza kitu, akainua ile simu na
kumkabidhi Dalali, ..
‘Pokea simu yako…’akasema, na Dalali akaichukua huku akimtizama huyo
mpelelezi machoni, kwanza niliona uso wa kujiuliza kitu kama hicho, alijua sasa simu inachunguzwa, lakini hakuona
mpelelezi akifanya hivyo, na sasa anarejeshewa…
‘Pokea simu yako…’akasema mpelelezi, na Dalali akageuka nyuma, na
akawa anaipokea ile simu…hakussema halloh, ila sauti kubwa ikasikika humu
ndani..ikisema;
‘Mbona nakupigia simu hupokei, bado upo nahao watu,..sasa sikiliza,
uwe makini sana..na kuanzia sasa usinipigie simu, kama nitakuhitajia
nitakupigia mimi, unasikia, kuna hali inayoendelea siipendi kabisa, yale mambo
yameanza kuleta matatizo, nilikuonya lakini….’ Kumbe mpelelezi alikuwa kaweka
spika, sauti ikawa inasikika.
Dalali alipoona hivyo, akawa anahangaika kuzima hiyo simu, lakini
hakuweza kufanya hivyo na sauti ikaendelea kusikika;
‘Mbona kimia…’ sauti ikasema na dalali akakohoa tu.
‘Kama bado upo na hao watu sawa,…..ila mimi nitapotea kwa muda…mpaka
hali itulie, na sitaki uongee lolote kunihusu mimi tena,..haya uliyataka wewe,
na nilikuonya kuhusu hilo, unaona matokea yake…sasa unaniharibia maisha
yangu,…siwezi kukaa ofisini tena, natafutwa, kwanini natafutwa..lolote
likitokea nitakuonyesha kuwa mimi ni nani…kwaheri…’simu ikakatwa.
Mpelelezi, akawa anamuangalia Dalali, Dalali akawa kanywea, lakini
kwa haraka akasema;
‘Huyu jamaa bwana…unajua …nilitakiwa nikutane naye, ni mteja wangu, …’akasema
Dalali akasema;
‘Ni mteja ndio lakini ni nani…?’ mpelelezi akauliza
‘Nimesema ni mmoja wa wateja wangu, wa kazi zangu, je nahitajika
kuwataja wateja wangu kwako, kwa kosa gani, kwanza , kwanini, nina haki yangu afande..’akasema Dalali
‘Anaitwa nani, ..?’ akauliza mpelelezi
‘Ninalinda haki za wateja wangu, kama kuna kosa nimefanya, basi,
lielekewe, ili hata nikimtaja nilindwe kisheria,..’akasema Dalali
‘Dalali…Dalali…nilikuoanya tokea awali, ..nilikuambia nini..?’
akauliza mpelelezi
‘Niwe mkweli…’akasema Dalali
‘Lakini umekuwa
muongo,..nauliza tena huyo uliyekuwa ukiongea naye ni nani..?’ akauliza
mpelelezi
‘Ni mteja wangu afande..’akasema
‘Ndiye huyo uliyekuwa ukiwasiliana naye awali mbona hiyo namba haina
jina la mpigaji, ..?’ akaulizwa
‘Hap-hapana afande, sio yeye, huyu ni mwingine afande,
lakini…’akataka kuongea lakini afande akamkatiza
‘Naomba hiyo simu yako..naona sasa hatuaminiani…’akasema mpelelezi,
na Dalali, akamuangalia mpelelezi kwa uso wa kushangaa.
Sasa hivi Dalali, akamkabidhi Mpelelezi ile simu, huku akionyesha
kutokujali, na mpelelezi akaichukua ile simu akawa anakagua kagua, kwa kubonyeza
bonyeza namba, …hatukujua anachokifanya, baadae akasema
‘Namba iliyopigwa sasa hivi, sio hiyo iliyokuwa unatuma
ujumbe,..niambia ukweli, ni nani huyu mtu..maana mimi nitafuatilia..na kwanini
akuambia anatafutwa na polisi mumefanya kosa gani…?’ akauliza mpelelezi
‘Huyu ni mmoja wa wateja wangu,…ni mambo yetu, wakati mwingine watu
hujiingiza kwenye kesi za kutapeliana,…siwezi kukueleza zaidi,….’akasema Dalali
‘Basi mimi nitakukamata kwa kosa la kujiingiza kwenye biashara za
kutapeliana..’akasema mpelelezi.
‘Afande, huo ndio utaratibu kama kweli unahisi nimefanya kosa, mimi
sijakueleza kuwa nimeingie kwenye bashara hiyo, ila mwenzangu kashukiwa hivyo,
na sio kweli kuwa kafanya hivyo, na…utaona hata wakienda mahakamani hana
hatia..’akasema
Mpelelezi akawa anainakili ile namba kwenye simu, yake, halafu
akageuka nyumba akatembea hatua mbili akiwa anapigia ile namba, …halafu
akageuka
‘Haipatikani..’akasema na baadae akawa anapiga namba nyingine
‘Haipatikani nayo pia…’akasema mpelelezi..
‘Mimi sijui kwanini kazima simu yake..’akasema Dalali
Mpelelezi baadae akanigeukia, na kusema;
‘Jamaa yako
huyo…anajifanya mjanja,…’akasema mpelelezi.
‘Niendelee
naye…?’ nikauliza
‘Hapana kwa
amri ya wakubwa zangu, wewe sasa upochini yaulinzi kama nilivyokuambia, kwa
makosa niliyokutajia, mengine utakwenda kuyaongelea huko mbele,…kazi yangu ni
hiyo kwasasa,…’akasema mpelelezi.
‘Afande hapa
tunacheza na muda!….’ nikasema
‘Sikiliza
mimi natimiwa wajibu wangu, siwezi kujadili amri ya wakubwa wangu..na kwa
taarifa tu, huenda kesho mnada ukafanyika..’akasema
‘Ndio maana
nilitaka nimalizane na huyu Dalali, ili uone kosa lipo wapi, ili na wewe
ukaweza kulitetea hili..nakuthibitishia kuwa hapa kuna tatizo, na hilo deni,
lina utata..na huo utata, tunaweza kuujua kwa kupitia kwa Dalali..’nikasema
‘Sawa ….kwani
napinga hilo, lakini kwanza natimiza amri ya wakubwa zangu..’akasema
‘Ni sawa
siwezi kukukatalia hilo, ila…jambo moja, ..nikuulize tu, mimi nimefanya kosa
gani kwa hivi sasa, kwa jinsi unavyoona wewe, sema ukweli wako kutoka moyoni ,
mimi nakufahamu sana wewe…, wewe ni mtu unayesimamia sheria, na wakubwa wako
wanaweza kukosea, kuna mtu kawaingilia huko juu,..’nikasema.
‘Hilo
halitasaidia kitu…’akasema akiangalia saa yake
‘Wanadai mimi
nimeingilia amri ya mahakama?, mimi naweza kufanya hivyo kweli hebu lifikirie
hilo kwanza, ..?’ nikamuuliza
‘Si ndio
hivyo umeshafanya, kwanini amri ya mahakama haijafuatwa, kwa maelezo ni wewe
umemtumia wakili kuweka pingamizi,..lakini je una kibali gani cha hii kesi,
huna, kwa ushahidi wangu huna kibali, au niambie umepatia wapi kibali..?’
akaniuliza
‘Afande mimi
nilikuwa naumwa, na nikamtuma wakili afuate taratibu zote,..na wakati anafanya
hivyo, tuone jinsi gani ya kukusanya ushahidi, na haya yanatakiwa yafanyike kwa
haraka kutokana na muda..’nikasema
‘Kwahiyo
kweli uliagiza amri ya mahakama isifanye kazi yake…?’ akauliza
‘Tuwe wa kweli
afande …mimi nina uwezo gani wa kufanya hivyo, ..haya unadai nimetoa
rushwa,…kwa pesa gani nilizo nao mimi..unanifahamu nilivyo, ..je hao watu wamepewa
shilingu ngapi, na nani..?’ nikamuuliza
‘Mimi sijui
hayo ni madai yaliyofikishwa huko ofisini…’akasema
‘Afande, je
unataka haki itendeke au hutaki, je kama ingelikuwa wewe ni marehemu sasa hivi,
familia yako inafanyiwa hivi, na umepewa namna ya kuangalia, ungelijisikiaje..tusisahau
kuwa na sisi ni marehemu watarajiwa…’nikamwambia
‘Sikiliza
hayo unayoyaongea sio jukumu langu, na sasa hivi tunaondoka,..sema nataka
kumalizana na huyu mtu kwanza…’akasema akimgeukia Dalali.
‘Basi mimi
naomba muda kidogo, tumalizane naye kwanza, ili niweke mambo yangu bayana..na
huko tutakwenda tu, najua hakuna jambo …’nikasema
‘Muda gani
unahitajia…’akasema sasa akiangalia saa yake.
‘Mhh…’kabla
sijasema kitu Dalali akadakia
‘Afande huyu
mtu ni mwongo, hana jipya, tokea awali, anadai ana maswali ya kuniuliza, haya
tumempa nafasi hiyo, kauliza nini cha kukusaidia wewe…hakuna, ni kubuni buni
uwongo tu,…sijui ni mtunzi wa hadithi za kufikirika nini…’akasema Dalali.
‘Hujakosea
ndio kazi yake…’akasema mpelelezi.
‘Ndio maana…nilikuwa
najiuliza hayo maswali yote yanatokea wapi,..afande huyo mtu ni tapeli,…uwe
makini naye…’akasema Dalali, na hapo nikaona kanipatia mwanya wa mimi kuingilia
kati.
‘Utapeli
wangu ni nini…?’ nikamuuliza Dalali
‘Kwanza
umekiuka amri halali ya mahakama,
kwasababu ilishahukumu kuwa nyumba hii ipo kwenye taratibu za mnada baada ya
mahakama kurizika na ushahidi, kuwa
kweli hilo deni lipo,…’akasema Dalali.
‘Na… na
mwenye deni aliweka nyumba hii kama dhamana,…na benki wana haki yao kisheria,
sihitaji kukufanulia tena wakati nilishakuelezea kila kitu..na mengine
yanayoendelea ndani ya nyumba hii ni kutokana na hilo deni, hakuna jingine,
deni lipo linamtesa kaka…’akasema Dalali
‘Hebu nimuuliza
hutu mtu, afande…, huyo mkopaji ni nani na ni nani alikubaliana na hilo kuwa
nyumba ipigwe mnada?’ nikauliza
‘Kutokana na
mahakama ni mwenye nyumba hii…’akasema Dalali
‘Huyo mwenye
nyumba hii yupo wapi ….?’ nikauliza
‘Mwenye
nyumba ni marahemu…’akasema
‘Ni marehemu
sio…sasa yeye alikubalije kuwa mnada upigwe wakati ni marehemu?’nikasema kwa
kuuliza
‘Si
aliandikisha kuwa nyumba yake iwe dhamana,..ina maana kwa kufanya hivyo, hata
akifariki nyumba hiyo inaweza kulilipa hilo deni, si ndio maana ya dhamana au, hata
kidini mtu akifa cha kwanza ni kuuliza madeni ya marehemu, au sio ?..........’akasema
Dalali
‘Ni nani kwenye
nyumba hii alilithibitisha hilo..au ushahidi gani uliowahi kutoka kwenye nyumba
hii au kwenu nyie, maana tangia awali ulisema marehemu alikuwa hapendi deni,…’Dalali
akanikatiza
‘Ushahidi
upo benki…humu ndani hata kama hakuna ushahid , lakini ushahidi wa kisheria
umepatikana, wanao wanaodai…kitu muhimu ni kuangalia mkataba
unasemaje..marehemu aliweka dhamana, na ujuavyo dhamana inawekwa kwa mali
zisizohamishika..’akatulia
‘Sitaki
nikufundishe sheria, lakini wewe unanilizimisha,…na taratibu zote za kisheria
zimefuatwa , sio kwamba ni maamuzi tu yangu mimi, hapana, na sio mimi nalifurahia
hilo, hapana, nafanya kwa ajili yakuhakikisha haki inatendeka…na kaka huko
alipo roho yake ipate kuwa huru…’akasema
‘Kwa taarifa
za kibenki hilo deni lilikuwepo tokea awali marehemu akiwa hai..ni kwanini hilo
lisijulikane kwenu..kwanini likaja kujitokeza baada ya kifo cha huyo marehemu..?’ nikamuuliza.
‘Inavyoonekana
labda bro, hakutaka hilo deni lijulikane kwa vile hakupenda kukopa, na nia yake
huenda ni kulilipa haraka iwezekanavyo..’akasema
‘Hilo deni
lina muda gani..?’ nikamuuliza
‘Mhh..kumbukumbu
za benki zitajionyesha, hilo siwezi kulijibu maana sijaweka mahesabu yake,…ila
banki wanaweza kukujibu hilo swali lako.
‘Afande tulichogundua sisi kwa muda mfupi tu,
hilo deni limewekwa kwa marehemu kinamna, …hilo deni sio la marehemu,…’nikasema na Dalali akadakia na
kuuliza
‘Una
ushahidi gani, hapo unaonyesha jinsi gani ulivyo mbumbu,..benk wanajua kazi
yao, haiwezekani eni lihamie kwa mtu mwingine kirahisi hivyo…’akasema
‘Mimi nina
ushahidi….unataka nikuonyeshe….’nikasema na jamaa alishtuka kidogo halafu
akacheka tena kicheko cha dharau, na kusema;
‘Ni deni la
nani, hizo hati aliweka nani sahihi , unasema eti una ushahidi, huna lolote bwana,
asidanganye watu hapa…mimi nimefuatilia kila kitu…mimi ndiye mwenye uchungu wa
hilo, nilihakikisha nimefuatilia hadi kwa wakubwa huko benki, unataka kusema
nini wewe..’akasema
‘Si
nimekuambia mim nina ushahidi, hutaki nikuonyeshe…?’ nikauliza
‘Nionyeshe…kama
utanionyesha mimi nipo tayari kufungwa…’akasema kwa kujiamini
‘Nikuonyeshe
ushaidi sio…?’nikasema na mpelelezi akawa makini kulisikia hilo, nikajua sasa
nimerejesha mjadala mahali pake;
‘Onyesha, na
mimi naapa ukinionyesha huo ushahidi …nipelekeni jela, …siwezi kuitekeleza
familia yangu, hii ni mali yetu, nitakuwa na furaha gani ikichukuliwa, ..ni
kitu hakiingii akilini..’akasema Dalali
Mpelelezi
akakohoa, na kusema
‘Umesema una
ushahidi kuwa deni hilo sio la marehemu, unaweza kunionyesha…?’ akauliza
mpelelezi
‘Ndio lakini kwanza nina ombi kwako…’nikasema
na hapo Dalali akacheka kweli na kusema
‘Unaona…huyu
mtu hana kitu, onyesha huo ushahidi bwana
‘Una ombi
gani….na ushahidi gani ulio nao wewe..?’ Akauliza mpelelezi
‘Ombi langu
nataka kuendelea kumuhoji huyu mtu, kuna maswali nilitaka kumuuliza kuhusu
uhalali wa hilo deni, na yeye anaweza kunisaidia kwa hilo,…kuna siri kubwa
imejificha hapo, nataka kuigundua…’nikasema
‘Ni ushahidi
gani ulio nao wewe…?’ akauliza tena mpelelezi
‘Ushahidi wangu wa kwanza ni yeye
mwenyewe….’nikasema na mpelelezi kwanza akatulia akiwaza jambo halafu akauliza
‘Kwa
vipi….?’ Akauliza huku jamaa anacheka kweli kweli, huku akionyesha kwa mikono
kuwa kipo wapi .
‘Afande wewe
hulioni hilo…?’ nikauliza
‘Niambie wewe…’akasema
afande hapo moyoni nikachekelea na kuanza kuelezea;
‘Haiwezekani
mtu awe na uchungu na familia, awe na uchungu na kaka yake, atokee mtu mwingine
kutaka kusaidia kuupata huo ukweli, halafu yeye awe mstari wa mbele kumpinga
huyo mtu, huo ni ushahidi namba moja, tumia hekima utaligundua hilo, YEYE NDIYE
USHAHIDI WANGU WA KWANZA…..’nikasema na huyo mpelelezi akaangalia saa yake,
halafu akageuka kumuangalia jamaa na jamaa alikuwa bado anacheka kwa dharau, na
alipoona mpelelezi anamtizama akatulia
‘Kwahiyo…’akasema
afande
‘Nipe muda
mchache tu. Utaligundua hilo zaidi..’nikasema
‘Sawa….muulize
hayo maswali…’akasema mpelelezi
Mpelelezi
aliposema hivyo, nikaona uso wa Dalali ukinywea, akabakia kimia akimuangalia
mpelelezi halafu mimi…baadae akasema
‘Afande mimi
naufuta huo anaouita ushahidi wake, tusipoteze muda hapa, ni hivi…’akatulia
kwanza , halafu akaendelea kuongea;
‘Afande…huyu
anasema mimi japokuwa ni ndugu lakini sionyeshi uchungu, je mimi sikufuatilia
benki, ushahid huo upo, nilifuatilia ngazi zoye hatua kwa hatua, na ikafikia
muda hata kugombana na watu wa benki, kaulizeni hilo
‘Lakini kuna
jambo moja, tuwe wa kweli, sheria inasemaje kuhusu deni…ngoja niende kama
anavyotaka yeye, eeh…hata kama angekuwa ni mtoto wangu wa kuzaa kakiuka sheria
siwezi kuipuuza sheria ya nchi..lakini zaidi ya hayo ni muito wa marehemu,
marehemu anataka deni lilipwe,ndio maana haya yanatokea je mimi sijaeleze hayo…’akatulia
‘Umemaliza
kujitetea kuhusu hilo…?’ nikauliza
‘Sijamaliza,..nataka
nikueleweshe kama mwalimu wa shule kwa mtoto wake,…naona kichwa chako ni kigumu
kuelewa…’akasema Dalali
‘Afande…kuna
amri ya mahakama..sisi tulikuwepo kwenye kesi, tukashindwa…imeniuma, lakini
nitafanyaje,…eeh, sasa kama imefikia hatua hatuna ushahidi hatuna cha
kujitetea, ndio nifanye fujo, au…’akatulia
‘Je mimi
raia mwema mwenye heshima zangu, nitawezaje kuipinga amri ya mahakama, pili la ziada..ni hilo... la imani, wengi hawaamini, lakini yakizidi huna ujanja,....ni
huo muito wa kaka yangu, hamjui
tu..nateseka usiku, silali, familia hii hapa inateseka,,….yote hayo yana uzito,
ndio maana nikawa mstari wa mbele kuhakikisha hilo deni hilolinalipwa sasa kwa
njia gani, hilo ndilo lilikuwa la msingi la kusaidiwa..’akatulia
‘Afande,…mimi
sina pesa, shemeji hana pesa, ulitaka tukaibe…eeh niambe bwana mtunga hadithi
za uwongo, afande kasema ndio kazi yako, mimi sijui…niambie sasa,….huo ushahidi
wako una mshiko hapo….hahahaha.’jamaa
akasema .
‘Umemaliza
kujitetea..?’ nikauliza
‘Umerizika
na hoja yangu, …?’ akauliza
‘Sijarizika …maana
mimi nilishaanza kuelezea hayo kwa undani,…nilikuwa nakuuliza maswali yenye
kubainisha kuwa wewe..uliamua kumtafuta mtaalamu ili kushinikiza hilo deni
lionekane ni la kaka yako, ..bado nilikuwa sijafikia maswala ya benki..’nikasema
‘Kwa vipi…?’
akauliza mpelelezi.
‘Umeona
yaliyotokea…mwenye uchungu hilo deni anasaidiwa kushinikiza hilo deni lilipwe
kwa kupitia mizimu,..ni kwanini…na wakala wa mzimu ni Dalali…akifanya udalali
wa mizimu, chini ya kivuli cha Mtaalamu.
‘Ni kwanini
kuwe na shinikizo la mizimu, kama ni mkopo wa benki, benki wanafuta sheria..wana
ushahidi wao wa kibenki, inatosha, au sio…, sasa kwanini iibuke hiyo mizimu,
kuisaidia benki..?’ nikauliza
‘Sawa Dalali
anasema ni shinikizo la marehemu maana huko marehemu alipo anateseka, kaacha
deni halijulikani, si ndio utetezi wake huo….
Nikageuka
kumuangalia Dalali…akatabasamu na kusema
‘Ndio
nashukuru umelielewa hilo…’akasema
‘Tuwageukie
hao hao mizimu tuwaulize..nyie mizimu ni nani..jibu la haraka ni vivuli vya
marehemu kwa njia ya roho au imani…kwa mujibu wa wazee wetu, …lakini je kitaalamu,
kiimani za dini , mizimu ni nini….ni vibwengo, au mashetani..’nikasema
‘Sio kweli..’akasema
Dalali
‘Kama sio
kweli kwanini wanatesa watu wasio na hatia…’nikauliza na hapo Dalali, akakunja
uso kwa kufikiri, na kusema
‘Unataka
jibu…nilishakujibu, ila wewe ni mgumu kuelewa..’akasema
‘Je wewe si
unachungu na hii familia, ..na wewe ndiye mwenye dhamana hiyo,…wewe ndiye
jemedari, kwenye vita ni nani anatafutwa,…si kiongozi wa jeshi, kiongozi wa
jeshi hapa ni nani…ili deni lishinikizwe kulipwa..?’ nikauliza
‘Hahaha…’akacheka,
kabla hajaendelea nikasema
‘Kiongozi ni
wewe..ndio maana umehangaika, sasa kwanini hiyo mizimu isikutese wewe au
familia yako, inakwenda kuwatesa mayatima, na mjane, ambao hata mwenyezimungu
anawatetea sana…’nikasema
‘Sijui….hayo
ni mambo ya mizimu..’akasema
‘Hao sio
mizimu ni mashetani,…mashetani yaliyotengenezwa..’nikasema
‘Hahaha, …umeishiwa….’akasema
‘Mbona
huulizi yametengezwa na nani…’nikasema
‘Kwanini
niulize hivyo…?’ akauliza
‘Kwasababu
hayo mashetani yametengezwa na mtaalamu…unabisha…?’ nikasema
Hapo
mtaalamu akajifanya kucheka sana, lakini niliona kicheko cha kujilazimisha tu.
‘Rejea mazungumo kwenye simu
iliyopigwa na huyo mtu asiyejulikana , alisema nini…?’ nikauliza;
‘Huyo ni
mteja wangu…’akasema Dalali
‘Alisemaje…nanukuu ‘’ila mimi nitapotea kwa muda…mpaka hali itulie,…..
na sitaki uongee lolote kunihusu mimi tena,..haya uliyataka wewe, na nilikuonya
kuhusu hilo, unaona matokea yake…sasa unaniharibia maisha yangu,…siwezi kukaa
ofisini tena, natafutwa, kwanini natafutwa..lolote likitokea nitakuonyesha kuwa
mimi ni nani…kwaheri’’ mwisho wa kunukuu...'
Dalali akabakia kimia
‘Huyo mtu aliyepiga hiyo simu ni nani...?' nikauliza
'Nilishasema ni mteja wangu...'akasema
'Mtaalamu ni mteja wako sio…’nikasema
‘Wewe ni Muongo, huyo sio huyo mtaalamu…’akasema Dalali
‘Ndio yeye, kaamua kutumia namba nyingine…na kapigia simu hiyo akiwa ufichoni…’nikasema
‘Thibitisha huo uwongo wako…’akasema
‘Kabla sijalithibitisha hilo…nataka ufahamu jambo moja…’nikasema
‘Jambo gani…?’ akauliza
‘Tumeshamfahamu huyo mtaalamu ni nani…’nikasema
‘Ili…iweje, haijalishi hata ukimfahamu, kwangu mimi yeye ni mganga wa kienyeji...’akasema.
‘Ni kwanini huyo mtaalamu amekimbia, hayupo huko nyumbani kwake..na ofisini
kwake hakosekanagi kwa muda mrefu, bila taarifa maalumu kwa mkewe, mkewe hajui wapi mumewe kaenda,…’nikasema
‘Mimi nitajuaje,...na, mimi siwezi kumfuatilia,...hata hivyo, mimi naweza kuthibitisha huo uwongo wako, ngoja nimpigie ….’akasema
‘Mpigie sasa hivi kama utampata…’nikasema
Dalali, akachukua simu akaanza kupiga, ….akatulia akasema
‘Hii inaita…’akasema sasa akiwa anacheka, na mpelelezi akamsogelea na kuichukua hiyo simu akabonyeza
kiwambo cha spika ya nje..kwa haraka, na Dalali, akawa kakunja uso..sasa mlio wa kuita ukawa unasikika.
'Sio sahihi afande...'akasema Dalali...na mara sauti ikasikika.
NB: NAISHIA HAPA
WAZO LA
LEO: Mtihani mkubwa wa duniani kwa hivi sasa…, ni kupenda mali, kupenda
utajiri, kila mwenye nafasi kwa wakati wake…bila kujali mali hiyo au utajiri
huo unapatikanaje,…watu wapo tayari kudanganya,…matajiri kuwanyonya masikini,
waajiri kuwanyonya wafanyakazi wao…wafanyabiashara kuwanyonya wanunuzi..nk..
inafikia hata kuwadhulumu mayatima, au hata kuua, watu wanaua hata watoto wao
..ili wapate mali. Hatujiuliza je hiyo mali itatufanya tuishi mielele…wangapi
matajiri wameshatangulia mbele ya haki…Tumuombe mola atusaidie katika kuushinda
mtihani huo, tupate riziki ya halali, na hata tukipata utajiri uwe ni wa
halali.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment