‘Sawa..si unataka
tupambane mimi na wewe, sawa mimi nitakaa, uniulize hayo maswali yako, na
uthibitishe hiyo kauli yako…kwa ushahidi, la sivyo, mimi na wewe tutapalekana
kubaya, sasa hivi sitanii tena, naona unataka sasa kumjua Dalali ni nani
akikasirika…’akakaa, huku akiwa kakunja uso.
‘Dada natumai upo huru
sasa,…usiwe na shaka na lugha yake ya kutishia amani watu, unasikia…., kuanzia
sasa tunaitafuta haki, …na haki hiyo tutaipata kwa kutafuta ukweli wa hilo deni,
je ni kweli ni deni la mume wako, au ni udanganyifu umetendeka…’nikasema
‘Uliza hayo maswali bwana…’akasema Dalali
‘Na huo ukweli utaanzia hapa hapa nyumbani…’nikasema bila kumjalia
Dalali
‘Shemeji huyu mtu hajui lolote …anachotaka yeye ni kutuchuuza,…mimi
naogopa sana kuhusu mtoto, je ikitokea tena itakuwaje, sio kweli kuwa mimi
naweza kuzuia hayo,…nitawezaje mimi, eeh.. toka lini mimi nikawa mganga wa
kienyeji..eeh, eti shemeji wewe si unanifahamu mimi nilivyo..?’ akauliza.
‘Lakini umeweza kumtibia, hebu nikuulize hiyo hali hadi sasa
imetokea mara ya ngapi, kwa kauli yako ..ulisemaje, kuwa ikitokea zaidi ya mara
tatu haitawezekana tena, je ..imeshatokea mara ngapi nab ado umeweza…’nikasema.
‘Jamani, mimi sifanyi haya kwa utashi wangu mimi, nafuata maagizo ya
huyo mtaalamu, na nimetimiza wajibu wangu, sasa ikitokea tena akisema
haitawezekaan tena, mimi sitakuja kulaumiwa, ..nitaondoka zangu…’akasema
‘Baba wa familia unakimbia au sio…huwezi kuondoka, hii ni familia
yako…’nikasema
‘Kwahiyo sasa umeshaifahamu sehemu yangu kuwa mimi ni nani…’akasema
‘Nafahamu sana ndio maana tunakuandama wewe, ili uwajibike…’nikasema
‘Nimesema nini, na watu hawatii…mtoto anateseka, mama upo, unataka
nini shemeji …sijui mnataka niseme nini, eeh,…watu hawajali…tamaa, tamaa
tu…mimi nimechoka..ikitokea tena mimi sipo…’akasema
‘Kwani mimi nimefanya kosa gani…?’ akauliza shemeji mtu
‘Kosa hulioni, haya kwanini yametokea,…shemeji, wakati mwingine hizi
lawama zitakuangukia wewe…kuteseka kwa mtoto, sasa hivi sababu ni wewe…’akasema
Dalali
‘Haitatokea tena dada, asikutishe huyu mtu…, hilo nakuthibitishia,
ilimradi shemeji yako yupo hapa, na akikimbia, atakumbana na nguvu za dola
..’nikasema
‘Kwanini unajiaminisha hivyo, mimi nitafanya nini ikitokea, tatizo
sio mimi, ndugu hebu nielewe…, kwanini unanitwika mzigo nisioweza kuubeba…’ akasema
Dalali
‘Nayasema hayo, kwa kujiamini kwa vile…yote mliyokuwa mkiyafanya
wewe na huyo mganga wako wa kienyeji yameshagundulikana…nikuambie hivyo, ili
unielewe, na..muda si mrefu, hayo madude
yenu yatakuja kuwageukia nyie wenyewe..’nikasema
‘Nini…’ akauliza sasa akionyesha mashaka fulani, halafu akatabasamu,
huku akitikisa kichwa kama kusikitika.
‘Ndio hivyo..ndio maana nimekuambia…usipoangalia hili tatizo kuanzia
sasa litakugeukia wewe mwenyewe, na wenzako watakuwa hawapo nawe..’nikasema
‘Hahahaha…..bro bwana, …ndio maswali yenyewe hayo…’akasema sasa
akimuangalia mpelelezi.
‘Ni nani aliyekwenda kwa huyo mtaalamu, si wewe ulikwenda kwake,
sasa swali ..ulikwenda kwake kufanya nini,…?’ nikamuuliza na hapo, akaondoa ile
sura ya kutabasamu sasa akaonyesha uso wa kujali, akasema;
‘Ndio maswali yenyewe hayo bro,… sio kwamba naogopa kukujibu, ila
nataka niwe na uhakika..?’ akauliza
‘Nauliza hivi Je huyo mtaalamu alikuja kwako, au ni wewe ulikwenda
kwake…?’ nikauliza, bila kujali swali lake
‘Sijakuelewa bado hapo, naomba tuwe wawazi, maana maswali mengine
yanaingilia utawala binafsi, kisheria naweza kusema siwezi kujibu hilo swali,
kwa maana halina mantiki na huu mjadala…’akasema
‘Hiyo ni hoja ambayo mtaalamu atakugeuka nayo, kuwa yeye hana hatia,
wewe ulikwenda kwake kama mteja, ukiwa na shida zako, ukataka kuangaliziwa..si
hivyo au kupigiwa ramli, au sio…, na yeye akatimiza wajibu wake, …’nikatulia
‘Hahaha bro, wauliza majibu
sio, maana umeuliza maswali na majibu unayo wewe mwenyewe,nikuulize tu, kwa
hayo maswali eeh.. unataka kuhakiki nini, kuwa mimi nimefanya dhambi ya kwenda
kupigiwa ramli au sio..lakini wewe ni mzazi kama mimi, na haya yanaweza
kukukuta hata wewe pia, sisi na shemeji ilibidi tuhangaike hivyo,..’akasema
‘Je wewe ulimwambia shemeji yako kuwa unakweda kupiga ramli, kuhusu
hali ya mtoto, na yeye akakubali, ya
kuwa wewe na yeye mlikubaliana kuhusu hilo…?’ nikauliza
‘Vyovyote utakavyosema mimi nishaelewa lengo la hayo maswali yako,
nia ni kunipata mimi matope, ili nionekane mimi ni mbaya, lakini
hutafanikia..’akasema
‘Nimekuuliza swali…’nikasema
‘Nilishakuambia huko sikuenda
mimi peke yangu, nilikwenda na ndugu yake shemeji..na hata hilo wazo la kwenda
huko, sikulitoa mimi mwenyewe, hilo wazo alilitoa huyo huyo ndugu yake shemeji..’akasema
‘Je na kwenda huko kwa huyo
jamaa yako siku hiyo ilikuwa ndio mara yako ya kwanza…au ulishawahi kwenda kuonana
na huyo jamaa kabla…?’ nikamuuliza
‘Yah…ilikuwa ni mara yangu ya kwanza…au..una maana gani kwa hilo
swali lako…?’ akauliza, akishtuka mtego niliomuwekea.
‘Ulikuwa hujawahi kuonana naye kabla ya siku hiyo..?’ nikamuuliza
‘Kuonana kwa maana ya ….ya kufuatilia hilo jambo, au…unajua
nikuambie kitu, huyo jamaa yupo na wateja wengi sana, huwezi kwenda kwake kama
huna jambo muhimu na yeye, na usichanganye mada, kwenda kwake kwa ajili gani,
weka wazi hapo….’akasema
‘Au nikuulize hivi, huyo jamaa yako, nikiwa na maana mtaalamu mnafahamiana
naye kwa muda gani…?’ nikauliza
‘Mhh… sikuwa na namfahamu sana kivile,…siwezi kusema kwa muda gani…’akasema
‘Una uhakika na hilo jibu lako…?’nikauliza
‘Nina uhakika kwa vipi, si nimeshakujibu, kama jibu la hilo swali
sio sahihi, wewe niambie jibu lake ni lipi....’akasema
‘Wewe na mtaalamu hampo na ukaribu fulani…?’ nikauliza
‘Mimi nina watu wengi nipo nao karibu, siwezi ….sijui…labda ufafanue
ukaribu kwa vipi…’akasema
‘Una ukaribu naye kuhusiana na maswala gani…?’ nikamuuliza.
‘Kazi yangu ni nini, ..ni udalali, na kazi ya udalali wateja wako ni
kila mtu mwenye shida hiyo, eeh, mimi nafahamiana na watu wengi sana…’akasema
‘Akiwemo huyo mtaalamu,…kweli si kweli…?’ nikauliza
‘Kufahamiana kwangu mimi na yeye, zaidi imekuja baada ya kupatwa na
hilo tatizo, vinginevyo…mimi sikuwa na ukaribu naye …., pengine tulijuana naye
kama alikuwa na jambo linalohusiana na kazi yangu…labda…’akasema
‘Dalali, nakumbuka afande hapo alikuambia uwe mkweli,…’nikasema na
hapo akageuka kumuangalia mpelelezi.
‘Sasa ulitaka nijibu vipi, hivyo nilivyokujibu ndio hivyo, sikuwa na
mazoea sana na huyo jamaa,…’akasema.
‘Kwahiyo kujuana kwenu zaidi, ni siku ile ulipokwenda na ndugu yake
shemeji, hukuwahi kwenda kwake kabla…?’ nikauliza
‘Nisikilize maana nimeshajua lengo lako…mimi kwenda kwake, kama
ilitokea kabla, ni kutokana na kazi zangu za Udalali…’akasema
‘Ulikuwa ukimtafutia wateja,..maana hiyo ni moja ya kazi za udalali,
au sio…?’ nikamuuliza
‘Hahaha…. hapana, bwana, jamaa huyo hakuhitajia udalali katika kuuza
kazi zake, yeye mwenyewe anajulikana sana…’akasema
‘Kuna kipindi mke wako alikuwa akisumbuliwa na maradhi,
ambayo,…ilibidi mumutafute mtu wa namna hiyo, je kipindi hicho ulikwenda kwa
nani..?’ aliposikia swali hilo akashtuka, na haraka akasema;
‘Hizo ni siku nyingi sana, na baada ya hapo ilishapita muda, sikuwa
na kumbukumbu naye sana, hata nilipoelekezwa tena, ndio nikaja
kumkumbuka…’akasema
‘Aliyekuja kukuelekeza baadae ndio huyo mzee Mtupe..?’ nikauliza
‘Ndio…’akasema
‘Wewe na mzee Mtupe mnaelewana sana…?’ nikauliza
‘Sio kivile..unajua huyo mzee ana tabia ya kuchunguza chunguza watu,
mimi siipendi hiyo tabia yake, tulikuja kukosana kwa hilo…’akasema
‘Alikuchunguza kuhusu jambo gani..?’ nikamuuliza na hapo akageuka
kumuangalia shemeji yake.
‘Mengine hayana umuhimu sana kuyaelezea,..mzee huyo ana tabia chafu,
mpaka watu wanamuhisi kuwa yeye ni mchawi..sio mchawi huyo mzee, watu
hawamfahamu tu…’akasema
‘Wewe una uhakika gani na hilo…?’ nikamuuliza
‘Huyo mzee ni uchimvi wake tu…ana na tabia za kuchunguza chunguza
watu na kujenga fitina, na fitina zake zinazoweza hata kuvunja ndoa za watu…’akasema
‘Huwa anajenga fitina gani kwa mfano…?’ nikauliza
‘Yeye anafikiria kila watu wakikaa karibu, mke na mume wana mambo ya
kimapenzi, sio hivyo, mimi kutokana na kazi zangu nakutana na watu wengi tu,
wawe wanawake au wanaume…’akasema.
‘Hata wake za watu…?’ nikauliza
‘Hajilishi..ilimradi nachunga maadili….’akasema
‘Kama hamkuwa mnaelewana kivile ilikuwaje yeye akakuelekeza huko kwa
mtaalamu..?’ akauliza
‘Siku hiyo wakati tunaongea ni namna gani ya kumtibia mtoto, bahati
nzuri na yeye alikuwepo, ndio akasema yeye anamfahamu mtu mmoja anaweza
kutusaidia, anajulikana sana…’akasema
‘Na hapo ndio ikawa mara yako ya kwanza kumkumbuka huyo mtu, si ndio
hivyo…baada ya kusikia kutoka kwa huyo mzee, ina maana kabla ya hapo, hukuwahi kuliongelea
la mtaalamu kabla,…?’ nikauliza
‘Sikuwahi…maana sikuwa na wazo hilo, na akili yangu haikuwa na
mawazo ya mtu kama huyo, nilishamsahau kiukweli…’akasema
‘Una uhakika…?’ nikamuuliza
‘Muulize hata shemeji…’akasema akimgeukia shemeji yake
Shemeji yake akashtuka, maana alionekana kuwa mbali kimawazo, na
haraka akasema;
‘Mhh…hapo samahani…shemeji unakumbuka uliwahi kunielezea hilo jambo
hata kabla ya siku ile, ukasema kuna mtu unamfahamu, ..na nakumbuka ulimtaja
kabisa hata jina, ukasema ni mtaalamu mnzuri…, naona umeshasahau…’akasema
shemeji yake.
‘Mambo mengi shemeji na huyu jamaa..anayesema ni ndugu yako
ananichanganya tu…’akasema
‘Umeona umuhimu wa shemeji yako kuwepo hapa, kukumbusha yale
uliyoyasahau, sasa..mimi nashangaa, Dalalai unakuwa msahaulifu sasa, awali
uliwahi kusema wewe Dalali, kutokana na kazi yako, unakumbuka sana mambo…je
mbona hili umelisahau.
‘Mimi ni binadamu bwana, kusahau sio kosa, au sio…’akasema,
akimtupia shemeji jicho kama la kutokupendezewa na jinsi alivyosema.
‘Haya shemeji yako kakumbusha,…kwahiyo ni kweli kuwa wewe ulikuwa
ukimfahamu huyo mtu hata kabla hujaenda kwake, na …hata huyoo mzee Mtupe
alipowashauri hivyo, wewe ulikuwa umeshakuwa na huo mpango wako…ni kweli si
kweli…?’nikasema na kuumuliza.
‘Huyo mtaalamu anafahamika na watu wengi, kumfahamu mimi sio
ajabu…na kama niliwahi kwenda kwake kabla,..naweza..ila sio jambo..la ajabu au
sio…na sikumbuki vyema…kama niliongea na shemeji kabla ya siku hiyo…’akatulia
‘Shemeji…hukumbuki…tulikuwa tunabishana sana kuhusu hilo,
sikulipenda, wewe ukawa unanisihi sana….hukumbuki kweli shemeji….’akaambiwa
‘Mhh…yawezekana…ila, …sio vizuri…’akasema akimuangalia shemeji yake
‘Sio vizuri kwa vipi, kukumbusha au…?’ nikauliza
‘Haya ni mambo ya kifamilia, …heshima ya mke ni kuwa na mume
wake,..sio kwa vile mimi ni shemeji basi aniumbue tu mbele za watu…’akasema
‘Samahani shemeji, mimi nilitaka kukumbusha tu…’akasema shemeji
yake.
‘Umefanya vizuri sana..ukweli ni jambo jema sana…’aliyesema hivyo ni
mpelelezi, na Dalali akageuka kumuangalia mpelelezi, na kusema;
‘Ni kweli, nashukuru kanikumbusha,..hamna shida,…sio kwamba nilisema
uwongo kuficha jambo hapana…’akajitetea Dalali.
‘Dalali…haya ninayokuuliza yameshafanyiwa kazi, sio kuwa nakuuliza
tu kupoteza muda, uwe mkweli ili ujiweke salama..’nikasema
‘Mimi nimekuwa mkweli kuwa asilimia kubwa, na nikiteleza kidogo,
…tusameheane, nimeulizwa mambo mengi sana akili nayo inachoka..na.., tatizo la
huyu jamaa unauliza maswali ya kunitega, ili niingie kwenye anga zake, nisema
jambo, ili nionekane muongo, na zaidi ni kama anataka kunishuku mimi kwa jambo
lisilo kuwa la kweli…mimi sihusiki kwa shutuma zake…’akasema
‘Sasa …nakuuliza tena je wewe na mtaalamu hamfahamiana sana, sio mtu
wako wa karibu ambaye mnakutana mara kwa mara..sio jamaa yako mliyeshibana
ambaye mnafanya shuhuli nyingine pamoja…’kabla sijamaliza simu yake ikaingia
ujumbe
Aliusoma ule ujumbe halafu akatikisa kichwa kama kukubaliana na hilo
jambo akasema;
‘Mtaalamu anasema, tusiwe na wasiwasi ila tuwe makini na mipango yetu,
mipango yetu iwe inalenga jinsi gani ya kulipa hilo deni, yeye huko atajitahidi
kuhakikisha kuwa angalau tunakuwa salama kwa leo…’akasema
‘Ni hayo tu…’nikasema
‘Ndio…’akasema
‘Hajakuambiwa jambo jingine…’nikamuuliza na hapo akabakia kimia
Nikageuka kumuangalia mpelelezi, na mpelelezi akawa anaandika jambo,
na mara simu yake ikalia,…akawa anaongea na simu kwa dakika mbli hivi,
alipomaliza mimi sikutaka kujua nini huyo mpelelezi alikuwa anaongea, nikasema
‘Dalali tusipotezeane muda
hapa, sema ukweli wako, kuhusu wewe na mtaalamu..je wewe na yeye hampo karibu
sana, na mara kwa mara unakwenda kwake..je huko unakwenda kufanya nini…?’
nikamuuliza
‘Bro,… thibitisha hiyo shutuma yako, hilo la kwenda kwa mtaalamu
mara kwa mara, umelitoa wapi, sio kweli..niende kwake mara kwa mara kufanya
nini…?’ akauliza
‘Dalali, maswali yangu yalikuwa bado, …hapa nilitaka kukuonyesha
ulivyo, kuwa hata haya yanayoendelea hapa, unayafahamu…sasa ni kwa kiasi gani
na kwanini inatokea hivyo, tunataka wewe uwe muwazi kwetu..je kuna ajenda gani
ya siri kati yako na mtaalamu..’nikasema
‘Hakuna muheshimiwa, mimi zaidi ya kazi zangu, na zaidi ya hili
tatizo la mtoto hakuna jingine,..mengine ni hisia zako mbaya tu…’akasema
‘Huyo mtaalamu wakati anakupigia simu kasema yupo wapi..?’
nikamuuliza
‘Atakuwa nyumbani kwake…’akasema
‘Una uhakika …?’ nikamuuliza
‘Mimi sasa nitajuaje…kama kweli hayupo nyumbani kwake au la…mfano
mimi nipo hapa, ukanipigia simu, si ninaweza kusema nipo nyumbani, ni nani
atajua, …kwa mtizamo wangu huenda yupo nyumbani kwake, kama hayupo huko mimi
sijui…hilo sio swali, na mimi sina mamlaka ya kujua wapi alipo…’akasema
‘Una uhakika, wewe hujui huyo mtu yupo wapi…?’ nikamuuliza
‘Mimi ninachoweza kusema, huyo mtu yupo nyumbani kwake, kama hayupo
huko mimi siwezi kujua …’nikasema
Nikamgeukia afande, na kusema;
‘Afande samahani…mtaalamu ni mmoja wa shahidi muhimu kwenye hii
kesi, kama ulivyoona hapa, kuna kitu kinachoendelea kati ya hawa watu
wawili…nataka kuthibitisha kuwa huyu mtu hapa, anadanganya yeye anajua wapi
alipo huyo mtaalamu…’nikasema
‘Kwani hayupo nyumbani kwake..?’ akauliza mpelelezi
‘Hayupo afande,na hajulikani wapi alipo..’nikasema
‘Kwahiyo unataka mimi nikusaidie nini hapo..?’ akauliza afande..mimi
nikasogea pale alipo afande nikamnong’oneza jambo, afande akatikisa kichwa
kukataa, akionyesha kuwa hakubaliani na mimi, akasema;
‘Una gani, una uhakika na hili jambo, sikiliza usitunge hadithi zako
hapa, siwezi kufanya mambo kitamithilya,… una uhakika gani sasa….?’ Akauliza na
simu yake ikaita,…na sasa akasema;
‘Nataka kwenda kuongea nje kidogo…’akasema na kutoka nje, tukabakia
watatu, na Dalali akaniangalia akiwa na tabasamu la kejeli.
‘Hivi wewe unataka kufanya nini, unanishuku mimi kwa kosa gani..?’
akaniuliza
‘Nataka kupima uaminifu wako…’nikamwambia Dalali
‘Ili iweje…?’ akauliza
‘Ili kweli tuwe na uhakika wa hilo deni, uaminifu wako ndio
utafichua siri ya hilo deni..’nikasema
‘Mimi sikuelewi…hilo deni na uaminifu wangu vinahusianaje, sio mimi
nilyekopa, na wala sikuwa na nalifahamu hilo deni, mbona unanichanganya akili
yangu..unanitaka nini wewe mtu..?’ akauliza sasa akionyesha uso wa kukerwa.
‘Subiria afande aje,…na kumbuka jambo moja, yeye alishakuonya uwe
mkweli, alikuwa na maana yake kubwa sana ya kuja kukusaidia, lakini kwa jinsi
tunavyokwenda umeonyesha kuwa wewe ni muongo..’nikasema
‘Mimi sijasema uwongo wowote.., na kwanini niseme uwongo, ili iweje…’akajitetea
‘Kwanini umeficha ukweli kuwa wewe na mtaalamu mnafahamiana..?’
nikamuuliza
‘Mimi ni kama docta, wakati mwingine unatakiwa kuficha siri za
wateja wako, nisingelisema nafahamiana naye,..na maswala ya waganga wa
kienyeji, unayafahamu, ..kama ulivyosema awali kuwa ramli ni dhambi, lakini
inabidi kufanya ..hata kwa siri, sio lazima nikuambie kila kitu bwana…’akasema
‘Ungelisema huo ukweli, tungelikuelewa,… lakini inavyoonyesha, kuna jambo zaidi ya hilo,..na umeficha ukweli
kuhusu huyo mtu kwa vile kuna jambo mumelifanya wawili, na hutaki lijulikane..’nikasema
‘Unataka kusema nini sasa, kuwa kuna kitu unanishuku mimi, ina maana
hata kuuliza maswali yako yote hayo, wewe unanishuku mimi kufanya ubaya, haya
ni ubaya gani huo nimeufanya mimi..’akasema
‘Dalali…sema ukweli wako..mimi ninaweza kuficha baadhi ya mambo,
wewe na mtaalamu mna ajenda gani ya siri…je haihusiani na hilo deni, labda kama
ulitaka kumtumia ili kulificha hilo deni labda…hebu niambie, ili niweze
kukusaidia..?’ nikamuuliza
‘Hahaha…bro…hizo hisia zako unazitunga kichwani…deni halina ujanja
hilo, hata kama utakwenda kwa mganga wa kienyeji, hilo haliwezi kufichika,..benki
wana ushahidi wote, na nimesikia huko, benki wametuma barua ya kulalamika
mahakamani…’akasema
‘Kakumbia nani hayo..?’ akauliza
‘Sina pokea ujumbe hapa, ..’akasema
‘Nani kakuambia..?’ nikamuuliza
‘Watu wangu,..hata mimi nafuatilia kujua ni nini kinachoendelea,
kama unavyofanya wewe, mimi ni dhamana ya hii familia, lazima nijue
kinachoendelea…’akasema
‘Ni mtaalamu au ni mtu wa banki kakuambia..?’ nikamuuliza
‘Sio lazima nikuambie hilo…’akasema na mara mpelelezi akaingia, na
alionekana kakunja uso, …hakuenda ile sehemu yake, alikuja na kunishika mkono,
akanisogeza pembeni, akaniuliza;
‘Unajua unaleta matatizo…umefanya mambo kinyume na utaratibu,
umezuia maamuzi ya kimahakama bila utaratibu, na …mumetoa pesa kama hongo,
kufanya zoezi hilo lisifanyike, hilo ni kosa kisheria…amri imetolewa wewe ukamatwe,…’akaniambia
‘Mimi nikamatwe…!! Kwa kosa gani..?’ nikamuliza
‘Kuzuia amri halali ya mahakama, na kutoa rushwa…’akasema
‘Mimi nina uwezo gani wa kuzuia amri halali ya mahakama…na ni nani
katoa shutuma hizo..?’ nikauliza
‘Nimearifiwa kutoka ofisini, …na mpelelezi mwenzangu kaitwa na
wakubwa,…ilivyo, wewe inabidi nikukamate hadi kituo cha polisi kwa shutuma
hizo…’akasema
‘Afande, wewe umekuwepo hapa, umesikia jinsi nilivyomuhoji huyo
jamaa, wewe huoni kuwa kuna kitu kwa huyu mtu…kuna dhuluma inayotakiwa
itendeke, na je…kwanini wewe ulitaka kumuhoji kuhusu hiyo ajali, ….?’
Nikamuuliza
‘Hayo ni mambo yangu…hayana uhusiano na hilo jambo lako…’akasema
‘Mimi naweza kuthibitisha kuwa kuwa yote hayo yana mahusiano…ajali,
deni na hawa watu wawili…’nikasema
‘Kwa vipi…?’ akauliza
‘Nipe nafasi hiyo…lakini kabla ya hilo jambo, nataka huyu mtaalamu
atafutwe mahali alipo, huyu mtu ni mtu muhimu sana kwenye hii kesi…’nikasema
‘Amri ya wakubwa wangu ni wewe ukamatwe, mim siwezi kulikiuka hilo
mengine yatafuata baadae, ..’akasema na nilimtupia jicho Dalali, nikaona akisoma
ujumbe kwenye simu yake, na akawa anatabasamu, na hata kusema;
‘Nilijua tu…tapeli mkubwa huyu…’akasema na Mpelelezi akageuka
kumuangalia, na Dalali alipoona anaangaliwa akashisha simu yake na kuweka
mfukoni.
Mpelelezi akaniachia mkono na kumsogelea Dalali
‘Nipe hiyo simu yako…’akasema mpelelezi
‘Ya nini afande, …?’ akauliza Dalali, akishangaa
‘Nipe hiyo simu yako..’akasema afande sasa kwa sauti ya ukali
NB:Tuishie hapa kwa leo.
WAZO
LA LEO: Ukweli na uaminifu unaweza kukusaidia kuepukana na majanga , ukajenga
heshima, na hata kusaidiwa sehemu ambayo ungeliingia matatani, Tujenge hulka ya
ukweli na uaminifu..ili tuwe salama wakati wowote, uwe wa shida au raha.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment