Dalali aliposoma ujumbe kwenye simu yake, niliona uso wake
ukibadilika, japokuwa alijitahidi sana kulificha hilo,…na kwa haraka akageuka
kama anaangalia nyuma, halafu akageuka kutuangalia, sasa uso ukiwa umejaa
tabasamu akasema;
‘Unajua nimepoteza muda mwingi hapa, napoteza pesa, napoteza, yaani
nyie hamjui tu, sisi wa kazi za kubangaiza, ambao hatuji mwisho wa mwezi,
mnatutesa kwakweli, siku moja kupotea bure ni hasara kwakweli, lakini sawa tu…..’akatulia
akiaangalia simu yake, kuna ujumbe mwingine uliingia, akawa anausoma,
alipomaliza akasema;
‘Haya kinachoendelea ni nini, maana nahitajiwa huko…?’ akauliza
‘Kinachoendelea ni kwanza utuambie huo ujumbe uliotumiwa umesema
nini….?’ Nikauliza, hapo akaniangalia kwa uso kwa kutahayari, na kusema;
‘Bro, hii ni simu yangu bro…, na mambo ndani ya simu yangu ni mimi
na watu wangu hayakuhusu, samahani kwa hilo…labda nikuulize hivi, kweli kuna sheria
zakuingiliana kwenye mambo binafsi..?’ akaniuliza halafu akamgeukia mpelelezi
na kuuliza.
‘Eti afande hebu tusaidie kwa hilo…labda mimi sina uhuru huo, labda…japokuwa
sheria hata mimi nazifahamu kidogo, hii sio haki, au sio afande…’akawa anamuangalia mpelelezi.
‘Inategemea, kama ni
mambo ya uhalifu, sheria ipo wazi….’akasema mpelelezi
‘Na nani ni muhalifu
hapa…?’ akauliza Dalali.
‘Dalali, watu wanataka
kula…familia ina njaa, je utafanya ulivyoagizwa au utakwenda kinyume chake,
hayo ni maagizo ya mizimu au sio, kuwa uhakikishe familia imekula…au
nadanganya…ujumbe umesemaje, sio hivyo, au…’nikasema na Dalali akaniangalia sasa
akinywea, na baadae akasema;
‘Wewe..nimekushakugundua
, kuna kitu mnanichezea, mimi sio mtoto mdogo kihivyo,… mimi ni mtoto wa
mjini..yawezekana watu wako wameiba namba ya mtaalamu…halafu wanatuma
ujumbe,..wakijua ni nini kinandelea hapa, halafu wana..ni..chezea akili, haiwezekani
wajue mhhh…’akasema, sasa akiangalia simu yake.
‘Unaona, nilikuambia
nini,…kuwa wenzako wote hawapo na wewe tena, sasa maamuzi ni yako, kusuka au
kunyoa, ila muhimu tunahitajia hii familia iwe na mazingira ..tunataka shemeji
yako aweze kuingia huko jikoni kwa amani..na wewe ndiwe wakala wa mambo hayo,
sijasema unahusika,ila wewe si unaelekezwa tu…na mizimu au sio…?’ nikamuuliza
na huku nikigeuka kumuangalia mpelelezi.
Mpelelezi akawa
ananiangalia kwa hali ya kutaka kuniuliza maswali, lakini hakuweza kufanya
hivyo,…najua alishaona akifanya hivyo ataharibu, kwahiyo akakaa kimia,na Dalali
akasema;
‘Ok..ok..ngoja tufanye
hivi….’ Sasa akatoa unga kwenye kichupa chake, …akasogea pembeni, akachukua
chetezo cha mkaa.., akaweka ule unga unga kwenye hicho chetezo, halafu…,
akachukua kibiriti, akawasha.
Moto ukawa utafikri ule
unga unga ni mafuta ya taa, na haikupita muda, kukajaa moshi, uliokuwa unaenea
taratibu, taratibu, na harufu kali ya manukato ikasambaa eneo lote..
Tukawa kimia,
tunasubiria…ule moshi ulipotulia, Dalali ambaye alikuwa kainamisha kichwa
karibu na kile chetezo, akasimama…na kutuangalia, hakusema neno hapo kwa hapo, ….baadae
akasema;
‘Ok,..nimefuata
nilivyoelekezwa, sasa shemeji unaweza kwenda kuandaa chakula…na, hata kuingia
chumbani,..hakuna tatizo,..hii ni kwa mjibu wa mtaalamu, kanitumia ujume wake
nifanye hivyo…’akasema
‘Umeonaeeh, na mimi
kumbe naweza kuongea na mizimu…’nikasema huku nikitabasamu, na jamaa akacheka
kicheko cha dhihaka, huku akisema;
‘Hahaha…bro,
bro….unasema umeongea na mizimu, hahaha…unanichekesha kweli, hao ni mizimu wa
familia, hakuna mwingine zaidi ya familia hii anayeweza kuongea nao,labda na
wewe uwe mtaalamu wa mambo hayo…’akasema
‘Labda na mimi ni
mtaalamu je…’nikasema
‘Lakini bro…wewe si
mchezo, …umenipatia changamoto, isingelikuwa haya matatizo, nilitaka tuwe
marafiki kidogo…’akasema
‘Kwanini…kwani sisi ni
maadui..?’ nikauliza, sasa nikijaribu kutengeneza hali ya kuaminiana.
‘Sikiliza…ninashangaa
jinsi gani ulivyofahamu niliyoandikiwa na mtaalamu…lakini sio tija, kwa vile
sio maswala yangu, mimi ni mtumishi tu, sina wasiwasi na hilo….sina shaka kabisa…’akasema
Wakati huo shemeji
alishaelekea jikoni, na baadae akarudi na kuulizia, ..
‘Kwahiyo hivyo vitu
vyote ni vya humu,…maana naona ni vingi sana…?’ akauliza
‘Ndio…ni vya humu, kwa
taarifa niliyopewa ofisini …ni bahati sana kupata msaada kama huo, maana mara
nyingi hutolewa kama kuna janga la kijamii….lakini haina shida, muhimu haya
mambo yaishe..’akasema mpelelezi
‘Tunashukuru sana afande…’akasema
Dalali, kukapita ukimia kidogo
Halafu Dalali
akanigeukia, na kusema
‘Sasa twaweza
kuongea,…maana akili hapa ilikuwa inaniwanga, najiuliza hawa watu watakula
nini..huko kwangu kwenyewe ..mmh, hata sitaki kulalamika hapa, lakini huko hakuna
shida…najua wife atachakarika,..maana kiukweli leo nimepigika, sina kitu kabisa
hapa mfukoni…’akasema Dalali.
‘Wewe ukikosa si
unaongea na mizimu yenu tu, wanakuleta chakula…’nikasema kiutani
‘Hahahaha, bro bwana,
acha hayo, mimi sio mtaalamu, hata wataalmu wenyewe hawafanyi hivyo, kula ni
jasho lako bwana, kama huna pesa huna..utalala njaa, hat yule mtaalamu
anategemea wateja waje ili apate riziki yake ya siku, hayo mambo yana masharti
yake..’akasema Dalali.
‘Mimi nimeongea na
mizimu yako, imesema haya mambo yana mkono wa mtu, na huyo mtu yupo ndani ya
hii familia…’nikasema, hapo Dalali, akaniangalia akiwa kanikazia macho, halafu
akacheka
‘Hahaha, bro bwana…usilete
masihara hapa, hii familia ni mimi na hawa wanafamilia niliokabidhiwa…sasa
ukisema hivyo,..ni nani unamshuku…?’ akawa kama anauliza.
‘Mimi sijui ila mizimu
ndio imesema hivyo…’ nikasema
‘Afande huyu mtu ni
mjanja sana, unajua kama una hasira unaweza ukakosana naye kwa haraka sana,
..ana mbinu mbinu za kuchokonoa mtu, akasirike ili aongee ovyo..lakini sio
mimi, mimi ni mjanja, …na hataamini, nitakuja kumshiak seehmu ambayo hataamini,
ndio atajua mimi ni Dalali,…’akasema
‘Una maana gani kusema
hivyo..?’nikamuuliza..na Dalali akacheka ile ya dharau, halafu akasema;
‘Unajua kiukweli
niwaambie, …haya mambo yapo..mizimu, ni tofauti na mambo mengine ya uchawi,
tusiyachanganye jamani, awali mimi nilikuwa siamini, lakini nilipokutana na
huyo mtaalamu , sasa naanza kuamini kuwa hayo mambo yapo..na sio mambo ya
kuchezea chezea…’akasema
‘Lakini mimi nasikia
hata hayo mambo ya mizimu kama ulivyo uchawi wengine huenda kufanyiwa kwa
wataalamu, ….wananunua huo utaalamu, kwa ajili ya kuwahadaa watu wengine…’nikasema
‘Kununua…hahaha, hiyo
ndio naanza kusikia kwako,..sikiliza mambo ya mizimu ni ni ya mababu wa familai
husika, sasa utayanunuaje, mimi hapo sikuelewi…’ akasema
‘Kama unataka kufanikiwa
katika mambo yako, si unayanunua ili uweze kufanikiwa au sio..kwasababu
nionavyo mimi hayo mambo hayana tofauti na uchawi..’nikasema
‘Hapana sio kweli, hapo
naona upo kinyume na mambo hayo, na hapo ndio naona hujui kabisa mambo hayo…halafu
,..ili iweje, hapana hata kama watasema nitakuwa tajiri, kwa kupitia mambo hayo
mimi..siwezi, ..unajua kuna mambo unatakiwa uwe makini nayo, mojawapo ni
hilo…kujiingiza kwenye mambo ya mizimu unajifungia kwenye maisha yako ya kawaida..., utaambiwa ukae hivi, usile hivi,
usifanye hivi, ni shiida….’akasema
'Kwahiyo wewe umeshaingia kwenye kifungo hicho au sio...?' akaulizwa
'Hapana..sio mimi...mimi ni mumbe tu, ...'akatulia
‘Ni kweli wewe ni mjumbe tu,.., kama
ulivyosema, maana hivi sasa hii familia inateseka, sababu si ndio hiyo hiyo ya
mizimu, je hiyo mizimu haina huruma, ina maana wewe na ujumbe wako, huna huruma na familia yako…ndio maana mimi nasema huo sasa ni uchawi tu,…’nikasema.
‘Familia hii haiteseki
kwasababu ya uchawi hapa..., kuteseka kwa hapa, kama nilivyosema awali..ni
sababu ya hilo deni, tukimaliza na hilo deni haya hayatatokea tena..ila kama
tutajifanya wajanja, ..si unaona mtaalamu kawaomba, kawazimisha kwa muda,
baadae watarudi tena, maana agizo lao halijafanyika, lakini kama tutakuja na
njia sahihi ya kulipa hilo deni, aah, hutawaona tena hapa…’akasema.
‘Nikuulize tu, huo
mtaalamu kawazimishaje, kawafanyaje hadi wakatoka humu ndani..hao mizimu
wenu..?’ nikauliza.
‘Hapo wewe wataka mimi niwe
kwenye kichwa cha mtaalamu au sio..’akasema
‘Mhh..lakini wewe si unajua-jua hayo
mambo, labda, yeye mtaalamu, kutokana na mizimu au sio, kawalilia hali, kawaomba kuwa tufanye hivi na vile, watuvumilie , si ndio hivyo, au...sasa najiuliza hivi, ina maana wao mizimu hawajui dhamira
yetu..?’ nikauliza
‘Mimi sijui lolote kuhusu hilo,…labda swali
hilo tungelimuuliza mtaalamu yeye mwenyewe, au sio…’akasema.
Tuliongea hayo maongezi
tukisubiria shemeji awepo maana tulitaka maswali yakiulizwa na huyo shemeji yake awepo kama shahidi, …
Na kweli , mara shemeji akaja kutuarifu kuwa chakula kipo tayari mezeni,
tukajumuika na kupata chakula, baadae maongezi yakaanza…
Na aliyeanzisha mjadala huo ni Dalali yeye mwenyewe...
‘Shemeji, ..sasa hivi mimi nimeshawaelewa hawa ndugu zetu, kiukweli nimegundua kuwa, wapo na nia safi ya kulimaliza hili tatizo,
hata mtaalamu kaliona hilo, na mtaalamu kafanya mambo yake, kawaomba hao mizimu watupatie muda, ili tutafute namna ya kulipa hilo deni, ..sasa sijui maana hawa jamaa zangu hawajaniweka bayana...'katulia.
'Ila kiukweli mizimu wamesikia kilio chetu...hatujui mpaka lini, kinachotakiwa ni juhudi zetu...zionyeshe dhamira ya kweli ya kulilipa hilo deni, kwahiyo ...eeh, shemeji mimi nakuomba, usiwe na wasiwasi kabisa…’akasema
Dalali.
‘Kwahiyo mimi nitakuwa
huru kuongea ninavyosikia, ..ukweli wa ninavyojua mimi,..?’ akauliza.
‘Sawa ilimradi iwe hoja
ya kusaidia hilo deni lilipwe..’akasema Dalali
‘Nauliza hivi…maana
awali sikutakiwa kulipinga hilo deni, …na kila nikifanya hivyo, kuna majitu
yanaotokea mbele yangu, je sasa hivi nikifanya hivyo hayatatokea tena, je
nikifanya hivyo mtoto wangu hatateseka tena, …?’ akauliza akiwaangalia watoto
wake.
‘Dada, sasa hivi lolote
likitokea mbaya wako atakuwa ni huyu shemeji yako..unasikia, kutokana na hao
mizimu, huyu ndiye anatakiwa kuwazuia, ana uwezo huo wa kuwazuia…’nikasema.
Dalali, akasimama…
‘Unataka kwenda wapi..?’
akauliza mpelelezi.
‘Kama mambo ndio haya
mimi sitaki kuendelea na haya maongezi, tulikuwa tunaongea wanaume mambo yetu,
utani nakadhalika, sasa kumbe huyu jamaa kachukulia kuwa ni ukweli, mambo gani
haya sasa…’akasema Dalali.
‘Sikiliza,…kama
likitokea baya jingine wewe ndiye utawajibika, hili sasa naliweka mikononi mwa
afande hapa, kama unataka nithibitishe kuwa wewe unahusika na haya subiria
maswali yangu, kama..unakimbia ina maana wewe kweli ndiye unahusika..’nikasema.
Dalali, akawa bado
kasimama, na mara simu yake ikaingia ujumbe akausoma, ..akatabasamu, ..akasema.
‘Sawa..si unataka
tupambane mimi na wewe, sawa mimi nitakaa, niuliza hayo maswali yako, na
uthibitishe hiyo kauli yako…kwa ushahidi, la sivyo, mimi na wewe tutapalekana
kubaya, sasa hivi sitanii tena…’akakaa sasa kakunja uso.
NB:Kwa leo inatosha,
siku mbili sijatuma muendelezo tulikuwa na msiba, mama yetu mdogo katungulia
mbele ya haki. Twamuomba mola amsamehe madhambi yake na ampe mkazi mema peponi Aamin.
WAZO LA LEO: Mara nyingi watu huona kusema uwongo ni jambo rahisi tu, halina
madhara…,lakini tunasahau madhara hayo yanayompata huyo tuliyemsema uwongo, je
tutawezaje kumlipa huyo mtu…ni rahis tu, kutamka, lakini twajua ni ni mzigo
gani tunaoubeba wa dhambi hiyo, tutakuja kujiteteaje mbele ya mola wetu.
Tukumbuke
jambo moja…za mwizi huwa ni arubaini, unapodanganya huna tofauti na kuiba,
umeiba uaminifu aliokupa huyo mwenzako, na uwongo mara nyingini mbio fupi, na mbio zake huishia ukingoni.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment