Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, July 11, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-20


‘Nataka ukweli, je mke wa marehemu alikubali kivipi, kuhusu hilo deni..ukweli wa kauli yake…?’ nikauliza kumchanganya kichwa.



‘Kuamini, ni kutokana na hali halisi,…ni lazima aamini kama mimi..mimi sijapenda kufananya hivyo, ni hali halisi…sasa subiria akiamuka, atayajibu hayo yeye mwenyewe, akikataa…haya,…’akatulia pale tulipohisi jambo…

‘Mimi kati sikuwahi kukubaliana na hiyo kauli yako, waka sikuwahi kusema mume wangu ana deni…’

Na sote tukageuka kuangalia kule sauti ilipotokea.

Tuendelee na kisa chetu…

**************

Kabla hata mmoja wetu hajasema neno, sauti ile ikandelea kusema;

‘ Mniwe radhi kwa hilo….najua nipo kifungoni, lakini nashindwa kunyamaza..na kwa hilo, nimeshindwa…mimi sikuwahi kamwe kukubaliana na hilo na sitakubaliana na hilo…ila sasa nifanyaje…’ilikuwa sauti ngeni, sauti ya kike

‘Kumbe ni shemeji…nilijua tu dawa itafanya kazi…’ilikuwa sauti ya Dalali

Mama mjane alikuwa sasa kakaa, kashikilia kichwa kuashiria kinamuuma, na mimi nikageuka huku na kule nikitafauta kama naweza kupata dawa, na kabla sijasema kitu Dalali akasema;

‘Mnaona niliwaambia..dawa zina fanya kazi, si ndiyo huyo kaamuka sema bado, ..hajawa sawa….’akasema Dalali.

‘Dawa au ujanja ujanja wenu…haya mfanyie na dawa ya kumuondolea hayo maumivi ya kichwa, huoni kicha kinamuuma, hakuna dawa ya maumivu ya kichwa humu ndani…’nikasema na jamaa hapo akanitupia jicho, kama ananionya, halafu akasema;

‘Uwe makini na lugha yako…sitaki mimi kuongea ovyo, maana yupo afande hapa namuheshimu sana..na wewe ni jamaa yetu kama ulivyoadai wewe , kuwa wewe ni kaka yake shemeji…..sasa mimi nisingelipenda tukavunjiana udugu huo, kama kweli wewe ni ndugu ya shemeji,  ila ukiendelea huenda nami nitashindwa, japokuwa sio tabia yangu hiyo…’akasema.

‘Kasema yeye ni ndugu yake huyu mama mjane…!?’ akauliza mpelelezi akionyesha kushangaa.

‘Ndio afande…muulize yeye mwenyewe kuhusu hilo, ila mimi sikuwahi
kumuamini..unajua afande, mtu akiwa anatumia njia ya uwongo, hata kusudio lake litakuwa na mashaka, ila tuendelee tu, …’akasema Dalali, na aliponiona mimi nipo kimia, akauliza

‘Seme je si ndivyo hivyo ulivyosema au….?’ Akaniuliza Dalali

‘Mtoto wangu, yupo wapi…?’  ilikuwa sauti ya mama mjane, ilinisaidia mimi nisiweze kuanza kujitete, sote tukamgeukia mama Mjane, …bado alikuwa kakaa chini, bado akihangaika na kichwa chake.

‘Shemeji mtoto hajambo,..yule pale kwenye sofa, humuoni..’akasema
Dalali na mama mjane akainua mikono na akawa anapikicha macho yake.

‘Mhh..macho yangu yamekuwaje, ..mbona siwezi kuona…’akasema mama mjane.

‘Dawa hiyo bado inafanya kazi, wewe umekurupuka kabla ya muda wake…’akasema Dalali…

‘Kwahiyo nifanye niweze kuona, …macho yangu jamani….’akasema mama mjane

‘Dawa yake ni ulale mpaka dawa imalize kufanya kazi yake la sivyo unaweza kuishia kutokuuona kabisa, na usijilazimishe kuongea…..lala , kaa kimia, muda utafika utakuwa salama…’akasema Dalali.

‘Unataka asiongee, asitoe ushahdi au sio..?’ nikauliza

‘Ushahidi gani….hivi wewe unajali afya yake au unajali hisia zako..kwani kuna ubaya gani akisubiria hadi afya yake iwe nzuri..eti afande, huyu mtu anataka nini..mimi ninachojali ni masharti ya hiyo dawa…’akasema Dalali.

‘Kwani wewe ni mganga wa kienyeji…?’ akauliza mpelelezi

‘Hapana,…mimi nafuata masharti tu…’akasema

‘Kutokwa kwa nani..?’ akaulizwa

‘Ni mtaalamu…aliyenipatia hizo dawa…’akasema

‘Muliongea lini…mapaka akakuelekeza hayo..?’ akaulizwa

‘Kuna muda nilimtumia ujumbe wa maneno…alikuwa hapatikani, ..ni wakati tunahangaika na jamaa yangu hapa…baadae ndio akanitumie maelekezo jinsi gani tufanye…’akasema

‘Kwahiyo unasemaje..?’ akauliza mpelelezi

‘Kutokana na hizo dawa, ngoja alale kidogo, ili dawa ziendelee kufanya kazi, baadae akiamuka kila kitu kitakuwa sawa, labda na sisi tuendelee kuichokoza hiyo mizimu…mimi sijui lakini, nafuta nilivyoelekezwa, aah…’akasema

‘Tuichokoze mizimu, una maana gani kusema hivyo…!?’ akauliza
mpelelezi.

‘Afande, hayo yatakuumiza kichwa tu…yaache kama yalivyo, haya ni mambo ya kifamilia zaidi, ndio maana tulishauriwa hivyo..kuyamaliza haya mataizo kinyumbani …ila sasa , tatizo ni kaam hili wakijitokeza watu wa nje, wakaja na mambo yao..ndio kunatokea haya matatizo...’akasema

‘Matatizo yalivyo humu yaonekana ni wewe na mtaalamu ..ndio chanzo cha hayo matatizo..’nikasema

‘Una uhakika…’akasema dalali, na mimi nikabakia kimia, nahapo ndio akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Hayo ya mtoto kupandisha homa, kuumwa, unafikiri ni nini, na lini tulimpeleka hospitalini akapona, muuze hata shemeji, analielewa hilo,..hayo ni mambo juu ya uwezo wetu..na aliyeweza kutusaidia ni huyi mtaalamu na hapa ninachokifanya ni kufuata maagizo yake tu…’akasema  Dalali.

Mara mama mjane akawa anapiga miayo, …na ilionekana kama anataka kuzindukana tena, kwani muda mfupi, alishashikwa na usingizi mnzito…

Dalali alipoona shemeji yake kazindukana,na sasa anataka kusimama, akamsogelea na kusema;

‘Shemeji, tulia kwanza…’akasema Dalali, lakini mama mjane akajitahidi akasimama na kutembea pale alipolala mtoto wake, akamshika-shika shavuni, ile ya kumpima na mkono kama bado anachemka homa….alipoona mtoto hana homa,akambebe, mtoto alikuwa bado kalala

‘Shemeji, usimuuinue huyo mtoto hapo alipo, subiria kwanza, dawa yake bado inafanya kazi…’akasema Dalali akumuashiria shemeji yake kwa mkono, lakini shemeji yake hakumsikiliza…

‘Sina muda wa kusubiria hapa…’akasema mama mjane, na aliposema hivyo, alikuwa ameshamchukua mtoto na akawa anatembea kuelekea kwenye mlango wa kuingia kwenye moja ya vyumba vya hiyo nyumba, nahisi ndio chumba cha watoto...

 Haikupita muda,  mara mama mjane akatoka huko chumbani, sasa akiwa kabeba begi la nguo, na vifaa vingine, mtoto mdogo yupo mgongoni na huyu mwingine  yupo pembeni yake., kamshikilia mkono.

‘Oh,…. vipi dada…kuna tatizo gani tena..?’ mimi nikauliza na mpelelezi akawa anaumuangalia huyo mama kwa mshangao pia. Nikamtupia Dalali jicho la kujiiba, nilishangaa kumuona  Dalali alikuwa haonyeshi kushtushwa na hicho kitendo cha shemeji yake.

Mama mjane akasema;

‘Tatizo gani!….haya yote ni  matatizo kwangu, hapa nilipo moyo hautulii, nahisi kama kuna lolote baya laweza kutokea kwa wanangu…’akasema sasa akiwa anaonekana anataka kutoka nje..ila wakati anaongea alikuwa kasimama, na alipoona tupo kimia akainua hatua moja , mbili, halafy akasimama na kusema;

‘Dada …nisikilize kwanza…’nikasema, hakutaka hata kuniangalia, akawa anaongea na huku akitaka kuondoka, ila …akasimama=, ila hakunigeukia akasema;

‘Jamani mimi nimeona  bora niondoke kabisa kwenye hii nyumba, niende kwa jamaa yangu mmoja…, hana uwezo, nayafahamu maisha yake, lakini sasa, nitakwenda wapi sasa….maisha yangu yalikuwa yalimjua mume wangu, ndiye ndugu yangu,….wengine …asilimia kubwa walikuwa wakitutegemea sisi…mume hayupo …ni nani wa kunisaidia mimi…’hapo akatulia

‘Lakini dada, bado huhitaji kutegemea ndugu, nina imani wewe utaweza kujitegemea wewe mwenyewe, muhimu ni kupambana na hili janga kwanza…’nikasema

‘Mimi sitaweza kuishi tena humu ndani..nimeingia tu huko ndani nimekutana na vitu vya ajabu-ajabu…, mtoto wangu huyu mkubwa analia anasema kuna simba…mimi mwenyewe naona watu warefu, nisioweza kuwamaliza…hapana naogopa sana, ..na kwanini niteseke, kwasababu ya nini, ni hii nyumba tu…..’akasema

‘Dada sikiliza…sisi tunataka kulimaliza hili, usikate tamaa,..hatua iliyofikia ni nzuri tu, na hayo ya mtoto yanafanyiwa kazi, na yote humu ndani yatakwisha, wao wanaona wamefanya jambo, lakini hawawezi kushindana na mungu,....niamini mimi..’nikasema.

‘Nikuamini wewe!!…wewe si uliona hali ya mtoto ilivyokuwa hapa…, je hali kama hiyo ikirudia tena kwa mtoto wangu itakuwaje..si ndio atakufa kabisa…hapana, …nimeota ndoto kuwa bora niondoke tu, na haki yangu..ipo, mungu atajua la kufanya…’akasema na sasa akawa anaaza kutembea kuelekea mlangoni

Mpelelezi aliyekua kimia, akasema;

‘Sikiliza shemeji, mimi ni askari mpelelezi, nipo hapa kwa ajili yako, ..na kama lolote litatokea kwa huyo mtoto au wewe, mimi nipo,…jitambue kuwa kuanzia  sasa upo kwenye mikono ya dola,…huyo anayehusika na haya mambo.., atatafutwa kwa njia yoyote ile,..unasikia,atapata taabu sana,…’akasema mpelelezi.

‘Wewe unasema tu,…huyu mwenzako aliniaminisha hivyo hivyo, ..kuna askari mwingine aliwahi kufika hapa, akasema hivyo hivyo,..dola dola, ..yenyewe dola haiamini mambo hayo, na mambo hayo ndiyo yanatutesa,…hapana bora mimi niondoke…’akasema mama mjane.

‘Wewe unahisi ni nani anakufanyia hivyo…maana kwa kauli yako hiyo
inaonyesha kama kuna mtu yupo nyuma ya haya mambo..na kwanini…mbona kauli yako inakwenda kinyume na alivyosema shemeji yako, eeh, hebu niambia ni nani unamshuku kuwa yupo nyuma ya haya mambo..?’ akauliza mpelelezi.

‘Mimi sijui, na wala simshuku mtu…ila ninachoona ni cha ajabu, ni kwanini hali ya mtoto wangu inakuwa hivyo,…mbaya , mbaya… kila nikitaka kufuatilia haki zao, haki ya nyumba, haki…..na …..mimi sijui…’akatulia kama anaona kitu mbele yake.

‘Kuna nini…?’ akauliza mpelelezi akiangalia huko anapoangalia huyo mama, lakini yeye hakuona kitu, akageuza kichwa kumuangalia huyo mama, na huyo mama bado alikuwa akiendelea kuangalia jambo…macho ndio yanaonyesha hicho anachokiona sio kitu cha kawaida ni cha kutisha

‘Hata sijui…’akasema huyo mama mjane, na mpelelezi akawa anaangalia tena huko alipokuwa akitizama huyo mma,..na sasa akaamu kabisa kusogea pale aliposimama huyo mama na kuuliza

‘Unaona nini, cha kukutisha hivyo eeh, mbona mimi sioni kitu unaangalia huko …?’ akauliza mpelelezi

‘Ndio maana sitaki tena kukaa humu ndani, kama ninavyoviona mimi nyie hamvioni, ….sasa nitalindwaje na watu ambao hawaoni kile ninachokiona mimi…, je mkiondoka hapa usiku mimi nitabakiaje…na kwanini nikienda kuishi kwingine watoto wangu wanakuwa hawana tatizo,…’akasema

‘Lakini hatuoni kitu…’akasema mpelelezi.

‘Mimi naona…na watoto wanaona…kwanini sisi tuone nyie msione,..ina maana tatizo ni hii nyumba, ngoja niondoke, wachukue tu hicho wanachokitaka….’akasema huyo mama kwa uchungu.

‘Lakini shemeji si ulishaambiwa ni kwanini hayo yanatokea, tatizo ni wewe unakiuka miiko, ulipewa masharti, au sio, mimi nilikuambia alivyosema mtaalamu, wewe unakaidi,..kwahiyo sio swala la nyumba, ni haki za marehemu, ni..hilo tu …..’ akasema Dalali

‘Ndio maana nimeamua niondoke,  siwezi  kuchezea maisha ya  watoto wangu tena,  eti kwasababu ya mali, kama ni jasho langu, kama ni jasho la watoto wangu, mungu mwenyewe atajua jinsi gani ya kutulipia, yote hayo mimi namuachia mungu, kwa mapenzi yake najua ipo siku, haki yao italipwa….’akasema huyo mama kwa huzuni, na shemeji yake akasema;

‘Lakini shemu ukisema hivyo unamlaumu nani sasa, benki au…, je kweli deni halipo, wao wametuonyesha kuwa deni lipo, na mume wako, bro…alikopa huko, ushahidi upo,…sasa ulitakaje, ni nani atalilipa hilo deni…?’ akauliza na shemeji mtuu alitaka kusema kitu, lakini jamaa akaendelea kuongea

‘Sisi kama familia hatuna uwezo wa kulilipa hilo deni, unatufahamu sana…sasa tufanyaje..maana benki wao wanataka haki yao,na deni hilo ndilo  linalomtesa mumeo wako huko alipo, kwahiyo, tatizo sio nyumba , tatizo ni deni, kama ipo namna nyingine ya kulilipa hilo deni, basi tuitafute,….’akasema shemeji mtu akiniangalia mimi, na mimi nikawa kimia tu.

‘Au wewe tuambie…una jinsi gani ya kuwezesha hilo deni kulipwa,….maana sio sisi, sisi hatuna lolote na hilo deni, deni ni la benki, pesa inayotakiwa ni kulipia deni la benk, sio ya mtu yoyote baki, au sio… ‘akasema Dalali

‘Unataka nikujibu…?’ akauliza mama mjane

‘Sio unijibu, utoe ushauri wako, unavyoona wewe labda…’akasema jamaa

‘Je mtoto wangu hataumwa….?’ Akauliza

‘Aaah..kwani ushauri wako upoje…?’ akauliza

‘Ushauri wangu upoje…eeh,.. ushauri wangu ni ule ule…na nilivyotaka
mimi, ni hivyo, haitakiwi ..na ilivyo ni kuwa  mimi nifunge mdomo, si ndio maana yake, sitakiwi kusema ya moyoni mwangu, sasa niambie…nifanye nini hapo…?’ akauliza

‘Mimi nimetaka kusikia ushauri wa jinsi gani pesa ya kulipia hilo deni utapatikana hilo ndilo mizimu inataka, sio kwenda kinyume nao, sijui unanielewa…’akasema Dalali.

‘Nitalipaje hilo deni ..la nani….?’ Akauliza huyo mama mjane na alipotamka hivyo, akaonekana kutulia ghafla, akatoa macho kuangalia mbele…halafu akasema;

‘Unaona sasa, kumbe sitaki kuongea lolote…nikae kimia, je nitawezaje
kukaa kimia, hata…hapa sio pa kuishi tena…’akasema huyo mdada, sasa akimshika mtoto wake kutaka kuondoka.

‘Nitakachokishauri shemu, ni kutoa mawazo chanya, yenye kusaidia, labda ulikuwa na wazo ano jingine la kusaidia,…’akasema

‘Naona wewe unanilazimisha niongee yale yasiyotakiwa mimi niongee….’akasema shemeji.

‘Wewe ongea tu…’akasema shemeji yake.

‘Niongee eeh.., unanitega au….sasa  nikuulize je nikitoa huo ushauri wangu, sitakuwa nimevunja hiyo miiko yenu…?’ akauliza na jamaa aliposikia hivyo, akabakia kimia, ni kama mtu kampiga kibao cha usoni . Na mimi hapo nikaona niingilie kati, na kusema;

‘Dada nakuomba usiondoke, …rudisha hiyo mizigo ndani, na kamlaze mtoto, …haya mambo tunayamaliza leo hii hii…, wewe niamini kabisa, na huyo mtoto hawezi kupatwa na hayo marue rue tena…’ nikasema



‘Unasema nini, mimi niingie tena huko ndani..hapana…’akasema



‘Sikiliza…huyu mtaalamu, shemeji yako yupo hapa….anajua jinsi gani ya kumponyesha huyo mtoto, na pia anafahamu jinsi gani ya kuyaondoa hayo marue rue huko ndan, abishe..’nikasema



Mama mjane akamuangalia shemeji yake, na shemeji yake akatikisa kichwa kama kukataa,…na mimi nikaona nizidi kutia mafuta;



‘Afande hili tatizo…lipo humu humu..huyu mtu wetu…anaweza kuyazuia haya yote na tukaendelea na kazi yetu…naona utusaidie kwa hilo…’nikasema na mpelelezi akawa kimia tu…na hapo Dalali akasema;



‘Unajua …wewe mtu unataka kuleta mambo mengine hapa..’akasema Dalali



‘Sileti mambo mengine, ila nina uhakika na ninachokisema..wewe dalali, ondoa haya matatizo kwa familia ya ndugu yako…na kama huwezi basi wewe na sisi tutaongozana hadi huko kwa mtaalamu wako….’nikasema  na kumuonyeshea Dalali kidole.



‘Unataka kusema nini…’akasema Dalali sasa akionyesha uso wa kutahayari



‘Hapana,… nyie msisumbuke tena, mimi nipo tayari niache kila kitu, wafanye watakavyo, kama ni nyumba wanataka waache wachukue…nawaombeni mnielewe hivyo, na mimi nimeshaamua hili, siwezi kurudi nyuma tena…’akasema  huyo mama



Mama mjane sasa akawa anatembea keshafika mlangoni, ….na kwa jinsi ilivyo ni nani atamzuia, nikamgeukia mpelelezi, kuona atafanya nini, nikamuona mpelelezi akigeuka kumuangalia Dalali…



Dalali, alikuwa kimia, sasa ni kama vile hajali.



‘Dalali..mzuie shemeji yako asiondoke, …la sivyo, wewe nitaondoka nawe hadi kituoni na huko tutajua ni nini cha kukufanya…’akasema mpelelezi



‘Afande, unamuamini huyu mtu…’akasema Dalali



‘Nimeamua mimi mwenyewe jamani…’akasema mama mjane sasa akiwa mlangoni.



‘Shemu sawa…unataka kwenda kwangu au…?’ akauliza shemeji mtu



‘Sijasema naenda kwako..’akasema mama mjane



‘Dada…nisikiliza kwanza.., kama wataka kwenda utakwenda, lakini mimi nakuomba kidogo tu dada, ..kuna mswali tunahitajika kumuuliza  shemeji yako,  tunahitajia na wewe uwepo…’nikasema na hapo nikamfanya huyo mwanamama asimame



‘Huyu shemeji yako ndiye atatusaidia kulimalizia hili tatizo najua kama hutakuwepo, anaweza kuongea mambo ya kukuweka  wewe kuwa unajua kinachoendelea, muda mfupi tu, alishasema wewe ulishakubaliana na hilo deni…’nikasema



‘Maswali gani,..?’ akauliza mama mjane



‘Wewe subiria tu…utayasikia, ..na wewe hutaamini majibi yake….’nikasema



‘Kama ni yale yale ya mali ya marehemu au deni,..hapana hayo ndio yanahatarisha afya ya wanangu…hebu jiulizeni kama ingelikuwa ndio nyie, mtoto wenu anaumwa hivyo, mngelifanya nini….au kwa vile?’ mwanamama huyo akageuza kichwa, akituangalia kwa nyuma.



‘Hebu niambieni ukweli…., au kwa vile yapo kwa mwingine……hapana,mimi ni mama nina uchungu na wanangu,….siwezi , …mimi nimeamua kumuachia mungu , najua mume wangu kafa, yote ni kwa mapenzi ya mungu,na haya yanayotokea pia ni kwa mapenzi yake au sio…..’akasema kwa sauti ya huzuni



‘Mwacheni aende,mimi nitafuatilia kila kitu…shemeji mim nipo, nitapambana na hawa watu, ni kweli kwa hali kama hii, naona wewe ukakae na watoto huko, au ikiwezekana kwanini usiende nyumbani kwangu….’akasema Dalali.

‘Nyumbani kwako,….hunitakii mema, unajua mke wako alivyo dhidi yangu…..’akanyamaza

‘Mke wangu…hana maneno yale yalishakwisha..sikiliza wewe fanya hivyo….nenda kwangu, haya mengine niachie mimi…’akasema Dalali

‘Dalali kwahiyo wewe unamshikiza aondoke, ina maana hukutulewa, au unamdharau afande…?’ nikasema na Dalali hapo akagwaya, halafu akasema

‘Sijamdharau afande, lakini tuangalia na hali ya hao watu, mimi namuunga mkono shemeji, ili kuondoka hayo mateso kwa mtoto…’akasema

‘Mateso gani..inavyoonekana ni kuwa unayafahamu hayo mateso…’akasema mpelelezi sasa kwa sauti ya kuwa yupo kazini.

‘Afande, mimi nijuavyo ni vile nilivyoagizwa sio zaidi ya hayo…’akasema Dalali

‘Sasa hivi umeagizwa shemeji yako aondoke humu au..?’ akauliza afande

‘Hapana huo ni uamuzi wake tu…’akasema

‘Sasa nataka asiondoke, kwa amri ya niliyopewa na wakubwa zangu, huyu
mwanamama akabakia humu ndani na lolote likitokea wewe utawajibika…’akasema mpelelezi.

‘Mimi sijasema aondoke..mbona hamunielewi..’akasema Dalali

‘Dada umesikia,..tafadhali…’nikasema
‘Kuna maswali ya msingi, ambayo shemeji yako anatakiwa ayajibu na uwepo wako utasaidia sana… na tukiyamaliza hayo..hatua zinazofuata mtakuwa pamoja naye kufuatilia, na kwa taarifa yako,…’nikasema na simu yangu ikawa inatoa mlio kuashiria kuwa ujumbe umeingia

Nikaisogelea pale mezani, nikaigusa kidogo, ili nione ni ujumbe gani, na Dalali akawa ananiangalia kwa makini, nikaona kuna ujumbe umeingia nikabofya kuufungua, ..sikuichukua ile simu pale mezani

‘Ok…sasa mambo yapo shwari…’nikasema

‘Unamaana gani kusema hivyo …’akaniuliza Dalali..na sikumjibu Dalali, mimi  nikamgeukia shemeji yake na kusema;

‘Kuna  hatua mbali mbali zimeshaanza kuchukuliwa,…kwa ajili ya usalama wa mtoto na wewe mwenyewe, haya ya humu ndani, huyu..shemeji yako ndiye atayaondoa yeye mwenyewe…’nikasema

Dalali akaniangalia kwa uso wa hasira na kusema;

‘Kwanini unasema hivyo…?’ akauliza

‘Unajua ni kwanini nasema hivyo…umewezaje kumtibia mtoto ambaye mlimchukua ndondocha…na mama yake ambaye mlimfanya hivyo hivyo…mimi sio mtaalamu wa mambo hayo, lakini nilishawahi kuyafanyia utafiti huo, wewe unajua na wewe unaweza kuyaondoa…’nikasema

 Dalali, akawa, kavimba..kiukweli nilikuwa nasema tu.

‘Kiukwenu umeshanichafua…’akasema Dalali,na sikutaka kubishana naye, mimi nikamwambia shemeji yake.

‘Dada ujue sasa hivi, haya maswala sio kati yako na ….hao watu, sasa ni maswala kati ya serikali inayotaka  kulinda raia zake, na hao wanaohusika,…ndio maana huyu mtu wa usalama yupo hapa…sasa hiyo mizimu na ije …ipambane na serikali…..’nikasema na huyo mpelelezi akaitikisa kichwa kukubali.

‘Lakini hamjaelewa,…tatizo ni deni…kwanini hamtafuti njia ya kulilipa..kama serikali ina nia nzuri na raia zake, basi,..isaidie kulilipa hilo deni…narudia tena tatizo ni hilo deni, mnaelewa hapo, sasa mengine yote hayatasaidia kitu , hata kama serikali ikiingilia kati…’akasema Dalali

‘Deni lipo sawa, linatakiwa lilipwe, hilo halina ubishi, lakini je deni hilo ni stahiki ya marehemu…hilo ndio tatizo, umenielewa bwana Dalali..,…je ni kweli kuwa deni hilo alichukua kaka yako, hayo ndio maswali tunataka kuyauliza kwa namna yake,…vinginevyo, nahisi kuna namna…’nikasema

‘Sasa ndio hayo maswali unataka kuniuliza mimi, ..mimi nitajuaje majibu yake…’akasema Dalali.

‘Kwahiyo unaogopa sasa…’nikasema

‘Sijasema nimeogopa…’akasema

‘Kama huogopi kweli, basi ngoja shemeji ayasikie majibu yake kutoka mdomoni kwako, na yeye akuthibishe…labda una mashaka kuwa kuna mengi tuyafahamu dhidi yako…na shemeji akiwa yupo hapa unaona aibu eeh…’nikasema

‘Maswali gani kati yangu na shemeji..?’ akauliza kwa sauti ya hasira

‘Utayajua tu…sasa ili uwe sahihi, kuwa huhusiki…mtulize shemeji asiondoke, na wewe uulizwe ujibu, kwa usahihi wake…’nikasema

‘Sawa, wewe si unataka kupambana na mimi, hamna shida,..shemeji rudi, …maana tunapoteza muda bure, usiwe na shaka, niachie mimi hawa watu……’ Dalali akasema kwa kujiamini,  mimi sikumjali nikamwambia huyo shemeji yake;

‘Huyu mpelelezi anayechunguza kuhusu kifo cha mumeo,..hilo ni swala jingine, yeye hakuja kukuuliza wewe chochote,..yupo mwingine ambaye anahusikana na kesi hii ya deni, yupo huko anafuatilia jambo, pindi tu anaweza kuja muonane naye, sasa ukiondoka tutakuwa tumekiuka maagizo….’nikasema

‘Shemeji rudi , ukae, mimi siogopi kitu, hata akija nani, mimi nina jiamini, sijafanya kosa,..nipo sahihi, ninachokifanya ni kutetea, maagizo, ni kutetea kaka yangu asiteseke huko alipo, na huyu mtu, anataka kujionyesha anafahamu sana, ngoja tumuone, haya uliza maswali yako wewe..…’akasema

‘Dalali, ujue kuanzia sasa upo peke yako…’nikasema na hapo akanitupia jicho, halafu akasema

‘Nilikuwa na nani mpaka useme nipo peke yangu…’akasema hivyo, kama anauliza

‘Sasa sikiliza nikupatia angalizo kidogo, wenzako wote wameshakiri ukweli..na mzigo wote wa lawama wamekutupia wewe…’nikasema

‘Wenzangu akina nani…?’ akaniuliza akiwa kakunja uso. Na mara simu
yangu ikaita, nikapokea na kuanza kusikiliza, nilipomaliza nikasema;

‘Usijali…ukweli wote sasa utabainika, …na haki itatendeka,…’nikasema na wakati huo mama mjane bado kasimama, hakubali kurudisha vitu vyake ndani, nikasema;

‘Dada ukweli sasa umeshabainika, …iliyobakia ni kukusanya ushahidi tu, mimi nawaahidi nyote mtakuja kulifurahia hilo…’nikasema

Mdada huyo akawa anatikisa kichwa kama kukatakaa….na shemeji akaonyesha ishara ya kama anasema unaona…haina haja..tunapoteza muda tu..kitu kama hicho, ..lakini mimi nikampuuza na kusema;

‘Je huniamini dada yangu..?’ nikauliza na mara mama mjane akageuka na kwenda kuweka mizigo yake karibu na mlango wa kuingilia huko chumbani kwake, na Dalali sasa akaonekana kama ana mashaka, anashika simu, kama anataka kubonyeza namba lakini anasita

‘Mimi nikimalizana na Dalali, itakuwa zamu ya mpelelezi naye ana mambo yake na mtu wa kuulizwa hayo yote ni wewe Dalali..na shemeji anahitajika hapa kama shahidi, je shemeji hutaji kufahamu ukweli wa kifo cha mumeo...?’ nikamuuliza

‘Mume wangu alishafariki vyovyote itakavyokuwa sizani kama itanisaidia mimi, nijuavyo ajali haina kinga..’akasema

‘Inaweza ikawa ajali yenye sababu..’nikasema na Dalali akanitupia jicho, lakini hakusema kitu, na hapo nikamgeukia mpelelezi

‘Naona tunaweza kuendelea au unasemaje…?’ nikauliza na mpelelezi akawa anaangalia saa yake.

‘Sawa…ila ni muhimu hili jambo limalizwe hii leo, na sitaki kupotezeana muda, kama unasema ukweli nataka ukweli uwe bayana,..unasikia,? akasema mpelelezi

‘Haina shida…’nikasema na ndio nikamgeukia mdada, na kusema;

‘Kuna vyakula…vimeingizwa vipo jikoni, kama unaweza kuendelea kutayarisha chochote, au….’nikasema na Dalali akasema

‘Naogopa hata kuingia huko jikoni…’akasema mama mjane

‘Hakuna kitu…kwa hivi hutaona kitu chochote tena, na kuhakikishia hilo…au sio Dalali, mbona unaogopa kusoma ujumbe kwenye simu yako…’nikasema na Dalali akaniangalia kwa uso uliotahayari, na mara akachukua simu yake na kuanza kusoma ujumbe;

NB: Ujumbe huo unasemaje
WAZO LA LEO:

No comments :