Mpelelezi akasimama, na kutembea hadi pale nilipokuwa nimesimama,
akaja na kuniangalia usoni….aliniangalia kwa muda bila kusema neno, halafu
akatikisa kichwa kama kukubaliana na mimi, halafu akasema;
‘Bado,..bado… una makosa…lakini sitaki upoteze muda kwa kujitetea,
nataka uonyeshe kuwa kweli hilo deni sio
sahihi…si umesema hilo deni sio sahihi, eeh..nataka nione hilo…vinginevyo,
unajua ni nini kitakachotokea…’akasema
‘Kwahiyo unaniweka rehani kwa kufanya kazi yako ili niwe huru kwa
makosa uliyonibandikia…?’ nikauliza
‘Mimi nafanya kazi yangu….na mkosaji ni mkosaji, haijalishi atajiteteaje, kama kafanya kosa, mimi kwa
mujibu wa sheria ambazo ndizo tunazisimamia ni lazima tumuhukumu kwa kosa lake,…unasikia,
..makosa yako yapo wazi, …’akawa anaongea kwa sauti ndogo, kama vile hataki
Dalali asikie.
‘Sawa…ila mimi nilitaka nikuonyeshe ukweli kuwa mimi sijafika hapa
kuisumbua hii famili, kama ilivyotamkwa,…hii familia inahitajia msaada mkubwa
sana,..bila msaada wetu haki yao itapotea na wenye nia ya kudhulumu
watafanikiwa,…je tutakuja kusema nini mbele ya mungu…’nikasema na Mpelelezi,
akatikisa kichwa, halafu akageuka kumuangalia Dalali…
‘Dalali, mimi ninataka ukweli kutoka kwako…, ukweli ambao utasaidia
haki iweze kutendeka,…nimewasikiliza kwa makini sana,…siwezi kusema una makosa,
hapana, mimi sijaona kosa lako….lakini bado nahisi kuna ukweli umeuficha….’akasema
‘Afande kama kuna ukweli nimeufucha, basi anibainishie hilo…mimi
naeleza yake ninayoyafahamu mimi, sijaficha kitu…sasa labda kama kuna jambo
linahitajika na mimi sijalifahamu…’akasema
Mpelelezi, akatembea na kurudi kukaa, huku akisema;
‘Dalali,..hebu kwanza nikuulize kitu, je una uhakika, ulichokisema,
kuwa wewe hujui lolote kuhusiana na kumbukumbu zilizopotea ndani ya hiyo
nyumba, kumbukumbu za kibenki ni sahihi…?’ mpelelezi akauliza
Dalali sasa akabakia kuonyesha uso wa kushangaa, na akatulia kidogo
bila kusema kitu, baadae akasema;
‘Afande ulitaka mimi niseme nini labda, maana mimi nimeongea ukweli
ulivyo, sasa nisemeje, kuwa nafahamu zilipo, kuwa …siwezi kudanganya afande,
hiyo sio fani yangu, mimi nafahamu ukweli ndio kila kitu…sasa niambie wewe
nimekosea wapi hapo…?’ akauliza
‘Ngoja niendelee kuwasikiliza,..au nduguyangu unasemaje, sib ado unaendelea
naye..ila usipoteze muda kutaka kujitetea, unasikia, …’akasema mpelelezi akiniangalia
‘Afande…mimi sio kwamba nawaingilia kazi zenu, ila kwa ushauri
wangu, kuliko kupoteza muda na hayo maswali, kwanini tusiende benki..au muende
benki, mkaongee na wahusika wa hilo deni..na kama kuna kumbukumbu
zimepotea,basi zitapatikana huko..mnaonaje huo ushauri wangu….?’ Akasema Dalali.
‘Unasemaje muuliza maswali, ni ushauri mnzuri, lakini…mimi siye
ninayekuuliza maswali hayo, nataka huyu mtu amalizane nawe, ili asije
kuniandika kuwa nimemuingilia kazi zake,..je ndugu mumemalizana naye…?’ akasema
Afande
‘Hata shemeji anaufahamu huo ukweli, tatizo bado hajaamuka, yeye
angelinisaidi kwa hilo, hata yeye keshachoka na haya mambo, tunataka nini, mali…hapana,
hatuwezi kuumiza mtoto kwasababu ya mali tu…’akasema Dalali.
‘Shemeji yako anaufahamu ukweli upi, hebu tuambie…?’akasema
mpelelezi.
‘Nimesema hivi,…kuhusu kutokuonekana kwa hizo kumbukumbu,…na…na
kuhusu deni lenyewe,…shemeji hata yeye anaufahamu huo ukweli….’akasema
‘Wakati mnatafuta hizo kumbukumbu, awali kabisa….shemeji yako
alikuwepo…?’ akaulizwa
‘Ndio…unajua…mimi nilifahamu hilo deni kabla…na nikafuatilia benki
kuhakiki,..benki wakanionyesha hizo kumbukumbu…nilishikwa na mshangao, lakini
kipindi hicho nisingeliweza kumuambia shemeji kutokana na hali yake…’akatulia
‘Kwa bahati nzuri, shemeji akapona…akawa na nafuu…lakini bado tuliambiwa
tusimsumbue na vitu vya kumshinikiza …akapatwa na presha…natumai hili
mnalielewa…..’akasema
‘Basi nilipoona sasa shemeji ananafuu ya kuelewa, nikaanza
kumuulizia kuhusu hilo deni..kiukweli alishtuka sana, mpaka nikajuta kwanini
nilimuuliza…akakataa katakata, hakutaka hata kusikiliza zaidi…na hilo
likamfanya hata apone haraka, ili afuatilie na yeye….’akasema
‘Basi….baada ya hapo ndio tukakubaliana twende mahakamani…tukampata
wakili, akasema atutusaidia..na hapo ndio ikawa kazi ya kutafuta ushahidi,…kumbukumbu,
ndio tukagundua kuw hakuna kumbukumbu yoyote ya kibenki…’akasema.
‘Ina maana wakati nyie mnatayarisha mirathi…wakati wewe unapewa
jukumu na kuisimamia hiyo familia, hamkutaka kuingia ndani na kukagua, kutafuta
kama kuna lolote, madeni, nk…hamkulifanya hilo…?’ akaulizwa
‘Tulifanya…tuliingia na wazee…maana nisingeliingia peke yangu,…na ni
kwa vile mimi nafahamu sana mambo mengi
ya kaka, nikaambiwa mimi ndio nilibeba dhamana hiyo, lakini hatukuweza
kulifungua hilo kabati…’akasema
‘Kwanini…?’ akauliza
‘Hakukuwa na ufungua wake…hatukuupata,…tumekuja kuupata baada ya
shemeji kupata nafuu, na yeye alifanya kubahatisha tu, maana aliutafuta sana,
kumbe kulikuwa na akiba za fungua, kuna fungua nyingi zipo pamoja, ndio humo
tupata ufunguo wake..hata shemeji hakuwa na ufahamu nao…’akasema
‘Na hamukuweza kuona hata nakala moja ya kumbukumbu za benki…?’
nikauliza
‘Hatukuona kabisa..tukatafuta sasa pamoja na shemeji, kila mahali
ambapo tunahisi tunaweza kupata …hatukuweza kupata…’akasema.
‘Sasa kwa mantiki hiyo, hata wewe huoni kuwa kuna tatizo hapo,
kwanini kumbukumbu hizo zipotee, …?’ akauliza mpelelezi.
‘Ni kweli inatia shaka…lakini benki wana hizo kumbukumbu,…tukaona
isiwe shida.. tutazipta tu huko benki…’akasema
‘Mlizipata…?’ akaulizwa
‘Ndio, kiasi tu cha ushahidi…’akasema
Mpelelezi akanitizama mimi, na mimi sikutaka kumuingilia hapo,
nikawa kimia tu, na Dalali akasema;
‘Tatizo kubwa afande, ni hayo yaliyokuja kujitokeza, ni mambo ambayo
wewe huyaamini ..lakini yapo, …huko kuteseka kwa mtoto,…sisi kama wazazi
tukaona haina haja, maana mtoto anateseka afande…’akasema
‘Kwa vipi…?’ akauliza afande
‘Muulize hata huyu mwenzako hapa, aliona nini kwa macho yake…, jinsi
mtoto alivyokuwa, je ni jinsi gani ya kufanya hayo yasitokee,…mtaweza kulizuia
hilo, maana sisi tumeshindwa, ndio maana tukaona tuache tu, hata mama wa mtoto
akasema, yeye sasa anamuachia mungu, maana ni kwa mapenzi yake, eeh..’akasema
‘Sasa kwanini mtoto ateseke kwa deni la benki…?’ akauliza mpelelezi
‘Nimeshasema ni kutoka na mzimu wa marehemu…unataka hilo deni
lilipwe…’akasema.
‘Ndio amtese mtoto wake mwenyewe…?’ akauliza afande.
‘Kama nilivyosema, ni mambo huwezi kuamini…unajua, ungelifika mapema
ungeliona hilo… sisi tulijua huyo mtoto ameshafariki…ndio huyu…akawapigia simu
polisi…’akasema
‘Lakini wewe uliona kuwa ni jambo la kawaida, mtoto kuteseka, mtoto
kupoteza fahamu hadi kuonekana kuwa kafariki…umesema hayo ni mambo ya kimzimu,
ya kifamilia, …si ndivyo ulivyosema…?’ akaulizwa
‘Ndivyo hivyo afande….’akasema
‘Mtoto ateseke hivyo,..hadi kuonekana kafariki….ndivyo mizimu
inataka hivyo, hao ni mizimu au ni mashetani wa kutesa watu…inatia shaka kidogo
hapo…’akasema mpelelezi
‘Unajua ..sio kwamba natetea, kwa hali ilivyo…labda wanafanya hivyo,
kwa vile wanatufahamu sisi wanadamu tulivyo..sizani kama wangelitoa taarifa tu,
sisi tungelikubali hilo, tungelipambana kweli…lakini hebu fikiria mtoto
anaumwa, anapoteza fahamu hadi tunahisi amekufa…ilinitisha sana, hata mwenzangu
hapa, aliona hilo, hebu muambie afande ilivyokuwa.…’akasema akiniashiria mimi.
‘Ulionaje hilo…kwani, kama ni kuumwa, si tatizo la hospitalini…?’
akauliza afande
‘Sisi tulijua kuwa mtoto ameshafariki…muulize yeye mwenyewe, ambaye
alichanganyikiwa, hata ingelikuwa wewe ungelifanya hivyo…’akasema
Afande akamtizama Dalali, na mimi nikaona hapo hapo inabidi nimalize
lile nililolianza, kabla ya kuingia kwenye tatizo lenyewe kiundani..nikasema
‘Afande, samahani kidogo…’nikasema
‘Ok endelea naye, nilikuwa naweka mambo sawa….’akasema mpelelezi.
‘Je ni nani alitamka kuwa mtoto amefariki…?’ nikamuuliza Dalali
‘Ni…lakini alionekana hivyo au sio, sema ukweli wako, wewe
ulimuonaje , mueleze afande ili aelewe hilo, usifiche kitu, ni vyema kila mtu
akaelewa, ili likitokea tatizo nisije kulumiwa mimi, kuwa sikusema…’akasema
‘Jibu swali ni nani wa kwanza kutamka kuwa mtoto amefariki..?’
nikamuuliza
‘Ni mimi…baada ya kuona dalili hizo…’akasema
‘Uliona dalili gani, mpaka ukafikia kusema mtoto amefariki..?’;
nikamuuliza
‘Mapigo ya moyo hayakuwepo kabia… mwili wote ulikuwa wa bariki, na
macho ya mtoto yalikuwa hivii…..’ akakodoa macho…’na..mimi mwenyewe nikayafunga
…kiukweli, alikuwa marehem…’akasema.
‘Kiukweli ukaona kuwa keshafaiki, halafu ukasemaje, kumuambia
shemeji ambaye wakati huo amezimia..?’ nikamuuliza
‘Ili bidi mimi niseme ukweli kuwa mtoto hatunaye tena…’akasema
‘Kwanini kama wewe ulifahamu kuwa shemeji hatakiwi kushtuliwa, wewe
ukakimbilia kumuambia hivyo, kuwa mtoto kafariki, kwa hali kama ile, si ndio
ulitaka kumuua kabisa,..ulitaka kutoa ujumbe gani kwa shemeji yako..?’
nikauliza
‘Lakini ilibidi nifanye hivyo, kuliko kusubiria, …na kiukweli hapo
hata mimi nilishachanganyikiwa,…sikumbuki nilisema nini…’akasema
‘Hukumbuki kweli?, kuwa ulisema nini… , ulichanganyikiwa kwa vile
uliona mtoto amefariki, si ndio hivyo unataka kusema…?’ nikauliza
‘Nilisema…anaonekana kama kafariki…’akasema
‘Sema kauli yako, uliyoitamka wakati ule, ulisemaje..?’ nikamuuliza
‘Nilisema…unajua nilichanganyikiwa..ndio huenda,…nilisema hivyo,
kuwa mtoto amefariki…’akasema.
‘Na nilipokukatalia kuwa mtoto hajafariki, wewe ulisemaje..?’
nikauliza
‘Haaah, unataka tuongee mpaka kesho, unapoteza muda bwana..kwani
hujui kilichotokea…afande huyu anaogopa kusema ukweli yeye mwenyewe, kwanini
unaogopa?’ akaniuliza kwa sauti ya kuonyesha namkera.
‘Unaona pale, …’nikasema nikinyosha kidole kwa askari polisi…
‘Yule ni nani, ni afande, pale anafanya nini…ananakili maelezo yako,…sasa
hivi sio porojo tu, maelezo yako yana umuhimu kwenye hili jambo..’nikasema
‘Sawa nimekuelewa….’akasema
‘Haya kama umenielewe,aa…na ukumbuke alipokuja hapa afande,
ulimuambia nini, kunihusu mimi, kuwa mimi nimekuja hapa na kuleta
usumbufu,..mimi ndiye nimepiga simu polisi, na kusababisha usumbufu kwa polisi
na gharama za kuleya gari la wagonjwa…,kwahiyo mimi ninatakiwa kuwajibika kwa
hilo..je nauliza tena,nilipokukatalia kuwa mtoto hajafa ulisemaje..?’ nikauliza
‘Nilikulaumu kuwa wewe hujui..mtu akifa anakuwaje…’akasema
‘Kwa hiyo wewe ulishathibitisha kuwa huyo mtoto amefariki,kweli si
kweli na ndio maana ukaniona mimi sijui kitu…si ndio hivyo…, je na mimi
nilifanya nini..?’ nikauliza
‘Ulimuendea mtoto, na wewe ukamkagua,..na ukaonekana kuwa na wewe
umeamini kuwa mtoto amefariki, na ndio hapo ukapiga simu, huko ulipopiga, kama
ni polisi, mimi sijui..nahisi ndio uliwapigia polisi maana nilisikia ukisema
afande , kitu kama hicho…..’akasema.
‘Je wewe uliamini hivyo, kuwa mtoto alikuwa kafa….?’ Nikauliza na
kabla hajajibu nikamuuliza
‘Je uliaminije kuwa kafa..ni baada ya kumkagua si ndio…, na kwa
uzoefu wako, uliamini hivyo kuwa mtoto hayupo duniani, ..na ndio maana ulitaka
kumuambia shemeji…na mimi nikakuzuia…’kabla hajajibu hilo swali, mpelelezi,
akasema;
‘Nimeshaelewa hapo, kwanini unaiuliza hivyo, nakufahamu sana ujanja
wako..lakini, …sizani kama hapa ni mahakamani, kuwa hakimu atakusikiliza na
kusema ulichofanya …sio kosa lako, ..mimi najua ni kosa au si kosa lako kwa
utaraibu wangu wa kikazi..wewe …eeh, uliza maswali mengine..’akasema mpelelezi.
‘Natumai hayo yameeleweka kihivyo…kuwa mimi sikufanya kosa kuwapigia
simu nyie mje na gari la wagonjwa maana hali ilikuwa mbaya, mtoto alionekana hana
uhai…sasa je..kama watu wazima tungelifanya nini..ukumbuke hapo tunazungumzia
mtu…kaonakena kafariki…’nikasema na kutulia kidogo.
‘Ndio maana nasema endeleeni, hilo nimeshaliweka kwenye kumbukumbu
zangu, ama kwa kosa lako, hilo sio mimi wa kuamua, unasikia, tukienda kituoni wewe
utajieleza, na kiukweli…sijui…..kibali chako kipo mashakani…’akasema
‘Mimi ..nilitaka kukupatia picha halisi ya kilichotokea humu ndani,..hadi
wewe kuambia uje hapa,… na zaidi nilitaka kukuonyesha kuwa hilo deni la
marehemu, sio kusudio la marehemu,..kupigwa mna da kwa nyumba hii, mimi ninaona
kuwa …, ni ukiukwaji wa haki za marehemu, swali ni je..ni kweli hilo deni
lilikuwa na marehemu…’nikasema kama nauliza.
‘Muulize mtu wako, au..unaniuliza mimi…?’ akaniuliza afande.
Na Dalali akadakia na kusema;
‘Kama sio deni la marehemu, kwanini aliweka sahihi yake…,..ushahidi huo
upo benki, ndio maana sikutaka mimi niongee hayo…na…kwanini aliweka dhamana ya
hii nyumba, yote hayo yapo wazi, kwanini hamjiulizi hayo na kwenda kuyamaliza
sehemu panapohusika,…’akasema Dalali kwa kulalamika.
‘Je wewe unajua ni kwanini..?’ nikamuuliza
‘Mimi sijui…ndio maana napata taabu, niambie wewe…’akasema
‘Kama wewe hujui, ni kwanini, ni kwanini uamini kuwa ni kweli…,
badala ya sio kweli..?’ nikamuuliza
‘Ni kutokana na ushahidi wa nyaraka walioutoa banki.ni kutokana
na…na..ushahidi wa mikataba, walioandikishana marehemu na benki, ni kutokana na
hukumu ya mahakamani..ndio maana mimi nikaona huenda ni kweli..…hayo yapo wazi
ndugu yangu, nitakataaje hayo,…’akasema
‘Je mikataba hiyo ipo, nyaraka hizo zipo, unazo nakala zake..?’
akauliza sasa huyo mpelelezi
‘Afande ndio hivyo vyote vipo…ndio maana mimi nasema hivi..hayo
maswali anayoniuliza mimi, sio sehemu yangu, hayo ni maswali ya kuwauliza watu
wa benki , ambao wana ushahidi wote huo…sasa ni kwanini anakuja kuniuliza mimi,…ni kama vile ananishuku mimi vibaya, ananitesa mimi kiakili… ‘ Akalalamika Dalali
‘Wewe usijali, mimi sasa nipo hapa, niyasikiliza hayo mambo yote, na
kama ni ujanja ujanja wake, wa kutaka kuuza magazeti, sijui na kupata wanachama
mitandaoni, mim nitamnasa hii leo…pili atawajibika kwa gharama zote
zilizojitokeza, na wewe una haki ya kumshitakia ukitaka..hatuwezi kuchukua gari
la wagonjwa hadi hapa wakati hakuna tatizo…’akasema mpelelezi.
‘Na pia awajibike kwa kumtesa mtoto na mama yake…maana akiendelea na
haya,..mimi nawaambia ukweli…..sijawajibika tena, sina uwezo huo…’akasema
Dalali, na alipoona mimi sisemi kitu akaongezea kwa kusema;
‘Najua huwezi kuamini hayo
afande… mpaka yakukute, hata mimi sikuwa nimeamini mambo haya….Kuna mambo ya
mizimu ya baba yake,…..aah,… eeh, lakini haina haja kukuambia, tutapoteza muda,
au sio yameshaeleweka…’akatulia
‘Unataka nikupe sababu kwanini nikusumbue wewe kama unavyodai kuwa
nawasumbua..?’ nikamuuliza na hapo akabakia kimia, na mimi nikaendelea kuongea,
‘Ni kwasababu, sisi tumeambiwa wewe ndiye uliyeachiwa majukumu yote
ya hii familia, kweli si kweli..?’ nikasema.
‘Ni kweli…mimi ndiye niliyeachiwa majukumu hayo…lakini ulitakiwa
unitafute tokea awali sio kuja moja kwa moja kwa hawa watu wasio na hatia,
umewatesa bure…’akasema.
‘Na pili ni kutokaa na majibu ya maswali yangu niliyokuuliza hapo awali,
ukasemaje, hujui, hujui…na kama hujui ni nani atajua, ..ukasema unahitajia
msaada, je sisi, tukujitolea kuutoa msaada huo tuna makosa…?’ nikauliza
‘Msaada wako unaumiza badala ya kusaidia, na nisema wazi, msimamo
wangu ni ule ule kuwa hilo deni lipo, na
ushahidi wote wanao watu wa benki, wao wana vidhibiti vyote, ukitaka zaidi
nenda ukaonane nao, ubishane nao, sio mimi,… tusipoteze muda hapa…’akasema
‘Wewe usijali kabisa kuhusu maswala ya benki, huko tutakwenda
kuhitimisha tu, mimi naona tatizo limeanzia kwako wewe, ambaye ulipewa dhamana
ya hii familia, na wewe ndiye ulikuwa karibu na marehemu, asipokuwepo yeye, wewe
unashika nafasi yake, ni kweli si kweli…?’ nikauliza
‘Sawa mimi ni mdhamini wa hii familia, lakini mimi sio mdhamini wa
hilo deni, hilo deni ni zaidi ya uwezo wangu, ndio maana ikafikia sehemu
nikaona bora tu, benki wafanya wanachokihitajia, maana ni haki yao,…tutawalipa
nini sisi, eeh, wewe hulioni hilo,sasa kama wewe una namna nyingine ya
kusaidia, tusaidie…’akasema, na mimi hapo nikatabasamu, nilichokitaka
nimekipata, nikasema;
‘Usijali, hata kama ni zaidi ya uwezo wako, lakini ukweli halisi wa hilo
deni ni upi, je marehem alikuwa kigeu geu, leo anasema hivi kesha anajipinga,..?’
nikamuuliza
‘Hayo unayasema wewe, mimi sijamsema marehemu vibaya…’akasema
‘Hujamsema vibaya…! Kumsingizia madeni sio vibaya…?’ nikauliza
‘Mimi sijamsingizia madeni bro..na sio mimi mwenye deni, uelewe
hilo, na ni wapi mimi nimemsingizia, hayo ni maswala ya benki, sio mimi, mimi
natimiza wajibu wangu tu…’akasema kwa sauti ya ukali kidogo.
‘Katika hulka na tabia za marehemu nimesikia wewe ukisema, marehemu
alikuwa mtu anayejiamini, anayependa kusema ukweli, na akisimamia kwenye ukweli
hageuki nyuma, au sio, na…watu walikuwa wakimuamini hivyo..je kwanini sasa
tusiendelee kumuamini hivyo…?’ nikamuuliza
‘Kwani ni nani kasema hamuamini hivyo, eeh,…?’ akaniuliza
‘Hamumuamini kwa vile mnasema yeye kajigeuka, yeye hakutaka deni,
lakini sasa kafariki hayupo, anapewa deni, tena deni lenye riba, nyie mnasema
yeye alichukua hilo deni, je ..hapo mnampinga, hamumpingi, kweli hapo
mnamuamini..kuwa alichokuwa akisema ni sahihi,…?’ nikamuuliza
‘Kwasababu ushahidi wa benk umelithibitisha hilo kuwa kweli hilo
deni lipo,…wewe ungelikuwepo mahakamani ungethibitishiwa hilo pia…, fikiria
mpaka hakimu anakubaliana na hilo, unafikiri yeye ni…. hajui kazi yake..usitake
kuikashafu mahakama..’akasema
‘Hakimu anatekeleza wajibu wake kutokana na nyie, ..walalamikaji
mlivyojenga hoja, na kuitetea, na kutokana na vielelezo mlivyoviwakilisha
kwake…lakini pia hakimu anategemea vielelezo vyenu,..mlilifahamu hilo, mkaenda
mahakamani bila vielelezo, bila mashahidi wenye kutoa kauli zenye mshiko kwa
hakimu,..mkitaka hilo litokee, kuwe na ushahidi wa kimahakama, kwa hali kama
hiyo…ulitegemea nini…na je kama hivyo, vielelezi viligushiwa,..?’ nikamuuliza
‘Ni nani aligushi sasa ni nani anaweza kugushi vielelezo vya benki,
wewe unawasingizia benki..una lako jembo,..una uhakika na unachokisema kweli
wewe…?’ akauliza
‘Nimekutolea hilo kama mfano, …maana nyie ndio walalamikaji, nyie
ndio mnaomtetea marehemu..je kama hamjajitetea vya kutosha, hamuwezi mkapata miujiza
kutoka kwa hakimu, ndio maana nasema tatizo limeanzia kwako, hukunielewa hapo…wewe.
Ndiye mwenye dhamana ya hii familia, kama hujaweza kuitetea vyema, ni lazima
…tuhisi hivyo,….na kwa kupitia wewe ndio tutaubaini huo ukweli halisi…’nikasema.
‘Kupitia kwangu!!! Kwa vipi…sielewi hapo……hahaha, utapoteza muda
wako bure…na utawatesa wanafamilia hawa bure, maana mimi sijuikitu…na..sijui nikueleze
vipi,..cha muhimu tuangalieni jinsi gani ya kulilipa hilo deni jamani, deni ni
deni, marehemu anapata taabuhuko alipo, jamani, hamna hata imani jamani…aah…’akasema
hivyo mwishoni kama kukata tamaa
Nikaona nimkatize, …kwa kuuliza;
‘Tutaangaliaje hivyo, ….tutalipaje deni ambali hatuna uhakika nalo,
je kama sio deni kweli la marahemu, huoni kuwa unawadhulumu hawa manusura,
mayatina na mjane,…huwafikirii na wao..?’ nikamuuliza.
‘Kwanini unasema hivyo, wakati uhakika, na ushahidi upo , zipo nyaraka
sahihi za benki,…hata mke wake, analifahamu hilo,..ndio maana hata yeye akaona
haina haja hata mahakamani, akashindwa kumtetea mumeo…’akasema
‘Una uhakika kuwa yeye, keshakubaliana na hilo deni kwa asilimia mia
moja…, kuwa kweli hilo deni ni la mumewe, ..?’ nikamuuliza
‘Ushahidi si kauona, yeye ni msomi, alipitia ushahidi wa nyaraka za
benki akaona kila kitu kipo sawa, ..na huko mahakamani, wakamusaidikishia hilo,
hakuwa na la kufanya..hebu sasa…nikuulize wewe ni nani anayemfahamu mumewe
zaidi ya mkewe, kwanini sasa mkewe akashindwa, kumtetea mumewe,…jibu ni wazi, kwasababu
vielelezo vyote vya hilo deni vipo, sasa ulitegemea yeye afanye nini…’akasema
‘Mkewe alilikubali hilo deni la mumewe kuwa ni sahihi…?’ akauliza
sasa mpelelezi
‘Hakuwezi kulikubali aawali,..hata mimi ni hivyo hivyo…ndio maana tukaenda
mahakamani, tukisaidiana naye,. Lakini huko mahakamani…tutajiteteaje hapo,…hebu
tusaidie na wewe afande…’akasema
‘Nakusikiliza wewe…’akasema afande
‘Kwa upande upande wangu nimeshatimiza wajibu wangu,…kuusema ukweli
wote, na kama kuna zaidi ni nyie mtuambie la kufanya..’akasema akimuangalia
mpelelezi.
‘Unasema mkewe marehemu..yeye..alikuja baadae kukubaliana na hilo
deni, ni kweli hivyo..?’ nikauliza hilo swali tena.
‘Sijasema hivyo, kuwa alikubaliana na hilo deni, moja kwa moja, kama
angelikubaliana na hilo deni, asigelisumbuka kwenda mahakamani..’akasema
‘Nauliza hivi, baada ya ushahidi huo, baada ya mizimu kutokea mkewe
akaja kukubaliana na hilo deni, si ndio hivyo…na hata kuja kukubali, kuwa sasa ni
bora hiyo nyumba ipigwe mnada, si ndivyo ulivyosema wewe, hebu tuweke wazi hapo..?’
nikauliza
‘Nikuweke wazi kwa vipi...?’ akauliza
‘Nataka ukweli, je mke wa marehemu alikubali kivipi, kuhusu hilo
deni..ukweli wa kauli yake…?’ nikauliza kumchanganya kichwa.
‘Hakuwa na jinsi..kama ilivyokuwa mimi…,ilibidi akubaliane na…na
ushahidi uliotolewa na kutokana na matukio yaliyokuja kutokea baadaei,..tutafanyaje
sasa….tuache mtoto ateseke…tuache..marehemu apate shida…ilibidi tukubaliane na hilo…’akasema
‘Ndio kauli yako hiyo,…kuwa wewe na yeye mlikuja mkakubaliana , kuwa
mkubali tu, yaishe, je akizindukana hapo
tukamuuliza,..akisema yeye kashindwa kwasababu tu ya mateso ya mtoto, lakini
moyoni bado hajakubaliana na hilo deni utsemaje…?’ nikamuuliza
‘Mimi sikuelewi…kwanini unanizungusha kwa maswali, nimekuambia hivi,
ilifikia sehemu akawa hana jinsi kwa
vile hana namna nyingine ya kujitetea,..deni lipo wazi…, ni deni sahihi
kisheria,..nyaraka zipo, unataka nini sasa, kwanini akatae hapo, na hayo ya
mtoto yamekuja baadae….’akasema
‘Kwahiyo akatamka kuwa yeye amekubali ..kuwa deni ni sahihi na
nyumba ipigwe mnada, si ndivyo ulivyosema…?’ nikauliza.
‘Sio lazima atamke hivyo, ….kivitendo, alikubaliana na hilo…hakuwa
na namna nyingine, ..yeye kama mama, kaona mtoto anateseka, kisa, ni ujumbe wa
kuthibitisha hilo, kuwa hilo deni lipo,..yeye angelifanya nini…unafahamu huruma
ya mama kwa mtoto wake…’akasema
‘Yah. Hapo sasa unakubali kuwa kakubaliana na hayo kwa vile mtoto
wake anateseka, anateswa, na hii ni kwa vile nyie mlilenga huko, mumutese mtoto
ili aje kukubaliana na matakwa yenu…’nikasema
‘Hivi unataka nikueleze vipi ili unielewe….eeh, mbona
unanilizimishia vibaya, …hebu tusubirie shemeji mwenyewe aamuke, aseme ukweli
wake, kuwa je hadi hatua hiyo hajakubaliana na huo ukweli…eeh,..maana akikana…akane
kwa ushahidi, ili tuweze kubatilisha huo ushahidi wa benki, pili…apambane na
hiyo mizmu mwenyewe, mimi sipo hapo…’akasema
‘Akubali kwa Vitisho..au sio…?’ nikauliza
‘Sio vitisho,kwani wewe hukuona, je mtoto alikuwaje,..mimi kama
mzazi nitafanya nini, kama ingelikuwa mtoto wako ungelifanya hivyo
hivyo…’akasema
‘Mama alikubali kwasababu mtoto wake anateswa, …na wanaomtesa
wanataka malengo yao yatimie…’nikasema.
‘Akina nani hao, wanaomtesa ili wapate nini,labda ungelisema basi
wanaofanya hivyo ni benki, si ndio wao wanadai deni lao…na je kweli , benki
wanaweza kufanya hivyo, kwanini wafanye kwa huyu mtu, wana madeni mengi tu….kwa
watu wengine…’akasema
‘Si ndio maana nasema kuacha benk…kuna watu wapo nyuma ya hili
jambo, maana kama ingelikuwa ni benki tu, mtoto asingeliteswa,..huo ni ushahidi
uliopo wazi…unadhihirisha kuwa sio benki wenye masilahi tu….na ni kweli benki
wanatimiza wajibu, lakini kuna mtu au watu wengine wanasubiria hilo ili matakwa
yao yatimie…’nikasema.
‘Mimi sijakuelewa hapo, ..maana hiyo pesa ikilipwa inakwenda wapi…?’
akaniuliza
‘Inakwenda benki…’nikasema
‘Sasa huyo mtu mwingine atapata nini…anapata faida gani..hebu
niambie wewe ndio maana nasema hoja yako haina mshiko…’akasema
‘Atapata nini…nitakuja kukuambia, atapata nini…ndio maana shinikizo
hilo, linakuja kwa nguvu zote,..’nikasema
‘Sema sasa hivi, atapata nini huyo mtu wakati pesa hiyo ni ya benki…’akasema
‘Hatua kwa hatua…mimi ndiye natakiwa kuuliza wewe maswali, ujibu
..unasikia, tumeishia hapo, wewe unadai shemeji yako kakubaliana na hilo deni,
..nataka kukuthibitishia kuwa shemeji yako hajakubaliana na hilo deni,…bali
kalazimishwa kukubali,…’nikasema
‘Kwanini alazimishwe..na nani…, mimi au…hiyo kauli ya kunihukumu,
siipendi, …afande ina maana tayari nimeshashukiwa kuwa mimi nipo nyuma ya hili
jambo…?’ akamuuliza mpelelezi
‘Sikiliza, nakuuliza tena…ni kwanini wewe unasema shemeji yako
amekubaliana na hilo deni,….?’ Nikauliza
‘Sasa kwa jibu la hilo swali lako, tuje kumuuliza shemeji,…kama
kweli atalipinga…’akasema
‘Kwa vile unajua umeshamuogopesha, mumeshamuegeshea mateso kwa mtoto
wake, kuwa akikataa mtoto wake ataanza kuumwa, si ndio hivyo..?’ nikauliza
‘Kwanini utake mimi nimjibie mtu maswali yake, ..bahati nzuri
shemeji yupo hapa, atazindukana tu, atausema ukweli wake…’akasema
‘Kuwa kweli kakubaliana na hiyo hoja kuwa ni kweli hilo deni ni la
mume wake..?’ nikauliza
‘Ndio kutokana na ushahid wa kibenki…na pili…’hapo akatulia
‘Kutokana na mizimu,..je shemeji yako anaamini hayo mambo, mpaka
akubaliane na mizimu yenu…?’ nikamuuliza
‘Kuamini, ni kutokana na hali halisi,…ni lazima aamini kama
mimi..mimi sijapenda kufananya hivyo, ni hali halisi…sasa subiria akiamua,
atayajibu hayo yeye mwenyewe, akikataa…haya,…’akatulia pale tulipohisi jambo…
‘Haya muamusheni sasa….’nikasema na hapo akacheka, kibenua mdomo,
halafu akasema;
‘Wewe huna hoja umeshaishiwa….shemeji alishakubali, ni wewe…’ kabla
hajamaliza mara….
‘Mimi si-si-jakubaliana na hiyo kauli yako…’ilikuwa sauti ngeni,
sauti ya kike, na sote tukageuka kuangalia kule sauti ilipotokea.
NB: Kidole kinauma
WAZO LA LEO: Tutafute mali kwa njia
za halali, tuutafute utajiri kwa njia za haki…, lakini sio kwa kutumia jasho la
mtu mwingine. Jasho la mtu mwingine ni ushahidi usiofutika, ulilidhulumu hilo,
ni deni, ni dhuluma, isiyofutika…, na ikifikia muda akanyosha mikono juu,
akamuomba mola wake, maombi yake, kilio chake, hakirudi nyumba, OGOPA DUWA YA
MWENYE KUDHULUMIWA, .
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment