'Tahamaki
shemeji anakuja kukamatwa...'alisema mama mjane
‘Kwa kosa
gani …?’ nikamuuliza na mara simu yangu ikawa inaingia ujumbe, na haikupita
muda, mtoto wa huyo mama naye akaanza kulia…
Tuendelee na kisa chetu
Baada ya kipindi cha kama mapumziko, hivi, mimi nasoma ujumbe kwenye simu, na mama mjane anahangaika na mtoto wake...baadae akawa kama huyupo tayari kuongea na mimi nikalazimisha tu kwa kusema;
'Unasema mlienda polisi....ulienda kusema nini huko...?' nikauliza na yeye akaanza kuelezea tena;
‘Rafiki yangu
mume wake ni polisi, kumbe aliongea na mume wake kuhusu tatizo langu, na mume wake, ndio akashauri mimi nilipeleke hilo swala polisi ili kufanyike upelelezi, na kama kuna udanganyifu kwenye hilo deni, ukweli utabainika
tu...kiukweli niliposikia hivyo nikaingiwa na matumaini mapya.
Ehe..ukasema shemeji akaja kukamatwa, ..ilikuwaje..?' nikauliza
‘Na kweli
mimi nilifanya hivyo….upelelezi ukaanza na siku kama ya pili yake, polisi
wakaja kumchukua shemeji, na bahati mbaya siku hiyo shemeji alikuwa hapa nyumbani…’akasema
‘Alikamatwa akiwa hapo kwako,...,
au aliitwa kituo cha polisi..?’ nikauliza
‘Askari
waliovalia kiraia, walifika hapa nyumbani, na kutoa vitambulisho vyao,
wakijieleza kuwa wao ni nani, na wanamuhitajia, shemeji waende naye kituo cha
polisi kwa mahojiano…shemeji akawauliza ana kosa gani, wakamuambia ni katika
kuisaidia polisi kutokana na tuhuma za deni la marehemu…’akatulia
Shemeji
akaniangalia mimi kwa macho ya kushangaa, maana , nilikuwa bado sijamuambia lolote
kuwa nimeenda polisi, na siku hiyo ndio nilipanga nije kumuambia …
‘Shemeji
ni nini kinachoendelea…?’ akaniuliza na polisi hawakumpa muda wa huo, wakaingilia kati na kusema;
‘Hayo
maswali na majibu yako utayapatia huko huko kituoni, usiwe na wasiwasi ..’wakasema.
Basi
shemeji kwa shingo upande akaongozana nao…na mimi nikaona sio jambo nzuri kukaa
kimia, nikampigia simu ndugu yake mmoja kumuelezea, ili kama kuna lolote, au likitokea lolote wao waweza
kusaidia.
‘Uliwapigia ndugu hao wa nini tena…?’ nikauliza
‘Niliona
ndio jambo nzuri, …mimi nisingeliweza kwenda huko, maana mtoto , huyu mkubwa
naye alikuwa akiumwa malaria…na hata kuja kwa shemeji hapo ilikuwa kunisaidia
apate dawa…’akasema
‘Ikawaje…?’
nikamuuliza
‘Waliniuliza
kakamatwa kwa kosa gani, nikawaambia ameitwa tu kutoa maelezo kuhusiana na deni
linalodaiwa kuwa ni la marehemu.
‘Hivi
shemeji, hayo si tulishayamaliza…?’ wakaniuliza na nikajieleza, lakini
ilionekana mimi ndiye nimemchongea ndugu yao kuitwa huko polisi..’akatulia
‘Sasa
aheri ingelikuwa ni kuhojiwa tu na kurudi,…hakuruhusiwa kuondoka huko kituoni
siku hiyo, na ndio ikaleta uhasama,…’akasema
‘Kwanini
sasa, …hakuruhusiwa…kuondoka siku hiyo…?’ nikauliza
‘Nasikia
alileta ubishi, hakutaka kutoa ushirikiano,…’akatulia kama anaogopa kuongea
zaidi au kuna jambo kaliona.
‘Ndugu
zake walisemaje….?’ Nikauliza akaitikia kwa kichwa halafu akasema;
‘Wao
waliendelea kunilaumu, kuwa chanzo cha haya yote ni mimi, najifanya sijui
lolote kuhusu hilo deni, wakati nilihusika kwenye matumizi…na huenda kaka yao,
yaani marehemu hakuniambia kwasababu ya tabia yangu mbaya..wakaongea sana,
sikutaka kujibishana nao kabisa, ila…’akatulai kidogo
‘Nilishindwa
kuvumilia walipoanza kuongea maneno mabaya… hata mimi sikupenda hiyo hali ya
shemeji kuitwa, kituo cha polis kujieleza, nilipendelea wamuhoji tu akiwa
nyumbani, lakini nisingeliweza kuingilia kazi zao..wao walisema ni taratibu za
kawaida tu..’akatulia
‘Ehe…’nikasema
hivyo tu
‘Mimi
nikawaambia hizo ni taratibu za kawaida za kipolisi, kuona kama wanaweza kupata
lolote, na mtu wa kumuuliza kuhusu hilo deni ni shemeji,..maana yeye ndiye
anajua zaidi,.’akatulia
‘Wao,
hawakunielewa, ndio wakaanza kuongea maneno mabaya ya kashfa, na hapo sikuweza
kuvumilia, ikabidi na mimi nianza kuongea vibaya,..ikawa sasa ni kujibizana
vibaya, ilifikia sehemu nikaongea hata yale ambayo sikupaswa kuongea…’akasema
‘Kama
yapi…?’ nikamuuliza
‘Kuwa shemeji
yangu alifanya vibaya, kama aligundua deni, asingeendelea kuliongeza, na
kwanini alinificha muda wote huo, ni lazima alikuwa akitumia deni hilo kwa
masilahi fulani….’akatulia kidogo
‘Na
huenda kuna ukweli ndani yake au sio,..ikawaje sasa..?’ nikauliza nikiangalia
saa
‘Kiukweli
kauli hii ilifika kwa shemeji, na hata alipoachiwa, alionekana kunikasirikia,
japokuwa alijitahidi kuficha hiyo hali, ..akaniambia, baada ya yeye kujitolea kwake kwa ajili ya
familia, hiyo fadhila kwake, na ya kuwa yeye hataacha kuwasaidia watoto kwa
vile ni watoto wao..ila mimi naonekana nina roho mbaya, sina shukurani….’akatulia
‘Wewe
ulisemaje..nikauliza
‘’Yaani
siku hiyo ndio niliwaona jinsi gani walivyokuwa wakinichukia, maana hata dada
zao walifika kwangu wakiwa na huyo shemeji, na kuanza kunibwatukia, wakiniambia
mimi ni mwanga, mchawi, eti huenda mimi ndiye nimechangia kaka yao kufa..sikufurahia
kauli hiyo, nikawafukuza ndani kwangu.
Wakaondoka
kweli, akabakia shemeji…yeye akawa muungwana kujaribu kunisihi kuwa
ninalolifanya sio sahihi, na kama nilipanga kwenda polisi ningelimfahamisha
mapema ili ajiandai kuwasaidia polisi, lakini polisi, wao wanafikia kumshuku vibaya…na
kuanza kumtesa.
‘Ni kweli
walimtesa..?’ nikauliza
‘Mimi
sijui…polisi walisema walimuhoji tu, na kutumia lugha ya vitisho kidogo…’akatulia
Basi
baada ya siku hiyo, ikawa sasa ni vita...hadi wazee wakaingilia kati,
kutusuluhisha, na huku polisi wakiendelea na uchunguzi wao, mara kwa mara
walifika kukutana na shemeji, na hata ndugu zake wengine, ikawa kama ni kero
kwao.
‘Basi
siku moja wakaja tena, shemeji na mawifi,…naona walijiandaa kwa shari, walianza
kuongea kwa busara kidogo, wale shemeji, lakini ilipofikia zamu ya mawifi, ndio
wakaharibu,…ilifikia hatua kutaka kupigana.
‘Kwanini
mpigane…?’ nikauliza
‘Kwa nini
waniambie mimi ni mchawi, eti nimloge mume wangu ili iweje sasa, hebu fikiria
hata wewe hilo linaingia akilini kweli, ..kiukweli mimi nilijitahidi kuvumilia,
wakati wanaongea, ikafikia muda nikashindwa, na nilipoanza kuongea, niliongea
kweli….’akasema
‘Lakini
hayo yote yalikuwa kwenye harakati za polisi kufuatilia na kutafuta ukweli au sio, na swala hilo la kutafuta ni nani
alifanya hujuma, kama kweli ipo, au sio….lilikuwa bado halijafika mahakamani au
sio,…kuacha ile ya mwanzo ya kutafuta ukweli wa deni kama ni halali au la?’
nikamuuliza
‘Ndio….ilikuwa
hivyo…’akasema
‘Ehe
…ikawaje sasa?’ nikamuulza
‘Baadaye tukasuluhishwa,
yakaisha kwa siku hiyo, lakini chuki ndani ya mioyo ilikuwa haimithilikia, hasa
kwa mawifi dhidi yangu, hata tukikutana njiani hawanisalimii, nikawasalimia,
wanaweza wakaitikia au wakakaa kimia tu…’akatulia
‘Wazee
wakaliona hilo, ikabidi tuitwe kikao, ..hutaamini, siku hiyo ya kikao,
utafikiri sio wao tena, wanajifanya watu wema kwangu, wakasema kama ninaona
wamenikosea, basi wanomba msamaha, kwani wamefanya hivyo kwa uchungu wa ndugu
yao, ..wamefiwa na bado wanaandamwa na mambo ambayo hawayayajui,…’akatulia
‘Nikawaambia
mimi sina tatizo, maana mimi ndiye muathirika wa hayo yote…kama ni huzuni, hata
mimi ninayo, na kinachoniuma ni kuwa mume wangu anabambikiwa deni, mimi
sikubaliani na hilo deni, ndio maana natafuta ukweli…
‘Kwahiyo
wewe unaumia kwa vile hilo deni linagusa masilahi yako,..lakini wewe hujali
masilahi ya ndugu yetu ..kwasababu kama deni lipo, yeye huko atakuwa na wakati
mgumu, kwanini mimi sitaki deni lilipwe ili roho ya ndugu yao iwe salama….wakasema
hivyo…’akatulia
‘Mhh,
ikawaje..?’ nikauliza
‘Mimi
sikuwa na kinyongo nao zaidi , ilimradi wamejiona wamekosa, basi nikawaambia
yamekwisha,…tumalizane kwa amani, mara mmoja wapo akasema;
‘Ili
tuone kama kweli umetusamahe, basi achana na mambo hayo ya polisi, maana
yanaleta picha mbaya kwenye familia yetu inaonekana kama sisi tumefanya hayo
makosa, wakati sisi hatujui hata chanzo cha hilo deni,..ni vyema tuachane na
polisi, na,..hayo mambo tuyamalize kinyumbani, ndivyo kaka yetu alivyokuwa
kifanya, hakutaka mambo ya kesi kesi, hasa za polisi…’akasema hivyo.
‘Ukawajibuje..?’
nikauliza, maana huyu mama akiongea jambo, usipomuuliza swali atakaa kimia tu.
‘Mimi nikawaambia hata tukiliongelea nyumbani hilo
deni atalipa nani, ni lazima tutafute ukweli wa hilo deni, kwani huenda kuna
mtu mwingine anatuchezea akili mbali na familia yetu, wao hawalioni hilo…na
watu wazuri wa kutusaidia ni polisi…, ‘akatulia
‘Sasa walipoona
sikubaliani na hilo, wakatoka nje, wakateta, baadae wakarudi mmoja wapo
akauliza;
‘Ina
maana shemeji, umeamua iwe hivyo, ndio mwisho wako…?’ akauliza
‘Mimi
naona tuwaache polisi wamalize kazi yao kwanza..’nikasema
‘Unajua
ndugu yetu, mtu anayekusaidia ndiye wanamshuku vibaya, ina maana kweli wewe
humuamini shemeji yako..?’ wakaniuliza
‘Mimi
siwezi kuwaingilia polisi,..sizani kama wanamshuku, wanaweza kumshuku yoyote,
mbona hata mimi wanafikia kunihoji..mbona hilo hamsemi…’nikasema
Kiukweli,
siku hiyo, hatukuelewama…wakaondoka sasa wakitoa lugha za vitisho …’akatulia
‘Walisemaje..?’
niakuliza
‘Kwanza
walianza kusema sina fadhila, sina shukurani, sijali jinsi ndugu yao
alivyojitolea kwa ajili yangu, basi kama ni hivyo na wao watafanya hicho
ninachokitaka….na watahakikisha,najuta, nitakiona cha mtema kuni…’akasema
‘Ni nani
alikuwa akiongea hayo…?’
‘Ni hao
ndugu zake shemeji hasa mawifi…walikuwa wakiongea tu, kila mmoja na lake, uzuri
wake pale walikuwepo wazee, na mmojawapo ni mzee Mtupe, ndiye aliyewasihi sana,
lakini mhh,…’akasema
‘Ikawaje…?’
nikauliza nilipoona katulia tu
‘Kiukweli
kikao cha kusuluhishwa siku hiyo hakikuisha vyema, ikabid kiahirishwe hadi siku
nyingine huku nikiambiwa nikae nifikiria …nikauliza nifikirie nini, nikaambiwa
hilo swala la kupelekana polisi, sio jambo jema, kwanini namsumbua huyo shemeji, wakati hana
kosa…’
Mimi
nikawaambia;
‘Lakini
sio mimi niliyemsumbua shemeji, hata yeye analifahamu hilo, na…ni utaratibu tu
wa polis katika kutafuta ukweli, hajaambiwa ana kosa…’nikawaambia hivyo, lakini
hawakukubali, wao wakataka nifute hiyo kesi ya malalamiko, ya kudai kuwa deni
sio halali, na wao watasaidia katika kuutafuta ukweli, …’akatulia
‘Ukakubali…?’
nikamuuliza
‘Sikukubali..unajua
walishanifanya na mimi niwe mkali,..niliona kama wanataka kunikalia tu, na kama
polisi walishaanza kazi yao mimi ningeliwezaje kuwasimamisha, mimi niliona ni
bora wamalize uchunguzi, ili hata na mimi nijirizishe..kwa kuendelea kuwa na
msimamo huo, ikawa nimejenga uhasama na
familia hiyo,…na ..sijui ni kwanini,..huenda ni bahati mbaya tu au la…’akatulia
‘Kwa
vipi…?’ nikauliza
‘Baadaye,..ni
hata wiki haikupita, mara mtoto wangu huyu mdogo akaanza kuumwa, kweli
kweli..kila ikifika muda wa kwenda polisi kufuatilia, mtoto anazidiwa, maana
mimi nilishaamua baada ya ushahidi huo wa polisi kukamilika tunakwenda moja kwa
moja, mahakamani, ..’akasema
‘Kwani hao
polisi walikuambia wamegundua nini…?’ nikauliza
‘Wao,…hadi
muda huo, walikuwa wamegundua kuwa kweli
hilo deni lipo…japokuwa, ya-we-ze-ka-na sioo halali ya marehemu,…sasa kama sio
halali , ni halali kwa nani, na ni nani kafanya hivyo, kwa vipi, ..ndicho
walikuwa wakiendelea kutafuta,…kwa tarifa hiyo, ikazidi kuwachanganya hao
wanandugu, kwa vile ndugu yao ndiye msimaizi, wakahisi vibaya..lakini mimi
mpaka hapo sikuwa na shaka na shemeji yangu kabisa kuwa yeye anahusika…’akatulia
kidogo.
‘Kwahiyo hadi hapo aliyekuwa akishukiwa ni
shemeji yako au sio, kutokana na uchunguzi wao, au yeye alikuwa akiandamwa na
polisi katika kuisaidia tu, na kilichomfanya awekwe ndani ni kutokana na ubishi
wake, au sio…?’ nikasema kwa kuuliza
‘Ndio
hivyo, wala yeye hakuwa mshukiwa, alitakiwa tu kutoa maelezo, na kutoa
ushirikiano tu, na wakati mwingine walienda naye hadi benki, sijui huko
waliongea nini, maana sikuambiwa…’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine
akasema
‘Kiukweli
hata mimi sikutaka ifikie hapo…maana sasa anayesumbuliwa ni shemeji , mtu
aliyenisaidia sana,..’akatulia
‘Hata
hivyo mimi ningelifanya nini, maana wanangu ndio wanaumia, na sasa nyumba
inauzwa, inapigwa mnada,..na yote haya ni baada ya mimi kusema tuyamalize
kinyumbani,nina imani kama ningewaachia polisi waendelee, basi,…huenda
wangeligudnua jambo…’akatulia
‘Ina
maana uliwazuia…kuendelea na uchunguzi wao…?’ nikauliza
‘Mimi
ndio nilishindwa kutoa ushirikiano, kila nikiitwa kituoni, katika mahojiano
sifiki,…’akasema
‘Kwanini…?’
nikauliza
‘Watoto..hasa
huyu mdogo, ndio alianza kuumwa kweli kweli…’akasema
‘Polisi
walifikia wapi, au hukuwahi hata kuongea nao…?’ nikamuuliza
‘Unajua
kichonipa nguvu kipindi kile ni pale polisi waliposema kuwa kuna uwezekano kabisa
hilo sio halai ya marehemu…wao walikuwa sasa wanahojiana na benki…kuona kuna
kitu gani kinachoendelea huko ndani kwao,…, ila kiukweli deni hilo lipo, halina
ubishi,..na ndio wakanishauri nitafute wakili mnzuri wa kusimamia hiyo kesi, huku
wako wakiendelea na uchunguzi , hata hivyo, sikuwa na pesa, na mtoto akawa na
hali mbaya sana…’akasema na kutulia kidogo
‘Baada ya
mtoto kuzidiwa, ndio mmoja wapo wa hao ndugu akaja kuniuliza;
‘Hivi
wewe una ubinadamu kweli, hivi nyumba ina thamani gani zaidi ya mtoto
wako…’akasema
‘Nikamwambia,
ukisema hivyo ina maana nyie ndio mnamloga mtoto wangu ili nikubaliana na
matakwa yenu…’nikamwambia ..haaa, akacharuka na yeye, eti nimemwambia familia
yao ni wachawi, ikazuka kesi nyingine ya mimi kuishuku familia ya mume wangu
uchawi,..yaani ilikuwa ni taabu, huku mtoto anaumwa, huku wanafamilia
wananisakama....’akatulia
‘Baada ya
hapo ikawaje..?’ nikamuuliza
‘Cha
ajabu wao wanashinikiza kama denii lipo kwanini nisiache tu nyumba ipigwe mnada
ili hilo deni lilipwe na pesa itakayobakia tujenge nyumba nyingine ,eti kwa
kufanya hivyo, kwenda mahakamani namshitaki marehemu aliyekopa hilo deni, na
zaidi pia nawafanya ndugu zake wateseka kwa kitu ambacho hakiwahusu, na
marehemu huko alipo, anawajibika kwa hilo deni, …..’akasema
‘Hakiwahusu
tena…?!’ kwa mshangao
‘Ndio
kauli yao hiyo…’akasema
‘Unasema
mtoto akaanza kuumwa, … hilo la kuumwa kwa mtoto wako linahusikanaje na hiyo
kesi, kwa mtizamo wako wewe, unahisi wao
ndio wamefanya hivyo, kuwa mtoto wako aumwe ili ushindwe kuendelea na madai
yako..?’ nikamuuliza
‘Unajua
nikiongea haya utadhani mimi naamini haya mambo ya kishirikiana,…mimi siamini
hayo kabisa, mimi namuamini sana mungu , nimelelewa hivyo na ….moyoni mwangu,
siamini sana mambo ya kulogwa, japokuwa yapo, siwezi kukataa….’akatulia
‘OK…’nikasema
‘Lakini hiki kilichotokea hapa, ..oh, labda uwe na
moyow a jiwe, mimi ninaishi maisha yasiyo salama, vitisho, na mambo ya ajabu
ajabu yanatokea kila siku, usiku hatulali, mara wanalia mapaka…sijui vitu gani
vinacheza kwenye bati juu..ni shida kweli, na kuna mtu kaniambia, ukilogwa
ukaondoha humu ndani, ndio basi tena…’akasema
‘Kwanini
huyo unamuamini, na kwanini akasema hivyo..?’ nikamuuliza
‘Sikutaka
nikuambie hiki, ila ni mume wangu ananitokea kwenye njozi, na moja ya jambo
analonisihi ni kuwa vyovyote iwavyo, nisikimbie, nisitoke humu ndani….unajua
hisia , nahisi kama kweli yupo ndio ananiambia hivyo, naogopa kumhini,
kumkatalia mume wangu, la sivyo, ningelishaondoka humu ndani….’akasema
‘Polea
sana…’nikajikute nimesema hivyo
‘Tatizo
sasa, wao wanawalenga watoto wangu, hawa watoto wana makosa gani….’akasema kwa
uchungu
‘Una
uhakika na hilo, kuwa ni watu wanaowalenga watoto, swali linakuja ni nani,…kaam
sio hao shemeji zako, au…?’ nikamuuliza
‘Huyu
mtoto mdogo, hakuwa na tatizo hilo kabisa, sasa kila nikitaka kufuatilia hilo
jambo..hiyo kesi, kwenda huko polisi, huyu mtoto anashikwa na homa kali mpaka
anakuwa kama ana dege dege, anapoteza
fahamu….,hebu niambie mtu kama wewe utaamini nini hapo, na utashangaa
siku hiyo ikipita nikaamua nisiende, mtoto anakuwa mnzima hebu niambie hapo ni
kitu gani hicho…’akasema
‘Ni ajabu
kabisa…’nikasema hivyo.
‘Ilipotokea
zaidi ya mara tatu,…siku moja nikasema potelea mbali ngoja niende….weeh,
nilipigiwa simu hata kabla sijaanza kuonegea na polisi, mtoto kapotea
fahamu…nilirudi nyumbani mbio,…nafika namkuta kweli mtoto kapoteza
fahamu…nilichanganyikiwa, tukakimbiza hospitalini, tunafika mtoto kazindukana ,
lakini hali yake ni dhaifu kweli….ningefanya nini hapo..’akasema
‘Ulihakikishaje…sio
kwamba nakupinga kwa hilo, lakini jinsi gani ulihakikisha kuwa mtoto anaumwa
kwa sababu hiyo…?’ nikamuuliza
‘Mtoto
anaumwa jamani…akianza kuchemka homa namkimbiza hospitalini, akipimwa hana
malaria hana tatizo, …anaishia kupewa panadol…..nikirudi na kusema niachane na
huko kufuatilia mtoto ni mzima kabisa, utasemaje hapo, …..sasa ulitaka
nihakikisheje jamani..’akasema
Pale kwa
kweli nilikaa kimia, nikiwaza yangu….
‘Niambie
wewe, kama ungelikuwa ndio mama ungelifanya nini..?’ akaniliza
‘Je
ulijaribu njia nyingine kwa watu wa dini, au tiba mbadala..?’ nikamuuluza
‘Hahaha,
usifikiri mimi sio mama mwenye uchungu na mwanangu, kote huko nilifika, lakini
sio kwa watu wa ramli, hapana,..hutaamini nikienda huko, mtoto akifika mbele ya
hao watu hana tatizo ni mzima kabisa,..hata ukimuambia mtu anaona kama
unamdanganya…nilipewa dawa, nikapata …maombezi, duwa nk…lakini kila ikifika
siku ya kufuatilia mambo ni yale yale…mtoto wangu anadizi kudhoofika, ’akasema
Ilipita
muda kidogo nikiliwazia hili, je mama kama mama atawezaje kupata haki zake kwa
hali kama hii, kama alivyosema kila akitaka kufanya jambo, mtoto wake anaumwa,na
keshahaikisha hilo…kwa mapenzi ya mama kwa mtoto wake itakuwa vigumu sana, hapo
itakuwa vigumu, sasa …nitamsaidiaje, nikaona ni lazima nifanye jambo, nikasema
‘Shemeji
wewe si unamuamini mungu?’ nikamuuliza
‘Swali
gani hilo, kama nisingelikuwa namuamini mungu kwa hali kama hii ungelinikuta
nimeenda kwa waganga wabaya,nikapambana na hao watu… lakini mimi namuamini sana mungu na kwa haya sijawahi kwenda kwa
waganga wabaya..ila kwa waganga wa dawa, nimewahi, siwezi kukudanganya…na zaidi
mimi namuomba mungu wangu..’akasema
‘Sasa
kama unamuamini mungu huoni kuwa huo ni mtihani tu, unajaribiwa tu , ili tu
usitete haki zako, mimi nakushaurii sasa tuifufue hii kesi …mimi kuna watu
nitawasiliana nao wataweza kwenda mahakamani, ….wataweka pingamizi
…..tusipoteze muda, unaonaje kwa hili…..’nikasema
‘Hapana…’akasema
‘Kwanini…hii
ni haki yako, au sio…’nikasema
‘Ni haki
yangu ndio, lakini sitaki …..kwanza nitaanzia wapi wakati nimeshakubaliana na
hawa wana ndugu tukasema basi yaishe, kama ni nyumba watauza , italipiwa deni
na kiasi kilichobakia tutajengea kibanda nyumba nyingine ya kawaida inatosha
hata kama ni kibanda cha vyumba viwili inatosha…’akasema
‘Wewe
niamini mimi, hapa kuna ujanja umechezwa, kuna mtu anakuzunguka, ili aifisidi
haki ya wanao,…nikubalie tuipiganie haki ya watoto, kwani ukiacha hivi hata
mume wako huko alipo atakulaumu, ina maana juhudi zote alizofanya zinapotea bure
na wewe upo hai….mimi kuna watu wangu watapigania hili hadi haki yako
itapatikana, niamini,…na watoto wata..kuna mtu wa dini atakuja atalimaliza hili
tatizo….’nikasema na yeye akabakia kimia
‘Sikiliza,
….’nikasema na mara mtoto akaanza kulia, yeye akamkimbilia na mimi sikujali,
nikasema
‘Ngoja
niwasiliane na watu wangu, nitakuambia….’nikasema nikapiga simu kwa watu wangu
nikawaelezea kwa kifupi ni nini kinatakiwa kifanyike, …kazi iaanza mara moja!
‘Sasa
sikiliza shemeji, usijali kuhusu mtoto, kila mtu kaumbiwa uhai wake,…sikiliza,
usilie,kwani, hebu kwanza….’nikasema mtoto alikuwa kalegea, ni kama ana….taka
kukata roho, hapo moyo wangu phaa
‘Unaona
ndiyo haya siyataki, hawa wanajua kila ninachotaka kukifanya, unaona …’ akawa
anamshika mshika mtoto wake ambaye kwa muda huo alikuwa na joto kali , keshapoteza
fahamu
‘Tumpeleke
hospitalini..’nikasema
‘Tunajisumbua
tu bure… , dawa ni kuachana na hayo madai,…’akasema mama mtu
Nilimuchunguza
Yule mtoto, kweli joto lilikuwa juu
kweli, ..na hapumui kabisa, ni kama kapoteza fahamu, mimi nikaonelea twende
hospitali tu, hivyo hivyo,..
‘Twende..twende..hamna
cha kujiandaa, mtoto yupo kwenye hali mbaya…’nikasema sasa nikimbeba, huyo mtoto nikitembea kuelekea mlangoni, lakini kabla sijainua mguu wa pili, mara mlango ukagongwa, sikujali huyo mgongaji, nikasema;
‘Twende…’nikasema
nikgeuka kumuangalia mama mjane, ambaye alikuwa kama kachanganyikiwa, anashindwa afanye nini, na mara mlango ukafunguliwa, sote tukageukia sasa kuangalia mlangoni,…
Kimia kidogo...baadae mama mjane akasema;
‘Aheri
umefika shemeji…’
NB: HAYA MAMBO YAMEANZA, KAMA NI WEWE UNGELIFANYA
NINI
WAZO LA LEO:
Mwenyezi mungu anaweza kutupima kwa mitihani mingi, ….magonjwa, kukosa
kazi, misiba na kila jambo lenye kutia
wasiwasi, na mashaka. Haya yakitokea, kamwe tusikimbilie kumshirikisha Mungu,
au kuwashuku wengine kwa mambo ya kishirikina,..wengine hufikia kwenda kupiga
ramli na mambo kama hayo, tukifanya hayo tutakuwa tumekufuru! Muhimu ni kuvuta
subira, na kufanya taratibu halali, huku tukimuomba yeye, kutubu makosa yetu na
hatimaye tutaishinda mitihani hiyo,…
Tumuombe mwenyezimungu atunusuru ni mitihani yenye
kuzishinda nafsi zetu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment