Nilipokea
ile simu, ilikuwa ni yule wakili ambaye alikuwa akiishughulikia hiyo kesi ya
huyo mama mjane na watoto wake…nilikuwa nimeshampelekea barua pepe, ya kumuomba
ajaribu kuifufua hiyo kesi tena, na pia ajitahidi kuweka pingamizi , ili mnada
wa nyumba usifanyike kwanza, kwani imekuja kundulikana kuwa deni hilo laweza
lisiwe la mdaiwa,…
Nilipomtumia,
hakunijibu hapo hapo, …alisubiria sana, baadae ndio akanindikia kwa kifupi,
‘Tutaongea….’hivyo
basi tu
Kwahiyo siku
ikawa nasubiri majibu kutoka kwake,…wakati huo huo nilikuwa nawasiliana na watu
mbali, ambao niliona wanaweza kunisaidia, sikuwa na wazo la kwenda polisi.
Niende polis kwa madai gani, hili nikaliweka pembeni kwanza
Sasa ndio
huyo wakili akanipigia…
‘Wewe
unasema tuifufute tena hiyo kesi, na tuweke pingamizi la kupiga mnada hiyo
nyumba, hii ni kutokana na barua pepe yako,….mhh, unajua vitu kama hivi
ulitakiwa uandike barua halisi ije pale ofisini, ipokelewe kwa utaratibu
maalumu, ..sawa, hata hivyo hamna shida…’akatulia na mimi nikawa kimia tu.
‘Sasa,
…nikuulize tu, una kitu gani cha ziada cha kuthibitisha madai yako..?’ akaniuliza
‘Usijali
kwa hilo…kitakuwepo cha ziada,…wewe nipe muda,
kwa masilahi ya familia hiyo…’nikasema
‘Sikiliza,
mimi ni wakili mwenye heshima yangu, najua kitu gani kinafaa na kisichofaa
kwenye kesi kama hizi,..kama nilivyokuambia, nilipokuatana na huyo mama,
kiukweli niliumia sana, nikaamua kuichukua kama ilivyo, bila kujali mambo
muhimu…’akatulia
‘Kiukweli
sijawahi kuumbuliwa..kama kesi hii,…unajua huruma, au hasira zinaweza
zikakufanya ukafanya jambo bila kufikiria,…hiyo kesi haina mshiko, kitu cha
kuibeba, hakuna ushahidi hakuna nyaraka….unajua,..sasa nikuulize, wewe umepata
ushahidi gani mpya labda …?’ akaniuliza
‘Kwanza
naomba ufanya kama nilivyokuagiza…kwenye hiyo barua pepe, mengine yatafuata tu,
nipo kwenye michakato ya kukusanya ushahidi, usiwe na wasiwasi na hilo…’nikasema
huku moyoni nikijua kuna kazi ngumu sana ya kulifanikisha hilo.
‘Ndugu
yangu, sio swala la wasiwasi hapa…ni utaratibu wa kisheria,..usijifanye hujui
hayo….’akasema akiendelea kulalamika.
‘Si ndio
hivyo,…nimekuelewa..au…’nikasema
‘Na
kuhusu swala la pingamizi, la kupiga mnada, hilo…unajua kosa alilolifanya huyo
mama, licha ya kumshauri sana, ..ni kule kukubali kuwa swala hilo watalimaliza
kinyumbani,..ni kwa vile alikiri kabisa kuwa hana pesa, na hana njia nyingine
za kuweza kulipa hilo deni,…je wewe una namna nyingine ya kumsaidia huyo mama,
kwenye kulipa hilo deni….?’ akauliza
‘Mimi
sina pesa, ila pesa ya malipo, ya wakili, kama wewe na gharama nyingine,
itakuja kupatikana tu,… muhimu ni wewe uwajibike kwa upande wako,…kuwezesha
kesi hiyo kusimama tena,…na…kama una wasiwasi na malipo yako, wewe andaa nyaraka
za kuthibitisha gharama zako, halafu baada ya kazi, utalipwa au..’nikasema.
‘Tatizo
sio malipo, kwani nilipoichukua hiyo kesi awali nimelipwa nini, unanifahamu
nilivyo…’akasema
‘Sasa
tatizo ni nini…?’ nikauliza
‘Kupotezeana
muda kwa kitu ambacho tulishakifanyia kazi…unanielewa hapo…’akasema
‘Ndugu
yangu, na wewe unanifahamu nilivyo, lini nilikuomba kazi kama hizi ikawa ni
kukupotezea muda, nikumbushe…’nikasema
‘Na hapa
kwenye pingamizi la mnada…mhh, unajua labda nishauri jambo, ..tunaweza kulifanikisha
hili kwa njia nyingine,...kama mtakubaliana nami…’akasema
‘Nakusikiliza
wewe muheshimiwa….’nikasema
‘Tunaweza
kuchelewesha kinamna, huo mnada, …lakini kwa njia hiyo itahitajika gharama, je mnaweza kuwa na pesa, kiasi
fulani, kufidia gharama za watu,…hao wa mnada, nk..umenielewa hapo…benki….nitajaribu
kuongea nao, tuone,…sijui unanielewa…’akasema
‘Sawa,
vyovyote uonavyo muheshimiwa, mimi nakusikiliza wewe, na kama kuna madai ya
pesa, gharama za kulipa, ningeliomba yafanyike kimaandishi, kuwe na nyaraka za
uthibitisho wa huduma hiyo, na malipo yatakuja kufanyika,..sio sasa, kwasasa
hakuna pesa ya kulipa, wewe kama wakili udhamini hiyo, …’nikasema
‘Oh…ndugu
yangu, mimi ndiye nidhamini, na hiyo pesa itatoka wapi, ..ndio maana nakuambia,
hapo umeingia kwenye sehemu ambayo hujui chimbuko lake, …na hizi mbinu za
kuchelewesha mnada,..pesa inahitajika kwa haraka, ..na sio rahisi kupata
nyaraka kwa ..utaratibu huo, wewe mwenyewe unajua kuwa hilo tutalifanya kinyume
na utaratibu…’akasema
‘Ndugu
muheshimiwa, hayo yote nakuachia wewe, fanya upande huo, na mimi nifanye upande
wangu, wa kukusanya ushahidi…ili haki iweze kutendeka, kumbuka huyu ni mama
mjane, na watoto wake, kumbuka yeye hajaomba hili litokee, kumbuka hata wewe
una familia, kumbuka…ndani ya hili kuna dhuluma,……’nikasema na yeye kwa haraka
akanikatisha.
‘Sikiliza…wewe hujui jinsi gani
nilivyohangaika na hiyo kesi ya huyo mama, kwa gharama zangu mwenyewe,..sijui
kama ameweza kukuambia hilo… lakini sio hoja, je nikuulize kwanza, je umeweza
kuongea na huyo shemeji wa huyo mama, ambaye ndiye msimamizi wa mirathi, ya
hiyo familia..?’ akauliza
‘Sijaongea
naye bado …yeye hayupo…’nikasema.
‘Ndio
maana….unajua …wewe unataka kufanya hivyo kwa kigezo cha huruma tu,..lakini
kama ungeliwahi kuongea na huyo jamaa, akakuelezea vyema, ungejirizisha kabisa…nakushauri
kitu kimoja, hebu kwanza ongea na huyo jamaa, ili tusipoteze muda,..’akasema.
‘Nitaongeaje
naye wakati yeye hayupo, na hata kwenye simu hapatikani…’nikasema
‘Ok,..ngoja
nione la kufanya…’akasema na kukata simu.
Nilipomaliza
kuongea na hiyo simu mama huyo mjane akawa na hamu ya kusikia nilichoongea ,
akaniuliza;
‘Wanasemaje…?’
akauliza
‘Bado…ila
tuwe na matumaini tu…’nikasema
‘Mbona
hujawauliza,kama kweli kesho wanakuja au hawaji kupiga nyumba mnada..?’
akauliza
‘Labda
nikuulize wewe kwanza, je upo tayari kwa mapambano,…ili kuinusuru nyumba
yenu…?’ nikamuuliza, bila kujibu swali lake,…nahapo akabakia kimia hakusema
neno. Nikamuelewa, na baadae nikamuuliza;
‘Unasema mlikwenda mahakamani, ..mlienda kwa dhumuni gani hasa,
ni nini ulikuwa msingi wa kesi yenu…?’ nikauliza
‘Msingi
wa kesi yetu ilikuwa kuhakiki kama kweli hilo deni ni la kweli au la….ina maana
mimi nililalamika kutokukubaliana na hilo deni…’akasema
‘Ok,…kwahiyo
kesi ikafanyika dhidi ya benki au sio…?’ nikauliza
‘Ndio…nikaambiwa
nipeleke vielelezo, vinavyoonyesha msingi wa madai yangu,…na sikuwa na vitu
vingi, zaidi ni hiyo statement ya benk, na mkataba,…’akatulia
‘Ambayo
ni ushahidi wa benk kuwa kweli mnadaiwa, …’nikasema
‘Hatukuwa
na namna nyingine ya kujitetea, nikatoa maelezo yangu, nikaulizwa ushahidi wa
maelezo yangu, au mashahidi..’akatulia
‘Ehe,…mashahid
uliwaita akina nani..?’ nikauliza
‘Mashemeji
zangu na yule mzee, lakini huyo mzee hakupatikana kutokana na dharura zake…’akasema
‘Na wao
waliongea nini cha kukusaidia wewe, yaani hao shemeji zako…?’ nikauliza
‘Walichoongea
ni maneno tu, kama ilivyokuwa mimi, na walipobanwa na maswali walijikuta
wakishindwa kujitetea, …’akatulia
‘Na
mahakama iliamua nini…?’ nikamuuliza
*****************
‘Hayo ya Mahakamani
we achana nayo tu, maana tulitakiwa tutoe ushahidi, tukatoa, ..kiukweli
ilionekana kama tunapoteza muda tu, japokuwa mahaka hawajsema hivyo, kuwa
tunapoteza muda….’akatulia
‘Wao mliowalalamikia
walisemaje…?’ nikauliza
‘Upande
wao, walitoa vielelezo vyote, walisema hilo deni lipo kisheria, sio kwamba
nasingiziwa, wakaniuliza kama
ulivyoniuliza wewe kuhusu sahihi ya mume wangu, kama ndio yenyewe, kama naifahamu….nikakubali
kuwa ndio yenyewe, maana naifahamu…’akatulia
‘Ehe,…’nikasema
hivyo
‘Na
wakili wao akadai kuwa sisi tunafahamu kuwa deni hilo lipo, ndio maana tukaomba
kuliendeleza, na kuna muda tulifanya marejesho kiasi,…kuthibitisha kuwa
tunalifahamu hilo deni,…ikafikia muda hatulipi kabisa,…na wanashangaa wakisikia
kuwa mimi nadai silitambui, wakati hata mimi niliweka sahihi yangu kuendeleza
hilo deni….’Akatulia
‘Je wewe
uliweka sahihi..nataka uwe na uhakika na hilo, je kweli uliweka sahihi…?’
nikamuuliza
‘Mimi
sijui…sikumbuki kufanya kitu kaam hicho…’akasema
‘Wakati umeanza
kurejewa na fahamu zako, na kuwa na hali ya kujitambua, je shemeji yako alikuwa
akifika kwako kuomba jambo, mfano, akitaka kwenda benki, au kwenye jambo ambalo
na wewe ni lazima uhusikane…?’ nikamuuliza
‘Ndio mara
kwa mara alikuwa akifika kwangu,..kuna vitu vilihitajia mimi na yeye
kushirikiana, asingeliweza kuvifanya bila mimi…’akasema
‘Kama
vipi…?’ nikauliza
‘Kuna
malipo yake ya kazini, alikuwa hajachukua kuna malipo…ambayo ilitakiwa sote
tuweke sahihi zetu, …’akasema
‘Hayo
unayakumbuka au sio, na uliweka sahihi, ..?’ nikauliza
‘Ndio..’akasema
‘Ok…kwenye
hatua hiyo ya kuwa wewe uliweka sahihi, ukasema hujaweka,…ulijiteteaje huko
mahakamani, au wakili wako alikusaidiaje nataka kusikia hapo kidogo…?’
nikauliza
‘Kwenye kipengele cha sahihi, wakili wangu, aliingilia
kati kuwa wao wanajichanganya…kwanza wamesema kuwa, mimi nilisahau, nilikuwa na
tabia ya kujisahau, kwahiyo niliweza kuweka sahihi na kusahau, ..kwahiyo hiyo
ina maana kuwa, mimi nilikuwa sijapona vyema,..’akatulia.
‘Ehee…ikawaje
sasa…’nikauliza , kwani muda huo nilikuwa nasoma, ujumbe wa maneno kutoka kwa
watu wangu.
‘Wakili
wangu aliendelea kusema, yawezekana kuna mtu alitumia mwanya huo wa kunifanya
niweke sahihi, kam ni kweli niliweka, maana sahihi ni yangu, na mimi nimekiri kuwa
sahihi ni yangu,..…, kukawa na malumbano hapo ya kisheria…mimi hata sikuyatilia
maanani…’akatulia kidogo
‘Basi
wewe uliweka sahihi, halafu ukasahau kuwa uliweka…’akasema wakili wo
Nilijaribu
kupinga lakini haikusaidia kitu…wakili wangu akaingilia kati…unaelewa, eeh,
basi…’akatikisa kichwa na mimi nikamuuliza;
‘Je una uhakika
kuwa kweli hukuweka hiyo sahihi yako..hebu jaribu kukumbuka vyema..?’ nikamuuliza
‘Sikumbuki
kwakweli…’akasema kama akijaribu kujikumbusha
‘Kwa hali
kama hiyo wewe mwenyewe unahisije, eeh… kuwa kuna mtu alikufanya ukasaini..au
kuna mtu kagushi sahihi yako…?’ nikauliza
‘Kwa hali
kama hiyo,..kiukweli hata mimi ..najiuliza tu bila majibu, siwezi kusema kitu,
na,. nitamuhisi nani sasa…nimeweza sana hilo,…’akatulia
‘Kama
binadamu ni lazima kuna mtu unamuhisi hisi au sio..?’ nikauliza
‘Mhhh…mtu,
ha-ha-pana,…nitamuhisi nani sasa…mtu wangu wa karibu, mwenye shughuli na benki
ni shemeji , lakini siwezi kumshuku yeye,.., nitamshukuje yeye, maana ..yeye
ndiye kanisaidia sana, atawezaje kufanya
kitu kama hicho …’akasema .
‘Kwahiyo
yeye shemeji yako alithibitisha mahakamani kuwa, wewe uliweka sahihi kuendeleza
hilo deni..?’ nikamuuliza
‘Ndio…na
ndiye aliyesema huenda kwa vile wakati huo nilikuwa na tatizo la kusahau ndio
maana sijakumbuka..’akasema
‘Mhh..ulikuwa
ukisahau..?’ nikauliza
‘Ndio
hapo nikaanza kumshuku shemeji yangu, kwanini ananishikiza kuwa kweli nilifanya
hivyo, wakati mimi nahisi sio kweli….’akasema
‘Wakili
wako alisemaje..?’ nikamuuliza
‘Kiukweli
wakili wangu alipambana na hilo, kuwa kumbe walifahamu kuwa mimi bado ni
mgonjwa ni kwanini walifanya niweke sahihi, …?’ wakaulizwa
‘Kuweka
sahihi haikuwa tatizo kwake, alishafanya hivyo kwa vitu vingine, kabla ya hilo
la sahihi ya deni, na hata docta akathibitisha kuwa kweli nilikuwa vyema
kiakili, …’wakasema
‘Kwahiyo
kam ulikuwa vyema kiakili, ni kwanini hilo waseme umeshau…?’ nikamuuliza
‘Ni kauli
ya shemeji…hata wakili wangu aliuliza hivyo kwa shemeji, na mwisho wake
akatamka maneno ambayo sikuyapenda…’akasema
‘Maneno
gani…?’ nikauliza
‘Eti,
mimi naogopa tu kusema ukweli, ila kweli niliweka sahihi, ..wakili wangu
akambana kumuuliza, je, ulimwambia ni deni…akasema ndio, hapo ndio alinifanya
niongee vibaya, hadi wakili wangu akanisihi nitulie.
‘Baadae
wakamuita shahidi ..ambaye ni docta aliyethibitisha kuwa mimi kipindi hicho
nilikuwa naendelea vizuri, kwani tarehe hizo niliwahi kufika hospitalini,
nakuonekana naendelea vyema..basi, ikaonekana mimi nadanganya, ..najua kuhusu
hilo deni, …iliniuma kweli kweli…hasa pale wakili wao aliposema;
‘Kwa
ushahidi wa docta inaonyesha mgonjwa hakuwa na hali na mbaya ya kushindwa
kuweka sahihi,… ndio maana hata akakumbuka sahihi yake, mgonjwa alijua kuhusu
hilo deni, hapa anafanya kudanganya mahakama…hapo nikaangua kilio…’akasema.
Kulipita
kipindi kidogo cha ukimia, ndio baadae nikauliza hivi;
‘Baada ya
hapo, si mlirudi nyumbani…, mkaja kukaa na shemeji yako kuongea, jinsi gani ya
kuendeleza hiyo kesi, au mlikasirikiana, na ndio mkaja kukata tamaa moja kwa
moja…?’ nikauliza
‘Hakukasirika
kivile,..yeye alikimbilia kinilaumu tu, … kwanini simuamini..wakati amekuwa
akiwajibika kwa ajili yangu na watoto, na anafanya hivyo akijua hiyo ni familia
yake,..kama alivyokuwa kaka yake….alisema mengi, ..mimi ndio nikamwambia;
‘Shemeji nisamehe
kwa hilo, …pamoja na hayo, bado mimi nataka kwenda mbele zaidi, maana nina
uhakika hilo deni sio sahihi kuna kitu kimechezwa hapo…’akasema hivyo na kukaa
kimia, kama ananisubiria mimi niulize swali, na ndio nikauliza hivi;
‘Akasemaje…?’
nikamuuliza
‘Yeye
alisema, nitafika muda nitashindwa maana ukweli imeshabainishwa, na cha muhimu
ilikuwa tukae tujadili tuone jinsi gani ya kupambana na hili tatizo…je kweli
tunaweza kulilipa hili deni, au… ila kama kuna namna nyingine yeye bado yupo
tayari kusaidia, maana hata yeye, hakuwa analifahamu hilo deni, kipindi cha
awali, akasema;
‘Hata
mimi shemeji nashangaa sana, na huenda …yawezekana, lakini kwanini kaka akanificha,
na wakati mimi ndiye nilikuwa mtu wake wa karibu, na wakati mwingine yeye ndiye
ananituma hata benki…’akasema hivyo
‘Alikuwa
anatumwa benk….kufanya nini….?’ Nikauliza
‘Sijui…wanajuana
na kaka yake, yeye alitamka hivyo..’akasema
‘Hebu
niambie kuhusu shemeji yako jinsi gani unavyomfahamu, kiuadilifu na jinsi watu
wanavyomuongelea huko nje, na haa kuhusu yeye na marehemu…?’
‘Kiukweli
shemeji yangu ni …mtu mwema sana, katika ndugu zake, yeye alikuwa kipenzi cha
marehemu,..kila jambo, atamuita yeye, hata kutaka ushauri wakati mwingine,
unajua mume wangu hakuwa mbinafsi,..alipenda kila jambo liwe wazi hata kwa
ndugu zake, alipenda kutumia, ‘kuna leo na kesho….’akatulia
‘Baada ya
maongezi hayo ikafuta nini..?’ nikauliuza
‘Yeye
shemeji, akasema atazidi kufuatilia zaidi, hasa huko benki kuona kama wanaweza
kutusaidia,, kwa vile sasa imeshathibitishwa kisheria kuwa kweli hilo deni
lipo, iliyobakia ni kuomba huruma yao,….na kwa vile mdaiwa keshafariki basi
huenda wanaweza kulifuta hilo deni.
‘Je ni
kweli alifuatilia…?’ nikamuuliza
‘Ndio,
kiukweli shemeji kwenye mambo hayo ya kufuatilia jambo, ni mwepesi sana, si
unajua kazi yake ilivyo…..alihangaika sana…akaja kuambiwa, deni haliwezi
kufutwa, maana ni kubwa sana, …kama hatuwezi kuendelea kulipa, kidogo kidogo,
basi, hatua nyingine itafuta kwa mujibu wa mkataba …’akasema
‘Je wewe
uliusoma huo mkataba vyema, unasemaje….?’ Nikauliza
‘Ni
mkataba wa kawaida wa kukopeshana, mtu na benk..kama, ujuavyo benk wana
taratibu zao, na umeelezea vyema kila jambo…na nyumba ikawekwa kama dhamana, na
kama itatokea tatizo la mdaiwa kufariki, nk..nyumba hiyo inaruhusiwa kupigwa
mnada…kisheria…’akatulia
‘Hata
hayo waliandika, kuwa ikitokea mtu kufariki, nyumba itapigwa mnada, …?’
nikauliza kwa mashaka
‘Ndio..ipo…niliona…’akasema
kwa kusita sita
‘Na kwenye
kumbukumbu zako, ..je deni hilo kipindi marehemu yupo lilikuwa linalipwa kwa
usahihi wake..ilivyojionyesha kwenye statement..?’ nikauliza
‘Kuna
madai kuwa hata marehemu wakati yupo hai , mkopaji (yeye marehemu) alishaanza
kuvunja mkataba, kwa kutokulipa kama
ilivyokubaliwa,kuashiria kuwa mkopaji alifanya makusudi,…mmh kuna maelezo hap
mengi tu,..ila kwa ushahdi walitoa barua ya kumuonya mkopaji…..na mambo mengine ya kisheria, sitaki hata
kuyakumbuka…..’akasema
‘Kwahiyo
kumbe, mkopaji alikuwa anafahamu….!?’ Nikauliza kwa mshangao.
‘Kwa
madai yao ndio…lakini mimi sikuwahi kumsikia mume wangu akilalamika kuhusu hilo
deni lolote, ndio maana mpaka leo siwezi kuamini hilo…’akasema
‘Ikawaje
sasa…?’ nikauliza
‘Shemeji
alikanishauri jambo, kuwa …. Labda na mimi nijaribu bahati yangu, niende huko
benki huenda watanionea huruma kwa vile mimi ni mjane na nina watoto…ikabid
kweli nifanye hivyo, lakini hakuna la zaidi , wao walitaka nikiri kuwa
nimeshindwa kulipa hilo deni ili taratibu zingine za kisheria zifuatwe, kitu
ambacho sikutaka kukubaliana nao..’akasema
‘Kwanini,
wakati mahakama imeshathibitisha hivyo kuwa dni hilo ni halali na mume wako
ndiye alikopa hiyo pesa..?’ nikauliza
‘Nilijua
ni mtego, na kwanini nikiri kuwa hilo deni ni sahihi, wakati, sio
kweli…sikukubali hilo kabisa, …ndio nikirudi nyumbani, na shemeji alipokuja
akaniuliza imekuwaje, nikamwambia nilivyoambiwa huko benk, ….mwishoni
akaniambia, unaona hata mimi niliambiwa hivyo hivyo…’akasema
‘Kwahiyo
ikawaje?’ nikamuuliza
‘Ukumbuke
kesi ya kwanza, ilikuwa ni namna ya kujirizisha kuhusu hilo deni kama ni la
kweli au sio la kweli, na ikathibitishwa kuwa hilo deni ni la kweli kisheria…sasa
katika kuhangaika ndio nikakutana na huyo rafiki yangu, nilisoma naye,
nikamuelezea wee, akasema ngoja akaongee na mume wake, mume wake ni askari
polisi…’akatulia
‘Oh…’nikaguna
hivyo.
‘Baadae
akanipigia simu, yaani huyo rafiki yangu, akasema mume wake kashauri kuwa , kwa
vile bado sijarizika na hukumu,…na imefikia hatua nashuku kuwa huenda kuna
mbinu zilifanywa kupatikana kwa hilo deni, basi,..nikafungue kesi ya madai ili upelelezi,ufanyike….’akasema
‘Kwahiyo
kumbe uliwahi hata kufika polisi,…ni…iih, kwa nia ya kuomba upelelezi ufanyike, ili
kujirizisha kama kweli hilo deni lilipatikana kihalali au sio, vizuri sana,… je
ulipofika huko walikuhoji vipi, maana hapo ulifanya sahihi kabisa..?’ nikauliza
‘Walinihoji
mambo mengi tu, na mengine ni kama walivyofanya huko mahakamani, nikawapatia
nakala ya hukumu,…baadae wakaniuliza ni kwanini siamini kuwa deni hilo ni
halali kwa marehemu..nikawaambia kila kitu, baadae ndio wakauliza, ni nani naweza
kumshuku kufanya hujuma kama hiyo..’akasema.
‘Ukawajibuje…?’
nikauliza
‘Mimi
niliwaambia nionavyo mimi, ..yaani niliwaelezea kama nilivyokuelezea, sikutaka
kuficha kitu, na nikaongezea kuwa mtu wa karibu sana ambaye anaweza kujua
zaidi kwenye hilo deni, sio kumshuku,
ila kufahamu na kuweza kusaidia zaidi ni shemeji, ila nikawapinga hiyo kauli
yao ya ‘kushuku’,…’akasema
‘Ukamtaja
shemeji yako,..wakati huo yeye hayupo au sio,….sasa Ikawaje..?’ nikauliza
‘Huyo mume
wa rafiki yangu alinitafutia askari mpelelezi mnzuri tu, ambaye anaelewa sana
mambo hayo,na haraka akaanza kazi yake,…na ,…tahamaki shemeji anakuja
kukamatwa…’akasema
‘Kwa kosa
gani …?’ nikamuuliza na mara simu yangu ikawa inaingia ujumbe, na haikupita
muda, mtoto wa huyo mama naye akaanza kulia…
NB: Leo
nipo kwenye wakati mgumu kidogo, ngoja niishie hapa kwa leo
WAZO LA LEO: Katika tuhuma,…wengi ni wepesi
sana kuwanyoshea wenzao vidole kuwa wamekosea, kuwa ni wabaya, nk….lakini
twashindwa kujituhumu wenyewe kuwa nasi twaweza kuwa na makosa kama hayo, na
pengine zaidi ya hayo tunayowatuhumu wengine. Ni vyema, tukajirizisha kwanza
kwenye tuhuma yoyote, kabla ya kuwanyoshea wengine vidole.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment