Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, June 5, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-7



'Na..kuna mzee mmoja, nimekutana naye hapo nje, nahisi alitokea humu, au alikuwa anapita tu, ndiye kanichelewesha hapo nje,’ nikasema.

'Mzee Mtupe nini...?' akuliza hivyo

'Sikuwahi kumuuliza jina lake, huenda ndio huyo huyo, alikuwa humu ndani au...?.'nikasema na kumuuliza

'Mhh, hapana,..ila nahisi atakuwa ni huyo mzee Mtupe, ndiye tupo naye karibu, ..kwani kakuambia nini...?'akasema na kuniuliza hivyo


'Mhh, ….nimeongea naye mawili , matatu,..unajua kwenye kazi yangu hii ya utunzi na ….kusaidia jamii, kila jambo lina nafasi yake, usidharau kitu hata kidogo,…ila ni katika kuongea tu, hajaniambia jambo ambalo linaweza kusaidi…., zaidi ya kuwaonea huruma tu,..na akaniambia nyie aliwaona kama watoto wake, si ndio hivyo...?' nikauliza akawa kama kashtuka kidogo, halafu akauliza.


'Basi ndio huyo huyo Mzee Mtupe  aah, ni kweli…tumezoeana naye sana kwani kakuambia nini, mpaka uje kumuulizia,…maana naye ni muongeaji sana..?' akuliza huku akiniangalia kwa mashaka, na akawa anaangalia mbele kama vile anaona watu wengine zaidi yangu. Hii hali yake ya kuangalia hivyo, wakati mwingine inanipa wakati mgumu. Ni kweli hata mimi huwa nahisi kama kuna hali kaam kuna watu, lakini huwaoni.


‘Hamna kubwa zaidi la kusaidia, lakini ni vyema kupata maelezo ya hapa na pale, ili kujenga mazingira mazuri ya kupata mashahidi, kama ikibid kwenda mahakamani tena…vipi watoto hawajambo…?’ nikauliza


‘Hawaja-mbo….ndio hivyo,…hata sijui nifanye nini…’akasema akimuangalia mtoto wake, kiukweli mtoto wake huyo mdogo, alikuwa katika hali ya unyonge, ya kutia huruma, tofauti na huyo mkubwa, na ile hali ilinifanya nizidi kuwa na hali ya kujiona natakiwa nifanye jambo, lakini sasa …nifanye nini, , je kuna nini kinachoendelea humu..je ukweli upo wapi…hapo hapo nikajikuta nimeuliza hivi


‘Unasema mzee nani. …Mtupe, ni jirani yenu sio…?’ nikauliza kutaka kujua zaidi, na yeye akaniangalai sasa kwa shauku, akijua kuna jambo nitakuwa nimeongea na huyo mzee.


'Huyo mzee..ndio ni jirani yetu, ni mtu ..aah, sana sana alikuwa karibu na mume wangu, …’akasema akionyesha hana shauku sana ya kumuongelea, zaidi alitaka asikie ni kitu gani kaongea huyo mzee.


‘Alikuwa karibu na mume wako!!,..sio na nyie nyote kama familia…?’ nikauliza na kutulia kidogo na kabla hajajibu nikasema;


‘Unajua ni kwanini nakuuliza hivyo,…nilitumai kama jirani yenu mwema..basi yeye angelikuwa ni msaada mkubwa kwako, au sio, au labda pengine anafanya hivyo…na kama tutaamua kwenda mahakamani tena basi ni lazima tujitahidi kupata mashahidi..’nikaongea hivyo kuficha yale niliyoongea na huyo mzee.


‘Aaah, ni kawaida, huyo ni mwanaume, kama ni kuzoeana anazoeana na mwanaume mwenzake, yeye alikuwa karibu na mume wangu, zaidi yangu mimi,..na kiukweli mume wangu alimuamini sana, kwa vile yeye ndiye aliyetusaidia kwenye kulipata hili eneo, akawa kama mzazi wetu mwenyeji.., japokuwa siunajua tena, hulka zetu wanadamu, ukiwa mzee ni mtihani,  watu wanamuongelea vibaya mzee wa watu…’akatulia.


‘Wanamuongelea vibaya kuhusu nini labda..?’ nikauliza.


‘Sitaki kuyaongelea hayo wanayoyaongea wao.., itakuwa kama vile kumteta mzee wa watu na huenda sio kweli,…, na hata hivyo, hayana maana au kwanini unaulizia,…mimi sipendagi kuongea mambo hayo..’akasema.


‘Ni mambo ya ushirikina, uchawi, na imani kama hizo au sio…?’ nikauliza


‘Ni mambo kama hayo…’akasema


‘Lakini, wewe tangia nije hapa, unasema kuna mambo yanakutokea, au sio..ni mambo gani hayo,..si ndio hay ohayo  mambo ambayo huyaamini…?’ nikamuuliza.


‘Ni kweli pamoja na imani yangu hiyo, haya yanayotokea kwangu na kwa watoto wangu yananifanya nianze kuingiwa na shaka, maana ni mambo ya ajabu ambayo sijawahi kuyaona katika maisha yangu kabla…, lakini vyovyote iwavyo, sitaki kujiingiza kwenye imani hizo za ushirikina au kukimbilia kumshuku mtu…’akasema.


‘Sawa nimekuelewa,…mimi nataka kufahamu tu, je watu wanamzngumziaje huyo mzee, kuwa ni mchawi,…?’ nikamuuliza na hapoa katikisa kichwa tu kukubalia hakuongea neno.


‘Ukiunganisha na hayo yanayokutokea, kiubinadamu, unajua hata ukiibiwa, unaweza ukamshuku hata rafiki yako,..sasa nikuulize tu, kimawazo, haikujii akilini kuwa mzee huyo anaweza kuhusika,…?’ nikasema kama kuuliza

‘Kuhusika na nini…?’ akauliza kwa sauti kali kidogo.

‘Kuwa ndio yeye anakuchezea, au anatumiwa na watu kukuchezea hivyo…?’ nikauliza

‘Hapana ..hapana, ili apate faida gani, mimi nahisi wanaofanya hivyo ni wale wanaotaka kufaidika, kwa namna moja au nyingine, unaifahamu hali ya huyo mzee kweli…?’ akaniuliza

‘Mimi simfahamu …’nikasema

‘Mzee wa watu, hana kitu, maisha yake yamekuwa ya mitihani mitihani tu…mimi sielewi ni kwanini watu wanamshuku hivyo,…haya yanayotokea ndio kiuhalisia yatakuwa ni watu wanafanya hivyo kunitisha ili nikubaliane na hayo wanayoyataka,..au niondoke kwenye hii nyumba, lakini ni nani,…ukianza kujiuliza hivyo, utagombana na kila mtu,..ndio maana mimi sipendi imani hiyo, mungu wangu anatosha…’akasema

‘Heni niambie ukweli, hao unaowaona sio watu, au wewe huoni kuwa ni watu wanaokuchezea…?’ nikamuuliza

‘Hapo hata mimi sijui… ni akina nani hao, na…kwanini…kama ni nyumba, si benk,…wanataka deni lao lilipwe wao watafaidikka na nini hapo..na ni ..hata siwezi kuelezea jinsi inavyoonekana, ni taswira, ..huoni sura,.. aah, sitaki hata kuelezea…, ’akasema akitikisa tikisa kichwa.

‘Huyo mzee, anasemaje kuhusu hizo shutuma dhidi yake…?’ nikamuuliza

‘Mhh…kwa vile umeuliza tu, ila sipendi,.. kama alivyokuwa mume wangu, na mimi pia sikutaka hiyo hisia itutawale, ndio maana mume wangu akawa karibu naye, ili kuondoa hisia hizo za watu, na mimi nikamjali huyo mzee kama mzazi wangu, anakuja hapa tukamkaribisha vyema tu, anaweza hata kushinda, kutwa nzima akifanya vikazi vidogo vidogo vya ufundi…sina ubaya naye kwa kweli, na hata yeye anashangaa ni kwanini watu wanamsema hivyo, sasa mimi sijui zaidi…’akasema

‘Kwahiyo kumbe anakuja hapa, akaweza hata kushinda kutwa nzima, au sio, na kwa namna hiyo mambo mengi yanayotokea humu ndani kwa kiasi fulani anayaona na huenda anasikia kile kinachoendelea humu ndani, au sio..?’ nikamuuliza hapo akanitupia jicho, halafu akasema


‘Mambo gani,labda, maana sizani,…na kwanini asikilize mambo yasiyomuhusu,…mimi siwezi kujua, kwasababu hata kama ni jirani, anapokuja hapa yeye ni mgeni tu, hawezi akafahamu mambo ya ndani kivile  labda sasa awe na nia mbaya..na hebu nikuulize…kwanini unayaongea hayo, kumuhusu yeye, mumeongea nini na yeye, nahisi kuna kitu..?’ akaniuliza.


‘Kama nilivyokuambia, kila linalotokea kwenye jambo unalolifuatilia, moyo unakupa shaka fulani kuwa huenda….’nikatulia kidogo

‘Na hii huenda, ni shuku….ili iwe shaka njema au mbaya, , na ni vyema kudadisi ili kuupata ukweli, ili kuondoa dhana mbaya…..Mimi na huyo mzee sijaongea naye kitu kibaya kivile,…sana sana alikuwa akiwaonea huruma…anasema yeye na mume wako walikuwa kama mtu na kijana wake, na kinachoendelea hapa kinamuumiza sana, lakini hajapata nafasi ya kuweza kusaidia…’nikasema.


‘Ndio hivyo ni kweli wao wawili walikuwa hivyo, mzee na kijana wake,  ila haya yanayotokea hapa hakuna anayaweza kutusaidia, sana sana ni sisi wenyewe na hao wanaotaka kufanya hayo,..ndio hivyo, na, akisema, hajapata nafasi, hapo sijui maana aliipata hiyo nafasi, sema ndio hivyo, alikuwa na dharura…’akasema.


‘Unasema huyo mzee ndiye aliyewasimamia,katika kupata hiki kiwanja,..na je katika kuhangaika kwenye kesi, mlimuita huyu mzee kama shahidi yenu..si ndio hivyo?’ nikamuuliza.


‘Tulimuita ndio..lakini kwa bahati mbaya hakuweza kupatikana, ndio hapa nasema aliipata nafasi hiyo kama angetaka,angeitumia, lakini si ndio hivyo, alikuwa na dharura. Lakini sasa haya ya nyumba sio tatizo la kiwanja au nyumba, ingelikuwa hivyo, yeye angelikuwa shahid mnzuri tu, tungejitahidi mpaka afike,…tatizo hapa ni la deni,..je huyo mzee angewezaje kutusaidia,..unaona eeh, ndio maana hatukusumbuka naye sana…’akasema.


‘Unasema siku ya kesi hakuwahi kufika kwa vile alikuwa na dharura, hakuwahi kuwaambia ilikuwa ni dharura gani..?’ mimi nikaendelea kuuliza bila kujali maelezo yake.


‘Alisema alipatwa na matatizo, ikabidi asafiri.., alikuwa anauguliwa, sawa, alisafiri kweli, lakini kwanini kila ikifikia siku ya kesi, inatokea dharura ya namna hiyo,…unaweza kuingiwa na shaka ya namna hiyo, lakini haijalishi…’akasema


‘Na bado anaendelea kufika hapa kwako…?’ nikauliza

‘Mhh..ndio anafika, lakini si unajua tena, mimi nitampa nini, kufika kwake hapa pamoja na ujirani, lakini ni pamoja na kupata vijikazi, na chochote kitu, mimi mwenyewe nahitajia kusaidiwa, ..anafika, na …halafu kinachonishangaza kila akija namuona ananiangalia kwa jicho..lisilo la kawaida,…’akasema

‘Lisilo la kawaida kama vipi….?’ Nikamuuliza

‘Kama chuki hivi…ndio maana sitaki kuongelea hayo, .. ni hisia tu, ila mzee wa watu sina shaka naye…’akasema

‘Hebu sema ukweli, wewe humuhisi au kumshuku kwa namna fulani hivi…?’ nikamuuliza.


‘Kumshuku kuhusu nini sasa wakati nimeshakuambia msimamo wangu…?’ akauliza


‘Labda hayo unayoyaona na yeye yumo…?’ nikamuuliza


‘Hapana…mimi hayo ninayoyaona huwezi kumshuku mtu, maana sio vitu vya kawaida, ni maumbile ya ajabu,..hayana sura halisi ya mtu japo miili yao ni ya watu,..usoni, nataswira tu, vivuli vivuli, …ni kaam watu lakini wanafunikwa na hali…ila inatisha ..lakini mimi namtegemea mungu, isingelikuwa kwa hawa watoto..ningepambana nayo mimi mwenyewe…’akasema

 ‘Kama nilivyokuambia, kila kitu kwangu ni muhimu ili kuweza kulifanikisha hili, ninaweza kukuuliza mambo ambayo unaweza kujisikia vibaya labda au hupendi kuongelewa.., lakini lengo ni lile lile, kuutafuta ukweli, ushahidi na mashahidi…nakuomba kitu kimoja, usiwe na shaka na maswali yangu..au ndio unaogopa hayo mazingaumbwe yao…’nikasema

‘Mazingaumbwe…!!, ’ akasema hivyo kwa kushangaga huku akiangalia mbele.


‘Hayo ya kukutishia uchawi nk…’nikasema


‘Kwa hali ninayokumbana nayo, japokuwa nina imani yangu, lakini mhh …sio rahisi kuwa na moyo wa jiwe…inatisha, maana wao wamegundua kama mama, wakigusa watoto, watanivunja nguvu,…unajua ninachokiona, huwezi kukielezea, mara unaweza kuona kama watu, lakini sura huzioni, au …wanakuwa warefuu…au misura ya ajabu ajabu,…’akasema na kutulia kama kakatizwa hivi, akawa katulia kimia

‘Umewaona tena..?’ nikamuuliza, hakunijibu badala yake akasema;


‘Ulitaka kuniuliza nini zaidi naona kama muda unakwisha, hivi ulisema walikupatia siku tatu, sasa leo ni…ina maana kesho, wanaweza kuja kupiga mnada nyumba, mungu sijui tutakwenda wapi, yaani, silali, nikiliwazia hilo..?’ akauliza, huku akiangalia mbele, kwa hali ile ile kama anaona vitu vya ajabu.

Nikaangalia huko mbele anapoangalia sikuona kitu, nikadharau

************

‘Shemu,..habu kidogo tutete kuhusu ndoa yako kama hutojali,…wewe na mume wako mlikuwa vipi,…?’ nikauliza na hapo akanitupia jicho la haraka, halafu akauliza


‘Sijakuelewa….’akasema


‘Yaani, ..unajua ukweli ulivyo kwenye ndoa, watu wanaweza wakaishi,unawaona kabisa ni wanandoa, lakini hawapo karibu sana, kuna migogoro ya hapa na pale, inatokea, au sio, sasa nauliza hivi kwa ujumla wake, wewe na mume wako mlikuwa vipi…?’ nikauliza


‘Mimi na mume wangu tulikuwa tunapendana sana…sikumbuki kama niliwahi kugombana na mume wangu…kivileee,..mmh.haijatokea, sikumbuki, ndio maana kifo chake kimeniua na mimi , hapa nilipo nipo kama nusu mfu…’akasema


‘Hakuna kipindi kulitokea migongano, mkawa hamuongei hivi, sema tu ukweli, kuna kitu najaribu kukitafuta, nione …usinifiche tu, niamini kwa hilo,…?’ nikauliza


‘Inatokea..lakini si ndio maisha, ni..mambo ya kawaida tu, kwa mume na mke, lakini sio kugombana mpaka, ile…hapana hiyo haijawai kutokea…’akasema


‘Na katika hilo kutokea ni kawaida ndio, hamjagombana labda kuhusu mali zenu, …maana nakumbuka wewe awali, uliwahi kusema, mume wako, alikuwa karibu sana na ndugu zako kuliko wewe,katika baadhi ya mambo, au sio…je hilo halikukukwaza moyoni…?’ nikauliza.


‘Mume wangu hakuwa na tamaa, mume wangu alijua mimi ndio yeye, kwahiyo sio kila jambo alitaka na mimi niwepo, alishawahi kuniambia, mimi nasimama badil yako, nakuwakilisha wewe, ndio maana mambo mengine si lazima wewe uwepo, nitakuwa nakupatia taarifa tu…’akasema

‘Kwa kusema hivyo, wewe ulifurahia, na je katika kugombana, ikitokea kama binadamu haijawahi kuhusu hivyo,kuwa kwanini hunishirikishi kwenye mambo ya mali…?’ nikamuuliza

‘Hapana,..mimi nilimuelewa, na sikuwa na mawazo hayo kabisa..ya mali, maana mali niliziona ni zetu mimi na yeye na familia na ndugu zake, kama wanafamilia pia, sasa kinachonishangaza ni haya yaliyokuja kutokea, wale niliowaona ni ndugu wamenigeuka…’akasema kwa uchungu.


‘Hapa sasa tunabakiwa na ndugu…sheemi zako,….’nikasema

‘Unasema…?’ akauliza hivyo

‘Hebu kidogo, tumuongelee huyu shemeji yako naye…inaonekana mumeivana sana,..unamuamini sana, au sio …humshuku lolote labda…, maana hili swali nilikuuliza awali hukutaka kunijibu…?’ nikauliza

‘Kiukweli, shemeji huyo ni mtu mwema tu, sina sababu ya kumuhisi vibaya, lakini sasa kwa haya yanayoendelea, inafika muda kila mtu humuamini, hasa shemeji zangu, …lakini nitakuwa napata dhambi kama nitamshuku huyu shemeji,..japokuwa oh, hata sijui nisemeje…’akatulia kidogo.

‘Kwanini labda, uwashuku shemeji zako, lakini huyu ambaye yupo karibu yako ambaye anaweza kufanya lolote usimshuku,……?’ nikamuuliza

‘Mimi…mmh, kibinadamu, au sio.., hebu fikiria hali niliyokuwa nayo, ulizia watu, ilifikia watu wote wakakimbia,..sio kule kukimbia kwa kuonekana wazi, ..watu walishachoka kuniuguza, wengine wakafikia kusema najilegeza,…lakini yeye mtu wa watu hakukata tamaa,…’akatulia

‘Sasa uone..iweje sasa mtu huyo huyo, aje anifanyie ubaya, mimi naona yeye hawezi, ..japokuwa, kuna mengi anayang’ang’ania, mimi sipendi, hapo ndio tunafikia kukosana,..na kwanini kila ikifikia hatua hiyo, anadai kama isingelikuwa yeye…hapo ndio nachoka…’akasema

‘Kwa hali kama hiyo ndio inakufanya, usimshuku,..japokuwa kuna hali inaonekana kuwa anaweza kuhusika, au sio…?’ nikauliza

‘Mhh…unajau yeye ni mmoja wa watu wanaoaminika sana, kutokana na shughuli zake, na  kwa jinsi alivyojitolea kunisaidia, nashindwa  kumshuku vibaya, nashindwa kusema lolote, sioni ushahdi wa kumshuku, lakini ni nani sasa…’akasema

‘Mimi nahisi wewe hutaki tu, ila kwa namna nyingine yeye, anaweza akahusika,..japokuwa mimi sijaweza kuongea naye, na unaogopa kwa vile watu wanamuamini,..lakini moyoni una shaka naye..?’ nikamuuliza

‘Ndio maana mimi nashindwa kuendelea na haya mapambano,  naingiwa na sintofahamu, na….na…sitaki kwenda mbele zaidi kwa vile, kila ninalofanya, naona kama napambana naye sasa, wakati ni mtu aliyejitolea kwangu tokea awali, hadi ilifikia mahali anataka kukosana na mkewe,, hebu fikiria mtu wa namna hiyo,…hata  sijui kama unanielewa…’hapo akatulia.

‘Kwa kifupi wewe unalipa fadhila bila kujua kuwa unajiumiza mwenyewe, ila kwa upande fulani unamshuku , angalia mashamba je alikuwa upande wako  na sasa nyumba je yupo uapande wako….?’ nikamuuliza

‘Hapana siwezi  kumshuku,….ni hisia tu, lakini ukichunguza sana, unaona kuwa hisia hizo hazina msingi, kwahiyo mimi siwezi kusema lolote baya kumuhusu yeye, ama kuhusu mashamba, yeye kama familia yao, ilibidi asimame na wenzake au sio, siwezi kumlaumu kwa hilo, kama ni kuwalaumu nawalaumu wote,…’akasema

‘Wewe na sheemji yako, tokea awali, wanaishi hapa, ..akaoa, ukilinganisha na sheemji wengine, yeye naona mumeivana sana, au sio,…na hata mkienda kuishi kwake hakuna matatizo…?’ nikauliza hivyo

‘Kuivana kwa vipi, hapana, ni kwa vile yeye kachaguliwa kuwa msimizi,..ndio ni ukweli kuwa hata alipokuwa hapa, yeye alikuwa karibu sana na mimi,…lakini ni kwa vile alikuwa akinielewa, anafanya vile nionavyo ni sahihi, ukilingansiha na wengine, lakini sio zaidi ya hapo

‘Na kwa namna hiyo, hata ukienda kuishi kwake, mimi sioni kuwa ni tatizo..’nikasema

‘Mmmh hapana..japokuwa kiukweli ingelikuwa ni yeye mwenyewe , ..hakuwa na shida…, lakini sizani kama  kutakuwa na amani, …kuna mke wake, familia yake, unaona eeh..sioni kama ni jambo jema…’akasema

‘Mke wake yupoje, …hakuamini au,..na umesema ilifikia anataka kukosana na mkewe kwa ajili ya kujitolea kwake kwenu,..yeye alisemaje labda..?’ nikauliza

‘Kibinadamu ipo hiyo, lakini hatuna nia mbaya…hizo ni hisia zake tu, niliwahi kuongea naye niliposikia hizo shutuma,nikamwambia,…na alinielewa,…sitaki tu kwenda kuishi kwenye familia yake ikibidi utafanyaje, lakini ni jambo la mwisho kufanya, ikibidi…’akasema

Hapo mtoto wa huyu mama akadakia na kusema;

‘Mama, ulisema …’kijana akataka kuongea jambo.

‘Wewe mtoto nilishakukanya wakati watu wazima wanaongea, usipende kuingilia, unanisikia, nisikie tena…’akasema huyo mama
Tuliendelea na mazungumzo mengine kudadisi ..nia ni kuona kama mzee, yule alichoniambia kina ukweli..lakini sikuweza kuupata huo ukweli. Baadae huyo mama akaelekea jikoni, na kipindi chote hicho sikuwahi kupokea simu, kutoka kwa watu niliowategemea, kufahamu je zoezi hilo la mnada bado lipo…na simu kutoka kwa wakili ambaye nilimuagiza afaney taratibu za kuweka pingamizi jingine
***************
Nilibakia pale na watoto..nikaona nimdadisi huyu mkubwa…

‘Mtoto, unaniamini mimi, kuwa naweza kuwasaidia…au sio…?’nilianza kuongea na yule mtoto, mama yake akiwa jikoni.

‘Nilimuambia mama wewe ni mtu mnzuri, lakini mama hataki niongee…’akasema

‘Lakini wewe unaniamini…mimi nataka niwasaidie, ikiwezekana msinyang’anywe nyumba yenu, sasa nikuulize maswali unijibu au sio…?’nikasema

‘Maswali ya nini…?’ akauliza kwa mashaka

‘Baba yako mdogo,..ni mtu mnzuri sana..?’ nikamuuliza

‘Ndio anatuletea zawadi, ….ila wakati mwingine wakiongea na mama, ..akiondoka anamuacha mama analia,..mimi sipendi, nahisi baba anamsema vibaya mama, sipendi…’akasema

‘Wewe hukuwahi kusikia wanachoongea..?’ nikauliza

‘Mara nyingi wakiongea wanatuambia twende nje…’akasema

‘Ni kitu gani kile ulitaka kusema, mama akakuzuia, niambie kama kinaweza kusaidia kuzuia nyumba yenu isichukuliwe…’nikasema

‘Baba mdogo alisema ni lazima nyumba iuzwe,..kwanini anasema ni lazima,..ndio maana nilitaka mama akuambie wewe,..ukaongee na baba mdogo, asilazimishe nyumba iuzwe…’akasema.
‘Kwanini sasa mama anakuzuia, usiniambie hayo..?’ nikamuuliza

‘Anaogopa, …mdogo wangu atakuwa anaumwa…’akasema

‘Ni nani anamfanya mdogo wako aumwe, ..unahisi ni nani, mama hajawahi kukuambia, au kusikia kwa watu …?’

‘Mama alisema….’akaanza kuongea kabla hajaendelea, mara mama mtu akatokea..

‘Mnaongea nini na mwanangu,..maana huyu siku hizi anajifanya kuongea, alikuwa sio hivi, ni mpole ajabu , lakini sasa hivi kila kitu anataka ajue, eti yeye anastahiki kusimamia mahali pa baba yake kwani yeye nimtoto wa kiume mkubwa, sijui ni nani kamfundisha hayo…’akasema

‘Ni babu….’akasema

‘Babu, mzee mtupe..?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukubali, na hapo nikamtupia jicho mama, mama alimuangalia mtoto wake kwa jicho la kumuonya anyamaze.

‘Ni vizuri lakini, kama keshaanza kulitambua hilo, kuwa na yeye anawajibika sio vibaya…’nikasema

‘Hapana huyu bado ni mdogo, bado hajaweza kuitambua dunia ilivyo, najaribu sana kumzuia, maana,…hujui ni nini kinachoendelea…’akasema

‘Ni sawa…lakini pia ni vyema kumkomoza kihivyo, hasa kwa kipindi kama hiki…’nikasema

‘Unajua nashukuru sana, naweza kusema nyota ya mtoto wangu huyu ni kali, yanayomkuta mdogo wake hayajamkuta na yeye,..kuna kupindi aliumwa sana, lakini sio matatizo kama hayo ya mdogo wake …’akasema akimuangalia mwanae huyu.


‘Lakini yeye anaweza kusaidia pia…huenda alisikia jambo ambalo linaweza kusaidia…’nikasema na kuuliza

‘Sitaki wanangu kujiingiza kwenye haya mambo, kuna mabaya yapo nyuma ya pazia, inabidi niwalinde kwa kila hali, hizi mali, nyumba,mashamba hayana  maana kwao kama afya zao zitatetereka, na hao watu, kama ni wao wanafanya hivyo hawana utu, kiumbe kaam huyu kawakosea nini…’akasema halafu akamgeukia mtoto wake na kusema kwa upole.

‘Sikiliza mwanangu nielewe, usijaribu kuniingilia au kuongea chochote bila ruhusa yangu, unasikia, wewe hujui lolote kuhusu dunia na watu wake, usijifanye unajua sana mambo ya wakubwa, muda wako bado, unanisikia lakini…’huyo mama akasema na mtoto akainamisha kichwa kwa heshima.

‘Ndio mama….’akasema hivyo.

****************
‘Katika kuwaza sana, kuna jambo najiuliza hapa, unasema shemeji yako alikuwa mwema kihivyo, najiuliza tu, yeye ndio alianza kulifahamu hilo deni la nyumba, au sio…?’ nikamuuliza

‘Ndio…’akasema

‘Sasa yeye kaona kuwa kuna deni kubwa, ni  kwanini sasa akaendelea kuchukue mkopo , kwenye hilo deni, na kwa vipi benk wakaendelea kumkubalia, hapa nakuwa na mashaka napo, ndio maana nataka niongee naye, atarudi lini…?’ nikamuuliza

‘Anadai awali hakulifaham hilo, yeye alipokwama kabisa, huwa anakwenda benki, na barua za mirathi, anaomba kuchukua pesa,..lakini awali hawakuwahi kumuambia kuhusu deni,….ndivyo alivyojitetea….’akasema

‘Na kipindi umepata nafuu, yeye hakuwahi kukuambia  kuhusu huo mkopo, kuwa anachukua lakini kuna deni huko benk..?’ nikamuuliza

‘Hakuwahi….., ila kuna siku alikuja akaniambia mambo hayaendi vizuri, anataka kufanya jambo, kwani benki wanaanza kumzuia kuchukua pesa zaidi, lakini ngoja akaongea nao, kama hakuna pesa, atakopa,…’akasema

‘Ikawaje…?’ nikamuuliza

‘Aliporudi akasema kuwa wamemkubalia lakini kwa shida, anashangaa kama  kaka alifanya hivyo, kwanini wao wamzuie,…’akasema hivyo,

Nikamuuliza kaka yake yeye alifanya nini…lakini hakusema kitu akasema tu, usijali, …nitamaliza nao…, nitahakikisha mpo salama, halafu akaondoka zake…’akasema.

‘Hebu niambie kidogo kuhusu shughuli za mume wako zilikuwaje kabla ya kifo chake….hakuna kipindi kilikuwa kigumu kwenu, huenda kipindi hicho aliamua kufanya jambo kwa nia ya kujikwamua na angelirejesha hilo deni kabla riba haijawa kubwa….?’ nikamuuliza

‘Hapana kwa mume wangu kuchukua huo mkopo sitakubaliana nalo mpaka kesho….ndio  mume wangu alifariki kipindi hana kazi, alishaamua kujiajiri, lakini hakuwa na hali ngumu ya kwenda kukopa, alikuwa na akiba yake tu, na mafao yake,, na kila mara alisema yeye ataendesha kila kitu kutokana na kile alicho nacho,…kidogo kidogo akawa anainukia kibiashara, na akawa kwenye hali nzuri tu….’akatulia

‘Lakini wafanyabiashara wengi kukopa ni jambo la kawaida, au sio…’nikasema

‘HAPANA, sio yeye, ..yeye alisimamia kwenye mtaji wake wa mafao yake akawa anakwenda mikoani, kuchukua mazao, analeta mzigo mkubwa anauza kwa jumla,…na awali alikuwa akifanya shughuli zake hapa Dar, huko kwenda mikoani ilikuwa ni mara ya pili, ….ndio ilikuwa ni mara ya tatu ndio akakutana na umauti…’akatulia hapo

‘Kwahiyo huo mkopo haukutokana na mume wangu ni lazima ulikuwa baada ya yeye kuondoka..au kuna namna huo mkopo ulitengenzwa, lakini sio wa mume wangu,..na hata kama angelikopa,…asingeliweza kunificha…’hapo akatulia

‘Kabla sijakuuliza jinsi gani mume wako alivyofariki, hebu kwanza niambie kuhusu yaliyotokea mahakamani…’nikasema

‘Mahakamani…?’ naye akauliza hivyo

‘Ndio maana tunataka turejee tena huko…ikibidi,..hebu niambie.., ulipofuatilia na kuwaonyesha  hivyo vidhibiti,  ilikuwaje…?’

‘Vidhibiti….sikuwa navyo zaidi ya taarifa kutoka benki…na nakala ya mkataba,…zaidi ni maelezo yangu tu…’akasema

‘Nataka uniambie kila kitu, jinsi kesi ilivyoanza , wakili alisema nini, wakili wako, na wakili wa utetezi , yaani wakili wa benki alisema nini, nataka nikuuliza hatua kwa hatua, nataka kuona uchochoro wa  kupitia…’nikasema

‘Ina maana unataka mimi nirudi mahakamani tena, na unajua ni kitu kitatokea kwa mtoto wangu…’akasema

‘Sikiliza…’nikasema

‘Hapana,…siwezi tena,…’akasema

‘Ina maana unataka nyumba hii ipigwe mnada, …safari hii mimi ndiye nitabeba jukumu hilo sio wewe kama ni kunifanya vibaya wanifanye mimi,..huoni wameshaanza, lakini mimi nitapambana nao, unasikia…’nikasema na yeye akabakia kama anawaza jambo.

Akageuza kichwa kumuangalia mtoto wake,..halafu akagueza kichwa kuangalia mbele, nikaona uso wake ukibadilika, kama kuogopa, macho yakionyesha, kuongezeka ukubwa, ule wa kutishika, na mara simu yangu ikaanza kuita..kuangalia nikaona ni namba ya wakili ambaye nlimuomba aweke pingamizi.

‘Ngoja kwanza nipokee hii simu…

NB: Ngoja kwanza na mimi niweka haya mambo sawa

WAZO LA LEO: Shiriki ni mbaya sana, haitakiwi wanadamu kujiingiza kwenye mambo hayo, maana japokuwa wanajiona wanafanikiwa (wanaofanya mambo hayo), wanawazalilisha wanadamu wenzao, lakin mwisho wa ushirikina wao huwa ni mbaya sana.

Na ili uyashinde hayo mambo, elekeza imani yako kwa mola wako, kuwa yeye ndiye muweza wa kila jambo, na yeye ndiye anayeweza kukusaidia, kuyashinda yote hayo. Dhiki, shida, matatizo yote hayo ni mitihani tu.

Ni mimi: emu-three

No comments :