Hali yangu ikawa tete, sijiwezi kabisa siku hiyo nilihis
kama nataka kufaa, ….ikabidi niende hospitalini, nikapimwa kila kitu , hakukuonekana
tatizo lolote kwenye vipimo, na wakati nataka kuondoka, docta akaniambia;
‘Hiyo hali kwa uzoefu wangu, ni bora ujaribu upande wa
pili…’akasema
‘Una maana gani docta…?’ nikauliza
‘Kiuzoefu wangu, matatizo kama hayo hutaweza kupata tiba
sahihi hospitalini, kuna njia mbili, nenda kwa watu wa dini upate msaada wao,…imani
inasaidia sana, au nenda kwa waganga wa
tiba mbadala, na wao wanasaidia, lakini kwa waganga wanaoaminika, sio wa
shiriki…’akasema.
‘Docta…ina maana…’nikataka kuongea.
‘Aaah, usinielewe vibaya, ni ushauri tu, mimi nimekuwa
katika hii fani kwa muda mrefu sana, najua ni nini ninachkushauri, lakini ni
uamuzii wako, ..dawa hizi hapa za
maumivu, tumia uone kama zitakusaidia, au nikuandikie uende hospitali za juu
labda huko watakupatia matibabu zaidi…’akasema na kuniangalia.
‘Ahsante docta nimekuelewa…’nikasema na kuondoka, nikafika
nyumbani nikajilaza kwenye sofa, nikawa nahisi njozi si njozi,….nikuwa kama mtu
aliyechanganyikiwa, nikaona sasa nitaharibikiwa, kwa haraka nikasimama,
nikatoka nje, na kuelekea kwa jamaa yangu ambaye kaiva sana kwenye dini,
nikamuelezea, akasema;
‘Hayo yanatokea, .. nitakusaidia,….’ Akasema na kweli alinisaidia,
kwani baada ya hapo, nikahisi nipo vizuri, japokuwa bado mwili ulikuwa mdhaifu.
Hiyo ni siku ya pili, kwa makubaliano yangu na yule jamaa ,
bado siku moja…
Tuendee na kisa chetu
**********
Nilipojiona nipo vizuri, nikakaa kutafakari tatizo la yule
mama, na hizo njozi zinazonitokea mara kwa mara,… kwanza nilianza kujiwekea
vikwazo mwenyewe, kuwa kwa vile yule mama alishakubaliana mambo yaishe
nyumbani, basi, haina haja ya mimi kujisumbua,…lakini, kabla sijamaliza kuwaza
zaidi mara simu yangu ikaita, ilikuwa sauti ya mwanamke;
‘Shemeji unaendeleaje…’ilikuwa sauti ya yule mama
‘Sijambo, vipi wewe na watoto..?’ nikauliza
‘Hapa nilipo …natamani hata kuikimbia hii nyumba, matatizo
yanazidi kuongezeka, ….yaani usiku sikulala, sasa hivi ndio mtoto kaweza kulala…nimeambiwa
tatizo ni mimi sikutaka kutimiza niliyoahidi, Natafuta mbinu nyingine ya
kuanzisha matatizo, ….sasa tafadhali, naomba tuyaache kama yalivyo, unasikia
shemeji…nashukuru sana kwa kujali, lakin kwa hatua hii, basii tena…’akasema
‘Shemeji nakuja…’nilijikuta nimesema hivyo na kukata simu,
…sijui kwanini, hali fulani ikanivuta na haikupita muda, nikawa nimeshafika
pale nyumbani kwa yule mama.
Wakati nakaribia kwenye hiyo nyumba nikakutana na mzee
mmoja, huyo mzee alikuwa akikagua hiyo nyumba kwa nje, katika kusalimiana,
tukajikuta tupo kwenye maongezi, baadae akasema;
‘Hawa akina mama jamani, …hawamuogopi mungu kabisa…’akasema
‘Kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza
‘Kuna kitu nakujua sana humu, nimekiona kwa macho yangu mimi
mwenyewe…kipindi kile nilitaka kumuelezea marehemu lakini roho ikawa inasita,
sasa najuta kwanini sikumuambia…’akatulia
‘Kitu gani..?’ nikamuuliza na akageuka kuniangalia, halafu
akasema
‘Kwanza…wewe ni nani na huyo mama, mjane…?’ akauliza
‘Mimi natafuta ukweli halisi ya yanayotokea hapa, huyo mama
anahitajia msaada wa kijamii kwakweli,…lakini nashindwa kuupata huo ukweli…’nikasema
‘Ukweli..hahaha..kesi
ya nyani unamuuliza ngedere, ..nyie watu jamani, ulizeni majirani…’akasema
‘Kwani kuna nini …majirani wanakijua zaidi ya wenye nyumba…?’
nikamuuliza
‘Unajua mimi nilikuwa karibu sana na hiyo familia,..yule
marehemu alikuwa kama kijana wangu, hata wakati ananunua hili eneo mimi
nilimsimamia, kwahiyo akaweka kama mzazi wake,…na unajua tena hali zetu wazee,
siku nikikwama, nakutana na marehemu
ananisaidia kwakeli mola amsaidia huko alipo kwa wema wake huo.
‘Kwa ule ukaribu wangu, eeh, nakawa nafika sana hapo nyumbani,,
wakati mwingine namkuta mwenyewe, wakati mwingine mkewe,….naweza hata
nikashinda hapo nikiwasaida kazi ndogo ndogo maana mimi kitaaluma ni fundi,…kwa
ajili ya ukaribu huo, nikawa najua ni
nini kinachoendelea, lakini sikuwahi kumuambia marehemu, unajua tena mambo ya
familia ya watu, sikutaka sana kuingilia, ila nilipanga nije kukaa na huyo
marehemu kama kijana wangu nimnasihi,..hata kama angesema anawaita…hao
wanaomzunguka, nilikuwa tayari kuongea mbele yao…’akasema.
‘Ok….unataka kusema nini labda, ..maana nina haraka
kidogo…’nikasema
‘Huyu mjane , sijui ni kwa kutokujua, au ni tamaa za
wanawake,..’akatulia kidogo..hapo nikahisi kitu kikigonga kichwani, nikasema
moyoni, mambo yanaanza kujileta yenyewe.
‘Ehe….kwavipi…?’ nikamuuliza
‘Kulikuwa na hali ya ukaribu kati ya mjane na shemeji mtu,
huyo ambaye kakabidhiwa kazi ya kuitunza hiyo familia, na…kinamna fulani,
hatuombei mabaya, kuwa labda walipanga njama za kifo cha marehemu hapana, sipo
huko…’akatulia
‘Kwani marehemu aliuwawa..?’ nikauliza
‘Alipata ajali…’akasema
‘Ehe…’nikasema
‘Mimi ninachozungumiza hapa ni tamaa ya mali,..kulikuwa na
njama za wawili hao, kumzunguka mwenye nyumba,… njama hiyo ilianzia hata
kipindi marehemu yupo hai, lakini marehemu hakulifahamu hilo,…’akasema
‘Njama gani labda labda…?’ nikauliza kwa mashaka, nikijua
fitina inaanza.
‘Kumfisidi marehemu,..wanawake wana maana hao, wewe
ulishauliza huyo mwanamke ni kabila gani kwanza, kabila hilo lina tamaa sana ya
mali…’akasema na mimi kiukweli sikuwa na mawazo hayo ya kikabila kabisa.
‘Mhhh..sijakuelewa…’nikasema
‘Sasa, sikiliza…lakini
sikuwahi kuona dalili ya mapenzi, hilo halipo, huyo mama, hana hiyo tabia
mbaya,…mimi naongelea hapa ni, tamaa tu, …shemeji mtu naye ana tabia hiyo,
kwahiyo wakakutana watu wawili wenye hulka sawa, …sisemi kabla tu linaweza kuwa
na hulaka hiyo, maana shemeji mtu yeye sio kabila hilo…’akatulia
‘Ok, endelea…’akasema
‘Shemeji mtu yeye, naye ..unajua kazi yake tena, ni ya tamaa
, tamaa…wewe unawafahamu madalali walivyo,..ghilina nyingi tu, akamuingia huyo
mama kwa lugha tamu, na mama bila kujitambua akaingia kwenye kingi…’akageuka
nyuma kaam kuogopa kusikiwa.
‘Sasa..mungu hamfichi mnafiki,..huyo mama kasoma
kweli,lakini akili ..siwalaumu, sio wote, lakini hawa akina mama, wengine
hawaoni mbali,… taama ya kutokuona mbali,akawa amekubaliana na shemeji mtu,
mengi yamefanyika humo…utayasikia mwenyewe ukiwa mjanja…na kwa vile sasa
hawaelewani kivile kwasababu wamedhulumiana, ni rahisi kugundua zaidi.’akasema
‘Mhh…siwezi kukuamini sana…’nikasema
‘Sio lazima uniamini, ila kwa vile ..nimekuona wewe ni mtu
mwema, unataka kuufahamu ukweli kiundani, endelea kuwahoji,…hii nyumba inapigwa
mnada,..kisa ni nini, eti ni deni, marehemu alikuwa sio mtu wa kukopa
yule..hilo deni limepikwa na wawili hao…chunguza mwenyewe utakuja kufahamu huo ukweli…’akasema.
‘Una uhakika gani na hayo maneno yako…?’ nikamuuliza.
‘Uhakika…nimekuambia mimi nilikuwa nashindwa hapo, ..wakati
mwingine nipo nje, napaka rangi nyumba, jamaa anakuja, wanaongea, msikio hayana
pazia,….kiukweli iliniuma, lakini, mungu yupo..sasa tatizo jingine huyo
mwanamke hakuwa kamfahamu huyo shemeji kuwa, huyo ndugu ni…hahaha, haaminiki,..mwenzake
alimtega, na sasa atakosa yote, dhuluma haina maana kabisa…na ipo siku dhuluma
yao itawatokea puani…’akasema
‘Una uhakika na hilo unalolisema, maana nijuavyo mimi, huyu
mama anahangaika kutafuta haki za watoto wake, atafanyaje ujinga huo, na
kuwaumiza watoto wake mwenyewe, hili haliingii akilini,, na huyo shemeji yake
atafanyaje jambo kama hilo kumharibia kaka yake..usije ukawa umesikia tu, au
kuhisi tu…’nikasema.
‘Hahaha…wakati wanafanya hayo, mke anawaza kujiwekezea hata
likitokea lolote awe na mali yake mwenyewe,…alishaona mume kabobea kwa ndugu
zake zaidi, mume hamuweki mbele mke kwenye mali zake, unasikia,mke inamuuma,
lakini afanyeje,..'akatulia kidogo
'Sasa ndio sijui ni wazo lake au ni wazo la shemeji yake,
wakaja kupiga jambo..hilo jambo siwezi kukuambia…nahisi marehemu alikuja kugundua hizo njama, kuna
kipindi wanandoa hao walikuwa katika mgongano, wakayafukia kiaina,, ..sasa chunguza
kisa cha mgongano huo,ilikuwa ni nini...'akatulia
'Hicho kisa...huo mgongano, sema, unajua tena kuogopakuingilia mambo ya watu, nilitaka nimtonye marehemu,...ila wewe, ukitaka ukweli anzia hapo, mwenyewe utakuja kuniambia…'akatulia
'Sasa
, kama mambo yangeenda vyema, kukawa hakuna kugeukana,...huyo mke angekuwa na mali yake, na shemeji mtu na mali yake, wanamfisidi marehemu…lakini mungu ana yake, kijana wangu katangulia mbele ya haki,...watakula wapi tena.
'Iliyobakia sasa ni kugombea mali...wanandugu
wengine waliligundua hilo mapema, walisubiria hiyo nafasi,..., ndio maana wakakimbilia kuchukua mashamba yote,
kumkomoa huyo mwanamke, na shemeji mtu si mjanja, akapata chake, mwanamke akakosa kote…sasa kipo wapi, ..haya nyumba nayo, ndio hiyo tena, kuna jambo humo….kuna mambo humo..’akasema
akinyoshea kidole nyumba.
‘Ina maana huyo ndugu mtu na ndugu zake sio kitu
kimoja,..au..?’ nikauliza
‘Huyo ndugu mtu, ndumila kuwili, mjanja sana, mtoto wa mjini…,
anakula huku na kule…achana naye kabisa, nawafahamu wote hao,…hahaha, eti nini…hahaha,
tuyaache hayo, kama upo karibu na huyo mama, mbane vizuri, utakuja kuugundua
ukweli wote wewe mwenyewe, ..'akanisogeela karibu, kama ananing'oneza.
'
'Ukweli ni kwamba mbele ya mali,..eeh, mali ni fitina,...binadamu sio watu wazuri, angalia sana hilo, kama kweli wewe ni mtetezi wa wanyonge, ..eeh, nimesikia hivyo kuwa wewe unafanya hivyo..au sio.'akanikodelea jicho.
'Mhh...'mimi nikaguna tu
'Si ndio hivyo,...sawa, hata hivyo,... hata sijui kwanini nimekuambia hayo, ila moyo wangu utafurahi, kama kuna mtu anataka kuutafuta ukweli, ili haki ije kutendeka kwa ajili ya marehemu, na watoto wake, lakini sio kwa huyo mwanamke au huyo shemeji mtu, watu wabaya sana hao…’huyo akaondoka zake
************
Mimi nikasogea hadi
kwenye hiyo nyumba, nikaingia ndani, hali ilikuwa kama siku ile, watu wanafika,
wanakagua nyumba wanaondoka, japokuwa sio kwa wingi ule wa siku ile,…na tangazo
bado lilikuwepo.
Nikamkuta huyo mama, yupo anafanya fanya usafi kwa nje…aliponiona
akashtuka kidogo, akaacha kile alichokuwa akikifanya na kunikaribisha ndani.
Nilimkagua usoni,, sikuona bashasha za
ukarimu, ni kama vile anashindwa kuniambia tu ondoka….na mimi sikujali,
nikawaangalia watoto, walikuwa wamekaa chini wanachezea vitu,…na nafsini nikawa
kwenye kuomba kinga ya mola wangu na majanga,…na maneno ya yule mzee yakawa
yananitawala nafsini mwangu;
Baadae shemeji akaja na kukaa, kunisikiliza….
‘Shemu, kiukweli hali yangu ilikuwa mbaya, nilijiona kabisa
naelekea kuzimu, na kwa ushauri wa docta, nikaenda kumuona mtu mmoja wa dini
akanisaidia…na baada ya hapo, nilijiwa na wazo kuwa hili jambo kama ulivyotaka
basi tuliache tu, kwa masilahi ya afya za watoto…’nikatulia na yeye hakusema
neno, akawa kainama chini.
Baadae akainua kichwa,..niliona machozi yakimtoka,
sikumuelewa hapo, nikawa nimemuangalia tu, akasema;
‘Sijui…niende wapi,…sijui ni nani anaweza kunisaidia,…sijui
kwanini imekuwa hivi…ina maana watachukua haki ya watoto wangu, sasa nitafanya
nini tena, lakini mungu yupo, kama ni kwa mapenzi yake iwe hivyo, nitafanya
nini, na..pia kama ni kwa mapenzi yake dhuluma hii ikome,nitashukuru pia,…oh, sawa
hamna shida…’akasimama ;
‘Shemeji nisikiliza kwanza…’nikasema
‘Hapana wewe unaweza kuondoka tu, sio kwamba nakufukuza,
hapana, ila mimi nina kazi nyingi za
kufanya, …kupanga panga vitu , na kuona wapi nikaviweke, kabla ….si ndio hivyo,
kesho hao watu wanakuja kupiga mnada au…?’
akauliza
‘Shemeji, sijamaliza kukueleza nilichotaka kukuambia, hebu
nikuulize shemeji yako alishafika mkaongea naye …’nikasema
‘Bado, …hajafika bado….’akasema
‘Sasa ni hivi shemeji, ….nilitaka…’nikasema na yeye
akanikatisha kwa kusema;
‘Nimeshakuelewa ….najua, kwa hali uliyokutana nayo, hutaweza
kufanya lolote tena, au sio, na kwa vile mimi nilishakubaliana kuwa haya
tutayamaliza kinyumbani, na kinyumbani ndio hivyo, shemeji alishanishauri kuwa
tuache nyumba ipigwe mnada tu,….hamna shida, unajua shemeji..hata ingelikuwa
mimi, nisingeliteseka kwa kitu kisichowezekana au sio…’akasema
‘Sikiliza shemeji …’nikasema
‘Nimekuelewa,……na kutokana na hali za watoto,
basi,iliyobakia tunyoshe mikono juu, au sio…’akasema
‘Hapana…baada ya kufikiri sana, kuna hali ilinitokea,
nilihisi taswara ya wewe na watoto wote mnalia, ..mnalia nini,…’nikatulia
kidogo.
‘Kilio chenu kinaashiria kuwa mimi nimewaacha,.. ni njozi
ilinitokea wakati nimelala, hata kabla….ina maana wakati unanipigia simu
nilikuwa ndani ya mapambano ya kufikiria, nifanye nini sasa….’nikasema
‘Sawa…nimekuelewa, hamna shida..’akasema
‘Nataka nikuulize maswali, majibu yake yatanisaidia
kuamua…’nikasema
‘Maswali gani tena shemeji, unataka kuanza tena …?’ akauliza
sasa akinishangaa
‘Hebu kwanza,
nikuulize, ulipoweza kufika benk uliona
jinsi gani huo mkopo ulifanyika, walikuonyesha huo mkataba, na ukasoma maelezo
yake, je ndani ya hayo maelezo kulikuwa na nini, je huo mkopo ulitolewa kwa ajili gani hasa.., kufanyia
biashara, kujengea au kufanyia kazi gani, …?’ nikamuuliza, alikaa kimia kwanza
bila kunijibu nikajua labda hataki kuongea tena, na ghafla akasema
‘Mhh, huo mkopo …walisema ulichukuliwa kwa mambo mbali
mbali, ikiwemo biashara,…hiyo biashara ni kwa ajili ya marejesho,…na haukuweka
vikwazo kuwa uwe kwa ajili ya biashara tu, kwa vile mkopaji ana dhamana
thabiti, basi, ….banki wao walikubaliana awe anachukua hadi kiwngo
fulani,..baadae kikawa kinaongezeka…sikuendelea kusoma zaidi kwakweli…’akasema
‘Kwahiyo unasema kuwa
mkopo haukuwa na kiwango….pesa inachukuliwa na kuna marejesho pia, au sio…na
marekesho yake ni kutokana na biashara aliyokuwa akifanya mume wako, ya halali,
au sio…, na dhamana ya mkopo huo, ikawa ni nyumba, au sio..hayo yote uliyaona au
sio?’ nikauliza
‘Ndio…..’akasema
‘Sasa kama sikosei, kuna sehemu awali ulisema mkopo huo
uliendelea hata baada ya mume wako kufariki, au..?’ nikauliza
‘Ndio..lakini…’akataka kutoa maelezo.
‘Ina maana shemeji yako aliendelea kuchukua pesa benki,…,
kwa ajili ya matibabu yako..?’ nikauliza
‘Ndio, yeye aliniambia hivyo, ….’akasema
‘Shemeji…. ukiwa na maana huyu aliyechaguliwa kuwa msimamizi
wenu…?’ nikamuuliza kuwa na uhakika zaidi
‘Ndio, yeye ndiye angeliweza kufanya hilo…., huyo aliyechaguliwa kama msimamizi wa mali ya
marehemu mume wangu…’akasema kabla hajatulia nikauliza swali la haraka haraka
‘Ulisema yeye alichaguliwa kuwa msimamizi wa mali ya
marehemu mume wako wakati wewe hujitambui au sio na baadaye ulipoanza
kujitambua mkawa mnashirikiana naye au sio?’ nikamuuliza
‘Ndio kama nilivyosema awali, kipindi hicho, nilikuwa
sijiwezi, sikuwa na utambuzi mnzuri,
nilikuwa kama maiti tu,….wanasema nilikuwa kama nimechanganyikiwa siongei, nipo
nipo tu, na nikiongea naongea mambo ambayo hayaeleweki…ni baada ya kuondokana
na ile hali ya `kuparalaize,’ na akili kunirejea tena,….kwa shida shida, maana
yameshakufika utafanyaje…..nilianza kupambana na hali yangu…’akasema
‘Kwahiyo hukuwa unaweza hata kuandika au sio………?’ nikauliza
‘Ndio…kwa kipindi kile…sikuweza hata kuinua mkono,….ulikuwa
mwil kama sio wangu….’akasema
‘Sasa kuhusu huo mkopo, ujuavyo wewe, kama ulivyoona, au kama
ulivyoanza kufuatilia, ni lini aulianza rasmi, …?’ nikauliza
‘Mhh…hilo sikuweza kuliona, maana walinipatia statement ya
karibuni, ila kunaonyesha kuwa kuna deni lilitoa kabla ya hapo,…’akasema
‘Na kwa maelezo yao, pesa ilikuwa inachukuliwaje, kwa kila mwezi, au mara kwa mara na kwa kiwangoo
gani, ni kiwango kile kile au kuna utofauti wa kiwango… maana nauona utakuwa ni mkubwa sana …’nikasema.
‘Hilo ndilo lilinifanya ning’ake, kwanini wamemsinginizia
mume wangu kuwa yeye ndiye aliyeanzisha hilo deni, na …nakuanza kukopa, huko benki
hata kabla hajafariki, …kwa shida gani tulikuwa nayo, na kwanini hakuaniambi,
hapo ndio sijakubaliana nao…na deni lenyewe ni kubwa, sio deni dogo, kipindi
chote tupo na mume wangu hali ilikuwa nzuri tu, maisha mazuri, kwanini aende
kukopa….’akasema.
‘Hayo uliyajulia huko benk, wao ndio walikuambia,, yaani wao
ndio walikupatia maelezo zaidi au ni kwa kusoma ule mkataba….?’ nikamuuliza
‘Siku nilipoamua kufuatilia, niliambiwa deni hilo ni la siku
nyingi, limeanzia kipindi mume wangu akiwa hai, na kumbukumbu zinaonyesha hivyo,
alikuwa anachukua anarejesha, ni statement ya benk inaonyesha hivyo, na
anachukua kiasi kikubwa, au kidogo,…na akirejesha, hakamilishi, inabakia
salio…salio likawa linakua…’akasema
‘Nauliza hivyo, aliyetoa hiyo kauli kuwa mume wako ndiye
alianza kukopa, ni nani..?’ nikamuuliza
‘Ni watu wa benk….’akasema
‘Hapo sasa tunakwenda sawa, watu wa benki ndio waliokuambia
hivyo au sio….’nikasema
‘Ndio hivyo….’akasema kama vile anajua nimemalizana naye,
nikamuuliza
‘Nirudi nyuma kidogo, …ulifanya yote hayo , kufuatilia, ni
baada ya kwenda mahakamani kufuatilia ili kuweka pingamizi si ndio hivyo…au ulikwenda kuangalia hilo
deni, hata kabla hamjakwenda mahakamani…?’ nikauliza
‘Ndio hivyo …..nilipopokea hiyo barua ya kuwa nyumba
itapigwa mnada deni lisipolipwa, …nilichanganyikiwa kabisa, sikujua ni deni
gani, na kipindi hicho shemeji alikuwa hayupo kasafiri sehemu ya mbali na
hatarajii kurudi karibuni, nikaonana na mtu ninayemfahamu, yeye ndio
akanisaidia, tukafungua pingamizi,…na ndio nikaamua kwenda benki kabla ya
kwenda mahakamani…’akatulia.
‘Ok, ikawaje…?’ nikauliza
‘ Basi nilipofika ndio nikaonyeshwa na kupewa maelezo
kidogo, awali walisema nije kwanza na muhusika, aliyekebidhiwa, lakini baada ya
kujielezea kuwa mimi ni mke wa marehemu, wakathibistiha hilo, basi ndio,
nikapewa maelezo …’akasema
‘Ikawaje..?’ nikamuuliza
‘Nilishindwa nifanyaje,..nikaona nimsubiria shemeji aje
kwanza,..katika kuhangaika nikakutana na rafiki yangu mmoja akaniambia, ni
muhimu twende mahakani iwekwe pingamizi…alipofika shemeji nikamwambia hilo.
Yeye akasema sawa….’akatulia
‘Ndio hivyo tukafika mahakamani kabla ya kesi, kuna
kusikilizwa kwanza, nikaambiwa nipeleke
vielelezo vya kusaidia hilo….nikauliza vielelezo gani…?, wakaniambia vya kuthibitisha madai yangu…sasa
hapo…uone, mimi ningevipata wapi hivyo vielelezo…’akatulia
‘Ndio nikarudi kwa huyo rafiki yangu akanishauri niende
benki, na ndio nikakutana na hiyo kauli, kuwa hilo ni deni ni la siku nyingi….halikuwahi
kulipwa kutokana na makubaliano,…kuna mkataba wa mkopaji na benki ulitaka deni hilo lilipwe kwa kiasii fulani
kila baada ya muda fulani, lakini haikuwahi kulipwa….,
‘Nikaomba tu nipewe hiyo statement,ili niweze kuipeleka mahakamani …ndio wakanipatia kwa haraka
nikarudi kule mahakamani, nikaambiwa
hiyo haitoshi, natakiwa nakala ya mkataba, hati za malipo na vitu kama vitatu
hivi,……ilikuwa kazi kuvipata kwa watu benki, maana ilibidi nirudi tena
mahakamani wanipe barua, ndio nikarudi tena benk wakanipatia…..’akasema
‘Na muda wote huo mnaongozana na shemeji yako…?’ nikauliza
‘Ndio…’akasema
‘Kwahiyo ndio ukagundua kuwa deni hilo ni la siku nyingi au sio, kama ni la siku
nyingi ni kwa muda gani, ni kipindi gani,…ina maana ni kipindi mumeo yupo,…na
kwahiyo haina shaka, ni kweli mume wako analifahamu hilo deni..’nikasema na
kabla sijaendelea akanikatisha kwa kusema;
‘Mume wangu hajachukua mkopo…nimeshakuambia unielewe, mume
wangu hakuwahi kuchukua mkopo, huo ni uwongo….’akasema kwa hasira,
‘Lakini huwezi jua, yawezekana mume wako alichukua mkopo huo
kwasababu ya kupanua biashara, hakutaka kukuambia hilo, sizani kama benki
wanaweza kutoa kitu cha uwongo…, hebu nikuulize wewe una uhakika gani kuwa mume
wako hakuwahi kuchukua huo mkopo,…. ?’ nikamuuliza
‘Nina uhakika, kwa hilo na kamwe sitokubaliana nalo kabisa,
….hebu jiulize yeye kila siku alikuwa akinikanya nisije nikachukua mkopo wenye
riba…na huo mkopo wa benk unaonyesha riba,…na wanasema kila mara wanatoa
statement ya kuonyesha hilo deni, mimi sijawahi kuiona hiyo humu ndani, ina
maana alikuwa akiweka wapi….’akasema
‘Ina maana wewe kila kitu cha mume wako, mambo ya biashara ,
na mambo mengine yote ulikuwa unayafahamu…?’ nikauliza
‘Kwa kiasi kikuba ndio, hakupenda kunificha jambo, biashara
zake zinakwendaje, hasara na faida, alikuwa ananishirikisha,na kwa vile na mimi
nafahamu mambo ya ofisini, huwa tunakaa pamoja kupanga matumizi,…na wapi pa
kupatia pesa za hayo matumizi, hajawahi kusema nimekwama hapa, ngoja
nikakope,..hajawahi hata kuniomba na mimi nichangia matumizi ya
nyumbani,…’akasema
‘Hebu nikuulize , huko benki walipokupatia hizo hati, hivyo
vielelezo, si vyote vinaonyesha sehemu
mume wako alipoweka sahihi yake…hata kwenye mikataba ya deni hilo,kuna sahihi
yake au sio, je nyaraka zote hizo uliwahi kuziangalia kwa
makini, hukuona sahihi ya mume wako,…?’ nikamuuliza
‘Ndio….walinionyesha vyoye hivyo,….’akasema
‘Na sahihi ya mume wako unaitambua vyema,….?’ Nikamuuliza
‘Ndio …naitambua vyema…’akasema
‘Na kwenye mikataba hiyo, uliona sahihi kuwa ni yake au
sio….?’ Nikauliza
‘Ndio ni sahihi yake…ndio hapo nikachanganyikiwa, lakini
haiwezekani, sio yeye, siamini kabisa….na kingine kwenye hilo deni jipya eti na
mimi nilihusika nikaweka sahihi yangu…sikumbuki kufanya hivyo, ila….’akasita
kidogo
‘Deni jipya, kwahiyo kuna madeni mawili, au zaidi ya hilo….?’nikamuuliza
‘Ni hivi deni hilo, sio la siku moja, linakua kila pesa
inapochukuliwa,…sasa deni hilo likaja kuongezeka hata mume wangu alipofariki,…lakini
baada ya kufariki, ilibidi kuwa na watu wapya wa kuendelea kuchukua pesa, na
utaratibu mpya, …shemeji akawekwa, na mimi, lakini mimi nilikuwa naumwa, yeye
kwa kibali cha benk akaendelea kuchukua pesa.
‘Ehee….hapo sasa….’nikasema
‘Hapo sasa ...una maana gani...?' akauliza
'Hapo ndio nataka kuelewa zaidi...'nikasema
‘Unajua labda hatuelewani…hiyo ni akaunti ya benki ya mume
wangu, kwenye hiyo akaunti, ndani yake kuna pesa zilichukuliwa kama deni, na sio mara moja,….pamoja na hayo, pia ni
akaunti yake ya pesa za biashara, kwahiyo kuna kuchukua na kurejesha,,…’akasema
‘Lakini sehemu hiyo ya mkopo, yaani pesa za mkopo si kuna
stakabadhi zake, …kuashiria kweli mkopo ulichukuliwa, ukaingizwa kwenye hiyo
akaunti, pesa ikawa inatumika, au sio…?’ akaulizwa
‘Ndio zipo….na pia, yeye eti kutokana na shughuli zake pia
aliomba awe anachukua zaidi ya salio lake, na kutokana na hiyo mikopo, ikawa
sasa inaonyesha, yeye anachukuza zaidi ya kuweka, deni linakua kila
siku,….kifupi hiyo ni akaunti yake endelevu, anachukua, anaweka, anachukua pesa,
anarejesha, cha ajabu , deni lilikuwa linaongezeka tu, kuliko
marejesho…’akasema
‘Kwa kipindi cha nyuma yeye alikuwa anaweka sahihi yake peke yake katika kuchukua pesa au sio, wewe
ulikuwa huhusiki, au sio…?’ nikamuuliza
‘Ndio…’akasema
‘Wewe ukaja kuongezwa na shemeji yako, na hyo ni kutokana na mujibu wa mirathi au sio kuwa wewe na shemeji mtu muwe wasimamizi wa mali ya marhemu, na wewe uliwekwa hasa hasa kwa ajili ya kusimamia, upande wa watoto..au sio?’ nikauliza
‘Ndio…’akasema
‘Lakini kwa vile ulikuwa unaumwa, wewe hukuwahi kuhusika, tokea awali au
sio..?’ nikauliza
‘Kuna sehemu wanadai na nilihusika,…baada ya kupata nafuu, lakini mimi
sikumbuki…kufanya hivyo,…’akasema
‘Una maana gani..?’ nikauliza.
‘Wanasema kwenye muendelezo wa hilo deni, sehemu za mwisho mwisho mimi nilihusika, …’akasema.
‘Kwa vipi…?’ nikauliza.
‘Wamenionyesha sahihi
yangu, kuwa niliweka sahihi, ya kuchukua pesa..na kweli sahihi yangu hiyo ipo..’akasema
‘Una uhakika ni sahihi yako…..?’ nikamuuliza
‘Ndio…’akasema.
‘Na je kwa kumbukumbu zako, shemeji yako akitaka kufanya
jambo wakati umeshaanza kujielewa, alikuwa akikushirikisha..?’ nikauliza
‘Mara nyingi, shemeji
alikuwa akija kwangu japokuwa sijiwezi kujiinua, baada ya kuanza kujitambua na
ananiambia anataka kufanya hili na lile, mimi naitikia tu kwa kichwa…maana
japokuwa nilikuwa sijiwezi kihivyo, kichwa kilikuwa kinaweza kutikisika, kuona,
kusikia…..’akatulia kidogo
‘Na kwa vile nilimuamini, na yeye ndiye aliyechaguliwa kuwa msimamizi wa kila kitu sikuwa na shaka
naye, na nilikuja kujua hiloo kuwa yeye ndiye msimamizi nilipojitambua,
walifika shemeji na baadhi ya ndugu zangu wakaniambia , kinachoendelea, nikiwa
kitandani, nikawaitikia tu kwa kichwa.
‘Na ndio nakumbuka pia, kuna kipindi alikuwa akija huku analalamika
kuwa hali ngumu, lakini akasema nisiwe na wasiwasi atajitahidi kuweka mambo
sawa….ni hivyo ninavyokumbuka mimi….’akatulia
‘Lakini hakuwahi kukuambia anataka kuchukua pesa benk ….?’
Nikamuuliza
‘Kwa hilo, hakuwahi,... sikumbuki kitu kama hicho, sizani,
labda kama aliniambia kipindi sijitambui…yawezekana, aliniambia kipindi hicho, na
huenda nikaitikia, lakini kusema kweli,
sikumbuki, na kwa vile alishapewa hayo mamlaka ya kufanya aonavyo ni sahihi,
labda alioona kuchukua pesa kama mkopo ni sahihi…’akasema
‘Kwa vile hukumbuki, yawezekana pia alikuambia uweke sahihi
ya mkopo, ukaweka, na umesahau kuwa ulifanya hivyo au sio?’ nikamuuliza
‘Hapana, hilo haliwezekani kabisa….nimejaribu kukumbuka,
..haijatokea, …wasinifanye mimi mjinga, na kwanini kama ni hivyo, anifanye
niweke sahihi kitu kama hicho, wakati anajua sijitambui…hebu kumbuka kipindi
hicho mimi ni mtu wa kulala….alinifanyaje mpaka nikaweka sahihi….mhhh, mimi
kwakweli hapo sikumbuki….sijui kwakweli..’akasema
‘Je unahisi shemeji yako anaweza kufanya hivyo, yaani
kufanya ujanja ujanja kwa nia mbaya ya kufisidi mali za ndugu yake , kwa
masilahi yake…kwa hisia zako tu,..?’ nikamuuliza, nahapo akabaki kimia kidogo,
na kwa muda huo mtoto wake yule mkubwa kidogo alikuwepo, akasema;
‘Mama muambie tu, baba huyu atatusaidia,…’akasema na mama
yake akamuangalia kwa sura ya kumuonya
‘Ukweli gani mtoto anataka uniambie,...shemeji ili niweze kulifanikisha hili naomba usinifiche kitu, mimi nipo hapa kwa nia njema kabisa, kwa hiyo usiogope, ..hayo ya
vitisho hayatatokea tena…’nikasema
'Sikufichi kitu....'akasema
'Na..kuna mzee mmoja jirani yenu, nimekutana naye hapo nje, mnafahamiana naye kivipi...?' nikauliza akawa kama kashtuka kidogo, halafu akauliza
'Mzee Mtupe au...?' akuliza
'Sikumuuliza jina lake....'nikasema
'Huyo mzee..kwani kakuambia nini...?'akasema na kuniuliza hivyo akionyesha uso wa mashaka;
NB: Hiki kisa kilikuwa hivyo, mwendo wa maswali na majibu,
ni kisa cha aina yake na ukweli ukaja kupatikana hivyo hivyo,msichoke…
WAZO LA LEO: Fitina
ni mbaya sana, usijaribu kurubuniwa, ili ujenge fitina , kwasababu ya masilahi
kidogo tu ya kukidhi haja ya tumbo lako, hujui hiyo fitina itakuwa na madhara
gani kwa jamii…neno dogo tu, au udanganyifu mdogo tu, unaweza ukafikia hadi
kuua, je huoni kuwa wewe ndiye utakayekuwa umeua….
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment