Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, May 30, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-5


‘Shemeji hapa kuna tatizo….’ Nilisema hivyo niliporudi ndani,

Kiukweli nilikuwa nikihema, maana nilikimbia nje nikazunguka sehemu zote sikuweza kumpata huyo mtu…na mtu wangu wa mitandao alinihakikishia kuwa huyo mtu aliyekuwa akipiga hiyo namba ya simu alikuwa maeneo ya hapo hapo alipopataja na akanitumia hata na ramani….sikumuona sehemu hiyo. Na baadae jamaa yangu akaniambia huyo mtu sasa ameshazima simu yake.

Kitu cha ajabu, nilipokuwa narudi, nilihisi hali ya mwili kuniishia nguvu…nahisi kama kuna watu wanaongea siwaoni,..ni hali ya ajabu kwangu, nikawa naomba duwa zangu tu, huku natembea, hadi nilipofika ndani, jasho linanitoka!

‘Ndio kuna tatizo umeona eeh, ..ulifuata nini huko nje…na umeonana naye?’ akaniuliza na hayo maneno nimeonana naye yakanifanya nimtupie jicho, maana nilitoka kwa haraka na sikumwambia naenda wapi.

‘Kuna mtu nilitaka kuonana naye huko nje lakini sikuweza kumpata…’nikasema

‘Ndio huyo mliyekuwa mkiongea naye kwenye simu…au sio?’ akaniuliza na hapo nikashtuka zaidi, maana japokuwa niliongea hapo, lakini hakufahamu kuwa namfuata huyo mtu niliyekuwa naongea naye kwenye simu, nikasema tu.

‘Ndio….’nikasema

‘Unajisumbua shemeji,…..unajua mimi nilihangaika sana, na cha ajabu kila nilichotaka kukifanya wenzangu walikuwa wakikifahamu, sijui kwa vipi, hata nikienda sehemu ya nje ….wanagundua tu…an hapa ulipotoka tu, nikahisi hiyo hali, na mtoto akawa kwenye hali mbaya, nika…ikabidi niwaombe wanisamehe...’akasema

‘Wakina nani sasa..?’ nikamuuliza nikiangalia huku na kule sikuona mtu

‘Naomba tu tuyaache haya, maana wamesema sasa hivi nikiendelea nitajuta, nisije nikawalamumu..’akasema

‘Akina nani hao…?’ nikauliza huku nikiendelea kuangalia huku na kule.

‘Huwezi kuwaona, mimi wamenifanya niwaone, ….ni ajabu kabisa, nawaona watu lakini wengine hawawaoni…’akasema

‘Sasa hivi wapo…?’ nikamuuliza

‘Siwezi kukuambia, kwa usalama wa watoto wangu…..’akasema,, hapo nikawageukia wale watoto, huruma ikaniingia, na kunifanya niwe njia panda, nidai haki yao, wapate shida, au niache kwa ajili ya usalama wao, kama alivyodai mama yao. Nilijua nikiacha, hawatapata huo usalama, nahisi itakuwa ndio mwanzo wa matatizoo makubwa zaidi ya hayo.

‘Hebu shemeji sasa niambie nilipotoka watoto walikuwaje, ni tatizo gani limewatokea…?’ nikauliza.

‘Hayo., tuyaache kama yalivyo…mimi naona niliyokuambia yanatosha,….’akasema akiwa anaangalia mbele kama anaona kitu cha kutisha.

Kwa hali kama hiyo nikaona niondoke kwanza, nione jinsi gani ya kusaidia, lakini bado nilikuwa sijaweza kupata mawasiliano na huyo mtu anayedai kuwa ndiye aliyeshughulikia hiyo kesi, nahisi yeye alikuwa akisubiria ujumbe wangu,

Nikamuangalia yule mama, ambaye kwa muda huo, alikuwa kainamisha kichwa chini, kwa haraka nikachukua simu yangu, nikaandika hivi;

’sawa nimekubali…sitisha hilo zoezi, ili haki itendeke..’nikaandika na kutuma, hutaamini, ilionyesha ujumbe huo umepokelewa.

Kwa haraka nikampigia mtu wangu wa mitandao, lakini cha ajabu siku ya huyo mtu wangu ikawa hapatikani…

Baadae nikapokea ujumbe wa maneno kwa namba ile ile, ukisema;

‘Nitajitahidi…niwezavyo, ila na wewe timiza ahadi yako,…nakupa siku tatu tu,…baada ya hapo tusije kulaumiana…’

Nikajaribu kumpigia mtu wangu wa mitandao, akawa hapatikani….nikaipiga hiyo namba, lakini ikawa inasema ‘haipatikani, jaribu tena baadae…’

Basi kwa vile nilikuwa na uhakika kuwa zoezi hilo litasitishwa, nikaona niondoke nirudi nyumbani , ili nijipange kwa mikakati mingine zaidi.

‘Sasa shemeji mimi naona niondoke, nirudi nyumbani mara moja,…nilikuwa na wazo, unajua kwangu kwa hivi sasa familia haipo, nipo peke yangu, kuna nafasi ya wewe kukaa na watoto kwa muda ni wazo langu tu,….kama upo tayari, tunaweza kuondoka nawewe, au…’akanikatisha

‘Siwezi kuondoka, bado kuna vitu vyangu humu ndani, kama unavyoona watu wanaingia na kutoka, wakija kuiba,…na zaidi mimi..nataka nithibitishe mwenyewe nyumba hii ikiuzwa, nataka …nione kama kweli mungu atanikubalia maombi yangu,..tumeambiwa duwa la mwenye kudhulumiwa linapita bila kipingamizi, …nataka nione,….nataka….’hapo akawa kama anataka kulia.

‘Hii nyumba haitauzwa,..unasikia shemeji..niamini mimi, hii ni haki yako wewe na watoto wako, kama kweli ni haki yako, haitauzwa,…unasikia,…niamini mimi…mungu yupo pamoja na wewe…’nikasema na akainua uso, kuangalia mbele nahisi aliona kitu. Mara akasema;

‘Wanacheka kwa dharau…’akasema na mara akainama kama anahisi maumivu,

‘Waache wacheke,…watakuja kulia…upo sawa lakini mbona hivyo…’nikasema na mara nikahisi masikio yangu yakizizima, yakilia nziiiiiiiii…ile hali ya kuumiza masikio, nikawa naomba duwa, lakini hali ikawa mbaya, nikawa najisikia vibaya,....haikupita muda, nikapoteza fahamu.

Nilizundukana,…

Nashangaa  nipo nyumbani kwangu…kwenye sofa la varandani, nimelala…

**************
Nilishangaa, nimefikaje hapo nyumbani kwangu..unajua awali nilihis kama nipo kwenye njozi, na wakati nawaza hivyo, mara akatokea yule mama, akiwa na watoto wake, wakanisogelea;

‘Nimefikaje hapa…?’ nikamuuliza

‘Ilitakiwa uondolewe hapo kwenye nyumba, la sivyo wangekuua….’akasema

‘Akina nani hao shemeji, niambie ukweli,…na umewezaje kupafahamu hapa nyumbani kwangu, wakati sikuwahi kukuelekeza…’nikasema na hapo akawageukia watoto wake na kusema

‘Siwezi kukuambia kwa ajili ya usalama wa watoto wangu…kwa jinsi gani nimeweza kufika hapa kwako kuna mtu anapafahamu hapa kwako ndiye tulikuja naye…’akasema.

‘Nani…!?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Ulipopoteza fahamu nilitoka nje kuomba msaada, bahati nzuri walikuwepo watu, wakaja ndani, na mmojawapo akasema anakufahamu, na wapi unapoishi, ndio nikamuomba tukuchukue….’akasema

‘Na usafiri, alilipia nani…?’ nikamuuliza

‘Huyo huyo mtu…’akasema

‘ Ni nani huyo…?’ nikauliza sasa kwa mashaka

‘Mimi simjui….ila nikaona nije na watoto wangu, kama ulivyosema, lakini nitakaa kwa leo tu, kuangalia hali yako, nimekuona wewe ni mtu mwema,…na pia nina mashaka ya watoto wangu , baada ya hili tukio, ninahisi lolote laweza kutokea,..je wakianza kuumwa, sitaweza kuwahudumia peke yangu…’akasema.

‘Sawa, basi,…jisikie upo nyumbani, jikoni umepaona….?’ Nikauliza

‘Ndio…nimepika hata chakula samahani kwa kuingia jikono kwako….’akasema

‘Ahsante…umefanya la maana , maana hata mimi hapa nahisi njaa…’ nikasema na yeye akaenda kuandaa chakula, nikabakia nikiwaza sana,…na mambo mengi yanatokea,…yenye utata,..nikiangalia saa, ni kama masaa zaidi ya matatu yalishapita tokea nipoteze fahamu, hadi kuletwa hapo nyumbani.

 ‘Hebu kwanza nikuulize hili, baba wa hawa watoto alikuambia nini kuhusu hiyo nyumba yenu…?’ nikamuuliza

‘Kuniambia nini….aah…?’ akaniuliza sasa akionyesha kuchoka, nahisi hakutaka haya mambo yaendelee zaidi.

‘Ni lazima kuna kauli aliwahi kuzisema, nahitajia kusikia zaidi kauli zake….ambazo naweza kuzitumia kama ushahid …achilia mbalia ushahidi mbele ya mahakama, lakini kauli za kunithibitishia mimi,  ili niwe na uhakika na ninachotaka kukifanya…’nikasema

‘Unataka kufanya nini tena shemeji,…?’ akaniuliza

‘Kinachowezekana….’nikasema

‘Kikubwa alichokuwa akinisisitizia mume wangu ni kuwa, hata kama yeye akitangulia mbele za haki , nisije kuiuza hiyo nyumba….’akasema.

‘Kwanini alisema hivyo, uliongea jambo la kutaka kuiza au…?’ nikauliza.

‘Hapana…yeye alikuwa akiongea hivyo tu,…alisema hiyo nyumba ni mali ya watoto wake na vizazi vijavyo,…alikuwa na ndoto za ajabu, yeye aliwazia mpaka vitukuu, kuwa wao wakizaliwa, wake kuikuta hiyo nyumba ikiwa bado imara, wamkumbuke kwa hilo…uliona ilivyojengwa ipo imara kabisa, lakini sasa nifanyaje, nimeshindwa kutetea kauli yake….’akasema

‘Daah…’nikasema hivyo huruma ikizidi kuniingia…huku nahisi kichwa kikiniuma sana.

‘Unajua ni kama vile mume wangu alifahamu kuwa ana—ondoka, kutokana na kauli zake, tukiwa wawili anaongea maneno kama  hayo ….oh…’akatulia

‘Kwani alikuwa anaumwa, ..na sijakuulizia zaidi …nitakuja kuyaulizia, hayo, alifariki vipi,…ila kwa sasa, niambie Maneno gani aliongea…?’ nikamuuliza.

‘ Si ndio hayo, ya kuniambia kuhusu nyumba, kuhusu watoto wake kusoma, alisema nyumba isije kuuzwa, sijui kwanini alipenda kulisisitizia, hilo, na akasema anataka watoto wake wasome sana, maana mali anayo, mashamba…kwahiyo hakuna shida,…na alitaka  watoto wake wasikae mbali na nyumba, alifikia hata kusema hata wakioa, waje kuishi humo humo, labda wapendewao wenyewe  kuondoka….’akasema na kutulia na kabila sijasema kitu, akaongezea maneno haya;

‘Utafikiri alijua atatangulia yeye…..’akasema hivyo na kutulia , tukawa kimia kwa muda, kila mtu akiwaza lake,…baadae nikasema

‘Na  unasema hakuwahi kukuambia kuwa nyumba hiyo kaijenga kwa deni…kwa mkopo wa benki..labda sio yote lakini katika kuikamilisha?’ nikauliza

‘Hahaha,… hilo hata mahakamani, waliliulizia na hakuna ushahidi huo,…waliona kuwa kweli nyumba hiyo ilijengwa kihalali, na sio kwa mkopo,…’akasema

‘Ok,… kwahiyo huo mkopo, hautokani na ujenzi wa nyumba kabisa, …’nikasema hivyo kama kuuliza

‘Ndio….’akasema

‘ Je huko mahakamani uliwaambia kuwa kuna kauli za marehemu za hivyo kuwa nyumba yake haitakiwi kuuzwa, walisemaje…?’ nikamuuliza, huku nikiangalia saa

‘Hayo yote niliwambia, lakini si maneno matupu, na yatasaidia nini, kama upo ushaidi kuwa eti yeye alikopa na akaweka nyumba kama dhamana,….’akasema

‘Na ndugu zake…’kabla sijauliza akasema

‘Naomba ….unielewe hapo, haya pia niliwaambia hao ndugu zake hata kabla ya hayo mahakama kuanza…ndio maana na wao wakasema watajitahidi kadri ya uwezo wao kulitetea hilo…lakini kwa vipi, hata wao, walisema hivyo, kuwa je maneno matupu yatasaidia nini…ndio hivyo..’akasema.

‘Oh hapo sasa nashindwa kuelewa, kama ndugu zake walikuwa upande wako kuhusu hilo, ni nani yupo nyuma ya hilo deni….’nikasema hivyo tu.

‘Hata mimi nashindwa kuelewa….’akasema

 ‘Hebu nikuulize sasa, wakati mlipokwenda mahakamani, ndugu za mume wako, wakati wanatetea walikuwa wakitoa kauli gani, za kuonyesha kuwa walikuwa upande wako, maana kwenye mashamba, si mlifikishana hadi mahakamani, ukashindwa,..?’ nikauliza

‘Kwenye mashamba wao, walikuwa washitakiwa, kwahiyo walikuwa upande wao, na mimi upande wangu …na niliposhindwa, walikuja wakaniambia kuwa hayo yamekwisha kwa vile mimi nilikuwa natafuta haki kama kweli imetendeka, kwahiyo tusameheane, na tuendelee kuwa kitu kimoja…’akasema.

‘Mimi bado hapo sijaelewa…kama walikuwa upande wako,…ni nani alithibitisha ukweli wa hayo madai , kuwa kweli mkopo huo aliuchukua mume wako, …?’ nikamuuliza

‘Sana sana…ni benk,…nyaraka zao…..na….hasa mkataba, kuwa kweli aliingia mkataba wa kuchukua pesa kwa mkopo….’akasema

 ‘Ina maana kati ya hao ndugu zake, hakuna hata mmoja aliyesema kuwa …anajua lolote kuhusu kuwepo kwa  huo mkopo….?’ Nikauliza.

‘Aliyesema ….kuwa alikuwa anafahamu kuhusu huo mkopo wakati mume wangu akiwa hai, hakuna… ila aliyekuja kugundua ….na ni baada ya kupokea barua kutoka benk, ni……shemeji ambaye ndiye kakabidhiwa hii familia….’akasema

‘Haiwezekani..kumbuka awali uliniambia kuwa, kaka yako aliwaamini sana ndugu zake, na alikuwa akiwashirikisha kwenye mambo yake kama familia,..iweje deni kubwa kama hilo asiwaambie ndugu zake..?’ nikamuuliza

‘Waliulizwa hivyo mahakamani, wakasema, wao hawakuwahi kuambiwa, au kusikia, ….na inawashangaza hata wao kuona kuwa kaka yao alichukua mkopo mkubwa hivyo, akaweka dhamana ya nyumba,… ila wao walisema kama angelikuwa hai, asingelishindwa kulilipa hilo deni kutokana na shughuli zake….’akasema

‘Ingelikuwa mapema, ningelienda moja kwa moja benk, lakini sitaweza kuongea nao, maana sina kibali cha kuniruhusu kuulizia mambo yenu ya kibenk,….mimi sio muhusika,  na kwahiyo sina namna nyingine, inabidi nije kuongea na shemeji yako.

‘Wewe ina maana bado hujakata tamaa…!!’ akasema kwa mshangao.

‘Kwanini nikate tamaa, hili lililotokea kwangu na hayo mengine yanathibitisha kuwa hayo yaliyotendeika na yanayotendeka, sio halali, kama yangelikuwa ni halali, hayo yote yasingelitokea, wewe hulioni hilo shemeji…’nikasema

‘Mimi ninajua yote sio halali, lakini sina uwezo wa kuthibitisha madai yangu, nitathibitishaje….’akasema.

 Nikachukua simu yangu na kujaribu kuipiga ile namba ya huyo mtu asiyejulikana, …akawa hapatikani, ..nikajaribu kuwapigia wale mawakili wawili, simu zao muda wote zinasema zinatumika,…nikaona kwa siku hiyo siwezi kufanya lolote..na hali yangu kiafya ilikuwa sio nzuri,mwili ulikuwa hauna nguvu kabisa, kichwa kinaniuma. Ilifikia kama kutaka kupoteza fahamu tena.

‘Mhh…hii ni nini, sijwahi kuumwa hivi kabla…’nikasema na huyo m-mama, akaniangalia kwa mashaka.

‘Pole…’akasema hivyo tu

**********

Familia hiyo kwa siku hiyo ilikaa kwangu, lakini wakasema kesho yake watarudi nyumbani kwao, kuona kama kweli hilo zoezi litafanyika au la… na usiku huo tuliongea kidogo, ,…

 ‘Shemeji Ili niweze kufanya jambo, nakutegemea sana wewe,kwanza ni maelezo yako, na unitajie kila mtu aliyehusikana na hiyo kesi yenu…, usichoke na wala usiogope …’nikasema na kwa muda huo mtoto yule mdogo akawa analia sana usiku huo…

‘Kwanini analia hivyo, au kuna sehemu inamuuma,…je huwa analia hivyo mara kwa mara…?’ nikauliza

‘Ndio hivyo, akianza kulia, …ujue kuna tatizo linakuja,…au ni ujumbe umetumwa, nisubiria neno, …wananitesea watoto jamani…kwa hivi sasa nahisi ni kwa vile nimetoa kauli ya kutaka kuendelea na hiyo kesi,…’akasema.
‘Hujatoa lakini…’nikasema hivyo, nikijaribu kusimama….nilishindwa, nikasema

‘Hebu mlete huyo mtoto hapa…’nikasema, na akamlete pale nilipolala…

 Nikamshika kichwani…, nikakumbuka namna ya kumsomea mtu kama kuna hali isiyo ya kawaida, nikawa nasoma…kimoyo moyo….na mara akatulia kulia, na baadae, akaonekana kulala, na baadae wanafamilia hao wakaenda kulala.

‘Ingieni chumba hicho, natumai kila kitu mtakikuta huko…’nikasema nikiwaelekeza chumba cha kulala

Kiukweli moyoni , japokuwa sipendi sana kuamini haya mambo, lakini kwa hali jinsi ilivyo, nikajua sasa napambana na watu ambao silaha yao ni nguvu za giza.

************

Kumbuka hapo tunakimbizana na muda, kama hiyo kesho huo mnada hautafanyika, basi huenda kesho kutwa, au siku yoyote hilo zoezi litafanyika,….usiku huo sikuchoka kujaribu kumpigia simu yule jamaa, na mawakili walioshiriki kwenye hiyo kesi, lakini simu zikawa na majibu yale yale…

Mimi niliona jambo jema nikuongea na wakili aliyeshughulikia hiyo kesi,..ili aweze kuweka pingamizi la huo mnada kufanyika, lakini yote yategemea ni nini waliandikishana….., japokuwa nakumbuka nilipoongea na huyo mama kabla hajaenda kulala, alisema hivi

 ‘Tulifanya hivyo sana,..pingamizi, pingamizi… lakini ikafika sehemu hata huyo wakili akafikia kusema, shemu, haya kayamalizeni kinyumbani, muone mtafanya,…’akasema nikamuuliza

‘Je banki watakubaliana na hilo…akasema wao kama wao, watafuta sheria zao, muhimu ni nyie make muone mtafanyaje, kama kuna namna ya kupata pesa,….muongee na benk muendelee kulipa kidogo kidogo…’akasema

‘Ikawaje sasa….?’ Nikauliza

‘Hizo pesa za kulipa kidogo kidogo ningezipata wapi…..’akasema

‘Kiukweli huyo wakili alisema hivyo, baada ya kuona watoto wangu wanateseka,..na wakatii huo mimi sina ushahidi wowote wa kunisaidia…’akasema.

************

Kesho yake hali yangu ikawa mbaya zaidi, na usiku huo, nikawa nalala nikiota marue rue, nakabwa, yaani ni shida, asubuhi ilifika, hata kuinuka kitandani siwezi, nilijaribu kuomba  duwa,…nikanywa na dawa za mauimivu, lakini hali haikuniwezesha kabisa,…na shemeji akaja kunijulia hali, akitaka kuaga kuwa anarudi nyumbani kwake.

Nilijitutumua ili asione kuwa nimezidiwa kihivyo….

‘Sasa shemeji…japokuwa naumwa…lakini bado…nataka kuwasiliana na hao watu, na nitajitahidi nionane na shemeji yako..na hao mawakili, hata kama ni kwa kukodi gari..najua haya ni mazingaumbwe wananifanyia…mimi siumwi kihivyo….’nikasema.

‘Achana na hii kesi, kwanza wewe sio wakili,…sio ndio hivyo…?, je …una nguvu gani za kisheria zaidi za kutengua nguvu ya mahakama, na angalia afya yako, usinione hivi shemeji, nimepambana sana, nimejaribu kila njia, na mpaka imefikia kukata tamaa, ujue…mimi wananifahamu , sio mtu wa kushindwa kirahisi, lakini kwa hatua ilipofikia, sioni sababu ya kuendelea…kwanza sina pesa…’akatulia

‘Kwahiyo huku nyuma watoto walikuwa hawana matatizo kama hayo yaliyoanza kutokea baadae…?’ nikamuuliza kujaribu kuona ni jinsi gani inavyotokea kwa watoto wake

‘Hawakuwa nayo, walikuwa na afya zao nzuri kabisa, hasa kipindi baba yao yupo hai, hawakuwa watu wa kuumwa umwa ovyo….’akasema

‘Ilikuwaje walipoanza kuumwa,…?’ akaulizwa

‘Kwanza nilipokea barua kutoka mahakamani kuwa kuna deni, kama nilivyosema awali,..shemeji hakuwepo, alisafiri, ikabidi mimi mwenyewe kuanza  kufuatilia hadi huko benki, na baadae shemeji aliporudi …nikamuuliza yeye akasema barua kama hizo zilishawahi kufika kipindi mimi ninaumwa, na hawakutaka kunishtua, ila wao walijaribu kulipa kidogo kidogo hilo deni, ili kuonyesha kuwa malipo yanaendelea..lakini wakafika sehemu wakakwama…’akatulia

‘Ni ndio nikamwambia, mimi hilo deni siwezi kulikubali,…na sikubali, inabidi twende hata mahakamani…’akasema.

‘Shemeji hakupinga hilo, akasema sawa….tukafuatilia pamoja naye,…kwanza tukapitia benki, tukatafuta mawakili…na hadi mahakamani….tukashindwa kesi,…kiukweli hatukuwa na cha kujitetea, zaidi ya kauli zetu tu,……’akasema.

‘Basi….baada ya hapo, shemeji akaniambia, kwa vile hatuna jinsi nyingine tukubaliane na hayo maamuzi, maana deni litalipwa, na bado tutapata pesa, ambayo tunaweza kujengea kibanda cha kujisitiri,na yeye yupo tayari, kunipatia sehemu ya kuishi kwa muda…sikukubaliana na yeye…’akatulia

‘Kwahiyo ikawa ni mvutano sasa wa mimi na yeye , yeye anaogopa kuwa tusipokubaliana na hilo agizo la mahakama, maana mwanzoni tulipewa muda wa kulipa , hatukulipa, baadae ndio tukaamriwa kuwa baada ya muda….sijui walitoa muda gani, basi, nyumba iliyoweka kama dhamana iuzwe…’akatulia

‘Siku hiyo nililia sana mahakamani, lakini ingenisaidia nini…benki baadae ndio wakaleta barua kuwa kutokana na deni hilo, na kutokana na hukumu ya mahakama, wao,hawana jinsi nyingine, zaidi ni kuipia mnada hiyo nyumba.

Nikaongea na shemeji,..nashangaa baadae anasema, basi tukubaliane tu na hilo, tuwaache wapige mnada, pesa itakayopatikana sehemu italipia deni, na sehemu itatusaidia sisi wenyewe,

‘Hapana shemeji, mimi sikubaliana na hilo…’nikasema

‘Sasa tufanye, hakuna cha kuuza hapa, huna mashamba huna lolote, na mimi sina mashamba makubwa, yaliyopo ni mali ya watoto wangu…siwezi tena kuuza, …na hata nikiuza, itapatikana pesa kidogo tu, haitasaidia kitu..niliwahi kuuza eneo, nikalipia kidogo, sasa hivi siwezi tena….’akasema hivyo.

‘Mimi ni bora waje waniulie humu humu ndani…’nikamwambia.

‘Sikiliza shemeji kwa hatua iliyofikia, cha kufanya, ni sisi tuweze kuoenga na wapiga mnada, ili ipatikane pesa nzuri, vinginevyo, tukisusia wakafanya wao wenyewe, huenda tukaambuliwa pesa isiyofaa…mimi naelewa sana hiyo kazi…’akaniambia shemeji.

‘Alikuambia yeye anajua mambo yam nada kwa vipi…?’ nikamuuliza

‘Yeye pamoja na shughuli zake nyingine …pia ni dalali, na wakati mwingine anasimamia mambo ya minada, kaam hivyo kupiga minada mali …kwahiyo , yeye anayafahamu sana mambo hayo ya minada, nk….’akasema, nahapo kitu kikanigusa akilini, nikahisi jambo, lakini sikuwa nauhakika nalo.

‘Ikawaje sasa…?’ nikauliza nikipoteza muda, huenda hali ikawa nzuri nikaweza kutoka.

‘Sasa wakati tunahangaika,..huku na kule..kutafuta mbinu, kutafuta njia nyingine. Mimi kila siku kiguu na njia kwa wakili,…kufuatilia, …ghafla, mtoto akaanza kuumwa, ikawa sasa ni kusumbuka naye, nashindwa kutoka…kila nikitaka kutoka mtoto anaumwa,  ..inabidi shemeji aende peke yake, akirudi majibu ni yale yale…’akatulia.

Wakati anaongea mimi nikawa najaribu kupiga simu kwa yule jamaa na jamaa yangu mwingine, ili niweze kufanya jambo, yule ambaye ni wakili ninayemfahamu simu yake ikawa inasema

 ‘Namba unayopiga inatumika,jaribu tena baadae…sasa ipo hewani lakini inatumika…’

Na huyu asiyejulikana simu yake ikawa haipatikani kabisa..na inasema niwe na uhakika na na hizo namba.

************
Shemeji kabla hajaondoka, akaniuliza;

‘Hebu nikuulize kwanza,  haya unayotaka kuyafanya…kwanza mimi sijakubaliana nayo, pili,  unayafanya bure, maana mimi sina pesa, mimi sina kitu,….ohooo….sina kama unavyoniona hivi, sina hata sent moja ndani…?’ akaniuliza na kusema hivyo.

‘Mimi sitarajii malipo kutoka kwako,….mungu mwenyewe anatosha, niamini kwa hilo….’nikasema

‘Lakini mimi bado nakusisitiza, sitaki haya mambo yaanze tena, naomba tafadhali…’akasema akionyesha wasi wasi mkubwa.

 ‘Ni lazima nikutane na wote waliohusika na hii kesi mmoja mmoja…, ili kuupata ukweli..hilo siwezi kuliruka, nah ii hali ya kuumwa, isikutishe, nitajua jinsi gani ya kufanya, wameshanichokoza na mimi…..’nikasema sasa nikiangalia saa.

‘Kwahiyo unataka kufanya nini…?’ akaniuliza nikawa nimemuelewa nikasema

‘Unajua kutokana na ujumbe wa yule jamaa asiyejulikana,  anasema anaweza kuahirisha zoezi la uuzaji wa nyumba, lakini ni kwa siku chache, nikishindwa kupata ufumbuzi, zoezi hilo litaendelea, …kwahiyo yeye alitaka nikubaliane na sharti hilo…’nikasema

‘Sharti !!!…kwani yeye anaweza kuzuia hilo zoezi…?’ akauliza

‘Yaonekana hivyo,….maana muda wa mnada haukupangwa na mahakama,…nahisi kuna kipengele kipo cha kukuwezesha wewe kufanya lolote kabla ya huo mnada, tatizo huyo muhusika hataki kunionyesha hiyo nakala ya hukumu,….ndio maana nataka kuonana naye..’nikasema

‘Keshakata tamaa, kahangaika sana…’akasema

‘Sasa huyu asiyejulikana ndio kanichanganya zaidi…unaweza kuhisi huyo mtu ni nani…?’ nikauliza

‘Kiukweli mimi siwezi kujua yeye ni nani, walionisaidia ni yule mliyeongea naye,…awali, huyo mwingine sijui ni nani, ..nakumbuka huyo wakili aliyekuwa akinisimamia hiyo kesi, alikuwa na watu wake, anawatuma,..tofauti tofauti, sasa sijui yupi ni yupi…’akasema.

‘Usijali…nitamtambua tu, na ujanja wake wa kunipa siku tatu, na haya yanayotokea, ….naanza kuingiwa na hamasa yah ii kesi,…’nikasema

‘Sawa mimi naondoka shemeji..ugua pole,..lolote litakalotokea nitakuambia, ni muhimu niwepo huko, ili shemeji akija anikute huko, ujue yeye ndio msimamizi wetu, na inatakiwa kila ninachokifanya nimuambie yeye,…….’akasema.

‘Sawa wewe nenda, nitakuja huko huko kuonana naye….’nikasema

‘Sawa….lakini tafadhali, usinihusishe kwa hivi sasa…’akasema akiniangalia kwa mashaka.

‘Wewe usijali, ….’nikasema nikijaribu kusimama, ….nikawa nayumba…nikaone niende kuoga labda nitapata nguvu,..ile nafika chooni, nikayumba na ghafla giza likatanda usoni….

NB: Je nitauweza mfupa uliomshinda fisi


WAZO LA LEO: Kamwe usikate tamaa kuidai haki yako, haki yako itakuwepo na watakaotaka kuichukua kwa nguvu, kama watashinda ni kwa muda mfupi tu,…endelea kuipigania haki yako,kwani mwenyezimungu atakuwa na wewe! Na ikishindikana, hakimu wa mahakimu yupo.

Ni mimi: emu-three

No comments :