*********
‘Lakini nikuulize
unaniuliza haya maswali yote ili iweje….maana wewe hujui yaliyotokea kwasababu
ya haya….na hadi mimi mwenye haki nikafikia kusema, basi yote hayo tumeshamuachia mungu,…hunujui mimi
ni nani, sio mdhaifi kihivyo, nimekuwa nikifanya kazi zinahusikana na maswala
makubwa ya kupambana na watu….lakini kwa hili..hapana, sitaki tena….sasa
sikiliza nimekuambia hayo niliyoweza
kukuambia,…yatosha,…nakuomba uondoke tu…’akasema na kujikuanyata.
************
Kauli yake hiyo ilinifanya
nivunjike nguvu kiasi, kwasababu hata mimi mwenyewe nilikuwa najiuliza, je
ninavyomuuliza haya maswali yote huyu mama wa watu, hivi kweli ninaweza kumsaidia,
maana kiukweli huyu mama mjane na watoto
wake wanahitajia msaada mkubwa sana tena wa haraka, isije ikawa na mpotezea
muda wake bure na kumzidishia majonzi.
Ningeliweza kufanya lolote kama ningelikuwa na watu wa
kunisaidia, watu wa kunisaidia mmoja wapo keshasema hawezi tena,.. kwa hatua
iliyofikia kesi hiyo, kwa kauli yake hiyo kesi kwa ajili ya kufanya huyo mama
apate haki yake ‘haina mshiko’ . Akiwa na maana kuwa, kesi hiyo haina nguvu ya
kuitetea, kwani nyaraka zote na ushahidi
wote unaonyesha usahihi, kuwa mashamba yaliyouzwa yaliuzwa kihalili, yalikuwa
mali ya wauzaji...na mlalamikaji hana ushahid wa hoja yake.
Sasa kwa hili la la nyumba….ambalo ndio muhimu kwangu,
nitawezaje kulitatua, nyumba ni kweli ni mali ya mjane na watoto wake, nyaraka
zinabainisha hivyo, wameipata kutokana na urithi…lakini nyumba hiyo,
inahitajika kupigwa mnada,
Nilipowaza hivyo nikahema, na kumuangalia yule mama akiwa
kajikunyata sasa akionyesha dhahiri anaogopa jambo…nahisi hiyo hali
inayoendelea hapo ndio inamtisha, sijui kuna nini zaidi kinatokea, na amesema
inatokea kwa watoto…
Niliwaangalia wale watoto , mawazo yangu yakanipeleka
kuwawazia watoto wangu…kuwa huenda na mimi inaweza kutokea hivyo, na
nisipofanya juhudi, inaweza kunikuta na mimi kama adhabu,..kwani akilini
nilikumbuka jambo.
‘Sikiliza katika
maisha yako, kumbuka jambo moja, wema unaowatendea wenzako hasa,…wanyonge wenye
uhitajio , ni akiba kwako, usiogope kuwatendea hivyo, kwani malipo yake
yatakuja kwko moja kwa moja au kupitia kwenye familia yako, na ukipuuzia, kwa
vile sio familia yako, au sio wewe, adhabu yake itakuja kwko wewe au kwa
familia yako…’ nikakumbuka usia wa jamaa aliyenifanya nijiunge kwenye
maisha haya ya kutetea jamii kwa njia ya visa.
Hapo hamasa
ikanijaa,…Sikukata tamaa, ndio hapo nikamkumbuka rafiki yangu mwingine aliyebobea kwenye sheria
za namna hiyo, huwa namtumia kwenye matatizo kama hayo, ikibidi lakini, ..sio
mara nyingi, kwa vile yeye ana majukumu mengi sana, ukilinganisha ya yule wa
awali
‘Ni swala la kujaribu tu…’ nikasema kwa sauti ndogo,
Nakamtupia macho huyo mwanamama, ambaye kwasasa niliona
michirizi ya machozi ikijichora usoni, mwake,..moyo wangu ukazidi kuumia…hapo
hapo nikasema;
‘Shemu unajua matatizo humjia mwanadamu, na yanapokujia
inabidi upambane nayo,maana hujui kwanini yamekujia, huenda ni namna ya kuvuka
daraja fulani la maendeleo, au kuondokana na dhiki, shida, au hara hatari
fulani,..kwahiyo hutakiwi kukata tamaa, ni ku jaribu kila uwezavyo, kupambana
na huo mtihani,..ila iwe kwa njia ya haki, usikate tamaa na hata kukufuru, kuwa
kwanini mimi tu, mbona mimi naonewa sana na mungu…’nikasema
‘Ndio hivyo kiubinadamu tena…., na usemavyo hivyo, unafikiri
mimi nilikata tamaa, hapana, nilijitahidi kadri nilivyoweza, lakini ikafikia
sehemu nikanyosha mkono, wewe hayajakukuta haya, yangekukuta halafu uwe ni mama
wa watoto kama hawa, nina imani ungelifanya kama nilivyofanya mimi, ni nini nataka,…mali
eeh…dhidi ya uhai wa watoto wangu, hapana,… wacha wachukue…’akasema
‘Ina maana waliwatishia au walifanya nini cha kuwaumiza
watoto wako….?’ Nikamuuliza
‘Sitaki hata kuyaongela hayo, wewe amini hivyo, ..na msimamo
wangu ndio huo huo….’akasema
‘Ni kweli kihulka,…inafikia hivyo, mama na watoto wake, na
ikizingatiwa, labda hukuwa na ndugu wa karibu wa kukusaidia, au sio…lakini mimi
sasa nimejitolea kuwa ndugu yako, tupambane kwa pamoja, kama kweli unaamini
hivyo, kuwa mali zilikuwa zako, na hilo deni kweli sio halali…’nikasema
‘Wenzako walisema hivyo hivyo, kiwapi…’akasema
‘Akina nani…?’ nikamuuliza
‘Si hao walisema watanisaidia, …’akasema
‘Nataka nionane nao, nione wapi walikwamia…’nikasema
‘Si umesema umeongea nao, wakasema nini…kuwa imeshindikana,
kuwa sina ushahidi au sio…ni kweli, ushahidi sina, nyaraka zote zinaonyesha
kuwa kweli sina haki..utafanya nini…hakuna,…’akasema
‘Mimi sikati tamaa haraka hivyo, ngoja na mimi
nijaribu,…nipe nafasi hiyo…’nikasema lakini moyoni bado nikiwa na mashaka.
Nitafanya nini sasa,…sana sana nitategemea miujiza ya mungu.
‘Hahaha…tatizo hujui tu, halafu nitakulipa nini, masikini
mie….usija kuja kujutia baadae kuwa umepoteza muda wako, hujapata kitu, na mimi
sina malipo ya kukulipa…’akasema sasa akiniangalia kwa mashaka.
‘Mimi sifanyi haya kwa ajili ya malipo, …na nikuambie kitu,
kesi kama hizi, hujilipa zenyewe, kama walikudhulumu,…watakulipa kwa adhabu
juu…lakini hayo ya malipo sio tija yangu, sifikirii hilo kabisa, tija yangu ni
kwa hawa watoto, na wewe mwenyewe..tija yangu ni haki yenu…’nikasema
‘Aaah..mimi naona unanipotezea muda wangu tu…na kuniachia
matatizo hapa…’akasema sasa akigeukia upande mwingine.
‘Sikiliza, wakati nasubiria simu fulani, mimi nataka kuendelea kukuuliza mambo machache
machache…, nakuomba tafadhali, jipe moyo, omba kwa mungu, sote tuombe kwake,
yeye ndiye tegemeo letu ..najua hii hali ya humu inakutisha, ningelisema basi
twende kwangu,…lakini hapana kwa hivi sasa twatakiwa tupambane na hao maadui
zako humu humu… sehemu nzuri ya vita ni eneo wanalolipenda maadui..…’nikasema
huku nikihisi mwili ukinisisimuka, na moyo kunienda mbio.
‘Mimi hivyo vita siviwezi kabisa,..nimeshanyisha mikono juu,
nimesarenda….’akasema na sauti yake ikakatishwa na mlio wa simu yangu, kwa
haraka nikaangalia mpigaji, ilikuwa namba ngeni kwangu.
‘Halloh ni nani mwenzangu…?’ nikauliza
‘Mimi ni rafiki yako katika harakati…’akasema, nikashangaa
kwa nini hajajitaja jina lake.
‘Jitambulishe…’nikasema
‘Ni hivi…nimepata fununu kuwa unataka kumsaidia mama mmoja
mwenye matatizo, ambaye aandai kuwa kadhulumuwa mali yake, …’akasema.
‘Anadai,…ina maana sio kweli…?’ nikauliza
‘Ndio ukweli ulivyo…’akasema
‘Ni nani kakuambia hayo kuwa mimi nataka kufuatilia hiyo
kesi..?’ nikauliza, na badala ya kunijibu swali langu akasema;
‘Unataka msaada wangu au hutaki…?’ akauliza..na mimi
nikahisi huenda kuna kitu naweza kukipata hapo,ila moyoni nilishahidi ni tapeli
fulani hivi.
‘Kwanza tutambuane, maana sio kila sauti ina muelekeo
chanya, siwezi kukubali au kukataa jambo
la sauti tu… muhimu tujuane wewe ni nani…’nikasema.
‘Hiyo kesi mimi ninaifahamu sana…tatizo kubwa inavyoonekana
mume na mke walikuwa wanafichana baadhi ya mambo yao,..hilo ni kosa kubwa kwa
wanandoa…angalia sasa, mume kaondoka, kamuachia mkewe na watoto matatizo, mke hajui ni nini mume wake alikifanya,…kuna
mali za watu zilitambulikana kuwa ni zao, kuna madeni……yote sasa yamebakia
mikononi mwa wanafamilia hao…’akasema
‘Ehe…endelea..’nikasema
‘Haya nakuambia kwa vile mimi nilikuwa bega kwa geba
kumsaidia huyo mama…’sauti ikasema
‘Sawa mimi nakusikiliza, endelea…ulimsaidiaje labda….’nikasema.
‘Ni kweli mama huyo na watoto wake wanahitajia msaada wa
hali na mali, nilikutana nao, nikafuatilia kila kitu hatua kwa hatua…na
ikafikai sehemu nikaona hakuna jinsi ya kufanya, lakini huyo mama akasisitiza
kuwa mahakama ndio itaamua, ikiamua basi, hana la kufanya, basi ikabidi tufike
hadi Mahakamani,… sheri a ilitubana,…huwezi ukakana nyaraka na ushahidi , huo
ni msingi mkubwa wa kushinda kesi,…huwezi ukaukana ukweli, au sio…maana wewe
unautumia sana…’akatulia.
‘Huwezi kufanya jambo kinyume na hayo,, ili tu umrizishe
huyo mama na watoto wake, kiukweli hata mimi nilipata shida sana, jinsi gani ya
kusaidia, nilitumia ujuizi wangu wote, ukichanganya na huruma ya ki-ubinadamu,
lakini …nilikwama, kwahiyo ninachoweza kukusaidia ni kuwa, kama wataka
kumsaidia huyo mama, kwa hivi sasa, acha mambo yaendelee kama yalivyo…’akatulia
kidogo.
‘Mambo gani sasa…?’ nikauliza.
‘Ya kisheria…’ akasema, na kabla sijasema zaidi akasema;
‘Kumbe hata jambo lenyewe hujalifahamu vyema…’akasema
‘Mambo gani hayo ya kisheria,..nifafanulie..?’ nikauliza.
‘Kama hayo yaliyopitishwa, kuwa nyumba hiyo ipigwe mnada,..hiyo
ni kwa mujibu wa mahakama, ni sheria imepitishwa hapo, huwezi kupingana na
mahakama…’akasema
‘Lakini naweza kukweka pingamizi, kama nahisi nimeonewa au
sio…?’ nikauliza
‘Ndio..lakini sio kwa kesi ya huyo mama unapoteza muda wako
bure…’akasema
‘Sikiliza…na kwa ziada, sio kwamba mahakama imependa imtupe
huyo mjane tu na watoto wake, mahakama imeweka namna ya kumsaida huyo mjane na
watoto kuwa, pesa itakayopatikana,iangalia pande zote mbili, nilijitahidi sana
hili kupatikana…’akatulia.
‘Kwa vipi…?’ nikauliza
‘Tulishaongea na benk, na wao wana ubinadamu wao,…unajua
benki zetu pamoja na kujalia biashara zao, lakini wana namna ya kusaidia jamii,
wao wamepanga namna ya kufanya, deni lilipwe, na kutokana na hayo malipo, wao
watasaidia katika sehemu ya hilo deni, liweze kumsaidia huyo mama pia..’akasema
‘Kwahiyo wewe ndiye ulitoa wazo hilo, au sio…?’ nikauliza
‘Ndio, ni kwa namna ya kuona jinsi gani hiyo familia na
yenyewe itapata chochote…’akasema
‘Mhh….endelea…’nikasema
‘Na, ..hata hivyo bado kutakuwa na pesa ya ziada kutokana na
mauzo ya hiyo nyumba ..pesa itakayobakia baada ya kulipwa hilo deni na nyingi
tu…’akatulia.
‘Ok….endelea…’nikasema
‘Unasikia, ..maana kiukweli nyumba hiyo ina gharama sana
akipatikana mteja mnzuri, bado mama atakuwa na kianzio cha maisha yake, anaweza
hata kujenga kibanda chake cha kuwakimu, lakini ni baada ya kutoa gharama mbali
mbali za utendaji…’akasema
‘Ambazo ndio hizo na nyie mnanimezea mate…’nikasema
‘Una maana gani kusema hivyo,..tatizo lako wewe umelichukau
hilo jambo juu, juu…’akasema
‘Sawa, ndio maana nataka nielewe…..na mlivyokubaliana ...huyu
mama na mtoto wataishije…?’ nikauliza.
‘Ehee…hilo ndio la muhimu la kusaidia, wewe kama msamaria
mwema, unaweza kuingiza mguu wako kwenye shemu hiyo, inakuhus kabisa, andika,
ili watokee watu wamsaidie huyo mama…’akasema
‘Sio niandike ili apate haki yake…’nikasema
‘Sikiliza…kinachotakiwa kwako wewe ni kuongea na …huyo
shemeji yake. Kwanza ungelikutana na huyo jamaaa wala usingelihangaika sana…anajua
kila kitu, na hata ukimuuliza huyo mama atakuambia ukweli…huyo shemeji yake ni
mtu mwema sana…, yeye yupo tayari
kumsaidia huyo mama, sehemu ya kuishi, niliacha wakiwa wanajadili hilo,
sijapata marejesho…’akasema
‘Kama hujapata marejesho, kwanini mnakimbilia kupiga mnada
hiyo nyumba, ndivyo mahakama ilisema hivyo…?’ nikauliza
‘Sikiliza, wewe ongea na shemeji yake huyo mama, yeye ndiye mwenye majukumu na ndiye aliyekuwa kapewa hiyo familia
kuihudumia, unaona hao watoto eeh, ni bado wadogo, na huyo mama alikuwa
hajiwezi kabisa huyo shemeji yake kajitolea kwa hali na mali…’akasema
‘Kwahiyo ni nini unachokifanya kwa hivi sasa kwa ajili ya
huyo mama…?’ nikauliza.
‘Mimi bado naendelea kuongea na benki, ili kuona ni namna
gani zaidi wanaweza kumsaidia huyo mama, kama kuwasomesha hao watoto..na zaidi
ya hapo, wao kam benki wana fursa nyingi, huyo mama alikuwa muajiriwa, wanaweza
hata kumuajiri…., banki ni watu wazuri sana, wana vitengo kama hivyo vy
kusaidia jamii.…’akasema
‘Naweza kuonana na wewe wapi..?’ nikamuuliza
‘Kwa hivi sasa nina shughuli nyingi, nimeamua kukupigia simu
tu, baada ya jamaa yangu kuniambia kuna mtu anaulizia tena kuhusu hii kesi,..kiukweli kesi hii ilishanichosha
sana..na ni mambo ya kawaida kwenye utendaji wetu, ila …kuna mambo mengi
nimekutana nayo, ni ya kawaida…ila ni kesi ngumu sijawahi kukutana nayo kabla…,
na hata hivyo, kila kitu kipo wazi…’akasema
‘Kwa kauli yako hiyo najikuta kuwa na maswali mengi…lakini
naona haifai kuongea yote hapa kwenye simu, sio vyema au sio, hakuna ushahidi
wa kudumu,…ila …kama wewe ndiye uliyekuwa ukiishughulikia hii kesi, japokuwa
sikujui wewe ni nani, nakuomba jambo
moja, kama kweli wewe ni mkweli…kama kweli wewe ndivyo ulivyo kama ulivyosema,
nakumba jambo moja…’nikasema
‘Jambo gani hilo…?’ akauliza kwa sauti ya mashaka.
‘Uahirishe kidogo hilo zoezi la kuipiga hiyo nyumba
mnada…’nikasema
‘Haaaah, wee, unataka mimi nipambana na sheria,… sio mimi,…mimi
sipo hivyo kabisa,.. hayo ni maamuzi ya mahakama ndugu yangu, hilo siwezi,
…kabisa kabisa…’akasema
‘Nikuulize jambo moja, je mahaama ndio ilipanga tarehe ya
kufanya huo mnada…?’ nikauliza n ahapo akatulia kidogo, halafu akasema
‘Hayo ni maswala ya benki…baada ya kuthibitishwa kuwa wana
haki ya kufanya hivyo, ndio wao wakapanga tarehe hiyo…’akasema
‘Katika hukumu, …ilisema nini kuhusu tarehe na haki za huyu
mama…?’ nikauliza
‘Siwezi kukusomea hilo kwa hivi sasa, kwanza wewe huna haki
ya hayo yote au sio, ni mpaka niwe na uhakika kuwa wewe unahitajia hayo kama
nani, kwa huyo mama…’akasema
‘Sasa hivi unanigeuka kuwa hujui ninachokifanya
mimi…’nikasema
‘Najua, lakini hilo unaloniulizia ni jambo la
kisheria,..unasikia,…kama ikibidi nitakuonyesha, lakini mpaka niwe na uhakika
wa kisheria kuwa wewe ni nani kwa ajili ya huyo mama…’akasema
‘Swali je unaweza kumsaidia huyo mama, ili hilo zoezi
liahirishwe au mimi niende mahakamani, kuweka pingamizi…’nikasema
‘Hahahaha..umenifanya mimi nicheke, unajua usiingile mambo
usiyo na ujuzi nayo,…hilo sio swala dogo kama unavyofikiria wewe, wewe huna
uwezo huo, ili lifanyike hilo, inahitajika wakili, mwenye uwezo
mkubwa,…’akasema
‘Kama wewe…’nikasema
‘Mimi ndio nimefikia hapo, siwezi tena kuifanya hiyo
kazi…’akasema
‘Kwanini, unaogopa…kuna kitu unakiogopa au sio..?’ nikauliza
‘Ndugu yangu nina kesi nafuatilia, siwezi kuongea na wewe
zaidi….’akasema
‘Ndio maana nataka tukutane na wewe, au niende mahakamani
nipate kibali cha kuonana na wewe..’nikasema
‘Sikiliza…ok, nitakupigia…’hapo akakata simu, haikupita
muda, akapiga simu, na kuniuliza;
‘Kwahiyo wewe umeshaongea na huyo shemeji ya huyo mama..?’
akauliza
‘Bado…’nikasema
‘Ongea naye kwanza..’akasema
‘Kwahiyo hayo yakiendelea, utafanya kama
nilivyokuomba…’nikasema
‘Siwezi, nakuambia ukweli ulivyo…’akasema
‘Sawa ngoja na mimi nifanye nijuavyo mimi…’nikasema
‘Utafanya nini ndugu yangu wewe…, usidanganyike, kama ni
huruma mimi nina huruma sana,..lakini kwa hilo, huna ujanja, utapoteza muda
wako, na pengine..ukaja kupata matatizo, na muulize huyo mama, shida gani
anayoipata, huwaonei huruma hao watoto ,kifupi mimi siwezi kufanya lolote kwa
hatua iliyofikia…’akasema
‘Mimi naona unakimbilia kunitisha, au…?’ nikauliza
‘Sio vitisho,….mimi nakuambia kama mtu ninayekufahamu na
kukujali,..hebu nikuulize wewe…umefika hapo kwa huyo mama, hebu muulize
vyema,…ni mambo ya ajabu yanatokea humo, sio kwamba mimi nayaogopa, hapana,
lakini ni mateso kwa hao watoto,…’akasema
‘Kwanini yatokee hivyo, kama hao watu wana haki ya hayo
waliyoyadai…?’ nikauliza
‘Mimi sijui… ila kwa vile sheria ipo wazi, kwanini tupoteze
muda, kwanini hiyo familia iendelee kuteseka, wakati kuna uhakika kuwa
hawatashinda hiyo kesi, mimi sioni haja ya kuwatesa hao watoto, unaona dhamira
yangu ilivyo, naangalia namna nyingine ya kuwasaidia, anyway..kama huwezi
kunisikiliza fanya upendavyo…’mara simu ikakatika.
Kwa haraka nikaichukua ile namba nikatafuta jinsi ya
kumtambua mtumiaji wa hiyo namba, na ilionekana ni namba mpya haijasajiliwa…
Nilitaka nimfahamu ni nani, kama kweli ni mwanasheria,
hatakuwa na namna ya kujificha, nikaiweka ile namba,…nikajaribu kama kumtumia
pesa, nikaona haisomi mumulikaji wa hiyo namba. Ina maana hiyo namba
haijasajiliwa, hapo nikawa na ushahid muhimu kwangu.
‘Oh lakini ni nani huyu…?’ nikasema kwa sauti, na yule mama
akaniangalia.
‘Eti ni nani aliyekuwa akiishughulia kesi yako…wakili
au…mtetezi ?’ nikamuuliza.
Yule mama akaniangalia kwa makini, nikama vile alikuwa
akiogopa kusema neno, na mara ujumbe wa maneno ukaingia kwa namba ile ile,
ukisema;
‘Mimi nitajitahidi kufanya utakavyo, lakini na wewe utii
sheria…acha hayo mambo ya kisheria yaendelee kama yalivyo,…sina muda tena na
hiyo kesi, kama upo tayari jibu endelea…’
Hapo nikatabasamu..nikamuangalia yule mama, yule mama akawa
ananiangalia tu kwa mashaka.
‘Ni lazima nimfahamu
huyu mtu ni nani…’nikasema sasa nikitaka kumpigia jamaa yangu mmoja mtu wa
mitandao, …najua hatanisaidia sana, maana kama namba haijasajiliwa huwezi
kumfahamu mpigaji wa hiyo simu.
Nikampigia huyo jamaa yangu, na kumuomba ajaribu kumtafuta
mpigaji wa hiyo namba,na wapi alipo
Baada ya muda akanipatia majibu;
Mpigaji wa hiyo namba, hajulikani maana hiyo namba haijasajiliwa,
ila huyo mpigaji yupo maeneo ya……..
Niliposikia hivyo, nikasimama,
Kwa haraka nikatoka nje….
WAZO LA LEO:
Kabla ya kutoa hukumu ya jambo lolote ni muhimu sana tuwe tumejirizisha kwa
kusikiliza pande zote, pamoja na ushahidi na mashahidi, laini pia , ni vyema
tukawachunguza hao wahusika vyema, maana wengine ni wajanja wa kuongea, ni
wajanja wa hali na mali. Wengine ni wadhaifu wa kuongea. Na ukichunguza
historia zao, unaweza kugundua tabia na mienendo ya wahusika, hili linaweza
kusaidia katika kufikia hitimisho ya kesi za kijamii.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment