Niligeuka kumuangalia yule mtoto akiwa kashikilia mikono
kama kuniomba niondoke, maana mama yake analia,…na nikiendelea kumuuliza
maswali mama yake nazidi kumfanya alie zaidi, lakini nitafanyaje, muhimu kwangu
ni kufahamu kila kitu.
‘Naweza kuongea nawe zaidi lakini peke yako…?’ nikamuuliza
na yeye akanielewa, akasema
‘Nikuambie kitu hakuna zaidi unaweza kufanya, ..hawa ni
watoto wangu japokuwa ni wadogo lakini angalau wanaufahamu wa kinachoendelea,
japokuwa wanamuamini sana baba yako mdogo…’akasema
‘Baba yao mdogo, ndio nani…?’ nikauliza
‘Yeye ndiye kakabidhiwa kwetu, kama baba yao mlezi…’akasema
‘Oh….kumbe pia baadae ninaweza kuongea naye, nione
kama…’nikataka kusema na y eye hapo hapo akanikatili na kusema;
‘Tafadhali, haya niliyokuambia usije kuongea naye huyo mtu, …kuwa
nimekuambia haya, utataka hata huo msaada mdogo ninaoupata nisije kuupata tena….’akasema
na nikaona kama anataka kulia tena.
Pale nikaona nifanye jambo….
‘Kesi yenu ilishughulikiwa na nani hasa…?’ nikamuuliza
‘Mhhna watu wengi, nimekutana na watu wengi sana, hata hivyo…ilifuata taratibu zote, kuanzia serikali za mitaa…hadi
huko kwa watendaji, hadi inafika mahakamani…na niliwahi kuongea na jamaa mmoja, mtetezi mkubwa wa haki
za wajane na mayatima, ni wakili mmoja hivi anajulikana sana kwenye utetezi…’akasema
‘Huyo namfahamu…’nikasema
‘Basi huyo anafahamu kila kitu…’akasema
‘Samahani kidogo..nataka kupiga na simu mahali, nitarudi…’nikasema hivyo
na kutoka nje..
Nilimpigia simu huyo jamaa wa watetezi wa mayatima na watoto
ni jamaa ninayefahamiana naye sana, nikikwama jambo , kwenye mambo yangu ya
utunzi, namfuata napata kumbukumbu muhimu kupitia kwake,…yeye anayeshughulia
maswala ya kisheria pia, nikataka kupata muongozo fulani kutoka kwake
kwanza,…je hili swala naweza kulifanyia kazi au la.
‘Halloh, ni mimi…’nikasema
‘Najua wewe ni nani namba yako ninayo, unasemaje mtunzi wa hadithi…’akasema,na mimi nikaanza
kumuelezea hili jambo, kwa jinsi nilivyoliona, akasema;
‘Oh,…nakumbuka sana hilo swala, lakini nikumbukavyo mimi, walishamalizana kifamilia, au sio…?’akasema
kama ananiuliza
‘Nahisi kuna utata mkubwa,…hebu pitia pitia kabrasha lake,
uone…nataka unisaidie sana hili jambo, kunaonekana kama kuna dhuluma ndani
yake…’nikasema.
‘Oh…nina kesi nyingi sana za namna hiyo…nashindwa hata
kuzimudu…sijui kama ninaweza kukusaidia, kwa sasa na kwa haraka hivyo…labda..ngoja
nione, kwani umeongea nao, wamekuambia nini…?’ akaniuliza.
‘Mhh..ndio najaribu, lakini hali ya huyu mama mjane bado ni
tete..na nahisi kuna jambo limefanyika nyuma ya mgongo wake…si unajua haya
mambo ya mali, na urithi, …mume anapokufa, inakuja kuleta tafrani baadae, na
anayekuja kudhulumiwa ni mke na watoto….’nikasema
‘Kwahiyo una maana hapo kuna dhuluma, sio kweli kwamba
walikubaliana kifamilia…lakini kisheria kila kitu kipo wazi…?’ akauliza na
kusema.
‘Ndivyo inavyoonekana hivyo,…kisheria nk….’nikasema.
‘Oh…sasa..unajua nashindwa,…na hiyo kesi ni siku nyingi
sana, inakuja, inarudishwa nyumbani na baadae ikawa ya kifamilia….walikubaliana
tena kwa maandishi, kila kitu kipo wazi, sasa sijui kumetokea nini tena….’akasema.
‘Nahisi kuna shinikizo, hayahufanyika kuhi zaidi..…bado
natafuta ukweli, lakini nitashindwa kuendelea bila ya msaada wako…’nikasema.
‘Kwanini labda,..ndio utashindwa maana sheria ilishapitisha
na kila kitu kimeonekana kipo sawa…na kila kinachoendelea hapo kwa hivi sasa ni
mambo ya kisheria, kwani kuna tatizo gani zaidi….?’akasema na kuuliza.
‘Sio kweli, sio kisheria, kuna jambo , nahisi hivyo…’nikasema.
‘Una uhakika…?’ akauliza
‘Ndio nautafuta huo uhakika..., ndio maana nataka msaada wako…’nikasema.
‘Unapoteza muda wako,...na nakuonya, hapo....najua... najua ni huruma nakadhalika, lakini
kisheria, kila kitu kipo sahihi, na sheria imeshapitishwa hapo, ..hakuna jinsi
hapo, mimi nimenawa mikono…’akasema.
‘Hii ni muhimu sana,…na sitaliacha hivi hivi,… hebu fikiria
hivi, umefariki ..samahani natolea mfano huo kwako ili ikuguse kidogo…, wewe
mfano, umefariki, umeacha watoto nyuma na mama, wewe ulikuwa na mali,..za
familia, yaani wewe na watoto wako, umafariki na mali hizo umeziacha…, kihalali ni mali za familia yako,
mke na watoto…., baadae zile mali zinageuzwa na kuwa sio za mke na watoto wako,
utajisikiaje…?’ nikamuuliza
‘Mimi ni marehemu au sio…?’ akauliza
‘Ndio, lakini una utashi wa kuona, yanayotendeka…nachukulia
kwa mfano…’nikasema
‘Hiyo haina mshiko kisheria… ushasema mimi ni marehemu,
sikiliza nikuambie, acha ndoto za utunzi wako, angali uhalisia wa jambo lenyewe
kisheria….’akasema.
‘Hujajibu swali langu…’nikasema
‘Nitajisikia vibaya, inauma..lakini sheria inasemaje,
nyaraka zinasemaje, ushahidi unasemaje, ndio mamabo ya kuangalia hayo…’akasema.
‘Kuna leo na kesho, yanayotokea kwa familia hiyo sio kwamba
ni wao waliumbiwa hivyo, fikiria sana hilo kwako wewe uliyepewa dhamana hiyo…’nikasema.
‘Ukisema hivyo, ni kama unanitupia lawama mimi, hujui nilivyohangaika, lakini inafikia sehemu unaona basi bwana, halafu vielelezo vyote vipo, kisheria, utafanya nini hapo….’akasema.
‘Hapana,...hapa kuna jambo, nahisi kuna jambo zaidi ya huo uhalisia,...mimi nataka unisadie..tuweze kuliweka hili jambo vyema,
imeniuma sana, imenigusa, nataka tuone uhalali wa hili jambo…’nikasema.
‘Ehe... sasa wewe wataka mimi nifanye nini, niitambuke sheria
au...?’ akauliza.
‘Utafute mbinu zozote za kuchelewesha hilo zoezi, …mnada,
nakadhalika…’nikasema.
‘Hahaha…mbona unakuwa mbumbu wa sheria..hayoo yamekwenda
kisheria, sio kwamba hatua hizo zilichukuliwa tu..hapana kuna utaratibu wake,
mimi huko siwezi kuingilia, nilishawajibika kwenye sehemu yangu, nikanawa
mikono, wenyewe walikubaliana hilo jambo likaongelewe kifamilia, nilijaribu kumsihi huyo mjane, lakini hakunielewa,...sasa ulitaka mimi
nifanye nini…’akasema.
‘Sikiliza hayo ya sheria..nk, ya mahakama, nk…achana nayo
kwa sasa, mimi naomba hilo jambo moja,...…’nikasema
‘Sikuelewi, wataka mimi nifanye nini sasa…?’ akauliza
‘Mimi nataka unisaidie jambo moja , fanya uwezavyo, huo
mnada kesho au kesho kutwa usifanyike…’nikasema
‘Unasema nini,…hahaha, mimi nitawezaje kufanya hivyo, mimi sio juu ya sheria, na sina uwezo huo,...hapana ,
mimi hilo Siwezi…’akasema
‘Kumbuka …leo kwa huyo mama kesho yaweza kuwa kwako, una
watoto, una mke, na wewe ulikabidhiwa dhamana ya hii familia, uitetee kisheria,
sasa je kama ni kweli imedhulumiwa, hebu fikiria hilo,….utakuja kubeba lawama
kubwa mbele ya mola…’nikasema
‘Tatizo hunielewi…tatizo wewe kila kila kitu unakichukulia
kihadithi,…kinadharia zaidi, kusadikika au kifkirika, acha mambo hayo, mengine hayafanyiki kihivyo… haya sio mambo ya
paukwa pakawa, unanisikia, ni sheria ndio inayoongoza, vielelezo na mashahidi,
na polisi pia…’akasema.
‘Lakini sheria inasimamiwa na watu..na watu hao hao wanaweza
kucheza na hiyo sheria, haki ikawa sio haki, mangapi tumeyafanya pamoja nawe
tukaja kugundua ukweli uliokuwa umejificha,..unanielewa lakini, mimi hapa hisia
zangu zinanituma kuwa kuna jambo limejificha, sio bure,. kuna watu hawana huruma na hawa mayatima na mjane,,,.tafadhali lifikirie
hilo,…’nikasema
‘Unataka kusema nini, unafikiri mimi sikulihangaikia hilo jambo…maana wewe hujalifahamu jambo vyema
kama sikosei...hujaufahamu undani wake..
'Ndio nataka, lakini tunacheza na muda hapa,..mnada ukifanyika kila kitu kimemalizika, utafanya nini tea hapo...'nikasema
'Hayo yanafanyika kisheria...sikiliza, wwe ukija kulifahamu utaona kweli wake kuwa hakuna cha kufanya hapo…na zaidi wameshakubaliana
na vielelezo sahihi vipo wewe, hujui tu.., mimi nakufahamu ni huruma zako, lakini huruma
zitasaidia nini kama mke na mume hawakuwa kitu kimoja, ..au nikuulize huyo
mjane kakuambia nini..?’ akauliza.
‘Utanisaidi au hutanisaidia…?’ nikauliza, na mara akakata
simu.
****************
Baadae nikarudi kwenye ile familia,…niliwakuta wanafamilia
hao wapo wamekaa vila vile, ….nikamsogelea yule mtoto mkubwa , yule mdogo
alikuwa kalala..
‘Hivi mumeshakula…?’ nikauliza
‘Tule nini sasa, tunasubiria baba yao mdogo kaahidi ataleta
chochoe, hajaonekana leo siku nzima, nahisi ndio anashughulikia hayo mauzo yah
ii nyumba…’akasema huyo mama
‘Ina maana, mnaishije humu…?’ nikauliza
‘Hayo yaache tu…mungu ndiye anajua…ningekuwa na afya yangu ,
ningeenda kuomba kazi hata za uyaya, ili watoto wangu waweze ku..ku…lakini
nitafanyaje migu bado haina nguvu,..najitahid lakini wapi…kila hatua nikodi bajaji,
pesa nitapatia wapi…’hapo akawa kama anataka kulia.
Nilijipapasa mfukoni, nikatoa chochote nikamwambia huyo mama
afanye jitihada wapate kula, ila mimi sitaondoka mpaka tuongee mawili
matatu….na huyo mama akatoka kidogo,…bado anatembea kwa shida, lakini niliona
ni bora afanya mazoezi kidogo,…nikasikia akamuita kijana mmoja akamtuma, vifaa, unga na dagaa..baadae vikaletwa, ….akawa
jikoni, na mimi nikawa naongea na watoto, na baadae simu ikaita;
‘Ehe niambia unasemaje sasa…?’ nikauliza
‘Nimeongea na watu wa benki…’akasema
‘Wanasemaje…?’ nikauliza
‘Kama nilivyokuambia hayo mambo yamekwenda kisheria,…hakuna
namna…’akasema
‘Wewe huwezi kufanya lolote kuweka pingamizi, kitu kama
hicho…mimi nakuaminia sana wewe, hebu fanya uwezavyo, kulichelewesha hilo
zoezi,…angalau tuweze kuliweka hili jambo kwenye mahakama tena..’nikasema
‘Siwezi…unanijua nilivyo, nikuambia jambo siwezi kweli
siwezi…’akakata simu. Ni kweli huyu jamaa yangu ni mpiganaji, mtetezi wa
wanyonge, kesi nyingi za namna hii zikipitia kwake, haki haipindishwi, na kama
kafikia kusema hivyo, basi hapa kuna jambo, hata hivyo sikuweza kukata tamaa, hisia zangu
zilituma kuwa hapo kuna dhuluma tu.
***********
Baadae familia ikapata chochote, halafu nikamgeukia yule
mtoto na kumuambia
‘Kwahiyo unapenda niongee na mama yako, nataka kusaidia tu,
sio kufanya mama yako aendelee kulia…?’ nikamwambia, wakati huo tumeshakuwa
marafiki, tumeonga naye mambo mengi tu, akawa kanizoe. Na nilipomuuliza hivyo,
….alimgeukia mama yake.
Mama yake akatikisa
kichwa kama kuwaambia wakubali tu, sijui kwanini nafsini mwangu niliona kama
natakiwa kuwajibika, lakini sikujua niwajibike kwa vipi,…kama rafiki yangu huyo
ninayemfahamu kasema hilo jamb haliwezekani, basi ..lakini hata hivyo, nikataka
kujua ukweli wa jambo lenyewe, ..
‘Mhhh…mimi bado hapo
sijaelewa,…hati za mashamba na mali ya mume wako walikuja kuchukua wao, ilikuwaje mpaka waweze kuzichukua
wao,..walizipataje,…, unanielewa swali langu lakini…?’ nikauliza
‘Nikuambie kitu, hawa shemeji zangu, wote walianzia maisha
yao humu, kaka yao alikuwa ndiye mlezo wao,…maisha yao yalianzia humu
ndani…baada ya hii nyumba kukamilika, ni miaka mingi nyuma,..hawakuanzia kuwa
mikononi mwake, leo…hata alipokuwa huko nje, alikuwa akiwasadia kwa hali na
mali,..
‘Kwahiyo kumbe wote mlikuwa mnaishi ulaya kipindi kile…?’
nikauliza
‘Ndio kimasomo na baadae kikazi….’akasema
‘Baadae mkataba ukaisha mkarudi hapa nchini…’nikasema
‘Ndio…’akasema hivyo, na nilipotaka kuuliza swali jingine
hakunipa nafasi akaendelea kuongea;
‘Na hata tuliporudii kutoka Ulaya,..tulianza kuishi hapa na
wao, walitoka kule kwenye nyumba ya wazazi wao, maana ilishachoka, walikubalina
wapauze..…na kwa vile wazazi walikuwa hawapo tena,…lile eneo, walkaliuza,
unajua tena mambo ya kifamilia, huwezi kuyaingilia. Hata mume wangu hakutaka
sana kuyaingilia hayo…zaidi ya kuwashauri, na wakakubaliana walichokubaliana,…sijui
zaidi…
‘Sasa kwa muda huo,…hawakuwa na sehemu ya kuishi, walikuja,hapa
wakawa wanaishi pamoja nasi humu ndani, …nyumba hii ni kubwa sana,…kwahiyo wao,
kama familia,…waliweza hata kuingia chumbani kwangu,….kuchukua kitu, wakitumwa
na kaka yao, kifupi wao walikuwa kama ndugu zangu tu…’akasema.
‘Ina maana…’nikataka kusema lakini hakunipatia nafasi,
akaendelea kuongea
‘Kwa vile walikulia humu, na walikuwa kama familia yangu,
kila kitu walikuwa wanafahamu wapi hicho kitu kipo, ikiwemo mikataba yote ya
mali za kaka yao, na hata walipoanza maisha yao,….waliendelea kufika
hapa,…’akasema
‘Ina maana wao kwa hivi sasa wameshaoa…wana maisha yao, wana
nyumba zao…au sio?’ nikauliza
‘Ndio wana wake zao, wana maisha yao, hata hivyo bado
walikuwa ni sehemu ya familia, tuliendelea kuwa kitu kimoja wakati kaka yao
yupo hai, wanakuja, wakiwa na tatizo, kaka yao anawasaidia…ninachotaka
kukuambia ni kuwa humu ndani walipafahamu sana, kila kitu walijua kipo wapi…’akasema
‘Kwani wewe hukuwemo humu kipindi hicho cha msiba..?’ nikauliza
‘Nilikuwemo, lakini kimwili tu..,….nina uhakika wao walikuja
kuchukua kipindi mimi sijiwezi,..nilizidiwa, hali yangu iliharibika kwa uchungu,
sikuweza kuamini, hadi leo akili badi haijakubaliana, nahisi kama mume wangu
bado yupo, siamini, sijui kwanini..kipindi hicho ….nilipoteza fahamu,…nikalazwa
hospitalini,…na … na siku nilipotoka huko, baadae ndio nikaanza
kujitambua..kidogo kidogo,….imenichukua muda sana, ni sizani kama nitakuja kuwa
vizur kama zamani ….’akasema
‘Je kwa hali hiyo, mashamba kuchukuliwa, ….wewe ulikaa kimia
tu, hukutaka kudai haki zako….maana hiyoo ni haki yako wewe na watoto wako au
sio….?’ Nikamuuliza
‘Nimeshakuambia hivi, hayo yote yalifanyika kipindi sijiwezi ,
kuuzwa kwa hayo maeneo….mimi nilipoteza fahamu , nikaja kupata fahamu, …nikawa naona
hivi…, lakini sijijui….nilikaa hivyo kwa muda mrefu,…ni-ni… nilikuwa nusu mfu…sasa
nahisi kipindi hicho ndio walikitumia, kufanya walichokifanya, na ndio muda
huo, walifika nyumbani na kuchukua hizo hati za mashamba,….sasa walichofanya
kwenye hizo hati mimi sijui,…’akatulia.
‘Una maana gani ukisema walichofanya kwenye hizo hati wewe
hujui….?’ Nikauliza
‘Maana hati zilikuwa na jina la mume wangu kama ndiye
mumiliki halali, sasa ….waliwezaje kubadilisha hizo hati na kuonekana kuwa
mashamba hayo ni ya kifamilia, ndio mume wangu kaandikwa kama msimamizi tu, sio
kama mali yake….’akasema.
‘Hizo hati uliwahi kuziona kabla…?’ nikauliza
‘Ndio…nimeshawahi kuziona, lakini sikuwa nimezitilia manani,…na
hapo mahakama ilitilia mashaka, niliposema sikutilia maanani, sina kigezo cha
kuthibitisha kuwa hayo yaliyoandikwa kwa sasa sio yale yaliyokuwepo, ..wakati
kuna sahihi na kila kitu…’akasema
‘Uliwaambia mahakama…?’ nikauliza
‘Ndio… niliwaambi kabisa hizo hati hazikuwa na maneno hayo
yaliyopo sasa, kuna maneno yamendolwa na kuongezwa mengine,….nikatakiwa kuthibitisha,
sina uthibitisho, sina mashahidi, mashahidi wote walisimamia upande wa
wanandugu hao….sasa,..mimi sijui hizo hati nyingine zilitokea wapi…’akasema.
‘Sasa hebu kidogo, nataka kuliweka hili jambo sawa,
uligunduaje kuwa hizo hati hazipo, na ukafuatilia kwa vipi…inavyoonekana
ulipita muda, si ndio hivyo, sasa kwanini ukaja kugundua kuwa hazipo au
zilikuwepo lakini zenye maelezo hayo..mapya…, na ulipogundua ulichukua hatua
gani..?’ nikamuuliza
‘Kiukweli, nisingeliweza kuligundua hilo mapema hivyo,
nilijua bado mashamba yapo,…sasa ni pale
nilipoweza kupata nafuu,….ni siku moja nikwama sana hatuna chakula, kuna
dawa zinahitajika,…watoto shule, maisha yalikuwa magumu kweli,, kumtegemea mtu
yataka moyo…ndio wazo la kuuza kipande cha shamba, likanijia.
**********
Siku hiyo niliongea na shemeji, yaani mdogo wa mume wangu,
nikamwambia;
‘Shemeji hali ni mbaya sana, na sipendi kuendelea kukupa
mzigo,….mimi nataka nitafute pesa…’nikamwambia shemeji
‘Utatafutaje pesa kwa hali hiyo, hali yako bado sio
nzuri…’akasema
‘Nitauza chochote kilichopo, …’nikasema
‘Oh…utauza nini sasa…?’ akauliza
‘Hata eneo la shamba…’nikasema
‘Eneo la shamba…!! Lipi hilo…?’ akauliza kama anashangaa
‘Ndio nitauza lile eneo la mume wangu, eneo letu, …si-ninaweza
kufanya hivyo…?’nikasema na kuumuliza
‘Unaweza, lakini eneo gani sasa…?’ akaniuliza kama ana
mashaka na ninachoongea, kipindi kirefu nilikuwa kama nimechanganyikiwa pia,
naweza kuongea hili , kesho hivi, kwahiyo hapo nikajua kama ananipima tu.
‘Si eneo aliloacha mume wangu, nayafahamu maeneo yetu
yote…’nikasema
‘Ok, sawa hamna shida, kama lipo eneo la mume wako, sawa..…sasa
sikiliza shemeji,…mimi nina miadi na wateja wangu, naondoka, utakuja kunifahamisha
wapi ulipofikia, ukikwama utaniambia au sio shemeji…’akasema na kwa haraka
akaondoka.
Mimi muda ule sikuwa na shaka, nilijua huo utaratibu wa
kuuza eneo hautasumbua sana, na kwa vile yeye ndiye msimamizi wetu, haitaleta
shida….ndio nikaingia ndani kwenye kabati maalumu ambalo mume wangu alikuwa akiweka
nyaraka zake.
‘Nilikuwa nimechukua ufungua wake, najua wapi
unakaa,…nikafika na kuchomeka ufunguo…kwanza nilihis ufungua sio wake,
unafungua, haikubali, nikavuta zile droo nashangaa kumbe hazijafungwa na
ufunguo,..ina maana zipo wazi, sio kawaida yake, hapo muda mwingi kumefungwa…,
‘Nani alifungua hili kabati….labda walifungua kipindi cha
kuhakiki mali za marehemu, hamna shida,…’nikajisemea hivyo, huku nafungua hilo
kabati,….ili nizione hizo hati,.. sikuona kitu zaidi ya nyaraka nyingine ambazo
hazihusiani na mashamba.
‘Ikawaje…?’ nikauliza nikiangalia saa.
‘Ikawaje tena, ….niliondoka hadi kwenye hayo maeneo, nakuta
yameshamilikiwa na watu wengine kuwauliza, wanasema wameuziwa na familia ya
mume wangu, …sikukata tamaa nikaenda hadi kwa serikali za mitaa, na wao
wakanithibitishia kuwa kweli maeneo hayo yameuzwa kihalali….’akasema
‘Kihalali kwa vipi…?’ nikauliza.
‘Walinionyesha nyaraka zote zinazoonyesha kuwa mali ile
ilikuwa ya kifamilia, na mume wangu alikuwa kama kiongozi tu, kwahiyo alipofariki
mali ile iliendelea kuwa ya kifamilia, na familia ni ya mume wangu, …’hapo akatulia akitaka kulia.
‘Mhh…basi yaonekana
uliumwa sana, ilikuwaje kwani, ni mshituko au…?’ nikamuuliza.
‘Kifo cha mume wangu kilinichukua sana, nilipatwa na
mshtuko, nikawa nimeishiwa nguvu mwili mnzima, wanaita kiharusi sijui, na
wanasema ni bahati yangu kuweza kupona haraka hivyo,… nilikuwa mtu wa
kitandani, siwezi hata kuinua mkono,…nilibakia hivyo kwa miaka kadhaa…ooh,
huwezi amini, lakini ndio hivyo…’akatulia.
‘Mume wangu akiwa hai, nilikuwa na kazi yangu, kutokana na
mshutuko huo, kuumwa huko, hata kazi niliyokuwa nayo nikafukuzwa, maana
walisubiria wee, ule muda wa mgonjwa kihalali ukapita, ikabidi waniachishe
kazi,…na pesa yote iliyobakia ya mume wangu ilitumika kunitibia,..kiukweli mimi
nilijua ni mtu wa kumfuta mume wangu huko ahera,…lakini….’akatulia.
‘Lakini nini…?’ nikauliza
‘Kilichokuwa kikinizuia ni hawa watoto…hebu fikiria sasa hivi
nipo hai wanafanywa hivi, je kama ningelikuwa nimekufa ingelikuwaje, yaani hapo
ndio namshukuru mungu kuwa alinijalia niendelee kuishi, japokuwa kwa hali
niliyo nayo, nimeshakata tamaa,…siwezi tena kupambana nao, lakini mungu yupo…’akasema
na kuinua mikono juu .
‘Pole sana…’nikasema.
‘Kwahiyo kwa miaka mingi nilikuwa kitandani sijijui…ikafikia
watu wananiona kama mnzigo, walioweza kuja kunisaidia ni ndugu zangu wa
kuzaliwa nao, na wao ikafika muda na wao wakachoka, maana na wao wana familia
zao, wana shughuli zao za kufanya…kuuguza mtu kama mimi ilikuwa ni kazi kweli,…siwezi kuwalaumu..’akatulia.
‘Na hao shemeji zako je na wake zao, walikuwa hawakusaidiii…?’
nikamuuliza.
‘Mhh, namshukuru sana huyu shemeji aliyekuwa amechaguliwa
kama msimamizi wetu…, kiukweli….sijui kwanini hili likatokea,….lakini
alijitahidi kuwa mwema kwangu.alinisaidia sana…hakukata tamaa, kunihudumia,
mengine ni ubinadamu tu siwezi kumlaumu…’akatulia.
‘Kwahiyo huyo shemeji yako, yeye ndiye alichaguliwa kama
msimamizi…au sio…kwa msingi gani labda.. kwa vile alikuwa mkubwa au ..si wapo
shemeji zako wengine…..?’ nikauliza.
‘Ndio yeye anafuatia, baada ya kaka yao yeye
anafuatia…’akasema.
‘Kwahiyo yeye ndiye
alipewa mamlaka yote, ikiwemo hiyo ya mali za marehemu, kuuza na..mambo yote ya
kifamilia au sio…..?’ akaulizwa
‘Ndio hivyo, lakini…’hapo akatulia
‘Lakini vipi ..?’ nikauliza na yeye akaweza kuongea hivi.
‘Unajua…..kutokana na hali yangu ilibidi ikafanyike hivyo,
na mimi hilo, japokuwa sikuwepo, japokuwa sikujua ni lini hayo yalifanyika,
lakini ilibidi hilo lifanyike, kiutaratibu, siwezi kulaumu hilo…unajua mimi
nilikuwa sina uwezo wowote hata wa kuongea mdomo huu ulipinda,..mate
yanajitokea tu… mikono ilikuwa kama sio yangu,..shemeji wa watu alijitahidi
sana namshukuru sana…unaniona naongea hivi, sikuwa hivi, nilikuwa mfano wa
maiti, we acha tu..’akasema.
‘Pole sana…’nikasema
‘Kiukweli nilijiona kama nimeshamfuata mume wangu, na
niliomba iwe hivyo, lakini nikiwawazia watoto wangu, nabadilika, najitahidi
angalau niweze kuinuka.
‘Sasa kwa kipindi hicho, maana ilichukua muda…ndio wakaja
kukubaliana wakiwemo ndugu zangu kuwa awepo mtu wa kuchukua hatua, na huyo shemeji
yangu ndio akachaguliwa akayachukua majukumu yote, ya mali, ya watoto, matibabu….akajitahidi
alivyoweza…na ubinadamu tena, sijui zaidi ya hayo….’akatulia akitikisa kichwa.
‘Mhh….naona hapa bado kuna maswali mengi,….nahisi wa
kuyajibu hayo atakuwa ni huyo shemeji yako, jinsi gani litokea wakauza hayo
mashamba, hati ilikuwaje,…itabidi nimuulize yeye,…’nikasema.
‘Umuulize..weeeh, chonde chonde…usije kujitakia matatizo, na
mimi kuniletea mabalaa mengine, sisi tumeshakabidhi kwa mola,..hatutaki tena
matatizo…’akasema.
‘Kwanini, mimi nataka kufahamu ukweli wote, huwezi
jua,…naweza kusaidia…’nikasema na yeye kwanza akaniangalia, …halafu akasema.
‘Sizani kama utaweza kitu kama yule bingwa wa kutetea
wanyonge kashindwa, wewe utafanya nini, wewe ni mwanasheria, wakili au nani
…’akasema hivyo.
‘Hayo mashamba mume wako aliyanunua kivipi…?’ nikamuuliza.
‘Kivipi kwa vipi, si alinunua kama wanavyonunua wengine,
ali…..’akasita kidogo.
‘Nauliza hivi, ….unajua kununua vitu, unaweza kununua kwa
pesa taslimu, au ukakopa pesa benk, kuna watu wanafanya miradi kama hiyo kwa
njia ya mikopo, wanakopa wanajenga, wanauza nyumba wanalipa madeni, labda mume
wako alikuwa na biashara kama hiyo…?’ nikamuuliza.
‘Hapana….mume wangu hapendi kabisa kukopa,..hakuwa na tabia
hiyo..’akasema.
‘Oh…sijakuelewa…’nikasema kwa mshangao.
‘Ndio hivyo, hakununua kitu kwa mkopo, si mashamba wala….’akatulia
‘Sasa..unanichanganya kidogo hapo,…kwanini sasa hii nyumba inapigwa mnada, na unasema, mume wako hakuwa
anapenda kukopa,, na hata kauli ya mtoto hapa, alidai kuwa baba yake hakuwahi
kukopa hizo pesa ilikuwaje sasa aje kudaiwa…, ina maana ni deni lilikuja baada
ya mume wako kuondoka, au ilikuwaje..labda
wewe hukuwa unalifahamu au..?’ Nikamuuliza
‘Nikuambie ukweli, katika kitu ambacho mume wangu alikuwa
hataki, ni kukopa, hasa mikopo yenye riba, mume wangu alikuwa mcha mungu sana,
na aliwahi kuniasa kipindi nilipotaka kujiunga na vikoba, kuwa riba ni sumu ya
mali halali, riba inatafuta baraka yote kwahiyo niachane na maswala ya kukopa kwa
riba,…’akasema
‘Sasa ilikuwaje mkopo huu ukatokea maana ni mkopo mkubwa
sana, au sio, mkopo wa kuweza kujenga jengo kama hili, au unaokaribia, au kwa
vile aliweka hii nyumba kama dhamana, au sio… itakuwa ni deni la mamiliona ya
pesa au sio …?’ nikamuuliza na hapo mjane huyu akajaribu kujinyosha na kusema;
‘Ndio maana nikasema haya huyawezi na mambo mazito….yaani hadi leo siamini na
sitaweza kuamini, mume wangu akope pesa bila kuniambia, …hilo sio kweli…’akasema
‘Mhh..hapo hata mimi nachanganyikiwa…’nikasema
‘Hayo ya mkopo, …ni mbinu za kuhakikisha kila kitu
tunanyang’anywa…mkopo huu sikukopa mimi, ..maana yaonekana hata mimi
nilishiriki,..na wala sijui ulivyokwenda hadi ikafikia pesa nyingi kiasi hicho,
hata mimi nashangaa, utakopaje, huku hujui jinsi ya kulipa, hiyo si mbinu
jamani…’akasema
‘Kwahiyo kumbe sio mkopo wa ujenzi wa hii nyumba…?’
nikauliza
‘Hapana, hii nyumba ilijengwa kihalali, haikujengwa kwa
mkopo, hilo wasingeliweza kulisingizia,…hati zote za nyumba zinaonyesha uhalali
wa jengo hili mume wangu alitunza kila kitu , jinsi alivyoingea na gharama zake…’akasema.
‘Sasa hili deni lilitokea wapi…?’ nikauliza.
‘Ni historia ndefu…kwa mujibu wao, mume wangu aliwahi
kukopa, lakini haikuonyesha wazi alikopa kwa minajili gani, anakopa
anarejesha,..ni …alikuwa na akaunti benk, hiyo akaunti ilimpa uhalali wa
kuchukua pesa zaidi, kwa mkataba uliopo,…yeye anatumia anarejesha, …hilo mimi sikuwa na
nalifahamu, mume wangu hakuwahi kuniambia hilo…
‘Sasa hadi kufikia kiasi kikubwa hivyo….halafu ..hapana sio
kweli…sizani kama mume wangu aliwahi kufanya hivyo…’akasema
‘Sasa ni nani alifanya hivyo…?’ nikauliza.
‘Atakuwa ni baba mdogo…’akasema mtoto wake na mama yake
akamuashiria anyamaze..
‘Kama mtoto anavyosema, yawezekana kuwa shemeji au msimamizi
wenu ndio alikopa, na wewe wakati anafanya hivyo, ulikuwa bado hujawa na
ufahamu, au ulivyoambiwa hilo deni lilitokea muda gani..?’ nikamuuliza
‘Lakini nikuulize unaniuliza haya maswali yote ili
iweje….sisi yote haya tumeshamuachia mungu, na nimekuambia hayo niliyoweza
kukuambia,…yatosha, naona huko tunapokwenda utakuja kuanza kuniletea mabalaa
mengine, sipendi tena…’akasema na kujikuanyata.
‘Samahani sana shemeji usione nakusumbua, nina nia njema na
nyie, nimeshahisi hapa kuna jambo,na mimi sitaweza kuondoka, mpaka niufahamu
ukweli, na sitaweza kulifanikisha hili, bila ya msaada wako…mimi eeh, natumia
kalamu kama silaha yangu, ninaweza kukusaidia sana…nimekuwa nikitumia, kalamu
yangu kuwasaidia watu wengi tu,…’kabla sijamalizia akasema
‘Mimi sitaki tena kuja kuonekana mbaya, mungu yupo, nasema
haya kwani kuna kipindi tulikuja kukorofishana na huyu shemeji yangu, akaongea
maneno mengi mabaya sana,…kuwa yeye kajitokea, bila yeye ningekuwa wapi, kwani
muda mwingi sana alijitolea kwa ajili yangu, akawa hahangaiki na familia yake
ananihangaikia mimi tu, mpaka anakosana na mke wake na kudhaniwa vibaya, sasa nimepona naanza kuleta kiburi…’akatulia.
‘Lakini vyovyote iwavyo ilibidi uulize, uhoji, maana hizo
mali ni halali yenu, na hilo deni, hulitambui au sio, ..si kweli kuwa una
mashaka na hilo deni, au sio…?’ nikauliza.
‘Ni kweli, hilo deni hadi kesho sikubaliani nalo…lakini
nimeshindwa, …na hata pale tulipotaka kufuata sheria za kimahakama, ..sikuweza
kabisa, …shemeji awali alitaka kunisaidia kwa hilo, lakini ikashindikana,..na
ilipofikia hapo, ndio akaanza kulalamika,…ndio maana imefikia muda nimeona
nimuachie mungu….inatosha’ Akasema sasa
akiwa hataki kuongea tena.
‘Kwahiyo kumbe uliweza kukusaidiia hadi kufika mahakamani
kudai mali yako,….au sio, sasa yeye atakusaidiaje wakati wao ndio waliodai kuwa
mali hiyo ni ya kifamilia,…?’ nikauliza
‘Nilijitahidi sana..na hutaamini , kwenye hatua zote hizo
nilikuwa sambamba na shemeji yangu, alinisaidia, kisheria na kila hali,…ikaja
kuonekana kweli ..yaliyofanyika yamefanyika kihalali, mashamba,..yaliuzwa
kihalali, ilikuwa ni mali ya wanafamilia wa mume wangu, sisi..ndio tulikuwa na
sehemu ya familia na walichofanya baada ya kuuza, sehemu yetu tulitengewa fungu letu la pesa , wanadai hiyo ndio ilinisaidia mimi kwa
matibabu..na..na…aah, hata sijui nikuambieje…’akatulia.
'Na nikuulize..kwanini unaogopa tukifufua hii kesi upya...?' nikauliza
'Siogopi,...lakini, hutaweza, kila kitu wanacho...na ..hata hivyo, naogopea sana maisha ya watoto wangi sitakie waje kuteseka tena,....hapana...'akasema
'Kuteseka kwa vipi...?' nikauliza
'Hayo tuyaache tu ...maana hata kiimani yangu ya dini hainitaki niamini hivyo,...japo dalili zote zilikuwepo, mim najali sana maisha ya watoto wangu kuliko chochote, kama ni mali wachukue tu, lakini wasininyanyasie watoto...'akasema
'Mhh....hapo sijakuelewa...'nikasema
'Ni bora usitake kujua zaidi kuhusu hilo...nimeteseka sana, nahisi wanafanya kila njia, ili nisalimu amri, na hapo walipofikia, siwezi tena.....tuyaache tu, ....sitaki jamani...'akasema
‘Na hebu nikuulize kwanza hili swali, kama hutajachana, hilo deni la hadi kupigwa mnada hii nyumba, lilikuwaje,... kisheria,....?’ nikauliza
‘Kisheria, kwa vipi…..?’ akauliza
'Mikataba nk....si lazima kuwe na mikataba, kuwa, ..wewe si unayafahamu hayo, huwezi kupata mikopo benki bila mikataba, au sio, sasa je hayo yote yalikuwepo, na wewe uliiona hiyo mikataba, ndio nataka kulifahamu hilo, unaweza kunisaidia majibu yake tafadhali.
'Mhh.....hivi wewe huhisi hali tofauti...?' akaniuliza
Kiukweli hata mimi pale nilihis mwili ukinisisimuka..lakini sikutaka kusema jambo, tangia niingie humo kulikuwa na hali kama hiyo.
'Ndio matatizo niliyo nayo hayo, tunaogopa hata kwenda kulala vitandani maana huko ndio balaa..ndio maana nasema hebu achana na haya mambo, kama ni mali wchukue tu, wasinitesee watoto, natumai umenielewa....'akasema
'Wewe si umesema huamini ...ushirikina, au sio...?' nikasema
'Siamini..ila upo,..na kwanini wapitie kwa watoto wangu...'akasema
'Kwani inakuwaje kwa watoto wako...?' nikauliza nikahisi kama joto, kama mtu asiyeonekana yupo karibu yangu...ni hali ambayo huwezi kuielezea,..lakini ni kama kuna mtu yupo karibu yangu...na nikaanza kujisikia vibaya,...kama nataka kupoteza fahamu hivi...
NB: MAMBO ndio hayo, msinione nilikuwa kimia , ni mitihni ya
hapa na pale….,
WAZO LA LEO:
USITENDE WEMA, ukiwa na malengo na kujinufaisha, wema
hulipwa na mwenyewe muumba, kama utataka unufaike na huo wema, basi huo sio
wema, hiyo ni biashara yenye kuhitajia malipo na malipo yake ukiyapata huo wema
haupo tena!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment