Mama yule sasa akanigeukia
lakini akiwa kainamisha kichwa chini, ….akainua kichwa kidogo, kiasi cha
kunitupia jicho,..sasa nikaweza kuuona uso wake, nilichokiona kwake ni taswira ya huzuni na kukata tamaa.
Ukimuangalia huyu mama kimavazi, kiukweli, nguo zake zilikuwa kuu kuu, na hali aliyo nayo
ni kama mtu aliyechanganyikiwa, nywele aliziacha zikawa timu timu, niliziona awali,japokuwa
aliponiona alikimbilia kufunika kichwa chake.
Alivyoniangalai ile ya haraka, niliona machozi,….hapo nikawa na uhakika kuwa kweli alikuwa analia.
‘Habari zenu….’nikasalimia na wote walibakia kimia, nahisi
walishachoka na hizo salamu.
‘Samahanii jamani nilikuwa nauliza tu, lakini naona kama
hampo sawa, kuna msiba, au kuna tatizo
gani limetokea..?’ nikauliza.
‘Msiba…?!’ akauliza huyo mama kwa mshangao, sasa
akiniangalia mimi machoni, kuashiria anashangaa na hiyo kauli yangu. Kijana wake yule mdogo akawa sasa anakodolea macho, yaliyojaa hasira, kwa muda ule nilijiuliza, ina maana kijana yule keshanikasirikia, keshaniona mimi ni mbaya wake, japokuwa hakuwa na ufahamu kuwa mimi sio dalali.
‘Kwa jinsi mlivyo,…mama unalia na hali yenu yaonyesha kama
mpo kwenye majonzi makubwa…’nikasema, na
yule mama akageuza kichwa kuangalia kwingine halafu akasema;
‘Hapa hakuna msiba kama ni msiba labda uulete wewe…, sisi
tupo salama tu, hatujambo kwa majaliwa ya mola wetu…, ila…. Hata hivyo, samahani
tunaomba usizidi kutuongezea machungu zaidi….’akasema.
‘Hapana mimi sina lengo hilo,…ila, kama binadamu kwa hali
niliyowaona nayo, inaniwia vigumu kuondoka bila kuwajulia hali, nia yangu ni
njema tu…’nikasema.
‘Sawa umeshatujulia hali, tumekuambia hatujambo, si inatosha
jamani, au kuna jingine … unataka tukusaidie nini…?’ akauliza huyo mama naona
alikuwa hayupo sawa.
‘Nataka kufahamu kama nyie ndio….sina uhakika, nyie mlikuwa
wapangaji wa humu ndani au…?’ nikauliza.
‘Wapangaji wa hii nyumba mhh!!....’akasema kwa mshangao hayo maneno huku akiniangalia
‘Nauliza tu…unajua tena, kwa hali niliyowakuta nayo lazima
niwe na ubinadamu wa kutaka kufahamu zaidi…na pia…’nikasema na kabla sijamaliza
akasema;
‘Hapana sisi sio wapangaji,….’akasema hivyo, sasa akitaka
kama kuondoka.
‘Oh, sasa mnfanya nini humu..au ..samahanini
lakini…’nikasema
‘Na mimi nikuulize wewe ni nani wakutuuliza maswali hayo
yote…mbona unatutia mashaka, maswali kama hayo niliwahi kuulizwa na watu wa
usalama au ndio kuna jipya limtokea tena..?’ akauliza
‘Samahanii kwa hilo,…kiukweli hali mliyo nayo imenigusa,
nilikuwa nimekuja…’kabla sijamaliza akasema
‘Basi yatosha, ulikuja kukagua nyumba, si ndio hivyo, basi
umeshafanya hivyo, au kuna kitu kingine wataka kuniuliza kuhusu hii nyumba,
nikuambie…nyumba ni hii ndiyo unatakiwa kupigwa mnada, ikague tu…’akasema
‘Mhh…samahanini lakini, …sina nia mbaya…’nikasema
‘Sawa nimekuelewa,…’akasema
‘Nauliza tu, nilitaka kufahamu zaidi labda nyie mlikuwa
mkiishi humu ndani kama wapangaji au..…?’ nikauliza
‘Kama wapangaji, sawa uonavyo wewe, si ndio hivyo tena, kwa
vile ni wapangaji hatuna haki tena,….na..lakini kwanini unataka nini lakini,
wewe ni nani…?’ akasema hivyo na mimi ikawa zamu yangu kushikwa na mshangao.
‘Nia ni kujua zaidi tu, hasa nyie ambao, nimewaona kwenye
hii hali, hilo la nyumba, aah, tuwaachie wenyewe, nataka kujua zaidi kutoka
kwenye masahibu gani yaliyowakuta…?’ nikauliza
‘Tulikuwa aah…bwana, mimi naona uondoke tu, kwa leo siwezi
kuongea lolote….’akasema hivyo.
‘Mhh, unajua shemeji, mimi ni msamaria mwema tu, …natunga
sana hadithi, visa, na…najaribu kuwa karibu na jamii, na nikiona watu wapo
hivi, inanigusa sana, natamani kuyaandika yale yaliyowasibu…’nikasema
‘Tunashukuru…’akasema hivyo tu
‘Kwahiyo, nyie ni nani hasa, na kuhusu kuishi hapa
kwenye hii nyumba, sasa eeh,. unajua nakumbuka jambo moja, mwenye nyumba hii alikuwa akiwajali sana watu, na zaidi ..nakumbuka siku moja nilikutana naye, akasema yeye anaijali sana familia yake, kwa kila hali, na wale waliopo kwenye mikono yake, hata wapangaji wake, nakumbuka sana hiyo kauli, sasa nashangaa kidogo..'nikasema.
'Unashangaa nini sasa...?' akauliza huyo mama akianiangalia kwa macho ya kujiiba
'Nyie hali mliyo nayo,...'nikasema hivyo nikiwazia jinsi gani ya kuweza
kupata maelezo kutoka kwa huyu mama, maana inavyoonekana hataki kuongea zaidi.
‘Wewe umeshasikia kuwa nyumba hii inapigwa mnada…wenye nyumba hii hawana chao
tena,...wawe wapangaji au nani,...inabidi watafute sehemu nyingine ya kuishi, nyumba hii sasa sio mali yao…tulishapewa
notice, nyumba hii sasa ni mali ya hao watakaoinunua, …kama ni wewe haya kagua uondoke
zako, mtuachie na majonzi yetu,….’akasema huyo mama.
‘Mimi sijui kabisa kinachoendelea,…na kiukweli, nilivutika
tu niliposikia tangazo…kutoka kwa mpiga mbiu kuwa nyumba hii inanadiwa,… inauzwa,
na inatokana na deni, alilokopa, hajalipa…’nikasema.
‘Kama umesikia hivyo basi inatosha wewe unataka nini tena zaidi….’akasema
huyo mama na mtoto wake huyo mkubwa,akamkatisha na kusema kwa sauti kama ya
ukali.
‘Mwenye nyumba hii hajakopa pesa yoyote, waongo hao…mwenye
nyumba hii alikuwa ni baba yangu..’akasema na kabla hajaendelea mama akamziba
mdomo.
'Baba yako...alikuwa una maana gani!?' nikauliza kwa mshangao, hakusema neno , kwa vile mama yake alikuwa kamziba mdomo.
‘Mungu wangu, ina maana,…oh…kumbe,…ina maana nyie,ni…..oh,
nimekumbuka hata sura za watoto zinafanana,..na baba yao, oh…sasa jamani mbona,
ungeliacha tu mtoto aelezee, msiwe na mashaka na mimi…’nikasema.
‘Huyu mtoto anaongea tu,….’akasema sasa akizuia machozi.
‘Hapana sasa naanza kuelewa, …kwani baba yenu yupo wapi kwa
hivi sasa bado yupo Ulaya, alisafiri tena eeh….?’ Nikawauliza wale watoto, na
wote wakainamisha vichwa chini….
Ikawa kama nimetonesha kidonda kilichoanza kupona.
Mama akaanza kulia, na baadae watoto….
*************
Nikabakia na mshangao….baadae huyo mama akasema;
‘Baba yao ni marehemu….’
‘Unasema….Mungu wangu, …ina maana…oh, kwake tumetoka na
kwake ndio marejeo yetu, poleni sana, nisameheni tu sikujua jamani…’nikasema
‘Ndio hivyo, kama ulikuwa hujui sasa umeshafahamu…’akasema
huyo mama.
‘Oh poleni sana, mimi
sikujua siku nyingi sijapita maeneo ya huku, nashangaa hata huo msiba sikuwahi
kuusikia…’niliishiwa cha kuongea.
Kiukweli sikuwahi kusikia kuwa mwenye hiyo nyumba sasa ni
marehemu,….sikumbuki kabisa kusikia hata mtu mmoja akisema hivyo…watu walikuwa
na hamasa tu ya kuiona hiyo nyumba…kwa nia tofauti wengine wakijifanya
madalali, ili waende kwa matajiri waje kupata cha juu, wengine wakiitamani tu.. wengine ndio hao
akina pangu pakavu, tilia mchuzi kupata taarifa za umbeya.
‘Ina maana huyu…hata
siamini, Yule jamaa sasa ni marehemu…’nikabakia nimeduwaa.
‘Mbona ni muda mrefu sana mume wangu alishatangulia mbele ya
haki, na wengi walishasahau, ila mwenye kovu usizani kapoa, mimi nimekuwa nikiombeleza
miaka yote hiyo…na haya yanayotokea sasa yananizidishia machungu, na kuzidi kunikumbusha
marehemu mume wangu,….’ Hapo akaanza kulia
Halafu akasema
‘Nina imani, …kama angelikuwa hai haya yote yasingelitokea…’akatulia
na akavuta pumzi ya kutaka kulia zaidi
‘Pole…poleni sana na
mnisamehe tu, sikuwa na lengo la kuwakumbuishia msiba huo…’nikasema
‘Najua ndio basi tena,sitamuona tena… sasa sina jinsi
inabidi nikubaliane na hali halisi.., inabidi nikateseke kama wanavyotaka wao,
wanafikia kusema si ulikuwa unaringa, sasa kipo wapi, si…ulikuwa hivi....jamani,
lini nilifanya hivyo, ‘akatulia akijizuia kulia.
‘Hiyo ni ya kawaida kutoka kwenye vinywa vya wanadamu , wengi
hawawezi kuzuia hisa na ndimi zao, huo ni mtihani kwakweli…’nikasema
‘Lakini nina uhakika kama angelikuwepo hai haya yote
yasingelitokea…nina imani hiyo kabisa, hii sio bure tu…kuna mkono wa mtu…’akasema
huyo mama kwa uchungu.
‘Mkono wa mtu, …una maana uchawi au…?’ nikauliza
‘Hapana mimi nipo mbali kabisa na imani hizo za kishirikina,
uchawi upo, lakini mimi sina maana hiyo kabisa,…ila wewe elewa hivyo tu…’akasema
Akilini nilikumbuka yale maneno mazito ya mtu wa imani akisema; ‘mpende umpendaye ipo siku mtaachana naye,
kipende ukipendacho ipo siku utakiacha, ipende uipendavo hii dunia ipo siku
utaicha,…itakayobakia kwako ni amali yako njema tu,……
Na wakati nawazia hayo Yule mama alikuwa bado analia, nikamsogelea
na kuanza kumliwaza kwa kusema;
‘Tukubali tu shemeji, japokuwa ni hali ngumu, utafanya nini
tena mola akiamua,..tunabakia kusema
Yote ni mapenzi ya mungu, au sio…’nikasema
hivyo na huyo mama,akahema kwa nguvu
halafu akanitupia jicho, hakusema neno…
‘Ni kweli, YOTE NI MAPENZI YA MUNGU…’akasema akiwaangalia
wanawe.
‘Poleni sana na mola aiweke roho ya marehemu huyo mahali
pema peponi, roho ya mpendwa wetu huyo,
alikuwa ni mtu wa watu kwa kweli….’nikasema hivyo , na mama huyo japo
alijitahidi kutulia lakini hali ya kutaka kuendelea kulia ilikuwepo, hata
watoto walikuwa wanalia kimia kimia. Iliniuma sana, kama ningelijua nisingelianzisha
hilo….
‘Shemeji cha muhimu sasa sio kulia zaidi, kwa kuonyesha
mapenzi yako kwake, wewe uzidi kumuombea
marehemu maghafira na najua , nimjuavyo
mimi, mume wako atakuwa mahali pema peponi, yeye alikuwa mtu mwema sana,
alikuwa mtu wa watu,……’nikasema
************
Ni kweli huyo jamaa alikuwa mtu mkarimu sana, pamoja na
kutokea hukoo alipokuwa ulaya hakuonyesha ile hali ya kuringa, hakuweza
kukupita njiani na gari lake kama anakufahamu ni lazima atasimama akuchukue, na
hata kukufikisha nyumbani kwako, lakini sasa ndio hivyo hatunaye tena…Yote
mapenzi ya mungu. Kweli wema hawana maisha.
‘Ni kweli yote ni mapenzi ya mungu, lakini haya yanayotokea
sasa, yanatuzidishia machungu, maana kila alichokiacha sasa kinachukuliwa, hebu
fikiria hata haya makazi yetu ya hapa duniani, sehemu ya kujisitiri aibu zetu
nayo ndio hiyo wanataka kuichukua,...'akatulia kidogo
'Hebu jiulize...hawajiulizi hilo...hawana mawazo hayo tena,..je sisi tutakwenda kuishi wapi, au wanataka na
sisi tuwe marehemu, lakini siku kama hazijafika, hatutaweza kufa au sio, sasa
kwanini wanatufanyia hivyo….’akasema huyu mama akiangalia juu, kuiangalia hiyo
nyumba!
‘Oh…’nikaguna hivyo na huyo mama akaendelea kuongea kwa
sauti yenye huzuni
‘Hawa watu sijui mwishowe wanataka nini kwetu, walianza kutunyang’anya
kimoja baada ya kingine, mara mashamba , mume wangu alikuwa na mashamba yake
aliyanunua akiwa hai, hayo yote yamechukuliwa…’akasema
‘Yamechukuliwa na akina nani…?’ nikauliza
‘Hahaha, unauliza ni akina nani....'akasema huyo mama akiniangalia moja kwa moja
'Ndio....'nikasema
'Ni ndugu zake, ambao walikuwa karibu naye,..hao, walikuja kugombea mali za kaka yao, huku wakigawana bila aibu,....'akasema
'Kwa utaratibu gani...?' nikauliza lakini hakunijibu hilo swali yeye, akaendelea kuongea
'Waligawana na…na yote hayo
yalifanyika kipindi mimi sijitambu, nimekuja kugundua hayo, wakati huo mali zoe zimeshachukuliwa, ..mashamba....nitafanya nini tena, maana na wao wameuza kwa watu wengine...'akatulia
'Mimi...nimekuja kujitambua muda umeshapita sana...haya.., mimi nitafanya nini, nikasema
hewala chukueni kama ni halali yenu, sasa hata hii nyumba jamani…’akatulia
kidogo
‘Yamegawanywa kivipi, maana kuna utaratibu za mirathi au sio…?’
nikauliza
‘Waligawana bwana....hawakujali hayo...watoto si wadogo...kila mmoja akija na visingizio vyake, mara
hili shamba lilikuwa la familia, na mmoja akifa shamba linatakiwa kurudi kwa
familia, zipo hat za makubaliano hayo,..mara hili eneo walinunua kwa umoja wa familia eti walichangiana ndugu
wakanunua kwa pamoja kwahiyo sasa
linakuwa mikononi mwa familia..mara....mimi akili bado ilikuwa hajakaa sawa..
'Sasa ulifanyaje ulipotulia
‘Mimi Sikutaka hata kugombana nao, maana hadi sasa kama unavyoniona, sijakaa sawa,..bado akili haijaka sawa jamani,mimi kwa muda mrefu nilikuwa kama mfu, sijitambui…na hata hivyo, ningelisema nini…’akatulia
‘Nauliza hivi, si kuna hati za mashamba si zilikuwepo, wewe si unajua wapi zilipo au…’nikasema
‘Hati….zilikuwepo,…lakini si walizichukua, muda huo mimi sijitambui...aah..hayo tuyaache tu,
ila nikajiuliza ina maana sisi sasa sio
miongoni mwao tena, sio familia yao tena, jamani hata mimi labda,…mimi si
mjane, sina haki, lakini hawa mayatima hawana haki na mali hizo…, ’akatulia
akiwageukia
watoto wake mmoja mmoja!
‘Lakini hebu ngoja nikuulize kipindi hicho mume wako
ananunua hayo mashamba, wewe hukuwepo, hukushirikishwa,…?’ nikamuuliza
‘Nilikuwepo sana, lakini si unajua tena sisi wanawake, na na…..
usijifanye hujui kuhusu wanawake, inapofikia kwenye mashamba na mali, siwezi kumlaumu mume wangu kwa hilo…kiukweli yeye aliniambia ananunua hiki na kile na wakati
mwingine tunakwenda naye, lakini yeye kwa upendo aliokuwa nao kwa ndugu zake,
kila kitu aliwaweka wao mbele…’akatulia
‘Ina maana kwa namna fulani, ..sema tu ukweli, labda mume wako, kipindi hicho hakukujali au hakujali kukushirikisha kwenye mambo kama hayo, alikudharau kwa vile wewe ni mwanamke…?’ nikauliza.
‘Sio kuwa hakunijali, hapana…aliona kwa vile ndugu zake
wapo, na yeye ni kaka yao mkubwa, basi wanakwenda pamoja, mimi napewa tarifa
tu, …baadae nakuja kuonyesha eneo, sikuwa na lawama kwa hilo, nilijua mume
wangu anaanya hayo kwa nia njema…’akatulia
‘Ok….nimekuelewa, lakini…’kabla sijauliza akaendelea
kuongea.
‘Unajua mume wangu
aliwaamini sana ndugu zake, aliwafanya wao ni sehemu ya familia yake na alitaka
maendeleo ya wote kama familia moja,
yeye hakupenda ubinafsi, na ndugu zake walikuwa muhimu sana…kila akinunua
sehemu anawagawia na ndugu zake, lazima akinunua eneo anawanunulia na wao…kwa
masilahi ya familia, na maendeleo yao pia..’ akasema
‘Ikiwemo na wewe pia au sio..?’ nikauliza
‘Mimi si ndio yeye, alichofanya yeye kipindi hicho ni kama
nimekifanya mimi, sikuwa na wasiwasi wowote na hilo…’akasema
‘Kwahiyo wewe una ushahidi kuwa mume wako ndiye alinunua
hayo mashamba, na kama alifanya hivyo si
kuna hati na kitu kama hicho, mume wako hakukuonyesha, au ilikuwaje katika
manunuzi, mume wako hakuwahi kuandikishana na hao wauzaji…..?’ nikamuuliza
‘Kipindi hicho sikuwa natilia maanani, hayo sijui hati,
kuandikishana, nilijua wao wote ni kitu kimoja,…hao ndugu zake niliwaona ni
kama mume wangu tu.. sikujua haya yatakuja kutokea, sikujua kuwa hawa ndugu
watakuja kunibadilikia hivi,….mimi sikuwa na wazo hilo kuwa nichukue hati,
au….niliwaona hawo shemeji zangu kama alivyo mume wangu kabisa kabisa…’akasema
kwa uchungu.
‘Sasa kwanini walikuja kubadilika….?’ Nikamuuliza na yeye
akaona kama kukerwa na hilo swali langu.
‘Hayo mimi sijui…na kiukweli tabia hiyo hawakuwa nayo kabisa
kipindi kaka yao yupo hai…’akasema.
'Sasa....'nikataka kuuliza
‘Mhh, kubadilika ile ya ku...…….walianza kubadilika pale walipooa…nakumbuka hata
alipokuwepo mume wangu, ndugu zake hawa waliishi kwa ushirikiano na kaka yao,
lakini baadaye walianza mabadiliko fulani,….hasa pale walipooa, hata hivyo kwa muda huo
walimuogopa kaka yao….walikuwa wakimuheshimu sana kaka yao...’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema labda tabia hiyo ya ubinafsi ilichangiwa
na wake zao..?' nikamuuliza kwa umbeya ili kutaka kujua hisia zake
‘Mimi siwezi kuwasingizia wake zao maana msimamo ni mtu
mwenyewe, kama mume unatakiwa uwe na msimamo wako ujue nini majukumu ya
familia, usiyumbushwe, lakini kwa hisia
hizo zipo, ila kwngu mimi siwezi kusema zaidi ya hayo mungu ndiye anajua zaidi
ya hayo....’akatulia.
‘Sasa hao wake wenza kwa shemeji zako, hawakuwa na
ushirikiano mwema kama walivyokuwa shemeji zako, maana mlitakiwa muwe pamoja au
sio, kwani haya yanaweza kuwakuta hata wao au sio..?’ nikamuuliza
‘Wewe hujui sisi wanawake, tuyaache hayo tu....'akasema
'Hapana shemeji, ...nataka kujua zaidi,..huwezi jua...'nikasema
'Sikiliza..., kama umekuja
kutizama nyumba ndio hiyo, kama una hitaji kuja kununua haya bahati ni yako, au
kama u dalali haya..….’akasema.
'Hapana mimi si mnunuzi...wala sio dalali kama nilivyokuambia awali...'nikasema
*************
Alikaa kimia kidogo halafu akasema;
‘Kilichonishangaza hata kushindwa kuamini ni pale tu mume
wangu alipokwisha kulazwa kaburini, hayo mimi nimekuja kuhadithiwa baadae maana kipindi kirefu mimi nilikuwa sijitambui….’ hapo
akanifanya nitege masikio
‘Ilikuwaje…?’ nikauliza
‘Hao walioitwa ndugu, ambao niliishi nao kwa upendo akiwemo kaka yao, walibadilika, uroho wa mali ya kaka yao uliwatawala, ....hawakukumbuka tena ule upendo wa kaka yao,
Huwezi amini hadi sasa ule upendo wa shemeji zangu kwangu haupo tena…yaani hata siwezi kuamini, hata
wengine wananisingizia mabaya, hata siamini, niwezeje kumuaa mume wangu…yaani
inaniuma sana...’akatulia pale mtoto wake mkubwa alipomshika akimuashiria asiendelee
kuongea zaidi.
‘Mama akiongea hayo anazidi kulia…’yule mtoto mkubwa akasema
akiniangalia mimi, alikuwa na kama umri wa miaka tisa hivi kwa kumkadiria.
Pale nilipo niliwaza, nifanyeje, maana nataka niujue ukweli,
lakini kila ninavyozidi kumuuliza ndio kama namchochea kulia zaidi, na mtoto
huyo keshanipa kama angalizo, nisiendelee kumuuliza mama yake maana namfanya
aendelee kulia. Hata hivyo sikukata tamaa, nilijua muda ndio huo, baada ya hapo
huenda nisipate nafasi hiyo, nyumba itakuwa imeshauzwa.
‘Je nifanyeje….’nikajikuta nimesema hivyo kwa sauti. Yule
mama akaniangalia, halafu akasema;
‘Huna cha kufanya shemeji…hili hakuna anayeliweza,...zaidi ya yule asiyeshindwa, hakuna mwanadamu tena wa kuliweza hili...iliyobakia tumuachie mola...nimeshanyosha mikono yangu juu, nikisema haya yote ni kwa mapenzi yake, kama ni hali yangu, ....nitaipata, lakini kama mungu kapitisha hivyo...basi ...ni kwa mapenzi yake...’akasema hivyo..
‘Lakini nataka kufahamu zaidi…’nikasema
'Inataka kufahamu nini, ili iweje,...ina maana wenzako, wasomi...hapana, hili liache tu.....liache tu,....
NB: Nataka kufahamu zaidi, najua na wewe unataka kufahamu
zaidi, tusubirie sehemu ijayo
WAZO LA LEO:
Dunia hii ni ya kupita tu..tuipende tuipendavyo, ipo siku tutaicha,…mali zetu
na majumba yetu, tuchume tuchumavyo, hata kwa ufisadi, lakini ipo siku mali
hiyo tutaicha, tuwapende wapenzi wetu tuwapendavyo, wake zetu, waume zetu,
watoto wetu, wazazi wetu, lakini ipo siku tutaachana nao. Tukumbuke jambo
muhimu, ni nini cha kuondoka nacho, chenye faida kwetu,…ambacho hutaweza
kukiacha, kitakuwa msaada wako, huko tuendapo… kwenye safari hiyo isiyo na
marejeo,…ni AMALI NJEMA TU.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment