Kisa kilianzaje….
‘Mnada ,mnada …. Kwa
niaba ya bank,… kampuni yenu pendwa ya Auction Mart, tunapenda kuwatangazia
mnada wa hadhara, tarehe …., wa kuuza nyumba kubwa ya kisasa, ili kulipia deni
la benki… fika ujionee mwenyewe…., fika ununue nyumba ya kisasa yenye kila
kitu, ikiwa na uwanja mpana, na sehemu kubwa ya kuegesha magari…’
aliendelea kutoa wasifa wa hiyo nyumba hiyo, huyu mpiga debe.
Watu wakawa wametega masikio,.. huku kila mmoja wetu
akijiuliza hiyo nyumba ni nyumba gani yenye hizo sifa nyingi hivyo, na kwanini
mwenye nyumba akafikia kiasi hicho cha kuachia nyumba yake ipigwe mnada, au
yeye mwenyewe kapenda ifanyiwe hivyo tu, kwa malengo yake.
Nikasikia jamaa mmoja akisema;
‘Hiyo itakuwa ni ile nyumba ya Yule jamaa aliyekuwa ulaya,
…’akasema.
‘Jamaa wa Ulaya…!!’ nilisema hivyo kwa mshangao…..
‘Kwanini,..mbona yule jamaa alikuwa anajiweza sana…’mmoja
akasema na kukawa na maongezi , unajua tena wabongo kujadili watu ni hulka
yetu,…hata hivyo kelele za pale zilinifanya nisifuatishe hayo maongezi yao, kwani
nilishaelewa ni nyumba gani hiyo:
‘Nyumba ya mtu wa
ulaya,…’
Maeneo ya hapo kwetu, ukisema nyumba ya yule mtu aliyekuwa
ulaya anatambulikana sana…na hata mimi mwenyewe niliwahi kupita maeneo hayo lakini ni siku za nyuma…kipindi hicho ndio
ilikuwa inamaliziwa maliziwa kwenye ujenzi wake,…na kila mtu aliyeiona hiyo nyumba,
alibakia kuisifia..na ukiuliza hii nyumba ni ya nani watu waliishia kusema;
‘Ni ya mtu mmoja kutoka
ulaya….’ Ikawa imetambulikana hivyo…’nyumba ya mtu kutoka ulaya..’ baadae
nyumba ya mtu wa ulaya…!
Ni siku nyingi, ni miaka naweza kusema hivyo… na huyo jamaa
mwenyewe niliwahi kuonana naye kipindi hicho hicho cha nyuma, na kwa vile
alikuwa mkarimu, nilibahatika kupata lifti ya gari lake, …ni muda kwakweli, baada ya hapo sikuweza kuonana naye tena.
Sasa kwanini nyumba yake inataka kuuzwa…ilinipa maswali
mengi kichwani,.., ina maana labda alijenga nyumba hiyo kwa mkopo ,au hata
sijui ilikuwaje, na je hana familia inayoishi hapo, mbona nasikia kama kulikuwa na watu wanaishi
kwenye hiyo nyumba,..labda ni wapangaji….
Na kama inauzwa huenda, hao wenye nyumba labda hawapo tena
hapa nchini, na kama wapo hapa nchini basi watakuwa wanaishi kwenye nyumba
nyingine.
‘Ngoja nikaitembelee hiyo nyumba, nijionee mwenyewe, na
huenda na mimi nikawa dalali wa kumtafuta mnunuzi,…’nikasema hivyo nikitaka na
mimi niwe mdadisi kidogo kupoteza muda.
Ni kweli udadisi huo
ulinisukuma hadi nikafika kwenye eneo la hiyo nyumba, na kiukweli, kila jambo
mungu ndiye mpangaji, hisia nanguvu za kunifanya nifike pale, zilikuwa sio
bure,..niliyokutana nayo huko, yalifanya nikiandike hiki kisa, ni ya huzuni,
utapeli, mauaji, na kwa kifupi, ni dhuluma tupu.
*************
Haya ilikuwaje…
Siku hiyo nikawa natembea kwa haraka huku nikiongea peke
yangu.
‘Nahisi jamaa alienga hiyo nyumba kwa mkopo, na kwa vile ana
pilika pilika nyingi huko Ulaya huenda kapitiwa au ni njia moja wapo ya kuuza
hiyo nyumba, apate malipo alipe mkopo na kubakiwa na chochote kitu,..!’
Mbwembwe za mpiga
hiyo mbiu, ziliwavuta wengi kwakweli, sikuwa peke yangu niliyevutika kwenda
huko, watu wengi walielekea huko kila mtu akiwa na lake kichwani, na sikuweza
kuongea na yeyote, maana kila mmoja ana lake….
Sio mbali sana, ni
sehemu ya kutembea kwa miguu tu…hutaamini kipindi nilipofika eneo hilo awali,
kulikuwa na uwazi mkubwa, kabla ya kufikia hiyo nyumba, sasa hivi karibu yote
imejaa nyumba,hata njia za kupita zimebadlika, ikabidi kuzunguka kidogo,…hatimaye
nikaiona hiyo nyumba kwa mbele yangu, huwezi kuipotea, ipo na mjengo wa
kitofauti.
Nyumba yenyewe ilijengwa kama juu ya mlima hivi, sehemu ile
imeinuka kidogo…kwahiyo ili ufike kwenye eneo lenyewe, ilipojengwa hiyo nyumba, inabidi uwe kama unapanda kimlima kidogo.
Sikuwa na wasiwasi, kwasababu hiyo nyumba ilikuwa inapigwa mnada nilijua sitapata
kizuizi cha kuweza kuingia ndani na kuikagua, japokuwa imezungushiwa ukuta
mkubwa,…
Nilipofika, niliwakuta watu wakiikagua hiyo nyumba , lakini
wengi kwa muda huo walikuwa nje ya geti, nikahisi huenda watu hawaruhusiwi
kuingia ndani ya geti, lakini sio hivyo, wao walishaingia na sasa walikuwa
wakihakiki kwa macho tu, wengine wakiipiga picha..siku hizi tena, kila kitu kupigwa
picha, selfie ..ndio hivyo!.
‘Vipi jamani naruhusiwa kuingia ndani…?’ nikauliza
‘Ruhusa…unaweza kuingia geti lipo wazi…’nikaambiwa!
Kwenye ukuta wa hilo
geti nikaona tangazo…
‘Kwa niaba ya…….’
Sikutaka hata kuendelea kulisoma tangazo lenyewe nikaingia
ndani…
Mashallah, …kiukweli ilikuwa ni nyumba kubwa, na mjengo wake
kwa mbele tu, ulikuwa ni wa kipekee,
wanasema ramani hiyo jamaa alikuja nayo mwenyewe kutoka ulaya,…na mafundi wake
walikuwa wa kimataifa, na ilijengwa kwa gharama kubwa sana …na kile aliyeulizwa
kuhusu muundo wa nyumba hiyo aliishia kusema huo ni muundo, wa kutoka ulaya.
‘Huu ni muundo wa huko huko Ulaya, unaona toka chini ilivyo,…imeanza
na mawe magumu, hakuna matofali zaidi ya waya za nondo....inakuwa kama
imewekezwa juu ya mawe ukiangalia kwa nje…basi ndani baridiii..utafikiri upo
ulaya…huhitaji kiyoyozi..jamaa aliona mbali huyo… lakini ndio hivyo tena…!’akasema
jamaa mmoja alipoona naangaza macho kuangalia yale mawe yalivyopangwa, ni mawe
makubwa,magumu…
‘Ndio hivyo tena…’na mimi nikasema hivyo nikiwa kama nataka
kuuliza, lakini huyo jamaa simu yake ikawa inaiita, kwahiyo akageuka upande
mwingine na kupokea simu, sikuweza
kuongea naye, na kwa vilenimefika mwenyewe nikaona nijionee mwenyewe.
Watu walikuwa wakiingia na kutoka, na kila mmoja aliyetoka
huko ndani aliongea la kwake, lakini mimi kichwani nilitaka kufahamu hatima ya
familia hiyo, wapo wapi,.pamoja na mengine, ukiwa mwandishi unakuwa na jicho la
tatu.
Nikawa natembea hatua za taratibu huku macho yakifanya kazi
yake ya kupiga picha eneo, na nyumba yenyewe,…
‘Mimi ndio maana naogopa kukopa, sasa mtu kakopa pesa nyingi
kiasi hicho cha kuwezesha kujenga nyumba ya gharama kiasi hiki, leo hii
inapigwa mnada, na je wao wenyewe watakuwa wanaishi wapi, maana hali kama hiyo
inaweza ikamfanya mwenye nyumba akadondoka kwa shinikizo la damu!’ nikasikia
mmoja akisema huku akikimbilia nje.
Na mimi kwa muda huo nikawa kama tajiri anayetaka kuinunua
hiyo nyumba, natembea taratibu nikigeuka kushoto na kulia,…huku nikivutiwa na
bustani na mua yaliyopandwa pembezoni mwa njia…
Sasa nikifika kwenye mlango mkuu wa nyumba yenyewe…marumaru
ziliwekwa kwenye njia, zenye nakshi
nzuri, na moyoni nikatamani , kama ningelikuwa na pesa, mhh, ningeli inunua hii
nyumba,….hahaha…itakuwa mwendo wa mamilioni kama sio bilioni, ikawa ni ndoto za
Alinacha, kuwaza kwa hamasa ya ‘Ngeli…’ ningekuwa, ningeli…ndio hivyo tena.
Kiukweli ni nyumna nzuri, na mazingira yake yanavutia, utafikiri
upo wapi vile, u-la-ya…..!
Sasa nikawa nipo kwenye mlango wa geti dogo la kuingilia
kwenye nyumba yenyewe, hapo …nikageuka kulia , kwa mbele zaidi nikaona eneo
kubwa limepandwa miti na migomba, na ..ndege walipita huku na kule, wakifurahia
mandhari
Sasa ..nikageuka kushoto, mara nikasikia sauti!
Mwanzoni nilijua ni watu waliokuja kuitizama hiyo nyumba
lakini haikuwa hivyo, ni hali kama upo kwenye magofu hivi, unahisi kama kuna watu lakini huwaoni, ..ndivyo nilikuwa nahisi kwa muda huo,..hata hivyo, kulikuwa na sauti nyingine, sauti halisia...ni kama mtu analia au
watu wanalia,....
‘Hapa kuna tatizo, nahisi…’nikasema na kweli nikahisi nywele
zikinisisimuka,…nikasita kutembea, nikageuka nyuma kuhakikisha kama sipo peke
yangu, maana nahisi kama hakuna amani tena..nikaona watu, nikajipa moyo kuwa
hakuna matata…
Kukawa kumetanda ukimia kidogo…hapo nikainua hatua moja , mbili , tatu, nikafungua lile geti dogo la nyumba,…lilikuwa
wazi unasukuma tu kidogo,…hiloo, likafunguka, na hapo tena nikakutana na ngazi za maru maru
za kuelekea juu, ni kama tano hivi, ili uufikie mlango wa nyumba yenyewe,..moyo
ukawa na wasiwasi, sijui kwanin, nahisi ni kutokana na ile sauti kama ya mtu
analia…
Sijui kwanini, nilianza kuhisi mashaka,…wasiwasi na hata
woga,…
Nikaona nisipoteze muda,… nikaanza kupanda zile ngazi ya
kwanza, ya pili ya tatu,nne, tano… nikawa sasa nauangalia mlango, nikataka
kugeuka kulia na kushoto, lakini sikuweza maana macho yangu yalinasa kitu,…pale mlangoni kuna
tangazo jingine, sio kubwa kama lile la kule nje...
Nikalisogelea sasa…lakini sikuweza kulisoma hilo tangazo,
macho yangu yakawa yamenasa kitu kingine, na akilini niliendelea kuhisi kama kuna hali ya watu wasioonekana hivi....mwili unasisimukwa, na macho yangu kwa muda ule,yakanasa kitu kingine kitu ambacho,..kilichonivutia zaidi...
Na kwa..., kupitia kwenye
mlango, uliokuwa nusu wazi, nikaona jambo...akili yangu sasa ikawa kama imefunguka na zile sauti za kama upo kwenye gofu, lililohamwa, halafu unahisi kuna majimizi hivi, zilikaniondoka,..ila bado moyo wangu ulikuwa na wasiwasi, ….
Nikasimama …kwanza sikuamini, maana nilijua humo kwenye hiyo
nyumba hakuna mtu mwingine tena,…mpaka inafikia kunadaiwa ina maana wenyewe watakuwa hawapo
inawezekana wapo kwenye nyumba nyingine au wapo ulaya, au labda hapo kuna
wapangaji bado au walinzi, ….mhh lakini niliowaona walinipa mshawasha wa moyo,
nikasahau hata kulisoma lile tangazo.
Ni akina nani hawa…? nikajiuliza.
Sasa nimesimama usawa wa kitu kama kibaraza…nikawa najongea
ili niweze kuona kupitia kwenye ule upenyo wa mlango uliopo wazi…
Kule ndani niliwaona watu,…walikuwa watatu, ni mama mmoja
akiwa kakaa mkao wahuruma, ule mkao wa mtu kukaa chini, miguu imejikunja na kichwa
kinakuja kulala kwenye magoti…na pembeni yake kulikuwa na watoto wawili,….ule
mkao sio wa kawaida…na hali zao sio za kawaida, zinatia huruma.
Mama Yule alikuwa kama analia, ….! Nina uhakika alikuwa
analia….
Kwanini analia, nikawa najiuliza sasa….na cha ajabu watoto
wake walionekana kama wanambembeleza, inawezekana ni watoto wake…sikuweza kuiona sura ya huyo mama
kwa haraka , kwani kichwa kiliinamishwa
na kuficha sura,…oh masikini, yaonekana wamakutwa na janga wakiwa
hawajajiandaa, moyo wa huruma ukanijia,..au labda wamefiwa, hata kama wamefiwa kwanini wapo
kwenye hii nyumba, na mbona wapo peke yao…!
Nikawa nimepigwa na butwaa,…..
Mtoto mkubwa alikuwa
upande wa kushoto kwake, akiwa naye kakaa chini na mkono wake mmoja wa huyo
mtoto upo kichwani kwa mama yake, na mtoto mwingine yeye alionekana sio mkubwa
sana, alikuwa naye kakaa akiwa kajiegemeza ubavuni kwa huyo mama, na alikuwa kainama kuficha uso,
huenda na yeye alikuwa analia.
Hali hii ikanifanya hisia zangu zote zipotee, hisia z nyumba
nzuri, hisia za…sasa nahisi napambana na hisia za huzuni, moyo wangu ukaelekea
kwenye Nyanja yangu ya jamii
‘Huenda humo pia kuna msiba,…’ nikajisema na mwili wangu
ukazidi kusisimukwa…
Hata hivyo akili
iliniambia hapa kuna zaidi ya hilo la nyumba, kuna jambo kubwa nyumba ya pazia,
na nyumba imekuwa ni sababu tu iliyoniwezesha kufika hapo, ….nikavuta pumzi na
kumuomba mola wangu, maana hali kwangu mimi kinfasi nilishahisi mashaka,…ni
namna nilivyojengeka kuhisi jambo, na nikihis jambo ujue kuna jambo.
Ndio nikaanza kusikia yale mazungumzo...
‘Mama sasa sisi
tutakwenda kuishi wapi…?’ Nilisikia sauti ya mtoto ikiwa kama inalia na
kulalamika.
‘Hata sijui…’sauti ya
mama akajibu kwa mkato kama kukerwa vile.
‘Kwanini wanataka
kuuza nyumba…sisi tutakwenda kuishi wapi, …?’ ilikuwa ni sauti ya mtoto mdogo wa pili.
*********
‘Hodi tena sijui ni
wenyeji au ni ….’ Nikasema sasa nikisukuma mlango, ili niweze kuingia ndani…
nikaona sasa nakabiliwa na mtoto mdogo machoni kajawa na hasira, nikashikwa na
butwaa, na aliyeweza kunisaidia ni huyo mama, akamshika mtoto wake, ….
NB: Mambo yalianzia hapo....tuendee….!
WAZO LA LEO: Sio vyema kujengeana dhana mbaya,
tukawa tunajenga hisia ambazo hatuna uhakika nazo..tukasambaza mapicha, maelezo
kwa nia mbaya tu…. Jiulize je kama sio kweli, na hapo ulishasema na kunadi kuwa
huyo mtu yupo hivi na vile..na sasa hivi kwasababu ya mitandao, habari huenea
kwa haraka sana. Hebu jiulize ungelikuwa ni wewe umefanyiwa hivyo
ungejisikiaje. Dhana mbaya kiukweli hazijengi, na madhara yake ni kuleta chuki
na uhasama katika jamii.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment