YOTE NI MAPENZI YA MUNGU
(Duwa ya menye kudhulumiwa)
‘Mama sasa sisi tutakwenda kuishi wapi…?’ Nilisikia sauti ya mtoto ikiwa kama inalia na kulalamika.
‘Hata sijui…’sauti ya mama akajibu kwa mkato kama kukerwa vile.
‘Mama kwanini wanataka kuuza hii nyumba…?' akauliza mtoto mmojawapo na kabla mama hajajibu mwingine naye akauliza
'Na sisi mama tutakwenda kuishi wapi, …?’ ilikuwa ni sauti ya mtoto mdogo zaidi.
Pale niliposimama niliweza kuona kwa ndani kupitia nafasi ndogo ya mlango uliofunguka nusu…,niliweza kuwaona, alikuwa mama, na watoto wawili, mtoto mmoja kakaa upande wa kushoto mwa huyo mama, na mwingine upande wa kuliani kwake.
Mmoja alionekana mdogo, alikuwa kama kamlalia mama yake, japokuwa kakaa sakafuni, na huyo wa pili ni mkubwa kidogo wa wa huyo mdogo, yeye pia kakaa sakafuni lakini kawa kama kamuegemea mama yake begani,…
Mama yeye alikuwa kainamisha kichwa chini huku kashikilia shavu! Ule mkao ni ule mkao wa mtu aliyetingwa na mawazo.
Kwa jinsi alivyoinama usingeliweza kumuona usoni,…ila kuna hali kama hayupo sawa, ni kama mtu aanyeyelia hivi,… nikajiuliza analia nini, …
‘Hawa watu ni akina nani, …haiwezekani wakawa ni wanafamilia, sizani kama wenye nyumba wapo hapo, sikuwahi kusikia kama wenye nyumba hiyo wapo au hawapo…labda ni wapangaji tu…’ nikawa najiongelesha kimawazo.
Mazungumzo yao yalinifanya nisogee karibu lakini sikubisha hodi kwanza, maana maneno yao yalifanya mwili uanze kusisimukwa...na kunifanya nigande kwanza,
Niligeuza kichwa na kuangalia nyuma kwanza,, niliwaona watu wakiendelea kupita pita huku na kule nahisi hata hao mama na watoto wake walishawachoka hao watu na kuwaona ni wale wale wenye lengo moja, la kukagua hiyo nyumba,
Wengi wao waliokuwa wakiingia na kutoka,...kabla sijaendelea kuwaangalia nikasikia, sautii ya mama ikisema.
‘Nimeshawaambia, tumuachie mungu mwenyewe tu, yeye ndiye atajua tutakwenda kuishi wapi…kwani haya yote yanatendeka kwa mapenzi yake, kwahiyo yeye ndio atajua tutaishi wapi…’akasema mama huku akijaribu kugeuka pembeni kuzuia machozi yaliyokwisha kuanza kumtoka, kwa wingi.
‘Tutakwenda kuishi wapi....hayo yote yanatendeka kwa mapenzi yake….yeye atajua tutaishi wapi…’ kauli hiyo ikaniganda akilini, sijui kwanini, na nafsi yangu ikatamani kusikia zaidii…
‘Lakini mama, baba mdogo si yupo,yeye atatusaidia, mwambie awazuie hao watu wasiuze nyumba …’ilikuwa sauti ya huyo mtoto mwingine...na kulitokea sauti sikuweza kusikia zaidi alichoongea
‘Baba mdogo..khaa..!? ..’sauti ikatulia nikaweza kumsikia mam akisema hivyo, halafu akatulia kidogo
‘Huyu baba yenu mdogo hatawasaidia kwa sasa…’akasema
‘Kwanini mama…baba ni mtu mnzuri?’ mtoto mmoja akauliza na kusema.
‘Hata yeye mwenyewe anataka hii nyuma iuzwe, hata simuelewi, …'akasema mama
'Mama..baba hawezi...'huyo mtoto mkubwa kidogo akasema
'Hata mimi simuelewi tena wanangu …hata sijui niwaambieje…mmh, …kwa hatua iliyofikia, iliyobakia tumuachiei mungu tu…’mama akasema.
‘Mama, sasa tutamuachiaje mungu, …wakati nyumba inataka kuuzwa, mungu atatusaidiaje…’akasema mtoto mdogo, kwa kauli ya kitoto inayoonyesha kutokuelewa uwezo wa mungu
‘Wanangu jamani…’mama akajaribu kusema lakini mtoto naye akaendelea kuongea.
‘Mama,…sisi tutakwenda kuishi wapi ...mimi huyo dalali akija hapa sitamruhusu , nitamzuia mama, nitapigana naye..eti kaka, tupigane naye.’.huyo mdogo akasema sasa akitaka kusimama.
‘Hata sijui wanangu,… niwaambieje ili muweze kunielewa, mbona mnataka kuendelea kuniliza tu, nina uhakika baba yenu angelikuwepo….angeli…., haya yote yasingilitokea, lakini tutafanyaje sasa..’akasema mama
Watoto walipoona mama yao analia, wakamsogelea na yule mkubwa kidogo akasema;
‘Ni mapenzi ya mungu mama…usilie..’ilikuwa suti ya mtoto mwingine, japokuwa likuwa mtoto lakini akili yake ilionekana kupevuka kidogo.
‘Ndio nyie mnataka nizidi kulia,..nyie aminini hivyo, kuwa hayo…eeh wananagu yanatokea kwa mapenzi mungu na mola wetu, ndiye anajua zaidi, atajua wapi tutakwenda kuishi..muamini hivyo, sawa wanangu..’ akasema mama.
‘Haya mama usilie tena, hayo yote ni kwa mapenzi ya mungu, tumuachie mungu si ndio hivyo mama, yeye ndiye atatuonyesha wapi tutaishi,…basi mama usiendelee kulia…’mtoto aliyeonekana ni mkubwa kidogo, akasema. Yule mdogo akawa sasa kajikunyata kwa mama yake, akionyesha huzuni, na hapo hapo akainua uso na kuangalia mlangoni, akaniona…
************
Niliposikia mazungumzo hayo, akili yangu ilianza kuchemka, nikawa nawaza zaidi ya upeo usiokuwa na na mawazo hayo kabla, nikawa najaribu kudadavua yale mazungumzo..ni kitendo cha muda mfupi tu….
‘Baba yenu angelikuwepo,…’ Huyo baba yao ndio nani, na huyo baba yao mdogo ni nani pia!
Mpaka hapo nikagundua kitu, kuwa baba wa hao watoto hayupo, huenda walikuwa wapangaji wa hiyo nyumba, na sasa hawajui wapi pa kuishi,…sasa huyo baba yao kaenda wapi, kwanini awaache wanafamilia hao, mama na watoto peke yao.
‘Hawa ni wapangaji tu..’nikajisema moyoni, kwani kwa kuwaangalia tu kwa macho ya haraka haiwezekani wawe..hapana..hawa ni wapangaji tu. Sijui kwanini akili yangu ilitaka kuwaza jambo ambalo huenda sio.
Pale pale kwa muda huo mfupi,nikajaribu kumkumbuka baba wa hiyo nyumba ambaye sifa zake zilienea kuwa yeye ni mtu wa ulaya, na familia yake ilikuwa nzuri yenye afya, alikuwa akiwajali sana familia yake, ndivyo watu walikuwa wakiongea hivyo,..
‘Kulitokea nini lakini kwa huyu mtu, iweje akubali nyumba yake iuzwe. Kwa maelezo ya mnadi, nyumba hiyo inapigwa mnada kwa kushindwa kulipa deni.
‘Deni la nyumba, au deni la nini…?’ nikajiuliza hapo kwa kimoyo moyo.
‘Au labda kasafiri, labda yupo ulaya, na huenda katingwa na mambo ya huko akashindwa kulipa deni fulani, sasa kwanini akubali deni hili lilipiwe kupitia kwenye nyumba yake, yaonekana ni deni kubwa sana…na hawa wapangaji watakwenda wapi masikini ya mungu, mama na watoto wake..’ nikawa najiuliza.
Sikutaka kuendelea kujitesa kwa mawazo, nikaona labda niwaulize hao niliowakuta humo ndani, na muda huo ndio yule mtoto aligeuka na kuniona nimesimama mlango nikichungulia kwa kupitia ule upenyo mdogo wa mlango,..mlango ulikuwa haujafunguka wote…
Hapo hapo ndio nikabisha hodi ….
‘Hodi jamani…?’ nikabisha hodi.
Wa kwanza kusimama ni yule mtoto mdogo, akajitutumua kama anataka kupanua kifua…kiukweli moyoni nilihisi kama kucheka, lakini huwezi, kilichotangulia machoni ni dalili ya machozi.
‘Mama…dalali huyo…mungu wangu..’ilikuwa kauli ya mtoto yule mwingine mkubwa. Naye akasimama, lakini kwa mashaka kidogo, Mama, akajiweka vizuri kujifunuka, kiadabu,..na alipoona yupo vizuri akawaangalia watoto wake..hata kabla hajaniangalia mimi..
‘Mama …’mtoto mdogo sasa anavuta tambo, akitaka kuja …mama akakurupuka na kumshika mwanae mkono.
‘Weeh, tulia, unataka kwenda wapi, usinitakie balaa jingine, njoo huku, bora nife kuliko kuwaachia nyie.. ..’mama huyo akawa sasa keshamvuta mtoto na kumweka pembeni yake na yule mwingine akasogea wote wakawa wamemzunguka mama yao,..mama kwa mikono yote miwili akawa kawakumbatia watoto wake, kama vile kuku anavyofanya kuwalinda watoto wake wasije kunyakuliwa na mwewe.
NB: Ni kisa kilitokea nyuma kidogo, na bahati mbaya hatukuweza kukimalizia, sasa nakianza upya na nataka twende nacho taratibu, tuzidi kumuombe mungu tukiendeleza…je mpo tayari na kisa hiki, kipo kingine kipya lakini naona tuanze na hiki kwanza.
WAZO LA LEO: Imani ya kweli ya mcha mungu, inaonekana kwa matendo yake, na hasa pale anapojitahidi kuwajali wenzake zaidi, anakuwa tayari kutoa kile anachokipenda kwa ajili ya wenzake, moyo wake unajali kuliko hata kujijali mwenyewe. Yeye anajua kuwa yote kayapata kutoka kwa mola wake, sio kwa ujanja wake, akili, uwezo, madaraka nk, ni sababu tu, …na kwanini sasa awe mchoyo kwa ndugu yake, rafiki yake, jirani yake.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment