Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, June 29, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-16


‘Mimi huko ofisini,…nimepata maagizo kwa wakubwa wangu, kuwa hapa kuna tatizo kubwa limetokea,  na kwa jinsi taarifa nilivyoipata, ….sio kitu cha mchezo,….sasa mimi nimefika, sitegemei kupotezewa muda wangu,…..haya niambieni…hapa kuna tatizo gani…?..’ilikuwa sauti yenye mamlaka.

Tukawa kimia….hata mie ambaye ndiye nilipiga simu, ilinibidi kwanza nitafakari la kusema,..namfahamu sana huyu jamaa,….hatuivani kabisa.

Mpelelezi alipoona kuna ukimia, akanigeukia mimi….

‘Niambie wewe, najua ni wewe ulyeipiga simu, na sizani kama ni yale mambo yako ya kutusumbua,..…sasa hebu niambie kuna tatizo gani hapa…?’ akaniuliza kwa sauti ya chini, kama vile hataki Dalali asikie, na mimi nikaona nisipoteze muda, nikasema;

‘Tatizo lipo, na lilikuwa ni tatizo kubwa sana….’nikasema

‘Lilikuwa…una maana gani…?’ akauliza akinikazia macho.

‘Kama unavyoona, huyo mama kalala hapo sakafuni, yule mtoto kule, alikuwa kazidiwa sana, hatukutarajia kuwa anaweza kuinuka…hali yake ilikuwa mbaya hadi kupoteza fahamu,… sisi tulishajua mtoto amekata roho, na hatukuwa na jinsi nyingine kama kuna kifo, utatoa taarifa wapi…na mama yake alipoona hivyo, ndio naye akadondoka na kupoteza fahamu…’nikasema.

‘Sikuelewi bado..mtoto kazidiwa,…halafu mumekaa nyumbani, mnawaita polisi, inakuja kichwani kweli…au …unajua jamaa yangu , usitake nifike huko ambapo sitaki kufika…’mpelelezi akasema
‘Tatizo lililopo lina utata mkubwa, na mimi niliongea na yule mpelelezi mwingine analifahamu sana tatizo la hapa, na nilijua angelikuja yeye, hata isingelileta haya maswali,..lakini kwa vile umetumwa wewe..basi lifanyie kazi…’nikasema

‘Lakini huyu jamaa yako…, kasema haya yaliyotokea hapa ni mambo ya kimila,…unajau tena sisi hatuwezi kuingilia mambo ya hivyo, tunawapa nafasi raia wafanye mambo yao, inavyoonekana hapa, ni wewe kuja kuingilia mambo yao, ..vinginevyo, uniambie wewe..niambie sasa, kuna tatizo hadi kuita polisi…?’ akaniuliza na mimi hapo nikatulia kidogo

Alipoona nipo kimia, akamgeukia Dalali…

‘Wewe umesema haya mambo yaliyotokea hapa ni ya kifamilia,…eeh, sijui kimila au sio…si ndio hivyo…?’ akauliza.

‘Ndio Afande…’akasema kwa haraka kama vile askari anapomjibu afande wake

‘Kama ulijua ndio hivyo, kwanini hukumuamba mwenzako,…maana taarifa iliyofika huko ofisin ni ya kuashiria kuwa hapa kuna jambo kubwa, ambalo linahitajai msaada wa polisi, ni sawa sisi tupo kwa ajili ya raia, kuona usalama wenu unaimarika,…sasa ..na zaidi taarifa ikasema tuje na gari la wagonjwa, na huduma za dharura..sielewi hapa, hebu niambieni nyie,…’akasema.

‘Kiukweli hali ilikuwa ni mbaya…na huduma hizo za dharura zinahitajika sana, kama nilivyokuambia kama angelifika mwenzako, haya yote usingeliyauliza, analifahamu sana hili tatizo….hii familia kwa sasa ipo kwenye hali mbaya, na..hatujajua hatima yake itakuwaje,…kama kesho,au lini, watakuja kufuukuzwa humu kwenye nyumba yao..hii nyumba inatakiwa kupiga mnada, je hii familia itakwenda kuishi wapi..’nikasema.

‘Je hilo ni swala la kuwaita polisi…?’ akaniuliza

‘Nilimuita mpelelezi mwenzako maana kuna kazi tulikuwa tunaifanyia kazi…lakini bado kulikuwa na ..tulihisi huyo mtoto kafariki, na maswala ya kifo,..taarifa yake tunaitoa wapi….’nikawa kama nauliza.

‘Lakini…bado mimi sijawaelewa…hasa wewe Dalali,…hebu niambie, kuna nini kinachoendelea kwenye hii nyumba, wewe si ndio msimamizi wa kila kitu hapa, hayo nimeambiwa huku ofisini, kuwa kila kitu nikuulize wewe,…hebu niambie kuna nini kinachoendelea kwenye hii nyumba, maana mimi nina kazi yangu nyingine hili nimepewa kama kazi ya ziada, nataka maelezo yakujitosheleza,kuna tatizo gani kwenye hii nyumba…?’ akauliza afande

‘Ni kweli afande…mimi ndiye nilipewa hilo jukumu la hii familia, baada ya kaka yangu kufariki, sasahaya yaliyotokea leo..naweza kuelekeza lawama zangu kwa ndugu yetu hapa…’akaninyoshea kidole, na mpelelezi akatikisa kichwa kama kukubaliana naye.

‘Yeye…, alipofika hapa, alitakiwa kwanza aje kuonana na mimi, ili niweze kumuelezea kila kitu, kuwa kuna mambo ya kimila, yenye masharti yake,…mimi sitakosea nikitumia lugha ya usumbufu, kaja kuisumbua familia, sijui, kwa…nini ilifikia hadi yeye kufika hapa, bado hilo sijaelewa, huenda alikuwa na nia njema tu….’akasema.

‘Je wewe ulikuwepo hapa Dar, au sehemu ambayo ni rahisi kupatikana…?’ akaulizwa

‘Simu si zipo bwana, huo sio utetezi kabisa, angelinipigia simu ningelimueleza, maana mimi nilikuwa safarini kurudi huku, mimi ningelimuambia anisubirie nifike kwanza,…kama nilivyosema awali, huenda alikuwa na nia yake njema, ila hakufahamu..kuwa kuna mambo ya kimila…ndio yakasababisha yote haya…’akasema.

‘Simu yako ilikuwa inapatikana, ..na nilivyopata taarifa, swala linalofuatiliwa hapa lilikuwa ni la haraka au sio, hebu…nikuulize wewe, je ulimpigia simu huyu Dalali, au sio, wewe ni dalali, nakukumbuka sana..?’ akawa anaongea akinigeukia mimi.

‘Ilikuwa haipatikani…alimpigia shemeji yake….’nikasema

‘Sio kweli, simu yangu wakati wote ilikuwa hewani, labda alipigia kipindi tupo sehemu ambayo haina mtandao…’akasema Dalali.

‘Yawezekana hivyo…lakini siungeliona simu zilizopigwa na wewe ukawa haupatikani, au sio…?’ akauliza mpelelezi, sasa akiwa kaniangalia mimi machoni, akiniangalia kwa dalili ya kuonyesha sasa kanipata.

‘Unajua afande..wangelijaribu mara nyingi, ..na hii familia ipo chini ya nani, ..ipo chini yangu, unaona kosa lilifanyika,, yeye angetafuta kila mbinu za kuwasiliana na mimi kwanza, ili nimpe tahadhari hizo, sawa huenda ni sababu ya mnada, lakini bado asingelitakiwa kuisumbua hii familia…’akasema

‘Kosa la usumbufu…’akasema mpelelezi

‘Mimi ndio naona hivyo..yeye kuja kuanza kumperekesha shemeji,..shemeji huyo ana mtatizo ya shinikizo la damu, hakutakiwa kabisa kupoteza fahamu tena… na matokeo yake ndio haya..nikuambie ukweli afande, kama huyu jamaa asingeliiingilia haya maswala, hii hali isingelitokea kabisa, kwahiyo lawama ni zake yeye, na zaidi, sikuona umuhimu wa kuwapigia nyie simu, …’akasema.

‘Kwahiyo wewe unamshukutumu huyu jamaa kuwa kaja kuleta usumbufu kwenye hii familia, au sio,..na ya kuwa yeye ndio chanzo cha  haya yote, yaliyotokea humu, na zaidi kawasumbua hata polisi, kwahiyo wewe unatoa taarifa hiyo kwangu, unamshitakia huyu jamaa au sio…?’ akaulizwa.

‘Hapana mimi sijamshitakia,..kama nilivyokuambia awali huenda alikuwa na nia yake njema, lakini yeye kakurupuka,..hakutakiwa kufanya hivyo..mimi kwa upande wangu nimemsamehe, hakuna tatizo, tatizo ni kwenu sasa, kawasumbua…mimi sijawapigia nyie simu, kama kupiga ni yeye, kwahiyo hilo swali, la ..kuna nini hapa, kwanini nyie mumeitwa, muulizeni yeye, mimi simokabisa…’Dalali akasema.

Mpelelezi akageuka taratibu kuniangalia, akabenua mdomo kidogo, kuonyesha meno, kama mtu anayetabasamu, ..halafu akasema;

‘Ndugu ..ndugu..yangu, hebu niambie…haya mambo yako utayaacha lini,….unajua, mimi sikutaka kabisa kuja  kupambana na wewe..unanifahamu nilivyo..nilishakuambia siku nyingi, haya maswala yana taratibu zake, je ulizifuata taratibu mlizowekewa, maana nyie mlijifanya kuwa mnasaidia jamii, haya niambia huku ndio kusaidia,..hilo liache, je wewe umefuata tartibu, hilo kwangu ni la muhimu sana…’akasema

‘Lakini…mimi kwa hivi sasa…sitaki jibu kwako, maana najua jibu lake nini, lipo wazi kiofisi..ila kama  nilivyokuahidi mara ya mwisho tukikutana mimi na wewe huenda ikaw ndio mwisho wako wa hii kazi yako, …isiyo na tija,..unataka nini, umaarufu, nenda kajiunge na siasa, au …anyway, tuyaache hayo kwanza..ila kwa hili, nakuahidi…, sitarudi nyuma…’jamaa akasema.

Mimi nikatabasamu kidogo, na kitendo hiki kilimfanya mpelelezi akunje uso, na kusema;

‘Unanidharau sio..ngoja utaona….’akasema huyo mpelelezi.

‘Ina maana kumbe mnajuana…ni mwenzako  kumbe…mnabifu…hahaha, sasa afande mchukue muondoke naye tu, ili niweze kuweka mambo yangu sawa, …mambo ya hapa, nitayamaliza mimi mwenyewe….’akasema Dalali.

‘Kama nimefika hapa, basi nataka kila kitu leo kimalizike, na siwezi kuondoka mpaka nihakikishe hili tatizo limekwisha,…kuongea hivi, sio kwamba nina tatizo na huyo mtu, ni maswala y autaratibu tu,…bado mimi nipo na wewe….’akasema mpelelezi, akimgeukia Dalali.

‘Hapa kwenye hii nyumba kuna tatizo gani, ambali linahitajia polisi…?’ akauliza sasa akimgeukia Dalali.

 ‘Lakini sio mimi niliyekupigia simu afande..’Dalali akasema.

‘Hilo najua..lakini bado kuna matatizo hapa kwenye hii nyumba, hakuna usalama, kuna matatizo ambayo yamekwenda hai ustawi wa jamii….na hadi mahakamani, …nab ado hayajafikiwa utatuzi,…hilo sio jukumu langu, lakini bado nataka kujua…maana nimetumwa, kiofisi…’akasema mpelelezi.

‘Muulize yeye, afande…’akasema Dalali.

‘Pamoja na yeye, mimi  nina mazungumzo na wewe pia, mazungumzo nyeti, unasikia, ok, ngoja niongee na huyu mtu …’akanigeukia mimi, na kusema;

‘Natumai kuna kitu umehis ambacho hakipo sawa, ndio maana umeamua kutusumbua, najua hizo ni moja ya mbinu zako,..mara nyingi nakupenda kwa kazi zako, ila unavuka mpaka…’akasema

‘Na sio kwamba naongea haya kwa kukupatia sifa, hapana, kuwajibika kupo pale pale,..sasa niambie je ulishamalizana na huyu jamaa..usije kusema mimi, nimekuja kuviruga kazi zenu, mnapenda kutusingiza ubaya, kuwa tunawazuia kuisaidia kijamii, najua mlivyo,..lakini mwenzako sasa hivi ananyea debe, tatizo ni hili hili, kujifanya mnajua mambo, ambayo haya hayawahusu..hizo sio fani zenu,…hizi ni kazi za watu wa usalama, mnafikiri sisi tumeajiriwa kwa kazi gani, eeh…?’mpelelezi akaniuliza na mimi nikasema.

‘Afande, mimi nakusikiliza wewe, ila nataka kukuambia jambo, hayo yote uliyosema, mimi nitakuthibitishia kwa vitendo, kuwa, hujasumbuliwa, kuwa hapa kulikuwa na tatizo kubwa, ambalo linahitajia, uwepo wenu…’nikasema

‘Ok….sasa kama hamjamalizana endelea na jamaa yako, ila ..ukimaliza hapa, tunaongozana mimi na wewe hadi kituoni, …unafahamu kosa lako ni nini….’akasema

‘Kiukweli mimi silifahamu hilo kosa langu…’nikasema

‘Utalifahamu tu, na safari hii lipo kisheria, sio mdomo tu, si ulisema nifuate sheria, safari hii nimefuata sheria, kwanza, unakumbuka kulitangazwa nini…blogs, mitandao, eeh,, hazitakiwi, mnatakiwa kusajili au sio…..pili, ukitaka kufanya mambo kama haya, ulitakiwa ufanye nini, hilo nalo sio kosa, eeh,..umevunja sheria baba, hilo unalo, au nimekosea…?’ akaniuliza huku akitabasamu kidharau.

‘Usijali afande….vyote hivyo, utavipata…bila shaka..’nikasema

‘Hahaha, umesahau kuwa mimi ni nani eeh… mimi ndiye mkuu wa kutoa hivyo vibali..hujasikia kuwa mimi ndiye bosi wa hicho kitengo,…sasa anyway, hilo tuliache kwa sasa, ila ukae nalo kichwani, ..’akasema na kumgeukia Dalali

‘Jamaa yangu hapa anasema hajamalizana na wewe…..unaonaje amalizane na wewe..namfahamu mtindo wake wa maswali na majibu, ..anatusaidia sana, ..’akasema

‘Kwahiyo yeye ni nani, ..ni mtu wenu..?’akauliza.

‘Sikiliza Dalali, yeye, kwa taarifa nilizozipata, ana shaka na hilo deni la marehemu kaka yako, kuwa sio halali, au sio, hata mimi nitafurahi kuyasikia hayo mambo…kama kweli deni lipo au halipo, mimi siwezi kumzuia kwa hilo, .. umenielewa?’ akasema na Dalali akaonekana kunywea, na mpelelezi akasema;

‘Ninawapa muda, wa masaa…eeh…’kabla hajamaliza, Dalali akasema;

‘Hamna shida afande,…nilishaanza kumjibu maswali yake, tatizo,..nilikuwa sijamfahamu vyema, nilihis labda ni  tapeli fulani, si unajua dunia imeharibika, ..ila kwa vile ni jamaa yangu, naomba usimuhukumu kwa kauli yangu kuwa kaleta usumbufu,..ni jamaa yetu, na shemeji yangu anamfahamu yeye.., au sio…’akasema Dalali akiniangalia mimi, na mimi sikumjibu kitu

Mpelelezi akaangalia saa yake, halafu akasema;

‘Lakini kabla sijawaachia uwanja wenu, nataka kuliweka hili jambo sawa…, haya mazingira ya humu ndani hayajanifurahishi, huyo mama hapo alipolala, sio sehemu salama,…je anawezwa kuhamishwa, akalala labda chumbani kwake, kama yupo salama, kama ulivyodai,…’kabla hajamaliza Dalali kadakia

‘Hapana, hapana…. afande, huyo hapo alipolala ndio hivyo hivyo, hapo dawa inafanya kazi, ukimuondoa hapo, dawa haiwezi kufanya kazi tena…na utaharibu kila kitu, muacheni hapo hapo alipo, haitapita muda ataamuka mwenyewe…’akasema

‘Oh…una uhakika na hayo mambo yako..mimi sitaki kuwaingilia mambo yenu ya kifamilia,..lakini sitaki pia kuharibu kazi yangu, nakuuliza tena, una uhakika na haya mambo yako…?’ akaulizwa Dalali , hapo Dalali, akabakia kimia kidogo.

‘Unasikia Dalali....mimi huwa napenda mtu mkweli, na ukiwa mkweli kwangu, siwezi kukusumbua, na kama kuna mambo ya kusaidiana, nitakuwa tayari kuweka nguvu zangu kukusaidia…, ila sitaki mtu mnafiki….’hiyo ‘mnafiki’ akaisema kwa nguvu, huku ananigeukia mimi, utafikiri alikuwa akiniambia mimi.

Na akawa ananiangalia, kwa sekunde kadhaa, halafu akasema;

‘Unaongea na mimi, au Dalali…’ nikamuuliza Mpelelezi, na yeye hakunijibu akatikisa kchwa tu, baadaye akamgeukia Dalali na kusema;

‘Dalali,…nitakuita hivyo kwa kazi yako,… narudia tena kukuuliza hili swali, una uhakika na hayo uliyoyasema, kuwa huyo mama yupo salama..na hali aliyokuwa nayo hapo, haina shida kiafya, na je hayo mambo yako ya mizimu sijui, sio mambo ya ubabaishaji tu…?’ akauliza

‘Afande hayo ni mambo ya kimila..’akasema Dalali.

‘Mimi nataka kuupata huo uhakika kutoka kwako, maana nikija kugundua kuna mambo ya ubabaishaji…sheria itafanya kazi yake,…unajua nitakacho kufanya, pili, nitasimama mahakani kutoa ushahidi mimi mwenyewe, kuhakikisha, unafungwa miaka mingi…, unanifahamu, sitaki wakina mama na watoto wasumbuliwe, hilo nitalisimamia mimi mwenyewe kuanzia sasa…’akasema mpelelezi.

‘Afande hakuna shida, familia hii ipo salama sema ni haya mambo ambayo, yalishamalizwa, sasa sijui yanarudije, na kurudi kwake, ndio huku, kuleta usumbufu, hilo nitalalamika tu, ila ukweli mnaoutaka nyie, ambao mimi naufahamu nitawapatia, sijui zaidi ya hapo…’akasema

‘Ukweli…sawa sawa, ukifanya hivyo, hutapata shida…’akasema mpelelezi

‘Sawa afande nimekuelewa, tutaongea….’akasema Dalali.

‘Sawa sasa..na endelea na mtu wako…’akasema afande sasa akichukua kidafutari chake na peni, halafu akageuka kuniangalia…

‘Mnaweza kuendelea, ila nikigundua kuwa ni njama zako za kujitafutia ujiko kwenye mitandao, nitakufunga kwa kuleta vurugu, na kupandikiza fitina kwenye familia za watu, kumbuka bado kuna gharama na usumbufu, uliousababisha wewe, hayo ni makosa yako…’akasema mpelelezi

 Mimi pale nilikuwa nasubiria taarifa ya mtu wangu, maana yeye ndiye nilimtuma kufuatilia hicho kibali, cha kufuatilia haya mambo, nilijua kabisa ,nikifanya haya mambo bila kibali, huyu jamaa atanifuatilia na hata kunifunga…nikajipa moyo, nikijua nipo upande wa ukweli na haki…

‘Unasubiria nini, muda…mimi nataka kusikia kila kitu, na hii itakuwa ndio nafasi nzuri ya kuupata ukweli wote,…mkimalizana hapo, nitakuulizia maswali kidogo kuhus kifo cha kaka yako, kuna utata fulani, nataka kuumaliza….na nawaahidi, nitafuatilia kila kitu kuhakikisha hii kesi imekwisha, ili nifunge ‘file’ la marehemu kaka yako….’akasema mpelelezi

‘Dalali….wewe…ulisema, haya mambo yanatokea hapa ni ya kimila?

‘Ndio….’akasema Dalali.

‘Na ukasema, mizimu ya marehemu kaka yako ndio imekuja kudai kuwa hilo deni, kweli ni la kaka yako…’

‘Ndio….’akasema.

‘Na hiyo mizimu inatokea wakati gani…?’ nikamuuliza.

‘Kama hivyo…mtu akija kuzuia hilo deni lisilipwe, au kutaka kuufahamu ukweli,…kuuliza uliza kaam ulivyofanya wewe,  basi hali kama hiyo hutokea. Marehemu kaka anajitokeza kwa ….mtoto wake, …’akasema.

‘Je mtu kama mimi ambaye sikujua hilo, nikaja kuuliza, hiyo mizimu hutokea..?’ nikauliza

‘Ndio…hutokea, kwa nia njema ili kukufahamisha tu..’akasema

‘Kwahiyo hiki kilichotokea hadi mtoto kupoteza fahamu, kilitokea ili mimi niupate huo ujumbe,…nia ni  kunifahamisha mimi au sio…?’ nikauliza

‘Ndio…’akasema.

‘Kwa kumtesa mtoto..!...na kama ni hivyo, ni kwanini sasa unasema mimi nimeleta  usumbufu kwenye hii familia, wakati mimi nilitaka kuufahamu ukweli,..kama ilitokea kwangu ili niufahamu huo unaouita ni ukweli, je mimi nimesumba nini hapo…?’ nikauliza.

Mpelelezi, akacheka, na kutikisa kichwa…

‘Afande hayo ni kweli, naona wewe huamini, lakini sisi imetusaidia sana la sivyo tungeliendelea kuamini hivyo, kuwa deni hilo huenda sio halali kwa marehemu kaka…’akasema Dalali.

‘Je nyie mlijuaje hilo, kuwa hayo yanayotokea kwa mtoto,au kwa mama, ni mizimu ya marehemu kaka yako…?’ nikamuuliza

NB: Kazi imeanza…

WAZO LA LEO: Tusiogope kutafuta haki zetu, japokuwa wakati mwingine tunajikuta kwenye mitihani, mitihani hiyo tuichukulie kama ngazi za kuifikia hiyo haki. Tukumbuke kuwa haki wakati wote ipo juu ya dhuluma.
Ni mimi: emu-three

No comments :