Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, June 27, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-15


Jamaa alipoona shemeji yake hazindukana akaenda , akaanza kufanya mambo yake, na wakati anayafanya hayo, mara mlango ukagongwa…mimi nikajikuta nikisema;

‘Polisi hao…’

Kauli hiyo, ilimfanya jamaa akae chini, ile ya kudondoka, Pwaah,…ilikuwa ni dalili ya kushtuka, na kweli usoni kulitanda kwingu cha uwoga, akawana kageuka kuangalia mlangoni…

Tuendee na kisa chetu…

**************

Na mara mlangoni ukagongwa tena…hakuna aliyesema karibu, jamaa akawa ananiangalia mimi kwa mashaka, …

‘Polisi kweli…?’jamaa akaniuliza akiniangalia, halafu akaangalia tena mlangoni

 ‘Ulifikiri mimi ninatania, eeh,…’ nikasema;

Cha ajabu sasa, jamaa badala ya kuendelea na ile shughuli yake, akasimama, na kwa haraka akauendea mkoba wake, na kuuweka kwapani, huyo anataka kuondoka; Lakini aliposikia huyo mgongaji anaendelea kugonga, akasita

‘Ni nani huyo…?’ akauliza na mimi sikumjibu swali lake nikauliza swali;

‘Wewe sasa unataka kwenda wapi, unaacha kumuhudumia shemeji, unataka kukimbia, huo ni ushahid tosha kwa polisi….’nikasema

‘Nilishakuambia,..mimi nilipitia hapa mara moja tu, kusalimia, sasa naondoka, mengine utamalizana wewe na askari wako, mimi naondoka zangu…sheemji hajambo, atainuka muda si mrefu, anahitajia kutuliza kichwa kwanza.’akasema

Na kabla hajamaliza kuongea mlango ukafunguliwa,…jamaa alishtuka utafikiri kagongwa na shiti ya umeme….

‘Hivi ni kweli, kwanini umafanya hivyo…?’ akaniuliza, na mimi sikumjibu, nikageuka kumuangalia huyo mtu aliyeingia.


                                  ***********

Huyu aliyeingia sio yule mtu niliyemtegemea, ila alikuwa na zilezile dalili za uaskari kanzu, nilishangaa ni kwanini yule niliyempigia simu awali sio yeye aliyefika…alipoingia akatusalimia..halafu kwa haraka akamgeukia Dalali.

Kwa muda ule,..Dalali alikuwa bado kashikwa na butwaa, akishindwa kuamua kukaa au kuondoka, Yule mpelelezi akajitambulisha na kutoa kitambulisho chake, akamuonyeshea  jamaa…Jamaa kwanza akawa sasa anazidisha kule kushangaa kwake,…na wasiwasi juu.

Kwa haraka jamaa  akagenigeukia, na kusema;

‘Haya yote  , yana maana gani..?’ akaniuliza akimwangalia kwanza huyo mpelelezi  na halafu akageuka kuniangalia mimi, akawa anaashiria kwa mikono kumuonyesha huyo mpelelezi.

‘Mimi sijui…muulize yeye mwenyewe, …’nikasema

‘Mimi nimefika hapa kukufuata wewe, nilifika nyumbani kwako nikaambiwa haupo, nikaelekezwa kuwa huenda upo hapa….’akasema huyo mpelelezi akimwangalia huyo jamaa

‘Kuna nini kwani, nimefanya nini, …na ni nani  huyo kakuambia nipo hapa?’ akauliza maswali mengi kwa mfululuzo, kuonyesha jinsi gani hakulitazamia hilo.

‘Ni maswala machache  ya kipolisi, sisi tunataka kujirizisha…, na hata hivyo, mimi nimepata maagizo kutoka ofisini kuwa kuna jambo la dharura kwenye hii nyumba, ndio maana tumekuja na gari la wagonjwa na huduma za kibinadamu,…’akasema

‘Ni nani kakupigia simu,…ni wewe, kumbe …?’ akauliza sasa akiniangalia mimi usoni, alikunja uso aliponiangalia mimi, na alipogeuka kwa huyo askari mpelelezi, akaukunjua, na kutabasamu ile ya kinafiki,,..baadae akasema;

‘Yaliyotokea hapa ni kutokuelewana tu, haya mambo ni ya kifamilia zaidi, hakuna tatizo kabisa..’akasema

Yule mpelelezi akagauka na kuangalia pale sakafuni, halafu akasema;

‘Unasema hakuna tatizo, sasa huyo mama hapo sakafuni, kalala,… ana tatizo gani..?’ akauliza mpelelezi

Dalali kwanza akanitupia jicho mimi la haraka, baadae akasema;

‘Huyo mama, huwa ana tatizo la kupoteza fahamu, hasa akipatwa na mshtuko…’jamaa akasema

‘Kwahiyo alipatwa na mshtuko..?’ akauliza mpelelezi.

‘Ndi—ndio…lakini ni kwavile mtoto wake ..alizidiwa kuumwa, na unajua tena akina mama..’akasema

‘Mtoto anaumwa nini…?..na  ndio..yule aliyelala pale, sasa kwanini hamjampeleka hospitalini, ..?’ akaulizwa

‘Sio tatizo la hospitalini…’akasema Dalali.

‘Una maana gani kusema hivyo..?’ akaulizwa huyo mpelelezi akiendelea kumchunguza yule mtoto kwa macho.

‘Kuna matatizo mengine ni ya kienyeji tu..sasa hivi  huyo mtoto hajambo, ungelikuwepo awali ndio ungelifahamu nina maana gani,..ila kifupi tu, hilo tatizo lake ni…eeh, maswala ya kimzimu, ..najua huwezi kuelewa hayo,..na…na… kuna dawa zake ukimpatia anapona, hakuna shida kabisa,…’akasema.

‘Mizimu!!!...ok, ok…haya na huyo mama naye ana tatizo gani..?’ akauliza

‘Naye ni mambo hay ohayo….kama nilivyosema awali, yeye, akipatwa na mshtuko, huwa inatokea hivyo, na hiyo hali ilianza kipindi mume wake alipofariki....’akasema.

‘Kwahiyo, ikitokea hivyo, mnafanya nini, maana kama ni mshtuko, bado ni swala la kwenda hospitalini, au sio…?’ akauliza.

‘Hapana kuna huduma zake,…kuna dawa zake,..ila kama hazitafanya kazi, basi itabidi tumpeleke huko hospitalini, maana hata awali, ..alipelekwa huko, ila kwa mujibu wa mtaalamu…haikutakiwa kufanya hivyo, ndio maana ilichukua muda sana kupona kwake…’akasema

‘Wewe ni docta..?’ mpelelezi akauliza.

‘Ha-hapana, mimi nafuta masharti na maelekezo ya mta-alaa-mu..’akasema

‘Mtaalamu ndio nani..?’ mpelelezi akauliza bila kuonyesha hisia zozote usoni.

‘Ni watu wa tiba mbadala…’akasema hakafu akanigeukia mimi akibenua mdomo vile, sikumuelewa kufanya vile mdomo ana maana gani

‘Ok,…. sasa mbona wakati naingia wewe ulikuwa kama unataka kuondoka, na wakati huo huo, huyo mama bado yupo kwenye hiyo hali…ulikuwa unataka kukimbia nini..?’ akaulizwa.

‘Kukimbia,…ha-hapana, kwanini nikimbie, mimi ni mlezi wa hii familia, labda, ni kwa vile sijakutambulisha kuwa mimi ni nani kwenye hii nyumba..unasikia,…na huyo mama anahitajia, kupumzika tu, atazindukana,…kuna mambo nilihitajika kuyafuatilia kwa haraka…’akasema

‘Dawa au..?’ akaulizwa

‘Kitu kama hicho, maana hata dawa zinahitajia pesa, au sio..’akasema

‘Mimi sijui….ila sasa tusipoteze muda, mimi nilikuwa nakutafuta sana wewe…kuna maswala nilitaka kuongea na wewe binafsi, ni muhimu sana, ..’akasema mpelelezi

‘Maswala gani..?’ jamaa akauliza kwa mashaka

‘Nilikuwa  nataka kuulizia maswala yanayohusiana na kifo cha kaka yako…’jamaa kusikia hivyo, akashtuka kidogo…na akanigeukia kuniangalia mimi, na halafu akasema;

‘Kuhusiana na kifo cha kaka yangu..leo hii…., mbona umeshapita muda mrefu tu…, kuna nini tena zaidi!?’ Akauliza kwa mshangao

‘Ndio….muda mrefu umeshapita, lakini hilo sio tatizo, kesi kama hizo, zinaweza kusimama kwa muda,..kwenu nyie mnaweza kuona hivyo,…kuwa kesi imesimama… lakini sisi kiofisi tunaendelea kulifanya kazi hilo jambo…’akasema mpelelezi

‘Sielewi afande  ….kwani kuna nini kimetokea mpaka muanze kufuatilia tena hili jambo…, au mumegundua nini, nauliza tu, afande…?’ akauliza jamaa na sauti yake ilikuwa kama inatetemeka.

‘Usiogope,  ni maswali ya kawaida tu, ya kujirizisha kabla hatujafunga jalada lake…, hata kama mtu kafariki  zamani, inawezekana kukatokea kitu cha kutufanya tuchunguze zaidi, hata hivyo, jalada la kaka yako lilikuwa halijafungwa, kesi yake bado ilikuwa inafanyiwa kazi, unasikia ….’akasema mpelelezi

‘Ndio nauliza kuna nini cha zaidi mumekiona eeh… maana mnataka kutukumbusha ya zamani, na haya tafadhali, mkija kuongea na mjane, mtazidi kumtonesha…na kwa hali yake ilivyokuwa,… naomba chonde, tusiyaongelee hapa, kama kuna jambo mumegundua, basi mimi nitakuja huko huko ofisini kwenu….’jamaa akasema

‘Hapana…ni mambo ya kawaida tu,,…ni kweli kuwa kaka yako alifariki kwenye ajali ya gari, kwa taarifa tulizo nazo ndio hivyo…’akasema mpelelezi

‘Ndio, na ndivyo ilivyokuwa..’akasema Dalali.

‘Hilo halina shaka,..lakini kuna mambo bado tunahitajia kuyaweka sawa ili kumbukumbu zetu ziweze kuwa kamilifu, kuna utata hapa na pale..na hayo, mimi sizani kama hata shemeji  yako, atayasikia,…sizani kama yatamuathiri kitu…yanaweza kumsaidia kutuliza moyo wake pia, maana kuna maelezo kuwa yeye hakukubaliana na baadhi ya hizo taarifa,..….kwahiyo usijali kwa hilo…’akasema huyo mpelelezi.

‘Ni nani alisema kuwa shemeji hakukubaliana na hilo..huo sasa ni uvumi tu, …sio kweli…’akasema

‘Taarifa za kipolis, zinasema hivyo…hilo halina ubishi, na sisi tuliendelea kuzifanyia kazi, na mimi hapa naendelea kuzifanyia kazi,…’akasema mpelelezi.

‘Sawa afande….sasa  ulitaka kujua nini kutoka kwangu….?’ Jamaa akauliza

‘Usijali, kwanza..nataka kuhakikisha humu ndani kuna usalama,…nataka uhakika wa huyo mama, nataka uhakika wa watoto wapo namna gani, ..ili tukiendelea na haya mambo kuwe na amani..’mpelelezi akasema

‘Hilo usiwe na shaka nalo…’akasema Dalali.
‘Na…huyu…mna ni nini na yeye…?’ akauliza huyo mpelelezi akiniangalia sasa, nilishamfahamu huyu mpelelezi, mara nyingi nikikuana naye kwenye tukio, huwa hatuivani, lakini sikulijali hilo,…nikabakia kimia, na aliyeongea na Dalali.

‘Huyu …?...eeh, na yeye alikuja na maswali yake hata simuelewi, nashindwa hata….sasa sijui nianze na nani, maana nyie watu, hamchoki kutusumbua, kwanini hamuangalia na maisha ya watu, tunaishije, maana hali zetu zina shida kweli, leo nimepoteza muda, na muda kwangu ni mali,…sijui kwanini hamlioni hilo..haya wewe mwambie mwenzako, wewe si ndio ulimuita….?’ Akaniuliza na mimi nikabakia kimia tu

‘Unasema sasa uanze na nani kwa vipi…kwani huyo ana kuuliza nini, na ni nani….?’ akauliza huyo mpelelezi akiniangalia kama vile hanifahamu, ..ndivyo alivyo,..namfahamu sana.

‘Huyu si mwenzenu, kwani nyie hamfahamiani…., au…?’ akawa kama anauliza na kuniangalia mimi kwa dharau fulani, na mimi nikawa kimia tu, sikusema kitu…

‘Ok, sawa…sio lazima tujuane, huenda anatokea kitengo kingine…ila mimi sizani kama nafahamiana naye, sura yake ni kama naifahamu,…lakini haina haja kwa sasa, muhimu nimekuja kwako, Dalali,…’akasema huyo mpelelezi

‘Mhhh….naona sasa, kumbee, nilijua tu.…hahaha, watu mnaumbuka sasa….’akasema jamaa

‘Kwanini unasema hivyo..?’ akauliza mpelelezi, akimuangalia Dalali, halafu akaniangalia mimi, hawa watu hapo nilijiona nipo kwenye mtego,…maana huyu mpelelezi, amekuwa akinitafutia makosa ili nionekane sifai, lakini hajanipata.

‘Muulize yeye mwenyewe, sitaki kuingilia haya mambo yenu…, maana hapa nina mengi ya kuniumiza kichwa….kwanza siku imepita bila bila…nitaishije na mimi nina familia …nina tegemezi…hamjui tu….’Dalali akasema

‘Nakuuliza wewe, maana  mimi sasa nipo kazini, kwani huyu mtu,  kakuuliza nini cha kukufanya  wewe uwe na mashaka naye..?’ akauliza, akimuangalia Dalali, hakuniangalia mimi, hata aliposema,…’huyu mtu…’

‘Unajua yeye nimemkuta hapa akiwa na shemeji yangu, na katika kuongea naye, akaanza kuniuliza maswali ya kipolisi polisi… mimi nikajua ni watu wenu, hata hivyo nafasi yangu haikunipa ahueni,…kiukweli nilishaanza kumtilia mashaka,…simuamini,..’akasema na huyo mpelelezi akaniangalia  tena kama anataka kusema neno, lakini akaghairi, na mimi kwa muda huo nipo kimia tu!

‘Maswali ya namna gani, alikuuliza, ya kukufanya usimuamini ….?’ Akamuuliza  huyo jamaa,

‘Aaah… muulize yeye mwenyewe,…’akasema

‘Nimekuuliza wewe..nijibu…’akasema mpelelezi.

‘Mhh…  eti haamini kuwa kaka anadaiwa benki , eti anahisi deni hilo ni la uwongo, sasa mimi sijui kwa vipi, na kwanini anaingilia maswala ya kifamilia, na wakati mahakama ilishapitisha hilo, ndio maana mimi nikamtilia mashaka….. ‘akasema.

‘Ila wewe unaamini kuwa hilo deni,..si hilo la marehemu kaka yako au sio…ambalo wewe…, unadai hata mahakama wamelipitisha, je nikuulize tu, wewe kama wewe, kweli , kutoka nfasi mwako unaamini ni deni la kaka yako…?’ akaulizwa swali ambali nilimuuliza Dalali awali, nikasubiria  kusikia jibu lake la sasa.

‘Baada ya kujirizisha, ndio..na ni baada ya  kufuatilia sana,..hadi mahakamani, kwa vile nilimfahamu sana kaka yangu…baada ya jitihada zote hizo,..ndio…eeh,  nikaja kuona vielelezo, ambavyo hata mahakama walikubaliana navyo,…sasa kitu ambacho hata mahakama wamekikubali, mimi nitasema nini tena hapo…eeh, ilibidi niamini tu, ….’akasema.

‘Lakini moyoni hujarizika au sio….?’ Akaulizwa

‘Jibu lipo wazi,…na zaidi, ni baada ya kupata ishara, ….hapo sasa hakuna ubishi tena…’akasema

‘Ishara gani….?’ Akaulizwa

‘Mizimu…ndio hiyo inayowatesa hii familia,..na nina imani tukimalizana na hilo deni, haya matatizo yote yatakwisha, na shemeji, na watoto wataishi kwa raha, mustarehe, itabakia kukumbuka tu, maana kiukweli kaka yetu alikuwa kipenzi cha kila mtu..’akasema

*************
‘Kwahiyo mtu amekuwa akikuulizia kuhusu hilo deni,..na alipokuulizia wewe ukaanza kuwa na mashaka naye…ndio hivyo..?’ akaulizwa.

‘Mhh…hebu fikiria hata wewe kitu kimeshapitishwa mahakamani, kwanini mtu aje baadae kudai,..na kwanini asiende huko..eeh, benki, maana wao ndio wanaodai, kwanini ananiuliza mimi, …huoni hapo kuna maswali ya kujiuliza…simuelewi….’akasema.

‘Ok, ok, mimi sioni kwanini uwe na mashaka na yeye , wakati anachokifanya ni kusaidia jamii,….mimi nimemuelewa lengo lake ni nini,..’Huyu mpepelezi akageuka kuniangalia mimi, halafu akageuka kumuangalia  Dalali

‘Kama nilivyokuambia, yeye huenda yupo kitengo kingine,..ila kwa vile umelitilia shaka hilo…la kutokumuamini,..basi..niachie mimi, hilo tutalifanyia kazi…, kuhakiki uhalali wake…ila kwa hali kama hiyo hata mimi umenitia kwenye mashaka,..ni kwanini unaogopa kumuambia ukweli mtu kama huyo, unawafahamu hawa watu kazi zao, n kuwatega watu, waseme uwongo, halafu wawapeleke magazetini, lakini tutapambana nao, usiwe na shaka na hilo…’akasema mpelelezi.

‘Mimi simuogopi kabisa, nimempa nafasi ya kuuliza maswali yake yote, na ….keshagonga ukuta, mimi najiamini na ninajua ninachokifanya…’Dalali akasema, hakuelewa mwenzake anamtega tu.

‘Sasa… wewe ukweli si unaujua, kwanini unaogopa kuusema, huo ukweli unaoufahamu wewe ili mumalizane naye, au kuna tatizo gani zaidi…..?’ akaulizwa

‘Hapana sijaogopa kusema ukweli wowote..…lakini ngoja kwanza, kuhusu wewe, eeh,..maana ninaona tutapoteza muda hapa, na mimi natakiwa kuwajibika…’akasema na kuangalia saa yake.

‘Hili swala tulishaliongelea na wenzenu, kipindi cha mwanzo, …..’akasema

‘Swala gani…?’ akaulizwa

‘La..la hilo unalosema umekuja kuniuliza….na wenzako, tuliongea nao, baadaye wakatuelewa, baada ya kuona ushahidi wote kutoka benki, sasa huyu anakuja na jambo lile lile,…ndio maana simuelewi, hata huyu…na ndio maana nikawa namtilia mashaka, kifupu sijamueelwa,….’akasema

‘Unajua hayo maswala ya benki yana watu wake…mimi sihusiki huko, kwahiyo siwezi kuliingilia hilo, mimi nimekuja na mambo yangu,…KUHUSU SWALA LA KIFO CHA KAKA YAKO, ambacho kimetokea kwasababu ya ajali, kama taarifa zilivyosema,.. sasa nilitaka kukuuliza baadhi ya maswali, ambayo yaliachwa bila kupatiwa majawabu yake…’akasema

‘Maswali gani hayo,ambayo mimi nayafahamu na kwenye taarifa hayapo, maana hiyo ni kazi ya watu wenu wa usalama barabarani, au sio..na kiukweli sikulipendelea hilo jambo lianze tena maana yule ni kaka yangu na mimi…nawakilisha familia, sisi, tuna uchungu zaidi yenu nyie…sisi kama wanafamilia, tulishakubaliana na mipango ya mungu,….tulishaanza kusahau machungu…’akasema kwa sauti ya huzuni.

‘Ni maswala ya kawaida tu ndugu yangu, haki lazima itendeke hata kama itachukua miaka dehari..…kwa jinsi ajali ilivyotokea na eneo lenyewe na  gari kuna utata fulani kati yake..’akasema na Dalali akawa katoa macho kumsikiliza mpelelezi, niliona kama ana hamasa na maelezo hayo.

‘Yote hayo yapo kwenye taarifa ya watu wa usalama au sio..kuna muda niligombana nao sana, hata shemeji,…kipindi kile tulikuwa na hasira ya kifo cha ndugu yetu mtusamehe sana…’akasema

‘Ndio maana nataka kumaliza hilo, tulifunge hilo kabrasha,…’akasema mpelelezi, na Dalali alipotaka kuongea mpelelezi akamkatili na kusema;

‘Lakini kabla hatujaenda huko, je wewe na huyu mtu hapa mumemalizana naye…kama sikosei huyu ni  mtu wa jamii, watu kama hawa wanatusaidia kwa namna moja u nyingine au sio, na nyie kama familia mnataka haki itendeke, hawa ndio wapo karibu yenu kuliko sisi, nilitarajia ungelimuunga mkono, au sio…?’ akauliza mpelelezo.

‘Ana kibali gani kuhusu haya mambo, na kuingiliana ki kazi tu, …ndivyo nionavyo mimi, maana kwa mfano kaja hapa kwenye familia, na kusababisha, watu waliopona, eeeh, waanze kuumwa tena, je huko ndio kuisaidia jamii, hebu niambie hata wewe.…?’ Dalali akasema.

‘Nikuulize wewe mtu wewe ulishamaliza naye, naye…maana nataka mimi na wewe tukitoka hapa twende kituoni,..unanielewa lakini, uniambie kibali cha kuyafanya haya umepatia wapi..?’ mpelelezi akaniambia, na mimi nikabakia kimia

‘Mjibu afande…kibalio umekipatia wapi, kumbe ndio nyie ..nilijua tu, yess…sasa moyo umeridhika, afande, nakuunga mkono, …atuonyeshe kibali chake….’jamaa akasema akiniangalia, na mimi nikatikisa kichwa kukubali.

‘Hilo la yeye kunijibu, lisikusumbue kichwa, nitakabiliana naye muda ukifika, ila kwanza nataka kufahamu je mlishamaliza naye..?’ akaulizwa

‘Kumalizana naye kuhusu nini tena, kama mtu hana hata kibali, niongee naye nini zaidi..eeh, afande, huyu sihitajiki kuongea naye tena…mchukue mkamalizane naye huko kituoni…’akasema Dalali.

‘Hapana…kama nilivyokuambia, huyu ni mtu wa jamiii…hatuna ubaya naye, ila ni muhimu afuate utaratibu,…sasa nakuulize wewe, je mlishamaliza naye ..?’ akauliza afande.

‘Kwahiyo wewe unakubaliana naye kuwa aniuliza maswali, wakati hana hata kibali, huo sio utaratibu, huoni kuwa atakuwa kavunja sheria…’akasema Dalali.

‘Hapo sasa wewe unanifundisha kazi..’akasema mpelelezi.

‘Hapana afande…ila kama wewe unamuhusu, sawa, mimi nipo tayari, siogopi kitu, aulize maswali yak yote, hata hivyo, nilishamuelezea kila kitu, sasa ..sijui anataka nini zaidi…’akasema Dalali

‘Mimi sitaki kumuingilia kazi yake , nikifanya hivyo, nitaulizwa sana, ..hawa watu wanawategemea sana watu wa siasa,…sasa, ..kama bado muendelee naye,…sina haraka kwa maswali yangu…’akasema mpelelezi, akikunja nne kwenye sofa, huku akimuangalia mama mjanepale alipolala..nahisi alihisi kitu.

‘Kama wewe umesema hakuna shida, sawa,,  …ila afande,..mimi nilitaka kuelewa kabla hatujafika huko, huyu mtu kwanini asiende kuwauliza watu wa benki, kama ni mtu wenu lakini… , na kama sio mtu wenu, huoni kuwa anaweza kuwa ni tapeli…kibali chake kipo wapi, eeeh,….sio kwamba nakuingilia kazi yako, lakini mimi kama raia mwema nina haki ya kuulizia hilo, au nimekosea…’akasita alipoona namwangalia, halafu akasema

‘Natumia neno hilo…tapeli, kwa maana yake sio kama namkashifu, unielewe hapo samahani sana..’akatulia halafu akaendelea kuongea…;

‘Maana…mimi nimeingia humu ndani, namkuta kamkabili shemeji kwa maswali, akadai, yeye ni kaka wa shemeji..uone alivyo muongo..eti yeye ni kaka wa shemeji, hapo hapo nikaanza kumshuku …’hapo akasita

‘Kwanini unasema ni muongo..?’ mpelelezi akauliza

‘Ndugu zake shemeji nawafahamu karibu wote..huyu katokea wapi, nisimfahamu…’akasema

Mpelelezi akanitupia jicho, halafu akamgeukia jamaa;

‘Usiongee mambo ambayo huna uhakika nayo…mimi nimekupa nafasi ya kujibu maswali yake, na baada ya hapo niachie hiyo kazi, nitadili naye, usiwe na wasiwasi..watu kama hawa nawatafuta sana, ili tuwafundishe maadili ya kazi zao…’akasema mpelelezi.

‘Uhakika kwa vipi afande..au mnajuana, usitake kunichezea shere…huyo mtu, amekuja hapa kutaka kumghilibu shemeji yangu… na sasa amesababisha hata mtoto kupatwa na matatizo na kwa kifupi sijamuelewa…’akasema.


Mpelelezi akaniangalia akitaka kama anataka kuniuliza kitu  lakini nikaona anasita akamgeukia jamaa na kumwambia.

‘Unasema kasababisha hata mtoto kupatwa na matatizo, una maana gani hapo..?’ akaulizwa

‘Hayo sasa ni maswala ya kifamilia..nikianza kukuelezea hapa tutakesha na huenda hata usinielewe…, na nyie ni watu wa serikali,  unasikia, serikali haiamini mambo hayo, ila sisi raia tunayaamini, ni maswala ya kienyeji, kimzimu, na vitu kama hivyo..’akasema

‘Sasa huyu …kasababishaje hayo, hadi mtoto apatwe na matatizo, na ni matatizo gani…maana alivyolala pale anaonekana hayupo vyema, au…na..huyo mama, hapo chini bado mimi sijakuwa na imani naye…nimuite docta afanye kazi yake…?’ akauliza huku akimkagua yule mama sakafuni kwa macho.

‘Hapana..afande utaharibu kabisa..hatuhitaji docta hapa….’akasema Dalali

‘Na je, huyo mama ataamuka saa ngapi, huo ulalaji sio wa kawaida kiafya....’akasema mpelelezi

‘Ataamuka tu…hapo alipo dawa zinafanya kazi, ni  maswala ya kimila….hutaweza kuelewa zaidi ya sisi wanafamilia wenyewe…’jamaa akasema akimsogelea huyo mama, akapeleka mkono shingoni, halafu akasema;

‘Yupo sawa…ataamuka tu…’akasema

‘Una uhakika…tusije kupoteza muda hapa, wakati kuna mgonjwa, na mgonjwa mahali pake ni hospitalini…, na je hawa watu wamekula, maana taarifa ya wakubwa zangu, hawa watu kwenye nyumba hii wanahitajia huduma  hizo,..?’ akauliza na hapo jamaa akageuka kuniangalia mimi

‘Sijajua..labda …mwenzangu kwa vile yeye alikuwepo mapema…’akasema
‘Mwenzako…si ulisema, ni tapeli au..kwahiyo ni tapeli mwenzako…’akasema mpelelezi

‘Aaah, afande hayo yalinitoka tu, ila..kiukweli hali ya hapa sio nzuri… kama chakula kipo bora kiletwe ile kuje kufanyiwa maandalizi, akiamuka huyu mama atapika tu,…’akasema

‘Kama huna uhakika na hali zao, basi hawa wagonjwa wapelekwe hospitalini,…usafiri upo nje…’akasema Mpelelezi.

‘Hayo sio maswala ya hospitalini,  afande, niamini mimi… ikimrejesha hospitalini tena, mtaharabu kila kitu….’akasema

Mpelelezi, akasimama na kumuendea yule mama, akachuchumaa, akawa anamchunguza mama mjane, akaweka mkono wake shingoni kwa mama mjane,…halafu akasimama,…akanigeukia mimi, akasema

‘Sitaki kuanza na wewe kwanza, nakuelewa, na leo nitakupata tu..ila kwa sasa…nimekuja hapa kwa ajili ya huyo mtu…’ hapa aliongea kwa sauti ndogo, ili Dalali asisikie, ila kwa ile sauti Dalali atakuwa kasikia, japokuwa kwa shida.

Aliposema hivyo, akageuka kumuangalia Dalali akasema;

‘Mimi huko ofisini,…nimepata maagizo kwa wakubwa wangu, kuwa hapa kuna tatizo kubwa limetokea, haya niambieni…hapa kuna tatizo gani…?’  huyo afande akanigekia mimi huku kakunja kumi na moja usoni

NB: Tuendelee….


WAZO LA LEO: Inapofikia kwenye kutatua matatizo ya jamii, hata kama mna upinzani fulani, uwe wa kisiasa au kiimani, tofauti hizo ziwekeni pembeni kwanza, muangalie jukumu lililopo mbele yenu kwa manufaa ya jamii,..(kama hilo tatizo halikinzani na imani zenu.) . Mara nyingi, makundi yanayojiunda kwenye jamii,…kwa nembo fulani… ambayo hayaangalii uhalisia, san asana, ni upinzani wa kishabiki tu yanakuja kuwa ni kikwazo cha mahusiano mema kwenye jamii…watu wanaumia,..kwanini tufanye hivyo,..umakundi usio na tija haufai., muhimu tuangalia kila jambo kwa umuhimu wake kwenye familia, sio ubinafsi mbele.
Ni mimi: emu-three

No comments :