‘Huna
haja ya kurudia swali lako, ….ila nikueleze jambo moja unielewe, sisi sote
hakuna mtu aliyejua kuwa hilo deni lipo…tumekuja kulifahamu hilo deni, eeh…
baada ya kupata barua kutoka benki, ya kutuarifu kuwa kuna deni kama hilo,…unasikia
sana…’akatulia na mimi nikawa kimia tu kumsikiliza.
‘Ilikuwa
ni mshtuko kwetu, kwa jinsi tunavyomfahamu marehemu…’akageuka kumuangalia shemeji
yake.
‘Basi…
kwa haraka mimi nilikwenda huko huko benki, kuwauliza, kwasababu muda huo
shemeji alikuwa hajitambui, ilibidi mimi niwajibike kwanza,..na nilijiuliza ni kwanini
taarifa hiyo haikuja mapema, wakati mimi niliwahi kupeleka barua ya mirathi,
kuwa mimi ndiye ninayestahiki kusimamia mambo ya benki,…hawakuniambia kuhusu
hilo deni,…wao wanakuja kusema kipindi ambacho tunajua hakuna deni...ilitakiwa
katika madeni ya marehemu hilo liwepo, hii ni kuonyesha , au huo ni ushahidi
wetu kuwa hakuna aliyekuwa akilitambua hilo deni..hata mahakama wanalitambua
hilo,…’akatulia.
‘Wao wakalisemaje..ulipokwenda
kuwatembelea…?’ nikauliza
‘Kuwatembelea…!!
Hiyo sio lugha sahihi…anyway…wao walisema,… wao eeh, walikuwa katika utaratibu
wao wa kuhakiki madeni,..madeni yapo mengi, na kipindi hicho walikuwa na
matatizo ya kiofiosi,..wanajua wenyewe ni matatizo gani, hawakutaka kuniambia,
..na wanasema walipofikia kwenye deni hilo,..ndio wakaligundua,
na..ilishawangaza ni kwanini deni kubwa hivyo bado liliendelea kuwepo, unasikia
..’akatulia
‘Hata
hivyo, wao walikuwa hawana wasiwasi na hilo deni, kwa vile lina dhamana yenye
mshiko…unaona, ni kama walitutega..ili tushindwe wafanye hicho wanachotaka
kukifanya..hizo sasa ni hisia zangu..,nikahangaika nao, nilionyeshwa kila
kitu…mimi ni mbishi hasa kwenye deni, na liwe la mashaka mashaka, lakini kwao
nilisalimu amri,…na nilichoka pale waliposema kuwa wao wan utaratibu wa kutuma
makumbusho(remeinder), kila mwezi…’akatulia
‘Uone,…ilivyo,
mimi sikukubali kirahisi kihivyo…wao walikuwa wakiandika barua kwa mdaiwa,
kumkumbushia, na bro…eeh I mean marehem…eeh, alikuwa akiandikiwa, sasa…kwanini
akawa msiri kiasi hicho, sielewi kabisa, mungu amsamehe tu kaka yangu, hakuwa
hivyo…siwezi kuamini, …’akasema
‘Hizo
barua zilikuwa zinapitia wapi..?’ nikauliza
‘Posta,…zilikuwa
zinapitia posta ,tatizo bro,… alishaachana na …kutumia hilo boksi…siku nyingi
tu, kumbe kule kwenye mkopo aliweka hilo boksi la posta,..na wao wakawa
wanatuma hizo barua zao za kukumbushia huko… huko, hakuna aliyewahi kwenda
huko, ni la nini tena wakati tunafahamu kuwa limesha-fungwa..huwezi hata
kufungua tena…’akasema.
‘Kimahakama,
hawakuhitaji huo ushahidi…maana ni muhimu kulithibitisha hilo…?’ nikamuuliza
‘Mhh….baada
ya ushahid wa kumbukumbu za benk,…kuonyesha hizo nakala za barua,… maana wao
walikuwa na nakal zao, na tarehe…zipo walionyesha, haikuwa na haja ya
kufuatilia huko posta, maana boksi lenyewe tulishafungiwa, nani angelifungua,
ni kujishitaki tena, na huko nako kuna deni,..lakini sio kubwa,..akili zimemezwa
na hili..,…’akasema
‘Kwahiyo
yote hayo uliyafuatilia wewe mwenyewe kuhakiki,..kuwa ni kweli, kuwa kulitumwa hizo
barua, na…nilikuuliza awali, wewe kutoka moyoni, ulijirizisha kuwa kweli hilo
deni lilikuwa la kaka yako, maana ulifuatilia wewe mwenyewe awali, au sio,
lakini je nafsini mwako uliijirizisha, na ukaamini kuwa kweli hilo deni ni la kweli, na ni la kaka yako..?’
nikamuuliza
Kwanza
akaguna mgono wa kama kucheka, akatikisa kichwa, halafu akamgeukia shemeji
yake…
‘Hivi
shemeji, hujamuambia ukweli wote huyu mtu…pamoja na huu ninaomuambia wa
ushahidi, mimi hapo ningelifanya nini, eeh, maana haya maswali sasa yananikera…shemeji
hebu nisaidie.. hivi bado hata wewe hujaamini kuwa deni hilo ni la kaka…hivi,
si tulishaongea haya na kuyamaliza, kwanini tena….mimi nitasema nini hapo, kuwa
..sio kweli, eeh, kwa vipi jamani, mbona mnaniweka kwenye wakati mgumu, haya
..na haya ya mizimu …hamuamini, wamejuaje…eeeh,..?’ alipomgeukia shemeji yake mimi sikujali,
nikaendelea na maswali;
‘Kaka
yako alikuwa akikushirikisha kwenye mambo yake karibu yote au sio…ikiwemo
kwenda benki kumchukulia pesa,…siku nyingine, nyingine, au sio… au hata kutuma kuweka
pesa kwenye hiyo akaunti yake…, ni kweli si kweli…?’ nikamuliza,hapo kwanza
akasita baadae akasema.
‘Ndio,..kiukweli
kaka aliniamini sana, nilikuwa mtu wake wa karibu sana, lakini mimi nashangaa, ni kwanini kwa hilo,
hakuweza kuniamini, akanificha…’akasema.
‘Na
hujawahi kutumwa kuchukua statement ya kumbukumbu za account yake..?’ akaulizwa
‘Hapana,
hilo hakuwahi kuniagiza,……bro yeye ..eeh, alikuwa akinituma kuchukua au kuweka
tu….na kuchukua, anajaza mwenyewe kila kitu, ila kuweka,…wakati mwingine najaza
mimi mwenyewe…’akasema.
‘Kwenye
mali zake, akinuanua vitu kama mashamba, nk..wewe ulikuwa mtu wake wa karibu, na
kama sikosei, aliwaweka mbele nyie ndugu zake kwenye hivyo vitu vikubwa zaidi
ya mkewe, ni kweli si kweli…?’ nikamuuliza. Hapo akasita halafu akamgeukia
shemeji yake, na kumuuliza.
‘Eti
shemeji hilo ni kweli, umelalamika nini…mmh…, kwa….ka-ka..yako kuwa kaka,
hakukujali …au ?’ akauliza na mimi nikamuwahi.
‘Nijibu
hilo swali wewe…, nataka nisikie kauli yako, kutoka kinywani mwako wewe…?’
nikauliza.
‘Sikiliza,
usitake kutogombanisha, ..kama shemeji alilalamika hivyo, kafanya makosa, kaka
hakuwa hivyo, kaka alikuwa muwazi kwa kila mtu…hakupenda mambo ya siri, kila
jambo aliliweka kwa mizani yake…’akasema na kutulia kidogo.
‘Ndio
kuna maswala ya kiume, alijua hili halina umuhimu kwa wanawake, aliweza
kulipeleka hivyo hivyo, ila kwa busara zake, shemeji anafahamu hilo…labda kwa
hivyo, wanawake wanaweza kulalamika kuwa wanaonewa,…ni hivyo shemeji eeh…?,
..lakini kwa kaka alikuwa makini sana, mtu akimlaumu kwa hilo anakosea, hakuwa
mchoyo, labda kwa ….’hapo akashtuka,…na akatulia halafu akasema.
‘Labda
kwa hilo la deni…..’akamalizia hilo baada ya kutulia kidogo
‘Ndio
maana mimi nina mashaka na hilo deni, kama hata wewe uliyekuwa karibu yake, si
wewe ulikuwa karibu yake kwa kila jambo, ikiwemo hilo la benki, na wewe hujui
kitu…kama kaka yako alikuwa hivyo, unavyosema, ..kuwa hakuwa mchoyo, alikuwa
muwazi ,…sizani angeliweza kuchukua deni kubwa hivyo, bila ya kuwashirikisha
nyie ndugu zake, bila ya kumshiriksiha mkewe, bila hata kuacha kumbukumbu kwa
mkewe…mimi kutoka nafsini mwangu, nahisi hilo deni lina utata…’nikasema
‘Siwezi
kukushangaa kwa hilo,..unasikia, ni sahihi yako kufikiria hivyo, hata sisi
yakhe...’akasema.
‘Basi
kama ni hivyo, tusaidiane kuutafuta ukweli…’nikasema
‘Unajua
wewe ni kama unaturudisha nyuma, yote hayo sisi tulifikiria,… yote hayo, yalituumiza
kichwa,…unaonaeeh..tukahangaika weeh…na hadi …ilipofika benki, tukahangaishana
nao, kiasi cha kutoleana maneno makali, kawaulize benki….na tulipofika
mahakamani, tukasalimu amri, wao wana vithibitisho…wana ushahidi uliokubalika kisheria…utafanyaje
hapo,..?’ akaniuliza
‘Tutafanyaje
hapo,tu-ta…’nikasema hivyo kwa msisitizo.
‘Tutafanyaje!!...hahaha,
sio mimi tena, labda shemeji..hapana mimi nimechoka…, lakini utafanyaje hapo..ni
wewe sasa, sis tulishahangaika vya kutosha…., hebu wewe utuambie labda, ni wapi tulikosea, tuonyeshe njia,…kama
tutaigudua tutakuambia huko hatukupitia,….sawa kwa hivyo tunaweza kushirikiana,
sawa..au sio shemeji?’ akamgeukia shemeji yake halafu akasema;
‘Shemeji
huyu..unasema ni ndugu yako,…kifupi huyu mtu anachotaka ni kutupozea muda,
…kwani huyu mtu ni wakili eeh, kama ni wakili eeh, ni hao wanatafuta pesa
tu…huku mtoto aendelee kuteseka, sisi tumeshachoka…au sio shemeji…!?’ halafu
akanigeukia mimi alipoona shemeji yake kakaa kimia tu, akasema;
‘Umesikia,….wewe
huna uchungu na mtoto maana sio damu yako,..hata kama ni kaka, huna uchungu huo
zaidi yetu sis…..sio kama mimi baba yake, au huyu mama yake, eeh,…..tumechoka,…’akasema
sasa akihema kwa nguvu
‘Hivi ni
nini mali..ni nini nyumba eeh..halafu hilo ni deni, lipo wazi..haya hebu
tuambie, una mikakati gani mipya, labda unajua labda mimi nakosea, au sio
shemeji, tumuache tuone hija zake au sio…’akaniangalia mimi huku akanikazia
macho, mimi nikatulia kwanza sikusema kitu, na ndio akaendelea kuongea
‘Ok…ok….labda
mimi nisichukulie hivyo, huenda, ukasaidia,..haya hebu niambie wewe, kwanini una
mashaka, na hilo deni, na mimi si naruhusiwa kukuuliza maswali au sio..…maana
hata sisi tulikuwa na mashaka hayo hayo…huenda kweli akatusaidia…’akamgeukia
shemeji yake
‘Au sio
shemeji, ..tumsikilize kwanza, hata mimi nitafurahia…ila muda sasa..sijui haya
kama hamjali hilo la muda sawa,….’akasema na kutulia
Alipoona
mimi bado nipo kimia, ….akanigeukia, halafu akamgeukia shemeji yake, akionyesha
mikono ya kushangaa, na kukata tamaa, halafu akasema;
‘Unaona
shemeji ni yale yale..kama ilivyokuwa sisi, kwa mtu anayemfahamu kaka, ni
lazima atakuwa na mashaka hayo…, siwezi kushangaa kwa hilo, lakini ili
kuyaondoa hayo mashaka, huyu mtu, yeye mwenyewe aende huko benki, akafuatilie,
sisi…mimi mwenyewe nilihangaika kufuatilia hilo, nikachemsha, maana hatujui , na hata shemeji naye akajaribu akachemsha,
ukweli ni kuwa hilo deni lipo, na ushahidi upo, hatuna ujanja nalo…’akatulia
kidogo
‘Ushahidi…’nikataka
kuongea, yeye akaendelea kuongea
‘Tatizo kaka
alichukua mkopo huo bila kumwambia mtu, na matokea yake ndio haya,…unaona,
hakuna anayefahamu uhai wake, ilitakiwa angalau amwambia hata mkewe, unaona
eeh…sasa hata mkewe alikuwa hafahamu,….. matokea yake ndio hayo…’sasa
akawageukia watoto.
‘Unajua
isingelikuwa watoto…isingelikuwa mtoto anaumia..mimi nilipanga nipambane nao,
hata kwa mwaka mzima,…lakini huruma,…mimi ni baba…yupo mama yake hapa,..kwanini
mtoto ateseke..kwanini hiyo hali iende kumgusa mtoto, unaona jinsi ilivyokaa
vibaya…mtoto wa watu anateseka kwasababu ya hilo deni, ….sisi tufanyaje kama
wazazi…’akawa kama ananiuliza
‘Je
tujali mali, au afya ya mtoto, na sio afya tu,…uhai wa mtoto….sisi baada ya
kuhangaika kote huko, tuliambiwa baada ya hapo, mmoja baada ya mwingine
ataelekea kaburini, …..kaanza mtoto, hatujui…hatuombei mabaya,….na najiuliza yu,
ni nini mali, mali ipo, na tutaiacha, kama alivyoiacha marehemu…si alikuwa na
mali, sasa hivi yupo wapi, inaniuma sana…’hapoa akaongea kama anataka kulia
‘Kwa-kwa….’akachukua
leso na kufuta usoni, halafu akasema….
‘Muhimu ndugu
yangu, ni jinsi gani ya kulilipa hilo deni, kama unafahamu namna nyingine sawa,
tusaidie kwa hilo tutashukuru sana…sisi kama familia,…hakuna mwenye uwezo
huo…’akatulia
‘Mlivyouza
mashamba si mngepunguza punguza ili kuonyeshe dalili ya kulipa lipa huku
mnafuatilia eeh, mimi nahisi kwa mashamba yote hayo ingelisaidia, au pesa za
shamba mligombea wana ndugu…?’ nikauliza
‘Mashamba…hahaha,
kumba unajua mengi, shemeji keshakuambia kila kitu, hahaha….unasikia nikuambie
kitu…’ kwanza alionyesha mshangao, halafu akaongea huku akijikwangua kichwani.
Na mimi nikazidi kutia mafuta;
‘Nyie si
mliuza mashamba yake au sio…mkisema ni mali yenu…mali ya familia kuu, sio mali
ya marehemu …lakini marehemu alikuwa sehemuu ya familia kuu, je sehemu yake
ilikwenda wapi, , au hilo halihusiani na deni…?’ nikauliza hapo, akagwaya,
halafu akamgeukia shemeji yake, na kusema;
‘Shemeji,
swala la mashamba si tulishalimaliza au sio…hilo halihusiani na familia hii,
mashamba yalikuwa mali ya familia yetu, familia kuu, kaka alikabidhiwa kama
msimamizi tu…, sasa hayupo,hatuwezi kusema ni mali yake…’akasema
‘Una
uhakika na hilo kuwa kaka alikuwa msimamizi tu..sio kwamba yeye alinunua , na
kila akinunua anawashirikisha na nyie, si ndio hivyo…?’ nikamuuliza
‘Hilo
sitaki kuliongea maana hayo ni maneno ya mitaani, undani wa hayo mashamba
naufahamu mimi na familia yetu..haikuhusu, na…kwa hilo, haina haja ya wewe
kuniamini au la, maana hayo hayakuhusu kabisa,…’akasema
‘Mimi
nimeongea hilo, kuwa kama nyie mngekuwa mkimjali kaka yenu,kama alivyokuwa hai,
basi kwenye mauzo ya mashamba hayo, kwasababu yeye alikuwa ni miongoni mwenu au
sio.., na alikuwa na sehemu yake..au sio..basi hiyo sehemu yake baada ya
familia kugawana, hiiyo sehemu yake ingesaidia kupunguza deni, na nyie kama
familia mngechanga kiasi ili kupunguza deni, au……’hapo akanikatisha na kusema
‘Yeye pia
alipewa fungu lake,…tena alipendelewa, akapewa sehemu kubwa zaidi, lakini
iliyouza hilo shamba, hiyo sehemu yake, ilitumika kwenye matibabu ya shemeji..shemeji
ni kweli sii kweli…?’ akamuuliza shemeji yake, na shemeji yake akainua uso kama
kutaka kusema mimi nikaingilia kati.
‘Sijakata
ushahidi, nataka wewe unijibu…’nikasema
‘Ni
lazima hilo tulithibitishe kwa kauli yake ili tusipotezeane muda, ....ndio
maana tokea awali nilikuuliza je shemeji hajakuambia ukweli wote, kama
alikuelezea maswala ya mashamba, basi angelimalizia na ukweli huo, kuwa
mashamba yalikuwa mali ya familia kuu, na yeye , marehemu alipewa fungu lake,
na fungu lake lilitumika kumtibia yeye, je kwa kufanya hivyo tulikosea…’akasema
kama anauliza
‘Kwahiyo
nyinyi kama ndugu zake, …mumesaidiaje kuhusu hilo deni…?’ nikauliza
‘Sisi
kama familia, tulisaidia sana, kutegemeana na hali zetu, deni la marehemu ni
deni letu sote,..lakini tufanyaje , hali zetu sio nzuri kihivyo,…awali tulichangishana,
si unajua tena, ndugu ni ndugu,…tunafahamu sana dhima ya deni, basi,
tukashikama mashati, ..kulipatikana nini basi..pesa ndogo tu, ambayo
haikusaidia kitu…’akasema na alipoona nataka kuuliza swali jingine kwa haraka
akasema
‘Unajua ndugu
muda ni mali,…tusipotezeane muda, cha muhimu ..ni jinsi gani ya kulilipa hilo
deni, ungetakiwa uje na mikakati hiyo..jinsi-gani-ya-kulilipa-hilo-deni ..vinginevyo,
kama walivyoamua wenyewe banki, hatuna ujanja, hatuna jinsi, ..kama unayo wewe
, haya endelea, uwanja ni wako, ila…’akasema akimgeukia mtoto, na mimi sikutaka
arudie rudie yale maneno ya vitisho, nikauliza kwa haraka.
‘Benki
waliamua nini..?’ nikamuuliza kama sielewi kitu
‘Si wewe
unafahamu taratibu za beni ukikopa kwao, dhamana ni lazima, au sio…inabidi
banki wafuate hivyo, kuwa kwa vile kaka aliweka dhamana ya nyumba, basi, wao
wataipiga hiyo nyumba mnada,….walitupatia muda wa kulipa ikaonekana hatuwezi,
basi wakatuita, na kutuelezea msimamo wao, kuwa ikipita muda huo wao, hawana
jinsi…watapiga nyumba mnada, na pesa
itakayopatikana italipa deni, na itakayobakia…wanakabidhiwa warithi..sio haba,
kuliko kukosa vyote, mimi nikawaambia sikubali ndio tukaenda mahakamani, kipo
wapi…hatukuwa na cha kujitetea, hatuna ushahidi wowote, ilikuwa ni aibu…’akasema
‘Kwahiyo kwa
msimamo wako, kwa hekima zako, wewe umeona ni vyema tuache, nyumba ipigwe mnada, ili lilipwe hilo
deni….huoni kuwa tutakuwa hatujawatendea haki hawa wanafamilia, mama na watoto
wake?’ nikauliza
‘Hii
ilikuwa nyumba ya marehemu na yeye ana mamlaka ya kufanya apendavyo,..hata kama
hayupo hapa duniani,.. au sio…labda nitumie lugha hiyo ili unielewe…kama
ilikuwa nyumba yake ndio maana aliweka kama dhamana, kuwa hata akiwa hayupo
deni lake litalipwa, au sio…kuna kosa gani hapo…’akasema kwa lugha nzito kidogo
‘Au
nimekosema ndugu yangu eeh, niambie …si ilikuwa nyumba yake hii, au shemeji,
niambie hii nyumba alijenga nani, eeh, au nadanganya,…eeh,…?’ akawa sasa anaongea
kwa lugha ya kama kukasirika, halafu baadae akashusha sauti na kusema
‘Na maswala ya watoto jamani eeh, na wao wana
riziki yao, labda mungu hakupanga hii nyumba iwe riziki yao, na mungu hana
lawama, eeh, yeye mwenyewe anafahamu jinsi gani ya kugawa amali,..riziki zake
kwa waja wake, na wao, …hizo pesa zitakazobakia watajenga nyumba kutegemeana na
uweo…tutasaidiana, nitafanya nini na mimi ni baba yako eeh…’akatulia
‘Wewe
unaamini hivyo, kuwa nyumba hii haikuwa riziki ya hawa watoto…?’ nikauliza
‘Sasa
nitasemaje hapo… mungu atawajalia hawa watoto watakuja kupata ya kwao, hata
mimi sio kuwa napenda iwe hivyo, hiyo ni amri ya benki, kama kuna namna
nyingine tusaidiane tu ndugu yangu,…au wewe niambie sisi tufanyaje au
tutawezaje kuzipata hizo pesa, maana sio pesa ndogo ya kusema tutakuja kulipa,
hatuwezi…?’ akasema
‘Mimi
sijakataa ..maana kama imefikia hapo ina maana ulijitahidi kutafuta njia
nyingine ukashindwa, hata huko kwa mtaalamu wako unayemuamini,..hata yeye
alishindwa ndio akaja na mipango hiyo ya kutishia amani, au sio….’nikasema
hivyo kumpandisha jazba, watu kama hawa unatakiwa ujaribu njia zote
Jamaa
kwanza akacheka, na kutikisa kichwa..haalfu
akasema, jamaa …anajua ….sivyo kama nilivyotegemea, akasema hivi;
‘Hahaha..hizo
ni imani tu, kwenye…deni, hasala benki, huwezi kufanya lolote…hayo unayosema
unayasema wewe…mungu akusamahe tu…’akasema hivyo
‘Lakini kwani
nadanganya, wapo wanadai kuwa wanaweza kulipoteza deni, kumvuta mpenzi, nk…sasa
wewe hukujaribu hilo,..nahisi ulijaribu ukashindwa, …na kama nilivyofahamu
hapa, ina maana mkopaji alikopa akiwa na malengo, alikuwa kapanga namna ya
kurejesha huo mkopo au sio…na kwa vile hamkuwa na taarifa ya huo mkopo, mtakuwa
vile vile hamjui jinsi gani ya kuurejesha
au sio…l?’
‘Ndio…hapo
tupo sawa, kabisa, kabisa, hatuna jinsi, hatujui kabisa yeye alipanga nini,…hayo
ya kusema ..eti..mtaalamu kafanya hivyo kutishia, sikulipenda hilo…ulitakiwa
uniombe radhi..lakini sawa, mdomo ni wako, unaweza kusema upendavyo, ila mimi
kama baba, kama mzazi wa hii familia, nitaangalia kile chenye usalama
kwao..unanisikia….’akasema akitikisa kichwa kukubali
‘Ndio maana,
mimi ninakuwa na mashaka na huo mkopo,
yawezekana huyo kaka yako hakuchukua huo mkopo…kama aliuchukua mkewe angelijua,
wewe ungejua, na kungekuwa na mradi…kitu cha kuzalisha, au shughuli kubwa ya
huo mkopo, na mkewe angeliweza kulijua hilo, au wewe unafahamu kaka yako
alikuwa na mradi gani mkubwa, zaidi ya hiyo shughuli yake, au alikuwa akijenga
mahali, au ndio hiyo alinunulia mashamba, hebu tuambie…?’’nikauliza.
‘Hakuna
mradi kama mradi aliouacha kaka,…nijuavyo mimi, miradi yake ilikuwa ya kuchukua
mizigo anauza, mzigo ukiisha anakwenda kuchukua mwingine ni hivyo tu, na ni
biashara ambayo hakuianza karibu, baada ya kuachana na shughuli za ajira,…na
akiba akawa anaweka benki…na ni pesa ndogo tu tuliyoikuta benki,… ina maana basi
alipoondoka alitoa pesa karibu yote, kwenda kuchukua mzigo, akijua akirudi,
atapata fadia kubwa, sasa sijui…maana hatukukuta kitu…kwenye gari lake,…,
hakuna pesa wala mizigo….’akasema
‘Hapo
sasa ndio naona kweli yeye hajachukua huo mkopo, wewe hulioni hilo…kuna namna,
kuna mtu kachukua huo mkopo kwa ujanja-ujanja,..akili yangu haikubali…, yaani
mpaka hapo, mimi naanza kupata picha, …..’nikasema
‘Unaanza
kupata picha gani, hebu tuambie, maana wewe sasa, …usipoteze muda, kwani wewe
ni wakili au una ..unawezaje kuzuia haya ya mahakama….’akasema halafu akacheka
kwa dharau,
‘Wewe
unasema alichukua pesa iliyokuwa benki karibu yote ili kuchukulia mzigo, huo
mkopo mkubwa hivyo ulikuwa ni wa nini,..kwanini kama alichukua mkopo eeh,
kwanini akombe tena balance yake ya benki… je alikuwa na account ngapi benk…kama
alikuwa na biashara, anauza pesa anaweka benki, na siku hiyo kwa kauli yako,
alichukua pesa karibu yote…je ni mzigo gani mkubwa hivyo, wa kununulia pesa
hiyo yote, mkopo na ..…hebu fikiria hapo…?’ nikamuuliza hapo akasita kidogo.
‘Huenda
alichukua kwa shughuli nyingine, sisi hatuwezi kulifahamu hilo….’akasema kwa
kunywea kidogo, nikaona sasa naanza kumweka sawa.
‘Kama
ipi…ambayo hata wewe huijui, au mkewe haijui, kuna mtu kachukua na deni hilo ,….’nikasema
na yeye akanikatiza kwa kusema
‘Mimi
siwezi kujua zaidi, kama ilivyo mkopo wenyewe. Na unaposema labda kuna mtu
mwingine alichukua, hebu niambie, huyo mtu mwingine angelichukuaje,…unakuwa
kama hujasoma bwana, mkopo uchukuliwe benki na mtu mwingine uwekwe kwa mtu
mwingine, kwa vipi…wewe kweli sikuelewi,…nakutilia mashaka na elimu yako….au huwaamini
watu wa benki au….’akasema
‘Nitakuja
kukuonyesha elimu yangu ipoje, usijali hilo, ila kwanza nataka uelewe kuwa hata
huko benk kunaendeshwa na watu, na watu wote sio sawa, na kuna ushahidi huo,
nitakuja kukuonyesha hilo,.na mahakamani pia,… ila kwasasa nakuambia hivi,…nina
mashaka kabisa na hilo deni halikuchukuliwa na kaka yako…unasikia, ndio kauli
yangu hiyo, jiandaeni kwenda mahakamani….’nikasema kwa kujiamini utafiki kweli
nimeshakuwa na ushahdii wa kutosha
‘Hilo
sasa ni jipya, …hahaha, twende wapi, yaani sijakuelewa hapo ndugu yangu,
hahaha, haya buana, maana unajiamini sana, hata mimi ilikuwa hivyo hivyo…’
akacheka kwa dharau, halafu akasema;
‘Ndio
hivyo…’nikasema sasa nikiangalia saa yangu
‘Wewe ni mtu
wa ajabu, nyie ndio mnaopenda kuzusha mambo…, hata wapelelezi wa polisi
hawakuwahi kusema hivyo,…wewe unasema hakuwahi kuchukua…sawa, hata wao walikuwa
na shaka shaka hiyo, je walipata nini…wanaishia kusema eeh, kweli deni lipo,
..lakini tuna shaka nalo, labda sio yeye alichukua, sasa…tuonyesheni huyo mtu
mwingine kwa ushahidi,…watasema nini hapo, sasa wewe umevuka mpaka kuwashuku benki,
hahaha….’akasema
‘Kwani
hao polisi walisema nini, kuhusu hiyo kuwa waonyeshe mtu mwingine kwa ushahidi …?’
nikamuuliza
‘Wao
walihisi kuwa mimi nilikuwa najua hilo deni , maana deni lilishathibitishwa
kuwa kweli lipo…ya kuwa kaka kweli kachukua, wao wakahisi kuwa huenda mimi nafanya mbinu labda, ili hilo deni
lifutwe, wakanibana kwa maswali, vitisho, hata wengine kuanza kunitesa,lakini
mkuu wao, akasema no…, huwezi kumtesa mtu hapa..….sasa wewe unakuja na hoja ya
kuwahuku benk, wao wana kila kitu eeh,…je wewe hujiulizi tu, hizo hati
alizosaini bro, zilikuwaje, kweli hazina sahihi yake, hilo
hujalifikiria,..nakufungua macho na akili hapo tu….’akasema
‘Mliziona
hati alizosaini, sawa, na sahihi ni yake sawa…si ndio hivyo, ndio kigezo chako
kikubwa hapo,..lakini pia watu wanaweza kuwa wajanja kwa hilo, sasa hizo
sahihi, na mikataba ndio itakuwa ushahidi wetu ….’nikasema
‘Hahahaha,
hivi wewe vipi,… samahani lakini mimi nina mashaka na elimu yako, kama wewe ni
wakili, haah, aisee, watu wanaliwa pesa yao bure tu…sijui lakini,…ila shemeji
huyu mtu, kama ni wakili eeh, umeliwa….’akasema akimuangalia shemeji yake
baadaye akanigeukia na kusema;
‘Hivi nikuulize swali, eeh, inawezekana vipi isiwe
kweli wakati kuna sahihi, ..haya achilia mbali sahihi, na dole gumba je…mimi
sikuelewi, ndio maana mimi natilia shaka, utaalamu wako, nisamehe tu ndugu
yangu,… ‘akatulia
‘Mimi
nina shaka na hata hilo dole gumba, …’nikasema
‘Eti,
nini, …jamani, ….huyu mtu vipi,….?’ Akauliza sasa akionyesha uso kwa
kutahayari.
‘Mimi nina
shaka na sahihi, na hilo dole gumba, mimi nina shaka na hilo deni kwa ujumla,
…na lazima tutafute ukweli wa hilo deni,….hilo deni sio sahihi, …sio deni la
kaka yako…’nikasema
‘Haya
wewe niambie, labda nishuke ni sawa na wewe, haya niambie wewe, toka lini mtu
akaweza kutumia sahihi ya mtu mwingine, sahihi umesema mtu anaweza kugushi,
haya hilo dole gumba….unawezaje kugushi, nakuuliza wewe…?’ akauliza
‘Ndio
hapo, mimi nataka tuifanyia kazi hiyo iliwezekanaje hivyo, watu wakagushi,
sahihi na dole gumba, …’nikasema
‘Oooh…kumbe,
nilijua tu, wewe wataka kupotezea wengine muda wao,…nakuambia hivi benk
wameleta vithibitisho vyao ndio hivyo…, hebu na wewe leta vya kwako, ili tuone
kama kweli sio deni halali…’akasema
‘Vitaletwa…’nikasema
‘Kama
kweli utalifanikisha hilo, mbona utatusaidia sana…’akasema akimminyia shemeji
yake jicho alifikiri mimi sijaona,…
‘Kwa
ushirikiano wako, hilo litafanikiwa…’nikasema
‘Kwa
vipi, mimi tena….ujue hapa tunapambana na muda, kesho, huenda huo mnada
ukafanyika japokuwa nasikia fununu tena, kuwa huenda, umesitishwa, hapo sielewi
ni kwanini, mimi mwenyewe…nimeongea na benki wakasema hawana jinsi nyingine,
zaidi ya kufanyika kwa huo mnada, na sio hapa tu, kuna wadeni wengi tu
watafanyiwa mnada…’akasema
‘Huo
mnada hautafanyika…’nikasema kwa kujiamini.
‘Eti nini,
hautafanyika, nani kakuambia, wakati kila kitu kipo tayari, unajua mimi
sijakuelewa wewe ni mtu gani, kwani wewe ni nani na unataka nini, una ushahidi
gani kuwa hilo deni sio la kaka, na …na
sasa unaongea kwa kujiamini kuwa huo mnada hautafanyika, unakaidi amri ya
mahakama,…bwana wewe usitupotezee muda, au kama una ushahidi utoe, eeh, unao
huo ushahidi….?’ Akauliza
‘Kwanza
tunachotaka kujua ni ukweli wa hilo deni, hilo deni ni halali,…ok, kwa
kumbukumbu za kibenki hilo deni lipo, lawezekana likawa nihalali,..lakini hebu
kwanza kabla hatujafikia huko kwenye vidhibiti vyenyewe, tuchangamshe vichwa
vyetu kwanza,.. tuanze kulipekenyua hilo deni, je hilo deni lilianzia wapi,
lini…?’ nikauliza
‘Kawaulize
watu wa benki….’akasema hivyo
‘Ni nani
wa kuwauliza watu wa benki, …ni mimi au ni wewe…?’ nikauliza
‘Ni wewe
mwenye shaka na hilo deni….’akasema
‘Ni wewe
uliyepewa hiyo dhamana, au unaikana hiyo dhamana, ukweli halisi unatakiwa
uanzie kwako, kabla hatujafika huko benki, kwasababu wewe ndiye uliyepewa hiyo dhamana…unakumbuka
mimi nilikuuliza awali je ulijirizisha kuwa kweli hilo deni ni la kaka yako
ulisemaje..?’ nikamuuliza
‘Lakini
sikukuambia kuwa alichukua lini, tarehe gani, hayo mimi sikuwa na shaka nayo,
kwasababu tarehe hazina maana, kama mkataba upo, na …” akatulia
‘Unaona
eeh, ina maana kiukweli hukujiridhisha vya kutosha,…. kwahiyo ili kusaidia
hilo, ili tujue huo ukweli, na undani wa hilo deni,..lini, lilianzaje, mtu wa
kuweza kutusaidia ni wewe….’nikasema
‘Kwa
vipi…?’ akauliza
‘Ehee…utasaidiaje,
ni kwa wewe kunijibia maswali yangu muhimu sana, ambayo, yatakuwa ushahidi
mahakamani….’nikasema
‘Mahakamani,
unarudia tena….mahakamani…?’ akauliza sasa akikunja uso, na kutupa jicho kwa
shemeji halafu kwa mtoto.
‘Shemeji
huyu ni ndugu yako kweli, ni nani huyu, huyu anataka kuleta matatizo mengine
kabisa, unamuona lakini ni kama ananitupia lawama mimi,…mimi sitakuwa kuja
kulaumiwa tena, kwa hayo yatakayotokea kwa mtoto wa-ko…’akasema akimuangalia
shemeji yake akiwa katoa macho, kama kutishia vile.
‘Sikiliza
mimi nina uhakika wewe ukinijibu maswali yangu ya msingi, tutakwenda sawa, na
maswali hayo na majibu yake yawe katika maandishi ili yaje kuwa ushahidi, na
kwa hayo hatutapotezi muda kabisa, maana ni kwa ajili ya masilahi yenu, au sio,
ni kwa ajili ya haki ya hawa waliochwa ukiwa, mama mjane na watoto..ni kwa
ajili ya kupambana na dhuluma kwa hiyo aliyetaka kutenda dhuluma, na kamwe
dhuluma haidumu…au sio muheshimiwa..?’ nikamuuliza
‘Kwahiyo
unataka kusema nini…?’ akauliza, na mimi nikatoa karatasi , kujifanya nataka
kuandika, lakini kwa jicho jingine nikawa naangalia ile simu kama bado
inachukua hayo mazungumzo, niliona kama imezimika hivi,
‘Nataka
nianze kukuuliza maswali, na iwekwe kwenye rejea, maana majibu yake yatatusaidia
huko mahakamani…’nikasema
‘Kwanini Mahakamani,
mahakamani,..mahakamani, huko tumeshafika sana,…sikiliza unataka kuniuliza
maswali gani, wewe uliza..’akasema kwa hasira
‘Ila
nakuasa kitu kimoja, …haya unayotaka kuyafanya wewe sasa ndiwe utakuwa na
dhamana ya huyo mtoto,…mimi sitaki tena hiyo hali imrudie huyo mtoto, na ikirudie unajua hatari
yake, eeh, mama yake huyu hapa analifahamu hilo,mimi sina uwezo wa kufanya
lolote, ndivyo mtaalamu alivyosema, hata angelikuwa nani, hawezi kumsaidia tena
huyo mtoto, kwahiyo sisi..tutampoteza mtoto kwa uzembe wenu, mimi sipo ….’
Akageuka kumuangalia shemeji yake
Shemeji
yake akawa kimia, kainamisha kichwa chini..
NB: Ni
nini kitaendelea hapo, ni maswali gani hayo, na je hayo maswali yatasaidia nini
wakati benki wameshathibitisha kuwa sahihi na dole gumba ni za marehemu…je na
hivyo vitisho vya shemeji ni kweli..mtoto anaumia kweli!
WAZO LA LEO: Tusiangalia sana masilahi kuliko
haki na ukweli, wengi wetu wanapopewa madaraka wanaegemea sana kumrizisha bosi
…au kufanya kwa ajili masilahi, bila kujali taaluma aliyoajiriwa nayo hata kama
ukweli upo wazi, na matokea yake anawaumiza hata wale wasiostahiki, tukumbuke,
madaraka ni dhamani, utakuja kuulizwa jinsi gani ulivyoyatumia hayo madaraka
yako.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment