‘’….sikiliza
kama wewe unataka kuyachokonoa haya mambo sawa endelea, …ila … Ila mimi nakuasa kitu kimoja, …hayo unayotaka kuyafanya
wewe, unanisikia eeh, yalishafanyika, sitaki kurudia rudia, matokea yake yakawa
hivyo…unasikia,…’akaninyoshea kidole, na kumuonyeshea yule mtoto.
Mimi
sikusema jambo, nikawa namsikiliza tu.
‘Sasa
eeh,… kuanzia sasa, wewe ndiwe utakuwa na dhamana ya huyo mtoto, na familia kwa
ujumla, … umesikia nilivyo kuambia…lolote likitokea …mimi simo..tusije
kulaumiana...’akasema akionyesha kama ananawa mikono.
Mimi nikawa na muangalia tu, baadae naye
akatulia, hapo na mimi nikaanza kuongea, nikasema;.
‘Hivi
kwanini nyie watu mnapenda kuwatumia watoto kwenye mambo yenu, ya kishirikina….’nikasema
hivyo na huku namuangalia kwa makini
Nilimuona
, akaonyesha dalili ya kushtuka kidogo, lakini akajikausha, halafu akatoa lile
tabasamu lake la dharau, akatikisa kichwa, halafu akasema.
‘Eti nini…?’
akauliza akiwa haniangalii moja kwa moja usoni…
‘Umenisikia
vyema, …haya yanayofanyika, kwa jinsi ninavyoona mimi, hivi vitisho..kumtesa
mtoto, kuna jambo, na nahisi haya yamefanyika kwa makusudi fulani,…, na wewe iavyoonekana,
unajua hili jambo,…’nikasema nikionyesha kujiamini na yeye hapo akakunja uso,
halafu akatikisa kichwa , baadae akatabasamu na kusema;
‘Unajua nini…
kwa vile ni mimi ndiye niliyekwenda huko kwa huyo mtaalamu, siwezi kunyamaza,
hata useme nini, mimi nafahamu madhara yake, kufahamu kwangu ndio huko zaidi ya
hayo, ni yako wewe…unasikia, . wewe hujui tu…’halafu akamgeukia shemeji yake,
akasema;
‘Shemeji
mimi naogopa sana hili jambo,… hivi likitokea la kutokea, tutasema nini,
utanilaumu mimi, utamlaumu nani, mimi sikukuambia…sitaki ije kuwa lawama
kwangu, najua hata mimi nitaumia, maana hao, ni watoto wangu, ni damu yangu,
kaka na mimi haina tofauti …’akasema, akimuangalai shemeji yake, halafu mimi.
Mimi
nikaendelea kukaa kimia, huku nikiangalia simu yangu ikiwa pale mezani,..nilikuwa
nasuburia taarifa muhimu kutoka kwa vijana wangu, niliona wamechelewa kunipatia
taarifa muhimu…nikaona niendelee kumchokoza huyu jamaa.
‘Wewe ni
baba yake au sio…?’ nikasema kwa kuuliza
‘Sikiliza
Bro, ni kweli mimi ni baba yake, na nimejitoa kwa kila hali, sasa ni nini
nakipata kwa dhamana hiyo…eeh,…, ni nani anayejali kujitolea kwangu huko, hebu
niambie…, na sasa hata wewe unafikia kusema hayo maneno ya kipuuzi kabisa..,
unajua inaniuama sana…’akasema.
‘Maneno
gani ya kipuuzi, wewe unayaona hivyo, lakini ni lazima ukweli usemwe au sio, na
hayo niliyokuambia ni ukweli mtupu…’nikasema
‘Ukweli
gani…?’ akaniuliza akinikazia macho
‘Kuhusu
hivyo vitisho kwa mtoto, ina maana gani hapo…kuwa labda na wewe unajua
kinachoendelea, ndio maana kila tukijaribu kuitafuta haki, wewe unatishia,
kwanini ufanye hivyo, kama huhusiki…’nikasema
‘Kuhusika
kwangu ni kama nilivyokuambia, ni kwa vile niliongea na huyo mtaalamu,
akaniambia jinsi inavyotokea, kuna kosa gani kwa hilo, ina maana ningelitakiwa
nikae kimia, au..hapana siwezi kufanya hivyo, maana hawa watoto ni wangu pia,
na siwezi…..’nikamkatisha hapo na kusema;
‘Ndio
ulikutana naye kabla..mkaongea naye, mkapanga..yawezekana kuwa hivyo, au
sio..ndio mlipokwenda na shemeji yako, mka…’akanikatisha
‘Kwanini
nifanye hivyo..?’ akauliza kwa haraka.
‘Naongelea
hili kwa mtizamo wa haya yanayotokea,..kwanini uwe mshabiki sana wa mambo hayo…’nikasema
na hapo, akanikodolea macho, nilijua labda atakasirika, lakini badala yake
akatabasamu, na kusema;
‘Unajua…mimi
sivyo, kama unavyofikiria wewe…nawafahamu sana nyie watu,…mimi nakustahi tu,
maana nimekutana na watu wengi kama wewe…, ila mimi, …bado nazidi
kusisitiza…bado nazidi kutoa angalizo, maana mimi nafahamu madhara yake…’akasema
‘Najua
unalifahamu hilo, …lengo la watu wako, ni kumtesa mtoto ili mfanikiwe malengo
yenu,..sasa niwaulize tu,..mtapata faida gani, nyie si muna watoto hebu fikiria
hayo yangelitokea kwa mtoto wako ungelijisikiaje, eeh…’nikasema
Na kwa
muda ule mtoto alishaamuka, akawa anajitahidi kukaa , lakini kwa jinsi
anavyoonekana, nahisi bado yupo kwenye mateso ya joto la homa, sikutaka kumtia
mama yake wasiwasi, nikatulia kwanza,…na mama yake, sasa akawa anamuangalia
mtoto wake kwa mashaka pia, …akamsogelea
Mama
mjane alipomshika mtoto wake tu, …nikajua sasa mtoto keshaanza kuchemka tena.
Kwa hali ile, mama, akawa sasa anaonyesha kuchanganyikiwa,…naona alishachoka na
mates ohayo ya mtoto wake..mimi nikajipa moyo, moyoni nikawa namuomba mungu,
namuomba anipe hekima. Ni kweli kwa hali ile ungelisema basi, ngoja tuache
tu..lakini je hiyo ndio njia sahihi,…
Jamaa
alipomuangalia shemeji yake, akasema;
‘Kama
mtoto keshaanza kuumwa kivile anavyoumwa,..na ikifikia kupoteza fahamu.., mimi
sina zaidi…na alisema ikifikia joto kuisha ghafla, na mtoto kuwa baridi ndio
basi tena…maana hiyo dawa haitakuwa na nguvu tena…mimi nilishawaambia..msije
kunilaumu, mimi sipo, kwanza ngoja niondoke zangu …’akasema sasa akitaka
kusimama kuondoka;
‘Unakwenda
wapi sasa, na kwani sisi tumefanya nini kibaya, eeh, niambie wewe mliyepanga
hayo, sisi tumefanya nini kibaya,…..?’ nikamuuliza.
‘Mimi
nimekuelezea inavyotakiwa iwe, hujataka kunisikiliza, sasa nikae hapa
nikisubiria nini..maana mimi sijui malengo yenu ni nini,..na hao mizimu wanajua
lengo lenu ni nin, mimi utanidanganya, je hao…nyie jamani, mnataka nini..
kumuua huyu mtoto au…mbona mna tamaa ya mali hivyo,…mimi sitaweza kulivumilia
hilo…na kama baba, bora wewe uondoke humu ndani…au sio shemeji…’jamaa akasema
akimuangalia shemeji yake
‘Mimi sitatoka
hapa mpaka tumalizane mimi na wewe…’nikasema
‘Wewe
kama nani…?’ akaniuliza sasa kwa sauti ya ubabe.
‘Kama mtu
anayejali wanyonge, anayejali haki za mjane na mayatima, ..na kwa hili
nitahakikisha haki imepatikana, …’nikasema
‘Hahaha…unajua,
..shemeji, huyo …unajua, ..hata sijui niseme nini, yule mtu wa kutetea mayatima
na wajane, anaitwa nani…alikuja hapa, alisema nini, kauli zao ni hizo hizo…mimi
sioni ajabu, maana kila mtu anatafuta riziki mezani kwake,..na huyo na wenzake,
kazi zao ni hizo, sisi hatuna pesa za kuwalipa, msipoteze muda wenu bure….’akasema.
‘Hahaha,
nani kakuambia nafanya haya kwa ajili ya malipo..sikiliza Dalali…hilo la mtoto kuumwa
wala usijali kabisa, mimi nitabeba dhamana yake…kama kweli sote tunamuamini mungu,
basi mtoto huyo, hayo ya mateso yatakwisha…, atakuwa kwenye kinga ya yule
aliyemuumba,…labda mmoja wetu hapa awe anahusika kwa hilo…’nikasema bila kujali
maneno yake.
‘Unasema…nini,…!!?
Nani anahusika hapa, usitake kutuchanganya hapa, anayehusika na lolote dhidi ya
mtoto ni wewe unayetaka kuleta mambo kinyume na matakwa ya mizimu…?’ akauliza
kama kukasirika.
Mimi pale
nikamsogelea yule mtoto, nikamshika, mwili ulishaanza joto, na niliona kama joto linazidi kuongezeka…sikukata tamaa,
nikachukua gilasi ya maji, nikaanza kuyaombea …huku nahisi machozi yakitaka
kutokana na maombi yangu,…niliona taswira ya huyo mtoto kwenye hisia, akiwa
hajiwezi, …nilihisi vibaya sana, ..baadae nikamsogelea yule mtoto…nikamshika
shavuni…joto kali sana.
Sikujali
tena,…sikutishika kama awali… nikamwambia huyo mama mjane;
‘Mpe mtoto
haya maji anywe, kwa nguvu za muumba, hayo yote kama ni kwa nguvu za giza
yatatoka hayo mapepo na mashetani, na vibwengo, mizimu na watu wake…, kama ni
kwa majaliwa yake yeye aliyetuumba,..basi tumuomba yeye atusaidie, amponyeshe
huyu mtoto kwa uwezo wake…’nikasema na mama akampa mtoto yake maji..
Haikupita
dakika moja…Mtoto alitokwa na jasho, utafikiri kamwagiwa maji, kwa muda mfupi
tu…akalala…
***********
‘Sasa tuanze
kuulizana maswali, kumbuka mimi ninachotaka kutoka kwako ni ukweli, na sina nia
mbaya, unasikia, …’nikasema, jamaa sasa ananitolea macho kama mtu aliyeona kitu
cha kutisha
‘Shemeji vipi
mtoto…’jamaa akasema akimuangalia mtoto…mimi nikasema;.
‘Mungu
atamjalia, na atamlinda, sisi tuendelee au sio..’nikasema
‘Oh….afadhali
kama mtoto katulia basi, afadhali lakini mimi naomba jambo moja, kwanini
tunafanya haya, wakati tunafahamu kuna hatari, maana kutulia huko ni kwa muda
tu, kama bado lengo lenu ni lile lile..hali itaendelea kuwa hivyo…’akasema
‘Wewe
unajuaje hayo..?’ nikamuuliza
‘Majibu
yangu ni yale yale….’akasema
‘Sikiliza,
wewe sasa naanza kukuhisi vibaya..’nikasema
‘Kwanini…?’
akauliza
‘Sema
ukweli wako, wewe kuna kitu unakifahamu na unatuficha, nahisi kuna njama
mumezipanga wewe na wenzako…’nikasema na yeye hapo akajirudi, akatulia.
‘Kitu
gani yakhe…kauli zako ni hizo hizo, jaribu nyingine, mimi sina zaidi ya hayo
niliyokuambia, unielewe kabisa, au…unataka nifanye nini, ili uniamini…?’
akauliza
‘Huko kwa
huyo mganga, ulionyeshwa na nani, sio kwamba mnafahamiana naye siku nyingi…?’
nikamuuliza
‘Kuonyeshwa
na nani kwa vipi…?’ akauliza
‘Wewe
ulisema mtoto alipoanza kuumwa, ulishauriwa uende huko, au sio..au wewe uliona
ufanye hivyo ili mukamilishe mipango yenu..?’ nikamuuliza
‘Ni kweli
kwenda huko nilishauriwa na mtu, mimi nilikuwa simfahamu huyo mtu..’akasema
‘Ni nani
alikushauri uende huko…?’ nikamuuliza
‘Haikuhusu,
ni nani, siwezi kukuambia…’akasema
‘Inanihusu,
..nataka kumfahamu huyo mtu mliyeshirikiana naye…, la sivyo, ni wewe ulipanga
uende huko, ili kufanikisha malengo yenu…ndio maana nasema wewe unafahamu ni
nini kinechoendelea, wewe unajua ….’nikasema
‘Nijuavyo
mimi ni hivyo nilivyowaambia…’akasema
‘Sio
kwamba mlipanga na huyo mtu, mnayemuita mtaalamu ili haya yafanyike ili
mfanikiwe kwenye malengo yenu…?’ nikauliza
Malengo
gani, wewe mtu mbona unaropoka sana, nakushauri kitu, uwe makini na hayo maneno
yako…nitake radhi tafadhali, …tatizo wewe huelewi mambo ya mizimu ndio maana
unaongea lugha chafu kama hizo, siwezi kukulaumu, nakusamahe tu....ungelifahamu
mambo hayo, wala usingethubutu, sasa sikiliza…’akasema sasa akininyoshea
kidole.
‘Hao
mizimu kama wanaitakia mema hii familia, familia ya marehemu, walitakiwa
wasifanye hivyo, nijuavyo mimi, eeh,.. marehemu aliipenda sana hii familia, …na
akajenga nyumba hii imara ili waje kuishi familia yake na hadi vitukuu, na
vitukuu, kweli si kweli…?’nikasema kama kuuliza.
‘Huko tunarudi
nyumba, na kupote muda, samahani lakini….’akasema
‘Nakuuliza
sasa ni kweli si kweli, nataka kusikia kauli yako … wewe hukuwahi kumsikia kaka
yako akisema hivyo..kuwa hii nyumba wataishi hadi vitukuu, je kwanini sasa
iuzwe….?’nikamuuliza
‘Kaka
eehn …ndio, niliwahi kumsikia akisema hivyo, tena mara nyingi sana, lakini
sasa, unajua ndio maana sisi hatukuamini, mpka tukafika mahakamani, unielewe
ndugu yangu…’akasema
‘Sasa
kwanini hao mizimu wawe kinyume na kauli ya kaka yako, kama sio maadui wa kaka
yako…na..kwanini unavurugwa akili na vitu kama hivyo hadi ufikie kuikana kauli
ya kaka yako,… ?’ nikamuuliza
‘Jibu ni
lile lile….’akasema
‘Ndio
maana mimi nakutilia wewe mashaka,
unanifanya nikushuku vibaya, maana kama kweli wewe ungelikuwa upande wa kaka
yako, ungeipigania hiyo kauli yake,..hadi hatua ya mwishi na ili, twende sawa,
nahitaji muda wa maswali mimi na wewe…’nikasema
‘Sikiliza,
mimi sijaikana kabisa kauli ya kaka… na sikuwa tayari kufanya hivyo,…mimi
ninachotaka kukifanya ni kuhakikisha, kwanza hii familia ipo salama, pili roho
ya marehemu inastarehe peponi, mimi nina uhakika kutokana na hili deni kaka
huko alipo anateseka,..na…na sitaki kitu kitokee kwa hii familia pia….’akasema
akionyesha uso wa uchungu, na mikono ikiwa mbele kama ananiomba mimi.
Aliponiona mimi nipo kimia, akamgeukia shemeji
yake, akasema;.
‘Shemeji mbona
upo kimia, kwanini hunisaidii…hivi umesahau tulivyohangaika hadi hayo yanatokea
kwa mtoto eeh,…muda wote najaribu kukuuliza ili unisaidie, lakini yaonekana
kama nipo kivyangu, ..haya bwana,…niachie nihangaike na watoto wangu, sitachoka
kwa hilo…’akasema.
‘Shemeji
yako, anafahamu kabisa kuwa hilo deni sio stahiki ya mume wake, shemeji yako,
anajua kabisa, hii nyumba haitakiwi kuuzwa, ila hana jinsi ya kufanya, jinsi ya
kufanya ni sisi tumsaidie yeye, je kumsaidia kwake ndio huko…kumtesea mtoto
wake…’nikasema
‘Ni nani
anayemtesea mtoto wake…hayo ni maneno yako..na siyapendi. Nisikilize, mimi
sitai hizo kauli zako, ..shemeji yeye anaogopa kujibu tu hapa, alishasema kama
ni nyumba iuzwe tu, yeye hataki tena hayo mambo, alishakubaliana na mizimu…ili
wao wawe na amani…sasa ni wewe unayekuja kuharibui…’akasema
‘Tunapoteza muda…au sio…’nikasema
‘Ingelikuwa
nimekwenda mwenye ungesema labda, lakini nimeshakuambia mimi nilikwenda an ndugu yake
shemeji, na kwa msisitizo mimi narudia tena, ile hali ya mtoto haitakiwi
ijirudie zaidi ya tatu,….’akasema na simu yake ikatoa mlio wa ujumbe wa maneno,
akaitizama
‘Sasa …..,
unaona eeh,….’akawa anasoma huo ujumbe, huku
anaongea…na akatikisa kichwa kama anakubali kitu.
‘Shemu,
mambo ya mahakama, yakianza hapa, mimi sijui itakuwa….tafadhali ndugu zanguni,
mimi inaniuma sana, mimi sasa ndiye baba yake, nitaulizwa kwa hili,….mnielewe jamani, shemeji hebu mwambie huyu ndugu yako...’akasema
akimwangalia shemeji yake
‘Tafadhali…’shemeji
akaanza kuongea, nikaona nikimpa muda huo naye ataungana na shemeji yake mimi
nikasema;
‘Sasa
kwani tatizo lipo wapi hapa, kwanini unaogopa
hayo maswalii yangu, mbona unakuja juu
kama unajihami, una wasiwasi gani, je mimi kwa kuulizana hayo maswali tutakuwa
tumekiuka hiyo miiko…ina maana hiyo miiko inasema tusiulizane maswali, tusitake
kujua ukweli, kama ni hivyo basi kuna kitu kingine zaidi ya hicho, mimi
nimeshamuomba mungu, mizimu imeondoka, haya tuendele…’nikasema
Kabla hatujaanza kuongea mara tukasikia sauti
ya ukelele kutoka ndani…sasa ni yule mkubwa, alikuwa kalala ndani, mara
akatoka, akiwa katoa jicho, ….la kuashiria anaogopa
‘Ni nini
na wewe..?’ akauliza mama yake
‘Simba….mama,
simba anataka kunitafuna….’akasema akionyesha ndani,…mimi nikawa nimetulia huku
namtupia jicho la kujiiba huyo jamaa, ambaye alionyesha na yeye uso wa
kushangaa,…kiukweli huwezi kumshuku lolote, kama anaigiza basi huyu jamaa ni
mtaalamu.
‘Hakuna
simba wewe ulikuwa unaota tu..’akasema mama mtu lakini usoni alionekana kuwa na
uso wa mashaka.
‘Hebu
nikaangalie huko ndani mimi mwenyewe, tusije kusema hakuna , kumbe kweli kuna
kitu…’akasema huyo baba mtu akitembea kuelekea huko ndani, alipokuwa kalala
huyo mtoto, baadae akarudi…akasema
‘Hakuna
kitu, hizo ni ndoto, lakini ndoto kama hizo, kaulizie, hayo ni mashetani…hebu
kijana wangu usiogope, hakuna simba, niambie vizuri, wewe uliota nini…?’ akawa
kachuchumaa akiongea na huyo mtoto.
‘Sijaota,
nimemuona simba huko ndani…alitokea mlangoni, akawa anakuja pale nilipolala
kitandani, nimemuona kwa macho yangu,..sijaota mimi..’akasema
‘Yupoje
huyo simba…?’ akamuuliza
‘Mkubwa
kama ng’ombe, ana meno ya kutisha…’akasema
‘Unaona..haya
haya….aliyasema huyo yule mtaalamu, hao..sasa ni mashetani…ni lazima yaje kwa
mbinu hizo, …maana hatutaki kuwatii mizimu…unajua nikuambie kitu ndugu yangu,
mizimu wao wanatupenda, ..na mara nyingi wanapambana na hayo mashetani, sasa
tusipokuwa upande wao, na wao wanayaachia hayo madude yapambane na sisi, ili
tujifunze…’akasema
‘Mashetani
sio..ndio ndio hao hao mizimu umekubali wewe
mwenyewe sasa…’nikasema
‘Nimeshakuambia
kuna mashetani na mizimu…mashetani ndio hao wabaya, wanataka kuumiza, lakini
mizimu wanasaidia, wanapambana na hao mashetani,..mizimu wao wanatusaidia
kutukumbushia…’akasema.
‘Kwa
kumtesa mtoto..au ni watu wanatumia mbinu hizo, kumtesa mtoto, ili mama yake
aogope, na kukubaliana na matakwa yenu…’nikasema, nilikuwa napoteza muda, maana
kuna jambo muhimu nilikuwa nalisubiria, na sikutaka huyu jamaa aondoke.
‘Chunga
kauli yako ndugu, mizimu wanakuwa mwilini kwa nia ya kukumbushia tu, maana deni
ni lazima lilipwe, halina ujanja wa kukwepa…’akasema akinionyeshea kidole.
Kukawa na
ukimia kidogo,halafu mimi nikasema;
‘Ndio tuendelee…sasa, kuna taarifa
nazisubiria, mimi ninataka wewe, na huyo mtaalamu wako, muwe mashahidi
mahakamani, muyaelezee hayo maneno mahakamani, ili tujirizishe kuwa kweli
hamjapanga hizo mbinu…’nikasema
‘Mimi
sikuelewi, hebu niambie kwanini unarudia rudia hayo maneno, una uhakika gani na
hicho unachokisema, maana hiyo sio kauli nzuri, nani kapanga hayo, mimi najua
kuzungumza na mizimu…?’ akaniuliza akigeuka kidogo kumwangalia mtoto, au
shemeji, halafu akageuka kuniangalia mimi lakini kwa jicho la pembeni.
‘Wewe unajifanya hujui….unajifanya hujui ni
kitu gani kinachoendelea kwa huyu mtoto, na kwanini yeye atumiwe kwenye shinikizo
la hilo deni,, yeye kama mtoto…hajui kabisa kinachoendelea..’nikasema
nikimkimuangalia moja kwamoja usoni, nia yangu ni kumchanganya kichwa,
akasirike. Mtu akikasirika huropoka ovyo…
Ilikuwa
kama nimemmwagia maji, akataka kusema kitu, lakini kikawa hakitoki, akatikisa
kichwa, halafu akasema;
‘Unajua
mimi nilikuheshimu sana, nilikuona ni mtu wa maana, sasa sijui nikuite nani,
nimejaribu kukulezea kwa busara, lakini wewe hutaki kunielewa, na sasa unataka shari
na mimi, unajua wewe hunifahamu mimi nilivyo, mimi ni mtu mpole sana, nina
tabia ya subira lakini ikija kunitoka, hutaamini,….’akasema akitikisa kichwa.
‘Nakufahamu
sana, wewe ni dalali, na mbinu zako za udalali zinajulikana, ukitaka kitu ni
lazima ukipate, si ndio hivyo ulivyo…, kwa njia yoyote ile utakipata, umekuwa
ukisema maneno hayo, kweli si kweli..?’nikasema.
‘Ni nani
kakuambia hayo, ni kweli ndivyo nilivyo, lakini sio kwa dhuluma, halafu dhuluma
kwa familia yangu, jipange vingine ndugu yangu…’akasema
‘Nitakuja
kulithibitisha hilo, kuwa wewe una tabia hiyo ndio maana ulikwenda kwa huyo
mtaalamu..’nikasema
‘Shemeji
huyu mtu ni nani kwako…..?’ akauliza
‘Unataka
kujua mimi ni nani eeh…?’ nikamuuliza, nikawa kama najipapasa hivi, akawa
ananiangalia,..nikajifanya kama nimekumbuka, nikasogea pale nilipoweka simu,
nikaichukua, nikawa naangalia kama simu bado inauwezo wa kupokea hayo
mazuungumzo, ilikuwa imesimama, nikaiweka sawa.
Kabla ya hapo, nikapiga namba ya askari mmoja
ninayemfahamu, nikaongea
‘Upo kituoni…mimi
ni afande wako..hahaha, hii namba ngeni ndio, ile ya mwanzo nimeiacha, kabisa, ni lazima..sasa..’nikasema
‘Nataka
unisaidie jambo dogo, unaweza kuja na gari, kuna yule mtu niliyekuwa
nikikuambia, ninaye hapa…’nikasema, na kutulia
‘Ndio
nataka twende naye hadi huko kwa mtaalamu wake, maana anawatesa sana hawa
watoto..’nikasema
Jamaa
sasa akawa ananiangalia kwa mashaka. Na
wakati huo huo, nilimuona mama mjane akihangaika na mtoto, nikamtupia macho,
..na mara mama huyo akasema;
‘Jamani
mimi nimechoka na haya mambo, mtoto anaumwa, na keshaanza kuwa baridi sehemu ya
miguuni, japokuwa usoni kuna joto sana..miguu utafikiri haina uhai,…jamani,
mtoyo wangu jamani, hii sio kawaida…’akasema mjane
‘Mimi
nilishasema, sina namna ya kufanya kama hali ya mtoto ikijirudia, kama homa
ikimpanda tena, dawa tuliyopewa haiwezi tena kufanya kazi,…. hiyo ni kutokana na mtaalamu alivyosema,…mimi kwa
hivi sasa siwezi kufanya chochote ni miiko niliyopewa, ile dawa haitakiwi tena
kutumika,…’jamaa akasema na hapo ndio akazidi kumchanga mama mjane
Mtoto
alikuwa kalegea, ilionyesha kabisa pale mama alipompakata yule mtoto shingo
kama sio yake, kalegea kupitiliza
‘Jamani
mwanangu imekuwaje…’akasema huyo mama, na mimi kwa haraka nikasogea, sasa
kumshika mtoto yule mtoto, sasa sio joto tena, mtoto keshakuwa mkavu, kakauka
kabisa,..macho kayatoa
‘Mungu
wangu..’mimi nikajikuta nimesema hivyo
‘Mumeona
eeh,mimi niliwaambia..’akasema jamaa
Mama naye
kuona vile, akadondoka….akapoteza fahamu…
NB: Imebidi
sehemu hii nikatishe hivyo
WAZO LA LEO: Binadamu tumefikia hatua ya
kuthamini mali zaidi ya utu wa mtu, watu wengine wapo tayari hata kuwafanya
watoto wao mazezeta, ili tu watajirike, wengine, wanaua kabisa,..tujiulize hizo
mali zitatufanya tushi milele, ..haiwezekani, kila nafsi ni lazima ije kuonja
umauti na mwisho wa yote ni hukumu, ambapo kila ulichokifanya hapa duniani
utakuja kuhukumiwa nacho…..wengine mateso yao wanaanzia kuyapatia hapa hapa
duniani, je hatujawahi kuyaona hayo?
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment