Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, June 13, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-11


‘….Mimi nikaona hakuna jinsi, mimi ni baba yake…nikaanza kazi ya kuulizia,maana hao watu wapo wengi, na wengine hawaaminiki…nikhangaika wee, ndio nikampata mtaalamu hasa kwa msaada wa mzee, mmoja,….’akatulia.

‘Usione hivi bro….tumehangaika na huyu mtoto….wewe unakuja na….lakini ndio hivyo, kama hayajakukuta huwezi kuamini…’akatulia.

Nikataka kuuliza swali, akaniashiria kwa mkono nitulia…

‘Sasa sikiliza…..tulipofika huko…ubosi ukanitoka, si unajua tena mambo ya huko, yalivyo, kuna msharti sharti,  la la kukokotezwa… ukifika huko utajionea mwenyewe, … ningelifanya nini tena, unavua viatu, unakalishwa chini…unajua tena, ningelifanya nini na mimi ndio baba wa mtoto eeh, na ndugu yake shemeji alijionea, ndio tukaanza kuambiwa ni nini tatizo la mtoto….’akatulia

‘Mliambiwa tatizo ni nini….?” Nikauliza na yeye akatikisa kichwa na akawa kama anacheka

‘Tatizo kubwa ni deni….’akahema kwa nguvu.

‘Deni…?’ nikauliza.

‘Marehemu aliacha deni, huko alipo hana amani, anateseka, kwahiyo yeye anataka deni  hilo lilipwe…’akatulia.

‘Deni alikopa kwa nani labda…?’ nikauliza na hapo akageuka huku na huku kama vile nauliza maswali yasiyo na maana.

‘Hivi,…hapo kuna haja gani ya kuuuliza…hebu nikuulize watu wanapokwenda kuzika, kwanini kwanza wanaanza kuuliza kamamarehemu alikuwa na deni…?’ akaniuliza.

‘Ni kawaida, maana huyo marehemu hataonekana tena, ..na kidini inashauriwa hivyo…’nikasema.

‘Umeona eeh,…sasa kuna haja gani ya kuwa na shaka hapo…na …huko kuuliza uliza, ..ndio kulipelekea hadi kuanzsha kesi, hebu tujiulize kesi hiyo ni dhidi ya nani eeh…inasikitisha, tunamshitaki marehemu kuwa katuachia deni….’akasema na alimuona shemeji yake kama anataka kuongea akamuashiria akae kimia.

‘Na…, na kingine yeye hataki mambo ya kesi kesi…hata akiwa hai, yeye alikuwa hapendi kesi na kweli , muulize hata shemeji, yeye anamfahamu zaidi, sasa kwanini sasa hayupo duniani,..tunaanza kukiuka masharti yake,i….lakini cha muhimu ni kuwa…hilo deni lilipwe kwanza, sasa kama kutakuwa na jingine la kutuhusu sisi wa duniani, haya, lakini kwanza deni li-li-pwe..’akatulia

‘Ni nani anasema hivyo…?’ nikauliza.

‘Nani anasema hivyo!!! Swali gani hilo…ok, ok, nimekuelewa,…anayetuambia hayo, ni kutoka kwenye kinywa cha huyo mtaalamu, lakini kwa muda huo tunasikia sauti ya marehemu kaka…’akasema

‘Kwa vipi …?’ nikauliza

‘Kwa muda huo, yeye, ..huyo mtaalamu, alikuwa kapandisha…’akasema

‘Kapandisha nini…?’ nikauliza

‘Mhh..jamani, huyu mtu ni wa wapi….kapandisha mashetani… na sauti tunayosikia kwa muda huo ni sauti ya marehemu kaka, ….’ooh, waungwana, nawaambia nimeondoka duniani nikaacha deni, hilo deni linanitesa huku nilipo…fanyeni kila mbinu hilo deni lilipwe haraka iwezekanavyo, hata kutoka katika mali yangu,..msichelewe, ….’  Akawa anaigiza sauti nyingine.

‘Mimi pale sikujivunga, maana nitadanganya, nitapatia wapi hizo pesa zote…nikasema hatuna  hizopesa tufanyeje, …deni hilo ni kubwa sana, …sauti ikasema;
 ‘hata kama ni nyumba  iliyokuwa yangu, na iuzwe ili deni lilipwe haraka,….vinginevyo,…’hapo akasita halafu akasema

‘Sauti ikasema , ikatoa onyo kuwa hilo deni lisipolipwa haraka, … mmoja baada ya mmoja ataondoka…kwa mateso ya ajabu,…..’akatulia akimuangalia shemeji yake.

‘Hiyo ilikuwa lini,…?’ nikauliza huku naangalia saa maana nilitakiwa kukutana na watu wangu, kuna jambo walitakiwa waniambie.

‘Lini kwa vipi….?’ Akaniuliza na yeye akiangalia saa yake

‘Yaani  ni muda gani tangia hilo tatizo la mtoto lianze?’ nikauliza

‘Mhh, eti shemeji, nisaidie hapo…hivi, mtoto alianza hayo matatizo lini,maana sikumbuki, mambo yamekuwa mengi, mara yeye ….unajua hata kuumwa kwa shemeji, kumbe mambo ni hayohayo, hatukujua, yalianzia kwake…..shemeji hali yake ilikuwa mbaya sana,..sasa kidogo unamuona hivyo , tena sio kidogo, unaona anatembea sema ….yupo imara kiimani, …..muulize mwenyewe ilikuwaje…’akasema.

‘Unasema yeye yupo imara kiimani, au sio…?’ nikauliza, na hapo akaniangalia kwanza usoni, halafu akasema.

‘Yah…’akasema hivyo

‘Ok,…sasa mimi nauliza kuhusu huyu mtoto kuanza kuumwa ilianza lini,…..?’ nikauliza huku naangalia simu pale mezani niliona kama imezima..lakini mara nikaona ishara kuwa bado inafanya kazi.

‘Tuseme eeeh…mimi nafikiri, hata mwaka haujaisha, ni karibuni tu, yalipoibuka haya maswala ya kesi kesi au sio shemeji.. ….?’akasema akimuangalia shemeji yake. Shemeji yake alikuwa kimia alikuwa kama hayupo, alionekana kazama kwenye mawazo.
Mjamaa akaendelea kuongea…

‘Yalipoibuka hayo maswala ya benki au sio,shemeji …?’ akauliza tena, na shemeji yake bado akabakia kimia, na yeye akaendelea kuongea

‘Tulipoanza kufahamu kuwa kuna deni, na wanaodai walipoanza kufuatilia,…na kwa vile kwa mujibu wa mkataba wao, marehemu alipoingia kwenye mkopo, yeye aliweka dhamana ya nyumba, unajua kaka angelikuwepo, hilo deni sio kitu kwake, angelilipa kwa jinsi alivyokuwa kajipangia mwenyewe…’akasema

‘Umejuaje hayo…?’ nikauliza.

‘Utakopaje bila kuwa na mpangilio…?’ akaniuliza.

‘Sasa ni hivi, …mtoto yeye alianza kuumwa, nakumbuka, ni pale …si ndio hivyo shemeji, ..pale tulipoanza kufuatilia,..na baadae ndio tukasikia, benki wanataka kupiga mnada nyumba…au sio shemeji.

‘Unajua sio kitu rahisi kukubali au sio…kwa jinsi tunavymfahamu kaka,alikuwa sio mtu wa kukopa kopa,..sasa ..tunasikia kuna deni, hatukuamini, tukaanza kufuatilia, polisi, benki, unaona, lakini tulikwama…vielelezo vipo, ushahidi upo, bado tukawa wagumu,….sasa hapo mizimu ikaibuka,…’akasema

‘Iliibuka kwa vile dili inataka kufichuliwa, au sio…?’ nikauliza

‘Unataka kusema nini hapo, sijakuelewa….?’ Akauliza akiniangalia usoni, niliona hali ya mashaka i machoni mwake.

‘Unasema huko kwa mganga ulikwenda na  ndugu yake shemeji, ni nani huyo.?’ nikauliza kama vile nawafahamu hao ndugu zake shemeji yake wakati hakuna hata mmoja ninayemfahamu lengo nikimuweka huyu  jamaa sawa asinishutukie mapema.

‘Kuna ndugu yake mmoja, …nimekuambia ni mkubwa wake shemeji,…shemeji, hebu mwambie ni nani yule..,…maana sasa naona nimechoka kuongea, tatizo unauliza maswali kama polisi, hao polisi wenyewe walinisumbua wee mwishowe wakasalimu amri….’akatulia

‘Si ninataka na mimi nifahamu au kuna ubaya, ndugu akitaka kufahamu matatizo ya ndugu yake kuna ubaya, au wewe una wasiwasi gani…?’ nikamuuliza

‘Wasiwasi, aah, wanini sasa, mimi ni baba wa hawa..mimi ndiye msimamizi, ..mimi ni …nimechaguliwa na familia, kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa, ni lazima niwajibike, ni lazima niwe…na shaka na watu wanaotaka..kuleta matatizo,..unasikia….’akasema

‘Unasema polisi walikuuliza maswali…’kabla sijamaliza akaendelea kuongea kwa kunukatiza

‘Ndio..Polisi waliniuliza maswali weeeh.., utafikiri mimini mhalifu, hawajui kuwa mimi ni mzazi wa hawa watoto, nina uchungu zaidi ya wao wanavyofikiria …’akatulia.

‘Sasa ndio nikakuuliza huyu ndugu wa shemeji mliyeenda naye ni nani…?’ nikauliza

‘Wewe unauliza kuhusu huyo ndugu yake shemeji, …huyo ndugu yake shemeji tulikuwa naye hapa, alikuwa akiishi na shemeji,..na yeye angelikuwepo angelikuwa ni shahidi yangu, kwa hayo yaliyosemwa huko kwa mtaalamu, yeye aliona kila kitu…na ili kuhakikisha kuwa huyo mtaalamu ni mkweli, mbona tulipofuatilia wanavyotaka wao hali ikawa nzuri,… muulize hata huyu  shemeji mwenyewe , mtoto akawa na afya yake nzuri tu, sasa nahisi kaanza tena, keshasahau…’akasema

‘Ninachojiuliza ni kwanini hayo yatokee kipindi hicho,  kipindi hiki yaani… kwanini hayakutokea huko nyuma, kwasababu  ….mume wa dada alifariki muda, au sio..sikubahatika kufika hapa…, lakini ni muda sasa, kwanini hayo matatizo yakudai kuwa ana deni, hayakutokea kipindi  cha nyuma baada ya mume wa dada kuondoka, kwanini yaje kutokea wakati shemu anatafuta ukweli…?’ nikauliza

‘Mhh….kwanini, kwanini…unataka mimi nijibu au sio…?’ akauliza

‘Mimi najiuliza,…lakini wewe unaweza kujibu,…si kumepita muda,..mtu kafariki, ukapita muda…baadae deni likagundulikana, …watu wakaanza kufuatilia, ndio mtoto anaanza kuumwa, au sio…ndio  nauliza hapo huyo, mtaalamu alisema nini, au wewe unasemaje?’ nikauliza

‘Sasa hayo mimi sijui….kamuulize huyo shetani anayemtokea huyo mtoto, ukiniuliza mimi…nitakuambia nini, … nitajuaje hayo ni kwanini, marehemu huko anajua ni kwanini,huenda katika kuhojiwa ndio ilikuwa imefikia muda muafaka wa hilo swali, …’akasema

‘Kwahiyo huyo anayemtokea huyo mtoto ni shetani..?’ nikauliza

‘Sasa utamuitaje,….eeh, hebu niambie wewe,….’akasema akiniangalia, halafu akasema;

‘Na ujue , haya mambo ni ya ajabu sana, unajua  marehemu anaweza kujitokeza kwa njia yoyote ile ili kuleta ujumbe wake…unaweza ukamuota kwenye ndoto, hiyo ni ahueni…na  huko kwenye ndoto unaweza kuonana na marehemu mkaongea, lakini kiuhalisia, hawezi kujitokeza mwenyewe,  si unajua hilo, maana akijitokeza mwenyewe…ooh,  si tutakimba, kwahiyo yeye kaamua kujitokeza kwa kupita kwa mtoto wake yeye mwenyewe...’akasema

‘Huyo Shetani sio,….?’ Nikauliza

‘Eeeh bwana, ….hunielewi…na sauti tuliyoisikia ni ile ile ya kaka, mimi naijua vyema sauti ya kaka, mimi si ndugu yake, ..hata yule ndugu yake shemeji, alithibitisha hilo …’akasema.

‘Lakini si umesema ni shetani, au nimekosea, kinachomtokea mtoto ni kama mashetani, ulisema hivyo, au sio....na nijuavyo mimi, shetani huwa hashauri  mambo mema au sio, anaweza kushauri mambo mkayaona mema kumbe yana mtego ndani yake…, yana ajenda ya siri….mtaona mnafaidikika lakini baadae huyo sheteni anawageuka, au sio.?’ Nikamuuliza

Kwanza alibakia kimia baadae akasema;.

‘Inategemea na aina ya shetani kuna….kuna, hayo madudu yanakuwa mazuri, yanakuja kwa nia njema tu..,…mizimu ya mababu ni ..wahenga wetu wema,…unielewe hapo, hivi nikuulize mababu zetu walikuwa watu wabaya…?’ akauliza

‘Mababu au mizimu…?’ nikamuuliza

‘Ndio hao hao..ukishafariki, wewe sio babu, au baba..si ndio hivyo, wewe ni maiti, na ukitutokea, utakuwa ni mzimu, au sio…mimi naona ili unielewe vyema, ngoja tusitumie neno shetani, unakuwa huelewi,….ni mizimu, yenye nia njema , inawezekana pia mizimu ikawa na nia mbaya mimi sijui..lakini utaangalia kisa cha tatizo lako,…eeh, sasa kwa hili ni deni, na kawaida ya deni ni kulipwa au sio....’akasema

‘Nikuulize kitu kwanza ili tuwekane sawa, naona unabadili maelezo yako ya awali kuhusu shetani, …’nikasema

‘Sio nabadili, nataka wewe uelewe, ..wewe si hujaelewa au sio..’akasema

‘Mimi nauliza hivi, ni wapi wamesema hivyo, shetani, ni wabaya, mizimu ni wazuri,…maana kwa vyovyote utakavyowaita ni hao hao, mizimi, vibwengo, hao wote ni mashetani, nijuavyo mimi…’nikasema

‘Aaah..wewe, mizimu, sio mashetani…’akasema kwa sauti ya taratibu kama kuogopa

‘Ndio  nijuavyo mimi, kwenye vitabu vya dini shetani ni muasi,shetani aliasi , alikataa amri ya mungu ndio akaamua kutupoteza na sisi wanadamu, au sio….sasa iweje tukubali maagizo yake, na yeye alivyo ana mbinu nyingi, anaweza kutumia mbinu kadha wa kadhaa, leo hii yupo kishetani , kesho kibwengo, mara mizimu..si ndio huyo huyo, au…?’ nikamuuliza na maelezo juu.

‘Sasa huko unapokwenda, aah,…. mimi sio mtaalamu nako, sina ufahamu huo ….mimi nafuatilia aliyosema huyo mtaalamu…yeye anajua yote,….yeye hiyo ni fani yake, na kuhusu kusoma dini, huyo mtaalamu kasoma dini, sio mchezo…’akatulia

‘Umejuaje kuwa kasoma dini….anaweza kusoma dini, lakini akatumia ufahamu wake, kughilibu watu, ili kupata tonge tumboni, …’nikasema

‘Wewe…anglikusikia,…sikia…huyo ..eeh, , dini anajua sana…, alituchambulia maandiko  wenyewe tukaduwaa, kwahiyo sio kwamba hajui dini, anaijua vyema na hata wewe ukienda ukamsikiliza utajua kuwa kweli anafahamu yote, …au nikupeleke kwake, ukamsikie yeye mwenyewe, kama hutaamini…….’akasema

‘Huyo mtaalamu unamuamini vipi…maana mtu na biashara zake bwana, ni lazima atajua jinsi gani ya kumteka mteja wake akili, si anataka kuvutia wateja wako…., sasa wewe ulimuaminije, unamfahamu vipi,…najua wewe ni dalali, unajua hayo au sio?’ nikamuuliza na nilipotaja neno udalali, nikaona anashtuka! Nilishamkumbuka huyu jamaa pamoja na kazi nyingine pia anafanya kazi ya udalali.

‘Hayo maswali gani sasa,….’akawa kama anataka kusimama, akageuka kumuangalia shemeji yake, halafu akasema

‘Unasikia, sisi tulichotaka ni mtoto kupona…unaona ndugu, hayo ya udalali yanakujaje hapa, hizo ni fani za watu kama udakitari nakadhalika au sio…’akasema

‘Kwani nimeukashifu udalali hapo…?’ nikauliza

‘Sikiliza ndugu,…sisi tulihangaikia mtoto, na katika kuulizia tukaambiwa kuhusu huyo mtaalamu, ndio tukaenda kwake,…ndio hapo na mimi nikamfahamu, ina maana mimi nilifanya makosa,, kwa vile mimi ni dalali, au una lako jingine, na kwanini unachunguza chunguza, …ili iweje,…hebu niambie unataka nini…unanishuku au….?’akasema sasa akionyesha kubadilika.

‘Hapana, …sina nia mbaya na wewe …najua wewe ni mzazi wa huyu mtoto na ulitakiwa kuhangaika sana, nashukuru kwa hilo, maana hata kwa jinsi ulivyoweza kumtibia huyu mtoto hapa, ooh, nimekuaminia…sasa mimi nataka unielewe,….hili tukio kwakweli limenigusa sana, ndio maana nataka kujua hatua kwa hatua, ili nisije kuhangaika na mimi, wakati wewe ulishafanya jitihada, au sio….’nikasema kumweka sawa.

‘Ndugu ..unajua nyie watu mnaojifanya wazungu , au nisema wa kileo, nikiwemo mimi, usinione hivi, mimi mpaka kufika huko, ooh, sio fani yangu mimi, mimi ni mtu wa kileo…lakini pia mimi nina hekima zangu, naishi na kila mtu, najibadili kutegemeana na mazingira..nyie ambao mnajifanya wasomi, manfikia wakati,…eeh ….mnasahau mambo ya kimila, wazee wetu hawakuwahi kwenda shule kipindi hicho, walikuwa wanajitibiaje…?’ akawa kama ananiuliza hakusubiria nijibu akasema

‘Wazee wetu, walikuwa wanajuaje matatizo yao, ni kwa njia hizo, tunazozipuuza ….kulikuwa hakuna hospitali, hospitali  kwa wazee wetu ilikuwa ni kwenda kwa hao wataalamu, waganga wa kienyeji,…na wao dawa zao zaidi ni miti shamba,…’akatulia akiniangalia kama namfuatilia

‘Unasikia sana..eh,…na ni lazima kuwe  masharti fulani fulani, uyatimize, au uyafuate, au sio….na zaidi walikuwa wakifuata mizimu na mambo yao yalikwenda vyema , hebu angalia hivi sasa  na usasa wetu…., mambo yanakuwa  magumu,maisha ni magumu….sababu ni haya  maswala ya kupuuza mambo ya kimila au sio..’akasema sasa akiongea kwa utaratibu.

‘Kwahiyo wewe kwa hivi sasa unafuata mambo ya mila, unaabudu mizimu, na naona umekuwa mtaalamu na wewe pia au sio?’ nikamuuliza

‘Sijasema mimi nafuata mambo hayo, wala sijasema mimi naabudu mizimu, lakini mambo yakizidi inabidi kufuatilia, na sio kuabudu, usinishirikishe kw nguvu…’akasema akinitolea macho, halafu akatabasamu kwa dharau, akasema

‘Sasa…mimi , sisi, yalipotufika shingoni..ndio tukafuatilia,…na katika kufuatilia ndio nikajifunza kuwa kumbe haya mambo  yapo,…sio ya kuupuzia,… maana huyu sio wa kwanza kwenye familia yetu kuna ndugu wanapandisha hayo mapepo, ….tulihangaika sana, tulipofuatilia tukaambiwa tulikiuka miiko,…mila fulani fulani hivi, za ..unanielewa lakini…… tukafanya walivyotaka hao mizimu…’akatulia

‘Kwa huyo huyo mtaalamu…?’ nikamuuliza

‘Hapana alikuwa mwingine…huko kijijini kwetu…’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine akaendelea kuongea

‘Na mizimu ni mababu na mababu zetu uelewe hilo, usipinge ndugu, utaingia matatani, na kiukweli….ndiyo haya yanamsumbua mtoto, …’akatulia

‘Lakini baba yake hakuwa mababu, au sio…?’ nikauliza

‘Hebu bwana uelewe…usitake kuniuliza, kwa kunichezea shere,…..baba yake alishafariki, huwezi kumweka kwenye hali kaam hii ya kiduniani, yeye anakuwa …hivyo hivyo, kama hao mababu…lakini hebu kwanza, hivi kama deni lipo, limeachwa na marehemu dawa yake ni nini, eeh, kama anayedai anahitajia pesa yake,…’akaniangalia,

‘Nikuulize wewe…’nikasema

‘Deni kama lipo, na kila kitu kipo wazi…sisi tuliopo duniani, hatuna ujanja, kama warithi wapo, kama vielelezo vipo,….na..unajua sisi tulihangaika kuhakiki hilo deni,…, ni kweli kuna deni, kaliacha kaka, na deni hata kidini latakiwa kulipwa hata kabla marehemu hajazikwa, sasa sisi hatukuljua hilo deni , hatuwezi kulaumiwa, tumekuja kulifahamu baadae,…ndio maana hata mimi niliposikia hivyo nikaamua kufuatilia..’akasema

‘Wewe ulipojaribu kufuatilia kulitokea nini kwa watoto wako…au ….maana si hivyo, ulikiuka miiko,au sio… kwa muda huo…ni kitambo eti.., sawa si sawa, kwanini kusitokee kitu kama hicho muda huo,..maana na wewe linakugusa, au niambia kuna mtoto wako naye alipata matatizo kama haya,…?’ nikauliza na yeye akatikisa kichwa kama kusikitika.

‘Unajua wewe hunielewi….na nimekumbia maswali mengine yapo juu ya uwezo wangu, ni kwanini, hayakutokea muda huo eeh, sijui nini, kwanin haikutokea kwa mtoto wangu, kwani hawa watoto ni wa nani, usitake kunibagulisha hapa, na maswali kama hayo, yapo juu ya uwezo wangu…, mimi siwezi kujua….mimi sina ujuzi huo, labda turudi kwa huyo mtaalamu tukamuulize…’akasema

‘Ok…,ok…naona muda unakwenda, …kwahiyo wewe unajua jinsi gani  ya kumfanya huyu mtoto apone… hiyo hali ikitokea, kama ulivyofanya hapa kwa mtoto, kwanini hukumfundisha shemeji ili ikitokea na yeye afanye hivyo..?’ nikamuuliza

‘Mbona nilishamfundisha, tatizo, shemeji haamini sana hayo mambo..lakini ni kwa manufaa ya nani, eeh,..je kuna raha gani mtoto akiteseka, eeh…sio kweli kuwa  ni mimi tu naweza kufanya hivyo, yeye pia anawezi, japokuwa kuna ya zaidi, yeye kama yeye hawezi …kuna miiko hapo, sasa siwezi kukuambia zaidi hayo ukitaka utaambiwa na huyo mtaalamu , nafuata alichotuambia, ….’akasema

‘Unapozungumzia miiko, ni miiko ya kivipi, …kwenye kutibia, au, maana mfano haupo mtoto kazidiwa, sisi tungelifanya nini, …?’ nikauliza

‘Huyu mtaalamu alinielekeza, kuwa hali hiyo ikitokea, na….haitokei mpaka mtu akifanya yale yasiyotakiwa, yaani  akikiuka miiko,..na nikuambie ukweli, pindi hilo deni likilipwa, hakutatokea tena kitu kama hicho, tatizo hapa ni hilo deni, ndivyo alivyosema huyo mtaalamu…kwahiyo mimi silali, nahangaika huku na kule kuhakikisha hilo deni limelipwa…na hakuna njia nyingine maana hiyo pesa ni nyingi sana…’akasema

‘Ok, sasa..ngoja, tuzipoteze muda, mimi nakuuliza swali la msingi, …unisikie, eeh,…je, wewe kwa uhakika wako, unakubali kweli kuwa, …kwa uhakika …useme kutoka moyoni, maana msije kukimbilia deni tu…ni lazima pia kujirizisha moyo, je wewe una uhakika kuwa kweli marehemu alicha hilo deni…?’ nikamuuliza sasa nikimuangalia kwa uso wa kutaka kauli yake ya kwanza.

Jamaa kwanza akatikisa kichwa, kama kusikitika, halafu akageuka kumuangalia shemeji yake, huku akionyesha mikono,ya …kama kupotezewa muda, au….halafu akaniangalia usoni kaweka tabasamu la kujilazimisha, akasema…

‘Hivi unajua mimi ni nani, kwa hii familia…?’ akaanza kuuliza

‘Nijibu swali kwanza, …wewe ni dalali, una uzoefu wa kujibu maswali au sio..lakini pamoja na hayo, nataka unijibu kutoka moyoni, mungu anakuona….unataka nirudie swali…?’ nikamuuliza

NB: Kisa kinaendelea, tuombe mungu tukimalize kabla hatujafungiwa, maana nimeambiwa ni lazima nijisajili….ili blog yangu itambuliwe…kwanza utoe laki moja pesa ya kuombea, halafu milioni, ada….kazi kweli kweli!! 

https://www.tcra.go.tz/images/headlines/FAQ-_Online_Registration.pdf


WAZO LA LEO: Hekima, na busara katika kuelimisha jamii, haitakiwi iwe biashara, hekima haiuzwi au kununuliwa, hekima ni neema kutoka kwa mola wetu, tusifikie mahali tukaanza kuifanyia biashara. Jamii ilivyo, huwa inakwenda kutegemeana na nyakati., na tusipokuwa makini, jamii inaweza ikaiga kila kitu kutegemeana na nyakati hizo,hata yale yanayoumiza, yapo mambo yanaumiza, hasa wanyonge, ili kupambana na uumizwaji huyo, ukandamizwaji huo, hekima na busara za watu zinahitajika, ili kuweka mambo yaendane sawa jamii ijijue wapo imekosea, na wapi iende…. Je ni nani wa kuelemisha, ni nani wa kuionya jamii,…waandishi nao wao wana nafasi yao kubwa tu, kwa hili….lakini je ikiwa uandishi, kutoa maadili, kunagharimishwa, je jamii itakuwaje..kila kitu sasa malipo..hata hekima jamani..? Ni wazo langu tu.

Ni mimi: emu-three

No comments :