Niliwasiliana na mdogo wa mume wa familia;
‘Vipi umepewa ujumbe wowote na kaka yako..?’ nikamuuliza,
nikasikia kama mngurumo wa gari kuonyesha kuwa yupo kwenye gari
‘Kaka ameshanipa ufunguo tayari, na hapa ndio nipo njiani, kwenda
kuuchukua huo mzigo, … lakini kwanini
mnafanya hivyo, hamuoni kuwa ni hatari, je shemeji akigundua…mimi naogopa sana
haya mambo yenu…’akasema akionyesha kuwa na wasiwasi.
‘Usijali, ni mambo ya kawaida, hayo ni kwa ajili ya kaka yako,
sasa hivi hali ilivyo ni lazima tufane jambo, vinginevyo, ..sasa, unasikia, fanya
hivyo, ukiwa tayari niambie, unasikia, sikiliza kwanza….’nikamuelekeza jinsi ya
kufanya.
‘Sawa nimekuelewa…’akasema
Kilichokuwa kimefanyika ni
namna ya kuhakikisha kuwa mke wa familia hayupo nyumbani, na acheleweshwe
kinamna ili kila jambo likamilike kwa wakati,
kwani mke wa familia hakuwa anafahamu ni nini kinachoendelea. Kazi hiyo
ilibakia mikononi mwa mume wake,…
Je ilifanyikaje…nahisi
nyote mtapenda kusikia sehemu hiyo,…ukumbuke haya yanafanyika muda ambao mke wa
familia anatarajia kurudi nyumbani.
*********
Mume wa familia aliigiza kuzidiwa…si
nilishaambia huyu mtu kuna hali ilitakiwa aigize kuumwa zaidi ya anavyoumwa,
hapa sasa uone ushahidi.
‘Docta najisikia vibaya sana..sizani kama nitapona…’mgonjwa huyo
‘Utapona tu usiwe na wasiwasi ni dawa hizo…unasikia, wewe lala na
tulia..’docta akasema.
‘Hapana docta, oh… kwa hii hali naomba umuite tu mke wangu, nataka
kuongea naye, nahisi kukata roho…aaah.’akasema huku akigugumia maumivu.
Kutokana na matatizo yake hayo, mara nyingi kila anachohitajia
inabidi apewe ili asiwe na msongo wa mawazo, kwahiyo docta kwa haraka akachukua
simu. Kiukweli hapa docta hakufanya kutokana na maagizo, hapa alifanya kazi
yake.
‘Halloh, mimi ni docta hapa, tafadhali nakuomba ufike hospitalini
haraka iwezekanavyo,…’docta akasema
‘Kuna nini, mgonjwa kazidiwa…?’ akauliza
‘Hali kidogo imebadilika, …anataka kuongea na wewe, ni muhimu uje,
maana imekuwa ni kero,..’akasema docta
‘Kero kwa vipi docta..?’ akauliza
‘Anataka kuongea na wewe, unajua kutokana na hiyo hali na dawa
anazotumia,anakuwa kama mtu anayeweweseka-weweseka ,..ni kawaida, hata hivyo,
kila anachohitajia kwa hivi sasa, inabidi tu tumpatie, ili asiwe na msongo wa
mawazo…..’akasema docta.
‘Lakini yupo vipi…?’ akauliza mke wa huyo mgonjwa.
‘Anahis maumivu…na ni kawaida, lakini ni muhim uje…’akasema docta.
‘Sawa nakuja docta, …nipo njiani, nilikuwa naelekea nyumbani,
nakuja sasa hivi…’akasema mke wa familia.
Wakati hayo yanaendelea huku nyumbani mdogo wa mume wa familia
alikuwa anafanya kazi aliyoagizwa, ….
Zoezi likakamilika!
Kitu kingine muelewe, huyu
docta naye alishawekwa sawa na Makabrasha, kwahiyo naye kila anachoambiwa
anakubali, ila kwa siki huyo docta alijua kabisa mgonjwa kazidiwa....Makabrsha alikuwa
sio mchezo.
Silaha ikaletwa sasa kazi jinsi gani ya kuingiza humo kwenye
jengo...ukumbuek jengo hilo linalindwa na mitambo ambayo ikihisi kitu kama
silaha itapiga ukelele..kuashiria jambo..
Nilishamuelekeza mdogo mtu ni nini cha kufanya, anachotakiwa ni
kuifunga ile silaha kwenye kamba ambayo niliining’iniza kutoka rosheni ya pili,…na
taa za upande ule nilizima.
Kwahiyo mimi nilishajiandaa kwa hili, nilikuwa na kamba ndefu,
inayofika chini, ujue lile jengo lina rosheni,lakini kwa ajili ya kuiingiza
hiyo silaha ndani, nilitumia rosheni ya pili,…
Baada ya ile silaha kufungwa kwenye hiyo kamba, nikaivua hadi juu,…sasa
jinsi ya kuifikisha kwenye chumba changu, nilitumia njia zangu nyingine, sio
muhimu kuelezea hapa, cha muhimu ilikuwa kuhakikisha kuwa mitambo ya kutizama
matukio na kengele ya hatari ilikuwa imezimwa, umeona hapo.
Nilifanya hilo, na kitu kingine muhimu, kuna huyu mtoto wa
marehemu, mtoto wa kufikia, huyu ni Makabrasha wa pili, yeye pamoja na kazi
yake ya uwakili, lakini pia alikuwa mtaalamu wa mitambo hiyo,…ndio yeye alikuwa
akiisimamia, yeye anafahamu kila kitu cha baba yake.
Siku hiyo nlifanya
uchunguzi wangu nikagundua kuwa mtoto huyo wa Makabrasha hayupo kwenye jengo
maana mara nyingi yeye hufika usiku. Na alikuwa na kikao chake sehemu nyingine…lakini
atafika hapo, sijui muda gani. Huyu ndiye niliyekuwa namuogopa hata kuliko baba
yake!
Nikaichukua ile silaha na kuificha chumbani kwangu, kwani
haikutakiwa kuwa mbali na mimi ili nikiihitaji nisipate taabu, nilihakikisha
kuwa hayo yote niliyafanya kwa ujanja wa hali ya juu, mitambo imezimwa, na
hakuna mtu aliyeniona nikiyafany hayo yote..…si unajua tena mimi ni nani.
Baada ya kukamilisha hayo, nikarudi kwenye
hicho chumba, hicho chumba kinafungwa muda wote, hakuna anayeruhusiwa kuingia
zaidi ya Makabrsha mwenyewe au mtoto wake,..au kama kuna tatizo ni fundi wao
maalumu.
Nilipoona kila kitu kimezimwa, nikarudi haraka ofisini kwangu,
nikijifanya sasa kuhangaika kwanin mitambo na umeme umezima,…pamoja na hayo
sikujua jinsi gani ya kufuta matukio kwenye mtandao, maana ni lazima pale
ilipoishia itanionyesha mimi nikiingia kwenye hicho chumba.
Sasa nikiwa kwenye ofisi
yangu, najifanya kuhangaika na simu kumpigia fundi, ili aje awashe umeme,
nikijifanya sijui wapi umeme ulipozimwa,..basi akiwasha niende kule kwenye
mitambo niwashe, haya yalitakwia yafanyike kabla mtoto wa Makabrsha hajafika…
Nipo nampigia fundi,….mara mlango wangu ukagongwa, nikajua ni
Makabrasha mwenyewe, huyu ningejua jinsi gani ya kumdanganya,…nikasogea
kufungua,..mbele yangu nikakutana na yule mtu ambaye, sikutaka kukutana naye
siku hiyo….
Mungu wangu huyu kaja saa ngapi!...
************
‘Mbona sipati ishara ya mawasiliano kutoka hapa, ni nani kazima
mitambo ya usalama wa jengo, na kwanini umeme umezimika, kuna tatizo gani.. ?’
akaniuliza akionyesha wasiwasi
‘Mitambo ya usalama wa jengo, ipo wapi hiyo...aah, mimi sijui
mambo yenu na wala sijui kama imezimwa, na kwanini izimwe!?...’ nikamuuliza kwa
mshangao.
‘Na..na.umeme ndio umezimika nahis kulikuwa na shoti…mimi sijui
ndio maana nampigia fundi…’
Na yeye hapo akaniangalia kwa mashaka, halafu akageuka..
‘Huyu mtu anakwenda huko kwenye mitambo..hapo nikajua nitaumbuka.
Basi kwa haraka na mimi nikaelekea huko, kwenye chumba cha mitambo
hiyo…nilimfikia lakini hakugeuka na hakujua mimi nipo nyuma yake, namfuatilia
kwa nyuma kiujanja….Naona, mawazo yake yalikuwa kwenye hilo jambo
analilifuatilia.
Akafika na kufungua mlango, akaingia ndani, na mimi kwa haraka
nikaingia, chumba kilikuwa giza, ila kwa mngurumo wa hiyo mitambo, …sijui
kwanini iliendelea kunguruma wakati mimi nilishazima..na umeme umezima…na
kulikuwa baridi sana....hakugeuka nyuma, akawasha sehemu ambayo mimi nilizima.
‘Unaona kuna mtu alizima hii mitambo,..atakuwa ni nani huyu…nani
mwingine anayeweza kuingia humu…kama sio huyu mwanamke, na kwanini aizime..huyu
mtu nina mashaka naye…’akawa anaongea peke yake.
Halafu akaenda kwenye meza
yenye komputa na sehemu ya kuangalia kinachoendelea kwenye jengo,,…akakaa, ni
baada ya kuwasha, sasa akatoa laptop, hiyo ipo ndani ya meza, inafungiwa,
akaiwasha na kuanza kukagua kitu, akawa anaangalia ni nani aliyekaribia hicho
chumba, ni wazi kuwa ningelionekana mimi, sikuwa nafahamu jinsi gani ya
kufuta matukio ya nyuma yake.
‘Ssshiit….’akasema hivyo tu.
Kiukweli jinsi alivyowasha
ile lapotop, niliona, japokuwa kwa shida, niligundua herufu alizobonyeza
kuwasha ile komputa, ikanasa kichwani….alipohakikisha alichokitaka akatoka
kwenye kiti chake sasa…akageuka nyuma, kama kutaka kutoka nje…
Ukumbuke nipo hapo ndani na sio mbali sana na hapo alipokaa,..na
kwa hali kama ile nisingeliweza kurudi nyuma na kukimbia, angelinigundua na
hapo ingelileta picha mbaya, na tendo hilo lingelionekana kwenye mitambo,
nikatulia tu
Alipogeuka, akaniona,,,…nilitakiwa niondoke kwa haraka, lakini
ikawa sio rahisi,…alipogeuka tu, akaniona. Akashituka na kuniangalia akiwa
kakunja uso, kuashiria hasira na mshangao!.
‘Oh, wewe mtu, unakuwa kama mzimu, yaani ulikuwa ukinifuatilia
nyuma, huku nilishawaambia hatakiwi watu kuingia huku, niambie umefuata nini,
na inaonyesha wewe ndiye uliyefika huku, ...?’akasema kwa hasira.
‘Baba yako alinituma kufanya usafi sehemu zote...kwani kuna wageni
muhimu alitarajia kuwa watakuja kumtembelea...’nikasema lakini nilifahamu
kabisa kuwa kama ni usafi, huwa eneo hilo sijawahi kufika kufanya usafi na,
yeye akasema;
‘Hata kama ni usafi, toka lini ukaja kufanya usafi eneo hili,
wakati mimi sipo, haiwezekani, na hata kama ulifanya usafi kwanini ukazima
mtambo mkubwa, ?’ akaniuliza kwa mashaka.
‘Mtambo mkubwa!!! Ndio mtambo gani huo…?’ nikauliza na yeye akawa
ananiangalia kwa mashaka. Hapo hakusema neno kwanza, mimi nikasema;
‘ Mimi niliona kuwa eneo hili ni chafu, ndio nikaja kulifanyia
usafi, ...na sijui kama nilizima, ndio kuna wakati nadeki, nikaona nisije
nikarushwa maji, nikaharibu vitu vyenu,…sijui lakini nilipozima nikaona kila
kitu kimezima, tatizo nilisahau kuwasha tena, kwani kuna kitu kimeharibika..?’
nikauliza
‘Wewe mtu sikuamini..nilishamuambia mzee, lakin..haya…’akasema
‘Tatizo ...mimi mambo yenu hayo siyajui…naogopa sana umeme..’nikasema
‘Ni nani alikupa ufungua wa chumba hiki?’ akaniuliza
‘Unauliza jibu, ninapotaka kufanya usafi, nilishawahi kuja kwako
kukuuliza ufunguo upo wapi, eeh…, mimi ninafahamu wapi funguo zote zilipo,
kwanini unaniuliza maswali mengi, mbona siku nyingine hujawahi kuniuliza, maswali
kama hayo kuna nini kwani, mbona mnanitisha…’nikasema sasa kwa hasira.
‘Wewe mwanamke mimi sio mjinga…’akasema sasa akinionyeshea kidole,
hakunifahamu kuwa mimi siogopi vitisho….nilitulia nione anataka kufanya nini.
Akasimama, aliponikaribia, akataka kugeuka, na mimi nikasema
‘Nani kakuambia wewe ni mjinga, kama hayo niliyofanya ni ujinga,
basi unamtusi baba yako aliyeniamrisha mimi nifanye usafi..na ni mara ngapi
nafanya usafi, na kwanini huendi kumuuliza baba yako, kama una wasiwasi na
mimi, mbona unaniwekea vikwazo visivyo na msingi..mzee wako ananiamini ndio
maana kaniajiri niwe karibu naye.’nikamwambia.
‘Mzee hajakufahamu kuwa wewe ni nani, mimi nimeshakufahamu…wewe
sio mtu mnzuri kabisa…’akasema
‘Sawa nitamuambia baba yako, amtafute mtu mwingine, ..si ndio
hivyo unataka au sio…ngoja akija,..leo itakuwa mwisho wa kuniona humu ndani..’nikasema
‘Leo iwe ni mwisho wako kuingia kwenye hiki chumba, tatizo ni kuwa
umezima mtambo mkubwa wa mawasiliano, na kwahiyo umetufanya tushindwe
kuwasiliana na humu ndani, ni hatari..na najua hili utakuwa umelifanya kwa
makusudi....’akaniambia.
‘Kwa makusidi !!! Mbona sikuelewi…ili iweje,…’nikasema
Niliona hiyo hali ikiendelea itazidi kuchelewesha mambo mengine,
nikajaribu kuifanya kazi yangu nyingine, plan B, taratibu nikatabasamu, na kusema
‘Samahani mrembo, unajua wewe ukikasirika, ndio unapendeza zaidi..’Nikasema
na kujirembua, nilishafahamu udhaifu wao, mtoto kama baba, akategeka, na
kunisogelea, huku akisema;
‘Tatizo lako wewe kwasababu ya tabia yako unahisi kila mtu ni kama
wewe....’nikasema huku nikijerembua.
‘Mhh..hahaha eti mimi mrembo, toka lini mwanaume akawa mrembo…’akasema
na mim nikawa nimeshafika karibu naye, na haraka akanyosha mikono kutaka
kunikumbatia…sikuwa na muda huo…
Unajua wakati mwingine ukiwa katika kazi kama yangu inabidi utumie
kila mbinu, lakini akili kichwani mwako. Na alipoliona lile jicho, mtoto kama
baba, akasawajika, nikamuona mate yakimtoka, akasahahu alichokuwa akiniuliza
mara akasema;
‘Kwanza nikulize lile ombi langu vipi,..?’ akanisogelea
baada ya kuzima kitu kwenye mitambi, sikujua ni kwanini, na akanisogelea
kujaribu kunishika na mimi nikasogea pembeni na kusema;
‘Ombi lako lipi, eeh, hivi wewe vipi..!!!’nikasema sasa nikibadilika
ghafla
‘Aaah, vipi tena…’akasema
‘Wewe mwanaume,..unajifanya upo sawa na baba yako au sio,
nilishakuambia upuuzi kama huo, siutaki, msinione nipo humu ndani mkafikiria
mimi ni Malaya, kwanza kuhusu huo upuuzi wako nitamuuliza baba yako...kama yupo
tayari kuchangia na mtoto wake...haya,’nikasema na yeye akageuka kuondoka
karibu yangu, huku akisema;
‘Hivi wewe baba unamuona mtu wa maana kwako, ombi langu kwako ni
siri yangu mimi na wewe, eti ukamuulize baba, unataka nilaaniwe nini....wewe
jivunge tu, ipo siku utaingia kwenye anga zangu, ..’akasema na mimi hapo
nikacheka. Nikaona sasa nimeshabadili muelekeo…
‘Kumbe unajua hilo, hehehe..mtoto kama baba…yatawashinda…’nikasema
‘Wewe cheka tu, unafikiri mzee yule atakuwa na wewe milele,
akikuchoka anakutupa chini, wangapi walikuwa naye sasa hawatakiwi tena,.. hata
kumsogelea hawawezi, yeye anamtaka mtu akiwa na shida naye shida zikiisha basi,
huyu mtu ni takataka.., ...wewe jidanganye kwake, ukifikiria
umefika....’akasema.
‘Kama alivyomfanyia mama yako au sio,…?’ nikauliza hivyo, na hapo
ikawa kama nimemshika sehemu mbaya, akasimama, akageuka, sura ilikuwa
imebadilika, ..…
‘Tafadhali, usimtaje mama yangu hapa, unasikia tuongee mambo
mengine lakini usimtaje mama yangu, tafadhali nakuomba…’akasema
‘Ukiendelea kunifuata fuata sitasita kumtaja mama yako, unasikia,…’nikasema
na hapo akageuka hakuniangalia sasa,…nikaona bado, nikasema..
‘Unafikiri mimi sijui… hata hivyo mimi sijawahi kukuambia
kuwa nina haja na baba yako, ...baba yako ndiye kanilazimsiha kuja kwa ajili ya
mambo yake, mimi nina mume wangu, nina maisha yangu mazuri tu, na mume wangu
nampenda, kama isingelikuwa haya mambo yenu unafikiri ningelikuwa hapa, na ipo
siku mtajuta kwa hayo mnayoyafanya....’nikamwambia.
‘Hayo unayafanyiwa ni yenu na baba, mimi siyajui, ...na vitisho
vyako, kwangu havina nafasi, nafahamu ni nini ninachokifanya kwa nafasi gani,
usinitishe kabisa, mimi ninafahamu sheria, na sijawahi kukulazimisha kwa lolote
lile, na hata hivyo ombi langu lipo pale pale, usiponitimizia najua jinsi gani
ya kukupata...’akaniambia
‘Hahaha utafanya nini...?’ nikamuuliza
‘Siri zako zote anazozitumia baba kwa ajili ya kukupata wewe
ninazo mimi, zipo kwenye mtandao, yeye akizihitajia mpaka aingie kwenye
mtandao, na mimi ndiye nimezihifadhi, sasa utanidanganay nini, nikiamua
kuzitumia dhidi yako, siutaumbuka wewe...sasa uamue moja kuwa na mimi au na
baba..’akasema.
‘Nakuambia hivi ni bora umenifahamisha hayo, nitamuambia baba yako
kila kitu, na hizo mbinu zenu..kumbe ndio mlivyo eeeh,..na ni bora aniambie
ukweli nipo hapa kuchangia mtu na mwanae..kanifanya mimi Malaya sio..keshaniita
mimi ni mtumwa wake, sasa wewe wataka kunifanya mimi ni Malaya, mtaniambia....’nikamwambia.
‘Hivi wewe una akili kweli,...kila kitu utamwambia baba,..utamuambia
baba, huyu baba ndio nani, eeh….ok, …tuyaache hayo, naomba yaishe, au sio,
samahani basi, namba tafadhali usije kumuambia baba....’akasema
‘Sasa tuelewane, ili nisimwambia baba yako, unifundishe jinsi gani
ya kutumia huo mtandao, jinsi ya kutengeneza picha na kuziweka kwenye huo
mtandao..’nikamwambia.
‘Unataka nikifundishe ili uje uzifute, ..hilo umenoa..’akasema
‘Kwahiyo unataka nikamuambia baba yako au sio..’nikasema
‘Sikiliza kama unataka nikufundishe, kwanza na mimi unikubalia
ombo langu, mimi nitakufundisha kila kitu unachotaka…tena tuanze leo, unasemaje…’akasema
‘Sawa…’nikasema
‘Lakini tumekubaliana, nitakufundisha lakini malipo yake ni ...maombi
yangu..’akasema sasa akitabasamu, uso umeshasawajika.
‘Kwanza unifundishe, malipo si baada ya kazi…’nikasema
‘Hahaha wewe mjanja sana, sikiliza kama kweli unataka hilo,
tukubaliane, mimi nipo tayari,...na safari hii sikubali, kama ulivyonidanganya
siku ile… la sivyo, na mimi nitaweza kukufanyia kitu ambacho hutaweza
kunisahau....’akasema
‘Kitu gani, hujui haya yote baba yako anayasikia..’nikasema
‘Hahaha, wewe hunijui eeh, mimi sio mjinga kihivyo,…nikuambie
kitu,..ujue na mimi ni wakili kama baba…kila ninachokifanya najua jinsi gani ya
kujilinda,…’akasema na mimi sikumjibu
Nikageuka kama kutaka kuondoka,..yeye akageuka, nahisi alitaka
kukiwasha kile kitu alichokuwa kakizima….
**********
Alipogeuka akazima kile kitu na kutembea hadi
mezani kwake hakugeuka, alishajua kuwa nimeondoka…akawasha ile laptop, akawa
anatizama matukio, akawa sasa anafuta baadhi ya mtukio, nahisi ni hapo
tulipokuwa tunaongea naye, alipomaliza, akazima ile laptop, akairejesha sehemu
yake...
Mimi nilikuwa pale karibu
na mlango, sijaondoka… na alipomaliza shughuli zake, sasa akawa anatoka, kutaka
kutoka kabisa humo ndani, akaniona nipo nimesimama, nimeshikilia ufagio,..hapo
hakushituka, akaniuliza..
‘Mimi nilijua umeshaondoka, sasa unasubiri nini, kama huna kazi ya kufanya, nenda nyumba
ukalale..’akasema.
‘Nishakuambia kwa maagizo ya baba yako, natakiwa kuhakikisha kila
kitu kipo sawa, ninafahamu ulipoingia kuna vitu umevuruga, kazi yangu ni
kuhakikisha kila kitu kipo katika mpangilio wake, ili wageni wakija kusiwe na
jambo la aibu...’nikasema
‘Ishia kule, nenda kaendelee na kazi zako huko,hapa sio sehemu ya
watu, hii ni sehemu ya mitambo, huku hakuna mgeni anaweza kuingia ...’akasema
na kutaka kuondoka.
‘Polisi je..?’ nikauliza hivyo, akashtuka, na kugeuka kuniangalia.
‘Polisi!!’ akasema kwa mshangao.
‘Hahaha, kumbe unawaogopa eeh, sasa ujue kuwa hao watu watakuja,
kama sio leo, ni kesho….’nikasema
‘Kwanini, kuna nini kibaya…?’ akauliza
‘Naondoka, kaam hutaki nifanye usafi humu, nitamuambia baba yako
umenizuia…’nikasema
Mimi nina akili za ajabu sana, ukinionyesha kitu, au nikaona
unavyofanya, akili yangu hunasa haraka sana, nilishaona jisni anavyoweka neno
lake la siri, nikalinasa bila ya hata ya yeye kujua.
Kwa muda ule nilijifanya mjinga kabisa nisiyefahamu kitu, hata
baba yake anafahamu kuwa mambo ya mitambo, mitandao, komputa sijui kitu….kumbe
!
Aliondoka hadi ofisini kwake, na huko nikamfuata nikitaka
anifundishe…, nia ni kuhakikisha akili zao, zinajua mimi ni zezeta wa mitandao,
na komputa, hakuogopa kunifundisha akijua kuwa mitambo ipo wazi, anaonekana kwa
kila anachokifanya.
Alinifundisha kidogo jinsi ya kuwasha komputa, na kuzima, jinsi ya
kufungua vitu kwenye komputa, ni vitu vya kawaida, baadae akasema niondoke
kwani ana kazi zake anataka kufanya, kabla hajaondoka,…hata hivyo kwa jinsi
ninavyomfahamu alionekana kama hayupo
sawa.
Baadae akaondoka
Usiku wake, nilitaka niingie kwenye hiyo mitambo, kwani ndio siku
peke yake ningeliweza kufanya jambo, nilichofanya ni kuchelewesha kununua
mafuta ya genetaror, nilijua mara kwa mra umeme unakatika, na mimi ndiye
niliyekuwa nahifadhi fedha za matumizi madogo madogo ya ofisi, na nilitakiwa
kuhakikisha mafuta ya genetor yapo,
Nilijua ikifika saa tatu, mafuta yatakuwa yamekwisha, na siku hiyo
umeme ulikuwa hakuna, huku nikiomba huyo mtoto wa huyo jamaa akaondoke na
asirudi, au anachelewa, nilishangaa kweli siku hiyo kwani mpaka saa tatu
alikuwa hajafika,....mara genetaror likazima, kukawa kizaa, zaa, giza, nilijua
kwa jinsi ili mitambo ilivyo ikifika nusu saa itakuwa imezima, hapo
nikajichelewesha kufuatilia, hadi nusu saa ikapita, ndio nikajitokeza
‘Mbona generator limezima, hujanunua
mafuta..’akaniuliza Makabrasha
‘Naona nimepitiwa mambo yamekuwa mengi, ...nimemtuma mlinzi
akanunue...’nikasema
‘Huo ni uzembe, unafahamu umuhimu wa umeme kwenye hili jengo,
huoni watu wabaya wanaweza kutumia mwanya huu kufanya lolote...na kwanini hata
ile mitambo ya akiba inayohifadhi umeme, umezima pia..ile inaweza kuhifadhi
umeme wa masaa 24..’akasema.
‘Mimi nilishakuambia mambo ya mitambo, komputa, mimi sijui…kama
hamukunielekeza jinsi ya kuwasha na kuzima nitajuaje..’nikasema
Hapo akachukua simu, akaongea na mtu wake ..
Mimi hapo nikaachana naye na kukimbilia kwenye hicho chumba. Kama
nilivyojua, sehemu ile ya kuangalia matukio ya jengo ilikuwa imeshazima, kwa
haraka nikakimbilia kwenye ile sehemu ilipowekwa laptop, ufungua wake nilikuwa
nao tayari,…nikaichukua na kuifungua, nikawasaha, nilijaribu mara moja ile
namba ya siri, ikakubali…
Nikatafuta sehemu hiyo inapohifadhia matukio..ile laptop ndio
yenye kila kitu, ndio Server, …kwahiyo kwa kutumia yenyewe niliweza kuongoza
mitambo yote humo ndani,…muhimu kwangu ni kufuta historia ya matukio ya nyume,
yale ambayo nahis sio muhimu kubakia nayo.
Ilichukua muda kidogo kupata kumbukumbu ninazozitaka, ....nilikuta
kumbukumbu nyingi za watu mbali mbali, ambazo kama zingeliwekwa hewani,
nafikiri watu wengi wangeliumbuka, sikutaka kuangalia zaidi, kwani mambo
niliyoyaona humo yanatisha,mimi nikazifutilia mbali, na kuhakikisha hazipo
kwenye sehemu ya mabaki ya vitu vilivyofutwa, nikaangalia sehemu inayoangalia
matukio ya jengo hadi umeme ulipozimika, nikazifuta.
Hapo nikapumua, sehemu ya kwanza ya mpango wangu ikakamilika.
Tuendelee…
WAZO LA LEO: Binadamu sio mtu au jiwe, ukasema utalichunga lisifanye
kile usichotaka, kama kiumbe huyu aliyeumbwa na mola wake, hamtii yule
aliyemuumba sembuse mamlaka…!!!
Kiukweli..ni kawaida ya wanadamu kukengeuka,…sheria ziliweka kwa
ajili yake kwa masilahi yake, labda na mali zake,lakini wavunjaji sheria ni hao
hao wanadamu..Na kiukweli wapo wanatajirika kwa hali hiyo ya kuvunja sheria, na
wengine wanakuwa masikini kwa sababu hiyo hiyo ya uvunjwaji wa sheria… KIONGOZI
ndiye anayebeba dhamana ya hili. Kumbe basi, kiongozi ni mtu muhimu kwetu, basi
tusifanye makosa kumchagua kiongozi asiyefaa,…!!!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment