Kazi imeanza….
Nikaenda sehemu wanapohifadhia picha za video ambazo
zilikuwa zinaonyesha mtu aliyefika kwenye hicho chumba karibu, nikajiona ni
mimi peke yangu nikaifuta hiyo kumbukumbu, halafu nikatafuta sehemu ya kuzuia
kamera za humo ndani zisichukue matukio hadi itakapokubaliwa tena ,nikaiweka
OFF.
Ina maana kuanzia hapo hadi hapo mtu mwingine atakapokuja
kuikubali kuonyesha matukio, kutakuwa hakuna kitu kitakachoonyeshwa,
nilipoamaliza nikatoka kwa haraka, na wakati natoka tu, genetaror likaanza
kunguruma na umeme ukarudi.
‘Oh huyo mtu kaniwahi, lakini bado…’nikasema kimoyo moyo
Nikatoka mle ndani kwa haraka nikawa natembea kuelekea ofisini
kwangu, mara bosi huyu hapa…
‘Ulikuwa wapi wewe nakutafuta sehemu zote,..naona mitambo ya
usalama humu ndani imezima, sio kawaida, hata umeme ukizimika inaweza kuhimili
hata saa nzima, ..kuna tatizo,....’akasema Makabrasha huku akielekea kwenye
chumba cha usalama, lakini baadaye akatoka huku akiongea peke yake.
‘Naona kuna tatizo kwenye mitambo ya usalama, ..siwezi kuingia
kwenye komputa ya usalama, sijui huyu mtoto kafanya kitu gani,..kabadilisha
neno la siri...kwanini anafanya hivyo bila kunipatia mimi taarifa, sasa
tutafanye hapa..’akawa anaongea huku akinipita na mimi nikamwambia.
‘Mimi sijui, lakini tunaweza kujaribu pamoja huenda tukagundua
jinsi gani ya kuingia, tukiwa wawili…’nikasema.
‘Hapana huko wewe huhusiki kabisa, ni mimi na yeye tu…’akasema
‘Kama yeye hayupo na hali kama hii imetokea itakuwaje…?’
nikamuuliza
‘Subiri wewe,…haya hayakuhus, ngoja nimpigie simu huyu mwanangu, japokuwa leo
tumekorofishana, lakini hili ni muhimu, ni lazima afike, kwa hraka…’akasema sasa
akishika simu kumpigia mwanae nikaona nimpoteze mawazo kwanza…
‘Mbona alishafika hapa…’nikasema
Ina maana kumbe alikuja kuzima na kubadili …kwanini lakini huyu
mtu ni muhuni sana, ana nini leo..’akasema kwa hasira.
‘Nahisi kuna kitu, alitaka kufanya, labda anataka kurekebisha,
nilisikia akisema kuna matatizo kwenye mitandao..ooh, unajua mimi sijui mambo
zenu…’nikasema
‘Alitakiwa aniambia mimi, yeye ni mwanangu tu, haya mambo humu ni
yangu sio yake, naona anataka kunipanda kichwa, …ni lazima niongee naye, au ni
kweli labda kuna kaliona, ikabidi afanye hivyo, alitakiwa aniambie au sio…’akasema
kama ananiuliza
‘Kapatiwa,…subiria si atakuja….’nikasema
‘Unajua leo sijisikii vyema, sipo hivi kabla, mwili wangu una afya
tele, lakini leo, ooh, nahisi natakiwa baadae nioane na dakitari…halafu nahisi
....kama kuna tatizo kama kuna kitu kibaya kinata kutokea,.tokea jana hali
haipo sawa..’akasema
‘Unaumwa, inabidi umuone dakitari, wewe si unaweza kumuita
mmojawapo akaja kuutibia hapa nyumbani….’nikasema
‘Hapana mimi siumwi,…unajua jana nilikorofishana sana na huyu
kijana wangu, namuona kabadilika ghafla,..mama yake anamfunza vibaya, sio yule
mwanangu wa zamani ambaye alikuwa akinitii kila kitu…’akasema
‘Kwani mama yake karudi..?’ nikauliza
‘Ndio,…huyu kila mara akiwepo inakwua hivi..nilishamuambia kijana
wangu asimsikilize mama yake…kwani mama yake hana nafasi kwangu, ilitokea
bahato mbaya tu nikazaa naye, sina ….mahusiano naye kabisa…’akasema
‘Lakini si umezaa naye, huo ni uhusiano pia….wewe ulipozaa naye
ulitegemea nini..?’ nikamuuliza
‘Wewe hujui tu…na…unajua akili yangu haipo sawa, nahisi kuna kitu
ambacho sio cha kawaida humu ndani, huwa mimi ninakuwa na hisia kabla ya tukio…na
hili limeanza pale tu nilipokorofishana na huyu kijana..maana aliondoka kwa
hasira, ndio maana hajafika mpaka muda
huu..’akasema
‘Mbona alifika halafu akaondoka, kwani mlikorofishana nini tena na
mtoto wako kipenzi?’ nikamuuliza
‘Unafahamu hawa vijana wana tamaa sana, wao wakiona kitu
kipo, hawajiulizi kimefika fikaje hadi hatua hiyo, hawafahamu kuwa sisi wazazi
wao tumetumia miaka mingapi hadi kulifanikisha hilo, hawajui jinsi gani
tulivyojijenga..unaona …’akasema.
‘Mimi hapo sikuelewi, nijuavyo mimi, wewe na huyo kijana wako
mumekuwa naye bega kwa bega kwenye maendeleo yako, na kama yeye anataka jambo,
basi ana haki, na nimegundua kuwa yeye ni mshauri wako muhimu sana..’nikamwambia.
‘Pamoja na hayo, kuna mambo mengi kayakuta, na sio kwamba
tumeshirikiana naye, hilo ndio anakosea, yeye, mengi kayakuta, …na kwa vile
nilimuona ni mtu anayefanana na mimi, ndio nikawa na mshirikisha, lakini sio
kwamba, yeye ni sawa na mbia wangu, hapana…’akasema
‘Kwani tatizo lipo wapi…?’ nikauliza
‘Unajue yeye anataka mengi kwa muda mrefu, ana tamaa zaidi yangu..’akasema
akiwa kasimama karibu yangu.
‘Kwani yeye anataka nini?’ nikamuuliza na akataka kuondoka, lakini
akageuka na kuniangalia machine akasema;
‘Huyu kijana analalamika, ni kwanini nimeamua kubadili mirathi,
kwanini sasa hiv nimeamua kumweka mwanangu huyu mkubwa kuwa mrithi wangu wa
kwanza, nay eye sasa nimemfanya kama mtu wa pili..anadai yeye ndio ana haki ya
kuwa mrithi wangu kama nilivyofanya awali..
‘Mimi sielewi, …’nikasema.
‘Unajua yeye hafahamu
mawazo ya kikubwa, mimi nimtu mzima natizama mbele zaidi yake,nimefanya hayo
baada ya kufikiria sana, hali imebailika, maisha yamebadilika sasa hivi mimi
sio yule mtu wa jana…’akasema
‘Umetajirika au sio…?’ nikauliza
‘Ni kweli hilo siwezi kukuficha, ndio maana nimeona huyo mtoto
wangu mkubwa ndiye anayeweza kuja kuendeleza kila kitu nikiwa sipo..na sio kwa
vile naandika hayo ndio najitabiria kifo…mbona hayo yalikwepo toka awali, kama
wakili hayo ni muhimu yawepo kwenye familia yangu…’akasema
‘Unahisi ni kwanini anaona yeye ndiye anastahiki kuwa mrithiw ako
zaidi ya huyo mtoto wako mwingine aliyemkubwa…?’ nikamuuliza
Ni tamaa tu,..na mwanagu huyu hakuwa hivyo, nahis kuna kitu mama
yake kambadili,..hajui kwanini mimi nimefanya hivyo…haya kaona, sasa anakuja
juu, ni kwanin nimefanya hivyo, yeye hana haki ya kuingilia maisha yangu..’akasema
‘Leo hii unasema hivyo, mimi nakumbuka ulikuwa ukitamba kuwa huyo
mtoto wako ni kila kitu au sio…?’ nikauliza.
‘Nimeona mbali,..unajua japo huyo kijana yupo mbali, lakini mimi
nafuatilia maendeleo yake kwa karibu, ….anajitahidi sana, kielimu, na…anafaa
kuwa kiongozi wa hii wa familia..na ukumbuke huyo ndiye mtoto wangu wa ndani ya
ndoa, unaona eeh, ...’akasema
‘Lakini kihalali, …hata ingelikuwa mimi ningedai hivyo hivyo,
kwasababu huyo kaka yao yupo nje, hajui chochote kinachoendelea hapa, na
nakumbuka uliwahi kuniambia huyo mtoto wako wa huko Ulaya hampatani kabisa,
hakujali…, na aliondoka na kukuambia hana haja na mali yako ..sasa kwanini
unajipendekeza kwake....?’ nikamuuliza
‘Wewe hujui mambo ya wazazi na watoto, hata kama mtoto hampatani
kwasababu kadhaa, lakini yeye atabakia kuwa mtoto wangu wa kwanza, na yeye
nilimzaa na mke wangu wa ndoa, ana haki zote itakuwa sio halali kumfanyia
hivyo, niliandika awali ile mirathi kwa hasira tu. …’akasema
‘Na huyu je…mbona ndiye anakutumikia kwa kila hali…?’ nikamuuliza
‘Huyu niliye naye hapa nimemzaa kwenye nyumba ndogo,..nilimsomesha
na kumuandikisha kama watoto wangu wengine, na nimeona anastahili kuwa karibu
na mimi, na ndio maana nimemuweka nafasi ya pili, atakuwa chini ya huyo
kaka yao anayeishi huko Ulaya, kuna tatizo gani hapo....’akasema.
‘Kwahiyo wewe na mtoto wako mkaishia wapi?’nikamuuliza
‘Yeye alikuja na mipango yake, uone jinsi mtoto huyu alivyo balaa,
kakaa sijui na mama yake, wakapanga mambo mengi tu, jinsi ya kugawanya mali
eti keshaandaa na mikataba ya kifamilia, kama vile mimi ninakufa
karibuni, kwenye mikatba hiyo, ambayo ni kama urithi, , ...na yeye awe ni
mrithi wangu , yaani kiongozi wa familia,..’akasema kwa hasira
‘Wanataka mimi nife au sio..si ndio maana yake hawa watu hawana
akili kabisa…, nimemwambia huo uchuro siutaki, kama ni mikataba ya urithi, mimi
nimeshaupanga na ninafahamu ni nani awe kiongozi wa familia, kama mimi
nikifa..lakini sijafa, na sitaraji kufa leo...siumwi,, sina tatizo la
kiafya..kwanini anakuja na mipango hiyo, wana matatizo sana hawa
watu....’akasema akijiangalia.
‘Lakini kufa sio lazima uumwe, wewe kama ulivyo, kutokana na
mambo yako unayoyafanya,una maadui kila kona, wakija kuku-ua watu, hata hivyo
kuandika mirathi, sio lazima mtu afe, ni katika kuwekana sawa kimajukumu au
sio..vyovyote iwavyo ni muhimu kila mwanafamilia afahamu nafasi yake au sio....’nikasema
‘Kweli hilo ni la kuangalia sana,..nahisi maadui wananitafuta…
ndio maana umeme ulipozimika, nimeshituka sana, sitaki uzembe huu utokee tena,
...unanisikia, ....sasa nisikilize kwa makini, kesho huyu mpenzi wako anakuja,
nilishakumbia hilo, au umesahau au uliona naongea tu, tafadhali kwenye kazi iwe
ni kazi tu ...’akasema
‘Mpenzi wangu gani, mimi ni mke wa mtu.?’ Nikamuuliza
‘Hebu acha utoto, nikisema mpenzi unanielewa ni nani,
..nimeshamweka sawa anakuja kuweka sahihi yake kwenye hiyo mikataba ambayo
itanifanya mimi, niwe na haki ya kumiliki kila kitu…’akasema
‘Mhh..’nikaguna tu.
‘Nilishawaelezea hilo..sio nafanya hivyo kwa kupenda,..amelipa
mdeni yangu kupitia kwenye hisa zake..ni halali kabisa,…kwahiyo wewe na wenzako
mlitambue hilo, ...na tatizo ni huyu mtoto wangu anakuja na sera zake za ajabu
ajabu, anataka na yeye awe na hisa,...anataka kunikorofisha, haya mambo
hayajakaa sawa, keshaanza kugombea mali, ni uchuro huu…I don’t like this...’akasema
kwa hasira
‘Mimi ninawashangaa kweli kweli, yaani mumeshaanza kugombea mali
za watu, hata kabla hamjazipata, mumeshaanza kumiliki hata kabla
humajamilikishwa, kweli akili zenu wote ni za kishetani wewe na mtoto wako,
na mimi nahisi hamtafanikiwa kwa hilo, na mkifanikiwa mtakuja kupigana
baba na mtoto wake, hiyo ni hatari....’nikasema
‘Kama mimi nipo hai, hakuna cha mtoto wala mama yao atakayeweza
kunitawala, mimi, unasikia…mimi ndiye
mwenye amri ya mwisho.., wote wanalifahamu hilo, najua kabisa huyo mtoto
anaendeshwa na mama yake, na mama yake nilishamwambia simtambui tena,
tulishamalizana mimi na yeye…’akasema
‘Kazi unayo, mali ya dhuluma kamwe haiwi na amani, nakuambia
ukweli..’nikasema
‘Sikiliza,..usitake kunifanya mimi ni mdhalimu, nimemdhulumu nani
hapa, umeona mwenyewe sera zangu, na nimejaribu kukuelimisha dhamira yangu,
umeona jinsi gani ninavyoitumikia jamii…na hili la mpenzi wako, ni lazima
lifanyike, ili na mimi niweze kuendelea kuwa juu…wakubwa huko wananisakama…’akasema
‘Wakubwa gani..?’ nikauliza
‘Sitaki niyaongee haya mara kwa mara, wewe unafahamu ni nani
nawaongelea, sasa …huyo mtoto natakiwa nimuweke sawa, aacha upuzi wa
kumsikiliza mama yake, mama yake hana nafasi kwangu, na zaidi mimi na mama yake...hatukuwahi
kufunga ndoa naye…yeye alikuwa mpenzi wangu wa kupita tu, nikampa mimba ndio
akapatikana huyo kichaa.’akasema kwa hasira.
‘Aaah, kumbe, una wangi sana, kazi yako ni kuzalisha tu, huyo
alikuwa mpenzi wako wa zamani, nahisi wapo wengi wa namna hiyo, huyo wakati huo
ulimuona mpenzi, sasa hafai, au ni kwa vile kazeeka,au?’nikamuuliza
‘Namfahamu sana huyo mwanamke, ana tamaa sana, hatuivani kabisa,
na mtoto wake kachukua tabia zake zote, na kama ataendelea na hiyo tabia sizani
kama tutaivana, na...namuona atakuwa kikwazo katika mipangilio yangu ya
kimaisha kinyume na nilivyotarajia, kabadilika kabisa, hajui mipangilio yangu
mingine..ni lazima niwe makini sana...’ akatikisa kichwa kusikitika halafu
akaendelea kusema;
‘Sawa mimi nakushauri hivi, kwa hali ilivyo ni bora make muongee
mkubaliane au sio, yeye ndio kama mlinzi wako au sio…yupo nawe wakati wote,..’nikasema
‘Ni kweli unayoyaongea,..mimi najiuliza tu ni kwanini siku hizi hanisikilizi mimi, na anakuwa akimsikiliza
sana mama yake, ujue huyu mtoto mimi ndiye nimefundisha ujanja wa kimaisha ,
alipomaliza kisomo chake akataka kufanya kama alivyosoma, nikamwambia dunia
hii, ina utaratibu, lakini ndani ya hizo taratibu kuna njia za mikato,..unaona
eeh..’akasema
‘Kumbe ni wewe ulimuharibu…’nikasema
‘Sio kumuharibu,..hivi niambie kiukweli kwenye hali za maisha yetu
kuna mtu anaweza kuinuka akawa tajir bila kufanya magendo,…sasa ni lazima
nimfundish, ujanja wa dunia hii…ukijifanya unasubiria mshahara tu, utakufa
masikini..ndio hivyo nikamuelekeza jinsi gani ya kuishi, kaiva sasa ananigeuka…’akasema
‘Ndio maana nawaambia dhuluma itawaandama hadi kaburini…’nikasema
‘Mhh..na wewe bwana, mbona hunielewi,…kwa namna nyingine upo
sahihi, kuwa kuna kitu kama hicho, lakini tufanyeje sasa, wakati wakubwa
wameamua kujitajirisha wao wenyewe, angalia hizi foleni za magari, makodi mengi yasiyomjali mtu wa chini, ..utafanaje
kazi namna hii, angalia tatizo la umeme, kweli unaweza kuwekeza hivi, wao
wakitaka kupita njia zinasafishwa, kwao umeme haukatiki…utafanyeje…’akasema
‘Ni hayo tu…?’ nikauliza
‘Natolea mfano kidogo kuwa ili ufanikiwe katika nchi yetu, huna
budi kupita njia za mkato, ukitaka njia sahihi utaumia, kuna watu wanakuwa ni
vikwanzo..hebu anza kufuatilia hati za kiwanja uone…au ..mifano ipo mingi…
utasubirishwa wee..kumbe ni namna tu inatakiwa, bado sana….kwahiyo ilibid
nimfundishe kijana aelimike…’akasema
Na sio hilo kazi..siku hizi watu binafsi, ukifanya kwao, eeh,…ujue
utanyonywa kupitiliza, usipo kuwa mjanja utaishia kuwa masikini…umeonaeeh,…haki
nyingi za mfanyakazi wanazikwepa, chunguza sana hili utaliona, sasa mimi kama
Makabrsha nataka hawa watu niwakomoe kihivyo, nyie hamjui tu…’akasema
‘Hutafanikiwa, …maana unatumia njia hiyo kujitajirisha huku
ukitafuta visingizio, hujui kiasi gani unawaumiza watu,….maana unatutumia sisi
watu wa chini kwa ajili ya visasi vyako kwa watu wa juu…’nikasema
‘Naona wewe hutanielewa, ni kwanini lakini…nilitaka wewe unielewe
ili umsaidia huyu kijana, umuelemishe ili tufanye kazi pamoja, wewe uwe mtu wangu
wa karibu pia..’akasema.
‘Tatizo wote wawili hamuaminiki, mtoto kama baba yake...au kama
wanavyosema mtoto wa nyoka ni nyoka..’nikasema kwa dharau huku
nikijifanya kutabasamu .
‘Huyo haniwezi kabisa na hataweza kunifikia mimi, yeye anachukulia
mambo kwa pupa, mimi natumia ujanja, hekima na akili, ndio maana unaona
nimefanikiwa kwa kiasi hiki kikubwa, unaona jumba hili, ni nani anaweza kujua
nimelijenga mimi kwa vipi,..ni akili, ..usione watu wana majumba, utajiri,
ukfikiria ni kirahisi hivyo…’akasema sasa akiangalia juu.
‘Dhuluma tu hiyo..’nikasema
‘Sio dhuluma jamani, nielewe…, ni kutumia akili, na ujanja, lakini
dhumuni kubwa ni kuwasaidia wanyonge, humu nimewekeza, angalia ajira kiasi gani
nimezifufua hapa, unakula, na huku unasaidia, siwezi kusahau dhumuni langu,
hapa nina mpango wa kuwajengea wazee sehemu yao,…ambapo wataweza kuwekeza, kila
mtu na ujuzi wake, ngoja haya mambo yawe safi, wewe utaona tu..’akasema.
‘Kwahiyo yote hayo umemfundisha mtoto wako?’ nikamuuliza
‘Tatizo yeye hataki kutuliza kichwa, yeye anataka mambo kwa pupa,
ana tamaa za haraka, hata sijui kwanini ameweza kufaulu masomo yake ya
uanasheria, kazi hii hataiweza kama atakuwa na tabia ya namna hiyo, ya pupa, na
ninavyomuona hatafika mbali..’akasema
‘Mhh..haya bwana..’nikasema
‘Sio nataka wewe unielewe, ili mkikaa kuongea umuelimishe…, hebu
angalia, anataka kunirithi nikiwa hai...sijui kwa hali kama hiyo, tunaweza
kukaa pamoja,....lakini mimi kama baba, nitamdhibiti tu, nimeshamfahamu vyema anakotaka
kwenda, sasa ataona vipi baba livyo mjanja, haniwezi kabisa...’akasema.
Na mara simu yake ikalia, akaipokea bila kuiangalia, na mara
akakunja sura ya uso wake na kuonekana kukasirika, akasema kwa sauti ya juu ya
hasira;
‘Kwanini unasema hutafika leo, wakati unafahamu umuhimu wa wewe
kuwepo leo, nataka uje hapa haraka,...kwanza kuna matatizo kwenye mitambo ya
usalama, na pia ni wajibu wako kuwepo hapa, ili tukamilishe kazi , achana na tamaa
zako hizo, nasema mimi kama baba yako uje hapa haraka,.....’akasema
‘Unasema nini, unanijibu mimi hivyo, kuwa hutafika,mpaka
nikubaliane na matakwa yako, ina maana unanilazimisha kufanya unavyotaka wewe,
hivi unaelewa unaongea na nani...unasema nini, ina maana umeshaota mapembe sasa
eeh,...’akawa anaongea huku mwenzako naye anaongea, maana sauti ya huko
nilikuwa naisikia, wakazozana hapo mwishowe akasema;
‘Sikiliza wewe mtoto, kama nimekuzaa mimi, utakuja hapa, kama una
baba yako mwingine usije , usijione kuwa umekuwa sasa,...na kujiona hunihitaji
tena, hujui ninaweza kukufanya lolote ukasahaulika katika hii
dunia..’akasema na kusikiliza simu kwa muda halafu akaibamiza simu chini , na
simu hiyo ikapasuka vipande vipande, na kusema;
‘Mwanaharamu mkubwa wewe...tutaona,....’akageuka na kuelekea
ofisini kwake, ukumbuke hapo tulikuwa tunaongea kwenye varanda, nilipokutana
naye wakati natoka huko kufanya mambo yangu,..hapo mimi nikachekelea kimoyo
moyo, nikisema ‘mipango inakwenda sawia…’ ukitaka kumshinda adui , wagawanye,
wasiwe na masikilizano..utwashinda kirahis sana..mimi huyoi nikurudi chumbani
kwangu, sikutaka kumfuata huko ofisini kwake, kwani nilijua kwa hali aliyonayo
hatutaweza kusikilizana.
Mimi kwa hali kama hiyo , ilikuwa kama vita vya kunguru, faraja
kwangu, nilitaka watu hawa wawili wawe hivyo, ili mipango yangu iweze
kufanikiwa,..na kimoyomoyo nikijua sasa sehemu muhimu imekamilika…
Mpaka hapo nilijipa moyo hivyo, hata hivyo, sikuwa nimeamini kabisa
kuwa huyo mtoto wa marehemu hatafika, namfahamu sana, yeye na baba yake
hawaeleweki, wao ni waarabu wa pemba, wanajua sana, utaona wamegombana hivyo
baadae kidogo wapo pamoja wanajadili mambo yao,…kwahiyo nikachukua tahadhari,..
Nilikwenda kuongea na mlinzi mmoja ninayemuamini , nikamwambia ,
kama huyo mtoto wa bosi akija , anipigie simu kwa haraka,...kwani sehemu kubwa
ya mitambo ya kunasa matukio ilikuwa haichukui picha, kwahiyo ningeliweza
kufanya lolote bila kujulikana, kwa kiasi fulani nilikuwa na amani kidogo,
nikasuburia muda muafaka, wa kumalizia kazi ambayo nilishaianza.
Nilikuwa najiamini maana sasa nina silaha, na nikiwa tayari , au
nikisikia kuwa huyo jamaa kafika nitakwenda kuichukua, sikuwa na haraka nayo
sana, nikatembea kuelekea ofisi ya siri ya Makabrasha, nikafungua, na
kulitafuta kabati maalumu anapoweka nyaraka zake, nikachukua kile
ninachokihitajia, na kurudi chumbani kwangu.
Kabla sijafika huko nikakumbuka kazi nyingine ya kufanya, kwani
siku hiyo niliipanga iwe siku ya mwisho ya kukaa kwenye hilo jengo, nikaelekea
sehemu ninapoweka vitu vyangu muhimu ambavyo nimevihifadhi mbali na chumba
changu, sikutaka waje wavikute chumbani kwangu, kama ikitokea kuvitafuta,
nikaviweka sawa, halafu nikarudi chumbani kwangu,sasa nikijiandaa kwenda
kuichukua silaha yangu, sikutaka iwe mbali na mimi na wakati nafika chumbani
kwangu, simu yangu ikaita, alikuwa mtoto wa Makabrasha,
‘Unasemaje?’ nikamuuliza kwa sauti isiyotaka kuongea,
‘Samahani sitaweza kufika kwenye shule niliyokuahidi, lakini ombi
langu lipo palepale,na kwanini mitambo hapo haifanyi kazi, ...umeingia
tena humo ndani?’akasema na kuniuliza
‘Umesema hutakuja, ina maana mkataba huo umekufa, labda useme kuna
jingine..na kuhusu swala la mitambo hayo unayafahamu wewe, wewe ndio mtaalamu,
huenda ulifanya hivyo makusdi kumuonyesha baba yako kuwa wewe ni zaidi au sio..?’nikasema
kama namuuliza
‘Wewe nimeshakufahamu, wewe unajifanya ni mjanja, lakini ujue kuna
wajanja zaidi yako, kuna kazi naifanya ikimalizika nitaangalia, kama nitakuja
au la, ..lakini kwa vile hatujaafikiana na mzee ninaweza nisifike, na kama
nikifika, nitahitaji maelezo ya kina kwanini umezima mitambo, na kwasasa siwezi
kuona chochote kinachoendelea hapo, utakuwa ni wewe tu...na hilo litakufanya
utimize ombi langu, la sivyo, mimi nitakuumbua kwa mzee ...’akasema
‘Una uhakika gani na hilo..na je nikimuambia mzee wewe
unanitongoza,..nia ushahid hujui kila nikiongea na wewe nakureodi kwenye simu…hahaha,
mimi ni mjanja kama wewe…au nimuambie?’ nikamuuliza
‘Utaona....mimi huwa sichezewi, mimi ni mtaalamu, nafahamu sana
hiyo mitambo, na kawaida yangu, nikitaka jambo ni lazima nilipate, muulize baba
atakuambia, ndio maana nipo naye karibu, ananifahamu sana,…’akasema
‘Mbona sasa kampa urithi kaka yako, ina maana wewe hufai, huna
akili iliyotulia, sema wewe una tamaa, utawazaje mambo ya urithi wakati baba
yako yupop hai, mna mipango gani wewe na mama yako…’nikasema
‘Nini..nimekuambia nini wewe…’akasema kwa hasira
Nakuulize wewe, maana baba yako kakasirika, sijawahi kumuona akiwa
na hasira kiasi hiki, nisikilize mimi, pamoja na yote mzazi ni mzazi kumbuka
ulipotoka..’nikasema kama kuuma na kupuliza.
‘Wewe hutujui…na kwa hili ni lazima nipiganie haki zangu, mfano tu,
je mzee kama hayupo, unafikiri huyo kaka yangu atanijali,..yeye na mimi
hatuivani kabisa,… je huyo kaka yangu anafahamu wapi tulipotokea, ni kwanini
tumefika hapa tulipo, sema ukweli wako,..’akasema na kukatiza nahisi alikuwa
akiongea namtumwingine.
‘Sasa…eeh ukiangalia hiyo mikataba aliyotayarisha baba, yeye
kanisahau mimi nimejaribu kumtayarishia mikataba mizuri tu, nikimkumbushia wapi
tulipotoka, yeye anakimbilia kumuingiza mama kwenye mazungumzo yetu.., eti mama
ndiye ananiharibu…’akatulia kuna sauti
ilikuwa kama inamsumbua.
‘Unajua nikuambie kitu , mama yangu masikini ana nini na yeye, alimpachika
mimba yangu eeh, akamtelekeza, mama kaishi maisha magumu hadi anajifungua mimi…siwezi
kusikia vizuri mtu akimuongelea vibaya, huyu ni mama yangu na mama yangu ni
kila kitu kwangu,…sitajali ni nani, kama mtu anataka kuwa asui yangu amuongelee
mama yangu vibaya,..sipendi…najua yeye ni baba yangu namuheshimu kwa hilo,
lakini pia awe akinisikiliza na mimi,..’akasema lakini akawa kama anakatiza.
‘Ni nani huyo mpo naye, ni Malaya zako nini…?’ nikauliza
‘Hahaha…acha hayo, sio kweli…’akasema, na nikasikia akiongea na
mtu, baadae akasema;
‘Sory, nipo na mtu karibu, ….sio kama unavyofikiria wewe…’akasema
‘Hahaha..mtoto kama baba, umalaya,
na sasa mnagombea mali ya dhuluma eeh, nina uhakika kuwa dhuluma hiyo
itawapeleka pabaya...na mwisho wake umeshafika, ..wewe njoo nakusubiri kwa hamu..’nikasema
‘Nini…!!1,…ina maana kweli unanitaka eeh, unasikia sikutaka kuja
huko, lakini kama kweli utanitimizia ombi langu, mimi naweza kuja kwa ajili
yako tu, sio kwa…na sikiliza kama unataka nije kwa ajili ya kupambana na
wewe..hilo mimi hunitishi, sikiliza nina uhakika ni wewe umezima hiyo mitambo,
sasa..ngoja tuone,….’akasema tamaa zake za mwili akazitanguliza mbele, na
alipogundua kuwa mimi nina maana gani ndio akasema hivyo.
‘Ni hivi baba yako
ameshakushitukia, kuwa wewe unanitaka na mimi, pili wewe una tamaa, na tatu,
hufai kwenye uongozi wa familia, kwahiyo kuanzia sasa ujue wewe huna chako
....’nikasema
‘Nini,..haa, unasema nini, tutaona…’ akasema sasa kwa hasira,
nikasikia sauti ya kike ikisema;
‘Kuwa makini…’
‘Ndio hivyo…sasa uje usije, huna maana kwake kwa sasa…’nikasema na
mara nikasikia akikata simu kwa hasira
huku akisonya.
NB: Je huyo jamaa alifika? na kama alifika kulitokea nini na
je ombi lake lilitimizwa,ni nini kitatokea kwa Makarasha, tuonane kwenye sehemu
ijayo ya shahdii huyu muhimu aliyekuwa karibu na Makabrsha..ambaye ni marehemu!
WAZO LA LEO:Tuwe
makini na malezi ya watoto wetu, kama tunafanya shughuli zisizo na manufaa kwa
watoto wetu kwa maisha yao ya badaye, ni bora tusiwahusishe. Tuwajengee watoto
wetu misingi mema ya maisha yao ya baadaye, tukikwepa makosa tuliyoyafanya, ili
wao waweze kuishi maisha bora, na kujenga kizazi bora cha baadaye.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment