Shahidi akaendelea...
Namkumbuka sana Marehemu kwenye kauli zake,
aliwahi kuniambia hivi;
‘Katika hii dunia, kila mtu na hamsini zake, kama una uwezo wa
kufanya hivi, na ukapata, basi fanya, kama kuna sehemu unaweza kuitumia kama
ngazi ili na wewe ulipate tunda fanya hivyo..mimi maadui zangu wakubwa ni
wakubwa, matajiri, hawa tutapambana nao hadi kifo..
Najiuliza tu , kwanini sasa polisi wanahangaika na watu wa chini,
wakati, kwa mujibu wa kauli ya huyu mtu yeye maadui zake wakubwa ni watu
wakubwa, matajiri, watu wenye nyazifa eeh, hao ndio wanaoweza kumuua, au sio,….
Yeye alifikia kutuambia, sisi tumekubali kuolewa na matajiri, sasa
tuamue moja, kuwa na yeye kupambana na mafisadi wadhumulaji, kama alivyowaita
yeye, au kuwa upande huo wa hao watu, anasema anapambana nao…kama
hatutashirikiana naye basi tupo upande huo…kama tupo huko, basi tutakuja kupata
shida, na tutakuwa miongoni mwa wasaliti wake.
Unajua huyu mtu, yeye pamoja ya yakuwa kasoma sana sheria, aliamua
kuigeuka sheria, au kuitumia sheria atalavyo yeye, au sio, kwa maneno yake ni
ili kwuasaidia wanyonge, ... akachanganya na ujanja-ujanja wake eeh, hasa
aliousoma vitabuni, …akakaa na kubunu njia zinazojulikana kama blackmail.Sijui
tafsiri yake ni nini kwa Kiswahili, ....’akasema na kumwangalia mwenyekiti.
Watu kama hawa wapo wengi, wanaishi kiujanja ujanja, wanakuja
kwako, wanakupima udhaifu wako, wanakuona una njaa kali, wanaanza kupenyeza
sera zao, na nyie bila kujua…maana keshawasoma, mnakuja kukubaliana naye.
Ndio maana dunia ya leo
imejaa vita unahisi ni kwanini..ni watu walishaumia, walikuwa wanasubira
kisingizio tu, ili waweze kuzitoa hasira zao..hili watu hawalioni..hivi ni
visasi kutoka ndani ya mioyo ya watu waliokuwa wakilalamika, wakisononeka, na
mtu wetu akaamua kuwasaidia kwa kuchukua kutoka kwa matajiri kuleta kwao,
Swali hapa iweje sasa, hao wanaotaka kusaidiwa ndio wawe wauwaji,…maana
polisi hadi sasa kwa ushahidi wao, wanaoshukiwa ni watu wa aina yetu, sio haooo
een maadui za marehemu,…
Nimepata muda wa kuishi na
marehemu na amekuwa kila siku akinihubiria ili nibadilika ili niwe kama yeye,..huyu
mtu ni mjanja kwenye ushawishi..
Siwezi kulikataa hilo, … ilifika mahali na mimi nikajenga chuki
nikiona ukweli ulivyo,kuwa hayo anayoongea yana namna ya ukweli fulani…
Hata hivyo kiukweli wangu, sikufikia hatua ya kutaka kuua, naogopa sana
kumwaga damu ya mtu asiye na hatia, na ikizingatia kuwa mimi nimejifunza
uaskari, na moja ya nidhamu ya uaskari, ni utii wa sheria bila shuruti,
kuwalinda raia wema…sasa kwanini leo mimi niwe mshukiwa, sawa yawezekana,
lakini kuna sababu au sio, ....
‘Nafahamu wengi watanishangaa, nikisema nimejifunza uaskari, naomba
mlielewe hivyo, na mlichukulie hivyo hivyo…’
Ndio maana nikatoa ombi kwenu, kuwa haya nitakayo yaongea hapa,
yaishie hapa hapa,, tukitoka hapa, kila mtu na hamsini zake, hayo mengine
waachieni wahusika, wanajua ni nini wanachokifanya, lakini kama mtu atajitia
kidomo domo, ....sawa nitakamatwa, kama mshukiwa, wa mauaji, lakini je ni kweli
nilifanya hivyo...?’ akageuka kuwaangalia watu.
Nafahamu mpaka hapo nimewachanganya watu…mmh…, maana mlitaka msikie
mnachokitaka nyie,..jibu la moja kwa moja ni nani muuaji, au sio.. lakini huko
siwezi kufika hara hivyo, ninachotaka kwanza, muone tukio zima, ili nyie
wenyewe mje kumpata muuaji halisi…..’hapo atakatulia kidogo akiwaangalia
wajumbe.
**********
‘Sasa naomba nianze maelezo yangu kwa jinsi ilivyokuwa ....’akamuangalia
mwenyekiti
‘Natumai kwa hivi sasa hakuna pingamizi…’
Alimuangalia mwenyekiti, mwenyekiti alikuwa katulia, kwa haraka akamwangalia
mume wa familia ambaye naye alikuwa sasa kageuza kichwa nyuma kumwangalia huyo
mdada anayeongea kwa hamasa, maana muongeaji alikuwa kiti cha nyuma cha mume wa
familia, kiukweli hapo alipo, alikuwa kama haamini macho yake kwa kile
anachokiona, kweli huyo mdada ni yule yule anayemfahamu yeye, au ni mwingine.
‘Ni hivi , kiuhalisia,..Mume
wa familia alikuwa ameshapona muda mrefu tu,…’akasema hivyo, wajumbe
wakawa kimia
‘Sio kupona kwa vile,… hapana, bado likuwa na majereha, unajua ile ajali
ilikuwa ni kubwa sana,..lakini sio kivile alivyokuwa akijionyeshea, mtu mpaka
kubebwa, ..na vitu kama hivyo,… kuna muda alitakiwa aigize, ili kukamilisha
mambo fulani fulani, hiyo ikiwa mipango ya Makabrasha…’akasema
‘Mume wa familia aliambiwa hilo ni kwa manufaa yake yeye mwenyewe
ili mambo yakamilike kwanza kwani akiwa amepona, basi atakuja kukumbuna na mkataba
wao, ambao ungemuhukumu kama mkosaji, mvunjaji wa sheria, kama walivyokubaliana
kwenye mkatana wao, si mshapata picha ya mkataba wao ulivyokuwa…’akasema
muonegaji kama anauliza wajumbe.
‘Ukiangalia ni sawa, maana yeye alishaharibu, alishavunja mkataba
au sio, kwa mujibu wa mkataba wao…na ili mkewe aendelea kuwa upande wake ni
yeye aendelee kuwa mgonjwa, umeona hapo walivyocheza…kwa hali hiyo mume wa familia
hakuwa na jinsi, ilibidi akubaliane na mtalaamu,, la sivyo ndoto yake ya muda
mrefu ingelifutika..
Kiukweli mimi nilikuwa naumia sana, maana hayo yanavyoendelea
nayaona, nayasikia, japokuwa nilijitahidi nisiyaingilie kiundani wake, …unajua
tena, na mimi nilikuwa na yangu kwa upande wangu, kama nilivyosema huyu mtu
alitunasa, na akawa anamvuruga kila mtu kwa upande wake..
Sasa tuende kwa huyu
marehemu,…
Mimi nikawa nimepewa kazi ndani ya ofisi ya Makabrasha, nikiwa
kama muhudumu wake maalumu, lakini nia na lengo lake ni lile lile, sisi, au
mimi niwe karibu naye, nisije nikaharibu mipangilio yake, kwahiyo nikawa
napangiwa kazi hata za usiku, hizi kazi za usiku, eeh zilikuwa na mambo yake…ujue
awali nilikuwa nafanya kazi huku na kule, yaani kwa bosi wangu na kwa huyu mtu.
Bosi wangu alikuwa halifahamu hilo…
Sasa siku zilivyokwenda ndio nikawa sasa nafanya kazi kiukweli
ukweli chini ya Makabrasha…, sio ile kama kibarua tena wa kazi maalumu za siku
moja moja… utaniuliza nilikuwa nafanyaje kazi kama hizo hata za usiku huku nipo
ndani ya ndoa yangu. Mume wangu hafahamu…
Kumbuka kuwa , kwa muda fulani, mimi niliaga kwenda kijijini,
kabla ya kuwawa kwa Makabrsha, ilikuwa nfanya hivyo kila mara kukiwa na kazi
maalumu za muda naaga kuwa nakwenda kijijini kwetu,…nikawa naenda na kurudi,
najua mwenyewe jinsi gani nilikuwa nafanya,..hata marehemu alikuwa nimeaga kwa
mume wangu kuja kwake, kipindi hicho za kazi za siku moja moja,…ila kipindi
sasa nipo kwake, nilimuelezea hali halisi, akaelewa.
Na hata bosi wangu hakuwa anafahamu hiyo kazi yangu ya muda kwa
makabrasha, na hata ikafika muda, kwa mujibu wa Makabrsha niache kazi nyingine
zozote nilizokuwa nafanya niwe namfanyia yeye kazi tu..ndio nikaomba kuacha
kazi kwa bosi wangu, na nilipoacha kweli nilikwenda kijijini nikaweka mambo
yangu sawa, sasa nikarudi jijin nikiwa mtu mwingine..
Na kwa muda huo sikuwa nawasiliana sana na mume, kiukweli
nilimtesa sana, hakuwa na raha akiniona
jinsi nilivyo..kwahiyo hata nilipomuambia kuwa nakwenda kuishi kijijini,
hakukataa, mume wangu alitaka niwe na raha, niwe na uhuru, niweze kubadilika,
niweze kuondokana na ile hali anayoniona nayo, mawazo…sina amani.
Hadi hapo utaona kuwa kazi
ndani ya himaya ya Makabrsha ilishaanza
siku nyingi hata kabla sijamuandikia rafiki yangu barua ya kuacha kazi kwake.
Kuacha akzi nyingine, shughuli nyingine, ilikuwa moja ya mikakati
ya Makabrasha ili aweze kuwa karibu nami, ili awez kunitumia, hakujali kama
nitavunja ndoa yangu au la. Na nataka muelewe hili, kuwa Makabrasha hakujua
undani wangu na rafiki yangu kuwa nafanya kazi gani kwake, alijua kuwa nafanya
kazi za kutangaza biashara zake tu, kiukweli kinje ndivyo nilivyokuwa
najulikana hivyo.
Kwahiyo sasa rasmi nikaingia ndani ya jengo ambalo hata mimi sikulifahamu
hivyo lilivyo kwa huko ndani, kuwa hilo jengo kwanza llikuwa likimilikiwa na
marehemu, na humo ndani kuna mambo mengi ambayo hayajulikani kwa watu wa nje,
na hata humo kuna wapangaji wa ofisi hawajui kinachoendelea huko chini, kuna
ofisi za chini kwa chini, chini ya ardhi….
Wakati naingia humo, mipango mikubwa ya Makabrsha ilikuwa tayari
imeshakamilishwa, mikataba imeshabadilishwa, na mikataba mipya imeshatayarishwa,
na kuwekwa inapostahili, sasa Makabrasha akaanza kutoa makucha yake,
akatayarisha mikataba mingine mipya ya kumuhalalisha yeye kama mumiliki mkuu wa
baadhi ya makampuni likiwemo hilo la mume wa familia, lengo limashafikia
penyewe, sasa Makabrsha sio yule wa zamani tena, mnanielewa hapo….
Hadi hapo, mume wa familia,
alikuwa hana nguvu tena, kwani alishawekwa kwenye mikono ya Makabrasha. Kashfa
nzito ilishajengwa hata kwa kizazi cha mke wa familia, japokuwa familia ya mke
ilikuwa bado gizani, haifahamu kinachoendelea, na ndilo lengo…na kiukweli hiyo
kashfa ilivyotengenezwa kama ingevuja,.. basi,.. hata kizazi cha mke wafamilia
, kwa mzee hapo, ingeliharibu jina , na mambo ya kisiasa yangeliharibika
kabisa..
Marehemu hakutaka kuifikisha hiyo kashafa haraka kwa adui wa mzee,
yeye alitaka kuitumia hiyo kashfa kwanza kwa masilahi yake, baadae ikibidi ndio
angeuvijisha, na hapo siju….
Ndio maana mume wa familia akawa anauma hilo kwa magego, sio kwa
ajili yake tu bali pia kwa ajili ya familia nzima ya mkewe, japokuwa chanzo cha
hiyo kashifa ilitokea kwa mume wa familia….mnaona ilivyo…sio kitu kidogo….
Kabla sijafika huko kwenye mpango rasmi…
Nikisema mpango rasmi, ina maana mpango ambao ndani yake
ilipatikana kifo cha Makabrsaha, huo mpango sikutakiwa kuu-ongelea hapa, au
kuongea lolote kuhusuiana na huo mpango,….huo mpango natafutwa nao, na kama
nafahamu lolote nipo hatarini..
Walitaka kuniua…hahaha, lakini mungu ni mkubwa,…polis
wakavumishiwa kuwa ni watu wanaotaka kulipiza kisasi cha marehemu,..sio kweli
jamani, ni kwa vile mimi ndiye ninayefahamu kila kitu…
Sasa huo mpango umetumika
kama ushahidi,… lakini katika namna ya upotoshaji, kwa namna maalumu..ndio
maana mimi nataka niongee hapa kila kitu jinsi ilivyotokea, ili kama ni haki,
basi haki kweli ije kutendeka..
Sasa kama mimi ndiye muuaji, au sio…nataka niwajibike kiukweli, na
nyie mkiwa mashahidi, na kama yupo mwingine aliyeshirikiana nami, basi
atanifuatia, au sio…nataka hili niliondoe kwanye nafsi yangu ili niwe huru…
Sasa.., ngoja niwarejeshe kwenye mazungumzo yangu ya mwisho na
mume wa familia; nawarejsha huko maana hayo mazungumzo ndio ushahidi mkubwa wa
polisi, huo ndio ushahidi unaowafanya mpaka sasa watuone sisi kuwa ndio wauwaji,
labda, ni kweli, labda sio kweli, mimi sitaki nijihukumu, nataka nyie na baadae
mahakama ije inihukumu kihalali, au sio…
Sasa tuwe tayari, na huu ushahidi…mimi nitauongea, ila ..kila kitu
kipo kwenye video, utayasikia haya nitakayoyaongea, video hiyo imechakachuliwa
kuna mengine hayapo……
**********a
‘Ina maana wewe hadi hapo umeshakubali kuwa wewe utakuwa mtumwa wa
Makabrasha wa kudumu…?’ nikamuuliza mume wa familia
‘Nitafanya nini kwa sasa, huyu jamaa ana siri zangu nyingi, ana
mambo yangu mengi, ambayo akimuonyesha mke wangu au wakwe zangu, nitafukuzwa
kama mwizi, kwahiyo inabidi nimkubalie kila kitu...’akaniambia na mimi nikawa
sina njia ya kumsaidia. Mimi nikamwambia
‘Kwa usalama wako ni bora ufanye hivyo maana humjui huyo mtu
alivyo, huyo mtu kwa namna nyingine ni mbaya, anaweza kuyafanya hayo, na
akahakikisha unazalilika mpaka utatamani kujiua,..lakini usichoke mimi nipo
nyuma yako maana pamoja na hayo namfahamu vingine alivyo..’nikamwambia hivyo.
Mimi nilishaamua kuwa nilimalize hilo, kwani kama nisipofanya
jambo, hali hiyo itaendelea kututesa katika maisha yetu yote, tutakuwa watumwa
wa mtu mmoja, na hata kama tutaendelea kuishi kwenye ndoa zetu, itakuwa ni ndoa
ya jina tu,..
Kwa mfano mimi nilitakiwa kumtii huyu mtu kama mtumwa wake, kila
anachokitaka nimfanyie, hata kuzalilika, sasa kulikuwa na manufaa gani hapo,..na
nitazalilika hivyo mpaka lini,..hata hivyo,..basi tena,.. nikaona nijitolee tu
muhanga, nifanye kazi yangu, nitimize wajibu wangu, ili kulimaliza hili tatizo
kabisa, lakini kwa vipi kwa mtu kama Makabrasha, wanasema mtu mwenye tabia hii
kamwe haiachi labda auwawe…’akasema na kutabasamu.
‘Usijali, mshirika, mimi nitajitolea kwa ajili yako....kama
utanikumbuka sawa, nafanya haya kwa vile nakupenda, japokuwa penzi kwako kwangu
kwa hivi sasa halipo tena, siwezi kukulaumu, japokuwa, inauma sana,....nimeshakuona
kuwa wewe unanitumia ili upate unachokitaka, huna tofauti na
Makabrasha...’nikamwambia siku hiyo.
‘Kwanini unasema hivyo, mimi mbona nakupenda sana, umeshasahau
tulivyoahidiana kule kijijini...kwa hali niliyo nayo, nashindwa kutimiza ahadi
zetu zote, unafahamu ni kwa nini…wakati mwingine haya yanayotokea ni kwasababu
nashindwa kuvumilia,..hata mimi nateseka kwa hilo nawaza sana, ..wewe hujui tu,
ndio maana naamua kunywa kupoteza mawazo…sasa yametokea haya ya kutokea,
sikupenda..ila nasema mimi ninakupenda, lakini kwa hali kama hii tutafanyaje,....’akasema
‘Najua..’nikasema
‘Wewe huoni sasa naumwa, na pia natakiwa niumwe ugonjwa wa
kuigiza,…lakini hata bila kuigiza kuumwa..kuumwa bado kupo, hali niliyo nayo sio rahisi kuelezea, wakati mwingine
nashindwa hata kuelewa mimi ninaumwa nini hasa..’akasema
‘Si umeumia, kwani hilo halijulikani..’nikasema
‘Aheri ya kuumia viungi kuliko kuumia moyoni, wewe hujui tu, aheri
ya kuumwa magonjwa yanayojulikana, kuliko kuumwa magonjwa yasiyojulikana,
nateseka tu wewe hujui..kichwa akili wakati mwingine inakuwa sio ya
kwangu..mimi hata sijui nimekuwaje…’akasema
‘Kiukweli kwa vile nampenda huyu mtu, iliniuma sana alipoongea
hivyo, siku ile nakumbuka nilitaka niongee na docta nijue huyu mtu ana tatizo
gani, sikuweza..kutokana na muda, lakini akilini nilihisi huyu mtu kuna kitu
kafanyiwa tofauti na matibabu yake..
‘Mimi nakuambia ukweli, hapa nilipo, siwezi kujijua naumwa
nini..lakini naahidi mimi nikipona tu na yeye akifanikiwa alivyopanga iwe,
nitatafuta njia ya kumkomoa, tutarudisha mali yetu yote...hata kama nikwa
kumua, mimi nitamua kwa mkono wangu.., sitaogopa hilo, maana yeye mwenyewe
hatujali, wewe huoni hilo…’akaniambia hivyo.
‘Chunga huo ulimi wako, …kauli yako hiyo ikisikiwa na wenyewe, itakuwa
ushahidi, hata akitokea huyo mtu akauliwa na mtu mwingine, wanaweza kutumia
kauli yako hiyo kama ushahidi …usipende kuropoka ropoka kauli kama hizo ovyo…’nikamkanya
hivyo.
‘Sawa mpenzi..nimekuelewa…’alisema hivyo huyo mume wa familia
Nayazungumza haya maneno alivyoyatamka bila kuficha kitu…maana
haya mazungumzo yapo kwenye ushahidi walio nao polisi! Ina maana hadi hapo
polisi wamesharizika kuwa wameshampata muuaji tayari, sasa jiulize kwanini
wamechukua muda kumkamata huyo muhusika, na kila kitu wanacho,…wanashindwa
kufanya hivyo kwasababu bado kuna utata au sio, hiyo pekee haiwezi kuhalalisha
kuwa yeye ni muuaji, ..lakini sio hivyo tu, tuendelee na haya mazungumzo kama
ushahidi wa polisi…
Kuna kitu wanakiitai …’motive’
au motisha wa kuyafanya hayo mauji…ni nini ..huyu mshukiwa ana kitu gani, cha
kuweza kuyafany haya, maana aliyemuua Makabrsha lazima ana jambo, je huyu mtu
ana jambo gani dhidi yake…hicho ndicho walikuwa wakikitafuta, je
walikipata,..sasa wakati wanatafuta wakajikuta wanapata taarifa nyingine za
utata!
Mwenyekiti nisamehe hapo kidogo, nitaendelea kutoa maelezo
kutokana na ushahidi wao kwa manufaa yetu na hata kwako pia..…
Alipozungumza hivyo, awali mwenyekiti alitaka kumzuia lakini
baadae akaonekana kutulia akamuangalia tu huyo muongeaji…kiukweli mwenyekiti
alionekana kuwa na wakati mgumu, nafikiri ni kutokana na huo mkanganyiko wa
ushahidi…
Wakati nipo naongea na mwenzangu,
tunamuongelea Makabrasha niliwahi kumwambia hivi
‘Kwa hivi sasa hatumuwezi tena Makabrasha, huyu jamaa keshajizatiti,
na kiukweli kama akiendelea kuwepo duniani, sisi tutaendelea kuwa watumwa wake,
na hata ndoa zetu hizi sizani kama tutaweza kuishi kwa amani na furaha..’niliongea
hivyo
‘Ni kweli, sasa ..oh, … mimi naona..tumuue huyu mtu,..hakuna
jinsi..’yeye akasema hivyo.
‘Nimeshakuambia, achana na hiyo lugha yako,…’nikasema
‘Sasa hebu niambie, utawezaje kuishi kwa amani kama huyu jamaa
kila siku anatutushia amani..na ukumbuke hadi sasa huyu jamaa yetu ameshafanikisha
mambo yake…’akasema
‘Bado wewe hujakamilisha na wewe ukikamilisha tu, kila kitu
kimeshawekwa mikononi mwake, na wewe itabidi utii amri kutoka kwake, kwahiyo
nafsi iliyobakia ni kupitia kwako, utafanyaje sasa…’nikamwambia.
‘Sawa nimekuelewa..hata hivyo sitaweza kumkatalia, maana
nikimkatalia itakuwaje, labda hapo hapo nifanye jambo,…iwe mwisho wa haya
yote,..au nitumie hiyo silaha, kum-maliza..japokuwa naogopa mimi…kwani
nim-maliza watu watajua, eeh, mimi naumwa nipo hospitalini…au nimtafute mtu,
anifanyie hiyo kazi, unasemaje..au sasa hebu nishauri, tutafanyaje kwa hali
kama hii..?’ akaniuliza
‘Sasa hivi unaniuliza eeh, tutafanyaje…, kamuulize
Makabrasha,…’nikasema hivyo.
‘Kwanini unasema hivyo, wewe ulitaka nifanye nini mimi…huoni hali
tuliyo nayo,…mimi nikijulikana tu, kuwa wewe na mimi kitu kimoja, unafikiri
itakuwaje, lakini Makabrasha anafahamu kila kitu ana ushahid wa kutosha, huoni
kuwa keshatuwahi, tufanyeje sasa…’akasema
‘Nakuambia haya kwa vile tokea awali nikikushauri, eeh… utulie,
tuwe makini, ukawa hunisikilizi, sasa hivi yamekufika shingoni unaniuliza
tufanye nini, mimi sijui la kufanya hadi sasa, kiukweli ndio hivyo, mipango ipo
mingi, lakini …siwezi ..nina wakati mgumu sana…’ nikasema nikionekana kuwaza.
‘Tusikate tamaa au sio..’akasema
‘Kiukweli ninachoweza kusema niliyo nayo mimi mwenyewe ni mazito
zaidi ya haya unayoniuliza wewe tufanye nini… kwahiyo kwa hivi sasa niache kwanza
na yangu, wewe endelea na Makabrasha wako, yeye si ndio wakili wako, na yeye
ndio bwana wako, nikiwa na maana wewe ni mtumwa wake..si ndio hivyo, k.’nikamwambia.
‘Hivi wewe unajiamini nini , wewe unafahamu vyema huyu mtu alivyo,
bila ya mimi na wewe kushirikiana, hatutafika popote, njama zake ni
kututengenisha, kutokosanisha…sasa mimi nakuonya kama una jambo dhidi yake,
unataka ulifanye kivyako, utakuwa unajitakia matatizo,achana na huyo
mtu....’akasema.
‘Mimi ni askari, ninafahamu ni kitu gani ninachokitaka kukifanya,
ninachohitajia kwa hivi sasa ni silaha tu,...sina silaha,na sitaki kuazima
silaha kwa aliyekuwa bosi wangu, nimeshaacha kazi kwake, na nataka iwe hivyo,
mhh...’nikamwambia.
‘Wewe ni askari!!!?...’akasema hivyo kwa mshtuko..
‘Ina maana zile ndoto zako umezifanyia kazi, hahaha siamini,..sio
kweli, bado wewe unaota ndoto zako..usidanganyike , kazi hizo hazikufai, wewe
ni mwanamke, ukijiingiza huko, utajiharibia maisha yako, na hivi, huo uaskari umejifunzia
wapi, hahaha…unafikiri uaskari ni mchezo eeh….’akasema kucheka sana..ukumbuke
haya yote yalikuwa yakirekodiwa na marehemu.
Nazungumza hapa nikiwa naangalia huo mkanda uliorekodiwa na
marehemu ambao sasa upo mikononi mwa polisi…
‘Kusema mimi ni askari sina maana ya kuwa mimi ni polisi, huoni
mitaani kuna migambo, usalama shirikishi, hayo yawezekana au sio, na mafunzo ya
hapa na pale yamenifanya mimi nijiamini hivyo, kuwa mimi ni askari ..’nikasema
‘Sawa vyovyote iwavyo, usije kujilinganisha wewe na Makabrasha, kuwa
utaweza kupambana na yeye, yeye kijizatiti kwa kila hali, unamfahamu alivyo,
sio...’akasema
‘Hahaha, mimi ndio nikukanye wewe , maana mimi namfahamu zaidi ya
unavyomfahamu wewe, nikuambie ukweli…’nikasema
‘Hahaha wewe mwanamke, haha,
yule ni rafiki yangu, tumakulia pamoja japokuwa ni mkubwa wangu, na mara nyingi
nikikwama nakuwa naye, hadi sasa, useme mimi simfahamu,….wewe ndio humfahamu
unaigiza ndoto zako tu, haya niambia lini umejifunza kutumia silaha?’
akaniuliza.
‘Mimi nafaham kutumia silaha kama unvyofahamu wewe kutumia kijiko
wakati wa kula,...’nikasema kwa mbwembwe , na yeye akaniangalia kwa macho ya
mshangao, nikaendelea kumwambia;
‘Nipe hiyo silaha uone nitakavyoitumia, hilo kwangu ni dogo sana,
na cha muhimu kwa sasa ni mimi kuipata hiyo silaha, sio jinsi gani ya kuitumia
au kutaka kujua nilijifunza wapi kutumia silaha, huu sio wakati wa kuulizana
hayo, ...cha muhimu kwa sasa ni muda, tunakimbizana na muda, sitaki huyu mtu
aendelee kuwatesa watu...’nikamwambia.
Hapo akatulia kwa makini, baadae akasema;
‘Mhh, haya,... ndio maana kila mara upo na rafiki wa mke wangu,
najua ni yeye kakufundisha ujinga huo.., lakini uwe makini na silaha,
mimi sipendi sana kushika shika silaha, sina ujanja huo...’akasema.
Haya wajumbe kwa polisi
hadi hapo wanaweza kumshuku tena huyu mtu, eeh, keshatoka hapo, kwa maneno
hayo, sasa endeleeni kuyashika hayo mazungumzo, ambao ndio ushahidi wa
polisi,.. awali muhusika alionekana ni mume wa familia, sasa uhusika wa mauaji
unamtoka, ni nani mwingine
Kwa kauli zangu niliwahi kusema , …najua kutumia silaha,..mumeona
hapo, pili natamani huy mtu afe akiendelea kuishi ni shida, au sio…nataka
nielezee kila kitu kama ushahidi wa polis ulivyo, ili nikitoka hapa na
kufikishwa kizimbani mje kuwa mashahidi wangu…kwa vile nastahiki au
sio..niendee au nisiendee…’akasema akimuangalia mwenyekiti.
Mwenyekiti alibakia kimia, hakusema neno, ila wajumbe kwa pamoja
wakasema.
‘Andelea, endelea..’wajumbe wakasema.
**********
Hapa bado nipo na mwenzangu
tunaongea,…kama ushahidi wa polisi ulivyo….
‘Mimi ninahitaji sana silaha kipindi kama hiki, lakini sitaki mtu
afahamu kuwa nina silaha,..hasa rafiki wa mke wako, na nimekuambia haya tu, iwe
siri yako, mimi nitamuwinda huyu mtu hadi kieleweke,…’nikasema
‘Mhh..haya bwana…’akasema mume wa familia
‘Kwa hivi sasa nahitaji sana silaha, na tatizo ni muda, ningeenda
kuazima kwa watu wangu ninaowafahamu, japokuwa sipendi iwe hivyo, lakini muda,…na
mimi sitaki ushahidi zaidi kwa watu wengine, nikiazima kwao, utakuwa ni
ushahidi , na kwa hili sitakie liwe hivyo…hapo nje wapo watu walionileta wananisubiria.’nikamwambia.
‘Oh, nimekumbuka jambo, ..unajua sisi tunayo silaha, silaha ya mke
wangu,…’akasema
‘Mhh..kweli,..lakini utaipataje..?’ nikamuuliza
‘Mimi ninaweza kukupatia hiyo silaha sio kazi kubwa kwangu, nina
ufunguo za makabato yote hadi hivi sasa…lakini mimi najiuliza tu, …nina
wasiwasi na hilo, wewe unahitajia silaha ya nini, unataka kumuua nani,
usiniambie umefikia hatua ya kutaka kumuua Makabrasha?’ akaniuliza kwa mashaka.
‘Hahaha, mimi sio muuaji bwana, ..na wala ….mimi sitaki kumuua mtu
yoyote, na sina mpango huo, ila ikibidi..sitasita kufanya hivyo kwa
kujilinda,..au ikibidi sana, kama ni lazima nitafanya hivyo kwa masilahi ya
wengi, ni bora nifungwe lakini wengi wawe huru au sio….’nikasema nikiwaza jinsi
gani ya kumfamisha mtu kama huyo.
‘Hapana hadi hapo unanipa mashaka..’akasema
‘Silaha ni muhimu sana kwangu kwa hivi sasa, kuliko wakati
mwingine wowote…’nikamwambia hivyo
‘Nakuomba tafadhali usije ukafanya makosa kama hayo, nakuhitajia
sana katika maisha yangu, na ukumbuke mimi ndio wewe na pendo letu ni la asili
haliwezi kufutika abadani…sisi ni kama mapacha kwenye pendo,…’akasema
akiniangalia kwa macho yaliyojaa huruma.
‘Mimi siwezi kufaya kosa kama hilo, niamini, mimi siwezi kuua,
nitafanya hivyo, ikiwa ni lazima, najua sheria, najua ….na kwanini niue, kama
ningelitaka kufanya hivyo ningelishafanya hilo jambo mapema sana, ...’nikatulia
na yeye akainamisha kichwa chini…hayo mtayaona vyema kwenye ushahidi, ..naongea
kama ilivyo
‘Sawa…naombea iwe hivyo…’akasema
‘Mimi nahitajia hiyo silaha kwa ajili ya kujilinda mimi mwenyewe,
na zaidi ni katika kujihami..na sio kwa muda wote, ni kwa muda maalumu
tu,..kwahiyo muda wake ukifika, nikiwa na hiyo silaha nitakuwa na amani sana,
ninakuwa kama nina wasaidizi watano nyuma yangu, ..’nikamwambia na nikweli
nikiwa an silaha, hunibabaishi, wanaonifahamu wanalijua hilo.
‘Unasema hiyo silaha ni kwa ajili ya kujihami, lakini hapo mimi
nahisi kuna kitu kikubwa unataka kukifanya, wewe unanificha, …sikiliza
sitapenda nije kusikia jambo kubwa limekutokea, nitajutia sana, na huenda na
mimi, nikajiua…’akasema
‘Kuna jambo nataka kulifanya usiku wa leo, na asubuhi yake, ni
muhimu sana niwe na wasaidizi wangu, na wasaidizi wangu ndio hiyo silaha..kama sitapata
silaha, sitawezi kulifanya hilo ninalotaka kulifanya..huyu jamaa yetu kajizatiti
kweli kweli, ana walinzi, ana mitandao ya ulinzi, ana mitambo ya ulinzi,..
kwahiyo hata nikiwa na silaha,…najiuliza nitafanya nini nayo, unaona hapo,
kwahiyo kama ni kwa ajili ya kumdhuru huyo mtu, hilo mimi siliwezi....’nikamwambia.
‘Naona wewe unalako jambo, na kwa huyo mtu, wewe utajitakia
matatizo makubwa, nahisi wewe hujamfahamu
Makabrasha vyema....na nikuulize hivi yule mtoto wake mkorofi si bado
anafika fika hapo kwa baba yake, je huyo mtu utawezaje kumdhibiti….maana yule ni
kichaa, eti kasomea sheria, mbona haviendani! ...’akasema
‘Umeona eeh..huyo huyo… mtoto kama baba,..’nikasema
‘Kwahiyo kumbe unataka kumuua huyo mtu…’akasema
‘Hapana, nani kasema nataka kumuua mtu,…nielewe mimi hapo, sina
haja ya kumuua mtu, sio kazi yangu kufanya hivyo,..kwani mpaka sasa
nimeshajitolea kiasi gani, kama ningelitaka kufanya hivyo, nisingejizalilisha
hivyo, unasikia, mimi naweza kufanya lolote, lakin kwanini nifanye hivyo,
hapana....’nikasema
‘Sasa haya bwana,….maana ni kweli hadi sasa tulishaamua kuwapa
kila kitu, ili tu..wasije kutuchafulia majina yetu, na sipendi kwakweli, lakini
hakuna jinsi, wa kulaumiwa ni sisi, najua kabisa,wakwe zangu watakuwa
wanasubiria hili kwa hamu, nifukuzwe kama mbwa, maana, ushahidi upo..ndio maana
nasema ni heri kujitolea hivyo kwasasa, huku tukitafuta njia muafaka, au sio…’akasema
‘Umeonaeeh, nashukuru sasa unaanza kunielewa, kuwa tatizo ni wewe,
wewe ndio mkosaji ,…’nikamwambia.
‘Sote ndio sababu ya haya yote…huo ndio ukweli..’akasema na mimi
hapo nikabakia kimia, akaendelea kuongea.
‘Sawa waweza kusema mimi ndiye nimewakose watu hao zaidi…najihisi
kuwa mbaya kuliko…, sijui kwanini,..hivi kweli ni kwanini..kwanini mimi nakuwa
na tamaa kupita kiasi, nilikosa nini,..mmh, haya yote yasingelitokea,…’akawa
anaongea kwa kujijutia, lakini baadae nikasikia akisema
‘Hata hivyo…kiuhalisia mikataba ile inanipa nafsi nyingine ya kufanya
jambo, huenda nikashinda, unajua huo mkataba, unanipa mimi mamlaka ya kufanya
kila jambo, kama mume wa familia....’akaniambia.
‘Upi huo..huo wa kugushi au,…hahaha, unafikiri mimi sifahamu janja
yenu..’nikasema
‘Mimi sijui kama ni wa kugushi..’akasema
‘Haya sawa, vyovyote iwavyo, lakini wewe hujaliangalia hilo kwa
mapana yake, hapo ulipo kwa lolote utakalolifanya kwa sasa, bado upo kwenye
matatizo, hasa ya ndoa yako..’nikasema
‘Sawa lakini kwanini tusjaribu kwanza…’akasema
‘Tusi-au usi…mimi sihusiki na hayo mambo yenu,…kumbuka kuwa huo
mikataba wa kugushi eeh, ni danganya toto, si chochoteni swala la muda tu..na
hata hivyo hata ukiutumia je ni kweli utakuwa na amani na mke wako,
atakubaliana na hilo..kiukweli nakuambia hili unisikie, hutaweza kuwa na amani,
mke wako hataweza kutulia kwa hilo, na hataweza kukupatia hicho
unachokitaka,..yeye sio mjinga, ni lazima atahangaika mpaka aupate ukweli, je
huoni kuwa akiupata huo ukweli ndio itakuwa njia ya kuyabaini haya yote..na
huku kwa upande wa pili unakuwa mtumwa
wa Makabrasha, hatujui mwisho wake utakuwaje unaona ilivyo...'akasema.
'Ni sawa, ..sasa tufanyeje,…?’ akauliza na mimi nikakaa kimia,
akaendelea kuongea.
‘Ndio maana mimi ikifikia hapo, nasema bora tu iwe hivyo…nitakuwa
mtumwa wa Makabrsha sawa, lakini nitakuwa na mali, au sio..na nina uhakika itafika
muda, maana usinione nipo hivyo, natafuta njia, nahangaika lazima kuna namna na
yeye eeh…nitamnasa tu, najua ipo siku ataingia kwenye anga zangu, ipo siku, ni
lazima nifanye jambo, ngoja nione cha kufanya…’akasema
‘Hahaha, kwa Makabrasha..unajisumbua,…, hapo ulipo kila
unachokipanga keshakifahamu, kama mwanga vile… wakati mwingine huyu mtu simuamini
kama ni mtu wa kawaida, kila ukipanga
jambo analifahamu kabla..wewe hujaligundua hilo ...?' nikamuuliza.
‘Najua, yeye atakuwa kawekeza namna ya kupata
mazungumzo…alishawahi kuniambia hilo, ana vifaa vya kunasia sauti, na matukio…lakini
hataniweza ..hata mimi ni mjanja pia, wewe utaona tu ..’akasema kwa kujiamini.
'Haya bwana, ..hivi nikuulize kitu, hivi wewe unaifahamu vyema familia ya mke wako..walivyo
, wakwe zako,…achilia mbali utajiri wao, unawafahamu kuwa wanakuchunguza kila
mara, unafahamu kuwa wana namna zao za kugundua mambo, na huenda
walishakufahamu ulichokifanya?’
nikamuuliza
‘Nawafahamu sana, uzuri wao, hawahangaiki sana na mambo ambayo sio
muhimu kwao,…wanajifanya kufuata sheria,..zaidi ya hayo, kama ujuavyo wananichukia
sana..walifikia sehemu wakasalimu amri..na kuniheshimu kama mkwe wao…ndio maana
kwa hili nitajitolea kwa ajili yao, wananidai kwakweli, nijaitolea kuhakikisha
kuwa hii kashafa imefutika…’akasema
‘Mhh….sasa nakuona umebadilika, sawa..lakini umeshachelewa, familia ya mke wako, sio ya kuchezea, mimi
nimeshaichunguza vyema tu, ni heri ya huyu Makabrasha anayetumia njia za mkato,
lakini familia ya mkeo wako ni watu wa sheria…kumbuka hilo, umeshakiuka sheria,
na sheria ndio itakuhukumu..kwahiyo hadi sasa jihesabu kuwa sio mkwe wao tena,…’nikasema.
‘Haahaha…ndio hapo nakubali niwe tu mtumwa wa Makabrsha,
alichofanya namvulia kofia…sasa nikuulize hadi hapa ulitaka mimi nifanye nini…?’
akaniuliza
‘Hdi hapa umeshachelewa, kama ungelinisikia toka mwanzo, haya yote
yasingelifika hapa, tamaa zako za kimwili, na akili fupi ya kufikiri ndio
imekufikisha hapo ulipo, na hata sijui itakuwaje huko baadae, lakini acha iwe
hivyo upate fundisho, mtoto mwingine bila kumchapa hawezi kukua, na wewe bila
kuonja jela, sizani kam utaweza kubadilika…’nikasema
‘Usinizalilishe kihivyo…’akasema kwa hasira.
‘Huo ndio ukweli sio tusi, ,...sijui kama kweli haya yataisha kwa
amani, na hata yakiisha kwa amani, sijui kama ndoa yako itakuwepo tena, na baya
zaidi unaweza ukaishia jela, wakikuhurumia sana, watakutupa kijijini ukawe omba
omba...’nikamwambia.
‘Thubutu, hilo halitatokea..ndio maana nakuambia hadi hapa
namshukuru sana Makabrasha, kafanya nisichoweza kukifikiria,…ok, likitokea la
kutokea, basi utafanya nini,..lakini muhimu jitahada…mimi nina imani
tufanikiwa,...’akasema
‘Hahaha, unajipa moyo sio, utafanya nini wewe kufanikiwa hizo
ndoto zenu za mchana…....?’ nikamuuliza
‘Tuyaache hayo, kwanza hebu niambie hiyo silaha unahitajia ni kwa
makusudio gani hasa, ..kiukweli ukiniambia ukweli mimi nitakusaidia, kuipata
hiyo silaha, ila nina mashaka na wewe hivi kweli wewe unaweza kuitumia..?’
akaniuliza.
‘Ni kuhusu huyo mtoto wake, yeye ndiye namuogopa sana, anataka
kunifanya mimi kama anavyonifanya baba yake, siwezi kuzalilika kiasi hicho,
silaha itanifanya nimdhibiti...nataka silaha ya kujilinda..’nikamwambia bila
kumfafanulia mambo mengine ambayo niliyapanga kichwani mwangu,sikuwa namuamini
sana kwenye mambo hayo ya kivita..
‘Kama kweli unahitaji hiyo silaha kwa jaili ya kujilinda sawa…
mimi nitafanya kila mbinu hadi niipate hiyo silaha,..hilo niachie mimi ,
nitachukua silaha ya mke wangu…’akasema
‘Kwa vipi…?’ nikamuuliza
‘Kwa vile ni vigumu kutoka humu,…mimi nitamtumia mdogo wangu..ila
tukubaliane kitu…maana ujua hiyo silaha sio yangu, kwahiyo hiyo silaha itakuwa
inaletwa kwako usiku kama ukiwa na kazi za usiku, asubuhi tunairudisha mahali
pake..unasemaje kuhus mpango huo…?’ akaniuliza.
‘Kama unaweza kuipata hiyo silaha, itasaidia sana, nahitaji
kuwa nayo sanasana usiku wa leo, na asubuhi utakapokwenda kukutana na
Makabrasha, baada ya hapo inaweza isiwe na kazi tena, sitaihitajia kila siku
...’nikamwambia na yeye akaniangalia kwa mshangao, hakuamini kuwa mimi ninaweza
kutumia silaha.
‘Sawa hilo litafanyika, usijali..’akasema
‘Sikiliza kwa makini, kesho ukifika kuonana na Makabrasha,..’nikasema
‘Wewe umejuaje hilo..!!!?’
‘Hayo sio muhimu wewe kufahamu fanya ninavyokuagiza,
unasikia..’akasema
‘Ok sawa, wataka mimi nifanye nini…?’ akauliza
‘Mimi nataka wewe uwe unamchelewesha ili nipate muda wa
kusimamisha mitandao yake ya ulinzi, na ...kwa vile mtoto wake, atakuwa hayupo,
...kama alivyodai, japokuwa simuamini, ...nitaweza kufanya mengine bila
kujulikana, yote inategemeana na muda, muda ni kitu muhimu kwenye mapambano
kama hayo...’nikamwambia.
‘Kwani unataka kufanya nini, mbona unanificha, maana mengi
yameshafanyika, mikataba karibu yote nimeshaisaini kukubali, umebakia huo mmoja
tu,.....na wewe mwenyewe umeshasaini mkataba wako, kilichobakia ni mume wako
tu, na yeye nasikia alishakubali kuweka saini yake ..’akasema mume wa familia.
‘Mhh..hayo ya mume wangu achana nayo…’akasema
‘Kwanini, au.kwanza niambie mume wako ulishaongea naye...?’
akaniuliza.
‘Kuhusu nini..?’ nikamuuliza
‘Kuhusu nini! Si kuhusu haya, ili…usije kuharibu kote kote, sitaki
uje kupata shida, maana hili ni letu sote, ni muhimu tutimize lengp letu kwanza
mengine yatafuata baadae au sio..?’ akasema
‘Siwezi kufanya ujinga kama huo, unafikiri mimi ni mjinga kama
wewe...kanisainisha huo mkataba, nimekubali kufanya hivyo, lakini siwezi
kuongea na mume wangu, kuhusu haya mambo, ..nafahamu kabisa mume wangu hawezi
kukubaliana na hilo.., sana sana, hiyo itakuwa, ni kunitafutia njia ya kupewa
talaka haraka..ndio maana nahitaji hiyo silaha...’nikamwambia.
‘Kumbe...ni kwa ajili yako tu…ili wewe usipewe talaka haraka, je
mim, itanisaidia nini hapo,..ujue mimi ndiye nabeba dhamana ya hiyo kitu,
kukitokea tatizo ni mini nitawajibika, au sio...’akasema kwa shingo upande.
‘Tatizo gani, mimi ni kwa ajili ya kujilinda, …hakuna…’kabla
hajamaliza
Kwenye simu yangu ukaingia ujumbe
ukiniarifu kuwa muda wangu wa kuongea na
huyo mtu umekwisha ninasubiriwa nje tuondoke.
‘Kuna nini…?’ akauliza
‘Natakiwa kuondoka, muda umekwisha..’nikasema
‘Ndio hayo…tutaendelea hivi mpaka lini..’akalalamika.
Kwenye huo ujumbe , pamoja
na hili la kuwa muda umekwisha wa kuongea na mgonjwa, pia kulikuwa nanyongeza ‘nisisahau
kuwa usiku wa leo kuna kazi…’
‘Kuna kazi..sawa..’nikajikuta nimesema hivyo, mimi nilifahamu
hilo, lakini kuna kitu kilinitia mashaka mume wangu, alinitumia ujumbe kuwa
anataka kuja huko kujijini, kunifuata , yeye anajua nipo huko kijijini…
itakuwaje…je akifika huko kijijini akinikosa itakuwaje…kiukweli hapo akili
ilishaanza kutatika.
‘Je hiyo silaha inaweza kupatikana kwa usiku wa leo,
...?’nikamuuliza nikiwa sasa najua hilo jambo lifanyika na mimi nitoweke,
niende kwetu kijijini, huko nitatulia kwa muda, nikisubiria matokeo.
‘Nitajitahidi..lakini….’akasema
Nikianza kuondoka, na wakati huo, mume wa familia alikuwa akitaka
kuongea jambo, mimi sikuweza kumpa nafasi tena.
Nilipofika mlangoni nikageuka kumuangalia mume wa familia, maana
alikatiza kuongea, sikuwa na uhakika na kauli yake, nikasema
‘Mimi naondoka, …ni muhimu..’nikasema
‘Hilo niachie mimi,
...silaha itapatikana, na natumai hutaifanyia jambo la kijinga...’akasema na
mimi nikasimama, ghafla nikageuka na kurudi pale kitandani, nikamwambia, kwa
sauti ya chini chini;
‘Usiku wa leo kuna tafrija kwenye lile jengo, itakuwa ni nafasi
nzuri ya mimi kuweza kuipenyeza hiyo silaha bila kujulikana,..je una uhakika
leo itapatikana,…?, kama kweli itapatikana usiku wa leo muda wa saa tano hivi,
itakuwa vyema, je mke wako hawezi kuhisi kuwa silaha yake haipo, hilo ni muhimu
kufahamu?’ nikamuuliza.
‘Mara nyingi haitumii hiyo silaha.., ipo kwenye kabati lake siku
zote, sijawahi kumuona akiichukua kwa muda mrefu sasa.., hata kama kuna tukio
la hatari, kama ilivyokuwa zamani, sijui kwanini, ipo tu..sizani kama atakuwa na wasiwasi
nayo...’akaniambia.
‘Basi wewe jitahidi, mtume mdogo wako,akaichukue ...mimi
nitawasiliana na yeye, nione jinsi gani nitakavyoichukua hiyo silaha, lakini
asifike sehemu ya mapokezi, anyway mimi nitaongea naye baada yaw ewe kuwa na
uhakika wa kuipata sawa, au sio..’akasema
‘Hilo kwa ajili ya kuipta haina shaka…mengine nyie wawili mtajua,
jinsi gani na wapi pa kukutana naye, kazi yangu ni kuhakikisha hiyo silaha
umeipata au sio…’akasema
‘Ni muhimu yeye asije kuonekana yupo na mimi, au kuonekana karibu
na hilo jengo, najua hata akionekana na mimi, nitakuwa sio mimi, hayo
nayafahamu mimi mwenyewe, ..ok, tumemalizana, au kuna jingine...’nikamwambia.
Na mpaka hapo tukawa tumekubaliana hivyo...na tulikuwa tukiongea
nje kwenye eneo analochukulia mazoezi ya viungo kwasababu ya matatizo yake ya
ajali.
‘Na kweli usiku ule nikaipata hiyo silaha, silaha iliyokuja kumuua
Makabrasha,...swali ni je niilipata pata vipi hiyo silaha, na ilitumikaje,
nitawaelezea yote hayo..kama mwenyekiti ataniruhusu….’akasema na kutulia
kidogo, akamwangalia mwenyekiti.
Mwenyekiti alikuwa akiangalia saa, na mara shahidi huyu akaenda
pale alipokaa mwenyekiti wakawa wananong’ona, sikujua wanaongea kitu gani,
lakini walipomaliza kuongea, mwenyekiti alichukua simu na kumpigia mtu, huku
akiwa kamuangalia huyo shahidi kama vile anaogopa jambo kutoka kwa huyo
shahidi.
. ...
NB: Je silaha hiyo ilifikaje kwa shahidi, na je ilitumikaje kumuua
Makabrasha na je kwanini shahidi huyu anaongea sana na mwenyekiti, tukutane
sehemu ya tatu ya hitimisho la kisa hiki.
WAZO LA LEO:
Kila hila mbaya, ina walakini wake, na mwisho wa hila mbaya, ni kuumbuka tu,
hakuna hila mbaye yenye kudumu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment