Watu wote walikuwa kimiya wakitaka kusikia kauli ya shahidi huyo
mpya, hasa pale alipotoa ombi,kwa mwenyekiti, la kuomba jambo ambalo hakuliweka
wazi, na mwenyekiti akiwa na mashaka na huyo shahidi akamuuliza ni ombi
gani hilo,
Tuendelee na kisa chetu..........
‘Kitu gani unachotuomba, ..?’ akauliza mwenyekiti
Badala ya shahidi kuongea, …yeye akatoka pale alipokuwa amekaa,
akimpita mumewe, na kutembea kwa haraka hadi pale alipokaa mwenyekiti na kuanza
kumnongoneza jambo…
Mwenyekiti, ilimshika kwa shutukizo, hata hivyo akawa makini
kusikiliza kile anachonong’onezwa, huku mke wa mwenyekiti akiwa anatizama
tukuio hilo kwa macho yenye shauku au mshangao fulani.
Kwa jinsi ilivyoonekana, mwenyekiti alionekana kama
kutokukubaliana na hicho anachoongea huyo shahidi, akaonekana kama kupinga, kwa
kutikisa kichwa mara kwa mara kama kukataa, lakini huyo shahidi hakuonekana
kukata tamaa,...
Baadaye mwenyekiti akasema , kwa sauti ambayo tulimsikia ;
‘Nitampigia yeye mwenyewe, atajua ni nini la kufanya lakini mimi
sitaki kabisa utaratibu huo...’akasema.
Shahidi akaonyesha ishara kuwa hataki hayo wanayoongea yasikiwe na
hapo mwenyekiti akashusha sauti..na wakaendelea kuongea kwa namna hiyo na
shahidi akazidi kusisitiza jambo, na alipoona mwenyekiti hakubaliani naye, akainuka
maana pale alikwua kamuinamia mwenyekiti.
Ilionekana sasa kakata tamaa, kwanza hakugeuka moja kwa moja kule
alipotoka, alichofanya ni kusogea kinyume nyume akiwa kama katahayari, hatua
moja mbili kinyume nyuma halafu kawa haraka akageuka na kurudi sehemu yake.
Alipofika pale alipotakiwa kukaa,…maana yeye alikuwa akiongea
akiwa pale pale sehemu aliyokuwepo, kinyume na wengine ambao walikuja mbele
sehemu maalumu ya muongeaji,..alipofika pale karibu na mumewe, mumewe
akamuuliza
‘Ulikuwa unamuambia nini mwenyekiti..?’ akauliza docta, lakini
mdada hakumjibu mumewe, moja kwa moja akaanza kuongea;
‘Nafahamu kabisa wote humu ndani ni watu wenye hekima, akili na
utashi wa kufikiri, haya nitakayowaelezea hapa ni mambo ambayo sikustahili
kuwaelezea, ni mambo ambayo nilitakiwa niwaelezee polisi,..kwa utaratibu
ulivyo, na hata mwenyekiti anafahamu hilo..’akatulia
‘Hata hivyo, mimi kwa uoni wangu, nahisi haki inaweza isitendeke,
kama hali ilivyo itaendelea kuwa hivi..mimi ndiye niliyehusika moja kwa moja na
tukio lilitokea ndani kwenye muhusika mkuu, hapa nikiwa na maana marehemu..na
ndio maana polisi wananihitajia au sio…’akatulia akimuangalia mwenyekiti.
Lakini kuna mambo yalifanyika hata polisi hawafahamu, na sikutaka
kuwaambia wao kwanza, kwasababu nafahamu kabisa watakumbilia kunishikilia, na
wakifanya hivyo kuna mambo meng ya ushahidi yatapotea…
Sasa kwa ajili ya kuliweka hili jambo sawa, nimeamua kumuomba
mwenyekiti aniruhusu niweze kuliezea hilo tukio kiundani zaidi, ili nyie muwe
mashahidi wangu, na sitaongea uwongo, nataka niuseme ukweli wote ulivyokuwa,…leo
nipo hapa, kesho naweza kuwa jela, na jela ni jela..huko nina maadui wengi, je
nisipotoka hai,..je kesi hii ikichezewa faulo,..najuo hilo ndilo linataka
kufanyika…’akasema
‘Na zaidi sitaki watu wakitoka hapa wawe na maneno yenye utata,
nataka nyie mkitoka hapa muwe na ukweli,..ambao utaweza kuwasaidia wenye haki
zao, kwasababu hili halitaishia hapa, hivi ni vita virefu vyenye hatua zake,
leo hii nitakamatwa mimi, kesho itajengwa haoja nzito, ..nina wasiwasi sana na
hili…’akatulia
Mwenyekiti sasa alikuwa akiongea na mkewe, wakawa nao hawakubaliani,
inaonekana hilo swala sasa linakuwa nyeti, na mwenyekiti anakuwa kwenye wakati
mgumu.
‘Najua nitakamatwa, na…mume wa familia …lakini je nikikamatwa
mtakuja kuamini hayo watakayosema polisi, …kuhusu muuaji, …hebu kwanza
niwarejeshe nyuma kidogo, nilipowahi kuongea na marehemu kabla ya kifo chake,
aliniambia maneno ambayo nayakumbuka sana, na leo hii naona kama yanaweza
kuleta mantiki japokwua tunaweza kusema aliyaongea kuhalalisha dhamira yake...
Mwenyekiti aliposikia hivyo, akainua simu yake na kumpigia mtu, na
kumfanya shahidi atulie kwanza, na mwenyekiti akawa anaongea na simu huku akiwa
kainama na alikuwa akiongea kwa sauti ndogo, kama vile hataki watu waliopo humo
ndani kusikia anachoongea, na alipomaliza akasema;
‘Samahani kidogo, nilikuwa naweka mambo sawa, ...haya shahidi
unaweza kuendelea na maelezo yako, lakini bado, sijarizika na hoja yako,
endelea kutokana na ulivyoamriwa, unasikia, sehemu za kipolisi hapana, sija…endelea....’akasema
mwenyekiti akionyesha kukerwa na kitu, na shahidi akatulia kwanza akimuangalia
mwenyekiti na baadaye akasema;
‘Ni hivi...Makabrasha hayupo peke yake, japokuwa wenzake, wameamua
kujifanya hawahusiki, na hata mimi sikuwahi kuwa na hawo wenzake kwa karibu,ila
niliwahi kusikia wakiongea na Makabrasha wakipanga mipango yao..’akatulia
akimuangalia mwenyekiti kwa uso wa kusubiria jambo.
Makabrasha alikuwa akitumika, …kuna watu wakubwa walikuwa juu yake
na wao hawakutaka kufahamika,..na kwa nafasi yangu siwezi kusema lolote kuwahusu
hao watu, lakini ni mambo ya kisiasa na upinzani wa Nyanja hizo,…
Kuna mtu mmoja ambaye alikuwa akifika mara kwa mara kuonana na
Makabrasha, …nitakuja kumuelezea
mwishoni kama mambo yakienda sawa huyo alikuwa kama mtu kati, na mambo yake sio
rahisi ni mjanja ..mwenyekiti, niendelee au ....’akaelezea huyu shahidi
akimuuliza mwenyekiti, na mwenyekiti akawa kimia tu, yaonekana alikuwa hataki
hicho anachotaka kukielezea huyo shahidi.
‘Kwahiyo hili jambo sio swala dogo kama mnavyolifikiria nyie,
...mimi nitajitahidi kuelezea upande wa mtu wetu tu, ambaye anatuhusu
sana,...huko kwingine hakuwahusu, kwahiyo ni bora nifuate sheria, lakini
nitaelezea yale yenye kulata tija...kwa manufaa yenu, na kwa manufaa yangu
pia,...’akainama kama anasoma jambo.
‘Nimesema nitawarejesha nyuma kidogo, ili muweze kunielewa, kwa
wenye kuelewa wataelewa, na hata mkisikia leo nimekamatwa, au ku-uwawa, mjue
jinsi gani ya kulieleza hili kwa jamii...’akasema sasa kwa sauti ndogo yenye
kukatisha tamaa.
‘Mwenyekiti nafahamu toka awali umekuwa makini na swala hili,
nafahamu ni kwanini, na nafahamu kuwa wewe na polisi mnaaminiana sana, lakini
nakupa angalizo, kuwa kumbukumbu nyingine walizokupa wewe, ni za uwongo, kuna
mambo wameyaficha..’hapo akasema kwa sauti na mwenyekiti akataka kumkatiza
shahidi.
‘Mwenyekiti hili inabidi nikuambie …maana naona utafanya nishindwe
kabisa kuelezea kile ninachotaka kukuelezea,…hao polisi, siwalaumu maana wao
wanafanya kazi kutokana na ushahidi…lakini ushahidi waliokuja kuupata ni wa uwongo,
ukweli halisi ulishaharibiwa,,,kwa makusudi, huenda ni katika mbinu zao kwa ajili
ya kufanikisha kazi zao, au ni kwa ajili tu ya kuficha ukweli...mimi huko
sitaongelea sana kuthibitisha hilo, lakini huo ndio ukweli, ..nakusihi
mwenyekiti usiegemee kwenye ushahid wao wa moja kwa moja, kama ningepata nafsi
ya kuliezelea hil kiundani ungelinielewa....’akasema
Mwenyekiti sasa akaniangalia mimi, na mimi pale nilipo nilitaka kumuambia
mwenyekiti amruhusu tu mzungumzaji ili tuusikie huo ukweli, akam ni ukweli ili
mambo yaishe, lakini kwa nafasi ya mwenyekiti ilikuwa ni ngumu sana,
nililielewa hilo, siwezi kumlaumu mwenyekiti..lolote atakalofanya sasa linaweza
kutafsiriwa vibaya,na inaweza kumweka mahali pabaya..
‘Nafahamu kabisa kuwa mwenyekiti hunifahamu undani wangu, zaidi ya
historia ya wazazi wangu, ila kwa hapa Dar, hukuwahi kunifahamu nilichokuwa
nikikifanya zaidi ungeliweza kunifahamu kwa kupitia kwa bosi wangu..zaidi ni
kunielewa kuwa mimi ni mke wa docta, na wewe ulikuwa mstari wa mbele kuipinga
ndoa yangu…’akatulia
‘Kiukweli mimi siwezi kukulaumu sana kwa hilo, ...kwa vile
unafahamu sana asili ya huko nilipotoka, na kwa hekima zenu, haya yanayotokea
kama tungeliwasikiliza nyie huenda haya yasingelitokea. Au sio ..?’ akawa kama
anauliza
‘Lakini mimi nasema tu vyovyote iwavyo, yote ni maisha, haijalishi
wewe unatokea nafasi gani katika maisha, uwe masikini au tajiri maisha
yanawezekana, au sio, lakin kama mzazi ulijaribu kutimiza wajibu wako, na kwa
hilo siwezi kukulaumu, ila sasa, dunia itabadilika vipi kama tukijitenga, ina
maana wenye nacho watabakia kuwa nacho na wasio kuwa nacho wazidi kudidimia,
hapo ndio namkumbuka marehemu....’akasema shahidi.
Marehemu aliniambia,…vyovyote iwavyo, tajiri hawezi kumuamini
masikini, akishajua kuwa wewe ni masikini, na unatokea daraja hilo, itampa
shida sana kumuamini mtu kama huyo..na vyovyote iwavyo, tajiri hatapenda
kushirikiana kwenye utajiri wake na masikini, kwanini, ..ni kwa dhana ile ile
ya kutokumuamini..
Marehemu alitokea kwenye
maisha duni, japokuwa alisoma, …ni maisha kama haya ya kwetu, …mimi nilikuja
kuliamini hilo, kama alivyokuwa akiongea marehemu, ndio maana nikawa
najichanganya, nikawa nahangaika , licha ya ndoa, wengi wananifahamu kama mama
shughuli, leo nipo hapa kesho nipo kule, hata mshirika wangu hajui zaidi ya
kunitumia kwa manufaa yake
‘Huyu mume wa familia hadi hii leo, hajaniamini kuwa mimi …nilivyo
sasa sio kam yule aliyekuwa kipindi kile,, na zaidi kanitambua tu kama mama shughuli..’akasema akimgeukia mume wa
familia, ambaye naye kama wengine alikwua akimuangalai huyu mdada, kama mgeni
fulani, sio kama yule mdada aliyekua akimfahamu.
‘Anayenifahamu vyema kwenye uhalisia wa sasa, ni rafiki wa
mke wa familia, kwani yeye ndiye aliyekuwa bosi wangu, yeye ndiye
aliyenibadilisha kutoka binti wa kijijini hadi kuwa mdada anayejitambua, mdada
jasiri..lakini ujasiri nilio nao una kikomo chake, maisha ya binadamu yana
mahali unafika uanshindwa, ndio maana hata docta aliponishauri mambo mambo ya
kujibadili, alivyotaka yeye, alishindwa, kwanini….maji yalishanifika shingoni..
‘Inabidi niwaambie haya ili mje kuyaunganisha na tukio nzima,
naomba msinichoke, nataka niliongee hili ili kila mtu alielewe ili kesho na
kesho kutwa msije kuongopewa,
Sawa mwenyekiti amekuwa akiniuliza hili swali mara kwa mara, je ni
wewe ulimuua, je ni nani kamuua marehemu..
Sio rahisi kulitamka jibu lake hivyo..naweza nikatamka, ndio ni
mimi, au ndio sio mimi..huoni hapo kuna ‘ndio’…yawezekana nimetamka hivyo
kumlinda mtu au kujilinda mimi mwenyewe, ndio maana nataka ukweli, na hali
halisi isikikwe kwanza, kabala ya hitimisho ..’akatulia
‘Ndugu zangu…nawaambia haya, ili siku ya kesi, mjazane mahakamani
ili ikiwezekana muwe mashahidi wa kuitafuta haki,…namuomba mungu kama mambo
haya yatakwisha kwa amani, basi sitaki tena kazi hizi za hatari..sitaki tena …’akaonyesha
mikono kama kunawa.
‘Lakini nataka maisha niliyopitia yawe ni funzo kwa wengine..,
kiukweli mimi nimeshajipanga kivyangu, maisha ni popote, hata kijijini
inawezekana....hilo nimeamini na ndivyo nataka maisha yangu yawe huko. Kama
sitakiwa jela,…
Mzungumzaji akamuangalia mwenyekiti, ni kama anasubiria kitu kwa
mwenyekiti, lakini mwenyekiti alikuwa katulia tu.
‘Mimi ninachotaka kuwaelezea ni jinsi gani ilivyotokea, siku
Makabrasha alipouwawa, hili mwenyekiti hataki, kwa vile linagusa taratibu za
kipolisi, lakini utalikwepaje wakati limefungamana na hii kadhia nzima,..’akasema
‘Ni kweli mimi nilikuwepo kwenye hilo jengo, lakini huwezi kufikia
hatua hii ya .......na kwanini ilifanyika hivyo, kuna mambo muhimu lazima
yafahamike kwetu , kwenu ..nina maana hiyo…..’akatulia kidogo akimwangalia
mwenyekiti, kama anachelea kuongea jambo, lakini mwenyekiti akamuashiria asendelee
kuongea hilo analotaka kuongea;
***********
‘Makabrasha alikuwa na maadui wengi, na wengi wao, walifikia hata
kumlaani,na inapofikia hatua wanadamu wenzako wanakulaani, wanatamani hata ufe,
ujue wewe huna thamani tena katika hii dunia, hata kama ni tajiri, lakini ndani
ya mioyo ya watu, wewe ni mfu, ...’akatulia.
Kwa jinsi ilivyo mzungumzaji alikuwa anasubiria kibali cha
mwenyekiti, na mwenyekiti alionekana naye akisubiria kibali kutoka kwa watu wa
usalama, kwahiyo mzungumzaji akawa anaongea kwa kutegea akivuta muda, muda
ukawa unakwenda.
Mwenyekiti alikuwa katulia kama anawaza jambo, lakini baadaye
akachukua simu yake na kumpigia mtu akawa anasikiliza na kuwafanya watu watulie
wakisubiria hata shahidi huyo alionekana mwingi wa wasiwasi , hadi mwenyekiti
alipomaliza kuongea na simu, halafu akaonyeshea kidole gumba, kuashiria mambo
yapo shwari..
‘Endelea shahidi uwanja ni wako, nimeshafikisha ujumbe wako, ila
kama ujuavyo, baada ya maelezo yako, hakuna jinsi, vyovyote iwavyo, utanisamehe
kwa hilo.....’akasema mwenyekiti na shahidi bado akiwa na wasiwasi akasema;.
‘Katika maisha yetu haya, watu wana matatizo yao, wengine hawajui
wataishi vipi, wanahangaika usiku na mchana, ili wapate angalau riziki
zao...lakini maisha ni magumu, usiombe..., watu hawa wenye maisha magumu, kamwe
hawana utulivu wa moyo…’akaguka huku na kule kama anawasiwasi fulani.
‘Nazungumzia maisha yangu nilipotokea au sio, nazungumzia maisha
ya watu kama Makabrasga walipotokea, nazungumzia maisha kama ya mume wa familia
alipotokea,…watu wa chini, watu ambao hawana amani ndani ya nafsi zao, japokuwa
kiwili wili utamuona yupo,...ndivyo maisha ya walio wengi yalivyo, watu kama
hawa wanatafuta upenyo litokee jambo watoe hasira zao, litokee jambo watumie
kama sababu...’akasema na kugeuka kumwangalia mume wa familia.
‘Watu wana matatizo yao makazini mwao, wananyonywa, wanachokifanya
hakiliangani kabisa na kile wanachokipata, nguvu kazi yao inatumika vibaya, kazi
wanayoifanya na malipo yake ni viti viwili tofauti, anayefaidika ni tajiri, na
hata akipata ziaida ya kupindukia ni nadra sana kukumbuka,...hakuna
anayewajali, wanahangaika, kupata, agalau huduma muhimu, angalau mahitajio
muhimu, lakini kipato chao hakikidhi hata hizo huduma muhimu. Watu hawa wakipata
njia, wanaweza kufanya jambo baya sana.
Watu wahali ya chini, wanachokipata
ni kama vile wenzetu wanavyosema tonge mdomoni, hata mdomoni kwenyewe ni kama
onja –onja, unategemea huyu mtu atakuwa na amani kweli...huyu akipata nafasi ya
kufanya unyama ataufanya unyama kweli, ..hata kuua kwake itakuwa ni sehemu ya
kama kulipiza kisasi..
Watu wana matatizo sana huko kijijini , usione watu wapo kimiya,
mtu analima mvua hakuna, pembejeo hakuna, anatumia jembe la mkono, mtu huyu
kila siku anakatwa kodi, kila anachonunua, ni kodi, akigeuka huku kodi, mtoto
wake wanadaiwa ada, yeye anaumwa magonjwa yasiyohesabika, akienda hospitalini,
hakuna dawa, akipatacho nini…anayefaidika san asana ni huyu mnunuzi anayekuja
kununua kwa mkulima na kwenda kuwauzia
wengine,..sio mkulima..huyu mtu akipata nafasi unafikiri atafanya nini..
Sio kwamba naongea haya kuwatetea watu, kama Marehemu, kama mume
wa familia au kama mimi, naonega
kiuhalisia, maana kwa bahati nzuri nimetokea huko na uzuri nimeweza kuishi na
matajiri, nimeyaona hayo hata kwenye kazi zangu, hivyo…ndivyo ilivyo,
asikudanganye mtu…ndio maana hata mwenyekiti hataki kuniamini..unafikiri ni
kwanini..ni hulka,..za matajiri dhidi ya masikini..
Mwenyekiti pale akakuna kichwa, kama kusikitika, lakini…hakusema
neno
‘Siku tulipoongea na
mwenzangu tuliyajadili haya maisha yalivyo, na siku nilipoongea na Makabrasha kabla
ya kifo chake yeye aliniambia hayo..ni muhimu sana myasikie...
Yeye alipenda kusema ‘system,’ akiwa na maana wale wenye mamlaka,
wale waliopewa dhamana, …na zaidi wenye uwezo, hasa wawekezaji,…yeye marehemu
aliwahi kuniambia hivi
‘Huko kwenye system(utawala, na wenye mamlaka, matajiri na
wawekezaji, akiwa na maana hiyo),...ndio haki za wanyonge zinapopotelea, wahujumu,
walaghai, wadhulumaji,mafisadi, wamejificha huko…, na huko ndipo kwenye watu
wanaojifanya ni watetezi wa wanyonge, wakija kwenye majukwaa wanakuja kwa lugha
nzuri tu, na wanajua jinsi gani ya kuwadanganya wanachi..
‘Mimi kama mimi, najau wengi wananichukia sana, ila mimi nimepata
kuutumia ujuzi wahuu na taaluma yangu hii kuchukua kile walichoiba kwa wananchi
na kukirejesha kwa wananchi…’akasema na mimi sikumuamini kwa kauli hizo..hadi
nilipofuatilia kwenye ofisi yake na kuyaona hayo kwa vitendo.
Hili hamuwezi kuliamini, ndivyo marehemu alikuwa hivyo, kwanini
hamuoni hilo, ukweli wa upande wake wa pili umefichwa, ila yeye alikuwa na
vitega uchumi vichache tu, mali yake nyingi, aliyokuwa akipata, yeye alikuwa
akiwapeleka masikini, wazee wasiojiweza kule kijijini kwao, ndio maana hadi leo
ukienda kule mtu huyo anaheshimika sana
Watu walikuwa wakijiuliza ni kwanini mtu mkorofi kama huyu hafungwi,
hakamatwi..huyu mtu aliheshimika, kwa wasiojiweza, alipata Baraka zao, kwa
upande huo alikuwa na watetezi, huku akitumia kila mwanya wa sheria kujilinda…’akatulia
‘Hili wengi wataliona ni la ajabu, maana mazuri ya mtu huyu yakichanganyikana
na mabaya yake..na mazuri yake ilivyo, hupotea tu..,..na hasa ukiwa kwenye
usawa wa mtu wa daraja la chini kama sisi, ni nani atakuamini hata utende wema
vipi..mimi mwenyewe kipindi nilichofanya kazi kwake nilikuwa nikishiriki kwenye
kazi za kuwahudumia wale wasiojiweza kutoka kwenye mfuko wake maalumu aliouweka
kwa kazi hiyo…
Makabrasha alikuwa akiwalipia,wasiojiweza shule, alikuwa
akiwasaidia mayatima, alikuwa akiwasaidia wagonjwa kwenda kutibiwa nje..,
angalia kumbukumbu zake, mtaziona hizo, lakini kumbukumbu hizi zilikuja
kupotea, mimi niliziona na shule alizojenga, nazifahamu, lakini hakutaka watu
wafahamu hilo, ni kwanini…mimi sijui.
‘ Zaidi ni kuwa huyu mtu alikuwa akitumiwa na huyo mpinzani wako
mzee, mpinzani wako alikuwa mjanja, alikuwa akiuma na kupilizia, akienda
kijijini, anawekeza kwa watu kama hao, na …ndio hivyo, mambo ya kisiasa yalivyo
au sio…
Labda sera hizi huyo mpinzani wako… alizipata kutoka kwa marehemu,
kuchukua kwa matajiri kurejesha kwa wayonge, japokuwa yeye alitumia njia hizo
mbaya kuzipata hizo pesa au mali, na yeye aliona njia hizo ndio rahis kwake,,
..huyo ndiye Makabrasha.
Simtetezi jamani..ila nazungumza hali halisi, na sisemi haya kwa
nia ya kutaka kujitetea hata mimi, ila kwenye ukweli tusema,..haya yatakusaidia
hata wewe mwenyekiti, kuwa katika maisha, msijiangalie nyie wenyewe kama
matajiri, kuwa masikini hafai kuoa au kulewa na tajiri, ili mfanikiwe jichanganyeni
na masikini, wasaidieni masikini, ili na wao wawaone nyie kwa jicho la rehema.
Swali kama huyo mtu
alikuwa hivyo, ni kwanini akauwawa,…..na ni nani hao waliofanya hivyo,…ndicho
wengi wanakisubiria hapa au sio…lakini ukweli kwanza uili mje muone mazingira
yaliyokuja hadi huyu mtu akauwawa..na sio rahisi kama watu wanvyoona..sio
rahisi mtu mwenye akili zake kubonyeza trigger…
Na hilo halikufanyika …kirahisi hivyo,…kumbuka mazingira ya
marehemuilikuwa ulinzi hadi akitembea ana vitu vya kumsaidia kumlinda, ikitokea
hatari akibonyeza kitufe fulani, walinzi wake wameshafika…na kila anachoongea
kilirekodiwa, mwisho wa siku anafuta kile alisichokitaka..huyu ndiye marehemu..
Swali alikujaje kuuwawa…kuna kitu mjifunze ukitaka kuficha kiatu,
sehemu nzuri ni sehemu kunapowekwa viatu au sio..na mbaya wa mtu ni mtuwe au
sio…adui wa mtu ni rafiki yake mkubwa,…sio rahis kwa mtu huyu aliyejilinda
hivyo kuuwawa kirahis hivyo tena ndani ya sehemu yenye kila zana zake za
kujilinda,…
Hamfahamu ofisi yake ilivyo..humu aliwekeza kila kitu chenye
kumsaidia kujilinda, nahisi alitumia pesa nyingi sana, na yeye alikuwa akisema,
akiwa ofisini kwake, anajihisi yupo salama kuliko sehemu yoyote…lakini humo
humo ndio alipouwawa,..jiulize ni kwanini, …
Polisi hadi leo, hawajawa na uhakika …japokuwa wanadai kuwa wameshaupata
ushahid lakini je ushahidi huo ni kamilifu,…kumbuka ukweli wote ulishaharibiwa,
kilichobakia ni yale yale aliyokuwa akiyafanya marehemu..yamemrudia,…sasa je ni
kweli kuwa hao washukiwa ndio kweli walifanya hivyo, na kama walifanya hivyo
walitumia mbinu gani…
Kumbuka ulinzi, kumbuka zana zilizopo hapo,..je masikini anaweza
kuvuka hivyo vihunzi…hahaha…ni movie yenye ujasiri…
Mwenyekiti, sasa naingia sehemu nyeti,…naomba univumilie, na naomba
haya mazungumzo …wakili, haya ni mazungumzo nyeti, weka vitega masikio vyema,
weka vitega sauti vyema, ili mkipae kile chenye uhakika,…najua baada ya
hili,..nitakuwa nikibebwa kama muuaji, lakini ..ni bora niongee huu ukweli, ili
mwisho wa siku, kama nitaonekana mimi ndiye muuji, basi niwe shujaa…’akasema na
kuinamisha kichwa chini.
‘Shujaa wa mauaji, hapana…’aliyesema hili ni mama
‘Nianze mwenyekiti…?’ akauliza mzungumzaji, akimuangalia huyo
mama, …na mwenyekiti, akawa anaangalia saa yake, na hakusema kitu pale pale
akaangalia dirishani, akanyosha kidole kuwa muongeaji asubiri kidogo…
WAZO LA LEO: Kifo hakina hodi, kifo kila mtu kitamkuta kwa wakati
wake, hata kama upo ndani ya handaki, hata kama wewe ni tajiri kupindukia ukawa
unalindwa hata ukiwa chooni, hata kama umejizungushia gilasi zisizopitisha
risasi, siku ikifika imefika,..hata kama wewe ni masikini, siku ikifika
imefika,…
Sasa kama hivyo, kumbe kuna mwenye mamlaka na uhai wetu, ambaye
hawezekani, asiye na mfano wake, alipangalo kuwa liwe litakuwa,basi ni kwanini
hatumuogopi yeye, tukamtii yeye, kwanini tunafikia mahali tunatakabari,
tunakiuka maadili mema, tunaghilibika kwa tamaa za mali, utajiri, utawala, kama
vile tutaishi milele, tuikumbuke siku hiyo ambayo, mtu ataicha mali yake,
watoto wake, mpenzi wake,…utawala wake, imebakia kauli,..’yote ni mapenzi ya
mungu…’
Ewe mola wetu tujalie tuwe na mwisho mwema…Aamin.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment