Kuna mtu alikuwa analia,
ikaja kugundulikana kuwa ni mume wa familia, ..na ndipo shahidi aliyekuwa
akizungumza akasema, ;
‘Utalia sana,na hapo ndio nimeanza…’
Tuendelee na kisa chetu
*********
‘Wewe niache nilie, ujue mwanaume akilia kuna mazito, wewe hujui
tu, wewe hujui ulivyoharibu, mumeniharibia maisha yangu, na kwa hili utakuja kunikumbuka, …hutafanikiwa
kamwe, na hiyo mipango yako na waliokudanganya, utakuja kujuta.. ’akasema mume
wa familia.
‘Kufanikiwa, au kujuta kwangu sio hoja, hoja ni ukweli wote
ubainike, ili haki iweze kutendeka, ndicho mimi ninachokitaka, baada ya huu ukweli … kila mtu atabeba mzigo
wake yeye mwenyewe,na maisha yataendelea tu…’akasema mzungumzaji.
‘Nilijua tu…haya sawa ngoja tuone…’akasema mume wa familia kwaunyonge.
‘Kwani.., wewe ulitakaje, kuwa haya yaendelee hivi hivi, wakati
ukweli upo bayana, na ukweli ni kuwa dhuluma haitadumu, ni lazima mwisho wa
siku utagundulikana tu, na ni heri nusu shari kuliko shari kamili. Kama
nilivyosema awali mimi sio yule binti wa kijijini asiyejua kitu, asiye na
ufahamu, ..elimu niliyopata japo kidogo, imenizindua, naifahamu sheria,
naifahamu haki, ..na kwa hili nafahamu kabisa huna lako, utegemee huruma za mke
wako tu..’akasema muongeaji.
‘Sawa…endelea kufungua bakuli lako, tuone mwisho wake
utakuwaje,…ukitoka hapa unaelekea jela, unafikiri ni nani wa kukusaidia….hao
watu eeh, hahaha unajidanganya tu..’akasema mume wa familia.
‘Ndugu mwenyekiti….’muongeaji akawa anataka kulalamika, ili aweze
kuendelea maana mume wa familia anamkatiza kila akitaka kuendelea. Na kabla
mwenyekiti hajasema kitu, mume wa familia sasa akasimama.
Wakili wake alipoona hivyo, akawa anajaribu kumzuia huyo mume wa
familia, haikueleweka lengo la huyu mume wa familia kusimama ni nini, kuwa laba
anataka , kuondoka au kumzuia muongeaji asiendelee kuongea.
‘Sikiliza,..niamini mimi haya yatakwisha, nakuambia ukweli haya
yatakwisha, si unataka turejee kule tulipotoka, sawa, haya lakini tatizo polisi
wanasubiria, jela inanukia…’akasema
Hapo mwenyekiti akaamua kuingilia kati na kusema;
‘Mume wa familia, usivuruge utaratibu, hebu kaa chini, nakuona
sasa unaleta vurugu, kitu gani unaogopa, muache shahid aendelee, hapa kila mtu
anataka kusikiliza ushahidi wake,..sitarudia tena kukuonya, kwasababu kikao
hiki kina kibali kisheria, hatukufanya tu kama kikao cha mitaani, unasikia,….’akasema
mwenyekiti.
Hapo mume wa familia, akageuka
na kukaa kwenye sehemu yake na wakili wake akawa anamnong’oneza kitu, wakawa
wanaongea sasa kwa taratibu, nikaona kama wanakubaliana jambo. Na kabla
muongeaji, shahidi hajaendelea wakili akanyosha mkono, kutaka kuongea, na hata
kabla mwenyekiti hajamruhusu wakili huyo akawahi kusema;
‘Samahani mwenyekiti…kuna ombi kidogo kwa mume wa familia, naomba
tumsikilize…’akasema wakili na kabla wakili hajamaliza kuongea, nahis
walishafahamu kuwa hawataruhusiwa kuongea, akasema;.
‘Kwa vile umesema mdogo wangu kakamatwa na polisi, na mimi ndiye
kaka yake, ninaomba mimi na wakili wangu tuende tukafuatilie utaratibu wa
dhamana yake…’akasema hivyo akauliza
‘Nani kasema kakamatwa na polisi, mimi nimeuliza unafahamu wapo
mdogo wako alipo, yawezekana kakamatwa..sawa. mimi sina uhakika na hilo, hayo
ni maswala ya polisi. Walichoniambia nikuwa tusiwe na wasiwasi na huyo mtu,
…kwahiyo huenda anaisaidia polisi..na watatoa taarifa kama kakamatwa au la..’akasema
mwenyekiti
‘Kwani Polisi wamesemaje hasa..?’ akauliza wakili.
‘Polis walisema wanamfuatilia, pale nilipotoa taarifa kuwa huyo
kijana ametoroka, maana ilikuwa niw ajibu wetu kutoa taarifa…wakasema watalifuatilia
hilo.
‘Na baadae nilipooongea nao tena, ndio wakasema wameshayaweka
mambo sawa tuendee na kikao,na wakatahadharisha kuwa kikao chetu kisingilie
maswala ya mauaji, ina maana kuna jambo kijana kaongea huko…’akasema
mwenyekiti.
‘Kwa kauli hiyo mpaka hapo ina maana mdogo wake mteja wangu yupo
mikononi mwa polisi …au sio?’akasema wakili
‘Yawezekana, ndio..sina uhakika huo, huenda yupo mikononi mwa
polis lakini akiisaidia polisi, kama atakuwa kakamatwa kwasababu kadhaa, ni
lazima watatufahamsisha, sisi ndio ndugu zake…’akasema mwenyekiti
Hapo mume wa familia akasimama, na wakili wake akamzuia wakawa
wanaongea na wakili akasema;
‘Mteja wangu anasema kama yeye haruhusiwi kutoka, bas I ngoja mimi
kama wakili wake nilifuatilie hilo, kwa niaba yake..’akasema wakili.
‘Hivi tunaelewana jamani,..huyo ni ndugu yetu, sote tunawajibika
naye, kama ni swala la kufuatilia, sote tutaungana na kuona vipi tutamtetea,
..eeh, lakini hadi hivi sasa tupo chini ya amri ya polisi, kuwa asije akatoka
mtu na kikao kikimaliza wao watakuja hapa, …’akasema mwenyekiti
‘Lakini mimi siwezi kuzuiwa maana, mimi ni wakili tu, kama mteja
wangu kaniruhus mimi nitoke nifuatilie hilo, ni wajibu wangu kutii, mimi nipo
kwa mamlaka yake sio kwa mamlaka ya hiki kikao..’akasema wakili
‘Haijalishi wewe ni nani mimi nafuata amri za watu wa usalama, …,
kwani wewe wakili hauwezi kufanya makosa, muhimu tusubirie, tukimaliza kikao,
wenyewe watafika hapa na kitakachoendelea baadae tutaambiwa, sawa, …shahid
endelea…’akasema mwenyekiti.
********
Shahidi akaendelea…
‘ Baada ya Makabrasha kumweka sawa mume wa familia, bado kulikuwa na
mambo hayajawekwa sawa kwa utaratibu wake, kwa upande wa wadhamini wake, hao
waliomtuma alishafanya kazi yake, lakini sasa alikuwa akikamilisha mambo
yanayohusiana na masilahi yake.
Aliniambia kwua katika mipango yake alihitajia kundi la watu,
ambao ataweza kufanya kazi nao, kuachilia mbali sisi ambao tunakutana mara kwa
mara, akasema bado anahitajia kiongozi ambaye atakuwa akiongoza hilo kundi.
‘Wewe si ndio kiongozi..?’ nikamuuliza
‘Hapana, mimi sitakiwi niwe kiongozi wa moja kwa moja, maana mimi
ni mtu wa sheria, kazi yangu kubwa itakwua kuhakikisha sheria zipo sawa, hata
hivyo …inavyoonekana mimi ndiye nitakuwa mkurugenzi mkuu kutokana na hisa
zangu…lakini nahitajia mtedaji mkuu, kiongozi wa kusimamia mambo yote.
‘Ni nani huyo..?’ nikamuuliza
‘Ndio namtafuta,..ungelifaa kuwa wewe, lakini bado ..wewe bado
unahitajia muda, yupo ambaye anafaa sana, lakini sijaweza kumshawishi…’akasema
‘Ni nani huyo..?’ akauliza mume wa familia
‘Haina haja kumfahamu kwasasa…ila zaidi ya hayo, tunahitajika
kumuandaa huyo mtu kuja kuwa kiongozi wa baadae, wewe mume wa familia utakuwa
na mamlaka yako, lakini hutaweza kuongoza hili kundi, hili kundi ni jingine,
linahitajia mtu mwenye uelewa wa mambo mengi na jasiri ..’akasema
‘Kwanini mimi sifai, usielete watu wako hapa kwanza kampuni ni
yangu, nay a mke wangu, bado unaona sisi hatufai, kwanini....?’ akauliza mume
wa familia
‘Mimi ninakufahamu sana, kiongozi tunayemuhitajia anatakiwa mtu
tofauti na mkeo kwasababu atakuwa mpinzani wa familia ya mkeo, …sihitajiki
kujieleza sana kwa hilo, muhimu muelewe hivyo tu…’akasema
‘Hapana mimi sitakubaliana na hilo…’akasema mume wa familia.
‘Kumbuka mimi ndiye mkurugenzi mkuu, ninayemiliki zaidi ya nusu ya
hisa, nina kura turufu…na uniamini, mimi nina maana yangu kubwa sana kulifanya
hilo, mwenyewe utakuja kuona,… tuombe
mungu tu nizidi kuwepo..’akasem
‘Una maana gani kusema hivyo, kumbe mwenyewe unajua kuwa
hutafanikiwa au sio..?’ akauliza
‘Kazi kama hizi ..ni za hatari, ..vyovyote iwavyo, lolote laweza
kutokea, hilo siwezi kulipinga, ila kwangu mimi ..kisheria nimeshaanza kuweka
kila kitu sawa, hata hivyo maisha hayana
ujanja, leo nipo kesho sipo,..ila nawahakikishia , kama nitaendelea kuwepo,
mali zote hizo zitakuwa kwenye miliki yetu, mikakati yote imekwenda sawa ni nyie tu
kushirikiana na mimi ili muwe na uhakika wa maisha mazuri, …’akasema.
‘Sisi tutakuwaje na maisha mazuri wakati hisa karibu zote
unachukua wewe..?’ akauliza mume wa familia
‘Je ni kipi bora kukosa kabisa au hata kupata kidogo, eeh, maana
kwa hali ilivyo ungelikosa kila kitu, hunishukuru mimi, …acha ubinafsi
hapa,..’akasema kwa ukali.
‘Kama ni ubinafsi unao wewe sio mimi…’akasema mume wa familia.
‘Sikiliza…hivi unajua kashafa uliyotengeneza, ..kashifa hiyo
ingekugharimu wewe kutimuliwa kwenye hiyo familia kwa fedheha, …pili ukumbuke
kuwa kutokana na kashfa hiyo familia hiyo ipo kwenye wakati mgumu…’akasema
‘Kwa vipi…?’ akauliza mume wa familia.
‘Unaona, ndio maana nikasema uongozi unahitajia mtu anayeona
mbali, anayefahamu mambo mengi kwa wakati mfupi, siwezi mimi kukufafanulia kila
kitu, unasikia,..au nikuulize wewe
ulitakaje, …?’ akauliza
‘Sisi mimi nilitakaje, wewe umetumia ujanja wa kuhakikisha
unanifirisi mimi, na familia yangu, unafikiri mke wangu atakubali kirahis
hivyo, eeh, na..hapana hilo la kutafuta watu wengine kuja kuongoza hata mali za
mke wangu sitakubaliana nalo..’akasema mume wa familia.
‘Tatizo bado hujanielewa,…unasikia,…kundi hilo, kwa namna moja halitamuhusisha
mkeo moja kwa moja, maana mkeo ni
familia ya kundi pinzani, mkeo ataingia pale tu tutakapogusa mali..mbazo
na yeye anazimiliki..vinginevyo yeye atakuja kuwa kama picha ..familia hiyo
itafirisika, na wewe utakuwa juu…’akasema
‘Hizo ndoto….hahaha..’akasema mume wa familia.
‘Ndoto, ni kwa vile wewe huwezi kufuatilia, mambo ya hisa, kushuka
na kupanda kwa tahamni za hisa za wawekezaji wakubwa, mkweo sasa hivi anayumba,
kisiasa na kiuchumi, ..hilo kwako tuliache, kidogo kidogo utakuja kunielewa..’akasema
‘Mimi nakubali tu kwa vile sina jinsi, kwa vile unanitishia amani,
vingnevyo nisingelikubali kabisa…’akasema mume wa familia.
‘Hizi jamani wewe mtu unataka nikupe nini,..ulitaka mimi
nikusamehe madeno yote, ina maana mim iwe kazi yangu kukufanyia kazi
zako,..nipate hasara, hebu niambie hayo madeni yangu yote ungeliwezaje
kuyalipa, hebu jaribu kuwa na akili pana…’akasema wakili.
‘Nitakuja kuyalipa na hisa zangu zote utazirejesha, ..hilo na
kuahidi ..’akasema mume wa familia
‘Hahaha, kwa hali uliyo nayo, sizani,labda mimi niwe sipo duniani,
..unafikiri hayo madeni ni kitu kidogo, ..eeh, hutaweza hilo sahau na ujipange
nnavyotaka mimi, nataka nyie muwe matajiri, kwanini hutaki kunielewa…’akasema
wakili huyo.
*********
Mikakati ikawa mingi, na mingine mimi sikuhusishwa kabisa niliweza
kuigundua hiyo mikakati, wakati nikiwa kwenye kazi zangu, na nikiwauliza
wanasema nisiwe na wasiwasi mane mengine sio lazima mimi nifahamu, ila kila
kitu kimeshafanyiwa kazi, iliyobakia ni mambo machache ya kukamilisha, na hayo
hayanihusu sana.
Kwahiyo mimi nikawa nasubiria, na wakati nasubiria ndio ikaja
taarifa hiyo ya ajali…
‘Ile ajali ya mume wa familia, ilitokea katika harakati zile za kuchukua
mkataba ule wa zamani ili ikabadiliswe na huo mpya wa kugushiwa, na hayo yote
yaliwekewa muda maalumu kwa mume wa familia kuhakikisha nakala zote za zamani
zmechukulia na kuharibiwa, na kuhakikisha kuwa hakuna nakala yoyote
itakayobakia.
Tatizo sasa mume wa familia akawa na ziada ya kazi ya kuongea na
mama mzazi, ili mtoto huyo aje kuwa sehemu ya warthi wake, aweze kutambulikana,
na hilo lilitegemea sana mama yake, kwahiyo pamoja na mihangaiko ya kubadili
hiyo mikataba bado alitakiwa kumshawishi mama wa mtoto huyo akubaliane naye.
Mambo yote hayo yakapangiwa muda,…sijui ni kwanini, nahisi ni moja ya mbinu za
marehemu kuhakikisha jamaa hapati muda wa kutafakari tena.
Muda, ukawa ni sehemu kubwa
ya kufanikisha malengo hayo, muda pia ukatumiwa kama namna na kumfanya mume wa
familia awe na wakati mgumu ili asipate nafasi ya kutafakari zaidi, muda ukawa
namna ya kuwaogofya wale wote wanahusika, kuwa wakichelewa kashfa zao zinatumwa
kwa walengwa..mume wa familia,..hakujua hayo yote yote wenzake wameyaweka
kwasababu maalumu.
Siku hiyo mambo yalianza
hivi----
Akiwa ofisi akapigiwa simu na Marehemu kuwa zile nakala zote za
mikataba yao, zinahitajika kwa haraka, …na pia akaulizwa vipi mama wa kichanga
keshamuweka sawa, maana yote ni muhimu sana, kwani asipomuweka sawa mama wa
kichanga, huyo mtoto anaweza asiwe na nafasi kwenye mipangilio ya watoto
wanaotakiwa kumiliki mali halali.
‘Kwanini, kwani hata asipokubaliana kwa sasa baadae si
inawezekana, kuna tatizo gani hapo..?’ akauliza
‘Tunahitajia sahihi ya mama,..tunahitajia kukubali kwake, hatuwezi
kupitisha jambo kama mama wa mtoto hajakubali, hiyo ni kazi yako kama kweli
unampenda huyo mtoto na kama kweli unamuhitajia kama mrithi wako wa baadae basi fanya juhudi
..’akaambiwa
‘Sawa…’akasema mume wa familia, hapo kichwa kinamgonga kweli,
akachepuka na kumeza zile dawa, alizopewa, ..muda mchache baadae akajihis
mwingine, akili ikawa na changamoto za dawa. Anarudi kwenye kikao hajaa vyema
zimu ikalia, akaambiwa;
‘Lakini pia zile nakala za mkataba wenu , wewe na mkeo,
zinahitajika kwa haraka, zoezi hilo halitaweza kufanyika kama hizo nakala zote
hazipo, msimamizi anayesimamia idara hiyo, kasema hataweza kukamilisha hilo
mpaka nakala zote ziwepo, ili ziharibiwe mbele yake..’akaambiwa.
‘Sawa…’akasema na kupekua kwenye briefcase yake, ndio akakumbuka
nakala mmoja haipo, ..akakumbuka alipoiacha, hapo kwa haraka akawaambia
wajumbe;
‘Jamani endeleeni na nikao, nipo, …msikatize kikao, kuna kitu cha
haraka nakichukua hapo nje…’akasema akitoka na briefcase yake, akaingia kwenye
gari, mbio, barabarani.
Akiwa barabarani, Makabrasha akaendelea kumsumbua na simu, ni kama anamuona
anavyohangaika,…akamwambia;
‘Na ukumbuke hiyo ndio salama yako, maana mkataba wa zamani
ukiwepo, na kashfa ulizokutwa nazo zikibainika basi hutapata kitu… umeelewa,
hiyo ni kwa faida yako,…’akaambiwa
‘Ni kweli…’akasema, na ni
kweli, kutokana na hizo kashfa, mbele ya mkataba wao alitakiwa akose kila kitu,
na zaidi ni ndoa yake kufa, na ndoa ikifa yeye ana faida gani tena,,,;akatulia
kidogo mzungumzaji, halafu akasema
Kama mtausoma vyema huo
mkataba, utaona hadi sasa mume wa familia hana ndoa, sisemi hili kwa uzushi, au
kutilia fitina, mkataba wao unasema nini
kuhusu madhambi kama hayo, na ushahidi upo wazi…au amkane huyo mtoto kama sio
wake, je anaweza kufanya hilo, hawezi kumkana, sasa chukulia hali hiyo, na ndio
umepata mwanya kama huo, ungelifanyaje, ndio maana mume wa familia akakurupuka,
hana amani, akili sio yake,….
Kwahiyo ndio akapanga akitoka hapo kwenye kikao chake cha kikazi…kikao
ambacho alikiacha kikiendelea,..ili iwe ni ‘kinga’ kwake kama ikitokea jambo
kuwa yeye siku hiyo alikuwa na kikao ofisini, …kwa usafri wa gari, alijua
atakwenda kwa haraka, na kurudi na kuendelea na kikao.
Ili kukamilisha mambo yote hayo akaona ampitie mzazi, mama wa
mtoto ili amuhakikishie mikakati yote na amshawishi kuwa mambo sasa yapo sawa, na kutokana na
shinikizo la yule mtu asiyejulikana, mtu wao..yaani wakili, ambaye ni
marehemu.., atalimaliza..
Alipofika huko akashangaa kumuona mke wa familia yupo na huyo mdada
aliyejifungua, na hili hakulitegemea kabisa,
yeye alijua kuwa mke wake atakuwa kazini, sasa iweje awepo pale, na kwa
muda huo huo akapokea ujumbe wa simu ikimuhimiza kuwa nakala za mikataba yote
ya zamani, zinahitajika kwa haraka iwezekenavyo. Na muda ni leoleo,
ikishindikana ndio basi tena..
Hapo akili ikazidi kuchanganywa,
alijua kabisa mkewe akitoka hapo atarudi nyumbani, na hataweza tena kuchukua
ile nakala ya mkewe , ambayo aliisahau kwa bahati mbaya usiku, yenye shida
ilikuwa ni nikala moja ya mkewe maana yake alishaichukua anayo…
‘Sitaweza kuongea na huyu mtu kwa leo, lakini ni lazima niwahi
kuzipata hizo nakala za mkataba ..kwa manufaa yangu..’alikuwa akisema hivyo,
alinihadithia jinsi siku hiyo ilivyokuwa na wakati mgumu kwake..
Ya mungu mengi, …wakati Makabrasha keshafanikisha namna ya kumweka
sawa msajili wa hiyo mikataba, na wakati huo wanasubiria nakala hizo walizokuwa
nazo wahusika wakuu,akaja taarifa jamaa kapatwa na jail, yupo kwenye hali mbaya..
Ukumbuke kabla ya hilo zoezi, Makabrasha alishafanya vitisho vingi
ambavyo vilizidi kumchanganya mume wa familia,…na mume wa familia kuna muda
akawa analalamika kuumwa na kichwa Makabrasha ndiye aliyemtafutia dawa, akasema
hizo dawa zitamsaidia sana hayo maumivi ya kichwa, mimi nilikuja kuzipeleka
hizo dawa kwa wataalamu baadae lakini zikaonekana ni dawa zakuharibu akili…’akatulia kidogo.
‘Kiukweli Makabrasha anaifahamu kazi yake vyema, kwenye kucheka
atacheka, kwenye kazi, vitisho, atakutisha kweli,...alijipanga vyema,kwahiyo kila
muda kwake ilikuwa ina mbinu zake na kila jambo lilikuwa na plani A na B,
ikishindikana moja nyingine itachukua nafasi yake, hakuwa mtu wa mchezo.
Hizo dawa alipewa kabla ya ajali na baadae akawa anaendelea nazo
baada ya ajali mwenyewe anasema akisikia kichwa kinauma sana, akinywa hizo dawa kichwa kinapona, lakini
hakujua hiyo ahueni ilikuwa inazaa tatizo jingine. Na ndio hayo yakawa
yanatokea baadae ni sababu ya hizo dawa, .hata mimi sikuwa na ufahamu wa hizo
dawa, nimekuja kuligundua hilo baadae sana...
Sasa alipogundua kuwa mkewe
hayupo kazini, yupo kwa rafiki yake, na anatakiwa kuwahi kuchukua zile nakala
azifikishe kwa walengwa, si ndio akatoka hapo kwa mwendo kasi, akili pale
ilikuwa sio yake tena, keshapata vitisho, kamuona mkewe na muda hautoshi, na
zile dawa huenda alizitumia asubuhi,zilikuwa bado kichwani akilini ikawa inaota
mengine, haoni kabisa kama yupo kwenye mwendo kasi, tahamaki ndio hiyo
ajali..ilikuwa ni ajali mbaya sana.
Ajali haina kinga….!
Ajali hiyo ingelichelewesha mambo mengi, lakini kwa Makabrasha
ikaonekana ni bahati nyingine nzuri tu kuitumia, tunaweza kusema kwake ilikuwa
ni bahati nzuri ya kufanikisha mambo mengine.., japokuwa ilikuwa ni ajali kwa
rafiki yake..
Hutaamini ajali hiyo ikaja
kutumiwa kama kisingizio cha kufanikisha mambo mengine mengi tu, kama mlivyosikia
kwenye maelezo yaliyotolewa awali. Mtu anaumwa yupo hospitalini, mara yupo
uwanja wa ndege, mtu anaumwa, yupo hospitalini mara yupo nyumbani….inaeleweka
kweli….! Lakini kiukweli ajali ile ilikuwa mbaya, na kuna madhara makubwa
aliyapata kwenye uti wa mgongo, hili halina shaka.
Sasa baada ya ajali ni nani anaweza kutumiwa ili kufanikisha hayo
yaliyopangwa, nakala za mikataba ile ni muhimu sana, akatafutwa mtu wa haraka,
ambaye yupo karibu na mume wa familia ambaye anaweza kuficha siri, hata kama…na
akipewa maagizo atayafanya kwa haraka..
Uwe na kujali fulani,…, ndio hapo wakamchukua mdogo wa mume wa familia, yeye kwa asilimia
kubwa hakufahamu chochote kinachoendelea zaidi ya kutumwa , na hakutakiwa
afahamu kitu gani kinachoendelea, kazi yale ilikuwa kumtii kaka yake,na kaka yake
ahakikishe hilo. Sizani kama alikuwa anafahamu undani wa hayo yote, kwani
nimjuavyo, kama angelifahamu undani wake, mengine asingelikubali.
‘Sasa hapo utajiuliza iweje wakati mtu hajiwezi yupo hospitalini,
maana hadi anafikishwa hosp alikuwa hajiwezi, sasa huyu marehemu alijua ampe
dawa gani ili aongee kila kitu cha kusaidia, na maongezi yake yasaidie…dawa
hizo zilitumika pia.
‘Na ajali iliyopotea mtu wa kwanza kufika kwenye hilo gari alikuwa
ni marehemu alifuata nini, na alijuaje kuwa ajali hiyo itatokea,… marehemu
alikuwa sio mtu wa mchezo..sijui siku ile walipokutana wakati mgonjwa yupo
taabani, waliongea nini...hilo tutamuuliza mume wa familia.
Nisije kulisahau hili….Kuna mtu mwingine ambaye alikuwa
kinara wa hayo yote, akiwa kama msaidizi wa Makabrasha, ambaye hadi sasa watu
hawajamgundua…huyu mtu ni hatari kuliko watu wanavyomfikiria…’hapo akatulia
kidogo.
Huyu mtu ni hatari hata kuliko Makabrasha mwenyewe maana tatizo
lake kunwa ni kuwa ana papara, hajatulia kama alivyokuwa akitulia baba yake kabla
hajaingia kwenye mapambano, mtu huyu ni nyoka yenye sumu, ni mbaya sana, si
mwingine ni mtoto wake mwenyewe marehemu.
Huyu aliweza kupenya kwenye sehemu mbali mbali na kupata taarifa
nyeti. Huyu anajua siri nyingi tu za baba yake,..na ndiye alitarajiwa kuwa
mrithi wake mkuu, kwa mtizamo wa wengi lakini ikaja kutokea tofauti, ..hapa
hatuna uhakika ni kitu gani hasa kilifanyika…maana imeshangaza kuona
aliyepewa majukumu hayo ya kifamilia ni
mtoto mwingine.
Ni kweli mtoto huyu kisheria ndiye aliyetakiwa kuchukua hayo
majukumu, lakini mtoto huyu hakuwa karibu na baba yake, hawakuwa wanaelewana
kutokana na tabia za baba yake, mtoto huyu alikuwa akitaka mambo ya halali, sio
kama alivyokuwa akitaka baba yake, kwahiyo walikuwa hawapatani kabisa, sasa
iweje yeye apewe majukumu ya kifamilia, majukumu ambayo ndani yake kuna
magumashi mengi.
Sasa maswali mengi nahisi
hapa polisi watakuwa wakijiuliza sana, huyu aliyetarajiw akwua kinaraka kwanini
hata kwenye mirathi awe ni mtu wa tatu…ujue huyu mtu kiukweli hata ndani ya
familia alikuwa hajulikani sana zaidi ya kujuliana na baba yake…. Na ukumbuke
huyo ni mtoto wa nje tu wa Makabrasha, hakuzaliwa kwa mke anayejulikana,
alizaliwa na mwanamke wa nje tu..Hapa kuna jambo,…sijaweza kuliweka sawa,
mtanisaidia..
***********
Mipango ilipokamilika na mikataba halali iliyokuwemo kabla ikaharibiwa,
na kuwekwa mikataba iliyogushiwa, na kilichobakia ulikuwa mkataba mpya ambao
ulionyesha dhamira ya Makabrasha, na huo ulileta sintofahamu, lakini kwa vile
Makabrasha alishajiandaa kwa hilo, akatoa vitisho vyake, na mume wa familia
akasalimu amri. Na kila kitu kikawa kimekamilika
Kilichokuja kuharibu sasa ni huo utaratibu wa nakala kuhifadhiwa
kwenye mtandao, sijui kwanini Makabrasha hakulifikiria hilo mapema, sijui
kwanini hata huyo mtu wa masijala hakuwahi kumuambia Makabrasha kuhusu hilo,
kama angelifikira hilo mapema, isingelikuwa kazi nguku kwa huyu mtu.
Kwa Makabrasha mambo ya mitandao anaifahamu sana , na ana watu
wake wanaoweza kufanya zaidi ya hapo,..na hadi hapo kila mtu anayehitajika
alishakuwa mikononi mwake. Nakumbuka siku zoezi hilo lilipokamilika, alifanya
shereeh fupi y akujipongeza na kujinadi kuwa sasa yeye ni kaam yule mtaalamu wa
kile kisa cha dunia yangu
Hadi hapo alikuwa ameshawaweka matajiri wengi mkononi, alikuwa na
hisa karibu kwenye makampuni mwengi makubwa, alikuwa akila sahani moja na
wanasiasa wakubwa, aliyekuwa amebakia ndio huyu mkwe wa mume wa familia. Sasa
aktika kuongea ndio nikagundua jambo
‘Sasa hata mkuu wangu hataniweza…’akasema
‘Mkuu wako!!! , kumbe kuna mtu yupo juu yako..?’ nikamuuliza
‘Hahaha, hivi ningelipatia wapi pesa nyingi ya kufanikisha haya
yote..yupo mkuu, na sio yupo, wapo, wakuu, wafadhili wangu…ila muhimu ndio huyo
mpinzani wa ..baba mkwe,…, lakini yeye hawezi kuniingilia kwenye mali zangu,
ana yake na mimi ninayangu, ila mimi nitamwezesha kufika juu, akifanikiwa yeye,
na mimi nimefanikiwa…’akasema na kucheka kicheko cha kishetani..
Tamaa ya Makabrasha sasa ilionekana wazi, kwani baada ya hapo, akatayarisha
mkataba wa makubaliano kati yake na wamiliki wa makapuni na yakimuweka yeye
kuwa kama mumiliki wa hisa nyingi kwenye kampuni ya mume wa familia,kama alivyozoanisha
kwenye huo mkataba.
Yeye hakuishia hapo,akatayarishwa mkataba mwingine ambao mali
yangu ikiwemo hospitali ya mume wangu yeye pia awe na hisa na nayo yalishafikia
hatua ya mwisho, na kama kikao kile cha kusaini huo mkataba kingelipita basi
ungelisikia makali yake, lakini hakikufanikiwa kwani ndio siku Makabrasha
aliuwawa...’akasema na kutulia, mwenyekiti alipoona mungumzaji katulia
akamuuliza.
‘Kwahiyo kutokana na maelezo yako wewe, inavyoonekana kabisa ni
wewe mlishirikiana na mpenzi wako, yaani mume wa familia kumzimisha huyo mtu au
sio..hatuingilii mambo ya polisi, ila hadi hapo inavyoonekana ni hivyo, mengine
ni kazi ya polisi, au sio, ? akauliza mwenyekiti akiangalia saa yake.
‘Ndugu mwenyekiti umenionya nisiingilie huko, lakini nikifanya
hivyo, ina maana kuwa ukweli halisi wa kifo hicho hautweza kujulikana …’akasema
mzungumzaji.
‘Kwahiyo unataka uendelee, natamani ufanye hivyo, ila uwe
makini..maana wahusika wenyewe wapo huko nje wanasikiliza..’akasema na wajumbe
wakatizama nje, hawakuona mtu, na mzungumzaji yeye akaendelea kuongea…
‘Kifo cha Makabrasha ni tukio ambalo halikutarajiwa…japokuwa huyu
mtu alikuwa na maadui wengi sana, lakini kutokana na jinsi alivyokuwa amejiweka
ulinzi wa kila namna kutoka ofisini kwake hadi nyumbani, alikuwa na
albi,..uhakikisho wa kujilinda kuwa hana kosa,
Kwa namna hiyo maadui zake, au yoyote aliyeathirika na mambo yake
alikuwa na kisasi naye, …tatizo ikawa ni nani wa kumvika paka kengele,..na watu
hujiuliza ni kwanini hakikutokea mapema, kwanini kifo chake kije kutokea muda
huo. Muda ambao kampeni zinaanza..muda ambao watu wake wangemuhitajia sana, kwa
mantiki hii polisi wanawaondoa watu wake kama washukiwa au sio…!!
‘Kumbuka kauli yake, ..sasa hivi hawataniweza tena, hata hao
mabosi wangu, ..kauli hii imeficha siri kubwa sana, kuwa kwa kusema hata mabosi
zangu ina maana kulikuwa na msigishano mwingien kati yake na mabosi zake
walishafikia sehemu wanamuogopa, lakini kwa polis hilo halina nguvu, kwanini,
jiulizeni sana hapo…’akatulia.
‘Lakini angalia haya aliyoyafanya, ina maana kama siku ile ule
mkataba ungeliwekwa sahihi na mume wa familia, basi…mume wa familia angelikuwa
hana chake, docta, na wengineo wengi, ambao walitegwa na huyu jamaa, na kwa
mtaji huo wangalipoteza hisa za makampuni yao, na wengine huenda ingekuwa ndio
mwisho wa utajiri wao, je hawa wanaweza kuwa washukiwa wakubwa, kwa mtizamo wa
polisi ndio…ndio maana hapa tunashukiwa, hapa ndio kutapatokana muaaji kwa
mtizamo wa polisi...
Mkataba ule ulikuwa na mambo mengi sana..iliyokuwa imebakia ni
sahihi moja ya mume wa familia, wengine kwa namna moja walisharubuniwa, kuacha
mume wangu ambaye bado alikuwa anasua sua, lakini hata yeye alishawekwa sawa,
anajua kwa vipi..
Hadi hapo swali la kujiuliza huo mkataba mkubwa ambao,
uliwajumuisha watu wengi, upo wapi…’akawa kama anauliza
Japokuwa kila mmoja alikuwa na mkataba wake wa kukubaliana ambao
ulikuwa ni siri kati yake na hao watu, ama kuuziana hisa au wanajua wenyewe,
lakini kulikuwa mkataba mkuu,…
Siku ile mume wa familia naye alitakiwa kufika, kukubali kuwa madeni
yake yatalipwa kwa kuuza hisa zaidi ya asilimia hamsini kwa Makabrasha, na
ilitakiwa siki hiyo kila kitu kikamilike, kwani akitoka hapo anakwenda kusajili
hiyo mikataba yake kwa wahusika.
‘Ina maana kulikuwa na mkataba mwingine ambao ni mkubwa zaidi..?’
akauliza mwenyekiti.
‘Ndio…huo ndio ulikuwa funga kazi, docta na wengineo walishaweka
sahihi zao, au sio docta,…? ‘ akamuuliza docta
Docta akaduwaa, halafu akatikisa kichwa kukubali, lakini sio ile
ya kukubali kabisa kabisa.
Siku ile aliyekuwa amebakia ni mume wa familia, yeye si mgonjwa,
yupo hospitalini,lakini hiyo hali indewe kwa makini, au sio…lakini pia ni
lazima na yeye aweke sahihi yake, ili nakala zote za mikataba zifikishwe kwa
wahusika, mume wa familia anauza kampuni yake kwa mtu mwingine kwa hasara…au
sio mume wa familia..’ akauliza muongeaji .
Kwa hali kama hiyo lolote lingeliweza kutokea, kwa hali kaam hiyo
watu wengi walikuwa na hasira na mtu huyo,….na walishajua kuwa siku hiyo ndio
siku ya hitimisho, wakichelewa …hawatakuwa na cha kwao…mauaji yakafanyika, na
mikataba ikatoweka, iliyobakia ilikuwa na mume wa familia, jiulizeni kwanini
ikawa hivyo..!
Ina maana huyo aliyefanya
hiyo kazi, ya kummaliza Makabrsha aliutaka huo mkataba mkuu..mkataba uliobeba
mambo mengi, ambao ungempa mamlaka Makabrsha, na mikataba mingine ya watu mbali
mbali pia haikuonekana tena..ukabakia wa mume wa familia..polisi waliwafuatilia
wale wote waliowahi kuandikishana na marehemu, lakini wote hawana habari…hawajui,
..ni kwanini.
Swali kwanini polis waendelee kuwaona watu kadhaa ndio wauaji,
wakati hali kama hiyo wauaji wanaweza wakawa mapapa makubwa tu…mumeona hapo
ilivyo..ni kwanini, hivi mnanielewa lakini, kwanini …washukiwa wawe akina sisi,
ambao, hatuna kitu …ni kwanini..
‘Ndugu mwenyekiti nahis hapo wewe una jibu zaidi ya sisi, ambao,
tunajikuta kama nyasi zinazoumia baada ya mafahali kupigana, lakini ni lazima
iwe hivyo…au sio mwenyekiti..’akasema shahidi na mwenyekiti akatabasamu na
tabasamu lake likakatishwa na simu
Simu ya mwenyekiti
ikalia…na mwenyekiti akapokea akawa anasikiliza kwa muda tu, na alipomaliza
akasema
‘Mpaka hapo, tunaweza kusema kuwa ..wewe na mume wa familia
mtakuwa mnafahamu ni nani muuaji, kama sio nyie wawili, kweli si kweli,…?’
akauliza mwenyekiti
‘Hahaha, mzee usiwe na pupa, subiria usikilize zaidi utaharibu
kila kitu, kama utawasikiliza hao watu … je mzee haupo tayari kusikiliza sehemu
ambayo itakusaidia hata wewe kwenye kupambana na huyo adui yako,…’akasema kama
anauliza
‘Ninahamu sana ya kusikia hilo, lakini polisi hawataki …’akasema
‘Unajua kwanini hawataki, ..?’ akauliza muongeaji.
‘Mimi sijui, lakini ni muhimu kufuata sheria, au sio..?’ akauliza
wajumbe
‘Lakini mwenyekiti, ngoja muongeaji aendelee ili tuone ukweli
ulipo, kwasababu huenda haki isitendeke hapo, nahisi kama siasa inataka
kuingilia haki…kwanini na sisi kama wanafamilia, tusifahamu ukweli,…’akasema
mke wake
‘Sawa ngoja tuvunje sheria kidogo, ili tusikie zaidi, ..sawa
shahidi unaweza kuendelea japokua tunakiuka sheria..’akasema mwenyekiti.
‘Sawa ndugu mwenyekiti, ila…kabla sijaingia sehemu hiyo ya pili,
nawaombeni kitu kimoja...’akasita kidogo, na kuchukau leso kufuta jasho.
Mwenyekiti hapo akashikwa na butwaa huku akiangalia saa yake na
simu ikawa analia kuashiria ujumbe wa sauti, yeye akazarau kuusoma huo ujumbe
akasema;
‘Kitu gani unachotuomba, ..?’ akauliza mwenyekiti akiwa kashikilia
simu tu, huku anamuangalia huyo shahidi kwa macho ya shauku, na mashaka fulani
‘Ni hivi ndugu mwenyekiti...’akaanza hivyo shahidi , huku simu ya
mwenyekiti ikianza kuita…
NB: Je itakuwaje, ndio hitimisho au?
WAZO LA LEO:Kila
mtu ana ndoto zake, na ndoto nyingine ni za kufikirika tu, hatuwezi kupanga
kununua gari , kujenga nyumba, au kufanya jambo kubwa wakati uwezo huo hatuna.
Tunaweza kuweka malengo hayo, kwa mipangilio ya kimaisha, lakini hatuwezi
kulazimisha yale yaliyo juu ya uweze wetu, tupange kutokana na uwezo na kipato
chetu. Zaidi ya hapo tutaingiwa na tamaa mbaya, ambayo mwisho wake ni kutenda
dhuluma.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment