Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, March 2, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-90


 Kiukweli kipindi hicho nilikuwa na furaha sana, furaha ya kuwa naolewa kwenda kuishi mjini na mtu mwenye uwezo, kwa muda fulani sikufikiria sana mapenzi yangu na mwenzangu, akili hiyo ilinitoka kidogo.

Lakini kabla ya hapo, nilikuwa nimekutana na mdada mmoja, ilikuwa ni bahati, tu,…nataka kulielezea hili najua wengi wanajiuliza ni kwa vipi nikawa nafanya kazi hiyo hatari ya upelelezi.

 Nahisi ilikuwa imepangwa iwe hivyo…, unajua mwenyezimungu humkadiria kila mtu na namna yake ya kutokea, riziki imepangwa hivyo, japokuwa ni muhimu kutafuta sababu, lakini iwe na uhalali fulani, ..siku moja alitokea kibaka, akamkwapua dada mmoja mgeni, sijawahi kumuona huyo mdada kabla,..ulikuwa mkubwa mnzuri, na kiukweli nihisi utakuwa na vitu vya thamani kama sio pesa.

Pamoja na maisha ya umasikini pale kijijini, mimi niliwachukia sana wezi,…basi yule kibaka alipomkwapua huyo mdada, akaanza kukimbia, akanipita mimi, nikaingiwa na hamasa, kwanini nisifanye jambo, kwanini watu hawaangaiki kumkimbiza yule mwizi, hapana lazima na mimi nifanye jambo

Nikaanza kumkimbiza, sasa watu wakawa wanaangalia kwa hamasa, mimi kama mwanake nitafanya nini…na huyo kibaka ni mwanaume, na  mwanaume kweli, anavyooneka, ana nguvu,…kiukweli kama angejizatiti, nisingeliweza kupambana naye kwa uonekano wa hivi hivi, lakini nilijiamini.

Kwa kukimbia mimi sio mchezo,…, yule kibaka alipoona aliyekuwa akimkimbiza nyuma yake ni mwanamke, mdada tu,…akasimama

‘We mdada unataka kuumia…’akaniambia nilimpomkaribia

‘Nipe huo mkoba wa watu, na wewe uwe salama, usitutie aibu hapa kijijini ..’nikasema

‘Hahaha, kwanza mkoba sio wako , pili wewe  ni mwanamke tu, huwezi kunifanya chochote na tatizo lako, hujui unayepambana naye, unajileta hadi huku,..kwenye mikono ya fisi utajuta kufanya…’akasema, sasa akiniangalia kwa macho mengine ya kutaka kufanya baya kwangu.

Nikawa nimeshamkaribia, hakuelewa kabisa malengo yangu, yeye akawa sasa kazarau, kasimama, ananiangalia mimi nitafanya nini kwanza, … hakuamini, maana nilichomoka kwa kasi na kuudaka ule mkoba mkononi mwake, na kuanza kukimbia, kuelekea mbele, na hata alipojaribu kunifuata hakuweza kunipata.

Baadae mbele nikageuza na kurudi kule kituoni na kumkuta huyo mdada aliyeibiwa mkoba bado kashikwa na bumbuwazi, nahisi kulikuwa na vitu vya thamani sana, nikamkabidhi mkoba wake, hakuamini, alisema

‘Oh, umewezaje wewe au…’aliishia hivyo, nikajua labda kahisi kuwa mimi ni miongoni mwa huyo mtu.

‘Uwe makini sana maeneo haya, …kuna vibaka..’nikasema

Na mara kwa mbali nikamuona yule jamaa akija,hakuogopa kurudi tena hakujali, nahisi maeneo ya pale wanamuogopa sana, sasa …alipofika pale akataka kunivamia mimi, kabla hata hajaniwahi mimi, akajikuta akipambana na huyo mdada, ilikuwa dakika mbili hivi, ..yule kibaka akawa kalala kwenye vumbi, mdomo unatoa damu, ilibaki historia.

Mimi pale nilipo nikawa na hamasa ya ajabu, alifanyaje, aliwezaje kumviringa na kumbamiza mwanaume yule …hadi jamaa akasalimu amri, nikawa najaribu kufanya kama yeye,..wakati huo watu wamejaa sasa..

‘Mwizi mwizi..sasa hata wale waliokuwa na hasira na huyo mtu wakawa wanatoa hasira zake, yule mwizi alipigwa na alikuja kuokolewa na mgambo wa kijiji..

Kiukweli tendo lile likawa mwanzo wa kunibadili, pale pale nilimuambia huyo mdada, wakati akiwa ananishukuru kwa kuweza kumuokolea huo mkoba , mimi nilisema tu

‘Napenda sana niwe kama wewe..’nilitamka hivyo tu, na huyo mdada akasema

‘Ombi lako limefika kwenyewe,..’akasema

Ni kweli kumbe huyo mdada alikuwa na ziara yake maalumu na katika harakati zake za kikazi akawa anatamfuta mdada jasiri anayeweza kumsaidia kwenye kazi zake na ndio ikawa mwanzo wangu wa kuanza kujuana na huyo mdada.

‘Ngoja nimalize hii kazi, lakini nitamtuma mtu aje kukupa mafunzo maalumu, tutawasiliana..ila nataka iwe siri, unajua kutunza siri wewe..?’ akaniuliza

‘Sana…’nikasema.

Basi huyo mwalimi kweli akaja, nikawa napata mafunzo maalumu, kwa siri..na ndani ya mafunzo hayo, kitu muhimu nilichojengewa ni usiri, asijue yoyote hata mpenzi wangu,..kuna namna walinijenga, nikakubaliana na hilo,.

Kiukweli hutaamini, nilitii, nikafanya hivyo, nikawa nimejiandikisha pale kijijini kwa mafunzo ye ushonaji, lakini humo humo, nakutana na huyo mwalimu wangu, napata mafunzo, asubuhi sana ni mazoezi, na jioni, akanijenga kiakili , ujasiri wa mwili ..na hayo yalifanyika kabla sijafika huku mjini.

Hivyo ndivyo nilivyoweza kuwa mdada mwingine, …mengine sio muhimu kuyaelezea hapa, au sio.. turejee sasa nirejee kwenye msingi wa maelezo yangu..

  Aliporudi huyo mshauri alituambiaje,…..

‘Nawabariki mkaolewe lakini ndoa zenu ziwe na lengo moja la ndoa tu ya makaratasi, mnanielewa…lakini ndani yake tuwe na mikakati mingine mnasikia, nataka kuwafundisha jinsi gani ya kutengeneza maisha ya baadae..mnielewe, sina nia mbaya kabisa,nia ni kuhakikisha na nyie mnakuwa watu, au sio…….. ‘akasema

‘Baso mimi sijakuelewa…’nikasema

‘Muhimu kwanza hilo lifanikiwe..la ndoa, mkipata ile hati ya ndoa, mengine niachieni mimi,…baada ya hapo, baada ya ndoa, nitakuwa na vikao vya mara kwa mara,..kwa mmoja au kwa wote wawili, nitawapatia mikakati muhimu, ila cha kwanza mpate hizo hati za ndoa, ni muhimu sana kwangu……’akasema

Basi ndoa zikafanyika…kwa sherehe na gharama ilikuwa juu yake, kiukweli ilitoa fora, sio kwamba tulifanya siku moja, hapana, kila mtu ilitokea kwa jinsi ilivyopangwa, ila sisi tulishazipanga siku hiyo,

Nipo ndani ya mume wangu naambiwa kuna mgeni, kutoka na kutana na mzee mzima, akaniambia …nina haraka, ila nataka kitu kimoja, fanya ufanyavyo, upate hati za biashara za mumeo..

‘Nini..?’ nikauliza , maana nilishasahau
‘Umesahau eeh, fanya hivyo…’akandoka.

Sikuweza kufanya hivyo, baadae ndio akapanga tukaja kukutana kikao akiwemo mwenzangu, kila mmoja alishajisahau, ndio akatukumbushia ile ajenda yetu

Alituelezea mikakati mingi sana, ukumbuke kipindi hicho mimi nilishaanza kujengekea kivingine, nilikubali tu pale …, lakini akili yangu ilikuwa na mtizamo mwingine wa maisha..mwalimu wangu alikuwa kajaribu kila awezavyo kunifanya binti wa kisasa, mwenye elimu nyingine, na nilishaanza kusoma masomo ya jioni, ndani yake kuna hayo masomo.

Pamoja na hayo moyo wangu hakuwa huru , haukuwa huru kwa vile bado nilikuwa nampenda sana mpenzi wangu wa asili, kile kitendo cha kuishi na mwanaume mwingine ambaye moyoni hayupo, ilikuwa kazi..kwa kipindi cha wiki moja hivi lakini nashukuru sana docta aijitahidi naye akanibadili kifikira ..yeye alikuja kugundua kuwa mimi sipo sawa, nakuwa nipo kam sipo,..aliligundua hilo mapema sana.

Mtu wetu hakuchoka na siku moja akatuita tena, akasema;

‘Sikilizeni kwa hivi sasa sahauni yaliyopita mnasikia, muwe na akili za kuona mbele, ili muonekane na hili lindi la umasikini, fanyeni ninavyotaka ..tafuteni hizo nyaraka haraka kabla sijaondoka..alisema anataka kusafiri.

Basi mimi nikajitahidi nikapata baadhi ya nyaraka ili tu kuona anachotaka kukifanya, na mwenzangu halikadhalika,..

‘Hizi sio muhimu sana…nitakuja kuwaambia ninazotaka..’akasema na hapo nikaona huyu mtu hana maana, kila ukimleta hiki anasema hicho sio chenyewe, tafuta hiki, nikaona ni ujanja ujanja wake, nikaja kumuambia kuwa mimi siwezi tena kufanya hivyo

Kuna jambo kubwa alipenda kutushauri,  tujizuie kupata watoto,ili watoto wasije kuwa ni kikwazo, na ikiwezekana tukutane sisi wawili kisiri tupate mimba, na hizo mimba tuwabambikie waume zetu hiyo ni moja ya mikakati yake aliyokuja kutushauri baada ya ndoa, ambayo haikuweza kufaulu.

‘Na muhimu zaidi mpate watoto wa kiume, mkiwapata hao, mimi nitakuwa mwalimu wao..’akasema na sikuelewa ana maana gani

 Mipango yake mingi aliyokuwa akituelekeza haikuweza kufaulu kwa vile kama mlivyoona, mwenzangu alianza kupata watoto na mke wake, na hilo lilimuuzi sana mshauri wetu, lakini hakukata taamaa akawa bado anatuelekeza mengine ya kufanya.. .na alisema, huyu kaharibu, lakini hata hivyo, kapata majike, hayo hayawezi kutuzuia kwenye mikakati yetu, muhimu nyie wawili mpate madume, na hayo madume myajenge yaje kuwa warithi wenu.

‘Ndoto ya madume ilimgusa sana mwenzangu, sijui aliambiwa nini na huyo mtu, na hayo yakiendelea, wao hawakujua kuwa mimi nimeshajengwa upande wa pili, nikiwa nao, nakuwa kama wao, nikitoka kwao nakuwa mwingine, na nikiwa na mume wangu nakuwa mke wa nyumbani, hayo niliyaweza..

‘Jingine kubwa ilikuwa, kutafiti undani wa familia tulizoolewa, tujue jinsi gani walivyopata utajiri wao..familia za wazazi wao,..alisisitizia sana kwa mwenzangu mimi hakuwa na mambo mengi kwangu, hayo nilikuja kugundua ni kwanini baadae.

Asikudanganye mtu, ukishaolewa au kuoa, akili yako yote inakuwa kwenye ndoa yako, ndoa inanoga,asikuambie mtu, hasa kama umeingia kwenye sehemu unayopata kila kitu, ndoto, na mipango tuliyopanga ikawa kama inayeyuka, na kila tukikutana kila mmoja anakuwa na dharura zake utaona tu, hata huyo mshauri tukawa tunampiga chenga, na hilo zoezi likawa kama limekufa, na kila mmoja akawa na malengo na ndoa yake.

Ni kweli moyoni bado kila mmoja alikuwa akimkumbuka mwenzake, lakini ki hali halisi, ni nani angekubali kuachia hali aliyo nayo, akarudi kwenye umasikini, hakuna, tulipokutana tena, akiwemo mshauri wetu, tukalibainisha hilo wazi kuwa ile mipango ya awali isitishwe, kwani haiwezekani. Ndani ya ndoa kuna vikwazo vingi, kwahiyo hayo tuliyoyapanga yasiwepo tena, kila mmoja kesharizika na ndoa yake.

Kauli hizo zikamkatisha tamaa mshauri wetu akatuona sisi ni wasaliti, akatuona sisi hatuna maana, na akaapa kuzisambaratisha ndoa zetu, na kusema hazitadumu, maana tumeolewa au kuoa, kwa ajili ya mali tu, na sio kwa ajili ya upendo.

‘Nyie mtaona, sizani kama ndoa zenu zitadumu, nawafahamu sana nyie mlivyo, kunguru hafugiki...mnafikiri mimi siwajui eeh, nitawachunguza juu chini, na ipo siku mtanikumbuka…’ikawa kiapo chake.dhidi yetu

Ndoa ya mwenzangu ilianza kuonyesha nyufa…, baada ya kuzaa watoto wale wawili, na katika makubaliano yetu ya awali ilitakiwa mtu asizae, kwani ukizaa watoto watakuwa vikwazo, mwenzangu yeye akazihirisha wazi kuwa yeye hayupo tena kwenye makubaliano hayo, akavunja miiko, mimi sio kwamba sikutaka kuza nasema ni mungu mwenyewe alinipa huo mtihani, sikuweza kushika mimba mapema.

Kiukweli mimi sikuwa hivyo sana, yaani kujali hayo ya huyo mshauri, kama nilivyosema nimeshajengwa kinamna, kitu ambacho sikuweza kukiacha,..ni mapenzi yangu ya moyoni, sijui kwanini, japokuw akiuwazi nilishaona kuwa mwenzangu hayupo nami tena, lakini sio mimi, moyoni muda mwingi nilikuwa namuwaza yeye,..hata hivyo kutokana na mafunzo yangu nikaona hakuna jinsi… nijipange kivyangu.

Baada ya mwenzangu kupata watoto wawili, nikaona mambo yanageuka, na mara mwenzangu akaja kunikumbushia ile mipango yetu, nikashangaa, na kumuuliza iweje sasa, na wakati yeye ana familia yake tana ana watoto wawili tayari, akasema, hana raha kwenye ndoa yake,..

Aliniambia hivyo,..hana-raha-tena-kwenye-ndoa- yake…yeye anaishi tu kwa vile ni sehemu yenye utajiri, lakini ndoa yake anaiona kama jela. Ohoo nikakumbuka ule usemi usemao, utasema hakifai, au hakitoshi kwa vile unacho, wakati ulipokuwa huna, ulikitamani.....sasa ndio yakawa kwa mwenzangu…sasa hana raha tena kwenye ndoa yake…

‘Sasa unataka tufanye nini?’ nikamuuliza

‘Tumtafute Makabrasha atusaidie,..’akasema

‘Hahahah, hapana, sikiliza achana kabisa na huyo mtu, huyo mtu sio mtu mwema, atakuangamiza, na kukuacha ukiumia, nimegundua kuwa huyo mtu ana malengo yake binafsi,...’nikamwambia,na kweli mwanzoni akanisikiliza.

Kumbe mwenzangu alishaingia kwenye mambo mengine ya ndani zaidi., akawa hawezi kuvumilia, akaanza kutembea na mfanyakazi wao wa ndani kwake, na sikuamini, mfanyakazi wake wa ndani ni mtoto mdogo sana kwake, ni lile umbile kubwa tu ndilo lilimponza, ..hayo alinificha kabisa, sikuyafahamu hadi huyo binti alipofika huko kijijini na mimba.

Huyo binti alipofika hakuonekana nilisikia tu yupo,  nikajitahidi hadi nikaonana naye, kwasababu anatoka sehemu ambayo mtu wangu wa moyoni yupo nilitaka kufahamu ukweli nikamuuliza kulikoni, akasema  ana mimba , mimba ya nani, awali hakukubali nilipotumia ujanja wangu akaja kuniambia ukweli, sikuamini, ikabidi niwasiliane na mwenzangu,  mwenzangu akanikatalia, kata kata…lakini ukweli ukaja kufahamika binti alipojifungua,  maana sura haijifichi.

Nikakutana na Makabrasha, na yeye akajifanya hajui, lolote, kumbe mwenzetu alishapata upenyo wa kuingiza mambo yake..hapo hapo kwenye hilo tatizo,.., akawa kapata nafasi ya kupata taarifa zetu za ndani, na aliyewezesha awali kulifanikisha hilo, yaani kupata taarifa za ndani, alikuwa ni huyo binti …

Huwezi kumlaumu, maana marehemu alikuwa ni mjanja sana, jinsi gani alivyoweza kuingia ndani ya kuwekeza vitu, ni,..kwa vile binti wa watu hakuwa mjanja wa kuligundua hilo, kwahiyo ikawa ni rahisi kwa mtaalamu kupandikiza vitu vyake,..na baadae binti alipopata mimba, na yaliyotendeka humo ndani akaja kuyapata kama ushahid wake wa kumnasa bwana mzee.

Kwangu mimi ikawa ngumu, na alipoona mimi ni mgumu na mjanja kwake, ndio akatafuta njia nyingine,kwasababu hadi hapo alishaniona kama tishio kwake, kwani najua njama zake, na pili sitoi ushirikiano anaoutaka yeye..

 Na jingine huyu Makabrasha alinifahamu toka siku nyingi, kuwa mimi sio mtu rahis sana wa kuingilika, kama alivyokuwa mume wa famila, na alinifahamu kuwa mimi ni mpinzani wake, kwahiyo akaona aniweke kwenye makucha yake kwanza, alichofanya ni kufuatilia nyendo zangu, kila ninalolifanya yupo nyuma yangu, na alinipatia kwenye kazi nilizokuwa nikipewa. Hakujua kuwa mimi nipo kazini.

Kuna kazi nyingine ilibidi ujifanye wewe ni changudoa, na inabidi wakati mwingine ujitolee kufanya hata yale yasiyowezekana kufanya ili kuupata ukweli, yeye akachukua kumbukumbu za matukio hayo, kama kinga yake, ujue kazi hiyo nilikuwa naifanya hata mume wangu hajui, hadi leo mume wangu hafahamu kuwa mimi nilikuwa siadii wa kujitegemea.

Kiukweli nilijitahidi sana kujificha, na ndicho bosi wangu alikipendea hicho, na siri ya hayo yote ni kuwa sikuwahi kumuambia mtu naifanya hiyo kazi zaidi ya bosi wangu..na kwa mume wangu yeye alijua nafanya kazi za kawaida za biashara za hapa za pale za mikononi, mali kauli, na hivyo, kumbe mwenzake nilikuwa na kazi za ushushu. Na alichoweza kukipata kwangu, huyu mtu ilikuwa sio kwa madhambi yangu, yeye hakulijua hilo, ila niliogopa je mume wangu akipata ushahidi huo itakuwaje..

Ukumbuke kuwa mimi na mpenzi wangu wa zamani pendo letu lilikuwa kama linaanza kufifia hivi, lakini sio moyoni, na mimi niliona tukiendelea kuwa karibu naye sana, hata yale ya siri yatakuja kujulikana,  kwahiyo siku mume wa familia akikwazika huko kwa mke wake, hana pa kwenda anakuja kwangu, tulikuwa tunakutana sehemu ambayo tuna uhakika hatutaonekana na hata tukionekana nisitambulikane.

Kama nilivyosema awali mimi nilishakuwa mtu mwingine, kuwa naweza kujibadili, naweza kujiweka kinamna ambayo mtu huwezi kunigundua, na nikifika kwa mtu wangu najirudisha kwa hali yangu..ni utundu tu kidogo wa kucheza na mavazi, ..na vipodosi , hata kuvaa ngozi za bandia, ..ni vitu vya kawaida , wala sio uchawi.

Lakini pamoja na hayo, mimi kwa vile nilishajitambua na nilishaona haya yanayoendelea hayana mwisho mnzuri, nilianza kutumie hekima ya kumweka mwenzangu katika njia sahihi, kuwa yeye ni mume wa mtu na mimi ni mke wa mtu, inabidi hilo tuliheshimu sana, vinginevyo tutakosa kote,…hilo likawa sasa linamkwaza mwenzangu.

Mimi nikawa najitahidi kulinda ndoa yangu yeye akitoka hapo hawezi kuvumilia tena, anatoka kwenda huko anapokwenda, kulewa na kufanya mambo ya aibu,.. nilikuwa naumia sana, maana wakati mwingine nayaona, ila sikutaka sana kumfuatilia kwenye mswala yake, kwasababu nilijua nitaumia,…kuna wakati mwingine unamuonea huruma, unafikia kumweka sawa, na hapo ..ndipo Makabrasha akapata ule ushahidi alioutaka yeye..

Ina maana aliweka vifaa vya kuchukua kila tendo tunalolifanya, nia na lengo lake ni kufanikisha kile alichokitaka...akilini na mafunzo yangu yalikuwa bado machanga ya kugundua vitu kama hivyo, japokuwa nilikuwa nafahamu vitu hivyo vipo, lakini sikuwa na….sikutilia maanani kuwa anaweza kutifanyia hivyo, kabisa…

Makabrasha, alipoona pia kuwa hayo aliyakusanya kama ushahidi wa kuninasa mimi hayampi mwanya wa kuyafanya yale anayoyataka yeye kuyafanya, akaamua kuingia ndani zaidi, alimshawishi mume wa familia ajitahidi kuwa name, alivyomshauri ili tupate mtoto wa kiume,..kumbe nia yake tendo halihis lionekane na liwe ushahid.

Alikuja kuweka seehmu ya sisi kukutana, hatukuelewa lengo hilo, kumbe humo alishaweka mitambo yake na bila kujielewa tukaja kunaswa..unajau tena huruma yangu iliniponza, nikafanya kile ambacho nilikipiga vita sana, ..na makabrasha akapata kitu cha kuninasa…

Ndani ya familia ya walengwa huko akaja kugundua hiyo mikataba, aliigundua katika mazungumzo yao, ..sasa jinsi ya kuipata ..ndio akatumia mbinu hiyo ya video za matukio, akagundua wapi ilipo, na..ilikuwa kazi rahisi kumshawishi mume wa familia kutoa ufunguo…

 Akawa sasa kafanikiwa kwa kiasi kikubwa,..na iliyobakiwa ikawa ni lugha za vitisho,akitaka kitu usipompatia, basi anaonyesha hayo madhambi, kuwa atayafikisha kwa mume wangu au kwa mke wa jamaa..

Hapo mume wa familia ikabidi afanye kila anachoambiwa,  angelifanya nini sasa, kwangu mimi bado ..japokuwa alikuwa na ushahidi lakini sana sana alitaka huko kwa mume wa familia,..baadae akafanikiwa kutimiza hatima yake ya kuingilia nyumba hiyo ya mume na mke wa familia kama alivyotaka yeye, kama alivyoelezea mwenzangu.

 Kuna mengi aliyoyafanya keshayaeleza aliyetangulia japokuwa kuna mengi mimi nayafahamu zaidi ya hayo…ila hadi hapo utaona kuwa ilifikia muda, mume wa familia akawa hana jinsi, ikabidi akubaliane na kile anachoambiwa na marehemu.

*********
 Nashukuru mungu kuwa hadi marehemu anaondoka, hakuwahi kunitambua upande wa pili wa kazi zangu, na hilo lilinisaidia sana,…nakumbuka siku moja alituita mimi na mwenzangu,..

‘Nduguzanguni, najua tulifikia mahali tukawa hatuelewani tena,..tukaondoa udugu wetu, urafiki wetu, nilijua itafika mahali mtakwama mtarudi tena kwangu, kwa hiari au kwa nguvu..sasa mumerudi kwangu, au sio..’akasema

‘Nawafahamu sana, kuwa huko mlipo hampo kwa mapenzi, na sasa nimepata ushahid huo, kuwa ndoa ya mume wa familia na mkewe haipo kwenye msimamo mwema, hiyo ni kuashiria kuwa siku yoyote ndoa hiyo inaweza kuwa marehemu, ..’akasema

‘Kwahiyo kabla ya hiyo ndoa haijafikia ukingoni, basi ni bora kuwa na mpango wa pamoja, kuhakikisha mali zote za familia zinakuwa mikononi mwa mume wa familia, lakini kwa vile mume wa familia ana mauchafu yake yakibainika atanyang’anywa kila kitu, sio vyema ikawa mikononi mwake, basi itafutwe namna mali hiyo itakuwa salama zaidi, kwahiyo mipango iwe ni namna gani mali hiyo itakuwa mikononi mwake

‘Mimi nayafanya haya kwa ajili yenu, ..mnasikia, nina uhakika ikiwa hiyo mali ikiwa kwangu kwanza kama wakili wenu , lakini pia kwa kumiliki hisa zaidi ya nusu, itakuwa ni salama zaidi.

 Hapo kwenye hisa mume wa familia akapinga, lakini akaja kuambiwa kama hili analiona gumu, basi alipe madeni ya huyo marehemu yote, kama ana uwezo huo..hakuwa na pesa, alishakuwa mtu wa madeni, alishafanyiwa mengi, ya kutoa pea ili apate picha au video, akakamuliwa hadi tone la mwisho, sasa akawa mtu wa madeni, isingelikuwa mke wangu angeliuza hata magari yakampuni..sasa akawa anakopeshwa na marehemu, hakujua anayefanya hayo yote ni marehemu,..

‘Marehemu alip[opiga mahesabu ya madeni anayomdai jamaa ikawa ni makubwa sana, jamaa hana uwezo wa kulipa,. Sasa afanyeje.., basi marehemu akasema njia ni rahis ni yeye kuyageuza hayo madeni kuwa hisa..alipe kwa kumuuzia hisa…ilikuja kuwa ngumu awali,  lakini mwisho wa siku mume wa familia akawa hana hoja,..ikabidi auze hisa kwa kulipa madeni ya marehemu..’akasema.

 Kila mume wa familia akipinga jambo, anakuja kuonyeshwa uchafu wake,  anadaiwa madeni, ..basi akawa mtumwa wa jamaa…na ikafikia muda sasa kashindwa akaja kwangu kuniomba msamaha, na kuomba ushauri…na alikuja kipindi ambacho hata mimi marehemu ananindama,..na ningemshauri nini mimi…, nilimuambia ukweli hayo umeyataka yeye mwenyewe iliyobakia kwasasa umuache huyo jamaa afanye atakavyo

‘Mimi siwezi nitamuua…’akasema

‘Wewe una ubavu wa kupambana na Makabrsha, hilo sahau, labda kama unataka kujitakia matatizo..’nikamwambia, lakini jamaa siku hiyo alitoka na ajenda ya kutafuta namna ya kumuua Makbrasha, na hata tulipokutana tena na tena akawa na ajenda hiyo hiyo, kuwa atatii yote, ila siku ya mwisho wa kusaini huo mkataba wa kukabidhi kila kitu hapo ndipo siku atafanya kile alichokidhamiria…

‘Mimi sipo, ..kama unataka kufanya mauaji, usinihusishe mimi kabisa..’nikamwambia

‘Nimekuambiatu..’akasema na siku zikawa zinakwenda nikaona wao sasa wapo sambamba, mikakati ya pamoja, ikawa inafanyika, hadi wakafikia kukubaliana kuwa hayo yafanyika kwa masilahi ya pamoja,..ndio ikapangwa mikakati ya kubadili huo mkataba wa familia, hayo yalifanyika bila ya mimi kushirikishwa.

‘Unajua pamoja na yote hayo mimi niliendelea kujitolea kuhakikisha familia ya mke na mume ipo salama, ilikuwa moja ya kazi angu kutoka kwa bosi wangu, kwa siri ajabu, lakini sikuweza kulitatua hilo, unauma na kupulizia, huku unafahamu mbaya ni nani.. nikawa sasa nafanya kazi mbili kwa waakti mmoja,

Kumlinda mpenzi wangu, na kuilinda familia na huyo shetani, asizidi kuleta madhara, na ili hilo lifanikiwe ikanibidi na mimi sasa niwe mtumwa wa huyo jamaa..


Nikaja kugundua kuwa sio marehemu tu, kumbe hata marehemu alikuwa akitumiwa, na kwa jinsi alivyofanya, isingelikuwa rahis kumdhibiti, ndio nikaongea na bosi wangu kuhusu hilo, lakini sikuwahi kumuambia kuhus mahusiaono yangu na mume wa familia, hilo lilikuwa siri kubwa sana kwetu anayefahamu ni marehemu na ili marehemu aendelee kulificha hilo,..ni mimi kuwa mtumwa wake

Katika kuhangaika nikajikuta mikononi mwa wapinzani wa mzee, sijui walinijuaje ila bado walikuwa hawana uhakika..na sio kwamba walinijua kutokana na kazi zangu ila wanasema wameona mimi nina kipaji cha kuwatumikia, umbo, sura..ujanja, kuongea, ..unajua tena,, wanakiniomba waniajiri kwao..

Kiukweli mimi niliwakatalia, japokuwa walikuwa tayari kunilipa mapesa mengi, ili niajiriwe na wao, ..walipoona kuwa mimi ni mgumu ndio wakamtumia Makabrsha, makabrasha akaja kuniambia hao watu wananihitajia, na hao watu ni hatari sana, wakikutaka uwafanyie kazi zao ukikataa, wanakuua, hawasiti kumuua mtu.

‘Sasa mimi nifanye nini..?’ nikamuuliza

‘Cha kufanya nitaambia utakuwa na mimi, nakuandaa ili baadae uje kuajiriwa na wao..’akasema

‘Mpaka lini..?’ nikamuuliza nikiwa na malengo yangu kichwani

‘Mpaka nitakaporizika mimi, maana nakuhitajia kwa kazi zangu, zikiisha basi, itabidi uende huko..’akasema.

‘Hapo una ujanja tena..ikabidi kwanza niandike barua ya kuacha kazi kwa bosi wangu, lakini sikuweza kumuambia dhumuni langu ni nini, ila nilitaka hata nikiingia huko, niwe na mikakati ya kulimaliza hilo kundi kwa namna yangu mwenyewe japokuwa najua hiyo ni hatari kubwa sana kwangu.

Nikamwambia Makabrsha nimekubali, lakini kwa masharti, kuwa aachane kabisa na familia ya mke na mume, aachana na kazi yake hiyo mbaya..

‘Hahaha, unajua hilo haliwezekani..’akasema

‘Kwanini…?’ nikamuuliza

‘Nitakuja kukuambia pale unakaposaini mkataba wa ajira kwangu, na mkataba wa kukubali kuwa umeachana na familia hiyo ya mpinzani wa bosi wangu..

‘Mpinzani wa bosi wako..?’ nikauliza kama mshangao

‘Ndiyo mambo ambayo utakuja kuyafahamu baadae..’akasema

Wakati huyu mdada anaendelea kuongea, kukasikika sauti, ya mtu kama analia..mdada akatulia kuongea na akitulia sauti hiyo inapotea badae akaja kugundua ni nani analia..

‘Sasa unalia, utalia sana, hapa ndio nimeanza, nilikuwambia leo ndio siku ya hukumu, upende usipende, hukuniamini, hapo ndio nimeanza…’akasema mzungumzaji


NB: Naishia  hapa kwa muda,


WAZO LA LEO: Ukweli unauma lakin ukweli ndio njia sahih ya kutatua magumu yote, tujifunze kuwa wakweli kwa watu wenye kuaminika, …
Ni mimi: emu-three

No comments :