Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, February 27, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-88



Sikuweza kuvumilia tena niliona liwalo na liwe, nataka kumpata mtoto wangu…

Tuendelee na kisa chetu..

**************

Kuna kitu kimoja tunajifunza kwenye kazi zetu, hata siku moja usitake hasira ndio zikutawale ukashindwa kuhimili nafsi yako, ukijua kuwa adui yako ana kila kitu. Ni muhimu sana kuwa makini, kwani adui wengine hawajali, kutoa roho za wengine sio kitu kigumu.

Kwahiyo pamoja ya kuwa niliondoka mle ndani kwa hasira, bado utaalamu wangu wa kiupelelezi niliulinda, nilitoka kwa tahadhari, na kuhakikisha kuwa sitafanya  makosa yatakayo mgharimu mtoto wangu.

Ujue kwa muda ule nilikuwa kwenye ofisi niliyopewa, ofisi yangu eti kama bosi mtarajiwa, kwahiyo nilipotoka pale nilikuwa kwenye ofisi za ghorofa ya juu, sio kule chini sehemu ya kulala…na anilijua siku hiyo sitakubali kwenda kule tena, mpaka nijua hatima ya mtoto wangu.
Nikatoka mle ndani ya ile ofisi nikawa natembea nikipita ofisi ya kwanza, ofisi ya pili nikasikia sauti, kwanza nilihakikisha mbele au nyuma hakuna mtu anayenifuata, nilijua huenda maeneo yote hayo yana video za kuchukua matukio, sikujali kwa hilo

Nilijifanya kama nataka kuingia kwenye ile ofisi, huku nikitegea siku kubahatisha tu, hao watu humo ndani wanaongea nini…

‘Nimeshakufanyia kila kitu unachokitaka, nimekutii, nimekusaidia na sasa umefanikisha kile ulichokitaka,kwanini bado waendelea kunifanya kama mtumwa wako, ...’sauti ya kike ikalalamika.

‘Ndio wewe ni mtmwa wangu ulielewe hilo, japokuwa nafahamu kuwa nakuonea, lakini ni kwa vile wakati mwingine hutaki kunitiii amri yangu, inabidi nifanye haya ninayoyafanya sasa hivi..’sauti ya kiume ikasema

‘Kiukweli nimechoka..’sauti ya kike

‘Sikiliza  ninachotaka mimi kutoka kwako ni utii, nikitaka hiki ukifanye, basi ukifanye mara moja, ndivyo makubaliano yetu yalivyo,...hata hivyo nisamehe, leo akili yangu haijakaa sawa,...nisamehe mtumwa wangu eeh,..’sauti ya kiume

‘Sitaweza kukusamehe kamwe..’sauti ya kike

‘Nisikiliza basi…mimi nakuhakikishia kuwa, hili likikamilika, wewe na wengine wote mtakuwa huru, usiwe na wasiwasi na hilo…haya mambo nataka yamalizike ili hata mimi nitulie, na kuanza kula raha za dunia,….habu nikuulize kwa hivi sasa kuna kitu unanidai...’sauti ya kiume ikauliza.

‘Nipe hizo kumbukuzi zote za mapicha machafu uliyochukua kutoka kwangu na kwa watu wengine, niziharibu, hapo ndipo nitaamini maneno yako, ili watu wawe na amani na ndoa zao...’ sauti ya kike.

‘Hilo kamwe lisikutie wasiwasi, ndoa zenu zitakuwa na amani kama nyie wenyewe mtajituliza na waume zenu, tatizo nyie mumekimbilia kuolewa kwa kutaka mali, na sio upendo, kwahiyo hilo sio kosa langu..au nimekosea…’sauti ya kiume

‘Sio kweli, sisi pamoja na hayo tulishaamua kutulia na waume zetu, mengine uliyatengeneza wewe, ili yatokee na upate unachokitaka..’sauti ya kike

‘Hapana sio kweli, mimi nilijua tu hamutaweza kutulia, hamtaweza kuwa mbali mbali, ipo siku mtakumbukana, na sikufany aharaka kwa hilo, taratibu kama yule ndege tai…anavyovizia mizigo,..kwahiyo sio kosa langu, ila mimi nawahakikishia kuwa kazi hii ilikuwa na mipaka na muda wake, ikikamiliza, haina haja tena, hizo picha, video, nitaviharibu, mbele yako, wewe nipe mud unimalize kazi hiyo iliyobakia,...’ikasema sauti ya kiume

‘Na malipo yangu je…?’ sauti ya kike

‘Malipo gani zaidi, ..bado kazi haijaisha unataka malipo, malipo yako utapata usiwe na shaka…’sauti ya kiume

‘Kazi gani imebakia,..mikataba si imeshakamilika su sio, sasa hivi unamiliki hisa, kuna mipesa kibai umeshalipwa na wahanga wako wa milungula,..bado huajtosheka unataka nini wewe, kiukweli wewe ni  shetani asiyeshiba madhambi..’sauti ya kike

‘Hahaha napenda sana hiyo lugha yako, kumbe unafahamu kuwa mimi ni shetani, basi mambo bado…kuna mambo bado hayajakamilika..’sauti ya kiume

Mara nikahisi kuna suti nyuma yangu…haraka nikajifanya kutembea hadi ofisi za mbele na nilipohakikisha hakuna mtu, nikarudi tena kusikiliza kwa muda kama ule ulikuwa mchana watu wanapita, lakini siku ile sikuona watu wakipita pita na hata wakitokea ni mtu anatoka kwenye ofisi fulani na kuelekea chini au juu.

Niliporudi pale nikasikia

‘Mimi nayaelewa hayo yote, kuwa ni mabaya na hayana mwisho mwema,  ndio maana njiandaa kuachana na tabia hiyo, nikikamilisha hili, natulia, ....nitakuwa na haja gani tena, wakati nitakuwa mkurugenzi mkuu wa makampuni kadhaaa, yenye mabilioni ya pesa, ....tatizo anayenichelewesha ni huyo mtu wako wako, ngoja akija kesho kutwa, eeh…’akatulia

‘Kesho kutwa au kesho..?’ sauti ya kike ikauliza

‘Kesho nina mambo mengine ya kufuatilia, kuhakikisha hiyo mikataba imefika sehemu husika, na kwenda kukutana na wafadhili wangu, kuwahakikishia kuwa mambo yapo kama ilivyotakiwa iwe, kwahiyo ushindi ni lazima…’sauti ya kiume

‘Sikiliza…mimi sihitaji kuingie kwenye siasa, nataka kuwekeza kijijini, mimi sitaki kuishi mjini, nataka maisha yangu yawe huko kijijini, hadi hivi sasa mume wngu anafahamu nipo huko…’sauti ya kike

‘Najua sana ni nini unakifanya huko, na hayo yote ulifanya kwa kuogopa au sio…sasa hutakwua an hajaya kuogopa, usitishike na wanaume akitaka kukuacha, muambie afanye hivyo, hataweza maana hai hapo atakuwa hana kitu…’akasema

‘Tatizo wewe unajiaminisha sana, unafikiri wao ni wajinga wakae kimia tu..’akasema

‘Ndio maana nilikuambia hivyo kuwa muda wa kuziharibu hizo picha na video bado, hukunielewa, hivyo vitu havijamaliza kazi zake, zitamaliza kazi zake pale tutakapohakikisha hao watu hawana kitu na hawana namna ya kufanya,..na wafadhili wangu wameridhika, na kushika hatamu…na mimi huku niwe na mamlaka ya vitega uchumi vyote..’sauti ya kiume.

Kukawa na ukimia fulani hivi…halafu sauti ikasema

‘Kuna nini, mbona umesimama kuongea, una mashaka gani na maneno yako au umeona nini…?’ sauti ya kike ikauliza

‘Kule ofisi ya bosi wako, hakuna ishara,…unaona hapa, kuna alama nyekundu kuashiria kuwa huko kuna tatizo,.. yaonekana kamera za kuonyesha matukio za kule hazifanyi kazi, kuna nini..unajua huyo bosi wako simuamini, ni hatari sana, yawezekana kafanya jambo…’sauti ya kiume ikasema

‘Huyo mnamsumbua bure, yeye ni mzazi, na sioni umuhimu wake kwa hili… muachieni akasome, na mpeni mtoto wake, hana tatizo na nyie..yeye kawakosea nini..unajua hadi hivi sasa mimi kama mimi sioni umuhimu wake….’sauti ya kike ikasema.

‘Wewe utakuja kuona umuhimu wake….na unanishangaza sana,…haya yaliyotokea hadi yeye kuweka sahihi hujaona umuhimu wake, wewe hujui kuwa huyo ndiye kiongozi wao wa usalama, huyo tukimweka mikononi, hao watu hawana ulinzi, hawana mtu wa kumtegemea…sikiliza kama haupo upande wangu niambie, nifanye vitu vyangu…’sauti ya kiume ikasema

‘Kwani mimi nilikuwa upande wenu, mimi mumenilazimisha na sina la kufanya, nitakutii, ili utimize mambo yako, lakini mkimaliza …hapo na mimi nitakuwa huru, na kiujumla mimi sitaki kujishughulisha na jambo lolote hata bosi wangu nilishamuambia hivyo…’sauti ya kike.

‘Wewe au mwingine, ukiishiwa pesa hukumbuko ulichosema, sikiliza wewe uwe upande wetu, sehemu  ambapo pesa hazikauki, unasikia,..oh, unaona hapa, hii alama bado inaonekana, na sioni chochote kule alipo huyo bosi wako, yule mlinzi kaenda wapo, nampigia simu hapatikani..’sauti ya kiume

Kukawa na ukimia kidogo, halafu sauti ikasema tena.

‘Nahisi mitambo ya pale imeharibika, kama sio yeye kafanya jambo basi kuna tatizo, ngoja niongee na mtu wangu…’sauti kasema na kukawa na ukimia fulani baadae sauti ikasema

‘Na huyu mshenzi sijui kaenda wapi, simu yake haipokelewi, sasa sikiliza hebu nenda wewe, kaangalie kinachoendelea unasikia, …’sauti ya kiume ikamsema

‘Sawa nitaenda, ila usiwe na wasiwasi na huyo mdada, nilishamuweka sawa, anajua madhara yake anampenda sana mtoto wake, hawezi kufanya jambo la ajabu, hebu angalia tena labda ni mitambo yako tu hiyo..’sauti ya kike ikasema.

‘Nisikiliza amri yangu…unasikia wewe nenda,…’sauti ikasema

‘Sawa bosi,…’kabla hajaondoka suti ikasema

‘Kabla hujaondoka,ule mkataba niliokuambia uuchukua kwa mume wako upo wapi, unajua kesho,  ndio siku nataka kwenda kuufanyia kazi,..unafikiri nimesahau eeh..’sauti ya kiume

‘Nilikuambia bado sijaupata, na nitaupate na mimi sipo naye, unajua mimi nipo wapi, unaniuliza kitu ambacho hata wewe unakifahamu, mimi nipo wapi, si nipo kijijini, au umesahau,..hata hivyo, mimi naona hayo ya mume wangu achana nayo, hayafai, hayana umuhimu, wa nini kwanza..?’ akauliza

‘Ina umuhimu sana, tunamuhitaji sana huyo mtu, achilia mbali na kazi yake lakini pia kisiasa, ana umuhimu wake,…ngoja nikimalizia hii kazi mimi mwenyewe nitamfuatilia, utaona nilivyo, …yeye mwenyewe atasalami amri, kuna video yake mbaya nikimuonyesha ni lazima atanitafuta…’akasema

‘Video yake!! Video gani hiyo..?’sauti ya kike ikauliza

‘Siwezi kukuonyesha wewe…ukiiona unaweza ukachanganyikiwa,  na sitaki uende  kuleta fujo,..wewe una umuhimu sana hapa, tatizo lako ulimuamini sana, hakuna msafi hapa, mimi wote nawafahamu madhambi yao, asikudanganye mtu, wewe tulia na mimi ule nchi,…’sauti ya kiume.

 Niliona nikiendelea kukaa pale ninaweza kushukiwa kwahiyo nikasogea hadi kwenye mlango, nikausukuma ule mlango kwa taratibu,.. nikaona unafunguka…mimi kwenye begi langu nilikuwa na kifaa, nikakitoa na kuchukua kitufe kidogo, kama kitenesi, nikakiweka hicho kifaa,..ni kidogo, huwezi kudhania ni kitu muhimu sana, nilipohakikisha kuwa mlango upo wazi, nikakitumbukiza kile kitenesi, kikawa kinaserereka kulekea  ndani.

‘Umedondosha nini…na mbona mlango kama upo wazi,..’sauti ya kiume ikauliza

‘Kumedondoka kitu, !! ni kidude cha kuwekea peni, mmh, na wewe una msikio, umesikiaje na wewe upo unaangalia mitambo yako huko..?’ sauti ya kike ikauliza

‘Kila kitu kinachofanyika kwenye maeneo yangu ninakiona hapa.., ila huyu bosi wako kawa mjanja…kwa hivi sasa simuoni kabisa, .., haya wewe nenda kamuangalie..hivi sasa ni mchana sitaki mimi kuonana naye,.., hiyo kazi ni yako, na akifanya ujanja tu..mtoto wake kiukweli atampoteza, sitanii hili, unanifahamu nilivyo.’sauti ikasema

‘Sawa bosi…ngoja niende..’sauti ya kike

Na mimi niliposikia hivyo, nikageuka na kuondoka, kwa haraka nikitaka kurudi ofisini kwangu, lakini kabla sijageuka, nikahisi mtu yupo nyuma yangu…

‘Unafikiri unafanya nini hapa…’ilikuwa sauti nyuma yangu na kabla sijamjibu kitu mara mlango ukafunguliwa akatokea mdada,…mmh, sijawahi kumuona huyu mdada kabla, muonekano wake ni kama mzungu fulani hivi, aliponiona kwanza alishtuka baadae akasema

‘Kwanini hujapiga hodi,…nilikuambia ukija upige hodi, sasa sikiliza bosi hana muda wa kuongea na wewe, twende huko huko ofisini kwako..’akasema huyo mdada.

Na jamaa yule aliyekuwa nyuma yangu akabakia kaduwaa, …tukawa tunatembea kuelekea kule ofisini kwangu na huyo jamaa sasa akawa anataka kufungua mlango kuingia kwenye hiyo ofisi aliyotoka huyo mdada, huyu mdada akasema;

‘Wewe, Bosi alikuwa akikuulizia muda mrefu, kakasirika sana, ukienda kuonana naye sasa hivi utalikoroga, wewe katulie kituoni kwako kwa muda, baadae ndio uende, kama atakuhitajia tena..’akasema mdada

‘Poa….kwani hukumuambia kuwa nilitoka kidogo..’jamaa akasema na kuondoka kurudi huko alipotoka.

Na sisi tukarudi ofisini kwangu, na huyo mdada aliyejiweka kama mzungu akasema;

‘Wewe vipi kwanini unataka kuharibu…?’ akaniuliza

‘Sina amani nataka kuonana na mtoto wangu..’nikasema

‘Sikiliza nimeshakuambia kila kitu kitakuwa sawa, wewe hakikisha unafanya kila wanachokita wao, kwanini hunielewi, utaharibu na utakuja kujijutia, …’kabla hajamaliza akaona kazi niliyoifanya kule juu..

‘Mungu wangu, huyu mtu akija kuona  hiki kwanini uemvunja hiyo taa,…?’ akauliza,

‘Wewe muite fundi, aje arekebishe kwa haraka lakini asirudishe hiyo video kamera, wewe huoni kuwa hiyo video kamera ilikuwa imefichwa kwenye hiyo taa,, je waweza kumuita fundi akarekebisha hilo tatizo kwa haraka..?’ nikamuuliza huyo mdada

Huyo mdada kwa haraka akachukua simu na kumpigia fundi, haikupita muda akaja fundi akapata maelekezo, na haikuchukua muda, kila kitu kikawa sawa.

‘Safi kabisa,…’nikasema

‘Sasa wewe rudi kwa jamaa yako endelea kuongea naye, nataka kupata ushahidi zaidi..’nikasema

‘Kwa vipi, ok, bosi nimekuelewa, ila tafadhali usifaney tena hivyo, fuata wanavyokuambia, mengine niachie mimi, …’akasema huyo mdada na kuondoka.

Nilisubiria kidogo, baadae  nikachukua simu yangu na kugeuza upande wa nyuma nikatoa kitu fulani kweney begi langu, nikakiweka kwenye ile simu,  baadae mitambo yangu ikaanza kufanya kazi….nikawa sasa nasiiliza kile wanachokiongea kule kwa huyo jamaa,, mpaka muda huo nilikuwa sijafahamu ni nani, huenda ni Makabrsha, lakini sikuwa na uhakika huo.

‘Umemkuta bosi wako, kafanya nini mbona bado mitambo haionyeshi kitu..hivi yeye hajui haya yote ni kwa jili yao, yeye akiwa mmojawapo..’sauti ikauliza

‘Yupo lakini hana amani, anamtaka mtoto wake…’akasema

‘Mtoto wake wa nini, hajui hayo ni kwa usalama wa mtoto wake, wewe unafikiri kama hao wenzetu wangelimchukua huyo mtoto ingelikuwaje, wangempima kwanza DNA, halafau ikawa ndio sababu ya kuharibu kila kitu…’akasema mwanaume

‘Ni kawaida kwa mzazi yote hasa mama wa mtoto, huwezi kumlaumu kwa hilo, ila nimeongea naye, baadae atarudi kule chini kujiandaa kwa ajili ya kile mlichomuagiza au sio..’sauti ya kike

‘Sawa hakuna shinda baadae nitakwenda mwenyewe kuona kuna tatizi gani..lakini sitaki akiwemo humo ndani..’sauti ya kiume.
.
‘ Sawa bosi, jihangaishe tu, lakini hawo hawo unawasumbua, ..hasa huyo docta, na wengineo, watakuja kuwa mashahidi siku ukiwa umesimama kizimbani...’ikasema sauti ya kike.

‘Thubutu, labda kizimba cha kaburini, lakini nikiwa hai , hivi hivi, hanipati mtu, wewe hunijui tu, kila kitu kina plan A na B, ..kwa hivi sasa wameshasambaatika na hakuna wa kumfunga paka kengele,…’sauti ya kiume.

‘Sawa bosi…’sauti ya kike.

‘Sawa bosi, sawa bosi,..unajifanya mtiifu kumbe kigeu geu…nakuambia ukweli baada ya haya, utakuja kuniona umuhimu wangu,  …hata hao watu wa usalama sasa hivi wananiheshimu, kuna tatizo kidogo, nasikia, huko kwa mdhamini wa mikataba, kuna kitu kimetokea, ..lakini nitamaliza hilo tatizi ..’sauti ya kiume ikasema.

‘Haya wewe jidanganye tu, umesema kuwa docta naye umepata video ya mapicha yake mabaya, ulimpataje madhambi yake, maana namuona ni mtu mtulivu sana,...?’ sauti ya kike ikauliza.

‘Hawo unaowaona watulivu, ndio balaa, wana mambo yao ya chini kwa chini, na wakati mwingine ni uwoga tu, nilimkamatisha kabinti kamoja karembo, ...huyo binti alifika kwake kama mgonjwa, na huyu bint anajua kazi badala ya matibabu, ikageuka kuwa kitu kingine,..sitaki uone hayo, hayo ni kwa ajili ya kazi, msamehe tu, hata ingelikuwa ni mimi nisingeliweza kuvumilia, hahaha…’akasema

‘Mjinga mkubwa wewe kumbe sio yeye, ni wewe ulimkamatisha kabinti, sasa unatarajia nini, kuwa utanitishia mimi, kuwa mimi nikiona hiyo video na mapicha hayo mabaya,tutaachana na mume wangu…, hahaha, hata kama nitamfuma akiwa mbashara, mimi sitaumia saaana…, maana najua mimi nina madhambi zaidi yake..’sauti ya kike.

‘Ni wewe, lakini sio yeye, docta ni muoga wa kufumaniwa, anajali sana ndoa yake, ila kwa …huyo mdada, alishindwa, na pia, …ile ya yeye n mpenzi wake wa zamani, pia ninayo, siwezi kukuonyesha,..japokwua sio mbaya kihivyo, lakini inaonyesha hisia za kuwa hao watu bado wanapendana, mimi kwangu inatosha akbisa kama ushahid..hao watote hawaniwezi ..kila mmoja nimeshamuwekea kinaso chake, …na wafadhili wangu watafurahi sana…’ akasema na mara sauti ikasimama.

‘Kiukweli mimi sitishiki tena na huo uchafu wako, fanya utakayo, lakini mimi nina imani ipo siku utaumbuka, na ...’akatulia kidogo, hapo nikaingiwa na wasiwasi, nikifikiria huenda wamekishitukia hicho chombo nilichokipenyeza mle ndani.

‘Mbona unasita kuongea, ongea tu..mimi nakusikiliza..’sauti ya kiume

‘Ni wewe nakuona kama unaangalia angalia chini, umeona kitu gani....’sauti ya kike.

‘Kuna kitu hakipo sawa, una uhakika yule mdada hajafanya kitu, ..?’ akauliza

‘Kama wewe huniamini, nenda ukaone mwenyewe..’sauti ya kike ikasema

‘Siwezi kwenda kweli kwa hivi sasa, ila nitakwenda, ni lazima kuna kitu kimefanyika, nitakwenda kuhakikisha, huyo mdada ni hatari....’sauti ya kiume.

‘Sasa mimi naondoka…kuna zaidi la kufanya..?’sauti ya kike

‘Usiondoke kwanza, nataka wewe uhakikishe huyo mdada akiondoka umemuweka sawa, unasikia, asije akaharibu,…nilitaka muende naye hadi uwanja wa ndege, lakini wewe utabakia huku nyuma kuhakikisha mambo fulani fulani, na mtoto tumemuhamisha, kwa usalama zaidi..’akasema

‘Ina maana huyo mdada hataondoka na mtoto wake..?’ akauliza

‘Hapana huyo mtoto atampata siku ile akiondoka, siku akirudi masomoni baada ya kuhakikisha kila kitu kipo shwari, huyo ndiye ndoana yetu kwa hivi sasa, na ni kwa manufaa yake, ili wenzetu wasije kumuona huyo mtoto maana mpaka sasa hawajahi kumuona sura yake..’sauti ya kiume

‘Na zaidi ya hapo utanihitajia kwa lipi zaidi au ndio nitakuwa nimemaliza kazi na wewe..?’ sauti ya kike ikauliza

‘Unahitajika kuwepo pia na huyo mwenzako akija, nataka huyo kidume wako, akubali kila kitu, aweke sahihi kwenye mikataba yote ikishamalizika hiyo kazi imekamlika, yeye hana kitu, atakwua chini yangu, na wewe utamfanya utakavyo, maana …usione kuwa mimi ni mbaya, nafanya hivyo, kwa vile yeye akibakiwa na hizo mali hana akili ya kuziendeleza, umeona anavyofanya , …tunahitajia watu kama mimi na bosi wako, na wewe…umenielewa, yeye ndio ataendelea kuwa na hisa, lakini mamlaka,hayawezi…unasikia…’akasema

‘Mimi sitaki kuonana na yeye, unajua mimi sijulikani kuwa nipo hapa Dar, unalifahamu hilo, pili, sitaki kuwa karibu na yeye kwa hivi sasa, uzalendo utanishinda, kanisaliti vya kutosha, nita…’hakumaliza

‘Najua najua hilo, pole sana….lakini usimlaumu sana, maana yote hayo yamefanyika ili kuhakikisha hili zoezi zima limekamalika, sizani kama wewe una haja ya kuwa na wivu, au sio…’sauti ya kiume na kukawa na ukimia fulani baadae akasema

‘Unaona eeh…nimegundua kitu kwenye hii mitambo, kule chumbani kwa mdada, ile kamera imevunjwa, na waya zimeharibiwa ni nani kafanya hiyo kazi, nahisi unalifahamu hilo..’sauti ya kiume

‘Mimi sijui..na mbona niliona ni taa tu imeharibika..’sauti ya kike

‘Mbona hujaniambi,..na ni nani alitengeneza..?’ akauliza

‘Ni yule yule fundi wetu, sasa vitu vidogo kama hivyo ni mpaka nikuambie au umenileta hapa kwa kazi..?’akaambiwa

‘Basi kwa ujinga wake…huyo fundi sijui lakini…atakuwa kaharibu zile waya za kamera…itabidi baadae niende kuifanya hiyo kazi mwenyewe…’sauti ya kiume.

‘Sawa..mimi sikulijua hilo…’akasema

‘Acha ujanja wako wewe, nakufahamu sana, wewe ni mnafikii …usifikiri mimi nakuaminii sana, hakuna kitu kama hicho,…sikiliza alichofanya huyo bosi wako hakiwezi kuniathiri kamwe, mweneywe utaona, najua kuna kitu kakipandikiza mahali, kama sio kwako basi kuna mbinu katumia, huko alipo anatusikiliza..’akasema

‘Mimi sijui hayo… na sizani kama kuna ukweli wa hilo, hawezi kufany ahivyo akijua kuwa mtoto wake yupo hatarini…’akasema mdada

‘Ni kweli, mimi sitasita kufanya lolote kwa mtoto wake, akijifanya mjanja,atakuja kujuta,…ngoja nione la kufanya..’sauti ikasema na mimi pale pale nikaharibu mawasiliano na kile kitufe kwahiyo hataweza kukigundua wapi kilipo. Hata akikigundua ataona kama kitenesi tu kisicho na uhai

Mimi pale nilipo, sikutaka kupoteza muda, kwa haraka nikachukua vitu vyangu, na kujiandaa kurudi chini, ili nikajiandae kwa ajili ya kwenda uwanja wa ndege, nilikuwa radhi sasa kufanya kama walivyotaka, kwa usalama wa mtoto wangu, sikuona kama kuna lolote zaidi, ilimradi nimepata uhakika wa usalama wa mtoto wangu.

Nilikaa kidogo pale chumbani, na  ulipofika muda ambao ndege inayotoka huko inafika, akaja mtu kunichukua hadi uwanja wa ndege na kama walivyotaka ndivyo nilivyofanya…

 Mzungumzaji hapo akatulia akimuangalia mwenyekiti na mwenyekiti alikuwa kimia, kama akiwaza jambo, na mdada akaendelea kuongea;

‘ Na yaliyokuja kuendelea hadi siku ile ya tukio ni kama nilivyowaambia awali..zaidi ni mambo ambayo sitakiwa kuyaongea hapa…maana hayo ni ya kazi za polisi, ila kama mwenyekiti ataruhusu hilo, kwa kibali cha polisi, kwanini tusiweke wazi, mnasemaje wajumbe

Mwenyekiti akatikisa kichwa kukataa.

*********
Mwenyekiti akachukua simu na kupiga namba akawa anaongea kidogo na huyo aliyempigia halafu akasema;

‘Je mume wa familia hayo yaliyoongelewa hadi hapo na huyu askari kanzu wenu au rafiki wa mke wako ni kweli,..unakubaliana nayo..?’ akauliza mwenyekiti na mume wa familia akabakia kimia

‘Natumai sasa kama wewe ni muungwana, na …mimi nakushangaa sana, hivi hadi hapo hujioni kuwa una makosa,…au wajumbe mnasemaje,..nilijua huyu mtu, utaungama nasisi kama familia, akiri kosa, na tuwe kitu kimoja ili kupambana na huyo adui yetu, eti jamani…’akasema mwenyekiti.

Mume wa familia akawa kimia tu, na wakili wake naye akawa kama anafungua makabrasha yake, hakusema neno.

‘Mume wa familia, tunaongea na wewe hapo sio sehemu ya wakili wako, maana  ukweli sasa upo wazi, na muongeji aliyepita ni mtu wako wa karibu, na zaidi ya hayo ni mtaalamu wa upelelezi, unasemaje mume wa familia...?’ akauliza mwenyekiti, na mume wangu akatulia kimiya kama sio yeye aliyeulizwa na baadae wakili wake akawa anamuongelesha jambo, lakini mume wa familia akawa anatikisa kichwa kukataa.

Baadaye sana mume wa familia akasema;

‘Tatizo sio mimi kukubali hayo yaliyoongewa,  au kukiri kosa, wangapi hadi hapo wana makosa, ni mimi tu mwenye makosa, hapana,… tatizo hapo ni huyo muongeaji, mengi kayaongea kutilia chumvi ili nionekane mimi ni mbaya, haya..si mumeshaona mimi ni mbaya, nina makosa, na wengine je, …mnataka mimi niseme nini hapo…’akasema

‘Tunataka wewe uthibitishe kwa kauli yako je hayo yaliyosemwa ni kweli au sio kweli, ili tuendelee..?’ akaulizwa

‘Kaongea mengi, kamuongea marehemu, kawaongelea watu wengi, na wengi ni kama mimi, kila mmoja ana makosa yake, hata yeye muongeaji ana makosa yake mengi , na mkumbue hayo aliyoyaongea nikipindi  mimi nilikuwa mgonjwa, sasa mimi nitawezaje kukiri kosa wakati sikuwa na ufahamu…’akasema

‘Unajua hueleweki, ina maana muda wote alichokuwa akiongea muongeaji hakuwa na sisi, swali nakuuliza tena, haijalishi yaw engine je hayo yanayokuhus wewe ni y akweli au sio ya kweli, maana hapa kikao kipo kwa ajili ya familia yenu,…je ni kweli au si kweli labda nikuulize hivyo..?’ akaulizwa

‘Niwaambie ukweli wangu kutoka oyoni au sio, kwanza ..huyu mtu muongeaji kwanza mimi simuamini, ndio ni mtaalamu wa kupanga hoja, lakini hakuwahi kutoa ushahidi au shahidi wa yoet hayo aliyoyaongea, ni nani shahidi wa kumuunga mkono hayo, ndio mimi au sio…ndio mnataka mimi niwe shahidi wake,..lakini mjue jambo moja kuwa huyu  mtu  ni mnafiki mkubwa, msaliti, na hayo aliyoyasema…’akasema

‘Kwahiyo hayo aliyoongea sio ya kweli..?’ akaulizwa

‘Ndio mengi sio ya ukweli, yapo ya ukweli hayaana ubishi, lakini mengine kaongezea uwongo wake, na kafanya hivyo, kwa vile keshajua kuwa rafiki yake kamshitukia, na akaona njia ya kujikosha na kutunga huo uwongo,, ...na kwa uwongo wake huo, nitahakikisha, kuwa unawajibika,..’ akasema huku akiwa kamwangalia mwenyekiti, na baadaye akamgeukia rafiki yangu na kusema;

‘Wewe, unafikiri kwa kuongea hivyo, umesalimika, unajidanganya, hata siku moja tajiri hamuangalii masikini mara mbili, ukikosea ujue huna maana kwake, umechezea shilingi kwenye shimo la choo, umenisaliti na mimi…, na kwahiyo wewe huna maana kwao, na huna maana kwangu......kabisa huna maana kabisa...’akasema

Wajumbe walimuangalia kwa macho ya kushangaa na alipoona hivyo, haraka  akisimama, na wakili wake akawa anamuangalia kwa alama ya kuuliza machoni, yeye hakujali hilo, akaanza kutembea kuelekea mlangoni, na watu wakabakia kimia tu, baadae kabla hajafika mlangoni mwenyekiti ndio akasema;

‘Mjumbe unajua unachokifanya ni kukidharau kikao, unakwenda wapi, wakati  kikao hakijaisha, unanidharau hata mimi mwenyekiti...’akasema mwenyekiti,

‘Siwezi kuendelea kukaa hapa kuzalilika, kila mmoja aliyesimama ananisimanga mimi tu, wengine wana mabaya yao, hamtaki waambiwe, mnajua na mimi ninafahamu kiasi gani kuhusu  mabaya ya wengine, kiukweli mimi siwezi kuvumilia tena, uwongo wenu umevuka mipaka najua kwa hivi sasa sina langu au sio, na mumejitahidi kuni dhalilisha, kunivua nguo sina thamani  tena hapa..na ushahid upo wapi, eehe, niambieni...’akasema na kabla hajamaliza sauti ikatokea kutoka kwa mmoja wa wajumbe, ilikuwa sauti ndogo iliyochoka…’,  ikisema;

‘Mimi ni shahidi wa hayo yaliyosemwa, ndugu mjumbe kabla hujaondoka, ningelipedna mimi kuyathibitisha hayo, aliyoongea mjumbe aliyepita...’ sauti hiyo ikasema na wakati huo wajumbe wengi walikuwa wakimuangalia mume wa familia, akitaak kutoka nje,  na aliposikia sauti hiyo akasimama

Na wajumbe wote wakageuka kumuangalia huyo muongeaji mpya, ni nani, na hata mwenyekiti akafanya hivyo.

NB: Ni nani huyu tena, anataka kusema nini


WAZO LA LEO: Ni kawaida kwa binadamu, kulalamika, pale anapotendewa ubaya, lakini binadamu huyo huyo, akimtendea mwenzake anaona ni jambo la kawaida tu,...ni bahati mbaya, ni ibilisi, nk ,  sio vizuri tukijenga tabia hiyo, kwani sote ni binadamu hakuna mwenye moyo wa sugu, usiohisi maumivu, ndio maana wahenga wakasema  mkuki ni kwa nguruwe,...
Ni mimi: emu-three

No comments :