'Aaah, umeniumiza, ...nini unafanya wewe...’sauti ikaniuliza,.
Ujue humo ndani kukizimwa taa ni giza kweli,
‘Kwani wewe nani na lengo lako ni nini?’ nikamuuliza
‘Wala usisumbuke kuwasha, nimekuja kukusalimia, tu, kesho asubuhi
nina kikao na wewe, ajenda ni moja, kukubaliana na hayo tuliyoyapanga,…’akasema
Tuendelee na kisa chetu..
**********
'Kikao na wewe, kama nani kwangu...?' nikauliza kwa hasira
‘Utanifahamu tu, ila kifupi mimi ni mjumbe tu , mjumbe hauwawi...au sio...'akasema
'Nyie ndio mbwa wa hao mabwana zenu...'nikasema
'Vyovyote iwavyo...muhimu ni wewe kutii amri, unasikia, hutajutia kwa hilo, ukikubaliana na kila kitu, wewe utakuwa bosi wetu, hilo lipo kwenye ajenda, sikufichi hilo, kwahiyo hapa nakuelekeza ila baadae nitakwua nikitii amri kutoka kwako, huoni jinsi watu hawa wanavyokupenda.
'Wananipenda au ni tamaa zenu.
'Sio tamaa madamu, haya ni kwa manufaa yako..kiukweli baada ya hapa, wewe utabadilika kabisa, kutoka kwenye kuita wengine mabosi, na wewe kuitwa bosi, tena muheshimiwa, unafaaa sana,..hilo ujiandae nalo, wewe utakuwa mtu mashuhuri na tajiri,..'akasema
'Mimi ni mjumbe tu , lakini hayo yameshawekwa wazi, unaandaliwa kuwa kiongozi , sifa unazo, na muhimu ni wewe tu ukubaliane na hayo utakayotakiwa uyafanye, mengine kwa hivi sasa ni kwa
manufaa yako, kukuhakikishia kuwa wewe na familia yako mpo salama, kiufupi huyu mtoto alikuwa anawindwa na watu wengi, wewe hujui tu.
'Nahisi hata wewe uliliona hilo ndio maana ukamuacha nyuma, lakini sisi tulijiandaa kabla ya hapo, kuwa mtoto hatapata madhara, atalindwa kwa nguvu zote, na hadi unaondoka hapa mtoto atakuwa salama, lakini sis tumeona atakuwa salama akiwa nasi, sio akiwa na wewe,...zaidi ni masilahi yako na mtoto huko mbeleni....’akasema.
‘Hujanijibu swali langu, wewe ni nani…?’ nikamuuliza
‘Utanifahamu kesho, samahani kwa usumbufu, nashukuru kwa kuwa
mvumilivu, ukifanya hivyo, na kufuata masharti yetu, ukatii yote na kuyafanya
yote tunayoyahitajia, hutapata taabu, wewe na mtoto mtakuwa salama hadi hapo ukirudi huko masomoni, na tutazidisha elimu yako ikibidi...'akasema
'Sina haja..'nikasema
'Haja unayo, sema hujafahamu nia njema yetu...na hujafahamu kuwa haya tunayafanya kwa ajili
yako, na familia yako, hebu jiulize hao waliojifanya wanakupeleka kusoma kweli wana nia njema na wewe, utakuja kuona siku ukimaliza masomo yako , kama kweli wanakujali, hapo walipo wanatafuta njia ya kukumaliza, sis ndio wenye nia njema na wewe,...mwenyewe utakuja kutushukuru kwa hilo . ..’akasema
‘Nimeshakuambia sina haja na msaada wenu, …’nikasema
‘Kwa hivi huwezi kuliona hilo, subiria mdua utafika utaliona hilo, sasa lala kwa amani, usingizi mororo....usijali..’akasema
na kuondoka...
Ndugu mwenyekiti kauli yao hii, kama ningelikuwa nataka kuwaamini wao, ningeliwaamini, nilikuwa najiuliza ni nani walifanya namna mpaka nikaja kuokolewa na hao watukutu waliotaka kuniharibu ....ni hawa walilijua hilo kabla, na ..huko tupaache kwanza au sio...
**********
Kiukweli baada ya huyo jamaa kuondoka, bado mwili wangu ulikuwa haujawa sawa, mwili ulikuwa hauna nguvu, viungo
vilikuwa kama sio vyangu, nahisi huyu jamaa alipulizia tena ayo madawa yao ya kunivunja nguvu,ili nilale u nisiweze kufanya lolote, kwani kweli pale nilipojilaza kitandani tu, usingizi mnzito
ulinichukua, hadi pale nilipozindukana, ..
Ilikuwa ni asubuhi...
Nilipofungua macho, niliona mwanga wa kawaida hakuna giza tena,
nikajaribu kukumbuka matukio ya usiku wake, nilijua kabisa hao watu walikuwa
wamenipulizia hayo madawa yao ili nilale, walinijua kama wangeliniacha huru, ningelifanya jambo, hata hivyo pale nilipozindukana tu akili yangu ilikuwa kwa mtoto wangu.
'Mtoto wangu yupo wapi, je ni kweli yupo salama...' ilikuwa hali hiyo, na ilinifanya nisiwe na amani.
Kwa haraka nikatoka na
kuingia bafuni baada ya mazoezi kidogo nikijua sasa nipo vitani,..nikaoga kwa
haraka na kurudi pale chumbani, kwa umakini nikagundua kuwa kuna mtu aliingia
wakati nipo bafuni, kuna mabadiliko, kuna vitu vimeondolewa, hali ya hewa haikuwa nzito tena, hali ya hewa ilikuwa shwari, utahisi kama upo ufukwenu mwa bahari, upepo mwanana, na humo ndani hakuna dalili ya kipozoe hewa!
Kwa vyovyote vile kuna mtu aliingia humo nikiwa bafuni, akafanya
jambo kwa haraka sana, sikujali hilo, mimi nikavaa nguo zangu kwa haraka na
kuanza kutoka, kuelekea ile sehemu ya maongezi, nisubirie kitakachofuata. Huku akili yangu ikiulize 'mtoto wangu yupo wapi, na je kweli yupo salama...
Kabla sijashika mlango wa chumbani ili kutokea sehemu hiyo ya
chumba cha mapumziko, mara nikasikia sauti ikisema;
‘Habari za asubuhi mpendwa, tunatumai umelala salama, japokuwa
haupo na amani , na tunajua hilo ni kutokana na kutokuweza kuwasiliana na mtu wako uliyempa mtoto ukiwa ndani ya ndege, usijali kuhusu hilo, mtu uliyempa mtoto wako,
anafahamu kabisa wewe ndiye uliyemuhitajia mtoto wako, na mtoto wako akaletwa
hapa kwetu sehemu salama zaidi..’akasema
‘Ssshit…’nikasema
‘Kwahiyo kuhusu mtoto wako, unakuhakikishia kuwa mtoto wako yupo
salama, atapata kila kitu anachohitajia apate, tunafahamu huduma zake zote..., cha muhimu ni wewe kufuata masharti yetu,
vinginevyo, mtoto wako unaweza usimuone tena katika maisha yako yote na hilo tunaweza,...’sauti
ikasema
Nilikuwa nimeganda pale
mlangoni nikisikiliza hiyo sauti, sikuona sehemu inapotokea ni kama sauti hiyo
ilitokea kila sehemu ya hicho chumba.
‘Ina maana hawa watu walifanya mbinu wakamchukua mtoto wangu, mmh
sitawasameeh kwa hili na anayehusika, siku nikipata muda, nita-m-maliza huyo mtu kwa
bastola,..’ nikajisema moyoni, na kweli nilidhamiria kufanya hivyo.
Nilitaka mtu kama huyo asiwepo tena hapa duniani, na kusumbua
watu, japokuwa nitakwua nimechukua sheria mikononi mwangu.
‘Huyu atakuwa ni Makabrasha tu…hakuna mwingine siku nikikutana naye siampa muda wa kujitetea hafai kuishi huyu mtu...’nikajisema hivyo.
Baadae nikatuliza kichwa, nikahisi kama ..yaani, naanza kuona jinsi wanadamu tulivyo, kuwa hatuna maana, pindi tu nilikuwa na mtoto wangu, sasa hivi hayupo, sasa hapo yupo hai, na sina uwezo wa kumuona..je...yaani niliwazia mbali sana...
Kiukweli hapo ilibidi nimkurubie mwenyezimungu...nilimuomba sana,.... mtoto wangu awe salama, hata ikibid mimi nife lakini mtoto wangu awe salama...kiukweli mimi sio mtu wa dini
sana, lakini kwa muda ule, dini ikanijaa moyoni. Nikatambua bila mola wetu, bila rehema za mola wetu, hatuwezi...hebu angalia tukio lilivyokuwa, wewe kama wangelitaka waneglifanya lolote, ningefanya nini pale...
Nikafika ile sehemu ya maongezi, ...na
nikakuta kila kitu kipo tayari mezani kifungua kinywa cha kila namna, kuonyesha kuwa wanajiweza…. ,
lakini kiukweli sikuwa na amani, nilikula kidogo tu, nikasogea kwenye magazeti
nikawa nasoma kupoteza muda..
Mara mlango ukafunguliwa, ….aliingia mdada, huyu sio kama yule wa
kwanza, kwa wajihi, japokuwa na yeye alijifunika usoni, watu wote hawa hawajionyeshi sura zao, kuanzia wanaume hadi wanawake,...yeye akachukua vifaa, halafu akasema;
‘Tuongozane tafadhali…’akasema na mimi nikawa namfuata
nyuma,..
'Tunakwenda wapi...?' nikamuuliza
'Wewe nifuat tu, usiwe na wasiwasi...'akasema huku tunatembea hadi sehemu ya mwisho ya eneo hilo la gorofa ya chini, na
baada ya hapo, unatakiwa kupanda ngazi kwenda juu, na huyu mdada akasema
‘Subiria hapa…’akasema na hapo hapo akapanda ngazi na kuondoka, na
haikupita muda mara akatokea mtu kwa nyuma yangu, nikahisi unywele wa nyuma ukisisimuka kuwa kuna adui nyuma, nikasubiria..mara sauti ikasema
‘Haya twende…’sauti ikasema nyuma yangu
‘Twende wapi..?’ nikamuuliza kisauti ya kibabe kumuonyesha kuwa siogopi, lakini sio kweli, kwa hali kama ile ni lazima uwe na mashaka.
‘Panda ngazi, utaambiwa wapi pa kwenda tukifika huko juu…’akasema
Nilisita kidogo, lakini baadae nikaona haina haja, ngoja kwanza
nitoke eneo hilo, nikafanya kama alivyotaka,..tukatembea hadi juu, nahisi ni
ghorofa ya pili juu, sikuwa na uhakika kwani tulikuwa tunatembea kwenye ngazi
tu.
Tulipofika juu , akasema;
'Subiri...'akasema na yeye akapita mbele yangu, maana kipindi chote hicho yeye alikuwa nyuma yangu...akawa ananikagua na mashine alipojirizisha akawa anaongea na simu kwa suati ndogo sikusikia kitu.
'Haya tembea twende mbele...'akasema na mimi nikafuata maelekezo yake, tukawa tuantembea kupita ofisi mbali mbali kuna majina yake mlangoni, hadi kwenda ofisi moja, haikuandikiwa
kitu mlangoni, nilijua ni ofisi pale tulipoingia ndani,.
'Ingia huko ndani na kaa kwenye kiti, na kuna chochote unachohitajia, ukitaka maji, vinywaji, chai, unaweza kujisaidia, ni ofisi yako kwa muda...'akasema na hakutaka kusema zaidi huyo akaondoka zake, na mimi nikaingia humo ndani.
Kilikuwa chumba cha ofisi chenye kila kitu cha
kiofisini, nikaambiwa nikae hapo nisubiri, na akma naihitaji chai, kinywaji, chochote kile naweza kujisaidia...lakini sikutaka kitu , nikaa kimia tu kusubiria, na mara
Sijakaa sana, mara mlango ukafungulia, akaingia jamaa mmoja kama kawaida zaidi usoni kavaa mawani makubwa, kuficha uso,na hata ndevu za bandia, niliona hilo kwa uzoefu wangu, akasema;
‘Samahani bosi, nimeleta huu mkataba, nimeambiwa uweke sahihi zako, lakini kabla
ya kuweka sahihi una dakika kama tano hivi, za kusoma kilichoandikwa, ili uwe
na uhakika kuwa watu hawa hawana nia mbaya na wewe, natumai, unaelewa wajibu
wako, mtoto wako yule salama ...’akasema na kuniwekea hilo faili mbele yangu,
nikalichukua na kuanza kufungua ukurasa mmoja mmoja, nikawa nasoma;
Ulikuwa mkataba wa hiari, ambao mimi nakubali kuwa nitafanya kazi,
chini ya kampuni iliyotajwa jina, na nitakuwa nikimtii kiongozi wake, hapo
kwenye kiongozi wakaacha nafasi , hakukuweka jina la huyo kiongozi. Sehemu
nyingine, inataka mimi nikubali kuwa mtoto huyo ana baba yake, jina , sehemu ya
jina hakuna kitu, mbele yake, ikasema,baba huyo ndiye mwenye mamlaka na huyo
mtoto, na mtoto atapata haki zake zote kutoka kwa baba huyo...na yeye kama mama
atapata haki zake.
‘Hivi ni mkataba gani huu wa kutegeana, kampuni gani, sioni jina,
baba wa mtoto simuoni jina lake..unataka niweke sahihi kitu ambacho hakipo
kamili, ni sheria gani inasema hivyo…?’ nikauliza
‘Hawajaandikwa hapo kwasababu maalumu, lakini ukiweka sahihi,
..naweza kuja kukuonyesha wataonekana…muhimu ni usalama wa mtoto wako au sio…’akasema
Kukawa na maelezo mengine mengi, ya hisa, na mimi nitapewa sehemu
ya hisa, kama nitakubaliana na yote hayo, na kutimiza maagizo yote, na nilitakiwa
nisimtambue mtu mwingine yoyote kama bosi wangu zaidi ya huyo aliyetajwa
hapo,....huyu aliyetajwa hapo ni nani, nilitaka kuuliza lakini nikaona haina
haja
Nikamaliza, kusoma, nikainua kichwa kumuangalia huyo mtu aliyeleta
hayo makabrasha, nikamuuliza
‘Kwanza mtoto wangu yupo wapi?’ nikamuuliza
'Samahani bosi, ...Mimi sijui maswala ya mtoto wako yupo wapi, niamini hilo, nilichoambiwa nikuhakikishie ni
kuwa mtoto wako yupo salama, ..ukimaliza kuweka sahihi, mimi nimemaliza kazi
yangu...'akasema na kutulia kidogo, na aliponiona nipo kimia akasema
'Je umemaliza kusoma huo mkataba, umeona ulivyo, mengi ni
kwa masilahi yako..sasa kama umemaliza kusoma, tafadhali…,weka sahihi yako, tumalize
kazi, ukizidi kuchelewa ndivyo utakavyozidi kuchelewa kumpata mtoto wako bosi.....’akasema
‘Mimi siwezi kuweka sahihi yangu mpaka nimuone mtoto wangu...sijui
kama kapata maziwa sahihi, muda kama huu alitakiwa kupata maziwa yake maalumu.’nikasema
na kabla sijatulia mara ukutani kukatokea maandishi, na taswira ni kama vile unaangalia
runinga, na mara mtoto wangu akatokea, akiwa kabebwa na mwanamke, na huyo
mwanamke alikuwa akimpa huyo mtoto maziwa ya mpira, yale yale ninayompa kila
siku, na mtoto wangu alikuwa katulia
Pale nilihis machozi yakinilenga lenga…nilitamani nisimame na
kufanya jambo, ili mtoto wangu afahamu kuwa mama yake nipo…lakini ningelifanya
nini, na huyo mtu akasema;
‘Natumai umemuona mtoto wako..yupo salama, na kila kitu anapata
kama ulivyokuwa ukimpatia, sasa sikiliza...sahihi yako ndio itakayofanya mtoto
wako aendelee kuwa salama, na ndio itakayokufanya umpate mtoto wako, ili mambo
mengine yaendelee…’akasema
Na mimi kwa haraka nikachukua peni, na kuweka sahihi yangu, hiyo
ni sahihi maalumu, ambayo, naitumia kwa wakati kama huo, huwezi kuona tofauti,
lakini mimi mwenyewe nafahamu wapi nimebadili.
Nilipomaliza kuweka sahihi, nikaweka peni chini, na yule mtu
akanishika mkono, akaniambia;
‘Hapa kuna sehemu ya kuweka dole gumba hapa tafadhali kidogo,…’akasema
na kunishika mkono, akaweka kidole gumbe mbele, ili niguse kitufe cha wino,
kidogo nilitaka kugoma.
‘Usilete ubishi madam,..mtoto wako…’akasema
Baadae nikaona haina haja,
akakiweka kidole changu kwenye wino, na kidole hicho akagandisha kwenye
zile karatasi, hakufahamu kuwa mimi nilishajiandaa kwa hilo, hiyo alama
itakayoonekana hapo, haiwezi kuonyesha usahihi wa dole gumba langu.
‘Nafikiri tumemaliza, subiri kuna sehemu unatakiwa
kwenda...’nikaambiwa, nikasubiri kidogo mara akaja mtu na kuniambia nijiandae,
kwani tunatoka nje ya jengo, na ninatakiwa kufuata masharti kama namjali mtoto
wangu.
‘Hivi nyie watu mna ubinadamu kweli…’nikasema
‘Kwanini madam, kuna kitu umefanyiwa kisicho sahihi, niambie ..?’
akauliza
‘Mimi ni mama wa mtoto, na mtoto wangu bado mdogo, anahitajika
kuwa karibu na mama yake…’nikasema
‘Wakati ukiwa huko unasoma, mtoto wako aliweza kukaa masaa mengi
bila ya wewe au sio, akawa anahudumiwa na mtu mwingine, yaya…au sio…na isitoshe
wewe humnyonyeshi mtoto wako, au sio, maziwa yako yana matatizo au sio…,
ulishauriwa usimnyonyeshe na docta, nipo sahihi…’akasema huyo jamaa kama
ananiuliza
Sikuelewa hayo yote aliyafahamu vipi , maana kiukweli sikuweza
kumnyonyesha mtoto wangu maziwa yangu, ilitokea chuchu zangu kuvimba na
nikimnyonyesha mtoto wangu napata maumivu makali, docta akanishauri
nisimnyonyeshe. Kwahiyo mtoto wangu alianza kutumia maziwa ya mpira bado mapema
tu.
‘Hiyo haijalishi,…mimi nahitajia kumuona mtoto wangu, angalau mara
moja kwa siku.. mimi sitaweza kufanya lolote mpaka nimuone mtoto wangu, nimguse,
awe karibu na mimi...’nikasema na mara kwenye ukuta nikaonyweshwa mtoto wangu, sasa
akiwa kashikiwa kisu kooni...
‘Shsssiti...nyie ni mashetani..’nikasema, sikutaka kusema jambo,
nikaondoka na hawo watu, tukashuka ngazi , sasa tukitoka nje ya jengo, na
tulipo fika nje ya jengi, karibu kuingia kwenye gari, huyo muongozaji akasema;
‘Tumechelewa, lakini haina shida, tunatakiwa kwenda kumuona
mgonjwa…’akasema,
‘Mgonjwa gani..?’ nikauliza
‘Mzazi mwenzako...’nikaambiwa hivyo, sikutaka kuuliza zaidi, nikahisi ni nani,
tukaingia kwenye gari, na gari likaondoka, hadi hapo nikaona niwe mpole tu, ili
nione mwisho wa haya mambo ni wapi.
Na kweli tukafika hospitalini, ni ile hospitalini alipokuwa
kalazwa, mume wa familia, nikaongozwa hadi sehemu alipolazwa, na kwa muda ule
ilikuwa sio muda wa kuona wagonjwa, lakini mimi nikaruhusiwa, nikaingia ndani
alipolazwa mume wa familia, alikuwa chumba cha peke yake.
Kiukweli nilipomuona huyu mtu, nilitaka nimvamie na kumparura na
makucha maana nilihisi kuwa ni yeye au hata kama sio yeye, kiongozi, lakini ni miongoni mwa hao watu wabaya wangu.
Nilishawachukia kikomo cha kuwachukia, we acha tu..
‘Vuta subira…’nafsi ikaniambia hivyo
Nikasogea hadi pale kitandani, na jamaa nilimkuta akiwa kalala,
lakini sehemu hii ya juu imeinuliwa kama kukaa hivi, akageuza kichwa
kiniangalia na tabasamu likajaa tele mdomoni mwake, mimi sikutabasamu,.
Na alitarajia kuwa
nitamsalimia, mimi sikufanya hivyo, na wala sikuuliza anaendeleaje, swali langu
likawa hivi;
‘Ina maana na wewe upo kundi moja na hawo watu, hao watu
waliomteka nyara mtoto wangu…?’ nikamuuliza. Na nilimuona akashtuka, unaona kabisa mtu akishtuka,
kuonyesha kuwa hajui au labda anaigiza kufanya hivyo.
‘Eti nini!!!, wamamteka nyara mtoto wetu, haiwezekani, ngoja
niongee nao...’akasema akionyesha mshangao, na sasa akawa anachukua simu, na
mimi nikamzuia na kusema;
‘Haina haja, ila nakutahadharisha, kama upo kundi moja na hawo
watu, ujue, kitakachotokea baadaye hutaweza kuamini kuwa mimi ndiye huyu
unayeniona hapa mbele yako, unasikia...’nikasema
‘Una maana gani kusema hivyo, mimi sijui chochote….’akasema
akitikisa kichwa kukataa hivi
‘Haya yaliyotokea sitaweza kuyasahau,..maishani mwangu, kuniweka
roho juu, mpaka sasa sijui mstakabali wa mtoto wangu, sijui yupoje, mnataka
nini kwangu, nakuambie ukweli hili utakuja kulijutia, wewe na hao wenzako,
...’nikasema
‘Unanilaumu mimi bure,…Mimi nimeletewa taarifa kuwa umefika kutoka
huko masomoni kwa dharura, sijui ni dharura gani, na baadae leo naambiwa
utakuja kuniona,…sasa..’akasema na mimi nikamkatisha na kusema;
‘Unajifanya hujui kinachoendelea huo mkataba wa hiasri kuwa mimi
nikubali kuwa wewe ni baba wa mtoto wangu, na utawajibika naye umetungwa bila yaw
ewe kufahamu..?’ nikamuuliza
‘Hayo nimeambiwa leo hii, alipokuja huyu mtu kunipa taaarifa hiyo,
na mimi sikuwa na pingamizi na hilo, mimi nimekubali kuwa nipo tayari
kuwajibika kwa ajili ya mtoto wetu, kwani hapo kuna kosa, kwanini nikate hilo,
nikifahamu hiyo ni damu yangu..na pia nikaambiwa umekubali kuweka sahihi
..kwanini mimi nikatae, sasa tatizo lipo wapi hapo...’akasema
‘Tatizo ni kuwa nyie hamnifahamu kuwa mimi ni nani...sawa mimi
sina zaidi, nashukuru kuwa nimekuona, na naona umepona, tofauti na nilivyoambiwa
kuhus hali yako, najua ni janja yenu, uzidi kuonekana unaumwa, au so...’nikamwambia
na yeye akawa kama kakumbuka jambo, na kujiweka kitandani kama mgonjwa
aliyezidiwa.
‘Usijabarague ndugu, kujiigiza huko itafika mwisho wake, hata kama
unaumwa, lakini sio kivile au sio, ipo siku mtaumbuka na haya yote yatasikika
kwa kila mtu na hata wale ambao hukutaka wasikie huu ukweli...’nikasema
‘Janja gani lakini, naumwa, na sijasema naumwa kivile, niliwaambia
hii hali yangu naweza kukaa nyumbani na kuendelea na kazi zangu, lakini wao
wakasisitiza kuwa ni muhimu nikae hapa kwa uchunguzi zaidi…’akasema.
‘Ok, sawa, endeleeni tu, na dhuluma zenu, tuone mtafikia wapi…’nikasema
‘Sikiliza mpenzi, haya tulishayaongea na hadi hapo natumai
utaelewa ukweli halisi kuwa hata mimi nayafanya haya kwa vile sina jinsi, hapa
ilipofikia sina jinsi ya kuzuia, ngoja yafanyike ya kufanyika na muda ukifika
utasema…’akasema
‘Tatizo lako ni tamaa, wewe na Makabrasha, na hao wanasiasa,
mnafikiri mtaweza kufanikisha mambo yenu kirahisi hivyo, wakikutumia wewe kama
chambo, haya yatafika kwa mkeo, na itakuwa mwisho wa ndoa yako na mwisho wa
ndoto yako ya utajiri wa haraka haraka..’nikasema;
‘Chunga ulimi wako, sikiliza hivi sasa wewefanya wtakavyo, kwa
masilahi ya mtoto wako, vinginevyo utanifanya mimi nichanganyikiwa, hivi yule
mtoto akipata madhara, unafikiri mimi nitaweza kuvumilia, usifikiri ni wewe tu
utaumia..’akasema
Aliposema hivyo, mimi sikutaka kuongea naye, nikageuka kutaka
kuondoka.
‘Sikiliza jitahidi ,...usiondoke bila kuniaga...’akasema na mimi
sikugeuka kumwangalia nikatoka nje.
Nilipofika nje, akaja huyo muongozaji wangu, akaangalia sasa na
kusema;
‘Mbona haraka mumemaliza kuongea..?’ akauliza
‘Kuongea kuhusu nini, sina cha kuongea na huyo mtu, …’nikasema kwa
hasira na huyo jamaa akanitupia macho ya mashaka, akashika simu yake akaongea na
wenzake, na mara gari likaja.
‘Sasa inabidi turudi mjengoni…’akasema
‘Sawa narudi huko, lakini nimuone mtoto wangu, kwani mtoto wangu
yupo wapi..?’ nikamuuliza
‘Wewe ulipoteremka pale uwanja wa ndege mtoto wako ulimuachia
nani, ..hukujali hilo, kwanini kama ulitaka mtoto wako muwe naye mbona ulimpa
mtu mwingine, huyo mtu unamuamini vipi…?’ akaniuliza
‘Ina maana huyo mtu ni mtu wenu pia..?’ nikamuuliza
‘Sijasema hivyo, …nazungumzi hiyo hali yako ya kutaka kuwa na
mtoto wako karibu, kuwa kama ungelikuwa na tabia hiyo tungelijua hutakiwi kuwa
mbali na mtoto wako, je nikuulize huko ambapo ulitaka akakae, eeh, ulitaka akae
muda gani, si mpaka ukiondoka, au sio..?’ akaniuliza
‘Hayo hayakuhusu, nilijua mwenyewe ni muda gani wa kumchukua..’akasema
‘Usijali kuhusu mtoto wako, yupo salama na ataendelea kuwa salama,
ushukuru kuwa kwa hivi sasa yupo sehemu analindwa hakuna kitu kitamgusa, kitu
kitamgusa kama wewe hutafuata masharti..’akasema
Basi mimi nikaendelea
kufanya wanayoyataka wao, ilimradi mtoto wangu awe salama, kwahiyo nilifuata
kila wanachokitaka, bila kupinga, hadi siku ya pili yake ndio nikaambiwa nitatoka
mle mjengoni muda ambao ndege yangu ya kutoka huko masomoni itakapotua hapa
Dar.
‘Una maana gani kusema hivyo..?’ nikamuuliza
‘Unasikia kwa kumbukumbu zako, siku gani ulitakwia ufike hapa Dar,
eeh, si umekata tiketi kwa haraka ukarudisha siku nyuma, basi siku ambayo
uliweka taarifa kuwa ndio utafika dar, ndio itatambulikana hivyo, leo ndio undio
unafika hapa Dar…umenielewa…?’ akaniuliza
‘Ujinga mtu huo..’nikasema
‘Kila kitu kimeshawekwa hivyo, leo ndio unafika Dar, muda ndege
ikitua na wewe utafikishwa pale uwanjani, na hapo ndio, utachukua usafiri
kuelekewa huko nyumbani kwako, ulipopanga kufikia haya yote ni kwa usalama wa
mtoto wenu, uhakikishe kila mtu unamuambia hivyo,..tunakufuatilia kwa hilo,
kosa dogo, mtoto hutamuona tena..’nikaambiwa
‘Ina maana mtoto wangu siwezi kumuona, nakumchukua..?’ nikauliza
‘Kwa usalama wa mtoto hutaweza kumuona, maana sio sisi pekee wenye
haja na huyo mtoto, unielewe hapo…mtoto wako utamuona siku ya kuondoka, wewe si
ulipanga iwe hivyo, una wasiwasi gani, kila kitu mtoto wako atakipata, hata
hivyo, ni muhimu mtoto aonane na baba yake, hilo tutaangalia jinsi
itakavyowezekana…’akasema
‘Yule mtoto hana baba, mnawazimu nyie watu,s itaki mtoto wangu aje
kuonana na huyo mpuuzi, mnasikia, mkitaka tuelewane mtoto wangu asionane na
huyo mtu mnasikia..’nikasema
‘Usijali kwa vile umeshaweka sahihi mkataba kuwa baba yake ana
mamlaka na mtoto,..na huo mkataba umeshapelekwa kwenye ngazi za sheria, utahifadhiwa
huko kama makubaliano halali ya kisheria, huna jinsi madam, kama ningelikuwa
mimi ni wewe nisingelisumbuka zaidi kwa hilo..kwani unakosa nini hapo, hayo
yote nikwa masilahi yako na mtoto au sio…’akasema huyo mzungumzaji.
‘Huyo bosi wenu yupo wapi…nataka kuonana na yeye..?’ nikauliza
‘Huwezi kuonana na yeye, yeye anatimiza wajibu wake kwa ajili ya
kusimamia familia zenu, kama unahitajia hilo, ni baada ya kila kitu kukamilika,
mengine yote utakuwa ukiongea na mzazi mwenzako..’akasema
‘Hili jengo analimiliki nani..?’ nikamuuliza
‘Hata mimi sijui madam, mimi natimiza wajibu wangu tu, maswala ya
jengo na utawala sio kazi yangu…’akasema.
Unajua walikuwa wakinitesa kiakili, maana sina tofauti na mfungwa,
..kwa hasira, nikachukua bakuli iliyokuwa na mboga, ile mboga nikaimimina
sehemu nyingine, niliona uzito wake, unaweza kufanya hicho ninachotaka
kukifanya, nikageuka kwa kwa haraka sana nikairusha ile bakuli hadi kwenye kile
kitufe nilichojua ni cha kuangalia matukio, kwa shabaha ile kikavunjia ...na
taa.
Nilitarajia mlio wa tahadhari, lakini sikuusikia, nikaona
nimefanikiwa jambo muhimu, kwa haraka nikasogeza meza nikapanda juu, na kuvuta
nyanya zake, kuhakikisha hakuna mawasiliiano kwenye hicho chumba, nikatoka nje,
na kuanza kutembea bila kujua nielekee wapi, nikaiachia hisia yangu iniongoze,
nilipanda hadi juu, nikaanza msako, wa kumtafuta mtoto wangu.
NB: Mdogo mdogo, ni hatua
ya ushahidi na ukweli
WAZO LA LEO: Ni
muhimu wakati mwingine tuwe na subira na mambo, tukiwa katika halali na
taratibu zilizokubalika. Tusikimbilie pupa pale tunapoona kuna hatari, au kuna
sintofahamu. Pupa ya mambo, uharaka wa kutaka kupata, hasira na tamaa ndizo
hufanya watu wakafanya mambo yasiyo sahihi. Kwanini tusifuate utaratibu,
kwanini tusitimize wajibu wetu kwa mujibu wa sheria, kwanini tusichume chumo
halali, kihalali, …tukumbuke subira huvuta heri.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment