Sasa
nikiwa nyumbani,… akili ikiwa haikubali kupokea hayo niliyoyaona , na
kusikia,…bado nahisi sio ushahidi wa kutosha, bado...maana nimeshawahi kusimama mahamani nafahamu ...jinsi gani ya kumshawishi hakimu...
'Hata hivyo, ..hii ni hatua kubwa sana...'nikajipongeza, na hapo ndio nikaamua nijitulize kidogo kitandani ili kupumzisha akili yangu,
lakini hata kabla sijafumba macho, mara nikasikia nina ugeni.
‘Nimekuambia napumzika, sitaki
usumbufu, mbona hunielewi mdogo wangu....’nikamwambia msaidizi wangu wa nyumbani kwa hasira.
‘Lakini huyo aliyefika ni baba yako dada…’akasema
‘Oh, baba yangu!!.., kuna nini tena jamani…' nilijikuta nasema hivyo, maana bba sio mtu wa kufika kwangu mara kwa mara na akitaka kuja ataniarifu, ili sipoteze muda wake akute sipo...
'Samahani kwa kauli yangu, haya ..mkaribishe
ndani, keshaingia ndani, ok, ok…haya nakuja…’hapo uchomvu ukaniishia, baba
akifika kwangu ni kama bosi wa kampuni yako uneyemuogopa, na kumuheshimu sana
kafika nyumbani kwako.
Kwa haraka nikajiweka vizuri na kuelekea chumba
cha maongezi, nikamkuta baba akipata kinywaji, huku kasimama, kuonyesha kuwa hana hata muda wa kukaa, ...yeye nyumbani kwangu ni kama
nyumbani kwake, akifika hasubiri kuhudumiwa, anakwenda kwenye jokofu anajisaidia mwenyewe… japokuwa anapaheshimu kama sehemu
ya mkwe wake.
Alikuwa kasimama akingalia nje kwa kupitia dirishani na aliposikia nyayo za mtu akageuka na kunikagua kwa macho hata sijamsalimia akasema;
'Bint yangu upo sawa kweli…?’ akaniuliza
aliponitupia jicho, unajua tena huyo ni mzazi wangu akikuangalia tu anafahamu
kuwa upo sawa au una matatizo.
‘Nipo sawa baba, ni majukumu tu ya kila siku…
na kuchoka choka kidogo..hamjambo wewe na mama, kupo salama huko..?' nikamuuliza hivyo
‘Upo sawa wakati upo nyumbani, unajua nilipitia
kazini kwako nikaambiwa hujafika leo, unaumwa…?’ akaniuliza
‘Hapana baba mimi siumwi, zaidi ni mume wangu, nilikuwa
na kazi, nikapanga kuwa nizifanyie huku nyumbani, lakini kila ukimaliza moja
inakuja nyingine,, mpaka nikaona leo sitaweza kufika kazini kabisa,..kiukweli
kazi nilizozifanya hapa nyumbani leo,
hata ningekuwa ofisini nisingezifanya hivyo..’nikajitetea
‘Lakini nyingi ni za kifamilia au sio..?’
akaniuliza kwa sauti ya kawaida tu
‘Ndio baba..’nikasema
‘Na hizo kazi za kifamilia , ndizo zinakufanya
hata ushindwe kutuliza kichwa chako kwa ajili ya kazi za ofisini ambazo pia ni muhimu
kwako, au sio..?’ akaniuliza nikajua baba ananitega kuna kitu kaja nacho
anatafuta njia ya kuniingia.
‘Baba lakini mimi ni mzazi, ni mwanamke wa
nyumbani pia, na zaidi unafahamu kuwa mume wangu ni mgonjwa, kwahiyo inanibidi
niwajibike kote kote…’nikasema
‘Sawa sijalipinga hilo, ..nafahamu sana, lakini
ukweli ni ukweli tu, kuwa majukumu ya nyumbani yamekuwa makubwa zaidi ya uwezo
wako, …au sio, au niseme mitihani ya nyumbani umakuzidi, na bado hutaki kusaidiwa, sio mbaya..lakini nina uhakika hayo unaykabiliana nayo kwa sasa yanakuchanganya kichwa, kweli si kweli…’akasema
‘Ni kawaida tu baba…’nikasema
‘Ni kawaida tu eeh, hahaha…niambie ukweli ni nini kinachoendelea
kwa hivi sasa ndani ya nyumba yenu..?’ kwanza alicheka lakini alipoongea hiyo 'niambie' akapandisha sauti.
‘Baba nimekuambia ya kawaida tu, ni yale yale...'nikasema
'Akatikisa kichwa kama kukubali, halafu akaniangalia kwa makini akasema
'Haya niambie, huo ukawaida wake...'akasema
'Baba kwani kuna nini, mambo ni yale yale bado napambana nayo hatua
kwa hatua naanza kuyakabili, najua mwanzo ni mgumu,…lakini hadi sasa nimeanza kuthibitishia baadhi ya mambo, ambayo yalikuwa yakiniumiza kichwa, na leo tu,
nilikuwa nahitimisha baadhi ya hayo mambo, …’nikasema,
‘Binti unanifahamu sana, nikija hapa kwako ujue ni jambo nzito,
..najua kuna wagonjwa, lakini mgonjwa huyo, yupo huko hospitalini na huko anafanya mambo
yake..ofisi kaihamishia huko..au sio.. hata hivyo, ni wajibu wangu kukutembea,
lakini siwezi nikaja kwa kukushtukizia kama hivi, bila sababu maalumu, naheshimu mila na desturi zetu kuwa hapa ni
nyumbani kwa mkwe wangu hata kama hayupo…’akasema
‘Baba lakini hapa ni nyumbani kwa watoto wako unaweza kufika
muda wowote utakavyo…’nikasema
'Binti…huyo jamaa anayetaka pesa kwa ajili ya
kuuza ushahidi dhidi ya mume wako ni nani…?’ akaniuliza na moyo ukalipuka paaah,
nikajua rungu jingine linaniangukia kichwani, kama baba kalifahamu hilo, je polisi..na je kuna nini kwenye huo ushahidi, na kwanini baba akalifahamu hilo…nikakaa kimia kwanza kutafakari
huo mtego wa baba.
‘Ina maana gani, yaani kila mara ninapofanya
jitahada ya kulisafisha jina langu, kwa sababu ya madhambi yenu, mnanipachika
mzigo mwingine… ni kwanini mnafanya hivyo, mnataka wazazi wenu tufe kwa shinikizo la damu...au, halafu mje kulia..wakati chanzo ni nyie…’akawa kama anauliza
'Baba kwani...'nikataka kusema lakini yeye akaendelea kuongea,....
‘Ilikuwa ni wewe, kwa kashfa ya mauaji,..unajua
jitihada gani nilizozifanya kuisafisha hiyo kashfa,…unakumbuka ilibidi hadi
nikutane na waandishi wa habari kuliweka hilo bayana kuwa hauhisiki na hayo
mauaji, baada ya ushahidi… haya, hayo
yakaisha, …sasa hili tena, kuna nini hapa kwenye nyumba yenu..’akasema kwa
ukali
‘Baba, hata mimi ndio…nimesikia na…bado..hakuna
uhakika kuwa ni kweli…ushahidi hakuna..’nikajitetea hivyo.
'Sikilizeni, hili naliongea mbele yako, hata
kama utanielewa vibaya, sitojali, maana kila
dalili zipo....mume wako huko kuumwa kwake kwasasa kuna walakini, yaonekana
kama anaiigiza tu...alishapona, ila anafanya hivyo kwasababu maalumu, hilo
nakuambia wewe ulisikie hivyo…' hapo nikabaki kimia.
‘Na hata kama
angelikuwepo yeye hapa ningelimwambia hivyo hivyo, …’akasema akinikodolea macho ya
kutisha, baba hana mchezo akikuangalia unatamani ujifiche.
'Baba..." nikata kuongea akainiashiria kwa
mkono kuwa hajamaliza kuongea.
'Najua utamtetea mume wako, najua kutokana na kauli
za madocta utasema ni kweli anaumwa,..sawa anaumwa,..nisije nikakufuru, lakini
hayo matendo anayoyafanya mbona yanapingana na ugonjwa wake…usifikiri mimi
sijui matatizo kama hayo yapoje,….mimi sijazaliwa kesho, watu kama hao
nimeshakutana nao sana..lakini hilo la kwake limezidi kipimo…’akatulia
'Baba lakini huyo aliyesema hivyo ni docta bingwa wa hayo matatizo...'nikasema
'Ni kweli, ..ni nani huyo docta bingwa
'Ni yule yule wa awali, nakumbuka uliwahi hata kuongea naye..'nikasema
'Ok...siku kadhaa alikuwa karibu sana na huyo mpinzani wangu wa kisiasa...unajua kwenye haya mambo kila kitu kimachunguzwa...kuonekana na huyo mpinzani wangu sio tija, maana yeye ni dakitari wa wote..lakini kwangu mimi inanipa maulizo mengi...lakini..'hapo akatulia
'Ina maana baba humuamini huyo docta...?' nikauliza
'Sio kwamba simuamini..lakini yeye kama docta anafuata vielelezo vyake, na huo ugonjwa, pamoja na mengine kinachoangalia zaidi nai matendo ya mtu, je mtu ukiijua huo ugonjwa ulivyo, ukaigiza sawa na hayo matendo, docta atagundua ...?' akasema
'Baba haiwezekani sio kwa madocta bingwa...'nikasema
'Mimi nikiwa shuleni, niliteguka nyonga, nikaenda kwa docta..na nikatibiwa, wakati natoka kwa huyo docta, nikajikakamua tu, ili kutokujilegeza, wakati kweli hapo naumia, huyo docta bingwa, akanijia na kusema siumwi...akachanga karatasi ya mapumziko,..lakini kweli naumwa...'akasema, na mimi nika kaa kimia
'Ninachotaka kukuambia ni hivyo, kuna magonjwa, docta anakuamini wewe, ukiigiza, hewala yeye atafanya nini, atahitimisha jinsi anavyoona kwa macho yake, hana makosa, ..unielewe hapo, mwenye makosa ni wewe unayeigiza, ..na hatari ya ugonjwa ulivyo ukiigiza ipo siku utakupata kiukweli...'akasema
'Baba mimi nawaamini sana madocta..'nikasema
'Hata mimi..sijasema siwaamini, ila kwenye tatizo, walakini hauchezi mbali hasa ukiwa unagusa kinyume na matarajio yako...tuombe mungu kuwa ni kweli, kuwa anaumwa kihivyo, lakini kama anaigiza, ...nakuambia hili, mume wako ataumbuka sana...'akasema
'Baba huyo mtu anaumwa, sema yeye anaweza akautumia huo ugonjwa...lakini mimi sina mawazo hayo mabaya, ninaamini kuwa anaumwa, mengine ..ni juu yake...'nikasema
‘Sasa sikiliza najua
utarejea kauli yako kuwa labda nayasema haya kwa kutokuwajali watu wengine, au
kwa vile sikupenda wewe uolewe na mtu kama huyo, au kama wengine wanavyosema kuwa labda nabagua,...lakini eeh, mimi kama mzazi sina makosa,
kwa hilo, yoyote atafanya jitihada kuhakikisha bint yake anaolewa sehemu salama,
na kwa hili wewe mwenyewe umeshajionea…na sitakosea nikisema bado…bado binti yangu upo kwenye mtihani mkubwa... ‘akahema
na kuangalia pembeni.
‘Baba lakini kwani kuna
nini…?’ nikamuuliza
"Kuna nini!!, mhhh....wajifanya hujui sio, …eti kuna
nini,...'akatikisa kichwa halafu akaendelea kuongea
'Binti...umejifanya kunificha mengi lakini
mengine hayafichiki,..je wewe husomi magazeti, hata kama ni ya udaku, lakini
ndiyo watu wengi wanayasoma, na hao watu wengi eeh, ndio hao wapiga kura wangu…unafikiriaje…wakisoma
kashfa kama hizo, unafikiri kwa mtizamo wako wao watasemaje, sio kwamba nawadharau, lakini akili zao zitawatuma hivyo, kuwa ni kweli,...upeo wa kufikiria kwa kila mtu unatofautiana, au sio…’akasema
‘Sisomagi hayo magazeti
baba…’nikasema
‘Ndio najua...mkurugenzi mkuu usome magazeti kama hayo,...hahaha, ni sawa wewe..huwezi kuyasoma
hayo maana hayagusi masilahi yako,..lakini kwangu mimi ni muhimu sana
kuyasoma, kila gazeti mimi nasoma hata yale yanayoandika uchafu....ili kujua kila kitu kwa watu wangu..., kila kitu kinachohusu wapiga kura wangu, ni muhimu kwangu,....na
wengi wa hao ndio hao, wanaoyaamini hayo magazeti, na mpinzani wangu ndiye
anayatuumia sana hayo magazeti unajua ni kwanini…’akasema
‘Kwani, wamesema nini baba…?’ ikabidi nimuulize
‘MKWE WA MWANASIASA MKONGWE ANASHUKIWA KWA KUMUUA WAKILI WAKE, kichwa cha habari kikubwa, na kidogo....'WAKILI MTETEZI WA WANYONGE…’ hicho kichwa cha habari hapo, …unafahamu
athari za maelezo hayo tu,..kwenye uwanja wangu wa kisiasa…na hapo hujasoma
huko ndani…huko, nasikia, nasikia zipo nyingi tu, zikianisha kashfa na uchafu dhidi ya mumeo…’akasema
‘Mauchafu gani…?’
nikauliza nikijifanya sijui lolote
‘Mumeo kamwe hawamtaji
kwa jina lake…kwangu mimi wananitaja kwa jina alngu mkongwe wa siasa so and so…,
ni kwanini…na ni kwanini yeye wanamtaja kama mkwe wangu...kwanini…uone kwanini
nawaonya sana kuhusu kashfa..’akasimama
'Baba mimi sijui maana sijalisoma hilo gazeti...'nikasema
‘Ukiangalia hata maoni
ya watu kunihusu mimi, kiwango cha uaminifu kwangu kinashuka na wambeya
wameshapata la kuongea, na ikitoka hapo, nisipofanya jambo hata magezeti haya ya
kawaida wataanza kundika…unataka mimi nifanye nini hapo, niendelee kukaa kimia au sio..., nikae kimia tu kwa vile wewe binti yangu kipenzi,...hutaki mimi niingilie
mambo yenu au sio, ..eeh, hebu hapo niashauri mimi…’akasema
'Lakini baba…’nikataka kujitetea, na yeye
akanikatisha kwa kusema;
'Lakini baba..lakini baba…najua unataka kusema
nini, kuwa familia yako haihusiani na
maisha yangu ya kisiasa, kuwa hizi ni familia mbili tofauti , kila mtu na
maisha yake,..au sio...hilo wewe wasema, lakini sio wapinzani wangu....'akasema
'Mhh...'nikaguna hivyo.
‘Umenielewa hapo, kama
ingelikuwa ni hivyo, utakavyo wewe, ni kwanini hao waandishi hawaandiki
wakirejea familia yako tu , wewe na mume wako, wanaandika kwa majina makubwa, ‘mkwe
wa…’ …kwanini, kwanini..…ndio maana ni lazima niwajibike…’akasema
‘Baba, niachie hiyo
kazi, naomba nilifahamu hilo gazeti , mimi nitakwenda ofisini kwao, ikibidi
tuwafungulia mashitaka..’nikasema
‘Utakwenda kufanya nini
wakati jeraha limeshavuja damu..unajifanya wewe unafahamu kuliko mimi,
eeh..haya nenda kaonane nao, ...utawaambia wasiandike kuhusu mimi,…unajua ni nini
wataandika kesho yake…unalifahamu hilo…BINTI WA KIGOGO WA SIASA KAVAMIA OFISI YA MAGAZETI, kitakachofuata ni nini, waandishi watafika nyumbani kwangu, hata wale waliokuwa wamekaa kimia, …’ akatulia akiangalia saa yake.
‘Kwahiyo baba wataka
mimi nifanye nini…?’ niamuuliza
‘Wapinzani wangu wa kisiasa
wameshaona uchochoro wakuniharibia mimi ni kupitia nyie wawili..hawachezi mbali
na nyie sasa mumekuwa 'super stars,..' lakini wa nini basi,...…wameshawasoma na kufahamu madhaifu yenu, na mume wako kafanywa
ndondocha, na sio ndondocha wa ucahwi,...ila wanamtumia,...bila hata ya yeye kufahamu,..sasa hivi wanatafuta kila mbinu za kuhakikisha mgogoro wenu hauishi, bali
unafichua kashfa zaidi na zaidi....’akatikisa kichwa kama anasikitika.
'Sasa baba....'nikataka kusema wazo langu lakin hakutaka kunipa muda.
‘Mimi siogopi kupambana
na hao watu…lakini nawahofia nyie…mtaumia,..na kwenye vita macho
hayaoni,..aliyepo mbele yako ni adui yako, sasa kama nyie mumewekwa kama kinga
yao, nitafanya nini…mwishowe nitaishia kusema bahati mbaya, na nani ataumia kama sio mama yako....’akasema
‘Kwahiyo baba unataka
kusema nini hapo..?’ nikauliza
‘Nitasema nini ..eeh,
niambie nitasema nini, wakati binti yangu, mkurugenzi mkuu wa kampuni A nd Z,
yupo, eeh,..mke jasiri, eeh…hata siku moja hawakutaji kwa MRS mumeo,wanataja
binti ya, na kwa mumeo, 'mkwe wa…' sijui unanielewa lakini…hata siku moja
hawawezei kutaja mazuri yako kwa kurejea jina langu, ila mabaya wanafanya hivyo,….ujue
ni kwanini nawaandama …mimi sitaki kupoteza muda wangu kwa maisha yenu..maana nyie sasa ni familia tegemezi, lakini kwa haya mimi nitafana nini...’
akatulia.
Hapo nikaanza kuvutia hisia kujua ni kwanini baba kafika
kwangu kwa hasira
*************
'Huyo mtu anayenitishia mimi, kuwa nisipojitoa
kwenye uchaguzi ujao, atauweka uchafu wa familia yangu ni nani..najua
keshawasiliana na wewe…sasa sikiliza , sitaki ufanye anavyotaka yeye, kufanya hivyo ni udhaifu..unasikia hata kama mume wako atakwenda jela…pambana kwenye haki na ukweli, unasikia...’akasema
‘Lakini hakuna ukweli
wa hilo au sio baba…?’ nikasema
‘Ninachotaka ni wewe
kutokukubaliana na yeye, kwa hivi sasa hawezi kukutana na wewe uso kwa uso,... anatumia mbinu
za simu tu, kukusumbua...anafahamu mkikutana na yeye atakamatwa, na sio kwamba polisi
wameshindwa kumkamata, lakini kuna kitu kinaendelea hapo, wewe huwezi kukufahamu, ila sisi tuliopo kwenye huo ulingi wa siasa tunakifahamu ni nini...unasikia bila kukuficha kinachoendelea kwa sasa ni
mambo yetu ya kisiasa…’akasema
'Kwahiyo baba, mimi nifanye nini..ndio swali la msingi hapo....?' nikauliza
'Kwanza jichungeni..niliwaambia jamani, kuweni mbali na kashfa, ukasema nini...hilo nikuachie kwa vile ni familia yako..haya nimewaacha matokea yake ndio haya...nilijua tu haya yatakuja kutokea, lakin nitafanya nini, na wewe ushapenda, haya kupenda sio kubaya, lakini mtu uliyempenda, habebeki...utaumia binti yangu...'akasema
'Baba mimi nalifanyia kazi, wewe mwenyewe utaona,...kama ni kweli, baba, niamini ...ila sitaki kufanya jambo bila kuwa na uhakika,...na uhakika huo, wataubainisha wao wenyewe, baba, niamini mimi...'nikasema
'Hahaha, siwezi kumuamini mtoto wangu, mtoto ni mtoto tu..kwa hivi sasa huwez kunidanganya,...'akasema
'Haya baba...'nikasema
‘Sasa narudia tena,…sitaki..umsikilize huyo tapeli, kama atawasiliana na wewe..nijulishe haraka…na kuanzia sasa nitaanza kuingilia
mambo yenu yote, kuanzia kazini, hata ya nyumbani…siwezi kuvumilia tena…na hii sasa ni vita ya kisiasa, najua yenu ni ya kifamilia, lakini wameivumisha iwe hivyo, sasa kazi ni kwako, uwe na baba yako au uwe na maadui wa baba yako...’akasema
'Unasema nini baba…! Huoni ndio utajiharibia kabisa, haya yangu usijiingize baba, nakuomba tafadhali, huyo mume wangu ninajua jinsi gani ya kumweka sawa, mpaka hatima yake, siwezi kumuacha, hilo baba nilishakuambia…’nikasema
'Najua...nafahamu sana,..ila nakuambia hivi, kama ni mume wako, kama ni familia tegemezi, kwanini sasa nipo mbali na nyie, madongo yakirushwa
kwenu yanailenga na mimi, je nitaweza
kuvumilia hayo, nikae kimia tu…, au nifanye kama mnavyotaka wewe na mama yako, kuwa niachane na
mambo ya kisiasa, hicho ni kifo cha kondoo,. mimi sikulelewa hivyo, nitapambana, unasikia, huyo ndiye baba yako…’akasema
‘Baba hapana, mimi
sijasema hilo, ila mimi sikupenda mambo yangu yahusishwe na nyie..mimi nina
familia yangu, na nyie ni familia tegemezi..japokuwa kwa namna fulanii tunategemeana, …ndio
maana nilitaka niende nikaongee na hao watu.., waandishi wa hilo gazeti….’nikasema
‘Usije kufanya kosa
hilo…’akasema sasa akitaka kuondoka, lakini hakuondoka, akanigeukia tena na
kuuliza swali hili….
‘Je ni kweli mume wako
ndiye aliyemuua Makabrasha…’baba akaniuliza
‘Hapana baba sio yeye…’nikasema
‘Silaha iliyotumika si
yako, na uliweka kwenye kabati maalumu, ni nani aliyefungua kabati lako na
kuitoa hiyo silaha..?’ akaniuliza
‘Baba kuna tetesi tu
bado nazifanyia kazi, ila nimeshamfahamu , nitakuja kukuambia kwa wakati muafaka ..’nikasema
‘Ni kweli kuwa mume
wako alifika huko kwa Makabrasha siku ya tukio, ..alikwenda kufanya nini..?’
akaniuliza
‘Nahisi ni kwa vile
huyo marehemu alishakuwa ni wakili wake, kwahiyo alikwenda kuongea naye maswala
yao..na ndio nimeanza kuupata ukweli huo leo, lakini bado naufanyia kazi,
haujawa na uhakika wa kiushahidi…’nikasema
‘Mume wako si alikuwa
mgonjwa..aliwezaje kufika huko..?’ akaniuliza
‘Kuna dalili, kuwa
akiingiwa na hisia fulani anakuwa na nguvu za ajabu ugonjwa hutoweka, akafanya
mambo, kihisia,..kwa vitendo..ni aina ya ugonjwa wa ajabu tu..’nikasema hapo
atabasamu na kusema.
'Ugonjwa huo unawezesha yeye kuongea, kufanya ya ukweli, hata marehemu aweze kuelewana naye,..marehemu hakuwa magonjwa, ..ya kuwa walikutana kwenye njozi, au...usinifanye mimi mjinga eeh, hivi..inakuja akilini hiyo,..ok, sawa, tuliacha hilo kama lilivyo...lakini mimi simini...'akasema
'Kufanya hivyo alivyofanya si ile ya kindoto za usiku, ila hilo la mchana akauwa na hisia za kawaida, akili za kawaida, ila anapata nguvu ya ajabu, ni kama mashetani hivi, yanamuongoza, kama nilivyoelezwa hivyo, ila ni katika aina hiyo y akuchanganyikiwa,..ipo hivyo baba...'nikasema
‘Ok..ok...'hapo akacheka, halafu akaendelea kuuliza,...'Pale kwenye jengo,
kuna vyombo vya kuashiria hatari, pindi mtu akiingia na silaha, pia yupo askari mkaguzi, ana ujuzi wa hali ya juu,...silaha ilipitishwaje, ujue huyo muuaji alikuwa nje..si ndio..na huko kote kuna hiyo mitambo ya ishara ya hatari, akasogea hadi chumba alichokuwa marehemu, na humo kwenye chumba kuna mitambo yake ya ziada, haikupiga kelele...umegundua nini hapo..?’ akaniuliza
‘Bado nalifanyia kazi…’nikasema
‘Pale kwenye jengo kuna
mitambo ya kurekodi matukio, je ni kwanini siku hiyo haikuweza kufanya kazi, au
je kuna mtu aliifuta…unamuelewa huyo mtu…?’ akaniuliza
‘Baba bado sijampata baba, mitambo ya kurekodi matukio, kama ilivyokuwa mitambo ya kutoa ishara ya hatari, imekuwa ni kitendawili baba, nahisi kuna jambo hapo…’nikasema
‘Uliweza kuongea na
mtoto wa marehemu mkubwa,..kuna lolote kakuambia kuhusu ni nani aliyehusika na
mauaji ya baba yake..?’ akaniuliza
‘Niliongea naye, lakini
hajasema kuwa ni nani, wanadai kuwa ni maadui zake tu…’nikasema
‘Unahisi ni kwanini
wanataka kuficha ukweli wa hayo mauaji ya baba yao, wakati ni watoto wake..?’ akaniuliza
‘Sijajua bado, bado nalifanyia kazi…’nikasema
‘Ni nani aliweza kuiba
mkataba wako ule wa ofisini, huo wa nyumbani,..sawa labda ni mume wako,ndiye
aliweza kuuchukua, kabla, je wa huko ofisini ni nani alifanya hivyo…?’
akaniuliza
‘Baba nitakuamba yote
hayo bado nakusanya ushahidi..’nikasema
‘Je ukiupata huo
mkataba utafanya kama mlivyokubaliana, jinsi mkataba unavyosema au utamsamehe mumeo wako..?’ akaniuliza
‘Baba kila kitu
kitajieleza kwa wakati muafaka,…kwa hivi sasa siwezi kusema neno…’nikasema
‘Huyo ni mume wa watoto
wako au sio…utasema nini kwa watoto wako iwapo utaamua kuachana na mume
wako..kama mkataba unavyosema, au si ndio hivyo....nasema kama, sio kwamba nataka iwe hivyo…?’ akaniuliza
‘Baba siwezi kukujibu
hilo swali lako kwa hivi sasa, muda ndio utasema….’nikasema
'Sasa ni muda, sio mkataba tena,..kwa vile unao, au sio...'akasema
'Sio hivyo baba...'nikasema
‘Na leo hii ulikutana na watu gani, ..?’ akaniuliza na hapo
nikashtuka..
‘Ni watu wa usalama..’nikasema
‘Je wameweza
kufanikisha lengo lako..?’ akaniuliza
‘Kwa kiasi fulani ndio…’nikasema
‘Kwahiyo huyo shemeji yako
kasema ukweli wote,..je kakubali kuwa kayafanya hayo, na je ni kweli mtoto wa rafiki yako, yawezekana kuwa yeye ndiye baba yake..?’ akaniuliza hapo maswali mengi kwa wakati mmoja, ni
kama vile hataji nijibu ila kuna kitu anataka nikielewe,..na hapo nikajua kuwa
baba anafahamu zaidi na y a ninavyofikiria mimi…
‘Baba naomba unipe muda,
nitakujulisha yote hayo ikibidi…kwani,eeh, nahisi kuna kitu umekigundua zaidi ya ninavyojua mimi,
unaweza kunieleza, maana bado nipo kwenye michakato ya kukusanya ushahidi..?’
nikamuuliza
‘Ushahidi!! Ushahid wa
nini, wakati una meno, hutaki kuyatumia, wakati…una kila kitu lakini bado
unakumbatia uchafu…mwanangu hii ni dunia, sio wote wanaokuchekea wakakuonyesha
meno, ni wazuri kwako, sio wote wanaosema 'i love you' wanamaanisha hivyo, wengine wanamaanisha kile ulicho nacho ambacho sio wewe…’akasema
‘Naelewa hilo baba..’nikasema
‘Nikuambie kitu, unaishi
na nyoka, tena mwenye sumu, lakini wewe hujui, ukiwa umelala wenzako
wanakuwangia…na sia maana ya uchawi, mimi siamini uchawi, ila nakuambia hivi,..tumia akili yako vyema..'akasema
'Baba usiwe na shaka na mimi...'nikasema
'Ni lazima niwe na shaka na nyie....kwa hayo yanayotokea, unasikia,,..ninachokushauri kwa
sasa, uwe makini na hilo..sitaki kukushauri jambo baya, kama nina uhakika kuwa ni baya, na siwezi kukaa kimia, nikijua unakwenda kuteketea, ina maana gani kuwa mimi ni mzazi wako,...ila ..vyovyote iwavyo,…usiwaamini
watu wote tena…na usikubali kila jambo bila kushauriana na wakili wako, na wakili wako ni mtu, unielewe hapo,ila muhimu…taarifa
yoyote itakayokuja kwako uwe makini nayo, unanisikia..’akasema
‘Sawa baba nimekuelewa
baba…’nikasema
‘Na rafiki yako anarudi
lini…?’ akaniuliza
‘Hajaniambia bado..’nikasema
hapo akashika kichwa kama kuna kitu kinamkera, halafu akaanza kutembea
kuondoka, lakini kabla hajatoka mlango akawa anaongea huku anatembea kuondoka.
‘Nilikuambia siku ile..mume wako anahusika na
kifo cha Makabrasha ukanibishia, sawa…sio mbaya,…nilikuambia mume wako
anatumika na wanasiasa ukaniona naleta
mambo ya kisiasa nyumbani kwako, nalo hilo sio baya...’ akatulia kama anawaza jambo lakini kila nikitaka kuongea ananikatiz kwa kuongea
‘Na...nilikuamba, marafiki zako ndio maadui
zako, wachuje ili ujue ni nani rafiki wa kweli,.. ukasema nini …nakufitinisha wewe
na marafiki zako…sasa nakuambia hivi…wanaokuja kwako kwa lugha za wema, hao hao
ndio chambo cha kupooza jitahada zako, usiwaamini, unasikia, sasa na hilo
puuza, na endelea kulala uone itakavyokuwa, mimi sijamlea binti yangu alale
kipindi cha vita… kwaheri..…’huyo akandoka zake.
Kiukweli baba alipoondoka sikuweza kulala tena,
akili yangu ilianza kuwaza mengi, nikaona nispoteze muda,..muda ni mali,
..nikavaa nguo zangu maalumu, nikahakikisha kila kitu kipo sawa, na haraka
nikatoka, nje…
‘Vita imeanza…’nilisema hivyo tu, na kwenye simu yangu ukalia mlio wa ujumbe, nikajua ni taarifa kutoka kwa watu wangu sikutaka kuusoma, kwanza ni kufanya nilichotaka kukifanya..kuhakiki ushahidi wa `shemeji..'
WAZO LA
LEO: Dunia
ilivyo sio wote watakaofurahia jitihada na maendeleo yako, wapo watakaokusifia
na wengine watakukatisha tamaa na wengine watakubeza, na hata hao watakaokuja
na kukusifia kwa jitahada zako na maendeleo yako, sio kweli wanamaanisha hilo
wanalolisema, kutoka kwenye nafsi zao. Hiyo ndio kiwalimwengu kilivyo. Muhimu
pambana na jitahada zako, huku ukimtegemea mola wako kwenye kila jambo la heri,
kwani yeye ndiye anayefahamu ya siri na ya dhahiri…muhimi simamia kwenye njia
ya kweli na ya haki..uatafanikiwa tu..japo mwanzo ni mgumu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment