Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, January 20, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-62



 Nilifika chumbani kwangu na kwa haraka nikaingia maktaba nikiwa na shauku ya kuuona huo mkataba, shauku niliyokuwa nayo ilikuwa haimithiliki, utafikiri nilikuwa nakwenda kugundua alimasi iliyofichwa, kwangu mimi huo mkataba ulikuwa na thamani kubwa, sio kwa ajili ya kulinda masilahi yangu tu, lakini pia kulinda utu wangu, kilichokuwemo humo, kilikuwa ni kwa ajli ya utu wangu, na kama utapotea basi mimi nitaonekana sina maana,, nitadhalilika,....

Nikawa natembea kwa haraka haraka,nikijua kuwa sasa ukweli utadhiri, na wale wote waliotaka kunidhulumu, na kuishia maisha ya hadaa nyuma ya mgongo wangu wataumbuka, ...na hilo nilishaliahidi kwa wazazi wangu kuwa nitahakikisha, nalifanyia kazi bila ya msaada wao, na wao waliniona kama mfa maji,....lakini sasa ukweli watauona, na kile nilichokuwa nimekiahidi mbele yao watakiona kwa macho yao. 
Sikutaka kubweteka, sikutaka kudeka,kwao kuwa kwa vile mimi ni mtoto wa kike, sitaweza kuishi bila ya msaada wao.

Nilitaka kuionyesha jamii, kuwa hata sisi wanawake tunaweza, tunaweza kutunza siri, tunaweza kutunaza dhamana, ...kwangu mimi kipao cha ndoa, nilikiona ni muhimu sana, ndio maana sikutaka kughilibiwa, kama nilijitahidi kufanya hivyo, japokuwa kulikuwa na mapungufu, kwanini mwenzangu afikie hatua hiyo kubwa ya kunisaliti, hapana, kama kafanya hivyo, ni lazima sheria ichukue mkondo wake, lakini sheria ipi, maana huo mkataba ndio ulikuwa ni sheria yangu..sasa umepotea

‘Kama nitaupata huo mkataba, nitawaonyesha watu kuwa hili linawezekana, kama kutakuwa na mkataba wa ndoa na mkaufuatilia, mwenye makosa akahukumiwa kutokana na amkubaliano yenu, basi kila mwanandoa ataogopa kufanya maasi, ....’nikasema huku niendelea mbele kuelekea sehemu iliyopo sheria yangu, mkataba wangu, utakaonilinda kwa hilo...

‘Na wale wote walionisaliti, itabidi wawajibike, sitajali kama ni rafiki yangu, au ndugu yangu...’nikasema huku nikifungua mlango wa maktaba, ambao sasa nilikuwa na ufungua mwingine mpya,japokuwa nilipotoka sikuwa nimefunga na ufunguo, ila nikitoka nje , nitakuwa nafunga sehemu zote nyeti...

‘Nikimalizana na huyu shemeji yangu, nitaanza kupambana na rafiki yangu, sitajali urafiki tena, mapaka kieleweke, na mwishi namalizia na mume wangu,...nina uhakika kuwa mume wangu kasaliti ndoa yangu, na ninachotakiwa kupata ni ushahidi, na ....na mkataab wetu utahukumu....’nikasema.

Nikalifungua kabati la mume wangu, kwa ufungua ambao unafungua kwa namba maalumu, ...hata uchonge ufungua, usingeliweza kufungua, nilifanya hivyo, ili kila mmoja awe na namba zake za siri, kwahiyo mume wangu akija nitampa ufunguo wake, na namba zake za siri.

Nikafungia hilo kabati lake, kwa ndani kuna sehemu tatu, nikavuta kidroo cha sehemu ya kwanza, niliona makaratasi ya malipo, stakabadhi za malipo na vyeti vya biashara, hakuna huo mkataba...

Nikafungua sehemu ya pili, hakuna kitu, hapo hasira zikaanza kunipanda ina maana huyu kijana kanidanganya, nikasema na kufungua sehemu ya tatu, hakuna kitu...nguvu zote zikaisha, na sikujau nifanye nini tena, na wakati nimekata tamaa, kwa pembeni nikaona bahasha kubwa,iliwekwa kwa kusimama, isngelikuwa rahisi kuiona, nikaitoa ile bahasha, ilikuwa nzito, nikaitoa, na kuigeza juu chini kukitoa kilichopo, kikatoka kitabu....

Kumbe ilikuwa sio kitabu , ulikuwa mkataba, na mwanzoni nilifikiria ni ule mkataba wa kawaida, lakini pale nilipoona alama yangu nikagundua, ni ule ule mkataba niliokuwa nautafuta, nikauchukua na kuanza kuufungua, kuhakikisha kuwa ndio wenyewe, na nilipojirizisha nikafunga yale makabati na kuanza kutoka.

 Wakati nainua mguu, nikakanyaga kitu, nikainama kukiangalia, kilikuwa kidude kidogo,cha  kuhifadhia kumbukumbu, unaweza kukiweka kwenye simu au kwenye komputa, nikakiokota, nahisi kilidondoka kutoka kwenye hiyo bahasha, waakti nilipoiinamisha juu chini kuutoa huo mkataba,na hapo nikakumbuka kauli ya shemeji yangu;

‘Shemeji kama kuna kitu changu naomba uniletee, ...

`Huenda hiki kitu ndicho anachokitafuta....’nikasema huku nikikiangalia kwa makini, moyoni nikaingiwa na shauku ya kujua kuna nini humo ndani, lakini kwa namna nyingine niliona nafanya makosa, nitakuwa nachunguza vitu vya watu, na mimi sitaki tabia hiyio, hata hivyo kwa hali ilivyo kwasasa hamasa za kufahamu ni kitu gani kimo humo ndani ikanijia, nikatoka hadi chumbani hadi kwenye laptop yangu, nikakichomeka, na maandishi yakatokea;

Diary yangu, kumbukumbu za kila siku.....’

‘Oh, kumbe ni kumbukumbu zake, hakuna shida..na wakati nataak kukichomoa, nikaona maelezo yaliyonivutia, nikayasoma kwa haraka..

‘Kumbe...’nikasema

‘Sasa nimekupata, kama atakuwa anaweka kila kumbukumbu za kila siku, kumbe nitaweza mambo muhimu ninayoyatafuta, amekwisha, hana ujanaj tena, ...’nikasema na kwa haraka nikaweka sehemu ya kunakili hizo kumbukumbu kwenye komputa yangu, ilichukua muda kidogo, na kumbukumbu zote zikanakiliwa kwenye komputa yangu, halafu nikakitoa kile kitufe, na kukiweka kwenye ile bahasha nikatoka nacho hadi kule bustanini.

‘Shemeji kwenye hiyo bahasha uliona kitu changu?’ akaniuliza

‘Kitu gani?’ nikamuuliza kama vile sijui,

‘Naiomba hiyo bahasha, umeshautoa huo mkataba unaoutaka, natumai sasa tumemalizana, uliouona eeh....?’ akauliza huku akichungulia ile bahasha kwa ndani, na mara akakitoa kile kitufe na kwa haraka akakiweka mfukoni

‘Ni kitu gani hicho?’ akaulizwa na wale maofisa wa upelelezi

‘Ni kifaa cha kazi zangu za ofisini, ni muhimu sana, ningelipoteza kazi za watu...’akasema

Mimi nilikaa kimiya sikusema kitu na hapo yule ofisa akaniuliza kama nimeuona huo mkataba na kama ndio wenyewe niliokuwa nautafuta, nikamwambia ndio nimeuona ndio wenyewe.

‘Shemeji kwa hali ilivyo huyu mtu inabidi tuondoke naye...’akasema huyo jamaa wa usalama

‘Hapana, mimi nimewaambia kila kitu, kwanini sasa mnanigeuka, ...tulikubaliana nini?’ akalalamika huyo shemeji yangu na mimi hapo nikamuonea huruma na kusema;

‘Kwa vile kakubali kushirikiana na sisi mimi sioni kwanini muondoke naye, ...mimi nitamdhamini, siku mukimuhitaji atakuja, mnaonaje ombi langu hilo?’ nikawauliza

‘Kuna mambo mengi bado anayaficha, hajakuwa mkweli, ndio maana tunataka tuondoke naye..tunauhakika akifika huko atasema kila kitu.’akasema

‘Nimewajibu kila kitu, sijaficha jambo lolote kwenu…kuweni wakweli basi, mlisema nikiwaambi akila kitu nitakuwa salama..na hebu niambieni ni jambo gani nimelificha?’ akauliza shemeji yangu akiwa kakasirika.

‘Tunashindwa kurudia swali mara nyingi,...wewe usituone kuwa sisi ni watoto wadogo, hapa tulikuwa  tunakuuliza maswali ya kukupima tu, mengi tunayafahamu,..’akasema mtu wa usalama na mwingine akaongezea

‘Hebu kwa mfano tu, hilo la kusema ulikwenda kutupa hiyo silaha porini halafu ikaibiwa hiyo sio kweli,ukweli ni kwamba kuna mtu ulimpa hiyo silaha, hilo umetuficha,hukusema ukweli, kuna mengi tunayahitajia kutoka kwako,na usiposema huo ukweli, utaozea jela...’akasema huyo mtu wa usalama, na kumfanya shemeji yangu atulie kimia.

‘Mimi naomba nimdhamini, kwa vile bado mnafuatilia mambo mengine, huyu niachieni mimi, nawashukuru sana, kwa msaada wenu, mimi bado nina maongezi na shemeji yangu, mkiwa tayari kumuhoji, mtaniambia, ila kwa leo naombeni tuishie hapa , kwani kile kitu muhimu nilichokuwa nikikihitajia nimekipata...kama kuna zaidi tutafahamishana...’nikasema

‘Huyu ni mhalifu, ..huo alio-ufanya ni wizi, japokuwa anamtupia lawama kaka yake , kamaa anaamini kuwa kaka yake ni mgonjwa , kachanganyikiwa basi singelifany hayo, …unaona eeh, angekuja kwako akuambie ili muone jinsi gani ya kumsaidia jamaa yenu…lakini ulifanya hivyo..?’ akaulizwa

‘Ha-a-pana, lakini sasa…’akasita kuongea

‘Lakini sasa nini…eeh tuambie awali tulikuuliza ukawa unsita kusema ukweli pia, hii inamaanisha ulidhamiria kuyafanya hayo uliyoyafanya, hii sio mara ya kwanza kuhojiwa kweli si kweli, ukaficha huo ukweli, hata kama waliokuhoji ni watu wengine, lakini ni watu wa usalama, umeacha mpaka sisi tukahangaika kuupata ukweli,…huyu ni mhalifu …’akasema.

‘Yeye hajui kuwa kila siku anafuatailiwa, hajui kuwa bado uchunguzi unaendelea,na hatua iliyofikia, ni ya kumalizia, tu, ...wote hawa watafikishwa mahakamni kujibu makosa waliyoyafanya, ikiwemo hilo la kumuua Makabrasha....hata kama sio yeye aliyefanya hivyo, lakini alishiriki kwa namna moja au nyingine...’akasema huyo mtu wa usalama.

‘Lakini mimi sijau..hata kaka hajafanya hilo…’akajitetea, na mimi nikaona niingilie kati ili kuokoa muda.

‘Sawa kama mumefikia huko, siwezi kuwapinga, ila kwa vile bado hamjakamilisha uchunguzi wenu, basi mimi naomba huyu mtu msimchukue kwanza, mimi namdhamini kwa kauli tu, namfahamu sana shemeji yangu huyu, siku mukimuhitaji, nitahakikisha anafika huko kituoni,...’nikasema na wale watu wa usalama wakakubaliana na mimi wakaondoka, na mimi nikabakia na shemeji yangu.

********

‘Shemeji sasa umefanya nini?’ akaanza yeye kunilaumu.

‘Ndivyo ulivyotaka wewe iwe hivyo au sio…’nikasema

‘Hapana shemeji umefanya kosa kubwa sana…’akasema

‘Hapo ni mwanzo tu shemeji, kuna mambo mengi bado nayahitaji kutoka kwako, ndio maana nikawazuia wasikuchukue, na usiponijibu leo, mimi nitawaambia hao watu waje wakuchukue,…sasa sikiliza haya mambo nataka tuyaongee mimi na wewe kwanza, ukiniambia ukweli, mimi nitajua jinsi gani ya kukusaidia ,...’nikasema

‘Mambo gani tena hayo shemeji hapa nilipo nimechanganyikiwa nafahamu kaka atakuwa ananisubiri na nimechelewa kwenda kumuona, na akisikia kuwa nime..yaongea haya sizani kama atanisamehe…unataka nini tena shemeji?’ akauliza kwa wasiwasi. Na mara simu yake ikaita

Aliangalia mpigaji halafu akasema;

‘Kaka huyu …’akasema akisita kupokea simu

‘Pokea, mwambie upo na mimi, unaogopa nini…’nikasema

Akaipokea , halafu akageuka kunipa mgongo, na kusogea mbali na mimi, akawa anaongea na kaka yake.

‘Nimezipata…nini, hapana, kabato halifunguki,…ndio, hapana sijui…ndio, kuna tatizo kidogo, nitaku-kuambia, …nakuja kaka, kwanini unasema hivyo, kwa ni nani…?’ akauliza na akawa anasikiliza kwa muda

‘Kama mimi nakuomba kama kuna jambo umelipanga, bora uachane nalo tu,..angalia afya yako kwanza, ..hawezi kufanya lolote kwa sasa, huyo ni muongo, na huenda kwa hivi sasa yupo mikononi mwa polisi, ndio maana na kuambia..sikiliza kwanza kaka…’akasema na kutulia akawa anasikiliza

‘Kaka, sikiliza nikuambie,…acha ubishi kaka…’akawa anaongea na kukatizwa katizwa na kaka yake mwishowe wakamalizana naye, halafu akanigeukia.

‘Kaka kachanganyikiwa kweli, anasema huyo mtu anayemdai….yupo mbioni kuonana na polis,..kwahiyo ..hata sijui, ana kitu gani…’akasema

‘Mwongo huyo, huyo ni tapeli, hata kama ana ushahidi, kwanini asiende kuwaona polisi…anajua na yeye ana makosa, hapo anatafuta pesa za kupata wakili, hakuna lolote anatafuta hapo..’nikasema

‘Sasa shemeji niruhusu niondoke…’akasema

‘Kwanza  tumalizane, …nashukuru nimeupata huo mkataba, lakini kuna jambo nataka kulifahamu ili mwisho wa siku nimalizane na nyie,…je ni nani huyo mwanamke aliyezaa na kaka yako..?’ nikamuuliza

‘Shemeji mbona huyo mtu mimi simjui, na kaka hajazaa na mwanamke yoyote, mimi nina imani hizo ni ndoto zake tu,...’akasema

‘Hajazaa na mtu, wakati hadi kwenye mikataba huo wa kugushi, kuna kipengele cha kumpa haki huyo mtoto, na huo mkataba uliandikwa hata kabla kaka yako hajapatwa na ajali…kwahiyo hapo hakuna kuchanganyikwa…’nikasema

‘Kiukweli mimi simjui..ila hilo la kuombea kupata mtoto wa kiume, nimemsikia sana akiliongelea, kwahiyo kwa matarajio hayo, sioni kwanini asiweke kipengele kama hicho…’akasema

‘Una uhakika na hilo jibu lako, maana nikigundua kuwa unanificha, basi sitakuamini tena, unanifahamu nilivyo, ninapokuahidi kitu, siachi kutekeleza, na ukinidanganya, siwezi kukuamini tena, na lile nililoahidi dhidi yako huwa sirudi nyuma.....’nikasema na yeye akaa kimiya, nikasema

‘Sawa kama hutaki kuniambai huo ukweli, mimi bado nalifuatilia hilo, kama nitagundua kuwa unafahamu au unahusika kwa hilo, kwa namna yoyote ile, basi, mimi na wewe hatutakuwa marafiki tena…’nikasema

‘Shemeji lakini nimekuambia kila kitu…’akalalamika

‘Wewe umekuwa kwangu, nimekusaidia kwa nguvu zangu zote kama mdogo wangu, kwanini hufanyi jambo angalau na mimi nikakuamini...’nikasema

‘Shemeji kwanini unataka kuniweka mimi kama rehani, mume wako yupo, ndiye muhusika mkuu, kwanini usimsubiri apone uje umuulize yeye hayo maswali, ukiniuliza mimi hayo maswali inakuwa  kama mtego kwangu, nichagua ama wewe au kaka…kama nilivyowaambia watu wa usalama hapa..mimi nafanya mengi kwa shinikizo, najikuta sina jinsi,...’akasema na mimi nikawa nimemuangalia tu, halafu akasema;

‘Hivi shemeji, hebu niambie haya niliyoyaongea leo hapa kwa hawa watu wa usalama, je akija kuyagundua haya niliyoyasema hapa itakuwaje, ...mimi najuta sana, nimeshindwa ...oh, nimemsaliti kaka yangu, kaka ambaye ananipenda sana, na ambaye kajitolea kwa hali na mali kwa ajili yangu...’akasema

‘Ina maana kaka yako ndiye aliyejitolea kwa hali na mali juu yako, unakumbuka mwanzoni kaka yako alikuwa akisemaje juu yako, alikuwa hakuamini, alishakuweka kwenye kundi la wavuta unga,mimi nikajitolea na kumhakikishia kuwa nitakusaidia hadi utabadilika, je ni nani aliyejitolea kwa hali na mali kati ya kaka yako na mimi..umesahau hayo eeh, kwasababu ya tamaa, kuwa mtamiliki kila kitu eeh?’ nikamuuliza

‘Shemeji nakushukuru sana..kiukweli hata kaka ninamuambia hilo, kuwa asije akafanya makosa mkaachana…wewe ni mtu muhimu sana kwangu, wewe na kaka mumejitolea kila mtu kwa nafasi yake, hilo nashukuru sana, ndio maana kuna mambo ambayo nimekuwa siyafurahiswi kuyafanya…’akatulia

‘Kama yapi…?’ nikamuuliza

‘Kama haya niliyowaeleza watu wa usalama…’akasema

‘Na haya ninayokuuliza je, je ulikuwa unafurahia mimi nikisalitiwa, kaka yako akifanya mambo kinyume na matakwa ya ndoa, na watu ambao wanataka kumrubuni tu …je huko ndio kunishukuru…’nikasema

‘Shemeji hayo mimi sijayaona kwa macho yangu…na nisingelikbali hayo yafanyike nikiwa naona,..na ndio maana nikajitolea na mimi kule kunapowezekana, ..wewe hujui tu ....lakini siwezi kusema zaidi, ninachoweza kusema kwa sasa ni ahsante kwa wema wako huo..’akasema karibu kunipigia magoti.

‘Nitakuamini pale tu utakaponiambia ukweli…’nikasema

‘Shemeji, nimakuambia kila kitu, na yale ambayo kaka hakutaka nikuambie, hebu jaribu kukaa upande wangu unionee huruma na mimi…hata kama unaona kwasasa namukuwa sio mtiifu kwako, lakini sio kwa nia mbaya, ni pale inapofikia hatua ya kuchagua kaka au wewe,hapo mimi mnaniweka kwenye njia panda....’akasema

‘Sasa sikiliza,shemeji yangu, wewe ni mtoto wa juzi, ulipolala ndipo nilipokuwa nimelala siku nyingi, nikaamuka na kufanya kazi, maendeleo yote hayo unayoyaona ni juhudu na kusimamia kila kitu kiende sawa, hebu angalia kampuni ya kaka yako inavyokufa, ni kwanini…?’ nikamuuliza

‘Madeni…’akasema

‘Kwanini kuwe na madeni mengi kiasi hicho, kwanini hamuahangaiki kutafuta wateja, kwanini hamnisikiliza kila siku nawaambia jinsi gani ya kuendesha kampuni, kampuni ni masoko, nyie mnafikiria njia za mikato, mnaona matokea yake,..rushwa, utapeli ndio umewafikisha hapo mlipo…’nikasema

‘Ni kweli, nimekuwa nikimuambia kaka sana kuhusu hilo, lakini hanisikiliza zaidi alikuwa karibu na marehemu..kila kitu marehemu atasaidia,…sasa sijui atasaidiwa na nani tena…’akasema

‘Haya, na mimi hamuniamini sio….’nikasema

‘Shemeji tunakuamini sana, na mara nyingi nilikuwa namshauri akuhusishe kwenye matatizo yake, lakini alikuwa mbishi, anasema yeye hawezi kumtegemea..mwa-mwanamke, ni kasumba tu…’akasema

‘Kwahiyo sasa ni juu yako, nimewabeba kiasi cha kutosha, nimewambembeleza kiasi cha kutosha, naona sasa ni muda wenu wa kuwajibika, na  bila kukuficha wewe na kaka yako, mpo kubaya..kuhusu  muuaji ya Makabrasha, ...unalifahamu hilo’nikasema

‘Lakini shemeji kiukweli sisi hatujalifanya hilo kabisa…na mimi sijui kaka alipokwenda kuongea na marehemu ilikuwaje,…hata hivyo nina imani hajaua, ..japokuwa wakati mwingine anaropoka tu..na hiyo bastola angeipata wapi, maana kama nilivyowaambia watu wa usalama mimi niliitupa…’akasema

‘Yawezekana kuna mbinu zenu nyingine au ulimpa Makabrasha kwa nia fulani, na wakati wanabishana huko ndani, ndio kaka yako akamuua, mwenzake au wewe ndiye uliyefika na kufanya hayo mauaji..kwa namna moja au nyingine nyie wawili mnahusika kwa maujai hayo…’nikasema

‘Shemeji nikuambiaje mnielewe, Makabrasha, yule ni ndugu yetu, hivi kuna mtu anaweza kumuua ndugu yake, na uone kaka alikwenda kuonana naye kwa ajili ya mambo ya kisheria, yeye alijitolea kumsaidia kaka, sasa tuje kumgeuka na kumuua, mbona haliji akilini...huo ni uzushi tu’akasema na kutulia

‘Elewa kuwa,..hiyo bastola ndiyo iliyotumika kwenye mauaji, na hiyo bastola ndio wewe uliiba kutoka sehemu niliyoiweka,..utawashawishi vipi polis kuwa wewe au kaka yako hahusiki na hayo mauaji, hapo hauwezi kukwepa mkono wa sheria, baba  maelezo yako uliyoyatoa hapa yanaonyesha hivyo,hayo tu yameshakufunga...’nikasema huku nikigeuka kwenye meza ndogo iliyokuwa pembeni yetu.

‘Unaona kile kifaa pale,  kinachukua kila kitu tulichoongea hapa, kwahiyo, kwangu mimi huna ujanja, pili nina ushahidi mwingine utakaokutia jela, ushahidi ambao, utaongea badala yako,nina imani ushahidi huo utaniambia kila kitu...’nikasema

‘Ushahidi gani huo shemeji...’akasema huku akiniangalia kwa mashaka.

‘Nikuulize kitu , hicho kitufe chako unahifadhia kazi za ofisini tu kama ulivyodai, au kuna mambo mengine ya binafsi?’ nikamuuliza

‘Nini..hii flash disk(kinyonyi)..aah ni mambo ya ofisini na mamba yangu binafsi, yanakuwepo, kwanini umeniuliza hivyo..?’ akaniuliza kwa mashaka.

‘Hapana nataka kujua tu, ..najiuliza kwanini ukaificha kwenye mkataba.’nikasema

‘Nilisahau, ..nahis ni wakati naifanyia kazi jana, huwa na andika kumbukumbu zangu humo,…’akasema

‘Kwahiyo jana ulikuwa unaandika yaliyotokea,…ni diary yako pia…?’ nikamuuliza na hapo akaniangalia kwa mashaka…na akatoa macho ya uwoga, akainamana na kusema;

‘Ina maana shemeji umefikia hapo siku hizi, mbona sio tabia yako, kuchukua vitu vyangu bila idhini yangu, una maana umeangalia kilichokuwepo...!?’akasema na kuuliza

‘Nimekuuliza tu…’nikasema lakini hakuamini

‘Shemeji shemeji..hapana ni lazima umeangalia kilichokuwemo humo, ni kwanini nilisahau…mungu wangu..’akasema sasa akionyesha kuchanganyikiwa.

‘Kwani kuna nini kikubwa, mbona unakuwa hivyo, unasikia, za mwizi ni arubain, hata ufanye nini ipo siku utanaswa tu..’nikasema

‘Kwanini lakini shemeji, humo kuna vitu vyangu sitaki mtu mwingine avione..nilikuwa nataka kuvihamisha kutoka kwenye…oops, makosa makubwa haya,..kwanini shemeji hujali siri za watu, nilikuambia hicho ni kitufe changu, wewe umefanya nini sijui…’akasema akinitolea macho.

‘Ni nani aliyeanza kuchukua vitu vya mwenzake bila idhini ya mwingine, mimi sikuwa na tabia hiyo, nilikuwa nakuamini kupita kiasi, lakini wewe na kaka yako mukanigeuka, na nimeona hakuna njia nyingine ila ni kufanya hivyo, na nitafanya vikubwa zaidi ya hivyo, .....sikutaka kabisa kufanya hivyo..’nikasema

‘Kwahiyo shemeji unataka mimi nifanye, nini,..hebu jaribu kuniangalia na mimi,...huku kaka huku wewe, kama ingelikuwa kwako, huku yupo ndugu yako, huku yupo shemeji yako, ungelimsaliti ndugu yako, kwa ..kwa.. mbona mnanionea bure,   ...’akawa analalamika.

‘Hayo ni juu yako, maana ukweli hauangalii kuwa huyu ni ndugu yangu au sio ndugu yangu, ukweli na haki ni msumeno hukata mbele na nyuma…ulitakiwa kuliangalia hilo, dhuluma ni dhuluma tu..’nikasema

‘Shemeji mimi nakuomba tafadhali, nipo chini yamiguu yako, kama umekiangalia hiki kitufe, naomba iwe siri yako, kuna mambo yangu mengi sana ya siri, nimefany makosa kukiacha hapo..nakuomba tafadhali,.....’akasema na kutaka kunipigia magoti , na mimi nikageuka kuondoka, nikisema;

‘Nimeshakupa muda wa kutosha, ...na bado hutaki kuwa upande wangu, na nafanya haya kwa manufaa yenu, hebu fikiria jinsi kaka yako alivyofanya, nini ingekuwa mwisho wake, unafikiri nyie mngelifaidi nini, jasho letu lote lingeishia wapi, si kwa hao watu wa njee, nab ado hata sijui tutafanya nini..’nikasema

‘Nafahamu hilo shemeji, lakini..nisaidie na mimi…’akasema

‘Unafahamu eeh, sasa fikiria jinsi gani y akuliweka hili sawa, fikiria jinsi ya kumuokoa kaka yako, na wewe mwenyewe, maana mimi sasa nimenawa mikono yangu..’nikasema.

‘Oh shemeji,...mimi hayo nilimuonya kaka, hakunisikiliza, kaka akiamua jambo lake, haambiliki, mpaka aone mwisho wake,...oh shemeji kama una.. umeangalia mambo yangu, umeniweka kubaya, nakuomba iwe siri yako, yaishie hapa hapa...’akasema huku akiangali huku na kule

‘Umejiweka mwenyewe kubaya, ..wewe na kaka yako mpo ukingoni mwa mto uliojaa mamba, mumejichimbia wenyewe kaburi, sitaki kuwatisha, ila nawaonya na kuwapa muda kidogo wa kusema kila kitu,bado muda mnao, jitokezeni mseme ukweli kabla mambo hayajaharibika..’nikasema

‘Kila kitu nimeshakuambia shemeji, unataka nini zaidi…’akasema

‘Bado sana…pamoja na yote ni nyie kutubu dhambi zenu, kusema makosa yenu yote, ili sheria iangalia mlichokikosea, na hilo lianzie kwangu,..kama mimi mliyemkosea hamtaki kutubu kwangu, je sheria ya mahakamani itafanyaje….. suluhu juu ya hili, inawategemea nyie wawili, sasa nenda kaongee na kaka yako, mjipange vyema...’nikasema na kuondoka.

‘Nitaongeaje na kaka wakati anaumwa?’ akaniuliza na mimi sikumjibu kitu, nikaondoka na kumuacha akiwa kasimama, kachanganyikiwa, na haukujua afanye nini....mimi sikumjali, nikaondoka kuelekea ndani.


Nikasubiri kama nusu saa, sikumuona akitokea, …baadae nikasikia gari likiondoka huko nje, nikajua keshaondoka, na mimi nikaichukua laptop yangu na kuanza kuangalia ni kitu gani kilikuwa kwenye kile kitufe (flash disk), alichokuwa nacho shemeji yangu...


NB: Kisa sasa kinafikia mteremko
 Lakini hadi sasa lipo swali kubwa;

‘Je ni nani aliyemuua Makabrasha, na je mdada atagundua ukweli wa msaliti wake wa ndoa, je atatimiza ahadi yake...tusubiri tuone.



WAZO LA LEO: Kuna watu inapofikia hatua ya kupata mali, wanapohisi kuwa kuna masilahi, wanapokuwa na uhakika wa kupata pesa, vyeo, ....hawaangalii tena utu na ubinadamu, wanasahau wema wote waliowahi kutendewa kinachobakia moyoni ni ubinafsi,....watu kama hao wapo tayari hata kuwadhulumu wazazi wao, au ndugu zao au jamaa zao…achilia mbali ya bosi kwa mfanyakazi wake. Mali , pesa , vyeo ni mtihani mkubwa kwetu, tuweni makini kwa hilo, tuangalie na kuchunga  haki ya mtu, tuangalie na kuchunga dhamana za watu, hayo ni madeni makubwa, kama tutahini.
Ni mimi: emu-three

No comments :